read

Saqifah Na Mantiki Ya Historia

Katika utangulizi wa kitabu hiki, nilimtahadharisha msomaji juu ya tabia na wepesi wa Mustashriq wengi, kukubali, bila kuangalia undani wake, mengi ya maelezo ya uongo na madai ya uongo ambayo yaliingizwa kwenye mzunguko, zamani sana, na wale wanahis- toria ambao walikuwa kwenye “orodha ya malipo” ya Serikali ya Damascus na Baghdad.

- zote zikiwa warithi wa Serikali ya Saqifah. Kwa mfano kuna makubaliano miongoni mwao kwamba Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) hakuchagua mrithi wake mwenyewe wala hakuwaambia Waislamuu namna wanavyopaswa kuchagua viongozi wao kwa ajili ya Serikali ambayo aliianzisha, na alifariki akiacha kila kitu, dhahiri kabisa, kwenye mashauri yao na hiari zao.

Baadhi ya mifano ya kukubali kusiko na udadisi kwa Mustashriq juu ya dai hili, ilitoka katika Sura ya 45. Ufuatao ni mfano mwingine zaidi.

“Muhamamd alifariki hapo Madina mnamo tarehe 8, Juni, 632, bila ya kuacha maa- gizo kwa ajili ya Serikali ya baadae ya jamii ya Waislamu…”

Habari hii inatokea kwenye makala yenye kichwa cha habari Caliphate, kwenye ukurasa wa 643, juzuu ya 4, chapa ya 14 ya 1973 ya Encyclopedia Britannica. Ni kipande cha propaganda cha dhahiri lakini hiyo Encyclopedia Britannica, kile kienezaji kikuu cha elimu, kimeikubali. Ni taarifa ya uongo ya kihistoria yenye kugawa mno katika Uislamu, lakini cha ajabu, inapita bila kupingwa, karne baada ya karne.

Hawa Mustashirki wanaweza wasilete pingamizi kwenye huu uongozi wa muda mrefu unaokubalika kwenye mila na desturi, lakini hata hivyo unazua maswali fulani ya msingi. Maswali hayo ambayo yanahusiana na maadili ya Uislamu na falsafa ya kisiasa ya Muhamamd Mtume wa Allah (s.a.w.) yameorodheshwa hapo chini. Yote yanasimama kwenye dhana ya kwamba Muhamamd (s.a.w.) haku…(rudia haku…) hakuteua mrithi wake mwenyewe wala hakutoa maagizo yoyote kwa maswahaba zake kwa ajili ya serikali ya baadae ya umma wa Kiislam. Kwa hiyo, wakati alipofariki, Umma wake ulijikuta wenyewe katika hali ya mfadhaiko mkubwa kabisa.

1. Je, Muhammad (s.a.w.) Mtume wa Allah (s.w.t.) na Muasisi wa Serikali ya Madina, alijiona binafsi ni mwenye uwezo wa kuchagua mrithi wake mwenyewe au la?

2. Kipi kingefaa, ni sababu za kubuni juu ya kushindwa kwa Muhammad (s.a.w.) kuteua mrithi wake mwenyewe?

3. Kwa vile Muhamamd (s.a.w.) hakuteua mrithi wake mwenyewe, je, aliik- abidhi jamii ya Waislamu jukumu hilo la kuchagua au kuteua kiongozi wao wenyewe?

4. Kwa vile jamii ya Kiislamu ilikosa mwongozo juu ya kuteua kiongozi, je maswahaba wa Muhamamad, kwa ridhaa yao ya pamoja, na kabla ya kuweka kiongozi (au hata baada ya kuweka kiongozi) waliandaa orodha ya masharti au miongozo ambayo wao waliishika (baadaye)?

5. Upi ulikuwa msimamo na mwenendo wa maswahaba wakubwa wa Muhamamd (s.a.w.) juu ya uongozi wa jamii ya Waislamu baada ya kifo chake?

6. Upi ulikuwa mwenendo (Sunnah) wa Muhamamd (s.a.w.) kuhusiana na uteuzi na uwekaji wa watumishi?

7. Ni ipi Fatwa ya Qur’an juu ya mwenendo (sunnah) wa Muhamamd (s.a.w.)?

8. Muhamamd (s.a.w) alifanya nini hasa kuhusu kurithiwa kwake?

9. Ni nini hasa kilichotokea baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w)?

10. Je, swala la urithi lina umuhimu gani katika historia kwa jumla?

Jaribio limefanyika katika kujibu maswali haya kama ifuatavyo:

Swali la 1: Je, Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), na muasisi wa Serikali ya Madina, aliona binaf- si yeye ni mwenye uwezo wa kuchagua mrithi wake mwenyewe au la?

Jibu: Hakuna hata mtu mmoja ambaye angefikiria, kati ya Waislamu wote, kwamba Muhamamd hakuwa na uwezo na kumuweka mrithi wake mwenyewe. Mwislamu hawezi kudhania kwamba Mtume (s.a.w.w) alikosa uwezo wa kuteua mrithi kwa ajili yake mwenyewe.

Waarabu walikuwa ni kizazi chenye sifa mbaya ya kiburi, cha wajinga, wenye ghasia na wasio na sheria. Muhamamd (s.a.w.) alizieneza sheria za Allah (s.w.t.) miongoni mwao, na akawalazimisha kuziheshimu na kuzitii sheria hizo. Aliunda taasisi ya kisiasa iliyoitwa Dola au Serikali ya Madina.

Katika Dola hiyo, madaraka yake yalikuwa hayana mpaka. Aliwachagua watumishi wake wote, wa kiraia na kijeshi. Aliweza kumuweka mtumishi au kumfukuza, bila kufuata msingi maalum, na bila ya kutoa sababu zozote kwa mtu yeyote kwa kufanya hivyo.

Mwelekeo wa tabia (sunnah) ya Muhammad (s.a.w.) ilikuwa thabiti na ya kudumu daima. Alikuwa kwa kweli, ni mwaminifu kiasi kwamba alikuwa takriban ni “mwenye kutabirika.”

Waislamu wote walijua kwamba angeteua na kuweka watu wenye uwezo katika nafasi zote muhimu, na pia walijua kwamba angefanya hivyo bila kushauriana nao. Wala haku- toa mamlaka kwa maswahaba wake wowote ya kuweka watumishi. Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.). pekee ndiye alikuwa na uwezo wa kuteua na kuweka mrithi wake mwenyewe, na hakuna yeyote ambaye angemfanyia hivyo badala yake.

Swali la 2: Kipi kingefaa, ni sababu za kubuni juu ya kushindwa kwa Muhamamad (s.a.w.) kuteua mrithi wake mwenyewe?

Jibu: Kama Muhammad (s.a.w.) angekufa bila ya kuchagua mrithi na atakayemfuata baada yake, anajiweka kwenye lawama ya kutotekeleza wajibu. Yeyote anayedai kwamba yeye hakuchagua mrithi wake, anashauri kwamba alikiacha chombo dhaifu cha Uislamu kwenye bahari iliyochafuka bila ya dira, bila ya usukani, bila ya nanga na bila ya Nahodha, na kukiacha kabisa kwenye huruma ya upepo na mawimbi. Ni kudhania kwamba hakuwa mwangalifu wa maslahi muhimu kabisa ya umma wa Kiislamu na kwamba alikuwa amezembea kwenye ustawi wa vizazi vya Waislamu, vitakavyokuja baadae. “Uzembe” kama huo kwa upande wake ungeweza kuwa na sababu tatu zinazowezekana, yaani:

a) Watu wote wa Umma wa Kiislamu wamekuwa wenye ufahamu mkubwa, wenye heki- ma, wacha-mungu na wenye kumpenda Allah (s.w.t.) na kila mmoja wao alikuwa amepata elimu kamili ya tafsiri ya Qur’an. Vile vile kila mmoja alikuwa analingana, katika kila hali na kila mtu mwingine. Ilikuwa haiwezekani kwa shetani kumshawishi au kumpoteza yeyote kati yao. Kwa hiyo, Muhammad (s.a.w.) angeweza kuacha wajibu wa kuteua na kuchagua mrithi wake kwenye fursa ya kubahatisha. Angeweza kufarijika kwa kudhani kwamba yeyote yule atakayefanywa kiongozi wa jamii hiyo kwa mkondo wa matukio, atakuwa ni mtu sahihi, na Serikali ya Madina na jumuiya ya waumini vyote vingeweza kuwekwa chini ya uangalizi wake.

Lakini hivyo sivyo ilivyokuwa na isingeweza kuwa hivyo. Haiwezekani hata kwa watu wawili kulingana katika uwezo, tabia na desturi. Muhammad (s.a.w.) alijua kwamba Waarabu wote waliokubali Uislamu, sio lazima kuwa walikuwa wote ni Waislamu waaminifu. Miongoni mwao, ilikuwemo idadi kubwa ya “wanafiki” au “Waislamu wachache.” Kuwepo kwao pale Madina kunashuhudiwa na Qur’an yenyewe. Waliukubali Uislamu kwa nje tu bali moyoni walikuwa wapagani. Walikuwa ndio maadui wa Muhamamd, wa Uislamu, na wa Dola aliyokuwa ameianzisha. Walifanya “safu ya tano” ya upagani hapo Madina, tayari kutumia fursa ya kwanza ya kuudhoofisha Uislamu.

Kama Muhammad (s.a.w.) angekuwa aiache Dola hii mpya bila ya kiongozi, kwa kweli angeiweka mkononi mwa hawa wahujumu wa kiitikadi, silaha zenyewe hasa ambazo kwazo watauangamizia.

Muhammad aliyajua yote haya, na alifariki, sio ghafla, bali baada ya maradhi ya muda mrefu, yeye alikuwa na muda wa kutosha kushughulikia mambo muhimu ya Dola, lenye umuhimu zaidi likiwa ni uteuzi wa usimamishaji wa mrithi wake mwenyewe. Kitu kimoja ambacho asingeweza kukifanya, kilikuwa ni kuitelekeza serikali yake, ambayo ilikuwa ni Ufalme wa Mbinguni Duniani, kwenye uangalizi wa mpenda fursa asiyejulikana au mpenda vituko mwenye majigambo.

b) Muhammad (s.a.w.) hakuupenda hasa Uislamu. Alitiwa shauku tu na malengo yake binafsi. Alitaka kuiweka peninsula yote ya Arabia chini ya mamlaka yake, na Uislamu ulikuwa ndio njia ya ambayo alifanikiwa nayo katika kufanya hivyo. Lakini mara alipotimiza lengo lake hakujali kwamba baada ya kufa kwake, ile serikali ambayo ameianzisha, ilikuwa imara au ilichanguka. Hakujali kama, baada ya kifo chake, Waarabu walibakia waaminifu kwa Uislamu ama walirejea kwenye uabudu masanamu na ushenzi.

Ni nini kitakachokuwa cha kipumbavu zaidi kuliko kudhania kwamba Muhammad (s.a.w.) hakuupenda Uislamu? Akiwa Makka, alivumilia mateso, njaa, kiu, kunyimwa, ufidhuli na uhamisho, yote hayo kwa ajili ya Uislamu. Wakati alipokuwa Madina alitakiwa kutoa mihanga mikubwa zaidi kwa ajili ya Uislamu. Wawili wa ami zake, binamu zake watatu, watoto wa kufikia wawili na ndugu mmoja wa kunyonya, na marafiki wengi waliuawa katika kuutetea Uislamu. Kwa wakati upasao, akawa mkuu wa Madina lakini hakuna chochote kilichobadilisha mtindo wa maisha yake.

Watu wengi wa jumuiya hiyo mpya walikuwa mafukara, naye aliwalisha. Aliwalisha chakula chake yeye mwenyewe kiasi kwamba mara nyingi, yeye na wanawe walilazimika kukaa na njaa. Hii iliendelea mwaka baada ya mwaka. Alifanya makafara yote haya na mengine yasiyo na idadi kwa ajili tu ya kuufanya Uislamu uweze kuwepo na uwe na nguvu.

Hapo Makka, Maquraishi walimuahidi Muhammad madaraka, utajiri na vivutio kama angeiacha kazi yake kama Mtume wa Uislamu. Lakini alivipiga mateke vyote hivyo. Katika kuvipiga mateke hivyo, alikuwa akiipiga mateke “tamaa.”

Labda haikumjia kwamba kulikuwa na kitu kama tamaa. Kiini hasa cha kazi yake kwa ajili ya Uislamu kilikuwa ni mapenzi yake tu juu yake. Mapenzi haya yalimchukua kutoka mwanzo hadi mwisho.

Alikuwa na “tamaa” moja tu katika maisha, nayo ilikuwa ni kuona Uislamu unakuwa ni wa kudumu. Aliitimiza “tamaa” hiyo kwani tunajua kwamba Uislamu ni wakudumu milele.

c) Muhammad (s.a.w.) hakuteua mrithi wake kwa sababu alikuwa anaogopa upinzani. Muhammad (s.a.w.) alikuwa haijui kabisa hofu. Aliushinda upagani katika wakati ambapo yeye alikuwa peke yake katika dunia nzima, na kwamba dunia yote ilikuwa imejaa uhasama dhidi yake. Upagani ulitumia nguvu zake zote ili kumvunja lakini ulishindwa. Yeye aliuvunja. Kwa kutumia ujasiri wake binafsi, alipata ushindi juu ya dunia nzima. Katika mawili kati ya mapambano ya Uislamu, Waislamu walishindwa, na walikimbia kutoka kwenye medani ya vita. Lakini yeye alisimama imara na hakukimbia, na kwa kweli, alikuwa ni kiungo cha kukusanyikia watoro wa vita. Utulivu wake wa akili ulihuisha ule ushupavu wa Waislamu, na wakarudi vitani.

Baada ya vita ya Hunain, Arabia yote ilikuwa chini ya miguu ya Muhammad (s.a.w.), na hakuna kabila au muungano wa makabila ambao uliweza kushindana na nguvu zake. Nguvu zake, ndani ya peninsula, zilikuwa kubwa. Suala la yeye kuogopa upinzani wa mtu yoyote, kwa hiyo haliji.

Swali la 3: Kwa vile Muhammad (s.a.w.w.) hakuteua mrithi wake mwenyewe, je, aliikabidhi jamii ya Waislamu jukumu hilo la kuteua na kuchagua kiongozi wao wenyewe?

Jibu: Kuteua Mtendaji Mkuu wa umma wa waumini lilikuwa ni jambo muhimu. Muhammad (s.a.w.) alitambua umuhimu wake. Lakini kwa sababu zisizojulikana, alijizuia kumteua. Sababu pekee inayowezekana kwamba hakumteua inaweza kuwa kwamba aliuachia umma jukumu hilo.

Lakini si Abu Bakr na Umar wala wanahistoria wa baadae wa Sunni, ambao wametoa dai hili kamwe. Hawajadai, kwa mfano, kwamba Muhammad Mustafa (s.a.w.) alisema:

“Enyi Waislamu! Sipendi nijichagulie mrithi wangu mwenyewe,” au “Siwezi kujichagulia mrithi wangu mwenyewe,” au “Sina uwezo wa kuchagua mrithi wangu mwenyewe. Kwa vile sina uwezo huo, ninakuachieni ninyi wajibu huo. Nitakapofariki, mnateua na kuchagua kiongozi wenu wenyewe.”

Hakuna hata mtu mmoja aliyejaribu kuhusisha kauli kama hiyo kwa Muhammad Mustafa (s.a.w.). Muhammad Mustafa (s.a.w.) hakuwapa maswahaba zake mamlaka ya kuteua hata mtumishi mdogo seuze kwa kiongozi mkuu wa baadae wa Dola ya Kiislamu!

Swali la 4: Kwa vile jamii ya Kiislamu ilikosa mwongozo juu ya kuteua kiongozi, je, maswahaba wa Muhammad (s.a.w.), kwa ridhaa yao ya pamoja, na kabla ya kuweka kiongozi (au hata baada ya kuchagua kiongozi) waliandaa orodha ya masharti au mwongozo ambao wal- iushika (baadae)?

Jibu: Masahaba wa Muhammad (s.a.w.) hawakuandaa, katika wakati wowote, mfumo wa masharti wa kuwaongoza katika kuchagua kiongozi. Katika jambo hili, walishika kanuni ya kuangalia manufaa yao. Kwanza waliteua kiongozi, na kisha wakaunda “masharti” au “kanuni” kwa ajili ya uchaguzi wake. Waislamu “walichagua” wale makhalifa wa kwanza “walioongoka” wanne. Uteuzi wa kila mmoja wao ulisababisha kugunduliwa kwa “masharti” mapya au “kanuni” mpya. Hizi “kanuni” nne ziliunganishwa ipasavyo katika fikra za kisiasa za Waislamu.

Lakini mara khalifa mpya akaingia madarakani huko Syria. Kuibuka kwake kulisababisha kugunduliwa kwa “kanuni” mpya ijulikanayo kama “ mwenye nguvu mpishe.” “Kanuni” hii ilizifanya zile “kanuni” nne za kwanza kuwa zisizotumika tena. Kutoka wakati huu, ukhalifa ukawa uwe ni tuzo ya mgombea aliyeweza kutumia nguvu ya kinyama kwa ukatili zaidi kuliko wapinzani wake. “Kanuni” hii imepata ukubalikanaji wa kimataifa miongoni mwa Waislamu katika historia yao yote ndefu .

Swali la 5: Upi ulikuwa msimamo na mwenendo wa maswahaba wakubwa wa Muhammad (s.a.w.) juu ya uongozi wa jamii yaWaislamu baada ya kifo chake?

Jibu: Waislamu wa Sunni wanasema kwamba Abu Bakr na Umar ndio walikuwa maswahaba wakuu wa Muhammad Mustafa (s.a.w.). Walikuwa ni wote hao, maswahaba wakuu, ambao walitwaa Dola ya Madina katika wakati ambapo Ali na watu wote wa Bani Hashim walikuwa wakishughulika na mazishi yake.

Mara tu Mtume (s.a.w.) alipofariki, maswahaba zake wakubwa walikusanyika katika Ukumbi wa Saqifah kudai uongozi wa umma. Uongozi huu, kwa maoni yao, ulikuwa ni muhimu sana kiasi kwamba hawakuweza kutulia hata kumzika bwana na mfadhili wao aliyefariki. Kushindania madaraka kwa wazi kuliibuka kwa dakika chache tu za kifo cha Mtume (s.a.w.). Zamakhshari, mmoja wa wanazuoni na wanahistoria wa kuaminika wa Sunni, anaandika kuhusiana na hili, hivi:

“Yalikuwa ni makubaliano ya maswahaba wote kwamba baada ya kifo cha Mtume iliwabidi wateue mrithi wake mara moja. Waliamini kwamba kufanya hivyo ilikuwa ni muhimu zaidi kuliko hata kushughulikia mazishi ya bwana wao. Ulikuwa ni umuhimu huu ambao ulimchochea Abu Bakr na Umar kuhutubia ule mkusanyiko wa Waislamu. Abu Bakr alisema: ‘Enyi watu! hebu nisikilizeni.

Wale kati yenu waliokuwa wakimuabudu Muhammad, nawajue ya kwamba amekufa; lakini wale waliokuwa wakimuabudu Allah, nawajue kwamba Yuko hai, na kamwe hatakufa. Kwa vile Muhammad amekufa, inawabidi sasa muamue ni nani atakayekuwa kiongozi wenu wa baadae.’ Wakasema: ‘Umesema kweli; ni lazima tuwe na kiongozi mpya.’ Sisi Sunni na Mu’tazili, tunaamini kwamba umma wa Waislamu ni lazima kwa wakati wote usikae bila ya kiongozi. Mantiki peke yake inaamuru hivi. Pia, Mtume wa Allah (s.a.w). alitekeleza sheria, na alitangaza rasmi amri kuhusu kuulinda Uislamu, na ulinzi wa Madina na ulinzi wa Arabia. Baada ya kifo chake, anapaswa awepo mtu wa kutekeleza sheria zake, na kutekeleza amri zake.”

Kutokana na ushahidi huu uliopita, ni dhahiri kwamba maswahaba wa Mtume (s.a.w.) walitambua ilivyokuwa muhimu kwa umma kupata kiongozi. Walijua kwamba kama hapakuwa na mtu wa kutekeleza sheria na amri alizozitangaza, umma wake ungeangukia kwenye vurugu.

Hali hiyo imejawa na kejeli. Masahaba waliridhika kwamba ilikuwa ni muhimu sana kwa umma wa Waislamu kuwa na mtendaji mkuu lakini kulikuwa na mtu mmoja ambaye hakuamini kwamba ilikuwa muhimu, naye alikuwa ni Muhammad (s.a.w.)! Ingawaje kama angeamini hivyo, angeupatia umma huo mtendaji mkuu. Alikuwa ndiye mtu pekee ambaye haikujitokeza kwake kwamba palipaswa kuwa na mtu wa kutekeleza zile sheria na amri ambazo yeye mwenyewe alikuwa amezitangaza rasmi.

Hao maswahaba wakubwa hawakuhudhuria mazishi yake. Kwao wao, kilichokuwa na umuhimu zaidi kuliko kuhudhuria mazishi ya bwana wao, kilikuwa ni kupata kiongozi mpya. Tatizo hili lilikuwa gumu sana lakini “walilitatua” kwa kumchagua mmoja kati yao, yaani, Abu Bakr, kama kiongozi mpya wa Waislamu.

Miaka miwili baadae, Abu Bakr alikuwa amelala akifariki. Juu ya kitanda chake cha mauti, alimteua Umar kuwa mrithi wake, na kiongozi wa Waislamu. Katika kumteua Umar kama mrithi wake, hakujua tu kwamba alikuwa anatekeleza wajibu wake muhimu sana bali ali- tambua kwamba kama hakufanya hivyo, atakuwa mwenye kuulizwa mbele za Allah kwa kushindwa kwake kufanya hivyo.

“Asmah, mke wa Abu Bakr, anasema kwamba wakati mume wake alipokuwa kwenye kitanda chake cha mauti, Talha alikuja kumuona, naye akasema: ‘Ewe Abu Bakr! umem- fanya Umar kuwa amir wa Waislamu, na unajua kabisa kwamba alikuwa dhalimu mno wakati ulipokuwa khalifa. Bali sasa kwa vile atakuwa na uhuru wa kufanya atakalo, sijui ni vipi atakavyowaonea Waislamu. Baada ya muda mfupi utafariki, na utajikuta mwenyewe mbele ya Allah (s.w.t.) Katika muda huo utatakiwa kumueleza Yeye juu ya matendo yako. Je, umeandaa tayari majibu yako?’
Abu Bakr akakaa juu ya kitanda hicho, na akasema: ‘Ewe Talha! je, unajaribu kunitisha mimi? Sasa sikiliza, kwamba pale nitakapokutana na Mola wangu, nitasema kwamba nilimchagua mtu aliye bora kama amir wa umma wa Waislamu.’

Abu Bakr aliongeza kwamba elimu na uzoefu wake juu umma ya Umar vilimthibitishia yeye kwamba hakuna mtu katika wa Waislamu ambaye angeweza kuubeba uzito wa ukhalifa vizuri zaidi kama ambavyo yeye (Umar) angeweza. Alikuwa, kwa hiyo, na imani kwamba majibu yake yatamridhisha Allah (s.w.t.)

Abu Bakr alijua kwamba atakuja kujitetea mwenyewe katika Mahakama ya Allah (s.w.t.) kwa kumteua Umar kama mtawala wa Waislamu. Aliridhika kwamba asingeweza kumchagua mtu mwingine bora zaidi kuliko Umar kuwa mrithi wake. Na wasiwasi wa Talha juu ya kuwajibika kwa Abu Bakr mbele Allah, unaonyesha tu uangalifu wake kuhusu wajibu wake wa “kuamrisha wengine kufanya mema na kukataza maovu.”

Kejeli tena! Masahaba wote walikuwa waabudu-masanamu kabla ya Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), aliyebarikiwa, hajawasilimisha kwenye Uislamu. Sasa, wao kama Waislamu wa dhati, walikuwa wanatambua kwamba walikuwa ni wenye kuwajibika kwa Allah (s.w.t.) kuhusu wajibu wao wa kuchagua mrithi wake.

Lakini cha ajabu, na cha kushangaza, alikuwepo mtu mmoja ambaye ni dhahiri hakuwa na ufahamu kwamba, siku moja, yeye pia atakuja kusimama katika Mahakama ya Allah (s.w.t.), na kuulizwa kuhusu wajibu wake wa kuchagua mrithi wake. Yeye alikuwa ni Muhammad (s.a.w.), Mtume Wake Mwenyewe Allah (s.w.t.)! Waislamu wanaamini kwamba Abu Bakr alikuwa tayari kutetea kitendo chake cha kuchagua mrithi wake, kwa majibu ambayo alijua, yatamridhisha Allah (s.w.t.) Je, wanaamini pia kwamba Muhammad, Mtume wao, alikuwa tayari kutetea kushindwa kwake kuteua mrithi wake mwenyewe, kwa majibu ambayo Allah (s.w.t.) atapata kuridhika nayo?

Baada ya kifo cha Abu Bakr, mrithi wake, Umar ibn al-Khattab, alitawala kama khalifa kwa miaka kumi. Katika miaka ya mwisho ya uhai wake, alionekana mara kwa mara akiwa katika lindi la mawazo. Kila alipoulizwa na marafiki zake, kama alikuwa akifikiria juu ya nini, alisema: “Sijui nifanye nini kwa umma wa Muhammad, na jinsi ya kuteua amir atakayeuongoza baada ya kufa kwangu.”

Ni wazi kwamba Umar aliona kuteua mrithi wake lilikuwa ni jambo la umuhimu mkubwa sana kwa jinsi alivyotumia muda wake mwingi na akili kwenye suala hilo.

Wasiwasi wa Umar kuhusu uongozi wa umma baada ya kifo chake mwenyewe, ulichangi- wa na Aisha, mjane wa Mtume (s.a.w.). Tabari, mwanahistoria huyu, anasimulia yafuatayo kuhusiana na hili: “Wakati Umar alipokuwa anafariki, alimtuma mwanae kwa Aisha kuomba ruksa ya kuzikwa karibu na Mtume na Abu Bakr. Aisha akasema: ‘Kwa furaha kubwa,’ kisha akaongeza: ‘Nitolee Salam zangu kwa baba yako, na mwambie kwamba asije akawaacha Waislamu bila ya kiongozi vinginevyo kutakuwa na vurugu baada ya kifo chake.’”

Aisha alionyesha wasiwasi mkubwa sana juu ya ustawi wa Waislamu kama vile tu ambavyo angepaswa kufanya. Wakati Umar alipokuwa anafariki, alimshauri asiuache umma bila ya kiongozi, ama sivyo, alionya, ghasia zitafuatia kifo chake. Inashangaza kwamba Aisha hakuwahi kumshauri mume wake mwenyewe kuteua kiongozi kwa ajili ya Waislamu, na hakumuonya kwamba ghasia zitafuatia kifo chake kama angewaacha bila ya kiongozi.

Lakiini Aisha, binti ya Abu Bakr, alikuwa na sababu nzuri tu ya kuwa na “makini” na mume wake, na hakulileta kwenye mjadala pamoja naye, suala la uteuzi wa mrithi, wakati wowote.

Swali la 6: Upi ulikuwa mwenendo (sunnah) wa Muhammad (s.a.w.) kuhusiana na uteuzi na uwekaji wa watumishi?

Jibu: Katika miaka kumi ya mwisho ya maisha yake, Muhammad (s.a.w.) aliandaa misafara ya kijeshi zaidi ya themanini. Aliwatuma wengi wao chini ya amri ya kiongozi fulani; mingine aliiongoza yeye binafsi.
Wakati wowote Muhammad (s.a.w.) alipotuma msafara nje, aliteua mmoja wa maswahaba zake kama kapteni wake. Aliwaamuru wale wapiganaji wa kawaida kumtii yeye, na akamfanya huyo kapteni kuwajibika kwake yeye mwenyewe Mtume. Pale msafara uliporudi Madina, alimhoji yule kapteni ili kupata taarifa. Haikuwahi kutokea kwamba aliwaambia watu wa msafara au kikosi cha upelelezi kwamba walipaswa kuchagua au kuteua kapteni wao wenyewe.

Katika kadhia ambapo Muhammad (s.a.w.) alipokuwa akiongoza mwenyewe msafara nje ya Madina, aliteua gavana wa mji huo, na akamfanya mwenye mamlaka ya kusimamia sheria na maagizo wakati wa kutokuwepo kwake yeye mwenyewe. Hakuwahi kuwaambia raia kwamba katika kipindi ambacho hatakuwepo, ilikuwa ni wajibu wao kujichagulia au kujiteulia gavana wao wenyewe.

Katika mwaka 630 ambapo Muhammad (s.a.w.) aliiteka Makka, na kuijumuisha kwenye ile Dola mpya, aliteua mtawala kwa ajili ya mji ule, na alifanya hivyo bila ya kushauriana ama na watu wa Makka au na maswahaba zake mwenyewe.

Montgomery Watt:

“Kiasi cha madaraka ya utawala wa Muhammad katika miaka yake miwili au mitatu ya mwisho kinadhihirishwa na uteuzi wake wa “wakala” kusimama badala yake katika maeneo mbalimbali, na kwa hakika na suala zima la uteuzi wa nafasi za utawala. Tokea mwanzoni Muhammad aliteua watu kufanya shughuli mbalimbali ambazo yeye alihusika nazo. Hivyo aliteua makamanda wa misafara ambapo yeye hakuwepo binafsi. Uteuzi mwingine wa kawaida tangu nyakati za awali kabisa ulikuwa ni ule wa Kaimu hapo Madina wakati Muhammad alipokuwa hayupo hapo mjini. (Muhammad at Madina, 1966)

Maxime Rodinson:

“Yeye (Mtume) ama aliteua kiongozi au alichukua mamlaka mwenyewe. Anaelekea kuwa alikuwa na kipaji cha kijeshi kama alichokuwa nacho kwenye mikakati ya kisi- asa. Alikabidhi baadhi ya shughuli zake kwa watu ambao walikuwa kama mawakala wake binafsi. Wakati wowote, kwa mfano, alipoondoka Madina, alikuwa akiacha mwakilishi nyuma yake. (Muhammad, kilichotafsiriwa na Anne Carter, 1971)

Hiyo ilikuwa ndio sera na mwenendo wa Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), katika kuteua na kuweka watumishi wake, na kamwe haukuwa na ukengeukaji ndani yake kwa wakati wowote.

Swali la 7: Ni ipi Fatwa ya Qur’an juu ya mwenendo (sunnah) wa Muhammad (s.a.w.)?

Jibu: Kwa mujibu wa Qur’an, vitendo vya Muhammad ni vitendo vya Allah (s.w.t.) Mwenyewe. Msomaji mwislamu anatakiwa atafakari juu ya maana ya Aya zifuatazo za Qur’an Tukufu:

وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ رَمَىٰ ۚ{17}

Wakati ulipotupa (ukufi wa mchanga), Sio wewe uliyetupa, bali ni Allah Aliyetupa…
(Sura ya 8; Aya ya 17)

إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّهَ يَدُ اللَّهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ فَمَنْ نَكَثَ فَإِنَّمَا يَنْكُثُ عَلَىٰ نَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللَّهَ فَسَيُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا {10}

Bila shaka wanaofungamana nawe,kwa hakika wanafungamana na Allah;Mkono wa Allah uko juu ya mikono yao:basi anayevunja ahadi yake, anavunja kwa kuidhulumu nafsi yake, na anayetekeleza alimuahidi Allah,Allah atamlipa ujira mkubwa. (Sura ya 48; Aya ya 10)

Waislamu wote wanaamini kwamba chochote alichokisema au kukitenda Muhammad (s.a.w.), kilikuwa ni wahyi kutoka Mbinguni. Kwa maneno mengine, alikuwa ni chombo ambacho amri za Mbinguni zilitekelezwa kupitia kwake.

Kama ilivyoelezwa kabla, Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w) hakuchangia pamoja na mtu yeyote yule mwingine mamlaka yake ya kuteua gavana kwa ajili ya mji, au jemadari kwa ajili ya msafara wa kijeshi. Yeye na yeye peke yake aliyatekeleza tokea mwanzo hadi mwisho.
La muhimu zaidi kuliko uteuzi wa gavana au jemadari, ilikuwa ni uteuzi wa mrithi wake mwenyewe, na mkuu wa baadae wa umma wa Waislamu. Hakukuwa na sababu ya kuigeuka sera na mwenendo wake mwenyewe, na kuuacha umma wake wote bila ya kiongozi. Tabia yake ilikuwa yenye msimamo thabiti, na ufuatao ni ushahidi wa Qur’an Tukufu:

فَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَبْدِيلًا ۖ{43}

“Hutapata mabadiliko katika mtindo wa Allah (wa utendaji), hutapata mageuko katika mwendo wa Allah (wa utendaji). Sura ya 35; Aya ya 43)

Huo (ulikuwa) ndio mwendo wa Allah (ulithubutu) uliokwisha pita zamani:

وَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّهِ تَبْدِيلًا {23}

Wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Allah (uliothubutu). (Sura ya 48; Aya ya 23)

Hakukuwa na mabadiliko katika mwenendo wa Mtume wa Allah (s.a.w.w). Hakuwatelekeza Waislamu ili waje kuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Alimteua binamu yake Ali ibn Abi Talib, kuwa mrithi wake, na kiongozi mkuu wa baadae wa umma wa Waislamu. Alimtambulisha Ali kwa umma huo kama mtawala wa baadae, katika Karamu ya Dhu’l-‘Ashiira, mara tu baada ya tangazo la kwanza, hadharani la ujumbe wake kama Mtume wa Mwisho na Mkuu kabisa wa Allah (s.w.t.) ulimwenguni.

Swali la 8: Muhammad (s.a.w.) alifanya nini hasa kuhusu kurithiwa kwake?

Jibu: Muhammad aliunda Dola mpya – Dola ya Kiislamu. Katika kuunda Dola hiyo ya Kiislamu, lengo lake lilikuwa ni kuanzisha Ufalme wa Mbinguni Duniani. Hili alilifanya kwa msaada na ushirikiano wa binamu yake, Ali ibn Abi Talib. Alimchagua Ali miongoni mwa maswahaba zake wote, kumfuatia yeye, kama mkuu wa Dola ya Kiislam, na kama Mtawala wa Waislamu wote.

Kumteua Ali kama mrithi wake, Muhammad hakusubiri mpaka alipokuwa ameiunda hasa hiyo Dola ya Kiislam, na kuiimarisha kama ufalme wa mbinguni na duniani. Alimtangaza Ali kuwa mrithi wake katika wakati ambapo Dola hiyo haijawa na uhai wowote. Alimtangaza Ali kuwa mrithi wake katika wakati uleule alipotangaza kwamba Allah (s.w.t.) amemtuma yeye kama Mtume Wake wa Mwisho kwa wanadamu.

Muhammad (s.a.w.) alimtaja Ali ibn Abi Talib kama mrithi wake kwenye Karamu ya Dhu’l-‘Ashiira huko Makka wakati yeye Ali akiwa na umri wa miaka kumi na tatu tu; na alitumia muda wa uhai wake wote kumuandaa yeye kwa ajili majukumu mazito yaliyokuwa mbele yake.

Miaka ishirini baadae, katika bonde kubwa la Khum, karibu na Ghadiir, Muhammad (s.a.w.) alifanya matengenezo ya mwisho katika kazi yake aliualika umma wake, kwenye mkusanyiko mkubwa, kukutana na mkuu wao wa baadae. Kwa kufanya hivyo, alifuata amri ya Mbinguni iliyohifadhiwa katika Aya ya 70 ya Sura ya tano ya Qur’an Tukufu; na alitimiza wajibu wake juu ya umma wake. Umma wake ulikuwa na haki ya kujua ni nani atakaye uongoza baada ya kifo chake (yeye Muhammad).

Muhammad Mustafa (s.a.w.) hakumteua Ali kuwa mrithi wake kwa kufafanua au kutafsiri tu sheria za Kiislam. Alimteua Ali kuwa mrithi wake kwa kuzitenda na kuzitekeleza sheria hizo. Kwa maneno mengine, alimteua Ali kuongoza serikali ya Kiislam.

Kama kuna sheria, lazima awepo mtu wa kuidumisha – katika dola ya mji wa Madina – kama kwingineko. Kitendo pekee cha kupitisha sheria hakina maana yoyote. Yenyewe peke yake, sheria haiwezi kuhakikisha usalama, ustawi na furaha ya mwanadamu. Baada ya sheria kupitishwa, ni muhimu pia kuunda nguvu ya utendaji, ya kuitekeleza. Kama sheria haiwezi kudumishwa, haiwi ni chochote zaidi ya kipande cha karatasi. Kama serikali inakosa mamlaka ya utendaji, haiwezi hata kuitwa ni serikali. Kwa hiyo, pale Uislamu ulipopitisha sheria, uliunda pia mamlaka ya utendaji.

Katika wakati wa Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), sheria hazikuwa zikifafanuliwa na kutangazwa rasmi tu; zilidumishwa na kutekelezwa pia. Yeye alizidumisha na kuzitekeleza.
Muhammad (s.a.w.) alimteua Ali kudumisha sheria za Kiislamu, na kutekeleza amri za Allah kama zilivyoshushwa kwake ndani ya Qur’an. Alimteua Ali kushika mamlaka ya utendaji juu ya Waislamu, baada ya kifo chake yeye mwenyewe.

Swali la 9: Ni nini hasa kilichotokea baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.)?

Jibu: Baada ya kifo cha Muhammad Mustafa, aliyebarikiwa, Ansari walijikusanya katika banda la Saqifah ili kuchagua kiongozi. Abu Bakr, Umar na Abu Ubaidah – Muhajirina hawa watatu – waliwatembelea. Waliwaambia hao Ansari kwamba kwa vile Muhammad (s.a.w.) hakuteua mrithi wake, iliwabidi wachagua mtu wa kujaza nafasi hiyo. Kitendo chao, walisema, hakikuwa tu ni halali bali pia kilikuwa ni muhimu sana, ikiwa ni kwa kuuokoa umma kutokana na vurugu na ghasia.

Hawa Muhajirina watatu waliingia kwenye majadiliano makali na Ansari mle Saqifah. Mada ya mjadala huo ilikuwa: ‘Je, mrithi wa Muhammad (s.a.w.) na mtawala wa Waislamu awe ni Muhajir (wa Makka) au Ansari (wa Madina).’ Wasemaji wakali waliijadili mada hii vya kuchosha.

Ingawa kulikuwa na mambo mengine muhimu ambayo hayakuwa kwa jumla yasiyohusi- ka kwenye mjadala huo, kama vile matakwa ya Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.), sifa zilizohitajika kwa mgombea au wagombea kwenye nafasi iliyowazi ya mtawala wa Arabia, na maslahi ya Uislamu na umma wa Waislamu, hayo hayakujadiliwa. Masuala haya hayakuwemo kwenye “ajenda” za mkutano huo mle Saqifah. Wasemaji hao, kwa hiyo, hawakutoka nje ya mada yao.

Hatimaye, kwa ustadi, uvumilivu na kwa maarifa, hawa Muhajirina watatu walilisuluhisha kwa mapatano tatizo hili, au, kiasi, walitunga “papo kwa papo” ufumbuzi wake.

Francesco Gabrieli:

“Katika lile baraza la vurugu lililofanyika kwenye makao makuu ya Banu Sa’idah hapo Madina, Umar, takriban kama kwa kushitukiza, alimuweka Abu Bakr kama khalifa au mrithi wa Mjumbe wa Allah. Kama matukio mengi na asasi nyingi, ukhal- ifa ulizaliwa katika ufaraguzi. (The Arabs – A Compact History,1963)

Ukhalifa au uongozi wa umma wa Waislamu ndio taasisi muhimu sana ya kisiasa katika Uislamu wote.

Kwa kweli, kuweko hasa kwa Uislamu kunategemea juu ya khalifa au kiongozi wa umma. Kwa hiyo, haisadikiki kwamba uliachwa si kwenye ubora wowote bali ufaraguzi! Itakuwa haishangazi kwamba ulimwengu wa Kiislamu umekuwa mara kwa mara umefunikizwa kwenye damu juu ya suala la urithi na uongozi.

Vita, mapambano ya wenyewe kwa wenyewe, mapinduzi, migogoro, uchochezi na ghasia zimekuwa haziepukiki wakati umma ulipochagua ufaraguzi mle Saqifah, badala ya kielelezo cha ki-ungu na “mpango” wa majaaliwa wa Muhammad Mustafa (s.a.w.), kwa ajili ya upokezanaji wa utaratibu mzuri na wa amani wa mamlaka kutoka kwake mwenyewe kwenda kwa mrithi wake.

Watetezi wa Saqifah wanasema kwamba kitendo cha Umar kilichochewa na shauku yake ya kuzuia uongozi wa umma kutokana na kuwa daima mali ya familia moja – hasa, familia ya Muhammad Mustafa (s.a.w.). Wanasema kwamba ukiritimba kama huo wa mamla- ka ungeweza kuwa ni “janga” kwa Uislamu. Hoja hii ambayo ni ngumu kueleweka, ya wanahistoria wa Sunni imekuwa ni kipokeo cha kawaida na kisichoeleweka cha siku-za- baadae kinachoimba maangamizi. Lakini hakuna hata mmoja kati yao ambaye amewahi kueleza ni kivipi.

Kama baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.) utawala wa Waislamu ungegeuka kuwa “mali” ya familia yake mwenyewe, hivi Waarabu wangeukana Uislamu, na kurudi kwenye uabudu masanamu? Au Waajemi na/au Warumi wangeivamia na kuiteka Arabia na kuwaangamiza Waislamu wote?

Katika mawazo ya Abu Bakr na Umar, kulikuwa na njia moja tu ya “kuuokoa” umma wa Muhammad (s.a.w.) kutokana na “janga,” na hiyo ilikuwa ni kwa kuikataa familia yake kwenye uchaguzi, na kwa kujitwalia serikali yake wao wenyewe!
Umar alikuwa na shauku kwamba ukhalifa usije ukawa ni wa kurithiana katika ukoo mmoja wowote ule, na kwamba unapaswa kubaki ukizunguka miongoni mwa Waislamu ili kwamba “kila kijana wa Kiarabu aweze kuwa na bahati ya kuwa khalifa.” Hata hivyo, licha ya ndoto na tahadhari juu ya mambo ya baadae ya Umar, ukhalifa ulikuja kuwa wa kurithiana ndani ya miaka kumi na sita ya baada ya kifo chake mwenyewe.

Lakini ulikuwa wa kurithiana siyo katika familia ya Muhammad (s.a.w.) bali katika familia ya maadui zake wakuu – wale watetezi wa upagani wa Makka - wale watoto wa Abu Sufyan na Hinda. Hivyo ndoto za Umar hazikuendelea zaidi ya miaka kumi na sita labda kama lilikuwa ni lengo lake kwamba ukhalifa uje kuwa wa kurithiana katika nyumba ya Abu Sufyan. Kama ilikuwa hivyo, basi lazima ikubalike kwamba yeye alikuwa ni mtu wa ajabu kweli kutokana na ndoto zake.

Abu Bakr na Umar walifanikisha muujiza wa ufaraguzi mle Saqifah.

Akizungumzia juu ya machafuko kufuatia kifo cha Muhammad (s.a.w.), na akitoa sababu zake za kwa nini binamu yake, Ali, alikataliwa katika kugombea ukhalifa, Sir John Glubb anaandika hivi: “Waarabu hawakuwa tayari kamwe kutoa heshima kwenye fahari, daraja, au fursa za kurithiana au vyeo.
(The Great Arab Conquests, 1963)

Uchambuzi huu, wa mwanahistoria huyu, wa tabia ya Kiarabu, unakwenda kinyume na ushahidi wa historia. Watawala wa kale wa Uturuki (Seljukes), Mamluki, na watawala wa Uthmainia (Ottoman Turks) waliwatawala Waarabu kwa karne nyingi. Waarabu waliwatii kama kondoo. Wao, kwa kweli, waliukubali ule usemi usio na uthibitisho wa kwamba Waturuki wawe wanaamrisha, na wao Waarabu wawe ni wenye kutii.

Hakuna yeyote anayeweza kusema ni kwa muda mrefu kiasi gani zaidi huo utawala wa Kituruki juu ya ardhi za Waarabu ungechukua kama Waingereza na Wafaransa wasingeusimamisha.

Katika kusalimu amri kwao kwa jumla na kwa kinyonge kwa Waturuki, Waarabu walikuwa wakitoa heshima kabisa kwenye “fahari, daraja au fursa za kurithiana au vyeo.” Kwa karne nyingi Waturuki walizitawala nchi za Kiarabu kwa ukali, na hakuna aliyewahi kusikia manung’uniko japo madogo sana ya upinzani kutoka kwa Waarabu.

Kwa hakika, Waarabu hawana tofauti na watu wengine ikiwa ni pamoja na Waingereza, ambao na mwanahistoria huyu mwenyewe anatokana nao. Kama wengine wanatoa heshi- ma kwenye fahari, daraja, au fursa na vyeo, Waarabu nao wanatoa heshima kwavyo. Haieleweki ni kwa nini Sir John Glubb ana shauku ya kufanya mambo ya kutukuzwa sana kwa Waarabu!

Mwandishi huyo huyo anaendelea kusema: “(Utawala wa) Kurithiana hakukukubaliwa na Waarabu kama msingi wa kufaa wa kupokezana mamlaka. Katika uteuzi wa wakuu wa kawaida, mgombea aliyefaa zaidi, wa familia inayotawala kwa kawaida ndiye aliyechaguliwa. Katika uteuzi wa khalifa, chaguo la kawaida kabisa, na lile ambalo katika nadharia ndilo lilifanywa katika kadhia za wale wanne wa kwanza, lilikuwa ni lile la kiongozi wa Kiislam anayefaa zaidi.

Kwa vitendo ugumu wa kuteua mgombea safi na hatari inayojitokeza ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mara nyingi ulisababisha matumizi ya haki ya kurithi kwa mtoto wa kwanza katika falme za Kiislamu za baadae. Waarabu, hata hivyo, kamwe hawakuutwaa ule utaratibu wa urithi wa moja kwa moja wa mtoto mkubwa.” (The Great Arab Conquests, 1963)

Mwanahistoria huyu, inavyoelekea, kwa mara nyingine tena, yuko kinyume na mambo. Pale anaposema kwamba kurithiana kamwe hakukukubaliwa na Waarabu kama msingi unaofaa wa kupokezana mamlaka, anapaswa kuweka wazi, kwamba Waarabu anaowazungumzia, walitokana na kizazi cha wakati wa Mtume (s.a.w.) mwenyewe, na sio na wale waliokuja baada yake.

Ndani ya miaka thelethini ya kifo cha Mtume (s.a.w.), Waarabu hao hao walikuwa wakinyenyekea kwa miguuni kwa yule khalifa wa Syria, na waliukubali urithianaji kama msingi unaofaa wa kupokezana mamlaka bila haya. Sio kwamba walimkubali tu Yazid, mtoto wa Mu’awiyah, kama khalifa wao halali, bali kwa miaka 600 iliyofuatia, yaani, mpaka kukomeshwa kwa ukhalifa wenyewe mnamo mwaka 1258, hawakuwahi kuuliza swali kuhusu haki ya mtoto wa khalifa kumrithi baba yake.

Geoffrey Lewis:

“Kwa khalifa wa tano, yule mwenye nguvu sana Mu’awiyah (661–680), cheo hicho (ukhalifa) kilikuwa ni cha kurithiana kiukoo. Utawala wake wa Bani Umayya ulichukuliwa nafasi yake na ule wa Bani Abbas mnamo mwaka 750.” (Turkey, 1965)

Dr. Hamid-ud-Din:

“ Kuanzia wakati wa Mu’awiyah, kiti cha ukhalifa kilikuwa ni haki ya kurithiwa ya Bani Umayya. Kila khalifa alimteua mwanae au ndugu mwingine yoyote kama mrithi wake, na Waislamu kwa unyenyekevu kabisa walimkubali kama khalifa wao, nao hawakuuliza maswali.”
(History of Islam, 1971, uk. 364 kilichotolewa na Ferozsons Ltd, Karachi na Lahore,Pakistan).

Waarabu pekee ambao hawakukubali urithianaji wa kiukoo kama msingi wa kupokezana mamlaka, walikuwa ni maswahaba wa Muhammad (s.a.w.) mwenyewe. Sababu yao ya kutokubali urithianaji kama msingi wa kupokezana mamlaka, ilikuwa ni mtazamo wa hekima. Kama wangekubali urithianaji wa kiukoo kama msingi wa kupokezana mamlaka, basi kungekuwa hakuna njia ya wao kuwa makhalifa.

Katika nadharia ya Shia juu ya serikali, urithianaji wa kiukoo hauchukuliwi kama msingi wa kupokezana mamlaka. Kwa mujibu wa nadharia ya Shia, haki ya kuchagua mrithi wake mwenyewe, ilihusika pekee kwa Muhammad Mustafa (s.a.w.), na sio kwa maswahaba zake; na yeye alimchagua Ali.

Na hakumchagua Ali kwa sababu ya udugu, bali kwa sababu ilikuwa ni amri ya Allah (s.w.t.) kwake yeye kufanya hivyo.

Pale Waarabu walipokataa kukubali kule kuteuliwa na Muhammad Mustafa (s.a.w.) kwa Ali ibn Abi Talib kama mrithi wake, hawakuwa kwa hakika wakitetea “kanuni.” Kukataa kwao kulikuwa ni mwanzo tu wa kuondoa kituo maalum cha madaraka na mamlaka kutoka kwenye nyumba ya Muhammad (s.a.w.). Mara tu “kanuni” ilipotimiza lengo lao, wao – Waarabu – walikuwa wa kwanza kuitelekeza.

Laura Veccia Vaglieri:

“Kuelekea mwishoni mwa utawala wake, Mu’awiyah, akitumia ustadi wake wote wa kidiplomasia, alimudu kuwashawishi wale watu mashuhuri wa himaya hiyo kumtambua mwanae Yazid kama mrithi kwenye utawala, bila kuigusa ile kanuni kwamba heshima kuu lazima itolewe katika muda wa kurithi. Kwa njia hii alipata muafaka. Kinadharia, hiari ya wachaguzi iliheshimiwa, kwa vile ilikubalika kwamba wanaweza kumkataa yule mrithi aliyeteuliwa na mkuu anayetawala (kwa kweli, ni watu mashuhuri wanne au watano tu waliokataa kuridhia ombi la Mu’awiyah), lakini kwa hali halisi hii ilidokeza kufutwa kwa mfumo wa uchaguzi, ambao ulikuwa ndio chan- zo cha matatizo mengi huko nyuma, na ilianzisha urithianaji wa kiukoo. Mageuzi ya Mu’awiyah yalifuatwa na makhalifa wote waliokuja baada yake, na yaliwawezesha Bani Umayya kushikilia madaraka kwa miaka 90, na Bani Abbas kwa karne tano.”
(Cambridge History of Islam, 1970)

Mu’awiyah alipuuza ile “kanuni” ya uchaguzi ambayo haikuwa ni chochote zaidi ya kichekesho hata hivyo.

Hata hivyo, katika shughuli yote hii iliyopinda ya “kuchagua” au “kupendekeza” au “kuteua” mtawala wa Waislamu, kulikuwa na “kanuni” mmoja iliyokuwa ikifanya kazi. ilikuwa ni ile “kanuni” ya kuwaondoa watu wa familia ya Muhammad Mustafa Mtume wa Allah (s.a.w.) aliyebarikiwa, kutoka kwenye mahali maalum pa madaraka na mamlaka. Saqifah, kwa kweli, ilikuwa ni vuguvugu ya nguzo imara, iliyounganishwa na kuchanganyika ya maswahaba wakubwa na wasaidizi wao ya kuwaondoa Bani Hashim kutoka kwenye serikali ya Kiislam. Kama ungekuwepo msimamo thabiti wowote ama kati- ka matendo ya makhalifa watatu wa kwanza, au, mwingine wa maswahaba, au wa Bani Umayya na Bani Abbas, ulikuwa ni katika kuitumia “kanuni” hii. Katika jambo hili, yalikuwepo makubaliano miongoni mwao wote. Ilikuwa ndio asili na kiungo muhimu cha sera yao wote iliyopangwa na kuratibiwa. Hata kwa zile falme ambazo zilikuwa zifuatie za Bani Umayya na Bani Abbas, ishara za Saqifah zilikuwa na nguvu, dhahiri na bayana.

Walifuata masharti, kwa uaminifu, takriban kwa ushabiki uliokithiri ya “sera” iliyoundwa kwenye ukumbi wa Saqifah. Kiini cha sera ile kilikuwa ni uadui wa wazi kwa Ali ibn Abi Talib, binamu wa kwanza wa Muhammad (s.a.w.), na kwa Bani Hashim, ukoo wa Muhammad (s.a.w.).

Swali la 10: Je, suala la urithi lina umuhimu gani katika historia kwa jumla?

Jibu: Suala la kurithisha au kuhamisha madaraka kutoka kwa mwenye cheo mmoja kwenda kwa mwingine, limekuwa moja ya matatizo magumu na yenye mzozo ya historia ya mwanadamu. Katika kadhia nyingi, tatizo hili limetatuliwa katika juhudi ambamo mbinu zote zinakubalika, na madaraka yamekuwa ni tunzo la yule aliyekatili zaidi kati ya wagombea. Ukweli kwamba taifa lina serikali ya kikatiba, hakuihakikishii kwamba itakingika kutokana na ugombaniaji wa madaraka. Ugombeaji wa Stalin na Trotsky baada ya kifo cha Lenin mnamo 1924, na kuuawa kwa Beria baada ya kifo cha Stalin mnamo 1953, ni miwili kati ya mifano mingi kutoka kwenye historia ya sasa.

Kwenye matukio yasiyo na idadi ndani ya historia, suala la urithi limechokonoa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambamo wanaume na wanawake wasio na idadi wameangamia. Wengi wetu tunaweza kushawishika kujigamba kwamba tumepitia zama hizo za kikatili ambamo maelfu ya wanaume na wanawake waliuawa kabla suala la ni nani atakayekuwa mtawala halijafumbuliwa.

Lakini hakuna sababu ya kutojali. Kugombea madaraka kunaweza kuibuka mahali popote wakati wowote bila kukwepa tu baadae kama ilivyotokea huko nyuma. Harakati za kichini chini huenda zinatokota wakati wote lakini kwa hakika zinakuja kuchemka wakati kiongozi wa nchi atakapofariki.

Geoffrey Blainey:

“Uchunguzi wa sababu zinazofanana kwenye vita nyingi za karne ya kumi na nane unaonyesha ishara moja ya wazi. Kifo cha mfalme kilikuwa mara nyingi ndio dalili ya vita. Kiungo kinawakilishwa kwenye majina maarufu yaliyotolewa kwenye vita nne muhimu. Kwa namna hii kulikuwa na Vita ya urithi wa Hispania, na vita ya urithi wa Uholanzi, na zilifuatiwa na vya urithi wa Australia na kisha wa Bavaria. Majina yao kiushawishi yanamaanisha kwamba suala la nani afuatie kwenye kiti kilichokuwa wazi lilikuwa ndio chanzo kikuu cha vita hizo.

Vita hizi nne za urithi hazikuwa ndio vita pekee ambazo zilitanguliwa na kushawishiwa na kifo cha mtawala. Mnamo mwaka 1700, watawala wa Saxony, Denmark na Urusi waliingia vitani dhidi ya Sweden ambayo mtawala wake kijana, Charles X11, hajakaa muda mrefu kwenye madaraka. Katika mwaka wa 1741 vikosi vya Sweden vilivamia Urusi, ambayo mfalme wake wa kabla ya mapinduzi, alikuwa na umri wa mwaka mmoja. Mnamo 1786 kifo cha Frederick Mkuu wa Prussia aliandaa njia ya mapambano ya Austri-Russia dhidi ya Uturuki katika mwaka uliofuata.

Na mnamo Machi, 1792 kifo cha Mfalme Leopold II huko Vienna kilikuwa ni moja ya matukio yaliyoashiria Tangazo la Ufaransa la vita dhidi ya Austria katika mwezi uliofuatia.

Katika vita zote nane za karne ya kumi na nane ziliashiriwa na kushawishiwa na kifo cha mfalme; na vita hizo zilianzisha nyingi ya vita kubwa za karne hiyo. Wala vita hivyo vya kukesha na mgonjwa anayekaribia kufa havikukoma kabisa baada ya 1800. Hivyo vita mbili kati ya Prussia na Denmark zilitanguliwa na vifo vya wafalme wa Kidenishi, vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani vilifuatia kifo cha raisi mnamo 1861, Vita Vikuu vya Kwanza vilitanguliwa na kuuawa kwa mrithi wa Austria.” (The Causes of War, 1973)

Kugombea madaraka ni tabia ya kudumu ya historia ya mwanadamu. Huko nyuma, kwa mara nyingi kifo cha mfalme kilikuwa ni ishara ya maasi katika nchi yake mwenyewe. Kama alikuwa ameikamata nchi pamoja kwa uongozi madhubuti, kifo chake kilichukuli- wa kama ni fursa ya kuishambulia serikali kuu, na kudai uhuru wa jimbo lenye upinzani.

Mara nyingine, kifo cha mfalme kilikuwa ni kukaribisha majirani wenye tamaa kuivamia nchi yake kwa matumaini kwamba huyo kiongozi mpya, kwa kukosa uzoefu, hatakuwa na uwezo wa kutoa upinzani wenye nguvu kwao, na watajitwalia nchi mpya wenyewe.
Historia ya tawala za Kiislamu imeloweshwa katika damu za Waislamu. Huko nyuma, wakati wowote mfalme au sultani alipofariki, wanae na ndugu zake walirukiana makooni kuchinjana. Wakati mwingine wadogo na hata watoto wachanga hawakuachwa kama walikuwa kwenye nasaba ya moja kwa moja kutoka kwa mtawala, na kwa hiyo, walikuwa wenye uwezekano wakuwa vyanzo vya matatizo. Wakati wa kifo cha mtawala, kuenea kwa vita na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, na maasi katika majimbo, vilionekana kuwa ni kawaida.

Wanahistoria wengi wa kisasa ambao wamesoma nadharia ya kisiasa ya Uislamu na uwezekano wake, na wamejaribu kuanisha sababu na athari, wameihusisha migogoro ya ndani ya Uislamu na vita vya “kushindwa” kwa Muhammad Mustafa (s.a.w.) kuteua mrithi wake mwenyewe. Kuna dokezo lililofichwa au mifano yenye shaka katika vitabu vyao kwamba “alihusika” nazo. Lakini baadhi ya mifano mingine haikufichika au kuwa na shaka kiasi hicho.

Edward Jurji:

“Hali ya kivita, iliyokuwepo kati ya Mtume na ndugu zake, ilifikia kikomo katika ushindi kamili wa majeshi ya Kiislam uliofikishwa kileleni na kuingia kwa ushindi kwa Muhammad katika mji alimozaliwa kwa kubomoa kumbukumbu za uabudu masanamu. Ingawa kazi yake ilibakia ya Kiutume, Muhammad alikuwa ameongeza kuja kutumia upanga wa kiongozi wa kijeshi na kusimamia mambo ya dola ya kisi- asa yenye hima, akitambua wajibu wa dola hiyo katika historia.

Kifo chake kilipo- tokea tarehe 8 Juni, 632, alirithisha kwa wafuasi wake urithi wa dini-na-siasa daima ulioelemewa na kusumbuliwa kwa karne nyingi na jukumu la kupata khalifa (mrithi) anayekubalika kujaza nafasi ya juu kabisa katika Uislamu. Ukhalifa (urithi) kama jambo, lililokuzwa na kimya cha kuchosha cha Mtume juu ya suala la ni nani angemfuatia, lilikuwa ni mzizi wa uovu mwingi, na balaa la ndani kubwa la Uislamu, chanzo cha mipasuko na mifarakano, na urithi wa kuhuzunisha wa machozi na damu.”
(The Great Religions of the Modern World, 1953)

Kwa mujibu wa mwanahistoria huyu, kilikuwa ni “kimya kinachochosha cha Mtume (s.a.w.) juu ya suala la, ni nani angemfuatia yeye, ambalo lilikuwa “mzizi wa uovu mwingi, balaa kubwa ya ndani ya Uislamu, chanzo cha mipasuko na mifarakano, na urithi wa kuhuzunisha wa machozi na damu.”

Hivi huu ndio “urithi” ambao Muhammad (s.a.w.) aliouachia umma wake? Ikiwa Waislamu wa sasa wanaamini kile kioja cha Saqifah kwamba hakuteua mrithi wake mwenyewe, basi watakubaliana na uamuzi wa mwanahistoria huyu. Lakini kama watakubaliana na uamuzi huu, itawabidi wapingane na Qur’an Tukufu ambayo imemuita Muhammad ni “rehma kwa ulimwengu mzima.”

Sir John Glubb:

“Mtume alifariki bila ya kuacha maagizo yoyote kuhusiana na mrithi. Ilipofahamika tu kwamba amefariki, watu wa Madina walikusanyika pamoja na wakaamua kuchagua mkuu wao wenyewe. Upinzani wa wadai wa ukhalifa ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Waislamu visivyokwisha, ambavyo labda vingeweza kuepukwa kama Muhammad angeweka sheria kwa ajili ya urithi (ushika makamu).”
(A Short History of the Arab Peoples, 1969)

Kama Waislamu wa sasa, baada ya kusoma fatwa hii ya mwanahistoria, bado wanashikil- ia kwamba Mtume wao hakuchagua mrithi wake mwenyewe, basi lazima wakiri kwamba vile vita vyote vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe vya historia yao, vilikuwa ni “zawadi” yao kutoka kwake – kutoka kwake yeye ambaye alikuwa ndiye mfano wa rehema. Je, vita, hususan vya wenyewe kwa wenyewe, ni laana au ni baraka? Kama ni laana – na hakuna laana kubwa katika dunia kuliko vita – hivi wataamini kwamba Mtume wao alikuwa ndiye mletaji kwao Uislamu – wa amani?

Kwa kweli, moja ya malengo ya Muhammad (s.a.w.), kama Mtume wa Allah (s.a.w.w), lilikuwa ni kufuta vita, na kurudisha amani ya kweli ulimwenguni. Vita ndio laana kubwa kabisa, na amani ni moja ya baraka kuu za Allah (s.w.t.) Yeye alikuwa ni Mtume wa Amani. Kwa kweli, harakati aliyoianzisha, yenyewe iliitwa Amani au Uislamu. Kama Mwislam anaamini kwamba Muhammad alikuwa mchocheaji wa vita na umwagaji damu, atakoma kuwa mwislamu.

Sasa chaguo mbele ya mwislamu ni rahisi: ama anaamini kwamba Muhammad haku…..(narudia) hakuteua mrithi wake mwenyewe, au anaamini kwamba alifanya hivyo. Kama anaamini kwamba Muhammad (s.a.w.) hakuteua, basi itamaanisha kwamba alileta huzuni na misiba yote iliyopita na ya baadae juu ya umma wa Waislamu. Imani kama hiyo itakuwa, kwa kweli, ni “ukosoaji” wa kimya kimya wa mwislamu, kumkosoa Muhammad kwa “kosa la kutofanya vizuri” kazi yake. Lakini ajiulize yeye mwenyewe kama anaweza “kumkosoa” yule Mtume wa Mwisho na Mkuu kabisa wa Allah (s.w.t.) na bado akawa ni mwislamu!

Kama mwislamu wa wakati huu anaamini kwamba Muhammad (s.a.w.) aliteua mrithi wake mwenyewe, basi lazima akiri kwamba ule mkutano uliofanyika pale Saqifah ulikuwa “hauna mamlaka” kwa sababu ulifanywa kwa ukaidi wa amri za Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.).

Maovu yote, mabalaa ya ndani ya Uislamu, mipasuko na mifarakano, ule urithi wa huzuni wa damu na machozi, na vita vya wenyewe kwa wenyewe visivyo na kikomo vya Waislamu, vilikuwa na chanzo chao mle Saqifah.

Uislamu umetoa uhuru wa chaguo kwa Waislamu wote. Kwa upande mmoja wanao uamuzi wa majaaliwa wa Muhammad (s.a.w.); na kwa upande mwingine, kuna ule uamuzi uliofanywa kwenye ukumbi wa Saqifah. Wanaweza kuchagua wowote wanaoutaka.

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Allah (s.a.w.w) na mfasiri wa Qur’an, alikuwa ndiye mwenye ujuzi zaidi kati ya wanadamu. Sio tu kwamba alikuwa na ujuzi wa historia, na ujuzi wa sababu za kuibuka, kupungua nguvu na kuanguka kwa mataifa, alikuwa pia na ujuzi na ufahamu wa asili ya mwanadamu.

Mikondo ya historia yote ilikuwa yenye kujulikana kwake. Kwa sababu alikuwa amejaaliwa na ujuzi kama huo, hakuliacha suala la urithi kwenye nafasi ya kubahatisha. Alikuwa ameanza utekelezaji wa ratiba ya kujenga upya jamii ya wanadamu, na alikuwa ameanzisha Ufalme wa Mbingnii juu ya Ardhi. Na alijua kwamba hataishi milele.

Muhammad (s.a.w.) alijua kwamba atakufa lakini ujumbe wake utaishi. Ujumbe wake uli- hitajia kuendelezwa. Kuendelezwa kulikuwa ni muhimu sana kwa mafanikio ya ujumbe wake, na chochote kilikuwa kisiukatishe, sio hata kifo chake mwenyewe. Kwa hiyo ili kutoa mwendelezo kwenye kazi yake, alimchagua Ali ambaye ingawa bado mdogo kwa miaka, alikuwa ndio mfano halisi wa sifa zote za uongozi katika Uislamu. Muhammad (s.a.w.) alitoa tamko la majaaliwa katika karamu ya Dhu’l-‘Ashiira kwamba Ali alikuwa ni waziri wake, mshikamakamu na mrithi wake. Lakini pia alikuwa amefanya uchunguzi wa maisha na uchambuzi yakinifu wa tabia na uwezo wa Ali, na akammwona yeye ni asiyelinganishika.

Ali alikuwa wa namna ya kipekee. Alikuwa ni mtu mwenye-uwezo zaidi katika Uislamu! Hata kama hakuna ushahidi wa kihistoria unaoweza kupatikana kwamba Muhammad (s.a.w.) aliteua mrithi wake mwenyewe, bado inawezekana kufanya tafsiri chache kutoka kwenye tabia na mwenendo wake. Alikuwa mwangalifu, mwenye hadhari na makini wa itifaki katika maisha ya ndani na ya nje. Busara, kuona mbali na upangaji makini uliainisha kazi yake. Madai ya kwamba hakuuambia umma wake ni nani atakayeuongoza katika vita na amani, na ni nani atakayeuelekeza katika dharura nyingine za maisha, ni kinyume kabisa na tabia yake.

Muhammad (s.a.w.) alikuwa ndiye mwalimu wa Waislamu. Aliwafundisha kila walichok- ijua. Juu ya elimu ya Uislamu, hakuwaficha chochote kile. Kudai kwamba aliwaficha taarifa yenye muhimu sana kwao, yaani, jina la mtu ambaye atashika usukani wa chombo cha Uislamu, baada ya kifo chake yeye mwenyewe, kunashindana na kanuni zote za maarifa ya kawaida na mantiki.

Itakumbukwa kwamba wakati Muhammad Mustafa (s.a.w.) alipokuwa yuko Makka, wakazi wa Makka walileta fedha na vitu vyao vya thamani kwake kwa ajili ya kuvihifadhi – kabla na baada alipoanza kuutangaza Uislamu kwa sababu walimuamini. Uaminifu na ukweli wake vilikuwa havina shaka yoyote.

Katika mwaka 622 A.D. Muhammad Mustafa (s.a.w.) alihama kutoka Makka na kwenda Madina. Kabla ya kuondoka Makka, alimfanya Ali mwenye-mamlaka kwa ajili ya kurudisha amana zote kwa wenyewe (wapagani) – wenyewe wale wale waliokuwa na uchu wa kumuua yeye kwa kutangaza Uislamu. Lakini amana ni kitu kitakatifu, na lazima kiheshimiwe na kila mtu, hususan na Mtume wa Allah!

“Amana zinaweza kuelezewa au kutekelezwa. Amana za kuelezwa ni zile ambapo mali imekabidhiwa au kazi inatolewa na mtu kwa mtu mwingine anayemwamini, kuitekeleza ama mara moja au katika dharura nyinginezo maalum, kama vile kifo Amana za kutekelezwa zinatokea kwenye madaraka, au nafasi, au fursa; kwa mfano, mfalme anashika falme yake kwa dhamana kutoka kwa Allah kwa ajili ya watu wake.”
(A. Yusuf Ali, Mtarjumu na Mfasiri wa Qur’an Tukufu).

Baada ya kuondoka kwa Muhammad kutoka Makka, Ali alirudisha amana zote kwa wenyewe.

Lakini kwa Muhammad (s.a.w.) hakukuwa na “amana” kubwa zaidi kuliko Uislamu. Allah (s.w.t.) aliweka juu yake wajibu wa kufikisha amana hii kwa wanadamu wote. Kwa hiyo, kabla ya kifo chake, ilimlazimu kumfanya mtu kuwa na dhamana ya kusimamia “amana” hii.

Muhammad (s.a.w.), Mtume wa Uislamu, alimfanya Ali mwenye-mamlaka ya kusimamia “amana” hii; na kwa usemi wake wa kisiasa – Serikali ya Madina. Dhamana bora ya usalama wa Dola ambayo Muhammad (s.a.w.) alikuwa ameianzisha, ilikuwa ni katika kuwafahamisha Waislamu ni nani atakayekuwa kiongozi wao baada ya kifo chake yeye mwenyewe. Usalama wa Dola hiyo utakuwa, kwa kweli, umehatarishwa vibaya kama angeshindwa kuwajulisha wafuasi wake ni nani atakayemfuatia yeye kama Mtendaji Mkuu.

Hakuna mwislamu ambaye angethubutu kudhania kwamba Muhammad Mtume wa Allah (s.a.w.), angesema au kufanya kitu chochote chenye madhara kwenye maslahi ya Uislamu. Wala ambaye angethubutu kudhania kwamba Muhammad (s.a.w.) angesema au kufanya kitu kisicho na mantiki.

Kuchukulia kwamba Muhammad (s.a.w.) hakuteua mrithi wake mwenyewe, na hakumtambulisha kwa umma wa Waislamu, hakuungwi mkono ama na ukweli au na mantiki. Ukweli na mantiki viko upande wake – kudumu na bila ukwepaji. Ilikuwa ni katika ule ukumbi wa Saqifah ambamo mantiki ya historia ilikwenda kombo.