read

Utangulizi

Hii Ni Historia Mpya Ya Uislamu. Ni historia ya vuguvugu la Uislamu ambalo lilianzishwa na Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) mnamo mwaka 610 A.D. huko Makka, na ulikamilishwa kwa msaada wa binamu yake, mshiriki na mshikamakamu wake, Ali ibn Abi Talib, mnamo mwaka 632 A.D. hapo Madina.

Inahusisha kipindi cha miaka tisini kuanzia 570 A.D. wakati yeye Muhammad alipozaliwa huko Makka, hadi mwaka 661 wakati mrithi wake, Ali ibn Abi Talib, alipouawa huko mjini Kufah.

Historia zisizo na idadi zimeandikwa huko nyuma na zitaandikwa wakati ujao. Maendeleo ya kuvutia ya Uislamu katika nyanja ya ulinganiaji katika nyakati zetu wenyewe; kufufuka upya kwa mataifa ya Kiislamu baada ya karne nyingi za usingizi mzito; kujidukiza kwa mafuta kama wakala mpya katika siasa za kidunia katika karne hii; bali juu ya yote na hivi karibuni kabisa, yale mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ndani ya Iran, yote Haya yanakuwa, kote Mashariki na Magharibi, kama vichocheo vya shauku mpya katika Uislamu.
Mapinduzi ndani ya Iran yamechokonoa mlipuko wa dunia nzima wa mvuto katika Uislamu, na vitabu vingi vipya vinaandikwa juu ya somo hilo – na wote, Waislamu na wasiokuwa Waislamu.
Siku hizi wakati viongozi wa dunia ya Kikristo wanapofanya kazi kimyakimya ili kufanik- isha ndoto ya siku nyingi ya imani ya umoja wa Kikristo, Waislamu wengi pia wanaangalia nyuma kwa hamu kubwa kwenye lile taifa bora wakati Uislamu ulipokuwa mfumo wa mawazo ya aina moja. Uislam, hata hivyo, ulikuwa mfumo wa mawazo ya aina moja tu wakati wa uhai wa Mtume wake, Muhammad aliyebarikiwa.

Mara tu alipofariki, ufa wa kwanza ulijitokeza katika ile “nguzo imara” ya Uislamu. Wafuasi wake – Waislamu – walikingamizwa kwenye makundi mawili. Katika kingamizo hili, wengi wa maswahaba zake walikuwa upande mmoja na watu wa nyumbani kwake kwa upande mwingine. Wakati watu wa nyumbani kwake wakiwa wameshughulishwa na mazishi yake, baadhi ya maswahaba zake walishughulika katika “kuchagua” kiongozi mpya wa kumrithi Mtume.

Katika ule mwanya kati ya kifo na mazishi yake, hili kundi la mwisho (la maswahaba) lilijikusanya katika banda la Saqifah hapo Madina, na likamchagua mmoja kati yao wenyewe kama mkuu mpya wa umma wa Waislamu. Wao, kisha wakawakabili watu wa ile familia iliyoondokewa kwa jambo lililokwisha fanywa na kuthibitishwa. Mkabiliano huu, kwa bahati mbaya sana, ukawa Sura ya kudumu ya historia ya Waislamu.

Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t,), Rehma na amani juu yake na juu ya Ahlul-Bayt wake, alitokana na ukoo wa Bani Hashim. Baada ya kifo chake mwaka632 A.D., binamu yake, mkwe wake na mrithi mstahiki wake, Ali ibn Abi Talib, alimfuatia yeye kama mkuu mpya wa Bani Hashim. Wengi wa maswahaba wa Muhammad, Mtume wa Uislamu, walikuwa wamelea uadui wa siri juu yake.

Hawakuweza kumuonyesha uadui wao wakati wa uhai wake Mtume lakini mara walipokuwa na amri juu ya serikali yake hapo Madina, walikuwa wameazimia, kutoiachia, kwa kukosea kwa namna yoyote ile, iangukie kwenye mikono ya Ali ibn Abi Talib.

Watu wa nyumba ya Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) hivyo walizuiwa, kwa nguvu kubwa ya wanadamu, sio tu kwenye urithi wa moja kwa moja bali pia kwenye nafasi zote za mamlaka na madaraka katika serikali za wafuasi wake zilizofuatia.

Marafiki, wafuasi na wanaounga mkono nyumba ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) wamekuwa kihistoria wakiitwa Shia; na marafiki, wafuasi na wanaowaunga mkono maswahaba, yaani, lile kundi lililofanikiwa kutwaa madaraka hapo Madina, limekuwa likiitwa Sunni. Nitayatofautisha pia makundi haya mawili kwa majina haya.

M. Shibli, mwanahistoria mashuhuri wa Kihindi wa Uislamu, anasema kwamba takriban historia zote za Uislamu zimeandikwa na wanahistoria wa Sunni. Kauli hii inamaanisha kwamba wanazuoni wa Shia hawakuandika historia yoyote ya Uislamu. Kwa nini hawakuandika? Hawakuandika historia kwa sababu ya wazi. Makhalifa wote, masultani na wafalme, wote walikuwa Sunni.

Aliyekuwa Shia hakuweza kuchapisha ufafanuzi wa historia ya Kiislamu ambao ulikuwa unatofautiana na ule ufafanuzi wa kiserikali, na hakuwa na haja ya kuendeleza kile alichoamini kuwa ni upotoshaji wa ukweli. Yeye, kwa hiyo, aliamua kutoandika historia yoyote kabisa.

Kwa namna hii, yalikuwa ni yale “maelezo” ya kiserikali ya historia ya siku za mwanzo za Uislamu ambayo yalipata kuenea na yakapata kukubalika. Lilikuwa ni jambo la kimantiki kabisa la kufanya kwa serikali za karne za mwanzoni za Uislamu kuingiza kwenye mzunguko, ile hekaya tu, ambayo ilikuwa inakubaliana na itikadi ya kundi lao.

Ilikuwa pia na mantiki kabisa kwa wafuasi wa sera za serikali hizo tunazozizungumzia, kutii itikadi hiyo. Na katika kutii itikadi hiyo ya kundi, kama walihisi kwamba ni muhimu kufunika ukweli, au kwa kiwango chochote, kufunika ule upande mwingine wa Hadith hiyo, ilikuwa na mantiki kabisa kufanya hivyo.

Hakuna jambo lolote la ajabu, la kushangaza au kushitusha katika mwenendo wa wanahistoria wa Sunni. Kitu chenye mantiki kabisa kwao kukifanya kilikuwa, na bado ni, kutetea uhalali wa matukio ambayo yalitukia ndani ya Saqifah, ambamo baadhi ya maswahaba, katika shambulizi la kuwahi kabla ya wengine, walitwaa serikali ya Muhammad, kiongozi wa Arabia.

Kile ambacho hata hivyo ni cha kushangaza na cha kushitusha, ni kwamba wanahistoria wa kimagharibi, yaani, wale Mustashriq, wamemeza, kama jambo la kweli kabisa, kila ambalo wanahistoria wa “baraza” la Kiislamu limewachotea wao kama “ukweli.” Hawa Mustashriq wanadhaniwa kwamba hawana upendeleo, sio wafuasi, na wasiohusika kwa jazba kwa hali yoyote ile. Matokeo ya mashindano fulani katika zama za kale za Uislamu, kwa njia moja au nyingine, yasingeweza kuleta tofauti yoyote kwao.

Na bado, vitabu vya wengi wao vinaonyesha, sio ukweli bali ufafanuzi na propaganda za kundi lililokuwa madarakani. Kwa maana hii, kazi zao ni uigaji wa vile vitabu “vilivyotiwa msukumo” na kile Wakomunisti wanachokiita “jamii inayotawala” ya Waislamu.

Vitabu vya Mustashriq vinaweza kuwa na maana ya kisayansi tu kama watachukua ushauri wa mwanahistoria mashuhuri wa Hispania ya Kiislamu, Dr. J. A. Conde. Yeye anasema:“Namna ya msiba unaojiingiza wenyewe kwenye mambo ya wanadamu unaweza kuelekea kudai kwamba katika uhusiano wa matukio ya kihistoria, yale yenye umuhimu wa hali ya juu kabisa, yashuke kuvifikia vizazi vijavyo kupitia kwenye njia zinazotiliwa mashaka kwa haki kabisa, za simulizi zilizoandikwa na makundi yanayoshinda. Mabadiliko ya falme, mapinduzi ya maana kabisa na kuangushwa kwa falme maarufu za kiukoo yote haya yanaelekea kuwajibika na kasoro hii.

Ilikuwa ni kutokana na Warumi kwamba historia ya kujitwalia kwao wenyewe iliandikwa; simulizi za upinzani wao na vita vya umwagaji damu dhidi ya wa- Carthaginia zimetufikia sisi kutoka kwao wenyewe; au kama waandishi wa Kigiriki nao pia wamelijadili suala hili, watu hawa walikuwa ni walipa kodi na wategemezi wa Roma, wala hawakuzificha zile sifa zisizostahili zilizokusudiwa kuunga mkono fadhila yake. Scipio kwa hiyo anaonekana kwetu kama mtu anayevutia sana kati ya mashujaa, lakini je, sio kwamba kwa kiasi fulani hivi, ni kwa sababu historia ya maisha yake ni kazi ya mashabiki na wasifiaji wake?

Ni kweli kwamba yule Hannibal mwenye daraja kubwa na maarufu hawezi kuonekana vinginevyo zaidi ya mashuhuri na kwenye heshima hata katika masimulizi ya maadui zake wabAya kabisa, lakini kama ile chuki isiyotulizika na sera za uchokozi za Roma zisingeamuru kuteketezwa kwa zile kumbukumbu za kisaliti (za wa-Carthaginia), jenerali huyu maarufu bila shaka angetokezea kwetu kwa sifa inayotofautiana sana na ile iliyowasilishwa na yule mshenzi katili, aliye elezewa na Livy na kukubaliwa na wasomaji wake kama ndio taswira ya Hannibal.

Kwa hiyo utambuzi thabiti na wa haki unatukataza sisi kutosheka wenyewe na ushahidi wa upande mmoja tu. Hii inahitaji kwamba tulinganishe mahusiano ya makundi yote kwa uadilifu makini, na inatutaka sisi kuyaonyesha bila ya lengo jingine zaidi ya lile la kuugundua ukweli.” (History of the Dominion of the Arabs in Spain - kilichotafsiriwa kutoka kwenye ki Hispania na Mrs. J. Foster, Juz. I, uk. 1)

Haiwezi kupingika kwamba Mustashriq wengi wametoa michango isiyofaa kabisa kwenye uchunguzi, elimu na ufahamu wa Uislamu. Ni kutokana tu na jitihada zao kwamba hazina nyingi zisizo na thamani, za historia, fani na fasihi za Kiislamu zimeokolewa kutokana na kusahaulika, na zimekuwa zimehifadhiwa. Inawezekana kabisa kwamba hazina nyingi kama hizo zingeweza kupotea daima kama isingekuwa kwa juhudi zao za kuziokoa.

Miongoni mwao kuna watu ambao wana ufahamu wa kushangaza wa kina wa mafunzo ya Kiislamu, na ambao elimu zao ni za ki-ensaiklopidia kwa upana. Wamesoma na kupata viwango vikubwa vya maelezo, na kisha wameyafupisha, wakayapanga na kuyahariri katika uchambuzi wa kistadi na wa ukosoaji. Wengine wao wamejitolea maisha yao na mali zao kwenye uchunguzi wa Uislamu, na k wao wao ulimwengu wa Kiislamu una deni kubwa la shukurani.

Lakini licha ya mapenzi na hamu ya elimu, na kujifunga kwenye ukweli kwa wanafunzi wa Magharibi, inaonekana kwamba wakati wengi wao wanapoufafanua Uislamu, historia yake na sheria zake, jambo fulani huenda kombo.

Ni vigumu kuamini lakini ni kweli kwamba baadhi yao wanaonyesha kushindwa kwa ajabu kupenyeza kwenye mwonekano wa kawaida na usiobadilika wa matukio kwenye mambo na nguvu, na ukweli ulio dhahiri ambavyo wakati mwingine vimefichwa kwa makusudi. Na baadhi yao wanashindwa hata kuona yaliyo dhahiri.
Nimenukuu hapo juu utaratibu wa kuandika historia ya kisa yansi na isiyo na upendeleo kama ulivyoelezwa na Dr. J. A. Conde, ambaye yeye mwenyewe ni Mustashriq maarufu sana. Kanuni hii, yaani ile ya, hakuna ubigwa wa hukumu na maamuzi katika historia, inat- ulia katika akili ya kwaida, na hauna kitu cha ajabu juu yake. Na bado, wengi wa Mustashriq wameyakubali, kwa wepesi wa kusadiki ambao ni wa kipumbavu, yale maele- zo ya matukio yaliyotokea punde tu kufuatia kifo cha Muhammad (s.a.w.), kama yalivyotolewa na lile kundi lililofanikiwa katika kujitwalia lenyewe utawala wake (Muhammad s.a.w.).

Mfano wa dhahiri wa uzuzu huo, na msingi wa kutotambua wa hawa Mustashriq, kuhusu suala hili, ni kule kukubaliwa na wao, kama “ukweli” wa kihistoria wa ile taarifa ya uwongo kwamba Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) alifariki bila ya kumteua mtu yeyote kama mrithi wake, na kwamba aliliacha suala la kumtafuta kiongozi wa umma wa Waislamu kwenye hiari ya wafuasi wake wenyewe.

Hakuna Mustashriq aliyesita na kufikiria, kwa kiasi ninavyotambua mimi, ili kuchunguza kama hili ni kweli au kama ni lenye uwezekano wa kuwa kweli kwamba Muhammad ali- watelekeza Waislamu bila ya kiongozi, na ikawabidi kumpata kiongozi katika mfumo usio na mipaka na unaoruhusu kila mbinu, wa kikatili, huru kwa wote na kushindana kwa ajili ya madaraka. Ili kuepukana na kazi ngumu ya kutafuta ukweli, Mustashriq wamekubaliana tu na wanahistoria wa Sunni kwamba Muhammad, Mtume wa Uislamu, hakuwa na chaguo au upendeleo katika suala la urithi wake mwenyewe; na lolote lililotokea ndani ya Saqifah kwa hiyo, lilikuwa ni sawa na halali, na pia lilikuwa kwa faida kubwa ya umma wa Waislamu.

Huu muegemeo wa uungaji mkono Saqifah wa Mustashriq umewaingiza kwenye njia ya upofu ambamo hawawezi kupata majibu ya maswali ya msingi katika historia ya Uislamu, na wanajikuta wenyewe wamenasa, kama walivyonasa wanahistoria wa Sunni, kwenye nyavu za ukweli wenye mashaka na hitilafu nyingi.

Wanahistoria wengi wa Sunni na wengi miongoni mwa Mustashriq wamefanya majaribio ya makusudi ya kuipunguza nafasi iliyochukuliwa na Ali ibn Abi Talib katika historia ya Uislamu. Wao, bila shaka, wanastahiki kwenye maoni na dhana zao hata kama hizi hazikuthibitishwa na ukweli. Katika uwasilishaji wangu, nimejitahidi kuweka mkazo juu ya ukweli.

Kwa kufanya hivyo, imekuwa ni matumaini yangu kwamba ukweli wenyewe utachukua nafasi kama “muamuzi.” Kwa vile ukweli ni “muamuzi” asiyekuwa na upendeleo, anaweza kutegemewa kurudisha uwiano kwenye uchambuzi wa nafasi zilizochukuliwa na wahusika wakuu katika historia ya Uislamu mchanga. Nimeuchagua (ukweli) na nimeutunga pamoja, kama lulu, kwenye “mkufu”, ili kwamba wingi wa ukweli huo uweze kuonekana mahali pamoja.

Historia haina mahakama ya juu inayotoa fatwa; inao waandika tarikh tu, wenye kuweza kukosea. Na bado, historia inaweza kupata mahakama yake ya juu yenyewe au mahakama isiyopendelea, kwenye mantiki ya ukweli.

Ninayo sababu nyingine na ya mawazo yakinifu ya kutegemea juu ya ukweli. Kwa kuandi- ka Hadith ya siku za mwanzoni za Uislamu, vipo vyanzo vikuu vitatu, navyo ni, Qur’an Tukufu (kitabu cha Uislamu kilichoteremshwa); Hadithi (kumbukumbu za matendo na maneno matukufu ya Muhammad, kama yalivyosimuliwa kwa sanad ya watoa habari au wasimulizi); na matukio kama yalivyoandikwa na wanahistoria wa Kiarabu. Kati ya vitatu hivi, kile cha kwanza, yaani, Qur’an, inakubaliwa na Waislamu wote kuwa ni takatifu kiasili. Kama mwislamu anapinga maandiko ya Qur’an, papo hapo anakuwa kafiri.

Lakini wakati ambapo maandikoko ya Qur’an, kwa kadiri Waislamu wanavyohusika, Hayakuvunjwa, Aya zake ni zenye kupatwa mara kwa mara na hitilafu na wakati mwingine (na) tafsiri zinazopingana, na hakuna kitu kama makubaliano ambamo, au ambayo tafsiri zake ni sawasawa. Hadithi vilevile zinapatwa na kikwazo; nyingi sana kati ya hizo ni za bandia ingawa kuna baadhi ambazo zinakubaliwa na wote, Sunni na Shia kuwa ni sahihi. Nimejaribu kwa hiyo, kuwa mchaguzi katika kuzidondoa zile Aya tu za Qur’an na zile Hadithi (maneno ya Mtume) zenye maelezo ambayo tofauti kati ya Sunni na Shia ni ndogo sana. Lakini ukweli wa kihistoria ni eneo ambamo hakuna nafasi kubwa ya mfarakano. Nimefanya udondozi wa mara kwa mara sana, kutoka kote, kwa wanahistoria wa zamani na wa kisasa, katika kitabu hiki, mara nyingi juu ya suala au tukio hilohilo.

Nimefanya hivyo ili kuwasilisha kwa msomaji zaidi ya hoja moja ya maoni au tafsiri zaidi ya moja ya matukio yenye umuhimu zaidi. Tukio hilohilo likiangaliwa kwa mitazamo tofauti huonekana tofauti kwa watazamaji mbalimbali na kwa hiyo, ni yenye kupatwa na tafsiri mbali mbali. Ni katika matumaini kwamba msomaji atashiriki katika maoni Haya ambayo nimejaribu, kwenye matukio mengi, kuacha zaidi ya mwanahistoria mmoja kuelezea kisa hicho hicho. “Wacha wataalamu waifanye kazi hiyo,” umekuwa ndio wito wangu katika kutafsiri upya mambo muhimu ya historia ya Uislamu.

Sababu nyingine ya kwa nini nimewasilisha ushahidi wa wanahistoria kwa kiwango kikubwa hivyo, ni kutegemeza tasnifu yangu na ushahidi, kiasi kwamba msomaji, kama akipen- da, aweze kurejea kwenye vyanzo ambavyo anaweza kuviona kama ni vya kuaminika kabisa.

Imesemekana kwamba kujasiri, kama kulivyo, katika kuchunguza yale yasiyojulikana, kupita kiasi, ni kutilia shaka yanayojulikana. Mengi ya yale yanayoitwa “mambo yanayofahamika” katika historia ya Uislam mchanga, ni dhana hasa za uchamungu au hata matakwa ya uchamungu ambayo kutokana na kung’ang’ania kurudiwa rudiwa na mlolongo mrefu wa vizazi vya Waislamu, yamepata “mng’ao kama sio hadhi ya “masharti ya imani”. Nilipozihoji baadhi ya dhana za Waislamu nyingi ambazo zinatambulika kama “ukweli” wa kihistoria, niligundua kwamba haziwezi kuhimili uchunguzi makini wa uchambuzi wa kukosoa.

Msomaji mwenyewe anaweza kwa hiyo, kuamua kama atazishikilia hizo au atakubali ukweli ambao baadhi yake atauona ni mchungu sana na mkali. Kuna wale watu ambao huwa wanauogopa ukweli. Ukweli unatishia njozi zao, visa vyao wanavyopendelea, na dhana zao. Hivi (vilivyotajwa) vya mwisho, kutokana na ufananaji (wa mawazo) wa siku nyingi, vimezoeleka sana kwao kiasi kwamba wanahisi ni salama na vinatosha kuishi navyo bila ya “udukizi” wa ukweli. Wanalinganisha ukweli na “ukosefu wa usalama.”

Hata hivyo, ukweli pekee ndio unaoweza kuwaletea wao usalama wa kweli. Ukweli ni lazima utetewe kwa gharama yoyoye ile, na watu wote, lakini hususan na wanahistoria.

Ukweli lazima ukubaliwe hata kama unamuumiza rafiki na kumnufaisha adui. Uaminifu wa kwanza wa mwanahistoria lazima uwe ni ukweli, na lolote lile liwalo lazima lisimpotoshe katika kuutafuta huo ukweli.

Vita vya mawazo na mgongano wa maoni unakuwa wa kuvutia sana pale ambapo mwenge wa uchunguzi unapogeuziwa mbali kutoka kwenye dhana za kifalsafa na itikadi dhahania za kisiasa kwenda kwenye tabia na mienendo ya (watu) shaksia ambayo ilifanya kazi muhimu katika matukio ambayo tunayachunguza. Historia huchimbuka kwenye uhai na uumbaji wa mhusika; inakuwa yenye kutikisika pamoja na watu wa kusawarika ambao “hufanya” matukio au kuyashughulikia au kuyapinga. (Wanaipamba) wanaiwekeza historia pamoja na elementi za “maslahi ya wanadamu”, na mguso wa mfululizo wa mambo.

Vyovyote vile historia iwavyo – ajali au vifo visivyozuilika, au shinikizo la hali ya maa- muzi ya kiuchumi, au vitendo vya viongozi wenye nguvu, au matokeo ya nguvu ambazo hakuna anayezijua, au matumaini ya pamoja ya watu – vyovyote historia iwavyo, Waarabu wenyewe wanaiona na kuitafsiri historia yao wenyewe zaidi kwa kigezo cha utendaji binafsi, kuliko kitu kingine chochote. Na wanaweza wakawa sahihi.

Hata hivyo, kama ilivyo katika kila jitihada, historia inatengenezwa na wale wanaotenda. Inategemea, katika mwingiliano wake, sio wa nguvu zisizoeleweka bali wa wanadamu. Migongano ya historia sio ya kati ya dhahania za falsafa, uchumi au elimujamii, bali kati ya wanadamu.

Imesemekana kwamba hata katika nyakati zake za kisosholojia, historia haiwezi kupuuza kipengele cha shaksia ya mwanadamu. Historia ya miaka 23 ya awali ya kazi ya Uislamu ambayo inajumuisha ujumbe wote wa Muhammad kama Mtume wa Allah (s.w.t.) imetengenezwa kwa sehemu kubwa, karibu na yeye mwenyewe, na vitendo vya mshirika wake, Ali ibn Abi Talib.

Huu ndio ushahidi wa historia. Lakini ni ushahidi ambao wanahistoria wengi kwa kawaida wamejaribu kuuficha. Ni kwenye ushahidi huu ambako nimejaribu kuvuta mazingatio ya wasomaji wa kitabu hiki.

Lakini licha ya kwenda upande kwa wakati uliopita na wakati wa sasa kwa uandishi wa historia wa kimagharibi juu ya Uislamu, kuna matumaini mapya kwamba wanahistoria wa wakati ujao watafanya marekebisho kwa ajili ya yaliyoachwa na mapungufu ya wanahistoria wa zamani.
Wanachotakiwa kufanya tu ni kutokuwa na upendeleo, na kutokuyakubali kibubusa yale maelezo na maamuzi ambayo yamekuwa ni istiari iliyochakaa ya historia ya Uislamu, bali kuugundua upya ukweli wao wenyewe kupitia ulinganisho na uchunguzi wa ushahidi.

Katika utangulizi wa Cambridge History of Islamu, Juz. I, kilichochapishwa na University Press, Cambridge (1970), P.M. Holt anaandika hivi: “Uchunguzi wa historia ya Uislamu sasa unapanuka, uhakika mwingi wa dhahiri wa uandishi wa zamani wa historia wa kimagharibi (mara nyingi unaoonyesha utetezi na maelezo ya wanahistoria wa mapokezi wa Waislamu) umepotea, na ni polepole kupitia utafiti wa kina ambapo ufahamu wa kweli zaidi wa mambo ya zamani unaweza kupatikana.”

Uhakika wa uandishi wa zamani wa historia wa Kimagharibi unaoakisi utetezi na tafsiri ya wanahistoria wa mapokezi wa Waislamu haujapotea bado lakini natutegemee kwamba utapotea, na ufahamu wa kweli zaidi wa mambo ya zamani utapatikana kadiri siku zinavyokwenda.

Jitihada ya kuitafsiri historia ya Uislamu, hususan ile historia ya karne yake ya kwanza, ni kama kuingia kwenye eneo lililotegwa mabomu; kuchemka kwake na migogoro, lawama kali na ubishani, na mtu anaweza kulisogelea tu kwa tahadhari sana. Hata hivyo, tafsiri inabakia ya msingi kwa kuielewa historia.

Bila ya tafsiri, historia inakuwa ni rundo la habari zisizoratibiwa na ni orodha ya matukio “yaliyokufa” na tarehe zisizo na uhusiano na kila mojawapo. Bado haya matukio “yaliyokufa” yanajirudisha nyuma kwenye maisha wakati athari zinapohusishwa na sababu, na uunganishaji wa mambo unapoanzishwa. Jambo linalohusiana na mambo mengine linakuwa na maana ya kihistoria; katika kulitenga kwake, linaweza kuwa halina maana kabisa.

Hata Nadharia ya Einstein ni kule kuielewa dunia sio kama mfululizo wa matukio bali kama mahusiano.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, kuna vitabu vingi kupita kiasi juu ya Uislamu lakini vingi ya hivyo ni tafsiri zilizokaririwa za kisa cha kuzaliwa na kukua kwake, na uzoefu wake wa kidini, kama kilivyokabidhiwa kwa waandishi wake na wanahistoria wa baraza wa serikali ambayo ilizaliwa pale Saqifah, na serikali zake zilizofuatia – zile serikali za Damascus na Baghdad. Kisa hicho, hata hivyo, kina upande mwingine pia.

Kanuni ya sheria ya zamani ya Kirumi ilikuwa ni audi alteram partem – (katika mgogoro wowote ule, sikiliza na ule upande mwingine); au audiatur et altera pars – (acha na ule upande mwingine usikilizwe). Tendo la pamoja la wanadamu – ambalo linaitwa siasa – limejaa misiba mingi, yenye kuvunja moyo ambayo imeyaharibu maisha ya kila mtu duniani. Mingi ingeweza kuepukwa kama sheria hii ingetiiwa na wote.

Utaratibu huu kwamba katika mgogoro wowote ule, pande zote katika suala hilo zinapaswa kusikilizwa – umefanywa ni kifungu madhubuti katika mifumo ya sheria ya mataifa mengi, lakini zaidi hasa katika ile ya Marekani na Ulaya Magharibi. Thomas Jefferson alikuwa akifafanua tu utaratibu huu, ambao bila ya huo hapawezi kuwepo na haki yoyote, wakati alipotamka kwa mshangao: “Tafadhalini sana, natusikilize kila upande kwa uhuru kabisa.”

Wanafunzi wa Uislam, wa Kimarekani na wa Ulaya, katika masuala mengi, wamesikia tu upande mmoja wa Hadith; kitabu hiki ni jitihada ya kuwasilisha ule upande mwingine. Ni pamoja na dhamira hii kwamba nikitoe kwa ajili ya uamuzi wa wasomaji wenyewe.

Kutoka kwenye woga unaonywea kwenye ukweli mpya; Kutoka kwenye uzembe ambao unaridhika na nusu-ukweli; Kutoka kwenye kiburi kinachodhani kinajua ukweli wote; Ewe Mungu wa Ukweli utuokoe!