read

Saad Ibn Ubadah, Ansari - Mgombea Wa Ukhalifa

Saad ibn Ubadah alikuwa ndio kiongozi wa kabila la Khazraj la Madina. Hawa Khazraj na Aus, makabila mawili ya Ansari, walikuwa wamejipatia sifa kwa utumishi wao kwenye Uislamu. Utumishi wao ulitambuliwa hata na Abu Bakr pale alipokuwa akibishana na kushindana nao mle Saqifah.

Katika vita vya Uislamu, Ansari walikuwa wakati wowote wako msitari wa mbele. Walipigana dhidi ya nguvu mkusanyiko wa waabudu masanamu wote wa Arabia. Abu Qatadam, Ansari mmoja, alidai, na kweli kwamba hakuna kabila katika Arabia yote lililotoa wahanga wengi kwa ajili ya Uislamu kuliko Ansari. Ansari wengi waliuawa katika kutetea Uislamu kuliko watu wa kabila lolote lile jingine.

Kulikuwa na wakati ambapo Uislamu ulikuwa “hauna makazi.” Hakuna kabila lililotoa hifadhi na ukarimu kwa Uislamu na kwa Mtume wake isipokuwa Ansari. Walimkaribisha Muhammad (s.a.w.) kuwa mgeni wao, na walimfanya kuwa mfalme wa mji wao – Yathrib (Madina).

Ulikuwa ni mji wa Ansari ambao ulipata heshima ya sifa ya kuwa makazi na makao makuu ya Uislamu. Ilikuwa ni katika mji wao ambamo Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.w). alijenga “jengo” kubwa la Ufalme wa kwanza na wa mwisho wa Mbinguni juu ya Ardhi.

Mnamo A.D. 623 (2 Hijiria), Muhammad (s.a.w.) aliongoza msafara kwenda Waddan, na alimteua Saad ibn Ubadah kuwa gavana wa Madina wakati wa kutokuwepo kwake yeye mwenyewe. Saad, kwa hiyo, alikuwa ndio gavana wa kwanza wa Madina.

Katika vita vya Uhud, Mtume wa Allah (s.a.w.w). alitoa bendera ya Khazraj kwa Saad. Katika vita hivyo hivyo, Waislamu walishindwa. Ukiacha maswahaba 14, kila mtu mwingine alikimbia kutoka kwenye uwanja wa vita. Saad alikuwa mmoja wa hao mashujaa 14 waliopigana dhidi ya adui, na kumlinda Mtume (s.a.w.)

Katika msafara wa Mustaliq na katika kuzingirwa Madina (vita vya Khandaq), Saad alishika bendera ya Ansari. Kwenye mwaka wa 6 Hijiria Mtume alikwenda kwenye msafara na alimteua Saad kuwa gavana wa Madina wakati wa kutokuwepo kwake.
Ansari walikuwa na viongozi wawili, Saad ibn Ubadah na Saad ibn Mua’dh. Saad ibn Mua’dh alifariki kutokana na jeraha alilolipata katika vita vya Khandaq. Baada ya kifo chake, Saad ibn Ubadah alikuwa ndio kiongozi pekee wa Ansari.

Humo Saqifah, Ansari walimwambia Saad kwamba alikuwa ndio mtu mwenye kufaa sana kuwa khalifa, na walitangaza kumuunga mkono kwao katika ugombea wake. Saad alikuwa maarufu kwa ukarimu wake. Wakati mwingine alikaribisha wageni wengi kiasi cha 80. Yoyote yule – rafiki au mgeni, aliweza kutegemea ukarimu wake.

Saad alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Abu Bakr. Miaka mitatu baadae, aliondoka Madina, kwenda Syria na akaweka maskani huko. Alikuwa yuko Syria wakati alipopigwa na mshale uliotupwa na mtu asiyejulikana, na kwa hiyo alikufa katika mazingira yanayotatanisha.

Saad ibn Ubadah alikuwa Ansari wa kwanza na wa mwisho aliyewahi kuwa mgombea wa ukhalifa. Yeye hakuwahi kuwa khalifa. Mle Saqifah, mlango wa ukhalifa ulifungwa nyusoni mwa Ansari, na waliwekwa nje kwa wakati wote, milele.