read

Muhammad Mustafa (S.A.W.) Na Urithi Wake

KAMA KIONGOZI, MUHAMMAD (s.a.w.) ALIKUWA KATIKA TABAKA LA WALE MASHUHURI KABISA - katika dunia nzima. Alijaaliwa na uwelewa wa kustaajabisha, uwezo wa kuona mbali na kipaji cha siasa. Katika miaka yake kumi ya mwisho ya uhai wake, alitakiwa afanye maamuzi muhimu sana katika historia ya Uislamu. Maamuzi yale yaliwagusa sio Waislamu tu au Waarabu bali wanadamu wote. Alikuwa pia anatambua kwamba vitendo vyake na maamuzi yake vingegusa vitendo na maamuzi ya kila kizazi cha Waislamu mpaka mwisho wa wakati wenyewe.

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) kwa hiyo, hakufanya uamuzi wowote, haid- huru uwe wa kawaida kiasi gani, kwa msingi wa kusudi maalum; wala kufanya maamuzi kwa utaratibu wa “kubahatisha.” Maamuzi yake yote yalikuwa ni ya kujaaliwa. Yalikuwa ni vigezo kwa umma wa Kiislam (taifa au jamii) kwa wakati wote. Ilikuwa ni pamoja na ujuzi na ufahamu huu kwamba alisema au kutenda kitu chochote na kila kitu.

Muhammad (s.a.w.) alifanikiwa, baada ya mapambano marefu na ya kikatili dhidi ya waabudu masanamu na washirikina wa Arabuni, katika kuanzisha Ufalme wa Mbinguni Duniani ili umma wake uweze kuja kuishi kwa amani na usalama, kupendwa na kuonewa wivu na wanadamu waliobakia. Ufalme wa Mbinguni Duniani ulikuwa ndio kazi ya maisha ya Muhammad (s.a.w.).

Alijua kwamba yeye ni binadamu, na atakuja kufa siku moja, lakini kazi yake, kama ilivyounganishwa kwenye huo “Ufalme” ingeishi. Alijua kwamba baada ya kifo chake, mtu mwingine tena angeendeleza ile kazi aliyoianzisha yeye. Alijua pia kwamba umakamu (urithi wa kazi yake) uliopangwa vizuri ndio nanga ya utulivu. Alijua yote haya na mengi zaidi ya haya. Hakuna mwislamu ambaye angeweza kamwe kuthubutu kudhania kwamba Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) hakuyajua yote haya vizuri zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Urithi wa Muhammad (s.a.w.) ulikuwa pia ni jambo la kunong’onwa sana miongoni mwa Waislamu wengi. Swali moja ambalo lilitawala sana katika akili za wengi wao, hususan baada ya kutekwa Makka, lilikuwa, ni nani atakayemrithi yeye kama Mkuu mpya wa Dola ya Madina, baada ya kufa kwake.
Swali hili linatoa nafasi kwa jibu moja tu, yaani, mwislamu bora zaidi! Mrithi wa Muhammad (s.a.w.) anapaswa kuwa, sio mtu wa daraja la pili, bali tunda bora kabisa la Uislamu; mtu ambaye Uislamu wenyewe utamkubali kwa fahari kama “chombo cha kipaji.”

“Chombo cha kipaji” kama hicho kilikuwa ni Ali ibn Abi Talib, Muhammad (s.a.w.) “alimgundua” yeye mapema maishani; alimuandaa na alimteua yeye kama mrithi wake, hivyo kuhakikisha ukabidhi wa mamlaka wa amani na utaratibu. Alikuwa na hamu kubwa sana ya kuzuia kushindania madaraka miongoni mwa maswahaba wake baada ya kifo chake yeye mwenyewe.

Lakini, kwa bahati mbaya, mpango huu haukufanikiwa, na urithishaji, baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.) haukuwa wa amani na wa utaratibu. Kulikuwa na kushindania madaraka kukali miongoni mwa maswahaba zake ambamo baadhi ya wagombea wapya wa madaraka walifanikiwa katika kukamata Dola ya Madina.

Kufanikiwa kwao kuliashiria mwisho wa ghafla wa Utawala wa Mbinguni Duniani, na kuliashiria, wakati huohuo, kuzaliwa kwa Dola ya Kiislam – Dola iliyoongozwa na watu ambao walikuwa Waislamu.

Utawala wa Mbinguni Duniani au Dola ya Kiislam haikudumu muda mrefu baada ya kifo cha Mtume. Kifo cha Taifa la Kiislamu, likiwa bado katika uchanga wake, kinaweza kuamsha udadisi wa mwanafunzi wa historia. Anaweza kushangaa ni kwa nini liliishi kwa muda mfupi kiasi hicho, na jinsi ilivyowezekana kwa hawa wagombea wapya kupindua mpango uliofanywa na Mtume (s.a.w.) mwenyewe kwa ajili ya ukabidhianaji wa amani na utaratibu wa madaraka, na kulazimisha kukubalika kwa mpango wao wenyewe juu ya umma wa Waislamu.

Lifuatalo Ni Jaribio La Kujibu Swali Hili

Wagombea wapya wa madaraka hawakuunga mkono ule mpango uliofanywa na Mtume (s.a.w.) wa kukabidhi madaraka. Wao na wafuasi wao walikuwa na ajizi nyingi za kuuhusu, na walikuwa wamekusudia kukamata Dola ya Madina wao wenyewe. Kwa ajili hii, walikuwa wamekwishapanga mkakati wa hali ya juu na walikuwa wameingia katika kazi ya kuutekeleza hata kabla ya kifo cha Mtume (s.a.w.).

Hila kuu katika mkakati wa hawa wagombea wa madaraka ulikuwa ni kueneza ile taarifa ya uongo kwamba si Kitabu cha Allah (s.w.t.) kilichoelezea maoni yoyote juu ya jambo la uongozi wa umma wa Waislamu, wala Mtume wa Allah (s.a.w.w). kuchagua mtu yeyote kama mrithi wake.

Waliwaza kwamba kama Waislamu wakiamini dai kama hilo kuwa la kweli, basi watachukulia kwamba Mtume (s.a.w.) aliiacha kazi ya kutafuta kiongozi wa baadae wa serikali yake kwa umma wenyewe, na katika umma huo, kwa kweli, kila mtu alikuwa huru kuingia kwenye orodha na kunyakua madaraka mwenyewe, kama angeweza.

Dr. Hamid-ud-Din:

“Qur’an Tukufu haikutaja kitu chochote kuhusu namna ya kuchagua khalifa. Hadithi za kutegemewa za Mtume (s.a.w.) nazo pia ziko kimya kuhusiana na hili. Kutokana na hili, mtu anaweza kuchukua uamuzi kwamba Shari’ah (Sheria Tukufu) imeliacha jambo hili kwenye mapendekezo ya Umma wenyewe ili uweze kuchagua viongozi wao kulingana na mahitaji yao wenyewe, na kulingana na hali itakayokuwepo wakati huo.”

(History of Islam by Dr. Hamid-ud-Din, M.A.{Honors}, Punjab; M.A.{Delhi}; PH.D.[Harvard
University, U.S.A.}, Published by Ferozesons Limited,
Publishers,Karachi,Pakistan,page188,4thedition, 4th printing, 1971)

Hila hii ilipata mafanikio ya kushangaza, na ina maisha marefu ya kustaajabisha. Ilitumika wakati huo na inatumika siku hizi.Huko nyuma ilikuwa ikitumika huko Mashariki tu; sasa inatumika kote Mashariki na Magharibi. Wachache huko Mashariki na hakuna yeyote huko Magharibi walioshindana nayo. Mafanikio yake yanathibitishwa na ushahidi wa wanahis- toria wafuatao:

Marshall G.S. Hodgson:

“Qur’an haikutoa, kwa mfano hasa, mambo ya kisiasa yanayoweza kutokea kwa kifo cha Mtume (s.a.w.)” (The Venture of Islam,Vol1, 1974)

Dr. Muhamed Hamidullah:

“Ukweli kwamba zimekuwepo tofauti za maoni, katika kifo cha Mtume (s.a.w.), unaonyesha kwamba hakuacha maelekezo ya wazi na sahihi kuhusu kurithiwa kwake.”(Introduction to Islam, Kuwait, 1977)

Francesco Gabrieli:

“Muhammad (s.a.w.) alifariki, baada ya kuugua kwa muda mfupi, mnamo tarehe 8 Juni, 632. Hakuweka au hakuweza kuweka ushahidi wa kisiasa na hakumteua mtu aliyekuwa anastahili sana kumrithi yeye.”
(The Arabs, A Compact History, New York, 1963)

G. E. Von Grunebaum:

“Mtume (s.a.w.) alifariki mnamo tarehe 8 Juni, 632. Hakufanya maandalizi kwa ajili ya mtu atakayemrithi.” (Classical Islam – A History 600 – 1258)

John B. Christopher:

“Tatizo la haraka sana lililoikabili Jumuiya changa ya Madola ya Kiislamu lilikuwa ni urithi kwenye uongozi wa umma pale Muhammad (s.a.w.) alipofariki; tatizo hili lilikutwa na kuanzishwa kwa ukhalifa.

Kwa sababu Muhammad (s.a.w.) hakufanya maandalizi kwa ajili ya mtu atakayemrithi, ile jumuiya ya Kiislam iliyoathirika ikageukia nyuma kwenye vigezo vya kika-bila vya kuchagua Sheikh mpya mara tu baada ya Mtume (s.a.w.) alipofariki.” (The Islamic Tradition, Introduction, New York)

Bernard Lewis:

“Katika asili zake, ile taasisi kubwa ya Kiislam ya ukhalifa ilikuwa ni ushitukizaji wa ghafla. Kifo cha Mtume (s.a.w.), bila ya urithishaji uliopangwa, kilihimiza mgogoro kwenye jumuiya changa ya Kiislamu.” (The Legacy of Islam – Politics and War – 1974)

George Stewart:

“Kuipitia upya historia, mtu anasita na kushangaa ni vipi ukhalifa umetokea kuwepo. Muhammad (s.a.w.) hakuacha usia wowote; hakumteua mtu yoyote kufuata katika nyayo zake, hakukaimu kwa yeyote mamlaka ya kiroho, na hakutoa funguo za Utawala wa Mbinguni kwa mtu ambaye ni Mtume…”

(George Stewart katika makala yake, Is the Caliph a Pope? iliyochapishwa katika kitabu, The Traditional Near East, kilichohaririwa na Stewart Robinson, na kuchapishwa na Prentice-Hall, Inc., N.J., 1966)

Robert Frost wakati fulani alisema: “Nadharia, kama ukiishikilia kwa nguvu ya kutosha na kwa muda mrefu wa kutosha, inapata kuthaminiwa kama kanuni ya imani.” Maelezo haya yanaweza kubadilishwa kidogo yasomeke kama ifuatavyo: “Uongo, kama ukiushikilia kwa nguvu ya kutosha na kwa muda mrefu wa kutosha, unapata kuthaminiwa kama kanuni ya imani.”

Wingi usio na idadi, wa wanahistoria wa Uislamu, wamedai kwamba Mtume (s.a.w.) hakumtaja bayana mtu yeyote kama kiongozi wa baadae wa Dola ya Madina baada ya kifo chake yeye mwenyewe. Kwao wao, na kwa wengine wengi, dai hili limekuwa ni kanuni ya imani sasa.

Lakini sio kwa Waislamu wa Shia. Wao wanatetea kwamba Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.w.t.) alitangaza kwa kurudiarudia na kwa msimamo ulio wazi kabisa kwamba Ali alikuwa ndio mshikamakamu wake na kiongozi wa Waislamu wote.

Muhammad (s.a.w.) alionyesha uelekeo kwa ajili ya umma wake, na aliwaonya wao wasiukengeuke baada ya kifo chake. Lakini umma ulikengeuka hata hivyo, na ukengeukaji huu umewafikisha, kwa kujua au kwa kutojua, kwenye kufufua mila ya kipagani.

Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.), baadhi ya maswahaba walikusanyika kwenye ukumbi wa nje ya Madina uliokuwa ukiitwa Saqifah, na wakamchagua Abu Bakr kama kiongozi wa Waislamu. Hapakuwa na kigezo katika Uislamu kwa ajili ya uchaguzi kama huo, lakini kilikuwepo kigezo kwa ajili hiyo katika asasi za kisiasa za nyakati kabla ya Uislamu.

Wanahistoria watatu wa wakati mmoja wa Pakistani wanaandika katika historia zao History of the Islamic Caliphate kama ifuatavyo:

“Baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.), tatizo muhimu na gumu sana ambalo Waislamu ilibidi wakabiliane nalo, lilikuwa lile la kuchagua khalifa. Qur’an iko kimya juu ya jambo hili, na Mtume (s.a.w.) pia hakusema lolote juu yake. Katika nyakati za kabla ya Uislamu, desturi ya Waarabu ilikuwa ni kuchagua wakuu wao kwa wingi wa kura. (Kwa kushindwa kupata kigezo kingine) kanuni hiyo hiyo ilifuatwa katika kumchagua Abu Bakr.”

(History of the Islamic Caliphate (Urdu), Lahore, Pakistan. Professor M. Iqbal, M.A., L.L.B.; Dr. Peer Muhammad Hasan, M. S., Ph. D.; Professor M. Ikram Butt, M.S.)

Kwa mujibu wa wanahistoria hao watatu waliotajwa hapo juu, kazi muhimu kabisa mbele ya Waislamu wakati wa kifo cha Mtume (s.a.w.) ilikuwa ni kutafuta kiongozi, kwa vile Mtume (s.a.w.) aliwaacha bila kiongozi. Kukosekana kwa kigezo katika Uislamu wenyewe kwa ajili ya kutafutia kiongozi, walilazimika kuchukua mila ya kipagani, na wakamchagua Abu Bakr kama kiongozi wao mpya.

Mtindo huu wa kutafuta kiongozi kwa ajili ya Waislamu ulikuwa haukubaliani na busara za Uislamu. Ulikuwa, kwa hiyo, ni upotofu, kama ilivyokwisha tajwa. Upotofu huu umezingatiwa na Mustashirki wengi; miongoni mwao ni:

R. A. Nicholson:

“Kwamba Muhammad (s.a.w.) hakuacha mtoto wa kiume ilikuwa labda haikuwa na maana zaidi kuliko kupuuza kwake au kukataa kuteua mrithi. Waarabu walikuwa ni wageni na mtiririko wa kurithiana katika mamlaka ya kifalme, ambapo wazo hilo lilikuwa halijaingia bado la mtawala mkazi mwenye haki ya ki-Mungu katika familia ya Mtume (s.a.w.). Ilikuwa inakubaliana kwa kinaganaga na mazoea ya Waarabu kwamba jamii ya Waislamu ichague kiongozi wake yenyewe, kama vile katika siku za upagani kabila lilichagua kiongozi wake lenyewe.”(A Literary History of the Arabs)

Profesa Nicholson anasema kwamba: “Waarabu walikuwa ni wageni na mtiririko wa kurithiana katika mamlaka ya kifalme. Anaweza akawa sawa. Waarabu, hata hivyo, walikuwa hawana uzoefu na vitu vingine vingi kama vile imani katika Tauhidi ya Allah (s.w.t.) na walikuwa na uzoefu mkubwa na masanamu yao ya mawe na miti; waliambatana nayo kwa ushupavu, na wengi wao wakafa kwa ajili yao.”

Hata hivyo, ule “ugeni” wa Waarabu kwenye mtiririko wa kurithiana katika mamlaka ya kifalme haukudumu kwa muda mrefu; ulidhihirisha kuwepo kwa muda mfupi sana. Kwa kweli, huo “ugeni” wao ulidumu kwa chini ya miaka thelathini (kutoka 632 hadi 661). Baada ya ile miaka thelathini ya ugeni na kanuni ya mtiririko wa kurithiana wa mamlaka ya kifalme, wakaja kuwa na ujuzi sana nayo, na ujuzi wao mpya umedumu mpaka kufika kwenye nyakati zetu wenyewe.

Kwa kuwa “wageni” na utaratibu wa mtiririko wa kurithiana wa mamlaka ya kifalme, Waarabu walikuwa wanapapasa gizani, ambapo ghafla wakajikwaa kwenye mfano kutoka kwenye zama zao wenyewe za kabla ya Uislamu, kutoka kwenye siku zile walipokuwa waabudu masanamu, na wakaudaka. Walisisimka kwamba walikuwa wamepata “wokovu.”

Francesco Gabrieli:

“Kwa kuchaguliwa kwa Abu Bakr kanuni ilianzishwa kwamba Ukhalifa au Uimam (Uimam katika suala hili ni kisawe cha khalifa) ulikuwa ubakie kwenye lile kabila la Makka la Quraishi ambalo Muhammad alitokana nalo. Lakini wakati huohuo mwenendo wa uwezo wa uchaguzi wa nafasi hiyo uliidhinishwa, kama ule wa bwana au kwa kukataa madai ya kurithiana ya familia ya Mtume (s.a.w.) (Ahlul Bait) inayowakilishwa na Ali.” (The Arabs, A Compact History, 1963)

Francesco Gabrieli anasema kwamba: “kwa kuchaguliwa kwa Abu Bakr, utaratibu ulianzishwa kwamba Ukhalifa utabakia katika lile kabila la Makka la Quraishi. Lakini hasemi ni nani aliyeanzisha “utarattibu” huu. Je, anayo idhini ya Qur’an au Hadith za Mtume (s.a.w.) za kuiunga mkono? Haina.

Kwa kweli, ulikuwa ni “utaratibu” wenye kusudi maalum uliotekelezwa na wale watu ambao walitaka kujitwalia Ukhalifa au Uimamu kwa wao wenyewe. Waliuona “utaratibu” huu ni wenye kufaa sana kwa sababu uliwawezesha wao kuikamata serikali ya Muhammad (s.a.w.w), na kuing’ag’ania wakati wakiwazuia watoto wake kutokana nayo. Lakini kivitendo kama ulivyo “utaratibu” huu, unayo idhini yake, sio ndani ya Qur’an bali katika “jamii ya kipagani,” kama ilivyoonyeshwa na mwanahistoria huyu mwenyewe.”

Bernard Lewis:

“Mgogoro wa kwanza katika Uislamu ulikuja wakati wa kifo cha Mtume (s.a.w.) mwaka 632. Muhammad (s.a.w.w) hajawahi kudai kuwa zaidi ya mwanadamu anayekufa – tofauti sana juu ya wengine kwa sababu alikuwa Mtume wa Allah na mwenye kuleta neno la Allah (s.w.t.) bali mwenyewe sio kama Mungu wala asiyekufa.

Alikuwa, hata hivyo, hakuacha maagizo ya wazi juu ya nani alikuwa amrithi yeye kama kiongozi wa Jumuiya ya Kiislamu na mtawala wa Dola changa ya Kiislamu, na Waislamu walikuwa na ujuzi wa kisiasa mdogo sana wa Arabia ya kabla ya Uislamu wa kuwaongoza wao.

Baada ya mabishano kiasi na kipindi kifupi cha mvutano wa hatari, walikubaliana kumteua Abu Bakr, mmoja wa waliosilimu mwanzoni kabisa na mwenye kuheshimiwa sana, kama khalifa, naibu, wa Mtume (s.a.w.) – hivyo kuunda, takriban bila ya kutegemea, ile taasisi kubwa ya kihistoria ya Ukhalifa.
(The Assassins,1968)

Kama ilivyoelezwa mapema, ile taarifa ya uongo kwamba Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w.w) hakuacha maagizo yoyote juu ya ni nani alikuwa amrithi kama kiongozi wa Jumuiya ya Kiislam, imekuwa ni Kanuni ya Imani kwa wengi wa wanahistoria, wa zamani na wa sasa, Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Mtu labda anaweza kuwapuuza hao wanahistoria wa Kisunni kwa kung’ang’ania kwenye “kanuni ya imani” hii lakini ni ajabu kwamba wanazuoni wa safu kama hiyo na sifa kama Nicholson na Bernard Lewis hawakufanya chochote zaidi katika vitabu vyao juu ya Uislamu kuliko kuandika tena mtindo usiobadilika wa historia ambao “ulirithishwa” kwao na wanahistoria wa mabaraza ya Damascus na Baghdad ya karne za mbeleni. Bernard Lewis, hata hivyo, amekiri, kama Nicholson na Gabrieli, kwamba wale Waislamu ambao walimchagua Abu Bakr kama khalifa wao, walikuwa na ujuzi wa kisiasa mdogo sana wa Arabia ya kabla ya Uislamu wa kuwaongoza.

Bernard Lewis anaendelea kusema kwamba ile taasisi kubwa ya kihistoria ya Ukhalifa ilizaliwa “takriban bila ya kutegemewa.”

Taasisi muhimu sana ya kisiasa ya Uislamu – Ukhalifa – ilizaliwa kwa hiyo “takriban bila ya kutegemewa!”

George Stewart:

“Cheo cha Ukhalifa kilikuja kuwepo sio kwa mpango wa makusudi au katika busara ya kuganga yajayo, bali takriban kutokana na kama ajali… Ukhalifa uliumbwa kutokana na ajali za ghasia za zama hizo ambazo zilifanya uzaliwe.” (The Traditional Near East, 1966)

Akiandika kuhusu jamii ya Kiarabu ya kabla ya Uislamu, Profesa John Esposito, anasema: “Kikundi cha familia kadhaa zinazohusiana kilitengeneza ukoo. Mkusanyiko wa koo kadha uliunda kabila. Makabila yaliongozwa na chifu (shaykh) ambaye alichaguliwa kwa makubaliano ya watu wa sawa na yeye – yaani, wakuu wa koo au familia zina- zoongoza.” (Islam – the Straight Path, 1991, uk. 5)

Katika kitabu hicho hicho (na mlango huo huo), Profesa Esposito anaendelea kusema – katika ukurasa wa 16: “..Jamii iliyoegemea kwenye ushirikishwaji wa kikabila na sheria na desturi ya kikabila iliyotungwa na watu ilibadilishwa kuwa jamii iliyounganishwa kidini (umma wa Kiislamu) uliotawaliwa na sheria ya Allah (s.w.t.)”

(Abu Bakr alichaguliwa na kuwa mkuu (sheikh) kwa “makubaliano ya mamwinyi – yaani wakuu wa koo au familia zinazoongoza.” Ilikuwa ni ile “sheria na desturi ya kikabila iliyotungwa na watu” iliyompa mamlaka. Kitu kimoja ambacho hakikutekelezwa katika kuch- aguliwa kwake, ni “sheria ya Allah (s.w.t.))

Wanahistoria wote waliotajwa hapo juu wanakubaliana katika kueleza kwamba:

1. Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), hakutoa maagizo yoyote kwa umma wake kuhusiani na mwenendo wa serikali ya baadae ya Kiislam, na hakumteua mtu yoyote kuwa kiongozi wake baada ya kifo chake yeye mwenyewe. Katika suala la ushikamakamu, hakuwa na msimamo wa wazi wa sera.

2. Wakati Muhammad alipokufa, Waislamu walilazimika watafute kiongozi mpya wa jumuiya hiyo. Kwa kukosa muongozo na kigezo, hawakuwa na chaguo bali kurudia nyuma kwenye taasisi na desturi za kisiasa za Zama za Ujahilia ili kupata kiongozi, na Abu Bakr akawa ndio chaguo lao.

Kama wanahistoria hawa wako sawa, basi ni kosa baya kupita kiasi kwa upande wa Qur’an Tukufu na Mfasiri na Mtangazaji wake, Muhammad (s.a.w.), kuacha kuwaelimisha Waislamu katika jambo la kuchagua viongozi wao.

Lakini halikuwepo na lisingeweza kuwepo kosa baya kupita kiasi kama hilo kwa upande wa ama Qur’an au Muhammad (s.a.w.). Qur’an imeeleza, kwa maneno ya wazi na makali, ni zipi sifa za kiongozi aliyeteuliwa na Allah (s.w.t.) na Muhammad (s.a.w.) aliuambia umma, kwa maneno ya kufahamika kirahisi na makali, ni nani mwenye sifa hizo. (Suala hili limeshughulikiwa katika mlango mwingine).

Wakati huu, hata hivyo, Abu Bakr alichaguliwa kuwa khalifa wa Waislamu. Amri ya Allah (s.w.t.) haikutekelezwa katika kuchaguliwa kwake. Kuchaguliwa kwake, kwa hiyo, kunazua maswali ya msingi, kama:

1. Matakwa ya Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.) hayakuonekana popote katika uchaguzi wa Abu Bakr. Kwa vile alichaguliwa na baadhi ya maswahaba wa Mtume (s.a.w.), alikuwa ni mwakilishi wao au mwakilishi wa Waislamu. Mtume (s.a.w.) peke yake angechagua mrithi wake, na hakumchagua Abu Bakr. Je, bado Abu Bakr anaweza kuitwa mrithi wa Mtume wa Allah?

2. Wajibu mkubwa katika mfumo wa jamii yoyote unatekelezwa na serikali au hasa, na kiongozi wa serikali hiyo. Qur’an inashikilia kwamba yenyewe ni pana na haikuacha kitu chochote cha muhimu. Lakini mashabiki wa Abu Bakr wanasema kwamba Qur’an haikuwaambia Waislamu namna ya kumpata kiongozi wa serikali yao. Kama wako sawa, sasa basi, je, tunaweza kudai mbele ya wasiokuwa Waislamu kwamba Qur’an ni mkusanyiko wa sheria ulio kamili na sahihi, na haikusahau jambo lolote muhimu la maisha ya mwanadamu kulifikiria?

3. Kama Muhammad Mustafa (s.a.w.) mwenyewe hakuwaongoza Waislamu katika nadharia na utendaji wa serikali, basi, je, tunaweza kudai mbele ya wasiokuwa Waislamu kwamba yeye ni mfano bora kwa wanadamu wote katika kila kitu?

4. Hivi mafundisho ya Muhammad (s.a.w.) yalikuwa pungufu na yasiyotosheleza kiasi hicho kwamba mara tu baada ya alipokufa, wafuasi wake walilazimika kutekeleza desturi, vigezo na mila za kipagani? Na kwa kuwa walifanya hivyo, je, hakuacha mwenendo wake kuwa wakutiliwa mashaka?

Ukweli ni kwamba Qur’an Tukufu ni kanuni pana na timilifu ya maisha. Lakini watakaopata uongofu ndani yake, ni wale tu watakaoutafuta. Hakuna ushahidi kwamba uongofu kutoka kwenye Qur’an ulitafutwa katika uchaguzi wa Abu Bakr. “Utaratibu” uliotekelezwa katika uchaguzi wake ulitolewa kutoka kwenye uzoefu wa kisiasa wa Arabia ya kipagani. Uongozi wake uliegemea kwenye desturi iliyochimbuliwa kwenye mamlaka ya kikabila ya kabla ya Uislamu.

Kama vile Qur’an ilivyo kanuni timilifu ya maisha, Muhammad Mustafa (s.a.w.), Mletaji na Mfasiri wake, ndiye mfano bora kwa wanadamu. Alijua kwamba alikuwa anapaswa kutii sheria zilezile za uhai na umauti kama walivyokuwa binadamu wengine. Alikuwa pia amejaaliwa na hisia za historia, na alijua ni nini kilitokea wakati viongozi wakubwa walipofariki.

Kitu kimoja ambacho asingeweza kukifanya, ni kuwaacha watu wake kuwa wapinzani kwa mara nyingine tena kama walivyokuwa katika Zama za Ujahiliya. Kitu kimoja ambacho kisingeweza, na hakikuweza kumtoka kwenye uangalifu wake, kilikuwa ni taratibu ya urithi katika Ufalme wa Mbingnii Duniani.

Abu Bakr alichaguliwa katika ukumbi wa Saqifah kama kiongozi wa serikali ya Waislamu kwa msaada wa Umar bin al-Khattab. Kwa hiyo, serikali yake, na vilevile serikali za warithi wake wawili – Umar na Uthman – wote watatu, walikuwa ni “matokeo” ya Saqifah. Nitazitaja serikali zao kama serikali za Saqifah ili kuzitofautisha na serikali ya Ali ibn Abi Talib ambayo haikuwa matokeo ya Saqifah. Serikali ya Ali ilikuwa ni ule Ufalme wa Mbinguni Duniani (uliorudishwa).