read

Ndoa Ya Fatima Zahra Na Ali Ibn Abi Talib

Allah swt. aliwapa ushindi Waislamu katika vita vya badr katika mwaka wa 2 wa Hijiria. Miezi miwili baada ya vita hivyo, Fatima Zahra, binti yake Muhammad Mustafa, na Ali, mwana wa Abi Talib walifunga ndoa.

Fatima Zahra alikuwa na miaka mitano tu wakati mama yake – Khadija (R.a.), alipofariki, na kuanzia hapo na kuendelea, baba yake, Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) alichukua wajibu wa kazi za mama pia kwa ajili yake.

Kifo cha mama yake kilileta pengo katika maisha yake lakini baba yake alilijaza kwa upendo na huruma.

Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliweka uangalifu wa hali ya juu kwenye elimu na malezi ya binti yake. Kama alikuwa ndiye mfano bora kwa watu wote, binti yake alikuwa awe mfano bora kwa wanawake wote, na alikuwa hivyo. Alimfanya yeye kuwa mfano bora wa uwanauke katika Uislamu. Alikuwa ni mfano halisi wa ibada na utii kwa Muumba, na alikuwa ni mfano halisi wa usafi wa ki-ungu na utakatifu. Katika tabia na hulka, alikuwa na mfanano unaovutia sana kwa baba yake. Fatima, binti huyu, alikuwa ni picha ya Muhammad, baba yake.

Kwa kufanya utii na ibada kwa Allah (s.w.t.) Fatima Zahra alipanda kufikia cheo kikubwa mbele ya Allah (s.w.t.) kama ilivyoshuhudiwa na Qur’an Tukufu. Allah (s.w.t.) alimpa utukufu mkubwa sana juu yake, na Mtume wa Uislamu (s.a.w.), kwa upande wake, alim- wonyesha kiwango cha heshima ya juu sana, moja ambayo hakuionyesha kwa mwanaume au mwanamke mwingine yeyote yule katika wakati wowote wa maisha yake.

Wakati Fatima alipokuwa, maswahaba wawili wazee – wa kwanza na kisha baadae mwingine – walimuomba baba yake wamchumbie. Lakini aligeukia pembeni kwa kuchukia, na akasema:

“Hili suala la ndoa ya Fatima, binti yangu, liko mikononi mwa Allah (s.w.t.) Mwenyewe, na Yeye pekee ndiye atamchagulia yeye mchumba”.

Allah (s.w.t.) alifanya uchaguzi Wake kama ipasavyo. Alimchagua mja Wake, Ali ibn Abi Talib, kuwa ndiye mchumba wa binti ya mja Wake mpendwa mno, Muhammad Mustafa. Alipenda kuwaona Fatima binti Muhammad na Ali ibn Abi Talib wakioana.

Miezi miwili baada ya vita vya Badr, yaani, katika mwezi wa Dhilqa’da (mwezi wa 11) wa mwaka wa 2 H.A., Ali alikwenda kwa Muhammad Mustafa, na akasema: “Ewe Mtume wa Allah, umenilea mimi kama mwanao mwenyewe. Ulinijaza na zawadi zako, ukarimu wako na wema wako. Ninawiwa nawe kila kitu katika maisha yangu. Sasa ninaomba wema mmoja zaidi kutoka kwako.”

Mtume (s.a.w.) alielewa nini Ali alichokuwa akijaribu kukisema. Uso wake ulichangamka kwa tabasamu pana, na alimtaka Ali asubiri kwa muda kidogo mpaka apate majibu ya binti yake.

Aliingia ndani, akamwambia Fatima kwamba Ali alikuwa anaomba uchumba kwake, na akamuuliza ni lipi jibu lake.

Akabakia kimya. Yeye Muhammad akatafsiri kimya chake kama idhini yake, akarudi kwa Ali, akamjulisha kwamba ombi lake limekubaliwa, na akamwambia afanye matayarisho ya harusi.

Katika siku ya mwisho ya Dhilqa’ada, Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliwakaribisha Muhajirina na Ansari, kuhudhuri karamu, katika tukio la kuolewa kwa binti yake. Alikuwa ndiye mwenyeji wao. Wakati wageni wote walipofika, na wakawa wamekwishakaa, alichukua, kwa mara nyingine tena, idhini ya kisheria ya binti yake kwa ajili ya ndoa na Ali ibn Abi Talib.

Muhammad Mustafa alimtukuza Allah (s.w.t.) na akamshukuru Yeye kwa ajili ya rehema Zake zote. Yeye kisha akasoma hotuba ya ndoa; akawatangaza Ali na Fatima kama mume na mke, na akaomba baraka za Allah (s.w.t.) ziwe juu yao wote. Wageni wote wakampongeza Mtume (s.a.w.) kwa tukio hili lenye baraka tele. Baada ya sherehe hii, wageni wale walikula karamu ya nyama ya kondoo, mkate, maji ya tende na maziwa.
Siku chache baadae, yaani, katika Dhil-Hajj (mwezi wa 12 wa kalenda ya Kiislam), Fatima Zahra ilibidi aiage nyumba yake ya kuzaliwa ili aweze kwenda kwenye nyumba ya mumewe. Baba yake alimsaidia katika kumpakia kwenye ngamiajike wake (Muhammad).

Madina ilivuma kwa sauti za Allah-u-Akbar. Salman Muajemi alishikilia hatamu za ngamiajike huyo, na akatembea mbele yake, huku akisoma Qur’an Tukufu. Mtume wa Allah (s.a.w.) alitembea upande mmoja wa ngamia-jike huyo, na Hamza, Simba wa Mungu, upande mwingine.

Vijana wote wapanda farasi wa Bani Hashim walipanda kama wasindikizaji wa Bibi-harusi huyo, pamoja na panga zinazomeremeta zikiwa zimenyanyuliwa juu kabisa. Nyuma yao walikuwa ni wanawake Muhajira na Ansari, na nyuma yao hawa wakaja Muhajirina na Ansari wenyewe. Walikuwa wakisoma qaswida kutoka kwenye Qur’an Tukufu kumtukuza Allah (s.w.t.) Usomaji huo wa qaswida uliwekwa vituo vya mara kwa mara na mrindimo wa sauti za Allah -u-Akbar.

Maandamano haya ya kitukufu yaliuzunguuka Msikiti Mkubwa wa Madina, na kisha yakaishia kwenye ukomo wake – nyumba ya Bwana-harusi – Ali ibn Abi Talib. Muhammad Mustafa akamsaidia binti yake kushuka toka kwenye ngamiajike. Akamshika mkono wake, na kwa ishara akauweka kwenye mkono wa mumewe, na kisha, akisimama kwenye kizingiti cha nyumba hiyo, akasoma du’a ifuatayo:

“Ewe Allah (s.w.t.)! Ninawaweka Ali na Fatima, waja wako wanyenyekevu, kwenye ulinzi wako. Uwe Wewe ndio Mlinzi wao. Wabariki hawa. Kuwa radhi nao, na uwape neema zako zisizo na mipaka, huruma, na fadhila Zako bora juu yao. Uifanye ndoa yao kuwa yenye matunda, na uwafanye wote imara katika upendo Wako, na ibada Zako.”

Ilikuwa kwa kweli ni siku ya furaha katika maisha ya Muhammad Mustafa. Lakini ni vipi ambavyo angependa kwamba mkewe mpendwa, Khadija, angekuwa pamoja naye ili wote kwa pamoja wakashuhudia ndoa ya binti yao.

Siku chache baadae, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikwenda kwa binti yake, na akamuuliza kama alimuonaje mume wake. Binti akasema kwamba alimuona ni mwenza bora katika kufanya ibada na utii kwa Allah (s.w.t.) Baadae, alimuuliza Ali alimuona vipi mke wake, na akasema alimuona ni mwenza bora katika kumuabudu Muumba. Nyakati nzuri kabisa za maisha kwa wote mume na mke zilikuwa zile walipokuwa wamekwenda Mbele ya Mola wao, na wakazama katika kumuabudu Yeye.

Kati ya Ali na Fatima Zahrah, kulikuwa na utambulisho kamili wa manufaa. Wote walilele- wa na kufundishwa na Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) na Khadija-tul-Kubra. Wote kwa hiyo, walikuwa na ukamilifu wa wazazi wao. Wote waliweka ibada kwa Allah (s.w.t.) mbele ya kitu kingine chochote kile. Hapakuwepo na nafasi kabisa ya kutoelewana kati yao. Mawazo yao, maneno na matendo yao, yote “yalizoeshwa” na Qur’an Tukufu. Ndoa yao kwa hiyo, ilikuwa timilifu tu na ya furaha tu kama ile ndoa ya Muhammad na Khadija ilivyokuwa.

Kama ilivyoelezwa kabla, furaha kuu ya Fatima ilikuwa ni kuwa na subira juu ya Allah (s.w.t.) Alitumia muda wake mwingi katika Swala. Furaha yake kuu ya pili ilikuwa ni kutekeleza wajibu wake kwa familia yake. Allah (s.w.t.) aliridhia kumpa watoto wanne – kwanza wavulana wawili na kisha wasichana wawili. Alisaga nafaka katika kinu alichopewa na baba yake kama sehemu ya mahari yake, na akawaokea mikate.

Kusaga nafaka siku hadi siku kulisababisha malengelenge kutoka kwenye mikono yake lakini hakulalamika kamwe kwa mume wake au kwa baba yake juu ya malengelenge hayo, na alifanya kazi zake za nyumbani kwa furaha kabisa.

Hizi kazi za nyumbani zingeweza kuwa kama za kushurutisha sana kwa Fatima Zaharah lakini alipata furaha na nguvu katika kumkumbuka Allah (s.w.t.) Kitabu cha Allah (s.w.t.) kilikuwa ndio rafiki yake wa kudumu. Alisahau uchovu wa kazi vile alivyokuwa akisoma vifungu kutoka kwenye kitabu hicho.

Na alipowalaza watoto wake katika kitanda chao, alisoma tena baadhi ya vifungu kutoka kwenye kitabu hicho hicho kama “nyimbo za kibembelezo” kwa ajili yao. Walikua huku wakiisikia Qur’an Tukufu toka utotoni mwao.
Aliligandisha Neno la Allah (s.w.t.) juu ya mioyo yao michanga. Kwa kupitia “mfyonzo” kama huu, Qur’an na watoto wa Fatima Zahrah vikawa havitenganishiki kwa wakati wote.

Katika mwaka huo huo, yaani, mwaka wa 2 H.A., Sala za hadhara kwenye sikukuu mbili kwa ajili ya Waislamu, yaani, Idd-el-Fitr na Idd-el-Udh-ha., zilifanywa kuwa sunnah (zenye kustahili) juu yao.