read

Orodha Ya “Watu Wa Kwanza” Katika Uislamu

Mtu fulani katika Uislamu alikuwa mwanaume wa kwanza au mwanamke wa kwanza kufanya au kusema kitu, na hili lilimfanya kuwa mwanaume au mwanamke mtangulizi. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya matendo ambayo yaliwafanya watendaji wake kuwa “watangulizi.” Orodha hiyo, bila shaka, kwa hali yoyote ile sio kamilifu.

(1). Hashim, babu-mkuu (babu yake baba) yake Muhammad ibn Abdallah na Ali ibn Abi Talib, alianzisha mfumo wa kibiashara wa Hijazi, ambao, kwa nyakati zile, ulikuwa ni mapinduzi katika maisha ya kiuchumi ya Arabia. Kwa kufanya hivyo, aliwabadili Makuraish kutoka wachungaji na kuwa wafanyabiashara matajiri.

Ibn Ishaq:

“Inadaiwa kwamba Hashim alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha safari mbili za mis- afara ya Makuraish, ya kiangazi na ya kipupwe, na wa kwanza kutoa (kuandaa) tharid (mchuzi) hapo Makka.”

(2). Khadija binti Khuwaykid, mke wa Muhammad Mustafa, alikuwa wa kwanza kusilimu.

(3). Mwanaume wa kwanza aliyeshuhudia kwamba Mungu ni Mmoja, na Muhammad alikuwa
ni Mtume Wake, alikuwa ni Ali ibn Abi Talib.

(4). Sehemu ya kwanza ya kukutania katika Uislamu ilikuwa ni katika nyumba ya Arqam bin
Abil-Arqam hapo Makka.

Betty Kelen:

“Uislamu wa mwanzoni ulikuwa ni vuguvugu la vijana, ambalo awali lilifikiriwa kama chama kisichokuwa na madhara. Walikuwepo katika siku zile takriban wanachama 40, na walikuwa wakipenda kukutana katika nyumba kubwa katika kiunga cha mji iliyokuwa mali ya kijana mmoja tajiri aitwaye Arqam wa kabila la Makhzum. Nyumba hiyo ya Aqram inakumbukwa na Waislamu kama sehemu ya kwanza ya kukutania ya Uislamu.”

(5). Akina Yasir walikuwa ndio “familia nzima” ya kwanza kusilimu (nje ya familia Mtume mwenyewe). Yasir, mke wake, Sumayya; na mwana wao Ammar; wote watatu walisilimu mara tu walipousikia mwito wa Mtume wa Allah swt. Watu wengine wamedai kwamba alikuwa ni Abu Bakr aliyekuwa mkuu wa “familia nzima” ya kwanza kusilimu. Madai haya yanakosa ushahidi. Mtoto wa Abu Bakr, Abdur Rahman, alikuwa ni mwabudu sanamu, na alikpigana dhidi ya Mtume wa Allah katika vita vya Badr. Baba yake Abu Bakr, Abu Qahafa, alikuwa pia ni muabudu masanamu ambaye alikuja kuwa Muislamu tu baada ya kutekwa Makka mnamo mwaka 630.

(6). Wapagani wa Makka walimtesa Yasir na mke wake Sumayya, na mtoto wao Ammar, siku baada ya siku, kwa kuukubali Uislamu. Wote watatu walikuwa ndio Waislamu wa kwanza ambao Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah swt. aliwabashira kwam- ba wataingia Peponi.

(7). Sumayya, mke wa Yasir, alikuwa Mu’min wa kwanza aliyekufa shahidi katika Uislamu. Mume wake, Yasir alikuwa shahidi wa pili katika imani. Wote waliteswa mpaka kufa na wapagani hao. Mtoto wao, Ammar, alikuwa amepangiwa kupata shahada ya kifo cha Kishujaa ingawa alifanya hivyo katika vita vya Siffin mwaka 657. Waligeuka, kwa namna hii, kuwa familia ya wote Mashujaa katika Uislamu – sifa ambayo hakuna yoyote aliyewahi kushirikiana nao. Allah swt. Mwenyewe aliwach- agua kwa ajili ya heshima hii kubwa.

(8). Mtu wa kwanza kusoma Qur’an kwa sauti ndani ya Al-Kaaba alikuwa ni Abdallah ibn Mas’ud, sahaba na rafiki wa Muhammad (s.a.w.w.).

Ibn Ishaq

“Yahya b. Urwa b. Zubeir aliniambia kutoka kwa baba yake kwamba mtu wa kwanza kusoma Qur’an kwa sauti hapo Makka baada ya Mtume alikuwa ni Abdallah ibn Mas’ud.”
(9). Mtu wa kwanza kuuawa kwenye viwanja vya Al-Kaaba alikuwa ni Al-Harith ibn Abi Hala, mpwa na mtoto wa kutwaliwa wa Khadija, mke wa Mtume. Pale huyu alipotangaza Umoja wa Allah ndani ya Al-Kaaba mbele ya mkusanyiko wa waabudu masanamu, walimfanyia ukatili wa kimwili. Al-Harith ibn Abi Hala aliin- gia kwenye ugomvi wa kujitetea. Wakamchoma kwa marudio rudio, na akaanguka chini amekufa. Kwa hiyo yeye akawa Shujaa wa tatu katika Uislamu.

(10). Ammar ibn Yasir alikuwa mtu wa kwanza katika Uislamu kujenga Msikiti. Alijenga msikiti wake hapo Makka penyewe.

Ibn Ishaq:

“Sufyan ibn Uyayna alitaja kwa idhini ya Zakariya kutoka kwa al-Shabi kwamba mtu wa kwanza kujenga msikiti alikuwa ni Ammar ibn Yasir.”

(11). Mas’ab ibn Umayr alikuwa ndio mtumishi wa kwanza katika Uislamu. Mnamo mwaka 621, kikundi cha raia kutoka Yathrib (Madina) kilikuja Makka. Walikutana na Mtume huko Aqaba; wakasilimu, na wao wakamuomba Mtume kuwapa kwenda naye Madina, mwalimu wa Uislamu na Qur’an. Mtume (s.a.w.w.) akamtuma Mas’ab ibn Umayr, binamu ya baba yake, kwenda pamoja nao. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kuchaguliwa mtumishi katika Uislamu. Mas’ab ibn Umayr alikuwa Mwakilishi wa Kwanza wa Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah swt., katika wadhifa wowote ule.

(12). Abdallah, mtoto wa Abd al-As’ad, alikuwa mtu wa kwanza kuhama kutoka Makka kwenda (Yathrib) Madina mwaka 622.

(13). Bilal alikuwa ndio “muadhini “ wa kwanza wa Uislamu. Sauti yake ilivuma hapo Madina kwa ukelele wa Allah-u-Akbar (Allah ni Mkubwa). Wakati Madina ilipokamilisha sifa zote za dola, ilijipatia hazina pia, na Muhammad (s.a.w.w.) akam- teua Bilal kuwa afisamsimamizi wa hazina hiyo. Alikuwa msimamizi wa Bayt-ul- Mal ya dola ya Madina. Hii ikamfanya awe Mtunza Hazina wa Kwanza wa Uislamu. Alifanya mgao wa mali zote. Yeye alikuwa pia anahusika na kugawa mali kwa wajane, mayatima, wasafiri na watu wengine masikini ambao walikuwa hawana njia ya kujikimu wao wenyewe.

(14). Hamza ibn Abdul-Muttalib, ami yake Muhammad na Ali. Alikuwa kamanda wa kijeshi
wa kwanza katika Uislamu. Mtume wa Allah swt. alikuwa amemtuma yeye akiongoza
Muhajirin 30 kwenda kuingilia kati msafara wa Makuraish, ukiongozwa na Abu Jahl. Lakini
hakukuwa na mapambano, na kikosi hicho kikarudi Madina.

(15). Gavana wa kwanza wa Madina alikuwa ni Saad ibn Ubada Ansari. Katika mwaka wa pili wa
Hijiria, Mtume mwenyewe aliongoza kikosi kwenda Waddan. Wakati wa kutokuwepo kwake,
Saad ibn Ubada alisimama kama mtawala wa Madina.

(16). Kamanda wa kijeshi wa kwanza ambaye watu wake walihusika katika umwagaji damu,
alikuwa ni Abdallah ibn Jahash, binamu wa Mtume. Yeye aliongoza kikosi cha watu saba
kwenda Nakhla.

(17). Vita vya Badr, vilivyopiganwa mwaka 624, vilikuwa ndio pambano la kwanza, katika
uwanja wa vita, kati ya Uislamu na upagani. Bingwa wa kipagani, Walid bin Utba, aliwatia
changamoto mashujaa wa Uislamu kwenye pambano la watu wawili wawili. Changamoto
yake ilijibiwa, kwa upande wa Uislamu, na Ali ibn Abi Talib, mwanaume wa
kwanza kusilimu. Ali alimuua Walid bin Utba baada ya dakika chache za ufundi wa kutumia
upanga. Huu ulikuwa ndio mwanzo wa pambano refu kati ya Uislamu na upagani.

Lilikuwa liishe kama lilivyoanza, kwa ushindi wa Uislamu juu ya upagani, na Ali alikuwa ndiye muasisi wa ushindi huo.

(18). Ubaidullah ibn al-Harith ibn Abdul-Muttalib, alikuwa Muislamu wa kwanza kuuawa katika
vita. Yeye alikuwa ni binamu ya Muhammad na Ali, na alikuwa ndiye Shahidi wa kwanza wa
vita vya Badr.

(19). Zayd ibn Haritha alikuwa ndiye Muislamu wa kwanza kuuawa kwenye ardhi ya kigeni. Mnamo Septemba 629, Mtume alimtuma yeye kama jemadari mkuu wa jeshi ambalo lilikuwa lishambulie Warumi huko Syria. Majeshi hayo mawili yalikutana katika vita vya Muutah, na Zayd aliuawa katika vita hivyo.

(20). Akib ibn Usaid alikuwa gavana wa kwanza wa Makka. Ilikuwa ndio ajira ya kudumu ya kwanza kufanywa katika Uislamu.

Akib alichukua mamlaka ya wajibu wake kama gavana wa Makka mnamo Januari 630.