read

Ufufukaji Wa Bani Umayyah

Bani Umayya walikuwa ni Ukoo mmojawapo wa Makuraishi Wa Makkah. Kama ilivyoelezwa kabla, walikuwa ni maadui wa jadi wa Bani Hashim – ukoo mwingine wa Makuraish. Wakati Muhammad, mtu wa ukoo wa Bani Hashim – alipotangaza kwamba alikuwa ni Mtume wa Allah swt., na akawataka Waarabu kutelekeza uabudu masanamu wao, na kuamini katika Mungu Mmoja, Bani Umayya walimpinga, na walipigana dhidi yake kwa miaka ishirini.

Lakini walishindwa. Mapambano yao ya muda mrefu na makali dhidi ya Muhammad na Uislamu yalifikia mwisho wenye kufedhehesha mnamo mwaka 630A.D., wakati alipoite- ka Makka. Walilazimika kukubali kushindwa, na “wakaukubali” Uislamu.

Ushindi wa Uislamu, hata hivyo, uliwasha mioto mipya ya chuki katika nyoyo za Bani Umayya dhidi ya walezi wake – Muhammad na Ali, kama ilivyoonyeshwa katika mlango mmoja uliopita. Walikuwa waangalifu vya kutosha katika kuficha chuki yao kwa Muhammad lakini hawakujaribu kuficha chuki yao juu ya Ali. Alikuwa ni Ali aliyeharibu sio tu zile nembo zenye kuonekana za dini ya Bani Umayya bali pia alileta kifo kwenye heshima zao.

Lakini mara wakaonyesha kwamba wanaweza kuwa chini lakini walikuwa hawajatoka nje. Wao, kwa hiyo, walivuta subira kwa miaka thelathini – hadi mwaka 661A.D. – wakati walipokuwa, hatimaye, na uwezo wa kuikamata ile zawadi iliyotafutwa kwa muda mrefu – ukhalifa wa Waislamu. Bani Umayya walikuwa ndio maadui wabaya sana kati ya maadui wote wa Uislamu. Kufanikiwa kwao kukamata ukhalifa wa Waislamu, kwa hiyo, kumeleta mshangao mkubwa miongoni mwa wanahistoria. Yafuatayo ni maoni ya baadhi yao juu ya ukweli huu wenye mashaka kuaminika katika historia ya Waislamu.

Edward Gibbon:

“Wale watesaji wa Muhammad walipora urithi wa watoto wake; na mabingwa wa uabudu masanamu wakawa ndio viongozi wakuu katika dini na dola yake. Upinzani wa Abu Sufyan ulikuwa mkali na sugu; kusilimu kwake kulikuwa kwa kuchelewa na kusiko na ari; imani yake mpya ilitiwa nguvu na haja na manufaa; alitumikia, alipi- gana, huenda aliamini; na madhambi ya nyakati za ujahilia yalifidiwa na sifa za hivi karibuni za familia ya Umayya. Mu’awiyah, mtoto wa Abu Sufyan, na yule katili Hind, alikwezwa mwanzoni mwa ujana wake kwa cheo au jina la mwandishi wa Mtume; uamuzi wa Umar ulimkabidhi serikali ya Syria; na alilitawala jimbo hilo kwa zaidi ya miaka arobaini, ama katika cheo cha chini au cha juu. Kazi iliyotukuzwa ya kuwatafuta wauaji wa Uthman ilikuwa ndio kichwa na kisingizio cha tamaa yake.
(The Decline and Fall of the Roman Empire)

E. A. Freeman:

“Ukhalifa ungeweza labda kutolewa kwa mwenye kustahili sana katika waumini; ungeweza labda kuwa wa kurithiana katika familia ya Mtume; lakini Muhammad asingeweza kamwe kudhania kwamba utakujakuwa ni wa kurithiana katika ukoo wa maadui zake wabaya kabisa.” (History of the Saracens)

R. A. Nicholson:

“Wakati wale makabaila wa Makka walipoukubali Uislamu, walisalimu amri tu kwa kisichokwepeka. Walikuwa sasa wapate fursa ya kujilipizia kisasi wenyewe. Uthman bin Afan, ambaye alimrithi Umar kama khalifa, alitoka kwenye ukoo mashuhuri wa Makka, Bani Umayya au kizazi cha Umayya, ambao ulikuwa siku zote ukiongoza katika upinzani kwa Muhammad, ingawa Uthman mwenyewe alikuwa miongoni mwa masahaba wa mwanzoni wa Mtume. Yeye alikuwa mchamungu, mtu mzima mwenye nia njema – zana nyepesi mikononi mwa ndugu zake wenye tamaa. Mara moja wao walipanda kwenye vile vyeo vyote vyenye faida na maarufu na wakaishi maisha ya anasa, ambapo mara kwa mara tabia zao mbovu zilisababisha kuzuka kwa swali la endapo hawa wafuasi wa dakika za mwisho hawakuwa bado wapagani nyoy- oni mwao.

Sababu nyingine zilichangia kuchochea manung’uninko ya jumla. Ukuaji wa haraka wa anasa na vitendo vya kifisadi katika miji mitakatifu na vilevile kwenye makazi mapya ulikuwa ni chukizo kwa Waislamu wachamungu. Wale Waislamu wabora wa kweli, Masahaba wa Mtume, wakiongozwa na Ali, Talha na Zubeir walijitahidi kuuchimba ule uungwana wa kiadui ambao uliwatishia kuwaangamiza. Kikundi kilichojitenga kijeshi kilikuwa tayari kwa uasi dhidi ya kiburi na uroho wa Bani Umayya. Maasi yalizuka ghafla, na mwishowe, khalifa huyu mzee, aliuawa ndani ya nyumba yake mwenyewe.
(A Literary History of the Arabs, uk. 190, 1969)

Nicholson amekosea katika kueleza kwamba Ali, Talha na Zubeir walijitahidi kuwachim- ba Bani Umayya ambao waliwatishia kuwaangamiza. Ali hakujitahidi kuwadhoofisha Bani Umayya ingawa Talha na Zubeir walijitahidi kumchimba Uthman, na walifanikiwa katika juhudi zao. Kwa upande wao, Bani Umayya walimtishia Ali – lakini hawakuwatishia Talha na Zubeir – kwa maangamizo. Kwa kweli, Talha, Zubeir na Aisha walipigana vita vya Basra (vita vya Ngamia) dhidi ya Ali, kwa msaada wa Bani Umayya.

Philip K. Hitti:

“Kati ya makhalifa wanane (wa Bani Umayya) katika kipindi cha 715 – 750 ni wawili tu ndio waliostahili ule urithi ulioanzishwa na Mu’awiyah na kutajirishwa na Abd-al-Malik na al-Walid. Hao sita waliobakia, watatu wao wakiwa ni watoto wa mama zao watumwa, walikuwa hawana uwezo, wengine wakiwa mafasidi kama sio wapotofu. Yule mrithi-ndugu wa al-Walid alikuwa anapendelea sana ulevi, uwindaji, na kusikiliza nyimbo na muziki kuliko kuendesha shughuli za dola. Mtoto wake alimpita baba yake. Alitumia muda mwingi katika nyumba zake za starehe huko jangwani, ambako mabaki yake bado yanaonekana, kuliko hapo makao makuu.

Anasemekana kujiingiza katika kuogelea katika dimbwi la pombe na kugugumia kiasi cha kutosha kushusha kina chake. Zaidi ya mwasherati asiyerekebishika, khalifa huyu wakati mmoja alitenda jambo la kufuru isiyokuwa ya kawaida; kuifanya shabaha nakala ya Qur’an kwa ajili ya mishale ya upinde wake. Bila shaka, kule kukua kwa haraka kwa utajiri, wingi wa watumwa na mahawara, kuongezeka kwa nyenzo kwa ajili ya kujiingiza kwenye starehe, na tabia nyingine mbaya za ustaarabu wa kitajiri wa mjini – dhidi yake ambazo watoto hao wa jangwani walikuwa hawakujengeka kwa kiwango chochote cha kutoathirika – walikuwa wameanza kudhoofisha nguvu ya Uarabu.” (Capital Cities of Arab Islam, uk. 78-79, 1973)

Arnold J. Toynbee:

“Moja ya mambo ya kejeli kubwa ya historia yote ni yale maangamizi ya ile nyumba ambayo Muhammad aliijenga. Muhammad alikuwa na muanguko mkubwa. Mtume huyu asiyefanikiwa alishindwa kwenye shauku ya kufanikiwa kama mtawala mweledi na mwenye mikakati. Lakini, katika kutafuta na kupata mafanikio ya kidunia huko Madina, Muhammad, bila kujua, alikuwa akiwafanyia kazi washindi wake huko Makka. Pale ilipokuja kwenye mashindano ya Siasa halisi (ya hali na mali), wafalme wa biashara wa Makka walikuwa na uwezo zaidi ya mwenzao wa mjini, mgeni wa biashara, na wenye uwezo zaidi sana kuliko binamu na mkwe wake Muhammad, hodari lakini asiye na uwezo, Ali.

Baada ya Muhammad kufanikiwa kukata njia ya msafara wa biashara wa Makka kwenda Syria, watu wa Makka walisalimu amri kwa masharti nafuu ambayo huyu mkimbizi wa Makka mwenye hisia za huruma, aliyowapa wao; lakini katika utii wa nje kwa Muhammad na Uislamu, Bani Umayya walificha ndimi zao mashavuni mwao. Hawakuwa na dhamira ya kuondoshwa madarakani kwa muda mrefu. Sasa kwa vile wameshindwa kwanza kuuzuia Uislamu na kisha kuurudisha nyuma, njia nyingine pekee kwao ilikuwa ni kuukubali harakaharaka baada ya kuukamata kwa hila ya kusilimu kwa maneno tu. Walisubiri wakati mzuri mpaka kwa Ali wakampa- ta mtu wao wa kumwonea na kwa Mu’awiyah wakapata mtu wa bahati yao.

Mu’awiyah alikuwa ni mmoja wa mabwana wakubwa kabisa, wanaojulikana kwenye historia, wa aina ya mtawala mjanja, mwenye subira. Analingana na Augustus, Philip wa Macedon, Liu Pang, na Cavour. Maskini Ali alizidiwa ujanja kabisa na yeye. Ndani ya kipindi cha miaka ishirini na tisa ya kifo cha Muhammad, ile ambayo Muhammad alikuwa ameianzisha, na ambayo warithi wake wameipanua kwa haraka sana na kuwa himaya kubwa, ikageuka kuwa ngawira isiyo na ubishani ya Mu’awiyah mwana wa Hindi: yule Malikia wa biashara, kigogo wa Makka ambaye alikuwa adui mkubwa sana wa Muhammad. Tofauti na Muhammad, Mu’awiyah alianzisha ufalme – Utawala wa Umayya – ambao ulidumu kwa miaka 90 na ukaitawala dunia kutoka Multan na Tashqand hadi Aden, na kutoka Aden hadi Gibralter na Narbonne.

Mu’awiyah na warithi wake, wakiwa wapagani wasiotubia katika yote bali majina tu (isipokuwa kwa Muislamu halisi mmoja tu, Khalifa Umar II), walifikia uamuzi wa kuupinga Uislamu kwa kujiingiza katika karaha mbaya sana katika ustaarabu. Walikuwa walevi wa pombe, na walipamba makasiri yao kwa nakshi na michoro ya rangi katika mtindo wa Kiyunani ambao ulikuwa umeenea huko Syria kwa miaka 1000 iliyopita.

Walifurahia katika kuvunja miiko ya Kiislamu katika taswira ya miundo ya maisha. Waliajiri wasanii wa Kikristo ambao walikuwa mahodari katika nyanja hii; na hawakupendezewa na taswira za wanyama na wanaume. Maagizo yao waliyoyapendelea sana yalikuwa ni picha za wanawake – bora zaidi wakiwa uchi, au angalau uchi mpaka kwenye kiuno.

Waliwezaje hawa Bani Umayya kusalimika na utovu wa heshima na kufuru hii kwa muda mrefu hivi hadi miaka 90? Wakati Jezebel na Ahab walipopinga ibada ya imani halisi ya Yahwah, adhabu inayostahili ilitolewa kwa haraka sana. Hivyo, ni vipi hawa Bani Umayya walimudu kuendelea hivyo vizuri sana kuliko Utawala wa Umar? Mtu anaweza asiwapende au kuwasifia Bani Umayya, lakini werevu wao unadai heshima zetu za kusita, na hawezi kujizuia kushukuru utaratibu wa kisanii wa kufanya mambo ambao wao wameturithisha sisi.” (East to West – A Journey Round the World, 1958. uk.214-5 – The Shocking Umayyads)

Toynbee anaweza kudai kwamba ni mwanahistoria mashuhuri lakini madai hayo hayalazimishi kufanya maoni yake, ambayo ameyaeleza kifahari sana, katika dondoo iliyopita, ama kuwa ni sahihi au hata yenye akili. Kwa kujitia kumdhihaki Muhammad (s.a.w.w.) na Ali, anasaliti tu dosari katika jicho lake mwenyewe, bainifu sana la Wamisionari wa Kiingereza wa karne ya 19 katika makoloni. Maoni yake yako zaidi kwenye aina ya tahakiki ndefu yenye lawama na matusi au mabishano, isiyokosa mguso wa rasharasha za kebehi, kuliko mchanganuo wowote wa mambo wenye shabaha na ukosoaji.

Yale maneno ya mwanzoni yanavutia sana. Toynbee anasema “moja ya kejeli kubwa ya historia yote ni yale maangamizi ya nyumba ambayo Muhammad alikuwa ameijenga. Muhammad alikuwa na muanguko mkubwa.” “Kejeli” hiyo lazima iwe ilikuwa na sababu lakini Toynbee hasemi sababu hizo zilikuwa zipi. Anatilia maanani zile athari tu.

Toynbee ni matokeo ya ule utamaduni wa kisasa wa Magharibi, wa kuthamini mali, wa kubadili asili ya mambo, na Waislamu wanaweza kutogundua kutoweza kwake kuyaelewa maadili ya kijamii ya Uislamu. Mafanikio ya Uislamu yalikuwa yametaarifiwa katika dhana ya kimapokezi (dhana ya Nabii Ibrahim) ya kafara. Muhammad na Ali walitoa mhanga sio tu utajiri wao wa mali bali pia walitoa mhanga uhai wa wengi wenye thamani kwa ajili ya kuufanya Uislamu kuweza kuwepo. Wakati, baada ya vifo vyao, Uislamu ulipohitaji makafara mapya, watoto wao walikuwa tayari kuyatoa. Wajukuu wa Muhammad (s.a.w.w.) na watoto wa Ali walitoa muhanga maisha yao huko Karbala kwa ajili ya mifano ambayo wote walikuwa wamejitahidi kuifanya isisahaulike milele.

Makafara yaliyotolewa na Muhammad, Ali na watoto wao, ndio ushindi na heshima ya Uislamu lakini Toynbee anayalinganisha na “kejeli.”

Muhammad hakuwa na “muanguko” – mkubwa ama mdogo – ingawaje Toynbee angeta- ka kwamba angekuwa na muanguko.

Toynbee alimwita Muhammad Mustafa “Mtume asiyefanikiwa” ambaye “alishindwa kwenye shauku yake ya kufanikiwa kama mtawala mweledi.” Alikuwa vipi “asiyefanikiwa”? Wajibu wake ulikuwa ni kufikisha ujumbe wa mwisho wa Allah swt. kwa wanadamu, na aliufikisha, na ulikubaliwa katika sehemu zote za peninsula ya Arabia ndani ya wakati wa uhai wake. Wala hakushindwa kwenye shauku yake ya kuwa mtawala mweledi. Yeye alikuwa mtawala mweledi. Ujumbe wake ulikuwa mpana, na moja ya kazi zake kama mjumbe wa Allah swt. ilikuwa ni kuwaelimisha Waislamu katika utaratibu wa mfumo wa kisiasa. Hili alilifanya huko Madina.

Muhammad (s.a.w.w.) hakuwa katika “mashindano” na wapagani au watetezi wa siri wa upagani wa Makka. Yeye alikuja ulimwenguni hapa kueneza sheria za Utawala wa Mbinguni, na sio “kushindana” na mtu yeyote, mwisho wa wote kabisa, na wala riba wa Makka na waabudu masanamu. Kusingizia kwamba alikuwa akishindana na Bani Umayya ni maoni ya kipuuzi kabisa kuliko yote ya Toynbee.

Waabudu masanamu wa Makka hawakuwa “wenye uwezo zaidi” ama kwa Muhammad au kwa Ali, naye Ali hakuwa “dhaifu,” na hakuwa “amezidiwa ujanja” na Mu’awiyah.

Toynbee hana uwezo wa “kuwahukumu” wao kwa mtazamo wa maadili ya kijamii ya Kiislamu. “Siasa halisi” yake (ya kujali hali, mali na mazingira) isingeweza kuwa na man- ufaa yoyote kwa Muhammad na Ali. Tafsiri zake zinaonekana wazi zimeathiriwa na utamaduni wake – wa kutafuta maslahi, utamaduni wa kidunia wa Magharibi ya kisasa. Hana utambuzi wa utamaduni wa Qur’an, na Qur’an inabeua “siasa halisi.”

Muhammad na Ali walikuwa wanaidhihirishia dunia kwamba katika siasa, kama katika dini, malengo hayathibitishi uhalali wa matendo. Katika Uislamu matendo yenyewe yanakuwa ndio malengo. Matendo ambayo maadui zao – Bani Umayya – waliyoyafanya ili kufikia malengo yao, yalikuwa na uhakikisho uliojengeka ndani yake wa “mafanikio”.

Lakini Muhammad na Ali hawakuamua mafanikio au kushindwa kwa vipimo hivyohivyo kama Bani Umayya walivyofanya au kama Toynbee anavyofanya. Kwa Muhammad na Ali, mafanikio yalikuwa ni kupata radhi za Allah swt. tu, na kushindwa kulikuwa ni upotezaji wa radhi hizo tu. Kwa kuamua kwa kipimo hiki, wote hao walikuwa wamefanikiwa sana. Mwenyezi Mungu awape rehma wao na watoto wao daima na milele.

Toynbee anaendelea kusema kwamba Bani Umayya hawakuwa na dhamira ya kuondoshwa kutoka kwenye madaraka kwa muda mrefu. Hivi hizo dhamira za Bani Umayya zilikuwa na maana yoyote mwaka 63O A.D., wakati Muhammad Mustafa alipoiteka Makka? Alikuwa ameteketeza ushirikina wao na mamlaka ya kiuchumi na kisiasa, na Ali alikuwa amevunja nguvu yao ya kijeshi.

Walimuangukia miguuni kwake, na wangebakia wameanguka daima kama Abu Bakr na Umar wasingewanyanyua, na wasingewarudishia madaraka ya kiuchumi na kisiasa. Ghafla, kilichokuwa kikionekana hakiwezekani chini ya Muhammad, kilionekana kutarajiwa chini ya Abu Bakr na Umar. Walikuwa ni hao wote walioifanya dola ya Waislamu kuwa “ngawira isiyo na ubishani ya Mu’awiyah mtoto wa Hindi.”
Mapenzi, heshima na shukurani ambayo Toynbee “hawezi kujizuia” kuzitoa kwa Bani Umayya, zinaeleweka vizuri sana. Yeye ni mwenzao kifalsafa. Wote wanaunganishwa pamoja katika uadui wao unaofanana kwa Uislamu na kwa walezi wake, Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na Ali.

“Hukmu” ya Toynbee juu ya Muhammad na Ali ni mfano wa kuigwa wa upuuzi mkubwa ambao wanazuoni maarufu wanaweza kuuzusha. Hitti na Toynbee wote wamevuta taswira ya baadhi ya makhalifa – warithi wa Mtume wa Uislamu – ile ambayo Banu Umayya wameitoa. Ukweli kwamba umma wa Waislamu ulilundikiwa makhalifa kama hao, kwa kweli ni “moja ya kejeli kubwa ya historia yote.” Lakini kejeli hiyo ina maelezo yoyote? Inayo, ndio. Kitabu hiki ni jaribio la kuielezea kejeli hiyo.

Bani Umayyah walifaidi umaarufu kiasi hapo Makka kama walezi wa hekalu la masana- mu na kama matajiri wala-riba wakubwa. Wakati Muhammad alipoiteka Makka, alikome- sha uabudu masanamu wao na ula-riba wao, na wakapoteza umaarufu.

Lakini kupoteza umaarufu huko hakukudumu kwa muda mrefu. Kulidumu tu kuanzia kule kutekwa kwa Makka na Muhammad mnamo Februari 630 hadi kwenye kifo chake mnamo Juni 632. Wakati tu “jua” la Utume lilipozama kwenye macheweo, ile “nyota” ya Bani Umayya ikachomoza juu yake.

Haitakuwa sahihi kuonyesha ufufukaji wa Bani Umayya kuanzia tarehe ambayo Uthman alikuwa khalifa wala hata pia kuanzia tarehe Mu’awiyah alipoutwaa ukhalifa bali kuanzia tarehe 8 Juni, 632, tarehe ya kifo cha Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa Uislamu.

Ni uhusiano gani kati ya kifo cha Muhammad (s.a.w.w.) na ufufukaji wa Bani Umayya? Kama ilivyoonyeshwa hapo juu, Muhammad alihusika na kupoteza umaarufu kwa Bani Umayya. Lakini mara tu alipofariki, waliruka kutoka kwenye ukosa umaarufu, ingawa sio kwa uwezo wao wenyewe.

Abu Bakr na Umar, wale watawala wapya wa serikali aliyoiun- da Muhammad (s.a.w.w.), waliwainua Bani Umayya kutoka kwenye ukosa umaarufu na kutoeleweka kwao, na wakawaweka kama nguvu katika mandhari ya kisiasa ya Uislamu.

Bani Umayya waliinuka na uamuzi mzito – kulipiza kisasi kutoka kwa Muhammad na Ali na/au watoto wao.

Kukubali Uislamu kwa Bani Umayya, baada ya kushindwa kwao kuuangamiza, kulikuwa ni ushahidi tu wa uthabiti wao. Walitambua kwamba mashambulizi yao ya kutokea mbele ya Uislamu yalikuwa yote yameshindwa, na kwamba walipaswa kujaribu kitu ambacho sio cha kawaida. Walifanya hivyo.

Mkakati wao mpya ulikuwa ni kuingia kwenye safu za waumini, wakijifanya kama ni Waislamu; kuyaangalia matukio kutoka ndani, na kisha kuushambulia Uislamu pale wakati muafaka utakapojitokeza wenyewe, kama ilivyoelezwa kwenye mlango wa huko nyuma.

Wakati muafaka ulikuja baada ya kifo cha Muhammad (s.a.w.w.). Taarifa ilikuwa imekwishapatikana ya ahadi ya Abu Sufyan, kiongozi wa ukoo wa Bani Umayya, kwa Ali, ya kujaza mitaa yote ya Madina na askari wa miguu na wa farasi, wakiwa tayari na radhi kufa kwa amri yake Ali, kama ataipinga serikali ya Saqifah.

Abu Sufyan alikuwa amerusha pigo la hatari sana kwa Uislamu lakini alikosa shabaha kwa mara nyingine tena. Alikuwa amejaribu kujipendekeza kwa Ali, mlezi wa Uislamu, lakini alishindwa. Ali alikuwa macho kama siku zote. Lakini Abu Sufyan hakuhangaishwa na kushindwa kwake. Ilijitokeza kwake kwamba kama angejaribu kujipendekeza kwa viongozi wa serikali ya Saqifah, angewakuta ni wenye kuvutika zaidi kuliko Ali. Aliwaendea na kweli walikuwa hivyo!

Wakati wa ukhalifa wa walezi wao, Abu Bakr na Umar, Bani Umayya walizizatiti nafasi zao kimya kimya. Hawakujaribu kuvuruga mambo na kuleta misukosuko. Wakati ulikuwa haujafika bado wa wao kufanya jaribio la kuvamia uwanja wa Uislamu. Wao, kwa hiyo, walikaa pembeni. Lakini Uthman alipokuja kuwa khalifa, walihisi kwamba wakati ulikuwa umefika wa wao kutupilia mbali tahadhari yao na uvumilivu wao, na wakaivamia dola hiyo kama tai, tayari kwa kumeza kila kitu.

Uthman akawafukuza magavana wote wa majimbo waliokuwa wameteuliwa na Abu Bakr na Umar, na akazijaza nafasi hizo na watu wa familia yake mwenyewe na ukoo wake. Yeye pia aliwapa Bani Umayya zile ardhi zenye rutuba nyingi na malisho kama mali yao binafsi, na akawapa zawadi dhahabu yote na fedha iliyokuwa ndani ya hazina ya umma.

Mnamo mwaka 656 Ali alichukua madaraka ya serikali mikononi mwake. Aliwafukuza magavana wote waliokuwa wakiipora nchi, na aliwaagiza Bani Umayya kurudisha kwenye dola ile ardhi yote, ada za himaya, maeneo na malisho ambayo walikuwa wamejitwalia kinyume cha sheria.

Lakini Bani Umayya hawakuwa na nia ya kuachia kitu chochote. Walisema wazi kwamba watang’ang’ania, kwa muda mrefu iwezekanavyo, kwenye nafasi zao za tangu huko nyuma, marupurupu yao na fursa zao, na kama Ali bado anazitaka, itambidi azichukue kwa nguvu ya silaha.

Ali alilijua hilo kwamba atakutana na upinzani mkubwa kama angejaribu kugawanya mali kwa usawa. Lakini aliuweka wajibu wake kwa Allah swt. na umma wa Waislamu mbele ya matakwa au kinyongo cha wale wa tabaka la juu katika Dar-ul-Islam. Hakuwa na uchaguzi katika suala hilo, na ilimbidi abomoe ngome za upendeleo bila kujali matokeo yake. Katika suala hili, hapakuwa na nafasi kabisa ya masikilizano.

Rais Jimmy Carter:

“Hii sio kazi ya mtu mwenye moyo dhaifu. Itakutana na upinzani mkali kutoka kwa wale ambao sasa wanafaidi upendeleo maalum, wale wanaopendelea kufanya mambo gizani, au wale ambao maeneo ya milki zao yanatishiwa.” (Why Not the Best? Uk. 148, 1975)

Kutangaza Nguvu Kulikuwa Hakukwepeki

Talha na Zubeir walikuwa nje ya mahesabu ya kivita, na makabiliano mapya ya Ali yalikuwa ni pamoja na wale maadui wa zamani – Bani Umayya – wale wahujumu wa itikadi ya Kiislamu. Makabiliano haya yalikuwa ni uthibitisho wa mafanikio ya Umar katika kuwakingamiza Waarabu kati ya maadui wengi na marafiki wachache wa Nyumba ya Muhammad, Mtume wa Allah swt.

Upinzani wa Bani Umayya kwa Ali ulikuwa ni udhihirishaji wa hisia za upagani dhidi ya Uislamu.

Kwa muda mrefu, chuki ya Bani Umayya dhidi ya Uislamu na Banu Hashim ilikuwa ikiungua polepole kama makaa ya moto lakini kwa kuingia kwa Ali kwenye kiti cha ukhalifa, ikageuka kuwa ndimi za moto unaonguruma, unaotishia kuunguza, kwa maneno ya Toynbee, “ile nyumba ambayo Muhammad aliijenga.”

Baada ya vita vya Basra, (vita vya Jamal), watu wote wa ukoo wa Bani Umayya walikuwa wamejikusanya nyuma ya Mu’awiyah, gavana wa Syria. Alikuwa ndio kiongozi wao, na alikuwa ndiye kiongozi wa hisia za kipagani dhidi ya Uislamu. Katika vita vyake dhidi ya Ali, alisaidiwa na kutenda jinai hiyo na Amr bin Al-Aas. Amr alikuwa sio Bani Umayya lakini kufanana kwa shauku zao kulichochea mfungamano wake na Mu’awiyah.

Ufuatao ni utangulizi mfupi wa historia ya Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas. Itamfahamisha msomaji kiini hasa cha upinzani wao kwa Ali.

Mu’awiyah Bin Abu Sufyan

Mu’awiyah alikuwa mtoto wa Hind na Abu Sufyan. Abu Sufyan alikuwa mume wa tatu wa Hind. Mwanamke huyu alikuwa mmoja wa maadui wachungu sana wa Uislamu, Mtume wake na familia yake. Katika vita vya Badr, baba yake, Utba, aliuawa na Hamza. Mwanawe mkubwa, Hanzala; kaka yake, Walid; na ami yake, Shaiba; waliuawa na Ali. Kwa sababu hii, aliweka nadhiri kwamba atakuja kunywa damu yao (M. Shibli katika Sirat-un-Nabi, juz. I, uk. 370, chapa ya 4, 1976, Azamgarh, India). Katika vita vya Uhud, Hind alipasua tumbo la Hamza, akatoa ini lake, na akalitafuna, na kuanzia hapo akawa “maarufu” katika historia kama “mla maini.”

Kama Mu’awiyah alikuwa mwana wa Hindi, yule mla maini wa Uhud, alikuwa pia baba yake Yazid, yule muuaji katili wa Karbala, aliyefungulia hofu kuu na kumuua mjukuu wa kiume mdogo na vitukuu vya Muhammad (s.a.w.w.). Mmoja wa masahaba wa Mtume waliochukua kiapo cha utii kwa Yazid alikuwa ni Abdallah bin Umar ibn al-Khattab. Alikuwa ni mtazamaji wa “nje ya ulingo” wa mauaji hapo Karbala, ndani yake ambayo kurasa za historia ya Uislamu zilichafuliwa na damu takatifu zaidi kabisa katika viumbe wote.

Yazid alijikweza kwa nasaba ndefu “yenye kutambulika” ya uhasama kwa Banu Hashim – Walezi wa Uislamu.

Wakati Mtume alipoiteka Makka mwaka 630, Abu Sufyan, Hind, watoto wao, Yazid na Mu’awiyah, na watu wengine wa ukoo wa Bani Umayya, wakasilimu. Jalal-ud-Din Suyuti ameandika katika ukurasa wa 135 wa kitabu chake, Tarikh-ul-Khulafai (Historia ya Makhalifa): “Mu’awiyah alisilimu pamoja na baba yake, Abu Sufyan ile siku ilipotekwa Makka. Walikuwepo katika vita vya Hunayn, na walikuwa miongoni mwa muallafatul- qulub.”

Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba baada ya kutekwa Makka, Mtume (s.a.w.w.) alimteua Mu’awiyah kama mmoja wa waandishi wake. Kama mwandishi, kazi yake, pengine ilikuwa ni kuandika barua za Mtume (s.a.w.w.).

Huko Makka na Madina, kote, Mtume (s.a.w.w.) alimfanya kila Muislamu kuwa ndugu wa Muislamu mwingine. Yeye kwa hiyo, alimpa Mu’awiyah naye pia “ndugu.”

Muhammad Ibn Ishaq:

“Mtume alifanya udugu kati ya Mu’awiyah bin Abu Sufyan na al-Hutat. Mtume alifanya hivyo kati ya baadhi ya masahaba wake, kwa mfano, kati ya Abu Bakr na Umar; Uthman na Abdur Rahman bin Auf; Talha bin Ubaydullah na Zubeir bin Awwam; Abu Dharr al-Ghiffari na al-Miqdad bin Amr al-Bahrani; na Mu’awiyah bin Abu Sufyan na al-Hutat bin Yazid al-Mujashi’i. Al-Hutat alikufa mbele ya Mu’awiyah wakati wa ukhalifa wake na kwa sababu ya udugu wake, Mu’awiyah alichukua kile alichokiacha kama mrithi wake.

Al-Farazadaq alimwambia Mu’awiyah: “Baba yako na ami yangu, ewe Mu’awiyah, waliacha urithi, ili kwamba mrithi wake apate kuurithi. Lakini inakuwaje wewe kuibugia mali ya Hutat wakati mali ngumu ya Harb ilikuwa inayeyuka mkononi mwako?” (The Life of the Messenger of God)

Kama ilivyoonyeshwa kabla, Abu Bakr alikuwa amemteua Yazid bin Abu Sufyan kama mmoja wa majemedari wake katika mapambano ya Syria. Syria ilitekwa baada ya kifo cha Abu Bakr – katika ukhalifa wa Umar. Alimteua Yazid kuwa gavana wa kwanza wa Syria. Mwaka 639 hata hivyo, tauni ilizuka huko Syria na Palestina, na ikaua maelfu ya watu, miongoni mwao ni Yazid bin Abu Sufyan na Abu Ubaidah bin al-Jarrah. Kwenye nafasi ya Yazid, Umar alimteua mdogo wake na Yazid, Mu’awiyah, kama gavana mpya.

Sir John Glubb:

“Kulikuwa na balaa la njaa huko Hijazi mwaka 639. Zaidi ya njaa hiyo, huo mwaka wa 639 ulishuhudia kuzuka kwa tauni huko Syria na Palestina. Waarabu wengi walikufa, mpaka idadi kubwa wakakimbilia jangwani kutoka kwenye ile miji iliyokuwa imetapakaa tauni. Kabla ya hili uhamiaji kwenye jangwa ungeweza kukamilishwa, hata hivyo, mkuu wa majeshi, Abu Ubaidah, alishambuliwa na kufa. Alizikwa katika bonde la Jordan. Yazid bin Abu Sufyan, ambaye alikuwa ameshiriki kikamilifu kama kamanda wa safu katika mapambano yote ya Syria alikuwa muathirika pia.

Yule khalifa asiyechoka aliamua kutembelea Syria mwenyewe ili kupanga upya utawala baada ya kupotea kwa viongozi wengi sana. Kwa kweli tauni hiyo ilikuwa mbaya sana miongoni mwa Waarabu, ambao 25,000 kati yao wanasemekana waliku- fa, kiasi kwamba ilihofiwa kwamba Wabyzantium wangeweza kutumia fursa hiyo kujaribu utekaji mpya wa Syria.

Katika nafasi ya Abu Ubaidah na Yazid ibn Abu Sufyan, Mu’awiyah ibn Abu Sufyan aliteuliwa kuwa gavana wa Syria.” (The Great Arab Conquests, uk.214, 1967)
Mu’wiyah alikuwa gavana wa Umar huko Syria katika kipindi kilichokuwa kimebakia cha ukhalifa wake. Wakati Uthman alipomrithi Umar kama khalifa, yeye pia alimthibitisha Mu’awiyah kama gavana wake. Mu’awiyah alitwaa uvumilivu wa kidini kuhusiana na Ukristo ndani ya Syria, na kwa uangalifu na ustadi sana akawalea watu wa Syria, kiasi kwamba akawa maarufu sana kwao.

Franceso Gabrieli:

“Mtoto wa Abu Sufyan alikuwa tayari amewekwa na Umar katika serikali ya Syria, kazi ambayo alikuwa ameshiriki chini ya amri za kaka yake mkubwa, Yazid. Miaka ishirini ya utawala wa busara ulimpatia mapenzi ya wageni wa Kiarabu waliokuwa wamejikita pale.” (The Arabs, A Compact History, uk. 74, 1963)

Mu’awiyah aliifanya Syria kuwa isiyoshindika, na alijifanya yeye mwenyewe kuwa asiyeweza kudhurika wakati wa ukhalifa wa walezi wake, Umar na Uthman.

E. A. Belyaev:

“Alipokuwa bado ni gavana tu wa Syria, Mu’awiyah aliunda himaya kubwa ya mali kwa ajili yake mwenyewe, ndugu zake, na wafuasi wapiganaji wake, akawa kabaila mkubwa kwa utwaaji wa kiasi kikubwa wa ardhi. Khalifa huyu wa Bani Umayya alikaa juu ya misingi imara ya kiuchumi na alikuwa na majeshi maaminifu zaidi kuliko wapinzani wake wa kisiasa. Alikuwa amegeuka kuwa gavana wa kudumu mwenye nguvu sana wa Syria tajiri na iliyostaarabika mapema sana katika siku za Umar, na baada ya kuwa amemaliza zaidi ya miaka ishirini katika nafasi hii muhimu, akawa kiongozi aliyejiandaa upya, wa utawala wa kikabila wa Kiarabu katika Syria.”(Arabs, Islam and the Arab Caliphate in the Early Middle Ages, 1969)

Ilikuwa ni kwa namna hii kwamba Mu’awiyah, mwanasiasa asiye na kifani, wa Waarabu, alivyoibuka kutoka kwenye mabaki ya juhudi zilizoshindwa kufufua zama za upagani, kugeuka, kwanza kuwa adui mkubwa wa Ali ibn Abi Talib, mrithi wa Mtume (s.a.w.w.), na kisha kuwa ndiye mrithi yeye mwenyewe binafsi!

Mu’awiyah alikuwa mtu wa uzushi mwingi.Aliubadili ukhalifa kuwa ufalme, na akajigam- ba wazi wazi: “Mimi ndio wa kwanza wa wafalme wa Kiarabu.” Ufalme, kwa kweli unakuwa ni wa kurithiana, na ilibidi uwe ni wa kurithiana katika ukoo wake. Yeye, kwa hiyo, alimfanya mwanawe Yazid kuwa mrithi wake.

Hata wale Waislamu ambao mwanzoni walipuuza au kufumbia macho maovu yake, walishtuka wakati aliposhusha kishindo hiki kwa ajili ya familia yake.

Uteuzi wa Mu’awiyah wa mwanawe Yazid, kuwa kama khalifa, ulikuwa ni uvunjaji wa dhahiri wa kiapo alichokuwa amekitoa kwa Hasan ibn Ali cha kutomteua mwanawe kama mrithi wake mwenyewe. Lakini Mu’awiyah hakuwa mtu wa kuzuiwa na kiapo chochote au kanuni ya maadili. Maadili mikononi mwake yaligeuka kuwa majeruhi wa kwanza.

Mu’awiyah hata hivyo, alikuwa anatambua kwamba Waislamu hawatamkubali kwa hiari Yazid kama khalifa wao. Yeye, kwa hiyo, aliunyamazisha upinzani kwa dhahabu na fedha au kwa hadaa na vitisho. Lakini kama silaha hizi zilishindwa, basi alitumia silaha ngumu kutambulika, ya siri na yenye uwezo wa kumuepushia hatari – sumu.

Alikuwa ni “muasisi” katika historia ya Kiislamu, katika fani ya kunyamazisha wakosoaji na maadui zake daima kwa njia ya sumu. Akitarajia upinzani kutoka kwa Hasan kwenye urirhi wa Yazid, alipanga kifo chake. Mwanahistoria Mas’ud, anaandika hivi: “Mu’awiyah alituma ujumbe kwa Jo’dah bint Ash’ath, mke wa Hasan, kwamba kama ataweza kumuua mume wake, yeye atamlipa dirham 100,000, na atamuozesha mwanawe Yazid kwake yeye.”

Mu’awiyah aliamsha shauku kwa Jo’dah ya kuwa malkia, na alipompelekea yeye sumu hiyo, kama ilivyopangwa kati yao, akaitoa kwa mumewe, na akafariki kutokana nayo. Mu’awiyah alimzawadia kwa kumpa dirham 100,000, lakini alijitoa kwenye ahadi yake ya kumuozesha kwa Yazid kwa kusema: “Ninampenda mwanangu.”

Abdur Rahman bin Khalid bin al-Walid, gavana wa zamani wa Hims (Emassa) alikuwa pia ameuawa kwa njia kama hiyo hiyo. Wakati mmoja Mu’awiyah alitembelea Hims; akaingia Msikitini, na akiihutubia jamaa, akasema: “ Nimekuwa mzee sana sasa na siko mbali sana na kifo. Mimi, kwa hiyo, nataka kuteua mtu kama
mtawala wenu.”

Mu’awiyah alikuwa akitegemea kwa siri kwamba ili kumfurahisha yeye, watu wa Hims wangependekeza jina la Yazid kama khalifa atakayefuatia. Lakini hakuna hata mmoja aliyemtaka huyo Yazid aliyeharibika tabia, kama khalifa. Kwa upande mwingine, watu hao walimheshimu sana Abdur Rahman bin Khalid bin al-Walid, na wakapendekeza jina lake kuwa khalifa wa baadae wa Waislamu.

Mu’awiyah alificha kutoridhika kwake na akarudi Damascus. Umaarufu wa Abdur Rahman ulimtisha, na akaanza kumtazama kama mpinzani mwenye uwezekano wa kiti hicho. Yeye kwa hiyo, aliamua kufanya kitu cha kufanya kiti hicho kuwa “salama” kwa ajili ya mwanawe Yazid.

Wakati fulani baadae, Abdur Rahman aliugua, na akawa mgonjwa wa kitandani. Mu’awiyah alimshawishi mganga wa Abdur Rahman kuchanganya sumu katika dawa yake na kuitoa kwake. Katika kufanikiwa kwake, alimuahidi kumpa (huyo mganga), kama zawadi, mapato ya Hims kwa mwaka mmoja mzima. Mganga huyo akakubali, na akampa Abdur Rahman ile “dawa” aliyokuwa ameichanganya. Ilifanya kazi yake na ikamuua. (Isti’aab, juz.II, uk. 401).

Baada ya kifo cha Uthman, Waislamu wengi walimkubali Ali kama mkuu mpya wa dola ya Waislamu. Lakini walikuwepo wengine wengi ambao hawakumkubali, na Mu’awiyah, kwa kweli, alikuwa mmoja wao.

Ahmad ibn Daud Dinawari, mwanahistoria wa Kiarabu, anaandika hivi: “Ulimwengu wa Kiislamu ulimtambua Ali kama mtawala mkuu wa Uislamu lakini Mu’awiyah na Bani Umayya waliobakia, ambao walikuwa wameifanya Syria ni ngome yao, hawakumkubali.”

Ali alituma mjumbe kwa Mu’awiyah kumtaka kiapo chake. Lakini badala ya kumjibu, Mu’awiyah alimweka kizuizini yule mjumbe kwenye baraza lake, na akamwalika Amr bin Al-Aas kutoka Palestina kwa “mashauriano.” Alinuia kuorodhesha msaada wake (Amr).

Amr bin Al-Aas

Amr bin Al-Aas alikuwa akiishi Palestina kwa wakati huu, na alikuwa akiyaangalia mandhari ya kisiasa. Yeye alisisimka kupokea mwaliko kutoka kwa Mu’awiyah, na aliruka kuikamata fursa hii. Lakini msaada wake, alimwambia Mu’awiyah, ulikuwa na bei, na ilikuwa ni Misri.

Kwa Mu’awiyah bei hiyo ilionekana kuwa ya juu sana lakini baada ya kusita kidogo alikubali kuilipa kwa kubadilishana na ushsuri na utendaji wa Amr katika vita ambavyo

alikuwa avifanye dhidi ya Ali, mrithi wa Mtume wa Allah swt., na mtawala wa Waislamu wote. Mu’awiyah alikuwa amteue Amr bin Al-Aas kuwa gavana wake huko Misri kama ikibidi huyu Amr atafanikiwa kuitwaa kutoka kwa Ali. Amr bin Al-Aas alitegemewa kuchukua nafasi muhimu, ikiwa kama ni mwenye kisirani, katika historia ya Uislamu.

Alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa ajabu. Uwezo wake unathibitishwa na nafasi za juu alizozishika wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr na Umar. Kulikuwa na kashfa katika kuzaliwa kwake; alizaliwa katika nyumba ya “ kahaba” huko Makka.

Edward Gibbon:

“Kuzaliwa kwa Amr wakati mmoja kulikuwa kwa aibu na maarufu sana; mama yake, kahaba mwenye sifa mbaya, alishindwa kuamua miongoni mwa Makuraish watano; lakini ushahidi wa kufanana ulimuamulia mtoto huyo kuwa wa Al-Aas, aliyekuwa mtu mzima zaidi kati ya wapenzi wake.”
(The Decline and Fall of the Roman Empire)

Washington Irving:

“Mmoja wa washambuliaji wa kuogopesha wa Muhammad alikuwa ni kijana aitwaye Amr; alikuwa ni mtoto wa kahaba wa matajiri hapo Makka, anayeelekea kuwa ameshinda katika kuwapumbaza macho Phrynes na Aspasias wa Greece, na ame- hesabu baadhi ya malodi wa nchi hiyo miongoni mwa wapenzi wake. Wakati alipomzaa mtoto huyu, aliwataja baadhi ya wale wa kabila la Kuraish waliokuwa na madai sawa kwenye ubaba. Kitoto hicho kilitangazwa kuwa chenye kufanana zaidi na Al-Aas, aliyekuwa mtu mzima zaidi kati ya wapenzi wake, ambapo kwa nyongeza ya jina lake la Amr, alipata jina la Ibn al-Al-Aas, mtoto wa Al-Aas.”

Ulimwengu umetunuku zawadi zake bora kabisa juu ya mtoto huyu mwenye kipaji, kana kwamba kwa kufidia dosari ya kuzaliwa kwake. Ingawa mdogo, alikuwa tayari ni mmoja wa washairi maarufu sana wa Arabia. Alimshambulia Muhammad kwa mashairi mafupi ya vipokeo yenye istihizai na vichekesho.
(The Life of Muhammad)

R. V. C. Bodley:

“Kulikuwa na Amr ibn al-Al-Aas, mtoto wa kahaba mmoja mrembo sana wa Makka. Wakubwa wote wa Makka walikuwa ni marafiki zake, kwa hiyo yeyote, kuanzia Abu Sufyani kwenda chini, angeweza kuwa ndiye baba yake Amr. Kwa kadiri mtu yeyote ambavyo angeweza kuwa na hakika, angeweza kujiita mwenyewe Amr ibn Abi Lahab au ibn al-Abbas au ibn yoyote yule miongoni mwa wakubwa wa juu kumi wa Kiquraishi.”(The Messenger, New York, uk. 73, 1949)

Makuraishi wakati mmoja walimtuma Amr kama balozi wao kwenye baraza la Abyssinia kudai kurudishwa kwa wakimbizi wa Kiislamu kutoka Makka ambao walitafuta hifadhi huko. Ujumbe wake, bila kutegemea, ulishindwa.

Mnamo mwaka 629 Amr aliukubali Uislamu. Baada ya kusilimu kwake, Mtume alimtuma yeye, kwa mara chache, kama kapteni wa misafara iliyoshambulia makabila ya wapagani. Msafara muhimu sana ambao aliuongoza wakati wa uhai wa Mtume, ni wa mashambulizi ya Dhatus-Swalasil ambamo aliongoza kundi la watu 500, miongoni mwao akiwemo Abu Bakr, Umar bin al-Khattab na Abu Ubaidah ibn al-Jarrah. Msafara huu, kwa bahati uli- fanikiwa.

Amr alikuwa gavana wa Umar huko Misri. Lakini wakati Uthman alipokuja kuwa khalifa, alimfukuza, na yeye akarudi Madina akijikaza kwa mfundo. Alikuwa ni “mtaalamu” kamili katika kubuni njama, katika kupandikiza mifaraka na katika kueneza chuki. Alizitumia taaluma hizi dhidi ya Uthman, na akafanya shambulizi la kumpaka matope na uchongezi dhidi yake.

Alijigamba wazi wazi kwamba amewachochea hata wale wachunga kondoo wa huko mlimani kumuua Uthman, na kujigamba kwake hakukuwa ni kupayuka ovyo. Uthman alikuwa amemwingiza kwenye mateso ya kisiasa lakini hakuwa na nia ya kuteseka katika ukimya milele wakati alikuwa anaweza kumuwaza yeye (Uthman) akimd- hihaki huko Madina, na aliweza kuwaona (mawazoni) wapenzi wake Uthman wakipiga makelele ya furaha huko Misri – jimbo ambalo yeye Amr alikuwa ameliongeza kwenye himaya. Aliazimia kuchukua hatua yeye mwenyewe.

Kupoteza madaraka ni moja ya matukio machungu sana ambayo yanaweza daima kumtesa mtu. Sio tu anakoseshwa uwezo wa kupanga matukio bali pia wa kuonekana kwa ishara na nishani za cheo.

Talha na Zubeir hawajawahi kupanga matukio. Walifanya jaribio la kutwaa ukhalifa kwa nguvu lakini walishindwa. Jaribio hilo halikuwagharimu maisha yao tu bali pia na sifa zao. Amr bin Al-Aas, kwa upande mwingine, alikuwa hasa amepanga matukio, na yaliyo maarufu vilevile. Lakini ghafla, Uthman akamfanya yeye kuwa duni. Tokea muda huo, yeye alijawa na kutaka kulipiza kisasi, na “alishughulika” kwa bidii na bila kuchoka, kumuangamiza muanzilishi wa kuvunjika moyo kwake – Uthman – khalifa aliyekuwa madarakani.

Punde tu Madina ilikuwa tayari kulipuka. Amr alikuwa amejijengea, katika siku za nyuma, kasri moja huko Palestina. Kabla tu ya mlipuko huo, alitoroka Madina, na akaenda kuishi kwenye kasri lake. Kisha akakaa kuangalia jinsi juhudi zake zitakavyoweza kuzaa matunda.
Aliposikia kwamba Uthman ameuawa, alisisimka sana, na akafurahia waziwazi juu ya “kufanikiwa” kwake.
Uwezo na kuona mbali kwa Amr kulikuwa hakuna shaka yoyote. Kwa kuondoka Madina katika wakati muafaka, na kwa “kuishi maisha ya kijijini” huko Palestina, alijiokoa mwenyewe sio kutokana na shitaka tu, wakati wa uhai wake mwenyewe, la kupanga maua- ji ya Uthman, lakini pia kutokana na shitaka la maandishi ya historia.

Jambo moja ambalo Amr alilifahamu lilikuwa kwamba asingeweza kujipendekeza kwa Ali. Waliwakilisha mitindo miwili isiyopatana, na falsafa mbili zisizopatana. Lakini alijua kwamba ushirikiano na Mu’awiyah ulikuwa unawezekana. Wote walikuwa wabinafsi wenye akili sana. Wote walishiriki katika mauaji ya Uthman, mmoja kwa kuwachochea watu kumuua, na mwingine kwa kuzuia kwa makusudi misaada yote juu yake. Sasa wote walikuwa na shauku ya kuvuna matunda ya mafanikio yao.

Kwa hiyo, Amr bin Al-Aas na Mu’awiyah bin Abu Sufyan – wale mabingwa wawili wa njama, wa majungu, wa utata na ukweli wa mashaka, wa ulaghai na udanganyifu, wa mafumbo (kutoeleweka) kwa makusudi na umakini katika lengo – wakabuni ushirikiano, wa kuwa nguzo na kutegemeana wenyewe kwa wenyewe dhidi ya Ali ibn Abi Talib. Ushirikiano wao uliegemea, sio kwenye itikadi bali katika kutathmini maslahi yao ya pamoja. Wakati Mu’awiyah alipompa Amr ile nafasi muhimu katika kampeni yake ya mfumo wa madaraka kama mpanga mikakati mkuu wa kisiasa, yeye (Amr) hakuikubali mpaka malipo ya uhakika haraka yalipopatikana juu yake. Malipo hayo yalikuwa ni Misri.

Kwa kuchukulia kidokezi kutoka kwenye “utawala wa watu watatu” wa Basra, Amr alimshauri Mu’awiyah kuanzisha kampeni ya propaganda dhidi ya Ali akimshutumu kwa mauwaji ya Uthman. Mu’awiyah mara moja akutekeleza ushauri huo, na akafungulia vita baridi dhidi ya Ali.

Katika Msikiti mkuu wa Damascus, bendera ya Bani Umayya ilikunjuliwa kila siku baada ya Swala ya mchana. Kulikuwa na vitu viwili vikivyokuwa vimening’inia kwenye bendera hiyo. Kimoja kilikuwa ni shati lililokuwa na madoa ya damu ambalo Uthman anadaiwa kuwa alikuwa amelivaa wakati anauawa, na kingine kilikuwa ni vidole vya Naila, mke wake, vilivyokuwa vimekatwa. Watu wa Syria walitembea kuizunguka bendera hii, wakil- ia, na kupiga makelele na kumlaani Ali, watu wa familia yake, na Bani Hashim, na kuapia kwamba watamalizia kisasi chao juu ya wauaji wa Uthman. Maprofesa Sayed Abdul Qadir na Muhammad Shuja-ud-Din wameandika katika kitabu chao, History of Islam kwamba huu ulikuwa ni mwanzo wa desturi iitwayo “tabarrii.”

Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas waliichochea Syria kwenye mpagao, kiasi kwamba kila Msyria alikuwa ameingiwa na wazimu dhidi ya Ali, na akawa na kiu na damu yake. Baada ya miezi mitatu, mjumbe wa Ali alirudi Kufa kumtaarifu yeye kushindwa kwa ujumbe wake huko Damascus.

Mu’awiyah alikuwa amechagua vita dhidi ya Ali. Lakini Ali hakutaka vita. Alikuwa na shauku kubwa ya kuepuka vita. Hakuna kitu kilichokuwa kinachukiza sana kwake kama kuona Waislamu wanauana wenyewe kwa wenyewe.

Akitarajia kinyume cha matumaini, lakini bila kutaka kubakisha juhudi yoyote ile, Ali alimuandikia barua Mu’awiyah. Katika barua yake, hakujaribu kumkumbusha Mu’awiyah kwamba Mtume wa Allah swt. mwenyewe alikuwa amemteua yeye Ali kama mtawala wa Waislamu wote. Kwa Mu’awiyah, yeye Ali alijua, hoja hii haitakuwa na uzito sana. Badala yake, alichukua mwelekeo mwingine wa hoja ambao ulikuwa na uwezekano wa kuwa na “mvuto” kwake.

Madhumuni ya barua yake yalikuwa kama ifuatavyo: “Nakuomba umtii Allah na Mtume Wake, na ujiepushe na kufanya kitu chochote kinyume na maslahi ya Waislamu. Wewe unajua kwamba watu wale wale ambao walitoa kiapo chao cha utii kwa Abu Bakr na Umar, sasa wamenipa mimi kiapo chao cha utii. Hakuna nafasi ya ubishani juu ya suala hili. Wewe unajua kwamba Muhajirina na Ansari waliwachagua makhalifa waliotangulia, na sasa wamenichagua mimi. Waislamu wengine pia wamenipa kiapo chao cha utii. Wewe pia, kwa hiyo, unapaswa kunipa mimi kiapo chako cha utii. Umeeneza fitna na uongo mwingi kwa kisingizio cha kisasi cha damu ya Uthman ambapo unatambua vema kabisa ni nani aliyeimwaga damu hiyo. Baada ya kutoa kiapo cha utii kwangu mimi, wewe wasilisha kesi ya kuuawa kwa Uthman, nami nitaihukumu kwa kuzingatia Kitabu cha Allah swt. na vigezo vya Mtume Wake, ili kwamba ukweli na uongo viweze kujitenga.”
Lakini Mu’awiyaha hakutaka kuacha tamaa zake. Aliamini kwamba kitu kimoja kinachoweza kumkwamisha katika kufanikisha tamaa zake, kilikuwa ni amani. Yeye, kwa hiyo, alijionyesha mwenyewe kama tu “mwenye mzio” wa vita kama wale wa “utawala wa watu watatu” wa Basra walivyofanya kabla yake. Alikuwa na jibu moja tu kwenye maombi ya Ali juu ya amani, nalo lilikuwa ni vita.

Kwa mtazamo wa Mu’awiyah, kelele za kisasi kwa kifo cha Uthman, ilikuwa ni uvumbuzi mzuri sana wa kupigana dhidi ya Ali.

Alilia machozi mengi sana ya mamba (ya ghilba) kwa ajili ya damu ya Uthman lakini kwa tabia yake yeye mwenyewe, wakati wote wa kabla na baada ya kuuawa kwa Uthman, alithibitisha kwamba hakumjali kabisa Uthman. Aliandaa jeshi la wapiganaji 80,000 wa kupigana dhidi ya Ali lakini hakutuma angalau watu wachache kwenda Madini kuuvunja mzingiro wa kasri la Uthman, na kuokoa maisha yake!

Uthman angeweza kuliwazika kwa kujua kwamba siku ingefika ambapo wakosoaji wake watageuka kuwa wapenzi wake, na maadui zake kuja kuwa watetezi wake – baada ya kifo chake. Alikuwa na wakosoaji wengi sana hapo Madina, miongoni mwao wakiwa ni Aisha, Talha na Zubeir lakini mkali sana kuliko wote, kama ilivyoelezwa kabla, alikuwa ni Amr bin Al-Aas. Huyu kwa kweli, anaweza kuwa ndiye mpangaji mwenyewe hasa wa mauaji ya Uthman.

Lakini kwa ugeuzaji wa mambo usio wa kawaida, yeye - Amr bin Al-Aas – yule mshiri- ka wa Mu’awiyah – sasa alikuwa anatembea, mbele ya jeshi la Syria, kudai “haki” juu ya kifo cha Uthman, kati ya watu wote – kutoka kwa Ali!

Kama Talha na Zubeir – watangulizi wake maarufu katika kazi ya kutafuta kisasi – Amr bin Al-Aas naye pia ni somo la kuvutia katika kugeuza tabia upinduaji wa uhusikanaji na dhihaka. Alikuwa ni mtu mgumu, kitendawili na kigeugeu anayedharau majaribio katika uchambuzi, upambanuzi na uainishaji wa mwenendo.

Moja ya malengo ya Mu’awiyah ya kuanzisha vita vya wasiwasi dhidi ya Ali lilikuwa ni kumlazimisha yeye kutwaa sera ya ukomeshaji wa kikatili juu ya wale watu wote waliokuwa wamekuja Madina kutoka majimboni kumuona Uthman. Sera kama hiyo ingemuingiza Ali katika utatanishi wa mapigano yasiyo na mwisho. Lakini Ali hakutwaa sera ya ukomeshaji. Alitwaa sera ya ushawishi, kwa masikitiko makubwa sana ya Mu’awiyah. Mpango wa Mu’awiyah haukufanya kazi.

Mu’awiyah alidai kutoka kwa Ali, kama wale “watawala watatu” wa Basra walivyofanya, kukabidhiwa kwake watu wasio na idadi ambao yeye alidai, walishiriki moja kwa moja au kwa kificho, katika mauaji ya Uthman. Madai haya yanazua maswali ya msingi kama vile:

1. Hivi gavana wa jimbo la nchi anayo haki ya kudai kutoka kwenye serikali kuu iliyowekwa kisheria kwamba imkabidhi yeye watuhumiwa wa kesi ya mauaji, hata kama mauji hayo hayakutokea kwenye jimbo lake husika? Na je, anayo haki ya kuitishia hiyo serikali kuu kwamba kama haikutekeleza madai yake, yeye ataanzisha vita dhidi yake?

2. Mu’awiyah hakuwa ama mrithi wala ndugu wa karibu wa Uthman; alikuwa ni jamaa wa mbali tu. Kuna mfano wowote katika historia ya mahakama ya nchi yoyote ile ambamo, sio yule ndugu wa karibu, bali jamaa wa mbali anayedai kutoka serikali kuu kwamba imkabidhi mamia au maelfu ya wale watu ambao anawashuku kuwa washiriki katika mauaji? Je, anaweza kuchukua sheria mikononi mwake mwenyewe? Serikali kuu ya nchi inaweza kuruhusu raia zake kuchukua sheria mikononi mwao wenyewe? Kama inaweza, kuna chochote kitakachobakia katika madaraka yake, na kutasalia chochote katika sheria na taratibu?

3. Mu’awiyah aliandikiana barua nyingi na Ali. Katika mojawapo aliandika: “Tutawawinda wauaji wa Uthman katika kila pembe ya dunia, na tutamuua kila mmoja wao. Hatutapumzika katika kazi hii mpaka, ama tunawaua wote au tunakufa sisi wenyewe.” Azimio la kupendeza kwelikweli! Lakini wakati Mu’awiyah alipoku- ja kuwa khalifa, alilitekeleza azimio lake mwenyewe?

Baada ya kujiuzulu kwa Hasan bin Ali katika ukhalifa mwaka 661A.D., Mu’awiyah akawa mkuu wa dola ya Waislamu. Wauaji wote halisi au wa kushukiwa walikuwa wanaishi katika himaya yake.

Je, alimkamata yoyote kati yao, ukiachiliambali kumuua yoyote kati yao? Je, alijitahidi japo kiasi cha kuanzisha uchunguzi rasmi katika mauji ya Uthman? Hakufanya hivyo. Shauku yake ilikuwa ni kuukamata ukhalifa. Mara alipofanikiwa na hilo, akamsahau Uthman!

Ukweli ni kwamba Mu’awiyah kwa kweli alitaka Uthman auawe. Yalikuwa ni matumaini yake kwamba kutakuwa na ghasia baada ya kifo cha Uthman, na ataweza kufanya hila ndani yake msukumo wake wa kutwaa madaraka.

Pale alipodai kutoka kwa Ali kukabidhiwa wale “wauaji” wa Uthman, alikuwa anajua kwamba walikuwa wametawanyika katika Hijazi, Iraqi na Misri, na kwamba ilikuwa ni vigumu kuwakusanya pamoja. Lakini ukichukulia kwamba ilikuwa inawezekana kuwakamata, bado haikuwa ni rahisi kuwaua wote. Lakini kama ingewezekana kuwaua wote, bado ingekuwa sio haki kuwaua wote kwa sababu ya kuuawa kwa mtu mmoja.

Kutafuta na kulipiza kisasi kwa ajili ya mauaji, ni haki ya mrithi/warithi wa muathirika, na ni wajibu wa serikali kutekeleza haki. Mu’awiyah alikuwa sio mrithi wa Uthman wala alikuwa sio kiongozi wa serikali ya Waislamu. Alikuwa si zaidi ya mrithi kuliko Aisha, Talha na Zubeir walivyokuwa. Shauku yake na yao ilikuwa ni katika kuukamata ukhalifa tu.

Kama Mu’awiyah hakuweza kushughulika katika wakati muafaka kuokoa maisha ya Uthman, alikuwa bado anayo nafasi ya kuthibitisha kwamba alikuwa ni mlipiza kisasi wa kweli wa kifo chake. Wakati walipiza kisasi wengine watatu, yaani, Aisha, Talha na Zubeir walimpinga Ali, Mu’awiyah angekwenda kwenye msaada wao. Hata hivyo, wote wanne walikuwa wametiwa msukumo na nia hiyohiyo.

Mauaji ya Uthman yameamsha kiu ya damu kwao wote. Kufanana kwa lengo kulipaswa kuunda uhusiano mzito baina yao. Lakini sababu yoyote ile iliyomzuia Mu’awiyah kwenda Madina kuokoa maisha ya Uthman, pia ilimzuia kwenda Basra kuwaongeza nguvu washirika wake wa “kiroho”.

Madai ya kwamba Mu’awiyah hakuwa na haja yoyote na Uthman, akiwa hai au amekufa, yanatiwa nguvu zaidi na majibu yake ya swali aliloulizwa na binti ya Uthman.

Wakati alipokuwa khalifa, alitembelea Madina. Hapo Madina, aliitembelea familia ya Uthman ambaye binti yake, aitwaye Aisha, alimuuliza yeye, kwa kukusudia hasa, kama alikuwa bado anakumbuka chochote kuhusu tangazo lake alilokuwa akilirudia mara kwa mara kwamba alikuwa anatafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha baba yake.

Mu’awiyah alimjibu binti huyo kama ifuatavyo: “Nimefanikiwa katika kurudisha amani katika nchi baada ya matatizo mengi, na wewe unapaswa sasa kufurahi kwamba unaitwa binti ya khalifa mmoja na mpwa wa khalifa mwingine. Lakini kama kwa ajli yako, ningekuwa mwenye kuwakamata na kuwaua wale wauaji wa baba yako, basi amani ile ingetoweka kwa mara nyingine tena. Ikiwa itatoweka, basi ninaweza kupoteza yale madaraka ambayo nimeyapata baada ya jitihada ngumu kama hizo; na kama hilo likitokea, basi wewe utashushwa kwenye hali ya mwanamke wa kawaida.”(Iqd-ul-Farid)

Mu’awiyah, myakinifu, alikuwa na uwezo mkubwa mno na wa kushangaza wa kutumia lugha ya utatanishi! Kwa Mu’awiyah, kufikia malengo yake, njia zote zilikuwa ni nzuri. Hapakuwa na kitu ambacho yeye hakuweza kukifanya ili kuwa khalifa wa Waislamu.

Aliweza kwa kweli, kwenda mbali zaidi kiasi cha kuweza kuwa mtwana wa mamlaka yasiyokuwa ya Kiislamu kupigana dhidi ya mrithi halali wa Mtume wa Allah swt., na mtawala wa Waislamu wote. Kwa kufanya hivyo, alikuwa anaunga mkono sera ambayo ilijitokeza kwenye mizizi hasa ya Uislamu.

Sir John Glubb:

“Ili kuweza kuwa huru kumkabili mpinzani wake (Ali), Mu’awiyah alikuwa amekamilisha makubaliano ya kusitisha vita na Byzantium ambamo alikubali kulipa ushuru wa mwaka kwa Mfalme.”
(The Great Arab Conquests, uk. 338, 1967)

D. M. Dunlop:

“Kabla Mu’awiyah hajafanikiwa kwenye Ukhalifa, wakati baada ya Siffin alibakia kwenye makabiliano na Ali, alijiimarisha mwenyewe katika mpaka wake wa kaskazini kwa makubaliano ya kusitisha vita na Byzantium, kwa masharti ambayo kwamba alikubali kulipa ushuru ambao ulikuwa unatambulika, kwa Mfalme Constans II, na mnamo mwaka 678 kuelekea mwishoni mwa Ukhalifa wake, baada ya kushindwa kwa uvamizi mkubwa wa Waarabu juu ya Constantinople katika vile vinavyoitwa Vita vya Miaka Saba na shambulio la Mardaites katika mpaka wake wa kaskazini, Mu’awiyah akalipa tena ushuru kwa Mfalme, wakati huu akiwa Constantine IV. Katika tarehe za baadaye majeshi ya Byzantium yaliivamia Syria na wakaitwaa tena Antiokia na Aleppo.” (Arab Civilization to A.D. 1500, 1971)

Hiki “cheo” kipya ambacho Mu’awiyah alikipata kama mtwana wa mfalme wa Byzantium, kilimpa uhuru wa kupigana vita dhidi ya Ali ibn Abi Talib, mrithi wa Muhammad, Mtume wa Allah swt. Alipigana dhidi ya Kiongozi wa Waumini, dhidi ya wakongwe wa Badr, dhidi ya masahaba wa ule Mti wa Kiapo, na dhidi ya Muhajirin na Ansar akiwa amelind- wa na Wakristo wa Himaya ya Roma Mashariki!

Lakini kwa Mu’awiyah, kuwa mwenye “kigeugeu,” dau halikuwa lazima liwe la ukubwa kama taji na ufalme. Aliweza kuwa kigeugeu katika mambo yenye umuhimu mdogo pia. Alikuwa kwa mfano, na hisia za kupenda sana pesa, na aliamini kwamba katika kuichuma, ugumu mwingi mno “uliopitwa na wakati” katika matumizi ya kanuni za Kiislam haukuwa wa lazima hasa. Jambo muhimu kwake lilikuwa ni kutengeneza pesa. Ibn Ishaq, mwan- dishi wa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.), amekwisha kunukuliwa tayari juu suala la kukamat- wa na Mu’awiyah kwa mali ya al-Hutat bin Yazid al-Mujashi’i, “kaka” yake, wakati wa kifo chake. “Udugu” huu ulifanya kazi wote kwa manufaa yake Mu’awiyah. Ili kujaza mifuko yake, aliweza hata kuuza masanamu. Mu’awiyah, mrithi wa Abu Bakr, Umar na Uthman, na khalifa wa Waislamu, aliweza kuwa mchuuzi wa masanamu kama alitegemea kwamba angeweza kupata faida katika shughuli hiyo.

Sir John Glubb:

“Sicily ilivamiwa zaidi ya mara moja na kundi la manowari za Waarabu wakati wa utawala wa Mu’awiyah. Hadith ya udaku inasimulia kwamba safari moja wavamizi walibeba ‘masanamu’ ya dhahabu na fedha, yaliyotapakaa lulu. Huenda pengine ina maana ya mabadiliko ya fikira za Waarabu kwamba huyu khalifa badala ya kuangamiza kabisa machukizo kama hayo, aliyapeleka India, ambako alidhania kwamba mauzo yao yatampatia bei kubwa.” (The Great Arab Conquests, uk. 355, 1967)

Uuzaji wa masanamu wa Mu’awiyah bin Abu Sufyan ulikuwa ni uibukaji wa wazi wa marudio ya uovu wa Bani Umayya. Vitendo vyake vilichochewa na juu ya misingi, sio ya manufaa yaliyoonyeshwa (ya Kiislamu), bali ya yaliyozoeleka (ya kipagani), ambayo yalikuwa ni sifa bainifu za jina na nasaba ya Bani Umayya. Yeye alikuwa, inavyoelekea, akitafuta, labda kwa kujificha, ule “Ujinga Uliopotea” wa nasaba yake. Yeye aliurudisha na kuupamba ule Ujahiliya wa kabla ya Uislamu. Upinzani wake kwa Ali, kwa hiyo, haukuwa tu au hata kimsingi wa kimaumbile tu; ulikuwa wa udhanifu. Uislamu kama nguvu ya kimaadili, ulipambana na tishio baya sana kutoka kwa Mu’awiyah na kwa Bani Umayya.