read

Mwaka Wa Kwanza Wa Hijiria

Kulingana na uchunguzi wa marehemu Mahmud Pasha al-Falaki wa Misri, siku ambapo Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Allah (s.a.w.), aliyofika Quba ilikuwa ni Jumatatu, tarehe 8 ya mwezi wa Rabi ul Awwal wa mwaka wa 13 wa Tangazo la Utume, tarehe ambayo inafikiana na tarehe 20, Septemba 622 A.D.

Katika Ijumaa iliyofuata, 12 Rabi ul Awwal (Septemba, 24), Mtume wa Allah (s.a.w.) aliondoka Quba, na akaingia Yathrib. Alifikia kwenye nyumba ya Abu Ayyub, kama ilivyoelezwa tayari.

Ujenzi Wa Msikiti Hapo Yathrib

Tendo la kwanza la Muhammad Mustafa, Allah (s.w.t.) ampe amani yeye na Ahlu-Bait wake, wakati alipofika Yathrib, lilikuwa ni kujenga Msikiti wa kumuabudia Allah (s.w.t.) ndani yake. Mbele ya nyumba ya Abu Ayyub palikuwa na eneo la wazi mali ya mAyatima wawili. Mtume (s.a.w.) aliwaita wao na walezi wao, na akawaambia kwamba alikuwa anataka kununua ardhi ile. Wakamwambia kwamba wangefurahi sana kuifanya ardhi ile zawadi kwake. Lakini alikataa kuipokea kama zawadi, na akasisitiza kuilipia kwa bei yake. Hatimae walikubali kupokea malipo kwa ajili ya ardhi yao. Malipo yakafanywa na uchimbaji wa kiwanja ukaanza mara moja.

Akielezea sababu kwa nini Mtume (s.a.w.) hakuipokea ile ardhi kama zawadi, M. Abul Kalam Azad anasema katika kitabu chake, Rasul-e- Rahmat (Mtume wa Rehma), (Lahore, Pakistan, 1970):

Mtukufu Mtume (s.a.w.) hakutaka kuchukua wajibu wa mtu yeyote. Ni nani anayeweza kudai kuwa muaminifu zaidi kwake kuliko Abu Bakr? Na yeye mwenyewe alisema kwamba anamshukuru sana Abu Bakr kwa msaada wake wa utu na mali kuliko mtu mwingine yeyote. Na tena, pale Abu Bakr alipotaka kumpa zawadi ya ngamia kwenye usiku wa kuondoka Makka kwenda Yathrib, yeye hakuikubali mpaka alipokuwa amemlipa Abu Bakr bei yake. Vivyo hivyo, huko Yathrib, alipotaka kununua ardhi kwa ajili ya kujenga Msikiti juu yake, wamiliki wake waliitoa kwake kama zawadi. Lakini alikataa kuipokea kama zawadi. Ardhi hiyo ilichukuliwa tu pale wamiliki wake walipokubali kupokea bei yake kutoka kwake ambayo aliilipa.Huu Msikiti wa Yathrib ulikuwa ndio bora sana katika urahisi wa dhana na usanii muundo.

Vifaa vilivyotumika katika ujenzi wake vilikuwa ni matofali yasiyochomwa na mota kwa ajili ya kuta, na makuti ya mtende yaliyozuiliwa na magongo ya minazi. Shubaka la Msikiti huo lilielekea upande wa Jerusalem upande wa kaskazini. Kila moja kati ya pande zile nyingine tatu ulitobolewa na lango. Sakafu ya Msikiti haikuwa na matandiko hapo mwanzoni, hata angalau mikeka iliyochakaa. Vibanda viwili pia vilijengwa kwenye ukuta wa nje, kimoja cha Sauda binti ya Zama’a; na kingine kwa ajili ya Aishah, binti ya Abu Bakr, wale wakeze wawili Mtume (s.a.w.) kwa wakati huo.

Vibanda vipya vilijengwa kwa ajili ya wake wapya kama walivyoingia katika miaka ya baadae. Ilikuwa ni mara ya kwanza ambapo Waislamu walifanya kazi kama timu moja katika mradi wa jamii. Katika miaka iliyofuatia, timu hii ilikuwa ijenge jengo kubwa la Kiislam.

Kwa kuhamasishwa na kuwepo kwa Mtume wa Allah (s.a.w.), kila mmoja wa Masahaba alikuwa anachuana ili kuwashinda wengine.

Miongoni mwa Masahaba hao alikuwa ni Ammar ibn Yasir, ambaye, kwa mujibu wa Ibn Ishaq, alikuwa ndiye mtu wa kwanza katika Uislamu kujenga Msikiti. Ibn Ishaq hakutaja bayana ni Msikiti upi ambao Ammar ali- jenga. Lakini Dr. Taha Husain wa Misri anasema kwamba Ammar alijenga Msikiti huko Makka kwenyewe na aliswali ndani yake, nyuma kabisa kabla hajahamia Yathrib.

Wakati Msikiti ulipokuwa unajengwa, lilitokea tukio ambalo Ibn Ishaq ameliandika kama ifuatavyo: “Ammar b. Yasir aliingia ndani wakati wakiwa wamemzidishia mzigo wa matofali, akisema, “Wananiua. Wananitwisha mimi mizigo wasiyoweza kuibeba wao wenyewe.” Ummu Salma, mkewe Mtume (s.a.w.) akasema: “Nilimuona Mtume (s.a.w.) akipitisha mkono wake kwenye nywele zake (Ammar) – kwani alikuwa ni mwenye nywele zenye mawimbi – na akasema, “Wapi, ibn Sumayya! Sio hao watakaokuua wewe, bali ni kundi la watu waovu.”

(Ubashiri huu unasemekana ulikuja kutimizwa wakati Ammar alipouawa huko Siffin Suhayli, ii, uk. 3)

Ali alitunga shairi la rajaza siku hiyo (Msikiti ulipokuwa unajengwa):

Yupo mmoja anayejitahidi usiku na mchana
Kutujengea sisi Msikiti wa tofali na ufinyanzi
Na mtu anayekimbia mavumbi mbali.

Ammar alilikariri na kuanza kulighani.
Alipolishikilia sana, mmoja wa Masahaba wa Mtume (s.a.w.) alidhani ni yeye aliyeleng- wa ndani yake, kwa mujibu wa kile Ziyad b. Abdullah el-Bakkai alivyoniambia mimi kutoka kwa Ibn Ishaq. Huyu wa baadae (ibn Ishaq) kwa kweli alimtaja mtu mwenyewe.

Alisema: “Nimesikia ulichokuwa ukisema kwa muda mrefu, Ewe Ibn Sumayya, na Wallahi nafikiri, nitakupiga kwenye pua!” Sasa alikuwa na fimbo mkononi mwake, na Mtume (s.a.w.) alikasirika sana na akasema: “Kuna nini kati yao na Ammar? Anawakaribisha wao Peponi ambapo wao wanamkaribisha motoni. Ammar ana thamani kwangu kama uso wangu mwenyewe. Kama mtu atakuwa na tabia namna hii hatasamehewa, hivyo muepuke.”

Sufyan b. Uyana ametaja kutoka kwa Zakariya kutoka kwa al-Shabi kwamba mtu wa kwanza kujenga Msikiti alikuwa ni Ammar bin Yasir.

(Suhayli anasema: Ibn Ishaq alimtaja mtu huyo, lakini Ibn Hisham alipendelea asi- fanye hivyo, kama kutomtaja mmoja wa maswahaba wa Mtume (s.a.w.) katika mazingira yanayoaibisha. Kwa hiyo haitakuwa haki kamwe kutafuta kumjua. Abu Dharr anasema: Ibn Ishaq alimtaja mtu huyo na akasema,: “Mtu huyu alikuwa ni Uthman b. Affan.” Wahariri wa Cairo wanasema kwamba katika ile Mawahib al-Laduniya, al- Qastalani, (kafa A.D.1517), amesema kwamba mtu huyo anasemekana kuwa alikuwa ni Uthman b. Mazun. Huyu mwandishi wa mwisho anaweza kupuuzwa kwa usalama katika nukta hii.)”

Katika eneo la ujenzi wa Msikiti huo, mtu anaweza kushuhudia vituko vyenye kuumiza sana katika Hadith ya siku za mwanzo za Uislamu – Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Allah (s.a.w.) akiondoa vumbi, kwa mikono yake mwenyewe, kutoka kwenye kichwa na uso wa Ammar ibn Yasir. Hakumpendelea sahaba mwingine yoyote kwa dalili za mguso, upendo na huruma.

Wakati Mtume wa Allah (s.a.w.) alipowalaumu maswahaba zake kwa kumwingilia Ammar, na akasema kwamba yeye (Ammar) alikuwa anawakaribisha peponi ambapo wao walikuwa wanamkaribisha motoni, yeye (Mtume) alikuwa, yumkini kabisa, anafasiri ile Aya ya 41 ya Sura ya 40 (Sura-tul-Mu’min) iliyoko ndani ya Qur’an ambayo inasomeka kama ifuatavyo:

“Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uokovu, nanyi mnaniita kwenye moto?”

Akitoa maelezo juu ya Aya hii, Abdullah Yusuf Ali, yule mfasiri wa Qur’an Tukufu anasema: “Inaweza kuonekana ni ajabu kwa mujibu wa sheria za dunia hii kwamba angekuwa anawatafutia wao wema, ambapo wao wanamtafutia maangamio yake; lakini huo ni upeo wa Imani.”

Yule sahaba aliyezozana na Ammar ibn Yasir wakati Msikiti wa Yathrib ulipokuwa unajengwa, hakuwa mwingine zaidi ya Uthman bin Affan, mmoja wa makhalifa wa baadae wa Waislamu. Alichukizwa na kufanya kazi kwenye vumbi na matope, na kufanya nguo zake kuingia tope. Wakati Mtume wa Allah (s.w.t.) alipomuonyesha kutoridhika kwake, ilibidi anyamaze kimya lakini tukio hilo lilimkereketa moyoni mwake, na hakulisahau kamwe. Miaka mingi baadae alipokuwa khalifa, na kuwa na mamlaka mikononi mwake, aliwaamuru watumwa wake kumuangusha chini Ammar ibn Yasir na kumpiga – mtu ambaye alikuwa na thamani kwa Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) kama uso wake (Mtume) mwenyewe.

Madai kwamba hakuwa Uthman bin Affan bali alikuwa ni Uthman bin Mazun au mtu mwingine yoyote yule, ambaye, kwa kumtisha Ammar ibn Yasir, aliamsha hasira za Mtume wa Allah (s.w.t.), ni jaribio tu la kujionyesha kwa wanahistoria “wanaojipendekeza” wa nyakati zilizofuata baadae.

Kwa wakati huu, Ammar ibn Yasir tayari alikwishapata sifa bora nne ambazo lazima ziwe zimemfanya yeye kuwa husuda wa maswahaba wengine wote wa Muhammad, Mjumbe wa Allah (s.a.w.). Sifa hizo zilikuwa ni:

1. Alitokana na familia ya kwanza ya Kiislam.

2. Alikuwa mtoto wa Mashahidi wa Kwanza na wa Pili wa Uislamu. Mama yake, Sumayya, alikuwa wa kwanza, na baba yake, Yasir, alikuwa shahidi wa pili katika Uislamu. Ilikuwa ni heshima ambayo haikupatwa na sahaba mwingine yoyote wa Muhammad Mustafa.

3. Alikuwa ndio mjenzi wa Msikiti wa kwanza.

4. Alikuwa ni kipenzi cha Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Allah (s.a.w.).

Allah (s.w.t.) awape rehemu Ammar ibn Yasir na wazazi wake.

Adhana Na Swala

Ilikuwa ni amri kwa Waislamu kuswali mara tano kwa siku. Walipaswa kusimamisha shughuli za kazi zao za siku, na kutekeleza wajibu huu. Lakini hapakuwa na njia ya kuwatahadharisha kwamba wakati umefika kwa ajili ya kuswali.

Kwa mujibu wa Hadith za Sunni, sahaba mmoja alimshauri Mtume (s.a.w.) kwamba lingepulizwa tarumbeta au kengele ingegongwa kuwatahadharisha Waislamu kabla ya wakati wa kila Swala. Mtume (s.a.w.) hakukubali ushauri huu, kama alivyosema kwamba hakutaka kuchukua desturi za Kiyahudi au Kikristo.

Abdillah bin Ziyad alikuwa mwenyeji wa Yathrib. Alikuja kumuona Mtume, na akasema kwamba alipokuwa nusu-macho au nusuusingizini, mtu alitokea mbele yake na kumwambia kwamba sauti ya mwanadamu ingetumika kuwaita waumini kwenye Swala; na pia alimfundisha hiyo Adhana (mwito wa Swala), na namna ya kuisoma.

Wanahistoria wa Sunni wanasema kwamba wazo hilo lilikubalika kwa Mtume, na akalichukua papo hapo. Yeye ndipo akamwita Bilal, akamfundisha jinsi ya kuwaita Waislamu kwenye Swala; na akamchagua kuwa Muadhini wa kwanza wa Uislamu.

Hadithi hizi hazifuatwi na Waislamu wa Shia. Wao wanasema kwamba kama vile Qur’an Tukufu ilivyoshushwa kwa Muhammad Mustafa, na Adhana ilikuwa vivyo hivyo.

Wanatetea kwa dhati kwamba ile namna ya kuwaita waumini kwenye Swala haingeweza kuachwa kwenye ndoto au ruya za Mwarabu fulani.

Wanaendelea kusema kwamba kama Mtume (s.a.w.) ameweza kuwafundisha Waislamu jinsi ya kuchukua udhuu, na ni vipi, lini na nini cha kusema katika kila Swala, angeweza pia kuwafundisha jinsi na wakati gani wa kuwatahadharisha wengine kabla ya wakati wa kila Swala.

Kwa mujibu wa Hadith za Shia, yule Malaika aliyemfundisha Mtume wa Allah (s.w.t.) jinsi ya kuchukua udhuu kujiandaa kwa Swala, na jinsi ya kuswali, pia alimfundisha namna ya kuwaita wengine kwenye Swala.

Yathrib Yawa Madina

Hili jina “Yathrib” mara likawa halifai. Watu wakaanza kuuita mji huo “Madina-tun- Nabi,” – Mji wa Mtume. Kiasi muda ulivyopita, matumizi yakafanya ufupisho wa jina hili utwaliwe kirahisi kama “Madina” – “Mji,” na hivyo ndivyo jina la mji wa Mtume wa Uislamu lilivyobakia tangu hapo.

Makundi Ndani Ya Madina

Wakati Mtume (s.a.w.) na wale wahamiaji kutoka Makka walipofika Yathrib (sasa Madina), waliyakuta makabila matatu ya Kiyahudi, yaani, Quainuqa, Nadhir na Quraydha, na makabila mawili ya Kiarabu, yaani, Aus na Khazraj, yakiishi kwenye mji huo.

E.A.Belyaev:

“Idadi ya watu wa asili ya Madina ilijumlisha makabila yake matatu ya Kiyahudi, Quainuqa, Qurayza na Nadhir; na ya makabila mawili ya Kiarabu, Aus na Khazraj.
(Arabs, Islam and the Arab Caliphate in the Early Middle Ages. 1969)

Hao Wayahudi walikuwa wakulima, wachuuzi, wafanyabiashara, wakopesha-fedha, wamilikiardhi na wenye viwanda. Wamekuwa matajiri kupitia matumizi ya riba na walitawala ukiritimba wa viwanda vya zana za vita katika Arabia.

Haya makabila mawili ya Kiarabu ya Madina, Aus na Khazraj, yaliishi kwa kilimo. Kabla ya kuwasili kwa Mtume, walikuwa wamefungana kwenye vita dhidi yao wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya vizazi vitano.

Walipigana vita vyao vya mwisho miaka minne tu iliyopita, yaani, mnamo 618 A.D., na iliwaacha wachovu sana na walegevu.

Walikuwepo pia Wakristo wachache wanaoishi Madina. Hawakukubaliana na Mtume wa Uislamu kwa sababu aliikana ile imani ya Utatu, na akahubiri Tawhiid ya Muumba.

Kundi la nne ndani ya Madina lilikuwa lichomoze baadae kidogo, likiundwa na “wanafiki” au “waliokosa imani.” Wakati wa ujumbe wa Mtume (s.a.w.) huko Makka, walikuwepo Waislamu wengi ambao walikuwa wafiche imani yao ya kweli kwa kuhofia mateso.

Hapo Madina, hali iligeuka. Watu hawa (wanafiki) walikuwa Waislamu jina; usoni walitangaza Uislamu lakini hawakuwa wakweli. Walikuwa chanzo cha nguvu isiyodhihirika ya uchochezi, hujuma na uasi.

Mkataba Au Katiba Ya Madina

Raia wa Yathrib walimtambua Muhammad kama mtawala wao, na akawapa “Mkataba wa Uraia” ambao unaaminika kuwa ndio waraka wa kwanza ulioandikwa katika Uislamu (mbali na Qur’an). Mkataba wa asili kama ulivyohifadhiwa na Ibn Ishaq, una masharti arobaini na saba (47). Yafuatavyo ni yale ambayo ni muhimu zaidi kati ya hayo:

• Migogoro yote kati ya pande zozote mbili ndani ya Yathrib itapelekwa kwa Muhammad kwa uamuzi wake juu yake.

• Waislamu na Wayahudi watakuwa na haki sawa.

• Kila kundi ndani ya Yathrib litafuata imani yao, na hakuna kundi lolote litakaloingilia katika mambo ya kundi jingine lolote.

• Katika tukio la shambulio lolote la nje juu ya Yathrib, makundi yote, yaani, Waislamu na Wayahudi, yataulinda mji.

• Makundi yote yatajiepusha na kumwaga damu ndani ya mji.

• Waislamu hawatakwenda vitani dhidi ya Waislamu wengine kwa faida ya wasiokuwa Waislamu.

R.V.C. Bodley:

“Muhammad alitengeneza mkataba na Wayahudi ambamo, miongoni mwa mambo mengine, iliainishwa kwamba Wayahudi na Waislamu wasaidiane pamoja katika mambo yote yanayohusu mji huo.

Walikuwa wawe washirika dhidi ya maadui wote wa kawaida, na hili bila ya wajibu wa pande mbili kwa Uislamu au Uyahudi. Sharti muhimu la mkataba huu linasomeka kama ifuatavyo: Wayahudi wanaojiunga wenyewe kwenye umoja wetu watakuwa na haki sawa na watu wetu wenyewe kwenye msaada wetu na madaraka yetu mazuri. Wale Wayahudi wa matawi tofauti wanaoishi Yathrib wataunda pamoja na Waislamu dola moja ya pamoja. Watafuata dini yao kwa uhuru kama Waislamu. Watumishi na washirika wa Wayahudi watanufaika kwa usalama na uhuru huo huo. (The Messenger, the Life of Muhammad, New York, 1946)

Muhajirina Na Ansari

Muhammad alibadili majina ya makundi yale mawili ya Waislamu ambao sasa walikuwa wanaishi Madina. Aliwaita wale wakimbizi kutoka Makka “Muhajirin” (Wahamiaji); na akawaita wale wenyeji wa Yathrib ambao waliwakaribisha wao, “Ansar” (Wasaidizi). Makundi haya mawili yalijulikana kwa majina haya daima baadae.

Hali Ya Kiuchumi Hapo Madina

Utajiri wa Madina ulikuwa karibu wote umekusanyika katika mikono ya Mayahudi. Hao Waarabu (sasa Maansari) waliishi kwenye umasikini na dhiki ya kudumu. Sababu moja ya kwa nini walikuwa masikini sugu, ilikuwa ni viwango vikubwa vya riba walivyokuwa wakilipa kwa Mayahudi kwenye mikopo yao.

D.S. Margoliouth:

“Ingawa tunasikia majina ya mmoja au wawili wa matajiri wa Yathrib, wengi wao wanaonekana walikuwa masikini. Hapo Yathrib wakati wa Mtume, kulikuwa na vazi moja tu la harusi; mapambo yalikuwa yakiazimwa kutoka kwa Wayahudi. Umasikini huu ulikuwa hasa ukikuzwa na ukopeshaji-pesa wa Kiyahudi.” (Muhammad and the Rise of Islam, Londln, 1931)

Lakini kama Maansari walikuwa masikini, Muhajirin walikuwa masikini zaidi. Katika kukimbia kutoka Makka, waliacha kila kitu walichokuwa wakikimiliki, na walipokuja Yathrib kutafuta hifadhi, walikuwa hawana kitu. Kwa kifupi, hali yao iligeuka kuwa ya kukatisha tamaa.

Walikuwa wafanye kitu ili wapate kuishi. Lakini kwa vile hawakujua kitu kuhusu kilimo, cha maana walichoweza kufanya kilikuwa ni kufanya kazi kama vibarua wasio na ujuzi katika mashamba na bustani za Wayahudi na Ansari.

D.S. Margoliouth:

“Ilikuwa mwanzoni imepangwa kuwa wale Wakimbizi wawasaidie Wasaidizi (Ansar) katika kazi zao za nje; lakini kwa kutokujua chochote cha utunzaji wa mitende, waliweza tu kufanya zile kazi za kitumishi zaidi; hivyo wengine hasa walikata kuni na kuchota maji; wengine waliajiriwa kwenye kunywesha mitende, wakibeba mifuko ya ngozi migongoni mwao; na Ali, angalau wakati mmoja, alipokea tende kumi na sita kwa kujaza ndoo na maji, na kuzimwaga juu ya udongo kwa ajili ya kutengeneza matofali kwa kiwango cha tende moja kwa ndoo moja; ambacho kwa shida kilimpatia mlo aliokula pamoja na Mtume.”
(Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Kuwafungamanisha Muhajirina kwenye maisha ya kiuchumi ya Madina, lilikuwa ni tatizo gumu sana, na lilielemea ubunifu wote wa Mtume. Hakutaka mtu yoyote wa jamii ya Kiislamu, sana sana wale Muhajirina, awe mzigo kwa mtu mwingine yeyote, na alifanya kila lile aliloweza kufanya kupunguza utegemezi wao juu ya Ansari.

Udugu Wa Muhajirina Na Ansari

Moja ya shughuli za mwanzo za Mtume (s.a.w.) za kuwajenga upya wale Muhajirina wasio na makazi pale Madina, na kuwafungamanisha katika maisha ya kiuchumi na kijamii ya mji huo, ilikuwa ni kuwafanya wawe “ndugu” wa Ansari. Miezi michache baada ya kuwasili kwake hapo Madina, aliwaambia Muhajirina na Ansari kwamba walipaswa kuishi kama “ndugu” wa kila mmoja wao, na akawaunganisha wawili wawili kama ifuatavyo:

Muhajir ndugu ya Ansari
Ammar ibn Yasir Hudhayfa al-Yamani
Abu Bakr Siddiq Kharja bin Zayd
Umar bin Khattab Utba bin Malik
Uthman bin Affan Aus bin Thabit
Abu Dharr al-Ghiffari Al-Mundhir b. Amr
Mas’ab ibn Umayr Abu Ayyub
AbuUbaidah Aamer al-Jarrah Saad ibn Maadh
Zubayr ibn al-Awwam Salama bin Waqsh
Abdul Rahman bin Auf Saad ibn Rabi
Talha ibn Ubaidullah Ka’ab ibn Malik

Ali ibn Abi Talib pekee ndiye aliyeachwa bila ya “ndugu.” Alikuwa anastaajabu kwa nini wakati Mtume wa Allah (s.a.w.) alimshikilia mikononi mwake na akamwambia: “Wewe ni ndugu yangu katika dunia hii na katika akhera.”

Muhammad ibn Ishaq:

“Mtume (s.a.w.) mwenyewe alimshika Ali mkononi na kusema: “Huyu ni ndugu yangu.” Hivyo Mtume wa Allah (s.a.w.) Bwana wa waliotumwa, na kiongozi wa Wacha-Mungu, Mtume wa Mola wa mbingu na ardhi, asiye na mshirika wala asiyelingana na yoyote, na Ali ibn Abi Talib wakawa ndugu.”
(The Life of the Messenger of God)

Edward Gibbon:

“Baada ya safari ya hatari na ya haraka kandoni mwa mwambao wa bahari, Muhammad alisimama hapo Kuba, maili mbili kutoka mjini, na akafanya kuingia kwake kwa uwazi ndani ya Madina siku kumi na sita baada ya kukimbia kwake toka Makka.

Wafuasi wake shupavu sana walikusanyika kumzunguka yeye; na walio sawa, ingawa sifa mbali mbali za Waislamu zilitambulikana kwa majina ya Muhajirina na Ansari, wakimbizi wa Makka na wasaidizi wa Madina.

Kufutilia mbali mbegu za wivu, Muhammad kwa hekima na busara akawaunganisha wawili wawili wale wafuasi wake wakuu kwa haki na wajibu wa udugu; ambapo Ali alijikuta binafsi bila mwenza, na Mtume (s.a.w.) kwa upendo mwingi akatamka kwamba yeye atakuwa sahiba na ndugu wa yule kijana mtukufu.
(The Decline and Fall of the Roman Empire)

Muhammad Husein Haykal:

“Wazo la kwanza kumjia yeye (Muhammad) lilikuwa lile la kupanga upya safu za Waislamu ili kuunganisha umoja wao na kufuta kila uwezekano wa kuibuka tena kwa mgawanyiko na uhasama. Kwa kulitambua lengo hili, aliwataka Waislamu kusuhubiana wao kwa wao kwa ajili ya Allah (s.w.t.) na kujifunga wenyewe wawili wawili. Alieleza jinsi yeye na Ali ibn Abi Talib walivyokuwa ndugu. “ (The Life of Muhammad, 1935)

Muhammad, Allah (s.w.t.) ampe rehma na Ahlul-Bait wake, aliwafanya Muhajirina na Ansari kuwa “ndugu” wa kila mmoja wao. Lakini Ali, kama yeye mwenyewe, alikuwa Muhajir (mhamiaji), na bado yeye (Muhammad) alimchagua yeye kuwa ndugu yake. Kwa kufanya hivyo, alikuwa akibainisha kile cheo cha kipekee na hadhi maalum ya Ali katika

Uislamu. Ali, ingawa bado kijana, tayari alikuwa amemzidi kwa cheo kila mtu katika kutu- mikia Uislamu bidii ya wajibu kwa Allah (s.w.t.) na Mtume Wake. Alikipata cheo hiki kikubwa kwa kutumia uwezo wake na tabia.

Hii haikuwa, hata hivyo, mara ya kwanza ambapo Mtume wa Allah (s.a.w.) alimtangaza Ali kuwa ndugu yake. Mapema, wakati akiwa bado yuko Makka, aliwafanya maswahaba zake wakuu kuwa “ndugu” wa kila mmoja. Jozi hizo za “udugu” zilikuwa za Abu Bakr na Umar; Uthman bin Affan na Abdur Rahman bin Auf; Talha na Zubair; Hamza na Zayd bin Haritha; na Muhammad Mustafa ibn Abdullah na Ali ibn Abi Talib.

Imam Nuurdin Ali ibn Ibrahim al-Shafi’i amemnukuu Mtume wa Allah (s.a.w.) katika kitabu chake Siirat Halabia (juz. 2, uk.120) alisema: “Ali ni ndugu yangu katika dunia hii na vile vile katika dunia ya Akhera.”

Makadirio Ya Wajibu Wa Muhajirina Na Wa Ansari

Hawa Muhajirina walikwisha poteza mali walizokuwa nazo huko Makka, na wote waliingia Madina wakiwa mikono mitupu. Walitokana na vikundi vya wilaya mbili. Kikundi kimoja kilikuwa ni cha wale watu waliokuwa wachuuzi na wafanyabiashara kitaaluma, na walikuwa matajiri sana. Walipokwenda Madina, waliingia kwenye biashara, wakafanikiwa kwayo, na wakawa matajiri tena.

Kundi jingine lilitokana na “watawa” wa Kiislam. Walikuwa masikini huko Makka, na walipohamia Madina, bado walichagua kuwa masikini. Walibeua utajiri wa kidunia, na hawakuchukua mamlaka ya kiuchumi mikononi mwao wakati wowote ule.Wawakilishi wa kundi hili walikuwa watu kama Abu Dharr al-Ghiffari; Ammar ibn Yasir na Miqdad ibn al- Aswad. Allah (s.w.t.) aliwasifia katika Kitabu Chake kama ifuatavyo:

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِنَ اللَّهِ وَرِضْوَانًا وَيَنْصُرُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ {8}

“(Sehemu yake) wapewe mafakiri Muhajirina waliotolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Allah na radhi zake, na wanamsaidia Allah na Mtume Wake. Hao kwa hakika ndio wakweli.” (Sura ya 59 Aya ya 8)

Maansari waliwafanyia wema mhajirina kutoka Makka kuliko vile ndugu za hawa Muhajir wenyewe ambavyo wangeweza kuwafanyia. Waliwaweka katika nyumba zao wenyewe, wakawapa vifaa vya matumizi ya nyumbani; wakawafanya washirika katika kilimo, au wakawapa nusu ya ardhi yao. Wale Ansari waliokuwa kwenye biashara, wakawafanya hawa Muhajir washirika katika biashara. Historia haiwezi kuonyesha ukarimu unaolingana na wa hawa Ansari. Walikuwa ni “wenyeji” sio tu kwa wale Muhajirina wasiokuwa na makazi na mafukara peke yake bali pia na kwa Uislamu wenyewe, uliong’olewa Makka, ukaota mizizi mipya hapo Madina, ukachipua na mara ukawa na uwezo.

Hawa Ansari walikuwa wa lazima kwa ajili ya kudumu kihakika kwa Uislamu. Wapi ungekuwa Uislamu uwe, na wapi wangekuwepo Muhajirina kama Ansari wasingewapa hifadhi? Wakati uhasama na waabudu masanamu ulipoanza, walikuwa ni Ansari, na wala sio Muhajirina, waliochukua sehemu kubwa ya mapigano. Bila ya msaada mkubwa na imara ambao waliutoa kwa Mtume, vile vita vya Waislamu visingepiganwa, mbali na ushindi uliopatikana. Walikuwa pia wapokeaji wa sifa na utambulikanaji wa Mbingnii, kama tunavyosoma kwenye Aya ya Qur’an Tukufu ifuatayo:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِنْ قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَنْ يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {9}

“Lakini wale ambao, kabla yao, walikuwa na makazi (huko Madina) na walikuwa wameami- ni, wakaonyesha mapenzi yao kwa wale waliohamia kwao, wala hawaoni choyo vifuani mwao kwa vile walivyopewa (Muhajirina), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushiwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.” (Sura ya 59; Aya ya 9).

Hawa Muhajirin, mwanzoni, hawakuwa na jinsi ya kuwalipa hao Ansari kwa ukarimu na wema wao.

Lakini je waliwahi kutoa shukurani zao? Inaonekana kwamba ukiwaondoa Muhajirin wawili, hakuna aliyeshukuru. Hawa wawili wa kuwaondoa walikuwa ni Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) na Ali, mshika makamu wake. Walikiri deni lao la shukurani kwa Ansari kwa maneno na vitendo pia, na kamwe hawakuipoteza nafasi ya kufanya hivyo. Hata hivyo, wote Muhammad na Ali, kama walezi pekee wa maadili ya Uislamu, walitambua kwamba Uislamu umepata mahali pa usalama hapo Madina pamoja na Ansari. Hawa Ansari kwa hiyo, walishika nafasi maalum katika mioyo yao.

Muhajirin waliobakia, yaani, wale matajiri miongoni mwao, hawakushiriki katika wasi-wasi wa Muhammad na Ali kwa ajili ya Ansari. Wakati madaraka yalipoingia mikononi mwao, waliwasukuma wale Ansari nyuma, na wakawashusha wahusike na dhima ndogo ndogo tu. Mwanzoni, waliwapuuza kabisa Ansari. Lakini kupuuzwa hakukuwa kubaya sana kulinganishwa na kile kilichokuwa kiwafike katika nyakati za baadae.

(Kati ya kipindi kilichoshughulikiwa na Sira na kuhaririwa kwa kitabu chenyewe inatishia misiba mikubwa miwili ya Karbala, wakati Husein na wafuasi wake walipouawa katika mwaka wa 61 H.A., na kilio cha Madina mnamo mwaka 63 H.A. wakati Ansari kama elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume (s.a.w.) wasiopungua themanini walipouawa. Imenukuliwa katika - Introduction to the biography of the Prophet by Ibn Ishaq).

Muhajirin waliwaghilibu watetezi wa wapagani wa Makka - Banu Umayya – juu yao. Banu Umayya walikuwa maadui wakubwa wa Ansari. Kama ukarimu wa Ansari kwa Muhajirin hauna kifani katika historia, utomvu wa shukurani wa hawa Muhajirin kwa wahisani wao pia hauna kifani. Wakati Muhajirina walipokuja Madina, Maansari ndio waliokuwa mabwana wa Madina. Ilikuwa tu ni kwa uungwana wa Ansari kwamba Muhajirin waliweza kuingia na kuishi Madina. Lakini mara tu Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) na rafiki na mlezi wa Ansari, alipokufa, wakakoma kuwa mabwana nyumbani kwao wenyewe. Kifo chake kilikuwa ndio ishara ya mgeuko wa ghafla katika ustawi wao.