read

Umar Bin Al-Khattab, Khalifa Wa Pili Wa Waislamu

Katika Nyakati za Ujahilia, Umar aliishi kama dalali. Shibli, mwandishi wa wasifa wake, anasema kwamba katika ujana wake alichunga ngamia.

Kabla ya kusilimu, Umar alikuwa mmoja kati ya maadui wenye msimamo mkali sana, wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.)

Pale Muhammad (s.a.w.) alipotangaza ujumbe wake, watu wengi walimkubali yeye kama ni Mtume wa Allah (s.w.t.) Umar alimtambua kama Mtume wa Allah (s.w.t.) baada ya miaka sita.

Wanahistoria wengine wanadai kwamba Umar alikuwa mtu wa kutisha sana, na aliposilimu, wale waabudu masanamu walishikwa na hofu juu ya maisha yao. Lakini hili ni suala la uongo unaojitokeza unaopingana na ukweli unaotisha. Wakati Umar aliposilimu, waabudu masanamu walibakia pale walipokuwa, na hakuna kilichobadilika kwao; lakini alikuwa ni Muhammad aliyelazimika kuondoka nyumbani kwake, na ikambidi atafute hifadhi katika korongo linalohuzunisha.

Aliishi kwa miaka mitatu katika korongo hilo, na katika miaka hiyo mitatu ya uhamishoni, maisha yake yalikuwa kwenye hatari mbaya sana kila mchana na kila usiku.

Katika kipindi chote hiki cha siku zaidi ya 1000, Umar, kama Waislamu wengine wengi hapo Makka, alikuwa ni mtazamaji mkimya wa mateso ya bwana wake. Hakufanya jaribio lolote la kumaliza mateso hayo.

Muhammad Mustafa (s.a.w.) alianzisha udugu kati ya Waislamu, kote - hapo Makka na kule Madina. Hapo Makka, alimfanye Umar kuwa “ndugu” wa Abu Bakr, na kule Madina, alimfanya yeye kuwa “ndugu” wa Utban bin Malik. Kwa kuwa ndugu yake yeye mwenyewe, Muhammad alimchagua Ali ibn Abi Talib katika miji yote miwili. Katika mwaka wa 3 A.H., binti yake Umar, Hafsa, aliolewa na Mtume (s.a.w.).

Umar alikuwa ni mmoja wa watoro wa vita vya Uhud (Baladhuri). Yeye mwenyewe alisema baadaye kuwa: “Pale Waislamu waliposhindwa kule Uhud, nilikimbia kuelekea mlimani.”
(Suyuti katika al-Durr al-Manthur).

Katika kuizingira Khaybar, Umar alifanya jaribio la kuiteka ile ngome lakini alishindwa. Umar alikuwa mmoja wa watoro wa vita vya Hunain. Abu Qatada, sahaba wa Mtume (s.a.w.) anasema: “Huko Hunain wakati Waislamu walipokuwa wakikimbia, nami pia nilikimbia, na nilimuona Umar pamoja na wengine.” (Bukhari na Kitabul-Maghazi).

Katika mwaka wa 8 A.H. Mtume (s.a.w.) alimtuma Umar kama mpiganaji wa kawaida pamoja na wengineo kwenda kupiga ripoti kikazi kwa Amr bin Al-Aas, kamanda wao, kati- ka vita vya Dhat es-Salasil.

Mnamo mwaka wa 11 A.H. Mtume wa Allah (s.w.t.) alitayarisha ule msafara wa Syria na akamteua Usamah bin Zayd bin Haritha kama kamanda mkuu wake. Alimuamuru Umar kutumikia kama mpiganaji wa kawaida kwenye msafara huo.

Ingawa Umar aliishi miaka kumi na nane akiwa pamoja na Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) yeye Mtume (s.a.w.) hakuwahi kumchagua kwenye nafasi yoyote ya mamlaka – ya kiraia au kijeshi.

Wakati Mtume wa Allah (s.w.t.) alipokuwa kwenye kitanda chake cha mauti, aliwataka maswahaba wamletee kalamu, karatasi na wino ili aweze kutamka wasia wake lakini Umar alimpuuza. Hakumuacha Mtume (s.a.w.) atamke wasia na mirathi yake.

Umar hakuwepo kwenye mazishi ya Mtume wa Uislamu. Alikuwa akizozana na Ansari katika banda la Saqifah wakati mwili wa Mtume (s.a.w.) ulipokuwa unazikwa. Umar alikuwa ndio mtengeneza ukhalifa wa Abu Bakr. Katika ukhalifa wa Abu Bakr, Umar alikuwa ndiye mshauri wake mkuu.

Bani Umayya walikuwa ndio mabingwa wa jadi wa uabudu masanamu na maadui wakubwa wa Muhammad na ukoo wake, Bani Hashim. Muhammad (s.a.w.) alikuwa ameyavunja madaraka yao lakini Umar akayafufua. Sehemu kuu ya sera zake, kama mkuu wa serikali ya Saqifah, ilikuwa ni kuwarejesha Bani Umayya. Aliitoa Syria kwao kama “ada” yao (anayolipa mtu kwa kupewa himaya), na akawafanya wao kuwa ukoo wa kwanza kati- ka himaya hiyo.

Mwanafunzi wa kisasa wa historia anaweza kukuta madai yaliyofanywa kwa niaba ya maswahaba wa Mtume (s.a.w.) kama yaliyotiwa chuku na yenye kukanganya. Anaweza kugundua ndani yake mgongano wa dhana zenye kupendwa, na ukweli wa kihistoria. Lakini kama atapenda kufanya tathimi ya hali halisi ya tabia walizofanya katika uhai wa Mtume (s.a.w.), hakuna njia bora ya kufanya hivyo mbali na kuyapa kisogo maneno ya kuonyesha nderemo na balagha, na kuweka mazingatio kwenye ukweli na ukweli pekee.

Matukio Makuu Ya Ukhalifa Wa Umar

Wakati Umar alipochukua madaraka ya ukhalifa, majeshi ya Waislamu yalikuwa yanapi- gana dhidi ya Wafursi huko Iraq na Warumi huko Syria. Jeshi lililokuwa Syria lilikuwa chini ya uongozi wa Khalid bin al-Walid, yule jenerali kipenzi cha Abu Bakr. Kitendo cha kwanza cha Umar kama khalifa kilikuwa ni kumfukuza kwenye ukuu wake wote, na kumteua Abu Ubaidah bin al-Jarrah kama kamanda mkuu wa majeshi ya Waislamu yaliyokuwa Syria.

Shibli anasema kwamba Umar alikuwa, kwa muda mrefu, na chuki ya siri juu ya Khalid kwa sababu ya maovu yake mabaya kupindukia. Umar kweli alimfukuza Khalid kwa sababu ya maovu yake mabaya mno lakini inaonekana kwamba chuki binafsi pia ilikuwa ikifanya kazi. Alikuwa na wivu juu ya umaarufu na kupendwa kwa Khalid.

Kama alichukia kuvuka mipaka kwa Khalid, alipaswa kumshitaki rasmi, na angeagiza uchunguzi kamili wa uhalifu wake katika kumuua Malik ibn Nuweira na katika kumtwaa bila haki mjane wake.

Kama Khalid angethibitika kuwa na hatia, basi Umar angepaswa kutoa hukumu juu yake kwa mujibu wa sheria ya Kiislam. Lakini hakukuwa na mashitaka wala uchunguzi. Khalid alifukuzwa papo hapo na alikufa katika umasikini na mashaka mnamo mwaka 21A.H.

Ukhalifa wa Umar ni mashuhuri sana kwa utekaji wake mwingi. Majenerali wake waliteka Iraq, Iran, Azerbaijan, Kirman, Seistan, Khurasan, Syria, Jordan, Palestina na Misri, na akaziunganisha zote na kwenye himaya ya Waislamu. Wote huu ulikuwa ni ushindi wa kudumu. Warumi waliipoteza Syria, Palestina na Misri daima; na huko Uajemi, ule ufalme wa Sassani ukakoma kuwepo.

Miongoni mwa matukio mengine ya ukhalifa wa Umar, lilikuwemo lile la kuzuka kwa tauni huko Syria mnamo mwaka 18 A.H., na njaa huko Hijazi katika mwaka huo huo. Kati ya hayo, ile tauni na njaa viliua zaidi ya watu 25,000 (Suyuti na Abul Fida).