read

Neno La Mchapishaji Usahihi Wa Historia Ya Uislamu

Hii ni historia ya vuguvugu la Uislamu ambalo lilianzishwa na Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) mnamo mwaka 610 A.D. huko Makka, na kuendelea alipohamia Madina mpaka alipofarika. Inahusisha kipindi cha miaka tisini kuanzia 570 A.D. wakati yeye Muhammad alipozaliwa huko Makka, hadi mwaka 661 wakati mrithi wake, Ali ibn Abi Talib, alipouawa huko mjini Kufah.

Historia zisizo na idadi zimeandikwa huko nyuma na zitaandikwa wakati ujao. Maendeleo ya kuvutia ya Uislamu katika nyanja ya ulinganiaji katika nyakati zetu wenyewe; kufufuka upya kwa mataifa ya Kiislamu baada ya karne nyingi za usingizi mzito; kujidukiza kwa mafuta kama wakala mpya katika siasa za kidunia katika karne hii; bali juu ya yote na hivi karibuni kabisa, yale mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ndani ya Iran, yote haya yanakuwa, kote Mashariki na Magharibi, kama vichocheo vya shauku mpya katika Uislamu.

Mapinduzi ndani ya Iran yamechokonoa mlipuko wa dunia nzima wa mvuto kati- ka Uislamu, na vitabu vingi vipya vinaandikwa juu ya somo hilo - na wote, Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Hili tena ni jaribio letu kubwa la kutoa kitabu kikubwa kinachohusu historia ya Uislamu na waislamu kwa luhga ya Kiswahili. Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.

Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya 'Al-Itrah Foundation' imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Al-Akh Ramadhani Kanju Shemahimbo kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu katika dini.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam.