read

Mwaka Wa Pili Wa Hijiria

Msafara wa kwanza ambao Muhammad Mustafa aliuongoza yeye mwenyewe, ulikuwa ni ile Ghaz’wa (kampeni) ya Waddan. Alimteua Saad ibn Ubadah kama gavana wa Madina, na akachukua kikundi cha wafuasi wake kwenda Waddan, kijiji kati ya Madina na Makka. Msafara wa Maquraishi ulielezewa kwamba ulisimama pale. Lakini msafara huo uliondo- ka Waddan kabla ya kuwasili kwa Waislamu. Wao, kwa hiyo, walipumzika kwa siku chache na kisha wakarudi Madina.

Mnamo mwezi wa saba (Rajab) wa mwaka wa pili wa Hijiria, yaani, miezi kumi na tano baada ya kuhamia Makka, Mtume (s.a.w.) alituma watu saba chini ya uongozi wa binamu yake Abdullah ibn Jahash, kwenda Nakhla, oasis iliyoko Kusini, ambako walikuwa wachunguze mienendo ya msafara fulani wa Maquraishi.

Huko Nakhla, Abdullah aliuona msafara mdogo wa Maquraishi uliokuwa ukirejea Makka. Wenye msafara huo walikuwa ni Amr bin al-Hadhrami, Uthman bin Abdullah bin al-Mughira, na kaka yake, Naufal, na Hakam bin Kaisan. Abdullah akawashambulia na kuka- mata mizigo yao. Amr bin al-Hadhrami aliuawa; Uthman na Hakam wakatekwa; na Naufal akafanikiwa katika kutoroka.

Msafara huu unachukuliwa kwamba ni muhimu kwa sababu ilikuwa ni mara ya kwanza ambapo palikuwa na mapambano kati ya Waislamu na wapagani.

Ilikuwa pia ni mara ya kwanza ambapo palikuwa na umwagaji wa damu kati yao, na Waislamu walikamata ngawira kutoka kwao.

Abdullah bin Jahash na kundi lake wakarudi Madina pamoja na wafungwa wao na ngawira za vita. Kati ya wafungwa wawili hao, Hakam bin Kaisan alisilimu na akaishi Madina. Uthman bin Abdullah alikombolewa na ndugu zake, na akaenda Makka.

Kubadilishwa Kwa Qibla – February 11, A.D. 624.

Katika miezi kumi na sita ya kwanza baada ya Hajira, Qibla cha Waislamu kwa ajili ya Swala kilikuwa Jerusalem (walielekea Jerusalem wakati walipokuwa wakiswali). Kisha Mtume wa Allah (s.a.w.) akapokea wahy (ufunuo) ukimuamuru kubadilisha sehemu ya mwelekeo kutoka Jerusalem upande wa kaskazini kwenda Makka upande wa Kusini.

Dr. Montgomery Watt na John Christopher wametoa “sababu” zao juu ya kubadilika kwa muelekeo wa Qibla. Wanasema kwamba, hapo mwanzoni.

Mtume (s.a.w.) alitegemea kwamba kuelekea Jerusalem wakati wa kuswali, kungefanya nyoyo za Wayahudi wa Yathrib kumnyenyekea yeye, na wangemkubali kama Mjumbe wa Allah (s.a.w.).

Lakini aligundua, wanaendelea kusema kwamba, ingawa alielekea Jerusalem, wakati alipokuwa akiswali, wale Wayahudi walibakia wenye kushuku ukweli na uaminifu wake. Kisha wanaongeza kwamba baada ya miezi kumi na sita, Mtume (s.a.w.) alikata tamaa ya kuwaingiza Wayahudi wale kwenye Uislamu.

Kwa mujibu wa Dr. Montgomery Watt na John Christopher na baadhi ya mustashirki wa Magharibi, mara Mtume (s.a.w.) alipopoteza matumaini ya kuwapata wale Wayahudi kwenye Uislamu, aliondoa shauku juu yao, na akaamua kuweka dhamira yake kwa Waarabu. Huku kubadilika kwa Qibla, wanadai, kulikuwa ni tendo la hisia za kuwaridhisha Waarabu.

Hatujui kama Wayahudi hawa walikasirika ama kama Waarabu hawa walifurahishwa na kubadilika kwa Qibla. Sisi, kwa kweli, wala hatujui ni Waarabu wa wapi, kwa mujibu wa Dr.Watt, ambao Mtume (s.a.w.) alikuwa anajaribu kuwafurahisha – ni Waarabu wa Madina ama Waarabu wa Makka!

Waarabu wa Madina walikuwa wameukubali Uislamu na walimtii Mtume. Kwao wao kitu muhimu kilikuwa ni kumtii yeye Mtume (s.a.w.) kwa vile alikuwa ndiye mfasili wa ujumbe wa Allah (s.w.t) kwa wanadamu. Walielekea Makka walipokuwa wanaswali na hawakuuliza maswali yoyote ya kwa nini Qibla kilibadilishwa.

Waarabu wa Makka walikuwa bado ni waabudu masanamu. Na wao pia walisikia habari za kubadilika kwa Qibla kutoka Jerusalem kwenda Makka.

Lakini hakuna ushahidi wowote kwamba mmoja wao yeyote, kwa kuridhishwa na kufurahishwa na mabadiliko haya, alikuja Madina na kujitolea kuwa mwislamu. Walibakia walivyokuwa, ama Qibla kilikuwa Jerusalem au Makka, kwao haikuonyesha tofauti yoyote.

Maelezo ya Waislamu ni rahisi na yenye mantiki; Allah (s.w.t.) amemuamuru mja Wake, Muhammad, kubadili Qibla, na alitii. Hii amri ya kubadili Qibla ilitolewa ndani ya Aya ya 44 ya Sura ya pili ya Qur’an Tukufu.

Katika mwezi wa Shaban (mwezi wa nane), mwaka wa pili wa Hijiria, kufunga katika mwezi wa Ramadhani (mwezi wa tisa) kulifanywa ni amri ya lazima kwa Waislamu. Wao, kwa hiyo, walifunga katika mwezi uliofuata (yaani, mwezi wa Ramadhani). Mwisho wa mwezi wa kufunga, walitakiwa kutoa Zaka-ul-Fitr, Zaka maalum.

Katika mwaka huo huo, kodi nyingine, Zaka-ul-Mal, iliwekwa juu ya Waislamu. Kodi hii inakadiriwa katika kiwango cha asilimia 2.5 ya mali ya mwislamu. Katika nyakati za Mtume, kodi hii ilikuwa ikilipwa kwenye Bayt-ul-Mal au hazina ya umma, na ilitumika katika ustawi wa masikini na watu wagonjwa katika jamii.

Lakini kama hakuna Bayt-ul- Mal, Waislamu lazima wailipe kwa masikini wanaostahiki, wajane, mayatima na wale watu katika jamii ambao hawana uwezo wa kujikimu wenyewe.

Vita Vya Badr

Vita vya kuvunja moyo kati ya Maquraishi na Waislamu vingeshadidisha kwenye uhasama wa dhahiri wakati wowote. Abu Jahl alikuwa mmoja wa “wachuuzi” katika Makka ambaye aliyeendeleza vitavisivyokoma vya kisirisiri dhidi ya Muhammad Mustafa na wafuasi wake. Ushari wake wa kiuzalendo uliiweka Makka katika hali ya wasiwasi wa kudumu.

V.C.Bodley:

“Wazimu wa Abu Jahl juu ya Muhammad ulibakia katika kiwango cha kuchemka. Aliweka vikundi vya mashambulizi daima kwenye hali ya kuendelea kushambulia, vikishambulia makundi yoyote ya Waislamu yaliyo pembeni ambayo yangeweza kushambuliwa kwa ghafla. Alifanya uvamizi kwenye vitongoji vya Madina na kuharibu mazao na bustani. Alimfanya Muhammad aone kwamba hisia zake hazijabadilika, kwamba makusudio yake bado ni ya kimauaji.” (The Messenger, the Life of Mohammed, New York. 1946)

Mapema mwezi March, 624, habari zilipokelewa Madina kwamba msafara wa Maquraishi ulikuwa ukirejea Makka kutoka Syria. Msafara huo haukuwa umebeba bidhaa tu bali pia na silaha. Ilikadiriwa kuwa msafara huo ulitengeneza faida ya dinari 50,000 (vipande vya dhahabu).

Silaha hizo na utajiri mpya uliopatikana vilikuwa vitumike, kwa mujibu wa habari hizohizo, kuandaa jeshi la kupigana dhidi ya Waislamu. Msafara huo uliongozwa na Abu Sufyan, mkuu wa ukoo wa Banu Umayya.
Muhammad Mustafa aliamua kuuzuia msafara huo wa Makka. Alimteua Abu Lababa kama gavana wa Madina, na akaondoka mjini hapo na kikosi cha watu 313. Kati ya hawa, 80 walikuwa Muhajir, na 233 walikuwa Ansari. Mwisho wa safari yao ulikuwa ni Badr, kijiji Kusini-Magharibi ya Madina ambako wakitegemea kukutana na huo msafara wa Makka.

Waislamu hawakulijua hilo bado kwamba hawangeuona kamwe msafara wa Maquraishi, na kwamba watakuwa, badala yake, wawe kwenye mapambano, kwenye uwanja wa vita, na jeshi la Maquraishi.

Wakati huohuo, wapelelezi wa Makka walimjulisha Abu Sufyan kwamba kundi la Waislamu limeondoka Madina, na lilikuwa likienda kwa haraka kuelekea kwenye msafara wake. Mara tu alivyosikia hivyo, aliiacha ile njia ya msafara ya kawaida, akauongoza ule msafara wake kuelekea Magharibi kwenye pwani ya bahari ya Red Sea, na kisha akageukia upande wa Kusini kuelekea Makka, vile vile alituma ujumbe Makka kuomba msaada. Mjini Makka Abu Jahl alikuwa tayari akishughulika kuchochea ghadhabu za watu dhidi ya Waislamu, kufuatia tukio la Nakhla.

Aliitikia kwa shauku sana mwito wa Abu Sufyan, na akakiongoza nje ya Makka kikosi cha wapiganaji 1000 chenye wapanda farasi 100, dhidi ya Waislamu. Msururu wa ngamia 700 ulibeba vifaa kwa ajili ya vita na mahitaji mengineyo. Askari wa miguu walivaa ngao na deraya.

Muhammad Mustafa hakujua kwamba jeshi limeondoka Makka na lilikuwa likisonga mbele kuelekea Madina kuulinda msafara wa Maquraishi, na kuwapa changamoto Waislamu. Wakati Mtume (s.a.w.) alipowasili kwenye maeneo ya Badr, alimtuma Ali kuchunguza nchi iliyozunguka pale. Katika visima vya Badr, Ali aliwashitukiza baadhi ya wabeba maji. Katika majibu kwa maswali yake, walimwambia kwamba walikuwa wanabeba maji kwa ajili ya jeshi ambalo lilikuja kutoka Makka, na ambalo lilipiga kambi upande wa pili wa vile vilima vya karibu.

Ali aliwapeleka wale wabeba maji mbele ya Mtume wa Uislamu. Kutoka kwao alijua kwamba ule msafara wa Maquraishi tayari ulikuwa umekwisha toroka, na kwamba Waislamu wale, katika muda ule ule, walikabiliwa na jeshi la Makka.

Sir William Muir:

“Katika kufika kwenye maeneo karibu na Badr, Muhammad alimtuma Ali, pamoja na wengine wachache, kuchunguza ile ardhi iliyoinuka juu ya chemchemu. Hapo waliwashitukiza wabeba-maji watatu wa maadui, wakiwa karibu na kujaza mifuko yao ya ngozi ya kondoo. Mmoja akatorokea kwa Maquraishi; na wale wengine wawili wakakamatwa na kupelekwa kwenye jeshi la Waislamu. Kutoka kwao Muhammad alitambua ukaribu wa adui zake. Walikuwepo watu 950; mara tatu zaidi ya idadi ya watu wa jeshi la Waislamu. Walikuwa wamepanda juu ya ngamia 700 na farasi 100, hawa wapanda farasi wakiwa wamefunikwa na ngao za chuma. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Taarifa hii muhimu ya kuhusu maadui ilipokelewa kupitia Ali ibn Abi Talib. Kitendo chake, kwa upande mmoja, kiliwatahadharisha Waislamu; na kwa upande mwingine, kili- wapora maadui ile fursa ya kuwashitukiza. Waislamu walikuwa tayari kuwakabili.

Hata hivyo, kuwepo kwa adui hai, mshari na mwenye kutisha, badala ya msafara tajiri, ndani ya umbali wa jirani sana, kulibadilisha kabisa hali kamili kwa Waislamu, na iliwabidi wafanye tathmini mpya ya hatari na uwezekano wa mkabiliano naye. Hawakuwa wame jiandaa vema, na walikuwa na farasi wawili tu na ngamia 70 pamoja nao.Wengine wao walikuwa na panga lakini hawakuwa na ngao na wengine walikuwa na ngao bali hawakuwa na panga. Mtume (s.a.w.) ambaye alivitambua vikwazo hivi vya dhahiri, aliitisha baraza la vita, na akalifikisha suala hili mbele ya maswahaba zake kwa tafakari na uamuzi.

Mtu wa kwanza aliyesimama na kuzungumza juu ya wakati huu mgumu, alikuwa ni Miqdad. Alizungumza hisia na mawazo ya Muhajirina aliposema: “Ewe Mtume wa Allah, fanya kile ambacho Allah (s.w.t.) amekuamuru kufanya. Tuko pamoja nawe, sasa na wakati wote; na hatutakuambia kile Wana wa Israeli walichomwambia Musa: ‘Wewe na Mungu wako mwende mkapigane dhidi ya adui; na sisi, tutabaki hapa, na kukaa hapa.’ Hapana, hatutawaiga wale Wana wa Israeli. Tutakufuata wewe na kuzitii amri zako.”

Muhammad alitoa baraka zake kwa Miqdad. Lakini Miqdad alikuwa ni Muhajir, na Muhammad alikuwa na shauku ya kujua ni nini Ansari watafanya. Yeye aliona kwamba wale Ansari wangepigana katika kuilinda Madina yenyewe lakini wasingependa kupigana nje ya mji wao. Akihisi shauku yake, Saad ibn Muadh, mmoja wa viongozi wa Ansari, alisimama na kusema: “Tumeshuhudia kwamba wewe ni Mjumbe wa Allah.

Tumekupa kiapo chetu cha kukutii wewe. Popote utakapokwenda, tutakwenda pamoja nawe. Kama kutakuwa na kuonyeshana dhamira na washirikina, tutasimama imara katika kukuunga mkono kwetu. Kwa vita na kwa amani, tutakuwa daima waaminifu kwako.”

Matamshi Haya yenye msimamo wa wazi ya kuunga mkono ya kiongozi wa Ansari, yalimridhisha Mtume, na akaomba baraka za Allah (s.w.t.) juu yao wote. Yeye alijua kwamba sio vita vya Badr wala vita vyovyote vile vingeweza kupiganwa bila ya msaada wa Ansari. Hawa Ansari walikuwa, kwa hakika, wa muhimu sana kwa ajili ya mafanikio katika mapambano kati ya Uislamu na upagani, kama ilivyoonyeshwa kabla.

Kwa namna halisi na kwa kiasi, Waislamu walikuwa kwenye upungufu lakini kasoro hizi zilifutwa na hamasa zao. Walikuwa na imani na uongozi wa kimajaaliwa wa Muhammad. Na walikuwa wameungana. Muungano na umoja wao wa dhamira vilikuwa viwe chanzo cha nguvu kubwa kwao katika mapambano yajayo na jeshi la Makka.

Kwa kuhakikishiwa msaada wa Ansari, Muhammad Mustafa alichukua uamuzi wa kukubali changamoto ya Maquraishi. Yeye na askari wa kawaida wa jeshi la Madina wanaelekea kutambua wazi kwamba matokeo ya mapambano na adui siku itakayofuata, yatakuwa yamezidi katika athari zake.

Sir William Muir:

“Muhammad alikuwa anayafahamu kabisa mazingira hayo magumu. Majaaliwa ya Uislamu yalitegemea juu ya matokeo ya mapambano yanayokuja.” (The Life of Mohammed, London, 1877)

Mtume (s.a.w.) aliwaamuru Waislamu kukita mahema yao juu ya ardhi ya pale waliposimama. Lakini kijana mmoja wa Ansari alionyesha faida za kuchagua sehemu nyingine ya kupiga kambi ambapo ardhi ilikuwa juu zaidi na imara, na pia alipendekeza kwamba Waislamu wachukue milki ya visima vyote vya Badr. Mapendekezo yake yalikubalika moja kwa moja.

S. Margoliouth:

“Hubab mtoto wa al-Mundhir, mdogo kwa Mtume (s.a.w.) kwa miaka ishirini, baada ya kuhakikisha kwamba walikuwa kwenye vita vya kawaida, na kule kuwa na ujuzi maalum wa vile visima vilivyoko jirani, alimshauri Mtume (s.a.w.) kukaa mbele ya vyote isipokuwa kimoja, ambacho katika mzunguko wake wangefanya hifadhi, ili kuwa na ugawaji wa maji wa kuaminika kwa ajili ya vikosi hivyo; kule kuwa na nguvu hii ya asili yenye thamani baadae kutasaidia. Mtume (s.a.w.) aliyakubali mapendekezo yake na akaliweka jeshi lake chini ya usimamizi wa Hubab. (Mohammed and the Rise of Islam, London, 1931)

Matukio mara yakadhihirisha kwamba mapendekezo ya Hubab yalikuwa mazuri sana, na kukubaliwa kwake na Mtume (s.a.w.) kuliwapa Waislamu faida kubwa ya kimbinu juu ya maadui.

Vita hivi vya Badr vilipiganwa katika mwaka wa pili wa Hijiria, kwenye tarehe 17 ya mwezi wa Ramadhani, mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislam (March 15, A.D.624). Lile jeshi la Makka lilitoka nje ya kambi yao mapema asubuhi kukutana na Waislamu. Majeshi haya mawili yakajipanga katika mpango wa kivita.

Mtume (s.a.w.) akachukua upinde mkononi mwake na akatembea kati ya mistari iliyopanga safu za Waislamu. Tendo lake la mwisho kabla ya vita kuanza, lillikuwa ni kumuomba Allah (s.w.t.) kutoa ushindi kwa waja Wake wanyenyekevu.

Vita vikaanza katika desturi ya Kiarabu ya taratibu za vita ambamo shujaa wa upande mmoja alipanda au kutoka nje ya msitari, na kuwapa changamoto mashujaa wa adui kuku- tana naye katika pambano la mtu mmoja mmoja.

Hii ilimpa fursa ya kujipatia sifa binafsi kwa kuonyesha ujasiri wake mwenyewe, nguvu zake na ujuzi katika upanda farasi. Majeshi hayo mawili yalifanya kama namna ya kibwagizo kwa ajili ya mapambano kati ya mashujaa wachache wanaojigamba. Baada ya Haya mapambano ya awali, ilikuwa ni desturi kwa majeshi hayo mawili kushambuliana, na kuingia kwenye mapigano ya mkono kwa mkono.

Kutoka upande wa Makka, wapiganaji watatu, Utba mtoto wa Rabia; Shaiba, kaka yake; na Walid, mtoto wake; walitoka kwenye nafasi ya wazi kati ya majeshi hayo mawili, na wakawapa changamoto Waislamu. Changamoto yao ilichukuliwa na Hamza, ami yake Muhammad na Ali; Ubaida ibn al-Harith, binamu yake Muhammad na Ali; na Ali ibn Abi Talib.

Walid ibn Utba alikuwa mmoja wa wapiganaji wakali sana wa Makka. Ali alijikuta akikabiliana naye. Walikuwa ndio jozi ya vijana zaidi, na walikuwa wa kwanza kuingia kwenye kupigana.

Zile jozi zingine mbili zikapumzika, kuwaangalia wale wapiganaji vijana waw- ili wakipambana. Vijana hawa wawili walitupiana mapigo machache, na kisha Ali akapiga pigo lake ambalo lilimuua Walid.

Mara baada ya Walid kuuawa, wale wapiganaji wengine nao wakashambuliana. Hamza akamuua Utba. Lakini Ubaida alijeruhiwa vibaya sana na Shaiba. Wakati Ali alipomuona Ubaida anaanguka chini, alimshambulia Shaiba, na akamuua pia. Kwa maadui zao wawili kufa, na hakuna mtu uwanjani, Ali na Hamza walimbeba Ubaida kumrudisha kwenye safu za Waislamu ambako alikufa kwa sababu ya majeraha yake. Alikuwa mwislamu wa kwanza kuuawa kwenye uwanja wa mapambano.

Sir William Muir:

“Ndugu hawa wawili, Shaiba na Utba, na Walid, mtoto wa Utba, walisonga mbele kwenye nafasi kati ya majeshi hayo, na wakawataka shari mashujaa watatu kutoka kwenye jeshi la Muhammad kupambana nao mmoja mmoja. Muhammad aki- wageukia jamaa zake, akasema: “Enyi wana wa Hashim! Amkeni na mpigane, kwa mujibu wa haki yenu.” Ndipo Hamza, Ubaida na Ali, wale ami na binamuze Mtume, wakatoka mbele.

Hamza alivaa unyoya wa mbuni kifuani mwake, na nyoya jeupe lilitambulisha kofia ya vita ya Ali. Kisha Utba akamwita mwanae, Walid, “Simama na upigane.” Hivyo Walid alitoka mbele na Ali akatoka dhidi yake. Walikuwa ndio vijana zaidi ya hao sita. Mapambano yalikuwa mafupi; Walid alianguka akiwa amejeruhiwa vibaya kwa upanga wa Ali. (The Life of Mohammed, London, 1877)

Sir John Glubb:

“Machifu watatu wa Makka, Utba, Shaiba na Walid, mtoto wa Utba, walijitokeza mbele ya msitari wa Maquraishi na kuwataka vita Waislamu watatu kukutana nao katika pambano la mmoja mmoja. Muhammad akiwageukia Muhajir aliita: “Enyi Bani Hashim, simameni na mpigane.” Watu watatu wakiwa wamefunikwa na ngao za chuma walitoka kwenye safu za Waislamu. Walikuwa ni Hamza, ami yake Mtume; Ali ibn Abi Talib, binamu yake, na mfuasi wa kwanza wa kiume; na Ubaida ibn Harith.

Ile jozi ya vijana zaidi ilishambuliana mwanzo, Ali akitoka mbele kukutana na Walid. Baada ya muda kidogo wa kucheza na panga, Walid aliangushwa na upanga wa adui yake mwislamu. Kisha Hamza akamshambulia Utba na akamkata na kumuangusha chini. Ubaida ibn Harith, shujaa wa tatu wa Kiislam, alipata jeraha baya sana kutoka kwa Shaiba. Ali na Hamza haraka sana wakamuua Shaiba, wakimbeba Utba kwenda kufia kwenye safu za Waislamu. (The Great Arab Conquests, 1963)

Badr ilikuwa ndiyo pambano la kwanza, katika uwanja wa vita, kati ya Uislamu na Wapagani. Ilianzishwa upande wa Uislamu, na Ali ibn Abi Talib, simba kijana, na ushindi wake ulikuwa ni ishara ya mafanikio ya Uislamu. Vita nyingine zote za Kiislam zilifuata mkondo huohuo; Ali alikuwa ndiye mshindi katika kila moja yao.

Maquraishi walituma mashujaa watatu dhidi ya Waislamu, na wote watatu waliuawa. Abu Jahl, kwa hiyo, hakuwa na shauku ya kuchukua majaribio zaidi na Ali na Hamza, na akaa- muru majeshi yake kusonga mbele. Watu wa Makka waliwashambulia Waislamu lakini hawakuweza kuvunja mipangilio yao. Walishambulia tena na tena lakini safu za Waislamu zilibakia imara chini ya ukamanda wa Ali na Hamza. Watu wa Makka walikuwa wakijikusanya kwa ajili ya mashambulizi mapya wakati Muhammad alipowaashiria Waislamu kusonga mbele. Ali na Hamza waliongoza mapambano ya kujibu shambulizi, na wote walileta mauji na fadhaa kwenye kundi kubwa la safu za adui.

Wengi wa viongozi na maafisa wa Makka waliuawa, miongoni mwao Abu Jahl mwenyewe. Baada ya kifo chake, waabudu-masanamu hao hawakuweza kujikusanya, na walianza kurudi nyuma. Waislamu walishikilia fursa yao, na kule kurudi nyuma kwa watu wa Makka mara kukawa ni msambaratiko. Uislamu umepata ushindi wake wa kwanza na wa muhimu sana!

S. Margoliouth:

“Kwa hakika inaonekana kwamba kushinda kwa pambano hili muhimu kulikuwa katika kustahili kukubwa kwa ushujaa wa Ali na Hamza. Mtukufu Mtume (s.a.w.) anasemekana kutoa sifa maalum kwa ujasiri wa Simak ibn Kharashah; Sahl ibn Hunaif; al-Harith ibn al-Simmah; na Kais ibn al-Rabi; wote wakiwa ni watu wa Madina. (Mohammed and the Rise of Islam, London, 1931)

Tor Andre:

“Kufikia mchana vita vilikuwa vimekwisha. Watu arobaini na tisa wa adui walikuwa wameanguka na Ali aliuwa watu ishirini na wawili, ama peke yake au pamoja na msaada wa wengine. Idadi kama hiyo hiyo walitekwa. Waumini walipoteza watu kumi na wanne katika uwanja wa mapambano.”
(Mohammad, the Man and his Faith, 1960)

Kama ilivyoonyeshwa hapo juu, Badr ndio vita muhimu sana katika historia nzima ya Uislamu, na moja kati ya zile maarufu katika historia ya ulimwengu. Ushindi ulihakikisha kuwepo kwa Uislamu, na uhai wa dhahiri wa jumuiya ya Waislamu ya Madina ambayo mpaka sasa imetokea, kwa vyovyote, kuwa ya hatari.

A.Nicholson:

“Lakini umuhimu wa mafanikio ya Muhammad (katika vita vya Badr) hayawezi kupimwa kwa uharibifu wa vitu aliousababisha (juu ya wapagani wa Makka). Tukitazama mambo ya maana sana yaliyohusika, ni lazima tukubali kwamba Badr, kama masafa marefu, ni moja ya vita vikubwa na vya kukumbukwa sana katika historia yote. (A Literary History of the Arabs, 1969)

Ali Ibn Abi Talib Na Vita Vya Badr

Msanifu wa Ushindi wa Waislamu huko Badr, bila ya shaka yoyote, alikuwa ni Ali ibn Abi Talib. M. Shibili, yule mwanahistoria wa Kihindi aliyeandika vitabu vya kutegemewa vya wasifu kwa Ki-Urdu vya Umar bin Khattab na vya Mtume wa Uislamu, anasema katika kitabu chake Life of the Apostle, kwamba shujaa wa vita vya Badr ni Ali ibn Abi Talib.

F.E.Peters:

“Badr ilikuwa ni ushindi kwa Waislamu, kwa jumla kama ilivyokuwa haikutegemewa; Waislamu walipoteza watu kumi na wanne na Maquraishi watu 50 hadi 70, pamoja na kiongozi wao, Abu Jahl. Ulikuwa ni ushindi mkubwa sana wa kisaikolojia na kulikuwa na wingi wa ngawira kwa ajili ya wale Muhajir waliodhikika kiuchumi. Hili halikuwa shambulio la hivihivi tu, hata hivyo. Lilipambanisha Waislamu dhidi ya wasio-Waislamu katika Vita Tukufu (Jihad), na akina baba dhidi ya watoto wao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Majeruhi wa Maquraishi walikuwa wengi mno, na kwa vile wengi wao walitokana miongoni mwa machifu wao, uongozi hapo Makka ulidhoofishwa kabisa daima. (Allah’s Commonwealth, 1973)

Uongozi wa washirikana wa Makka kwa hakika ulidhoofishwa daima hapo Badr. Shujaa aliyehusika na hili alikuwa ni Ali. Yeye peke yake aliwauwa watu wa Makka 22, na kumi na wawili wao wakiwa ni wale watu maarufu wa ukoo wa Bani Umayya. Jeshi la Waislamu lililobakia liliuwa wapagani wengine 27.
Miongoni mwa ngawira za vita vya Badr ulikuwepo upanga ambao ulikuwa uje kuwa ndio upanga maarufu kabisa katika historia nzima ya Uislamu. Jina lake lilikuwa ni Dhul-Fiqar.

Washington Irving:

“Miongoni mwa ngawira za vita vya Badr ulikuwa ni upanga maarufu wenye hali ya kupendeza uitwao Dhul-Fiqar. Muhammad daima baadae aliushika akiwa vitani, na mkwe wake, Ali aliurithi baada ya kifo chake.” (The Life of Muhammad)

Abdullah Yusuf Ali, yule mtarjuma na mfasiri wa Qur’an Tukufu, anasema kwamba vile vita vya Badr vinaitwa Furqan katika elimu ya Kiislam, kwa sababu ilikuwa jaribio la kwanza la nguvu kwa njia ya vita, katika Uislamu, kati ya nguvu za wema na uovu. Furqan ina maana ya kibainishi kati ya ukweli na uongo; uamuzi kati ya nguvu za Imani na Ukafiri. Vita vya Badr vinaitwa kwa jina hili.

Wafungwa Wa Kivita

Waislamu walikamata wafungwa wa kivita hamsini. Waliletwa mbele ya Mtume (s.a.w.) ambaye alikuwa aamue wafanyiwe nini. Alishauriana na maswahaba zake katika jambo hilo. Umar allimshauri awauwe wote, lakini Abu Bakr akamshauri kuwaachia huru kwa fidia. Mtume (s.a.w.) akaukubali ushauri wa Abu Bakr.

Kwa vile hapakuwa na nyumba ya kizuizi hapo Madina, Mtume (s.a.w.) aliwagawanya wale wafungwa miongoni mwa familia za Waislamu. Familia hizi ziliwatendea wafungwa wao kama vile walikuwa wageni. Baadhi yao walilisha chakula chao wenyewe kwa “wageni” wao na wenyewe wakakaa na njaa. Kwa kweli waliwafedhehesha wafungwa wao kwa mashaka yao juu ya ustawi wao.

Wale wafungwa matajiri waliachiliwa kwa fidia. Wale wafungwa ambao hawakuweza kulipa fidia lakini waliweza kusoma na kuandika, walitakiwa kuzifundisha sanaa hizo kwa watoto wa Kiislam, na walipofanya hivyo, pia na wao waliachiliwa. Wale wafungwa waliokuwa mafukara sana, waliachiliwa bila ya fidia yoyote.

Matokeo Ya Vita Vya Badr

Ushindi wa Badr uliwapa Waislamu heshima kubwa sana. Lile tishio kwa usalama wa Madina liligeuzwa, na Muhammad Mustafa aliweza sasa kuweka misingi ya Ufalme wa kwanza na wa mwisho wa Mbingnii hapa Duniani.

S. Margoliouth:

‘Hakuna tukio katika historia ya Uislamu lililokuwa na umuhimu zaidi kuliko vita hii (ya Badr); Qur’an inaviita sawa kabisa – Siku ya Ukombozi, siku ambayo kabla yake Waislamu walikuwa wanyonge, baada yake wakawa wenye nguvu. Utajiri, umaarufu, heshima, mamlaka, vyote vilipatikana au kwa hali yoyote vililetwa karibu na hiyo Siku ya Ukombozi.”(Mohammed and the Rise of Islam, London, 1931)

Tokeo moja la kusikitikia la vita vya Badr, hata hivyo, lilikuwa kwamba ushindi wa Uislamu uliwasha mioto mipya na mikali zaidi ya chuki na uhasama katika vifua vya Banu Umayya dhidi ya Muhammad Mustafa na Ali ibn Abi Talib. Chuki zao na wivu juu ya Bani Hashim ilidumu vizazi vingi.

Lakini baada ya vita vya Badr, uhasama wao ulielekezwa kwa Ali na kwa watoto wa Muhammad Mustafa.

Kama kwa Waislamu, Ali alikuwa ndio alama ya ushindi wa Uislamu, kwa Banu Umayya, alikuwa ni alama ya kuangamia kwa ushirikina wao na heshima zao. Kwa hiyo, wao, vizazi vyao vilivyofuata, na marafiki zao na wanao waunga mkono, kamwe hawakumsamehe Ali kwa jukumu alilotekeleza hapo nyuma, wakati na baada ya vita vya Badr.

Chuki yao inaeleweka. Alikuwa ni Ali, na ni Ali peke yake ambaye alishambulia, sio tu pale Badr, bali katika kila pambano, kwa mashambulizi makubwa, ile nguvu iliyolingana sawa na kumakinika ya upagani, na akaiangamiza.