read

Ni Nani Aliyeandika Historia Ya Uislam Na Vipi?

Historia, imesemekana, ni propaganda (uenezaji habari) wa kundi la upande wa washindi. Hii ina maana kwamba katika kila mgogoro, yule mshindi anaweza kuichezea historia kiasi inavyomridhisha yeye, na hakuna chochote ambacho yule aliyeshindwa anaweza kukifanya juu ya hilo.

Ule upande ulioshinda unaweza kuzua Hadith na kuitangaza kama ukweli mtupu bila ya hofu ya kupingwa na mtu yoyote. Hauna tu ule uwezo wa kuzua Hadith yake wenyewe; unayo pia nguvu ya kuipachika Hadith ya kundi linalowapinga.
M. Shibli, mkuu wa wanahistoria kiislamu wa Kisunni wa India, anaandika katika kitabu chake maarufu cha wasifu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), Sira-tun-Nabi, Juz. I, chapa ya 4, kilichochapishwa na Maarif Printing Press, Azamgarh, U.P., India, mwaka 1976:

“Miongoni mwa zile nguvu zote za kutoka nje ambazo zinadhuru na kuathiri uan- dishi wa historia, hakuna ambayo ina uwezo zaidi kuliko ya serikali. Lakini itakuwa siku zote ni chanzo cha fahari kwa Waislam kwamba kalamu yao kamwe haikukandamizwa na upanga. Kazi juu ya utungaji na ukusanyaji wa Hadith ilianzishwa wakati wa enzi ya Bani Umayya.

Kwa miaka 90 mizima, kutoka Sindi huko India (India-Pakistan) mpaka Asia Ndogo na Andalusia huko Hispania, Ali na watoto wa Fatima walikuwa wakilaaniwa kutoka kila mimbari ya Msikiti baada ya kila hotuba ya Ijumaa. Maelfu na maelfu ya Hadith zenye kumtukuza Mu’awiyah zilitengenezwa, na zikaingizwa kwenye mzunguko.

Katika enzi ya Bani Abbasi, Hadith zilivumbuliwa zenye kutabiri kuzaliwa na ubora wa kila khalifa wa Bani Abbasi kwa jina lake. Lakini ni yapi yalikuwa matokeo ya juhudi hizi kubwa? Wasimulizi (wakusanyaji wa kauli za Mtume) walitangaza hadharani kwa wakati huo huo (katika kipindi cha ukhalifa wa Bani Umayya na Bani Abbasi) kwamba Hadith hizi zilikuwa za uongo, na wakazikataa. Leo hii, tunajivunia kusema kwamba elimu ya Hadith imeepukana na matusi yote na uchafu wote ule.”

Takriban, lakini sio kabisa!

Kwa upande wa Hadith zisizo na idadi, jaribio la kuondoa taarifa potofu kutoka kwenye maelezo ya Hadith, au kuisahihisha, halikuufikia kamwe ule uwongo wa asili.

Hata baada ya uondoaji wa maneno machafu, kama ulikuwepo, sehemu ile ya maelezo ya Hadith ambayo inahusiana na maisha binafsi ya Muhammad, Mtume wa Uislam aliyebarikiwa, inakuwa imejaa yale ya ajabu, ya kushangaza, ya ubunifu na ya uongo.

Hizi ni Hadith nyingi ambazo zinamfanya aonekane kama ni mtu wa tamaa na ufisadi; mtu wa visasi na ukatili; mpenda maslahi na asiye mwaminifu; na msaliti na asiye muadilifu. Kisha zipo simulizi nyingine ambazo zinaweza kuitwa tu zenye lugha chafu.

Lakini ushahidi wa historia unakwenda kinyume na maelezo hayo mafupi juu ya wasifu wa Muhammad. Angeweza kuwa na mambo yote haya lakini hakuwa hivyo. Ni muhimu kwa hiyo, kwa Waislam na wasio Waislam vilevile, kutenganisha upuuzi na takataka kutoka kwenye uhakika na ukweli katika kuichunguza historia ya Uislam.

Ni vipi “simulizi” kama hizi ziliishinda akili ya kuzaliwa na mantiki, na kujipenyeza kwa hila kwenye maandishi ya Hadith na vilikuwaje vile vitendo na kauli ambazo zinaweza kuitwa tu kwamba ni za kuchukiza, zikavumishwa kama tabia ya mtu ambaye maisha yake hasa yalikuwa ni mfano halisi wa utakatifu wote, ukweli, uaminifu na wepesi?

Shibli amefanya jaribio la kijuujuu hasa la kujibu swali hili katika kifungu cha maneno kilichonukuliwa hapo juu. Anasema kwamba “wakala” wa nje mwenye nguvu sana mwenye kuathiri uandishi wa historia katika zama za Bani Umayya na Bani Abbas (661-1258) alikuwa ni serikali. Serikali ya siku zile ilikuwa na uwezo wa kuifanya historia iandikwe kwa “vipimo” vyake yenyewe. Himaya zote zilihisi kwamba zilikuwa huru kubadilisha historia au kuizuia historia, na wakati wowote walipoona ni kwa maslahi yao kufanya hivyo – kubuni ‘historia.’

Wakati ambapo Hadith nyingi zilibuniwa kwa sababu za kisiasa, zilikuwepo pia zile Hadith ambazo zilibuniwa kwa sababu za kianasa tu. Wapenda anasa wa mabaraza ya Damascus na Baghdad walitafuta “hifadhi” kwa ajili ya starehe zao ndani ya Hadith hizi.

Hadith ina maana ya maelezo. Kama mtu alimuona Mtume akifanya kitu au kumsikia akisema maneno fulani, na akasimulia jambo hilo kwa watu wengine, itaitwa ni Hadith au sunnah. Masahaba waliona ni wajibu wao kuzihifadhi sunnah zote za Mtume (s.a.w.w.) kwa faida ya umma wa Waislam kwa nyakati zote.
Hadith pia inaweza kuwa ni maoni ya Mtume juu ya mtu fulani. Kama alitoa sifa kwa sahaba wake yeyote, au kama alimkosoa mtu yeyote, maneno yake yalipata utangazwaji mpana sana miongoni mwa Waislam. Wakati wa ukhalifa wa Mu’awiyah, nyingi ya Hadith hizi zilikuwa katika usambazwaji. Alikuwa mwepesi kutambua umuhimu wake, na akaamua kuzifanya ni silaha ya kisiasa katika kampeni zake dhidi ya Ali ibn Abi Talib na Bani Hashim.

Mu’awiyah ambaye alikuwa ndiye muasisi wa ule ufalme wa kiukoo wa ki-Bani Umayya, alijishindia “nishani’ nyingine. Aliasisi “kiwanda kidogo” cha kutengenezea Hadith. Warithi wake, na baada yao, wale makhalifa wa Bani Abbas, walikilea “kiwanda” hicho ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kikishughulika na kutengeneza Hadith kwa wingi. Ingawa Shibli anadai kwamba Hadith ziliondolewa maneno machafu na wakaguzi wakosoaji, wang’amuzi na wachambuzi wa hali ya juu, yalikuwepo mengi ambayo yalikwepa kugunduliwa na hao, na yanakubalika, leo hii, na kundi kubwa la Waislam, kwamba ni sahihi.

Mu’awiyah aliteua timu ya watu kuunda maelezo yenye kufaa kwake yeye binafsi na kwa maadui wengine wa Ali, na kuyahusisha kwa Mtume kama Hadith zake mwenyewe. Wakati huo huo, alizuia au alijaribu kuzuia zile Hadith halali ambazo zilikuwa zinamsifu Ali, na akaiagizia timu yake kutengeneza Hadith za kushusha hadhi yake.

Wajumbe wa timu yake wakatunga Hadith za uwongo za tofauti zote, na wakaziingiza kwenye mzunguko.
Baada ya kifo cha Mu’awiyah, kampeni hii iliendelezwa na warithi wake. “Waandishi wanaowatungia,” “maafisa uhusiano,” na “wajenga-majina” wao, kwa ustadi kabisa wakachanganya Hadith za uongo na zile za halali, na historia ya usanisi (ya kuungaunga) pamoja na historia ya kweli, wakitumaini kwamba “mchanganyiko” huo “utadhihirika” kama sehemu ya elimu ya mapokezi matukufu ya Waislam.

Mu’awiyah alikuwa na sababu nyingine moja ya kuingia kwenye kazi ya “utengenezaji Hadith.” Alijua kwamba vizazi vya wakati ujao vitamuona kila mtawala wa Waislam kinyume na yule kiongozi mkamilifu – Muhammad (s.a.w.w.). Alijua pia kwamba kama watafanya hivyo, watamkuta yeye anahitilafiana kabisa na Muhammad. Alikuwa akitambua pia kwamba hata angefanya nini, asingeweza kupanda kama Muhammad; alijua kwa kweli kwamba asingeweza kufikia hata vile viwango vilivyovikiwa na watumwa wa Muhammad.

Lakini ilionekana kwake kwamba ingawa isingewezekana kwake yeye kufikia ule usawa ambao Muhammad akisimama juu yake, iliwezekana kwake yeye kumshusha Muhammad hadi kwenye usawa ambao yeye Mu’awiyah alisimama juu yake kwa ile njia nyepesi ya kufifisha nuru ya sifa zake Muhammad (s.a.w.w.), kiasi kwamba na yeye pia aonekane kama binadamu wengine wa kawaida.

Mu’wiyah alitegemea kwamba ukosoaji wa wanahistoria dhidi yake utakuwa hauna nguvu sana kama wangeonyeshwa kwamba hata yule mtu mkamilifu kabisa – Muhammad, Mtume wa Allah swt. Mwenyewe – hakuwa huru kabisa kutokana na dosari za mwenendo. Ni wazi kabisa, mengi ya yaliyomo kwenye maelezo ya Hadith yalikuwa ni njama kwa ajili ya mauaji ya tabia ya Muhammad, Mtume wa Allah swt.

Mu’awiyah na wale wawekezaji wengine wa “kiwanda kidogo” chake walikuwa “wamefanikiwa” katika jaribio lao la uuaji wa tabia ya Muhammad. Waliyachanganya maelezo ya Hadith pamoja na simulizi, visa na “matukio” yasivyokuwa na idadi, makusudio ya yote hayo yakiwa ni kumfanya Muhammad aonekane, machoni mwa vizazi vijavyo, kuwa chini kuliko unabii.

Ufuatao ni mfano wa moja ya sunnah za “kuchapishika” ambayo imetufikia sisi. Imeandikwa na Hakim Muhammad Said katika makala iliyochapishwa na Hamdard Academy, Karachi, Pakistan, mnamo mwaka wa 1972, katika kitabu kinachoitwa Tadhkira-i-Muhammad:

“Mara tu baada ya ndoa yao, Muhammad, Mtume wa Allah, alipendekeza kwa mwali wake mpya, Aisha, kwamba wakimbie wote kushindana. Aisha alikuwa amepungua na mwembamba, na alimshinda mbio mume wake kwa urahisi. Miaka kadhaa baadae, Mtume alimtaka Aisha kukimbia dhidi yake kwa mara nyingine tena. (Alikuwa ame- ongezeka uzito katika ile miaka ya tangu lile shindano la kwanza). Wote wakakimbia, na safari hii Mtume akamshinda mbio Aisha. Maoni yake yakawa: ‘Safari iliyopita ulikuwa wewe ndiye mshindi, ewe Humayra (jina la utani la Aisha) lakini safari hii mimi nimeshinda, na sasa matokeo kati yetu yamelingana.” (Huenda kule kushindwa katika lile shindano la kwanza kulikuwa kunakera katika akili ya Mtume miaka yote hii.)
Muhammad, Mtume wa Allah swt., alikuwa na umri wa miaka 54 wakati alipokimbia katika mashindano na msichana wa miaka 9 au 10, na alishindwa; na alikuwa na umri wa miaka 60 wakati alipokimbia dhidi yake kwa mara ya pili, na akashinda!

Waislam wanatetea hadhi ya Mtume wao. Hivi “sunnah” hii ambayo wengi wao wanaamini kwamba ni ya kweli, ni yenye taswira hasa ya hadhi hiyo?

Inaelekea kwamba wale “wasimamizi” na wale “mameneja uzalishaji” ambao Mu’awiyah amewaajiri katika “viwanda vyake vya Hadith,” walikuwa na haja moja tu, nayo ilikuwa ni wingi. Walikuwa wamekibuni “kiwanda” hicho kwa ajili tu ya uzalisha- ji wa “sunnah” kwa wingi. Ni dhahiri kwamba hawakuwa na haja ya “udhibiti wa ubora” wa mazao yao.

Walipandikiza uwongo kwenye vitabu vyao, na kila uwongo ukaacha baada yake, kama unavyofanya wakati wote, “tone la sumu,” lililochafua akili ya vizazi vya Waislam. Baadhi ya mazao yao (ya Hadith) ni matovu ya adabu kweli kweli.

Hayo, kwa kweli, hayachapishiki. Wakosoaji na maadui wa Mtume (s.a.w.w.), bila ya kukwepa, wameonyesha shauku kubwa katika kuzikubali kama ni sahihi, na wamezinukuu katika vitabu vyao.

Wakosoaji na maadui hawa wa Mtume, hata hivyo, hawakuzingatia yale mambo ambayo usahihi wake hauna shaka yoyote. Kwa mfano, wameliacha lile suala la kwamba, huko Makka, Makuraish walimuahidi yeye (Mtume) mwanamke au wanawake wazuri zaidi kama malipo ikiwa ataacha kutangaza Uislam. Walisahau vile vile ule ukweli kwamba Muhammad alikuwa mtawala wa Madina, na kwamba angeweza kuoa msichana yoyote yule. Machifu wa Waarabu wangejivunia kumpa yeye mabinti zao.

Mtume (s.a.w.w.) alioa wanawake wengi hapo Madina lakini wengi wao walikuwa ni wajane, na wala hawakuwa wadogo sana pia. Isipokuwa Khadija tu, wanawake wengine wote waliingia nyumbani kwake wakati alipokuwa kwenye miaka ya katikati ama ya mwishoni mwa hamsini.

Waliingia maishani mwake katika wakati ambapo kudunda na kuchangamka na mng’ao na nguvu za ujana wake zilikuwa zimetoka siku nyingi, na nafasi yao ilikuwa imechukuliwa na mizigo inayoendelea kuongezeka ya Dola inayoendelea kukua, na matatizo mengine yenye utata na ukubwa wa hali ya juu zaidi, yakimwachia muda mdogo sana au mwelekeo wa upoteaji wa muda kama huo kama inavyosimuliwa katika nyingi ya “sunnah.”

Kwa ukusanyaji wa Hadith, Mu’awiyah alikuwa ametoa maagizo yafuatayo:

1. Hadith zote za Mtume zenye kumsifu Ali au zinazounga mkono ubora wake kwa namna yoyote
ile, lazima zizuiwe.

2. Mtu yeyote anayesimulia wema wa Ali au kunukuu Hadith ya Mtume kuhusu suala hili, atafanya hivyo kwa kujihatarisha mwenyewe. Msaada wake toka serikalini na ujira vitazuiliwa kwake. Nyumba yake na mali nyingine zitakamatwa. Ushahidi wake kama shahidi hautakubaliwa katika mabaraza, na atatenganishwa na Waislam wengine.

3. Kwa upande mwingine, kila sifa zinazoweza kufikirika hazina budi kuhusishwa na Abu Bakr,
Umar, Uthman, na bila shaka kwa Mu’awiyah mwenyewe. Watu wahimizwe kuteneneza ”Hadith” za Mtume zenye kuwasifu hawa watu wanne na marafiki zao. Yeyote yule
atakayebuni Hadith kama hiyo, atakuwa ni kipenzi kwenye baraza la kifalme, na atapata zawadi
nono katika cheo au pesa taslim au mashamba na kadhalika.

Kwa kulingana na uundwaji wa “kiwanda kidogo”chake kwa ajili ya utengenezaji wa “Hadith” za Mtume, Mu’awiyah pia alianzisha “viosha akili” kwa ajili ya Waislam. Alianzisha desturi ya kuvuruga kumbukumbu za Ali na wanawe kutoka kwenye mimbari ya kila msikiti ndani ya himaya yake ili kwamba watoto wa Kiislamu wawe wamezaliwa, wamekua , na wamekufa wakisikia laana nyingi juu ya Ali, na wasijue yeye alikuwa ni nani.

Vizazi vizima viliishi na kufariki katika ujinga. Uwongo uliingizwa kwenye mzunguko na serikali kwa kiwango kikubwa sana kiasi kwamba ikawa ndio dhana ya maisha yao. Mu’awiyah na warithi wake waliviweka “viosha akili” vyao katika kushughulika kama vile tu kile “kiwanda kidogo” chao.Mu’awiyah aliandaa kila njia ya kuendeleza vita vya propaganda dhidi ya Ali na Banu Hashim.

Msukumo wa shambulio hilo aliloanzisha dhidi yao, umedumu hadi kufikia nyakati zetu sisi wenyewe. Alifanya vita vyake kuanzia misikitini. Viongozi wa swala ndani ya misikiti hiyo walilipwa ili kuweka tafsiri za kipekee na za ajabu juu ya Aya za Qur’an katika jaribio la kumuonyesha Ali kwenye upungufu. Walijaribu kuwashawishi Waislamu wa kawaida kwamba itakuwa ni kwa maslahi yao katika “dunia zote mbili” watamuunga mkono Mu’awiyah dhidi ya Ali na Bani Hashim.

Michael C. Hudson

“Wenye madaraka wana fursa ya vyombo vya habari na mikono ya elimu ya dola, na wanawadhibiti kupitia ruzuku wale wenye mamlaka ya kidini wenyewe.” (Islam and Development, uk. 16, 1980)

Ni lazima sasa ieleweke kwa msomaji kwamba historia ya Uislamu iliandikwa kwa maelekezo ya lile kundi ambalo lilishikilia vyombo vyote vya madaraka mikononi mwake. Na ni lazima pia iwe dhahiri kwake kwamba mengi ya maelezo ya kihistoria “yalioshwa” kwenye vile “viosha akili” vilivyoanzishwa na Mu’awiyah kabla hayajaingia mikononi mwake yeye msomaji. Mu’awiyah alikuwa ni bingwa mkamilishaji sana wa sanaa ya propaganda.

Sir John Glubb

“Athari kamili za propaganda hiyo hazijawa dhahiri bado, hata hivyo, tayari ni dhahiri kwamba mataifa mazima yanaweza kutiwa kasumba ya maoni potofu na viwango vya maadili maovu. Ni akili chache, kama zipo, zenye nguvu ya kutosha kuweza kukataa mawazo yanayochomozwa kwao wakati wote.”
(The Course of Empire – The Arabs and Their Successors, 1965)

Kama Hadith yoyote ya Mtume wa Uislamu ilikuwa yenye kusifu Ali, usimuliaji wake ulipigwa marufuku na Mu’awiyah. Marufuku haya hayakuondolewa wakati alipokufa mwaka wa 680. Hayakuondolewa hata pale ufalme wake, wa Bani Umayya, ulipoanguka mnamo mwaka wa 750, na hayakuondolewa hata katika karne ndefu za ukhalifa wa Bani Abbasi.

Bani Abbasi waliwaangamiza Bani Umayya lakini walichangia pamoja nao chuki yao dhidi ya Ali na kwa kizazi cha Muhammad (s.a.w.w.). Katika suala hili, malengo na maslahi ya serikali ya Saqifah, Bani Umayya na Bani Abbas walikutana; ulikuwepo upatanifu wa kiitikadi miongoni mwao wote.

Bani Umayya na Bani Abbas walifanya kila lililowezekana kuzima ukweli wa historia. Wengi wa makhalifa wao waliwakataza raia zao kusema au kuandika kitu chochote kuhusu Ali isipokuwa uwongo. Ukweli ulikuwa kizuizini na uwongo ukawa umeenea kwenye miliki zao. Na bado, Ukweli ukajithibitisha wenyewe. Ukweli umefika na uwongo umetoweka; hakika uwongo (kwa asili yake) ndio wenye kutoweka.
(Sura ya 17; Aya ya 81)

Maelezo ya kweli yalijitolewa na vyanzo ambavyo, katika masuala mengi, vilikuwa na uhasama kwa Ali. Hata wale maadui zake wakali sana kama Bani Umayya na Khariji, walikiri usafi wa tabia yake. Kama ilivyoelezwa hapo kabla, M. Shibli, mwanahistoria wa Kihindi, alionyesha kwamba Waislamu wa ki-Shi’ah hawakuandika historia yoyote.

Historia yoyote tuliyonayo, kwa hiyo, imetufikia sisi kutoka kwa wasiokuwa Shi’ah au kwenye vyanzo vyisivyokuwa vya ki-Shi’ah. Imetufikia kutoka kwenye hifadhi za nyaraka za serikali za Saqifah, Bani Umayya na Bani Abbasi. Kisa cha vitendo vitukufu vya Ali ibn Abi Talib, kama ule mng’aro wa Ukweli wenyewe, umejichuja kutoka kwenye hifadhi hizo.

Lakini wanahistoria wa kisasa hawatishiwi na serikali yoyote kwa kuandika historia ya kweli wala hawashawishiwi na ahadi za zawadi nono kwa kuandika historia za uwongo. Wanapaswa kwa hiyo, kuchunga vishawishi vya kuzima au kupotosha ukweli.
Kama watanywea hata leo hii kwenye vishawishi hivi, kama wengi wa watangulizi wao walivy- ofanya wakati uliopita, basi inawezakuwa na maana tu kwamba wanatoa uaminifu wao sio kwenye kanuni bali kwa watu; sio kwenye ukweli bali kwenye taasisi na serikali; na sio kwenye hadhi zao bali kwenye misimamo ya hisia zao.

Uaminifu ni sifa tukufu alimuradi hauwi wa upofu, na kama hauondoi ule uaminifu wa hali ya juu kwenye ukweli na kwenye heshima, basi wanapaswa kukomba vinundu na mabaki ya historia, na wanapaswa pia kukataa vishawishi vya kuzusha kitu kinachoitwa “Meyers’ Law” (Sheria ya Meyer) katika vitabu vyao. “Meyers’ Law” inaweka masharti kwamba: “Kama ukweli haulingani na nadharia, basi ukweli huo uache kabisa.”

Mwanahistoria bila ya kukwepa atakutana na ukweli ambao unaweza kuwa haumpendezi lakini ni lazima asiuzime. Yeye lazima aeleze mambo yote kama anavyoyagundua ikiwa anataka kutetea ukweli.

Lakini mwanahistoria huyo, kama yeye ni Muislamu, hana uchaguzi katika suala hili. Hayuko huru kuandika historia ya “msukumo” au ya “maneno ambatani.” Yote anayoweza kufanya, kama anaandika historia, ni kung’ang’ania kwa uthabiti kabisa kwenye ukweli.

Kama anaandika “historia” ya uwongo kwa sababu yoyote ile, atastahili tu ghadhabu ya Allah swt. Hapa, kama mahali pengine popote, Qur’an Tukufu, Kitabu cha Allah swt. kiko wazi, chenye mkazo, na yenye kauli moja katika hukumu yake kama ifuatavyo:

وَلَا تَلْبِسُوا الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُوا الْحَقَّ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {42}

“Na wala msichanganye haki na batili, na mkaficha haki hali ya kuwa mnajua.” (Sura ya 2. Aya ya 42)

نَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنْزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِنْ بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ {159}

“Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha katika dalili zilizo wazi na muongozo, baada ya sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni – Hao hulaaniwa na Mwenyezi Mungu, na laana ya wenye kulaani (pia).”(Sura ya 2. Aya ya 159)

Kama wanahistoria wa Kiislamu watazifanya hizi Aya mbili za Qur’an Tukufu kuwa “nyota ya uongozi” yao, watalindwa na makosa, na watalindwa pia kutokana na kuwa ama mawakala ama waathirika wa propaganda hiyo, watambue au wasitambue.

Katika kujaribu kuchafua jina la Ali ibn Abi Talib; katika kujaribu kudunisha kwa makusudi utumishi wake kwa Uislamu; na kwa kujaribu sana kuficha matendo yake mema, nyuma ya pazia la propaganda, kwenye kizazi cha baadae, maadui zake walikuwa wakitupa mavumbi kwenye uso mng’aavu wa jua.

Waliibua mawingu ya mavumbi katika muundo wa propaganda kali sana na iliyoendelezwa dhidi yake, na bado, jua hilo lil- iangaza zaidi na zaidi.

وَيَمْحُ اللَّهُ الْبَاطِلَ وَيُحِقُّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ ۚ{24}

“Na Mwenyezi Mungu ataifuta batili na ataithibitisha Haki kwa maneno Yake. (Sura ya 42; Aya ya 24)

Allah swt. alilibariki jina la Ali kwa milele yote. Jina lake ni alama ya upendo wa Allah swt., na ni alama ya Haki na Ukweli. Jina lake litadumu kwa muda mrefu kama Mapenzi ya Allah swt, na Haki na Ukweli, vitadumu katika dunia hii.