read

Utangulizi Wa Vita

Kama ilivyoonyeshwa hapo kabla, magavana wa Ali walikuwa hawakuweza kuingia Syria na Kufa kwa sababu ya upinzani wa magavana wa Uthman kwake yeye. Lakini Syria na Kufa havikuwa ndio vituo pekee vya uchochezi wa maasi. Matatizo yalikuwa yanapikwa kwa ajili ya Ali ndani ya Madina yenyewe yakitishia usalama wa dola. Yeye kwa hiyo, alilazimika kuahirisha kuchukua hatua juu ya matatizo yanayoibuka kutokana na uchochezi wa maasi katika majimbo ya mbali kwa muda fulani.

Kama ilivyoonyeshwa hapo kabla, wakati Ali aliposimikwa kwenye cheo kama khalifa wa Waislam, watu wawili wenye nguvu sana hapo Madina, yaani, Talha na Zubeir, walikuwa wa kwanza kutoa kiapo cha utii kwake. Wote wawili, kama wengine wengi, wamekuwa matajiri sana katika utawala wa wale makhalifa watatu wa kabla ya Ali. Waliendelea kupata utajiri zaidi na zaidi, na sasa, kwa kupanda kwa Ali madarakani, walitaka pia kuwa magavana wa yale majimbo yenye utajiri ya Basra na Kufa. Walipokuwa wanatoa kiapo cha utii kwa Ali, walikuwa sirini wakitumainia kwamba kama nipe nikupe, Ali angewateua kama magavana. Lakini Ali aliwateua watu wengine kama magavana, na hakuwapa wao kitu chochote. Hili liliwatoa matumaini. Ingawa walivunjika mioyo, hawakufikiria sana juu ya kukatishwa tamaa kwao, na wakiwa watu wenye ubwana, waliamua kujishughulikia wao wenyewe.

Talha na Zubeir walibuni mbinu ya kumghilibu Ali. Walimwendea kwake, na wakamjul- isha kwamba wanakwenda Makka kufanya umra (hijja ndogo). Mara tu mabwana wakubwa wawili hawa walipokuwa Makka, walivunja kiapo chao cha utii kwa Ali. Walitamka kwamba walikuwa wametoa kiapo chao kwa mashaka mengi akilini mwao. Kwa wakati huu, Aisha, binti ya Abu Bakr, na mmoja wa wajane wa Mtume, alikuwa pia yuko Makka. Alikuwa amefanya Hijja lakini hakuwa amerudi Madina pale aliposikia kwamba Ali amekuwa khalifa, na alitangaza kwamba atalipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha Uthman. Talha na Zubeir walimwendea nyumbani kwake huko Makka. Walimpa maelezo juu ya yale matukio ya Madina.

Kile alichokisikia kutoka kwao, kilimtia nguvu katika azma yake ya kuwa mtetezi wa Uthman. Kwa Talha na Zubeir alikuwa amepata waungaji mkono wenye shauku kubwa katika “shughuli” yake. Hili lilifanya ule “utawala wa watu watatu” wa Aisha, Talha na Zubeir, uliopangwa kwa makabilano na Ali, mrithi wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), na kiongozi wa haki wa Waislam. “Kiungo muhimu” cha huu utawala wa watu watatu kilikuwa ni chuki juu ya Ali.

Utambulisho wa kila mmoja wa “watawala” hawa umetolewa hapa chini ili kumwezesha msomaji kuuelewa mfuatano wa yale matukio ambayo yalisababisha kutokea kwa vita vya pili vya wenyewe kwa wenyewe katika Uislam.

Talha Bin Ubaidullah

Baba yake Talha, Ubaidullah na baba yake Abu Bakr, Abu Qahafa, walikuwa ni ndugu. Mama yake Talha alikuwa ni binti ya Hadhrami, na baba yake, Ubaidullah, alikuwa ni mume wake wa pili. Kwa muda mfupi, alikuwa pia mke wa Abu Sufyan, baba yake Mu’awiyah lakini alikuwa amemtaliki.

Talha alimuoa Umm Kulthum, binti ya Abu Bakr, na hili lilimfanya kuwa shemeji yake Aisha. Pale Abu Bakr alipomteua Umar kuwa mrithi wake, Talha alipinga kwa nguvu sana, na alimvuta nadhari yake juu ya kiburi cha khalifa-mteule huyo. Baadaye, wakati Umar mwenyewe alipokuwa anafariki, alimfanya Talha kuwa mjumbe wa kamati yake ya uteuzi.

Talha alivunja kiapo chake cha utii kwa Ali kwa sababu huyu Ali hakumfanya kuwa gavana wa Basra. Huenda alikuwa na sababu hizo hizo kwa upinzani wake, hapo mapema, kwa Uthman, ambaye pia hakumchagua kuwa gavana.

Baladhuri, mwanahistoria wa Kiarabu, anasema katika kitabu chake, Ansab-ul-Ashraf juz. 1, uk. 113: “Miongoni mwa masahaba wa Mtume wa Allah, walikuwepo wachache waliomke- mea Uthman kwa ukali sana kama alivyofanya Talha.”

Pale kasri la Uthman lilipozingirwa na waasi, alikuwa ni Talha ambaye aliwazuia watumwa wake (Uthman) kuingiza maji ndani yake. Usiku, alilirushia mishale lile kasri lakini Uthman alikuwa analijua hilo. Tabari, yule mwanahistoria, anasema katika Tarikh yake, juz.111, uk. 411: “Uthman mara nyingi alikuwa akiomba: ‘Ewe Allah! Nakuomba uniokoe na madhara ambayo Talha anaweza kunifanyia. Yeye ndiye ambaye amewachochea watu dhidi yangu, na ndio yeye aliyesababisha nyumba yangu kuzingirwa.”

Chuki ya Talha kwa Uthman lazima ilikuwa imezidi mno. Hakuweza kumsamehe kupoto- ka kwake hata baada ya kufa kwake. Aliamuru jeneza la Uthman na wabeba jeneza wake wapigwe mawe. Uthman hakuweza hata kuzikwa kwenye uwanja wa makaburi ya Waislam; ilibidi azikwe kwenye makaburi ya Wayahudi.

Zubeir Bin Awwam

Mama yake Zubeir alikuwa ni Safiya, binti ya Abdul Muttalib bin Hashim. Kwa hiyo mama yake alikuwa ni shangazi yake Muhammad (s.a.w.w.) na Ali.

Zubeir pia alikuwa amemuoa mmoja wa mabinti wa Abu Bakr, na hii ilimfanya kuwa she- meji yake Aisha. Kama Talha, yeye pia alimpinga mkwe wake dhidi ya uteuzi wa Umar kama khalifa. Na wakati Umar alipokuwa anafariki, alimfanya Zubeir pia kuwa mjumbe wa kamati yake ya uteuzi.

Ibn Saad anasema katika Tabaqaat yake kwamba Zubeir alikuwa pia ni tajiri sana kama Talha.

Zubeir alishiriki tamaa ya Talha ya dhahabu na uchu juu ya madaraka ya kisiasa. Alikuwa akitegemea kwamba Ali angemtendea kwa namna ile ile kama Uthman alivyowatendea binamu zake wawili, yaani kwa kumfanya yeye kuwa gavana. Hata hivyo, alikuwa ni binamu yake Ali.

Lakini Ali hakumtendea binamu yake, Zubeir, kama Uthman alivyowatendea binamu zake. Kulipokuwa hakukubakia mashaka yoyote akilini mwa Zubeir kwamba Ali hatamchagua yeye kuwa gavana, alivunja kiapo chake cha utii kwake, na akasimama katika maasi dhidi yake.

Zubeir alichangia chuki yake na Talha kwa Uthman, na mara kwa mara aliwasukumiza wale waasi wamuue Uthman. Ibn Qutayba, mwanahistoria wa Kiarabu, anasema kwamba siku chache baada ya Ali kupanda madarakani, Talha na Zubeir walikuja kumuona Ali, na mabishano yafuatayo yakatokea kati yao:

Talha/Zubeir: Hivi unajua ni kwa nini tulichukua kiapo cha utii kwako?

Ali: Mlichukua kiapo cha utii kwa sababu zile zile kama Waislam wengine –kunitii mimi.

Talha/Zubeir: Hapana. Tulichukua kiapo hicho kwa matumaini kwamba utalipiza kitendo chetu hicho kwa kutupa sisi fungu katika serikali. Hata hivyo, ilikuwa ni kwa msaada wetu sisi ndipo ukawa khalifa.

Ali: Ninaweza nikawatakeni ushauri katika masuala ya serikali lakini hakuna kitu kama “fungu” kwa ajili yenu katika serikali.

Talha na Zubeir waliaibika sana kwa kukataa kwa Ali kugawana madaraka pamoja nao, na yafuatayo yalikuwa ndio maoni yao juu ya matokeo ya kukutana naye:

Talha: Hapo Madina, walikuwepo wajumbe watatu wa kamati ya uteuzi. Kati yao, mmoja (Saad bin Abi Waqqas) alikataa na kiapo chake cha utii kwa Ali lakini Zubeir na mimi tulimpa yeye viapo vyetu. Wote sisi ndio tuliofanya iwezekane yeye kuwa khalifa lakini amesahau mapema sana kile tulichomfanyia yeye.

Zubeir: Tuliiandaa orodha ya makosa ya kijinga ya Uthman, na tulimlaumu yeye, yote kwa ajili ya Ali. Wakati wa ghasia hii, Ali alikuwa amekaa nyumbani kwake. Kisha, kwa msaada wetu sisi akawa khalifa. Lakini mara tu alipokuwa khalifa, akasahau huduma zetu, na akatoa vyeo vya zawadi vyote kwa watu wengine.

Madhumuni ya maoni haya yaliletwa kwenye nadhari ya Ali. Yeye alimwita Abdallah ibn Abbas, na akamtaka ushauri wake juu ya jambo hili. Ibn Qutayba anaandika katika kitabu chake Kitab-ul-Imama wa-Siyassa, kwamba Abdallah ibn Abbas alisema: “Ni maoni yangu kwamba ungemteua Talha kuwa gavana wa Basra, na Zubeir kuwa gavana wa Kufa. Hii itawaridhisha wao na kuwanyamazisha.”

Ali alisita na kuwaza juu ya ushauri wa binamu yake, na kisha akasema: “Hapana. Sidhani kama ninaweza kukubaliana na wewe katika hoja hii. Ninawajua wote vizuri sana. Kama nitawafanya kuwa magavana, basi udhalimu, uonevu na uny- onyaji vitaachiliwa huko Basra na Kufa, na kilio cha wale wanaoonewa kitagubikwa tena. Kama ningekuwa niteue watu kama Talha na Zubeir kama magavana, basi itanipasa nimvumilie Mu’awiyah pia kubakia kama gavana wa Syria.”

Ibn Qutayba anaendele kuandika zaidi:
Amr bin Al-Aas, Talha na Zubeir walikuwa wa kwanza kumshutumu Uthman. Walikuwa ndio wa kwanza kuwachochea watu wazi wazi kumuua Uthman. Talha na Zubeir walikuwa wa kwanza kuchukua kiapo cha utii kwa Ali, na wote hawa walikuwa ndio wa kwanza kuvunja ahadi yao ya uaminifu.”

Tangu pale Umar alipowateua kuwa wajumbe wa kamati ya uteuzi, Talha na Zubeir walikuwa wameweka tamaa ya kuja kuwa khalifa. Lakini Abdur Rahman bin Auf akamfanya Uthman kuwa khalifa badala ya yeyote kati yao.

Fursa ya pili ya kuweza kuwa khalifa ilikuja mara tu baada ya kifo cha Uthman. Lakini safari hii, walihisi kwamba Waislam walikuwa hawawataki wao. Walitambua kwamba kwa lolote lile watakalofanya, Waislam hawatawakubali. Kila mmoja hapo Madina alikuwa ameona kwa macho yake mwenyewe mwenendo wao juu ya Uthman wakati wa kuzingirwa kwa kasiri lake.

Talha na Zubeir vile vile walifahamu kwamba haikuwa ni Ali aliyekuwa akiwakumbakumba wengine ili kupanda juu (cheo cha ukhalifa) bali walikuwa ni Waislam waliokuwa “wanakumbakumba” kumuweka yeye hapo. Kuchaguliwa kwa Ali kama khalifa kulikuwa ni kwa hiari, na upingaji wowote ule uliokuwepo kwa ajili hiyo, ulitoka kwake mwenyewe. Talha na Zubeir pia walijua kwamba kama wangekataa na kiapo chao cha utii kwake, watajidhihirisha wenyewe wazi wazi mno. Kwa kutotaka hili kutokea, walichukua kiapo cha utii kwa Ali.

Walipoona ukhalifa uko nje ya uwezo wao, Talha na Zubeir walitupia macho Basra na Kufa kama zawadi ya kujifariji kwao. Walitegemea kwamba Ali hatapuuza hadhi yao kati- ka umma, na kama wajumbe wa kamati ya uteuzi ya Umar. Vile vile wao walisadiki kwamba Ali hataacha kutilia maanani heshima na ushawishi wao kwa watu wa Basra na Kufa.

Lakini Ali hakuvutiwa na hadhi zao na ushawishi, na hakuwapa wao Basra na Kufa.

Talha na Zubeir walitambua kwamba Madina imethibitisha kuwa ubao mbovu hasa wa kuchupia wao kwa ajili ya malengo yao. Wao, kwa hiyo, waliamua kwenda Makka, na kujaribu bahati yao huko. Ali hakufanya jaribio lolote la kuwazuia wao. Talha na Zubeir waliondoka Madina na uhaini mioyoni mwao.

Kama Ali angewateua Talha na Zubeir kuwa magavana wa Basra na Kufa, wangeimarisha nafasi zao katika majimbo yao husika, na kisha wangekana kiapo chao kwa serikali kuu. Umma sasa ungejikuta wenyewe unatawaliwa na watawala wanne wanaojitegemea na wenye uadui – Talha huko Basra; Zubeir huko Kufa; Mu’awiyah huko Syria; na Ali huko Hijazi. Katika kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe isiyozuilika miongoni mwao, Dola ya Kiislam angevunjikia kwenye vurugu na kuwa “serikali” ya makabila ya Kiarabu kwa mara nyingine kama ilivyokuwa katika Nyakati za Ujahilia.

Ilikuwa ni busara na kipaji cha Ali ambavyo viliiokoa Dar-ul-Islam (Dola ya Kiislam), kutokana na maangamizi hayo ya kuhuzunisha.

Ni ukweli unaofahamika vema kwamba maamuzi na sera za kiserikali, katika masuala mengi, yanaamuliwa na mashinikizo ya makundi ya maslahi maalum. Talha na Zubeir, na wafuasi wao waliunda kundi kama hilo. Walitia shinikizo lakini lilipokutana na upinzani, waliingia vitani.

Aisha Binti Abu Bakr

Aisha alikuwa binti ya Abu Bakr, khalifa wa kwanza wa Waislam. Alizaliwa miaka minne baada ya Mtume wa Uislam kutangaza ujumbe wake, na alikuwa na umri wa miaka tisa wakati alipoolewa naye. Alikuwa ni mke wake wa tatu. Kwa vile alibaki bila kuwa na mtoto, alimtwaa Abdallah bin Zubeir, mtoto wa dada yake, kama mwanawe mwenyewe. Ilikuwa ni kwa mazingira haya ndipo akaitwa Umm Abdallah, mama yake Abdallah.

Aisha alikuwepo katika vita ya Uhud. Bukhari anasema kwa idhini ya Anas kwamba alimuona Aisha na Umm Salama wakileta maji kwenye mifuko ya ngozi, na kuyatoa kwa wapiganaji waliojeruhiwa ili wanywe. Aisha alimchukia sana Ali. Alimchukia sana kiasi kwamba hakuweza hata kumtaja jina lake. Bukhari amesimulia tukio lifuatalo:
Aisha anasema kwamba pale hali ya Mtume wa Allah swt. ilipokuwa mbaya, aliomba ruhusa ya wake zake wengine ili atumie muda wake wote chumbani kwangu kwani alitaka mimi nimuuguze. Siku ile alikuwa katika chumba cha Maimuna. Kwa vile alikuwa dhaifu sana, ilibidi afanye kusaidiwa na watu wawili waliomtoa kutoka kwenye chumba cha Maimuna kumleta chumbani kwangu. Mmoja wa watu hao waw- ili alikuwa ni Abdallah ibn Abbas.

Maelezo ya Aisha ya Hadith hii yalifikishwa kwa Abdallah ibn Abbas, na yeye akasema kwamba yule mtu mwingine aliyekuwa amemsaidia Mtume wakati alipokuwa anatoka kwenye chumba cha Maimuna, alikuwa ni Ali.

Wanahistoria wamejaribu kutafuta sababu za kwa nini Aisha alimchukia Ali. Moja ya sababu inasemekana kuwa ni lile tukio la ifk, yaani, “ule uwongo.” Kadhia hiyo ilitokea katika mwaka wa sita wa Hijiria. Wakati jeshi la Madina lilipokuwa linarudi kutoka kwenye msafara wa kwa Banu Mustaliq, Aisha ambaye alikuwa amefuatana na Mtume, kwa kughafilika aliachwa nyuma. Alikuja kutokea baadae akiwa na muongoza ngamia. Kadhia hii ilisababisha uropokaji fulani miongoni mwa watu, na kusababisha sana ugonjwa wa moyo kwa Mtume (s.a.w.w.). Anasemekana kutafuta maoni ya Usama bin Zayd bin Haritha na Ali ibn Abi Talib katika suala hili. Usama, inavyoelezwa, alimwambia Mtume kwamba Aisha alikuwa hana hatia kabisa lakini Ali anasemekana kwamba alisema kumwambia Mtume kwamba haikuwa lazima kwake kuvumulia maudhi kama hayo kwa sababu angeweza wakati wote kupata wanawake wengine wa kuwaoa.

Aisha pia alidai kwamba Ali alimpiga mtumishi wake wa kike katika jaribio la kumtaka aeleze ule “ukweli.”

Mtume alishikwa na fadhaa bila kujua ni upi ukweli wa jambo hilo wakati wahyi mpya uliposhuka kutoka mbinguni ambao ulimwondolea Aisha tuhuma za hatia zote au lawama. Kutokuwa na hatia kwake kulikubalika na tukio hilo lisilopendeza inavyoonekana likafungwa kabisa.

Ingawa kadhia hii ilikuwa na mwisho wa kufurahisha kwa Aisha, hakumsamehe kamwe Ali kwa ule “ushauri” wenye kudaiwa kwamba yeye alimpa mumewe, yaani, kwamba alikuwa amemwambia wanawake wengine walikuwa wanapatikana kwa ajili yake wakati wote, na kwamba hakupaswa kuhuzunika sana juu ya tukio hilo.

Ikiwa kama Ali alitoa ushauri kama huo kamwe kwa Mtume, basi hakuwa amefanya chochote zaidi ya kufafanua ile Aya ya tano ya sura ya 66 ya Qur’an (Surat Tahriim) kama ifuatavyo: Kama akikupeni talaka, bila shaka Mola wake atampa badala yenu, wake wengine walio bora kuliko ninyi….(at-Tahriim, 66:5)

Kwa mujibu wa Aya hii ya Qur’an, walikuwepo wanawake ambao walikuwa wabora zaidi kuliko wake za Mtume, na Allah angeweza kuwatoa kwake yeye.

Hadith ya kwamba Ali alimpiga mtumishi wa Aisha, haikubaliani na hulka yake. Alikuwa ndio muungwana kabisa wa watu, na hata katika uwanja wa mapambano, hakutaka kuwa wa kwanza kumshambulia adui yake. Alimtaka adui yake amshambulie yeye kwanza. Ni pale tu adui alipokuwa amepiga dhoruba ndipo Ali alipojihisi kuwa huru kujitetea mwenyewe. Haiwaziki kwamba angeweza kumpiga msichana asiyejiweza. Wakati jeshi liliposonga mbele, Aisha aliachwa nyuma, alikuwa peke yake kabisa, na mtumishi wake hakuwa pamoja naye. Ni vipi angeweza kujua kilichotokea kama hakuwa na bimkubwa wake? Hata kama mtu angetishia kumuua, bado asingeweza kueleza chochote.

Sir William Muir, mwanahistoria wa Kiingereza, ameonyesha kwamba msimuliaji wa Hadith hii alikuwa ni Aisha mwenyewe, na hii, yeye anasema, “inafanya ushahidi wake kuwa wa kutiliwa shaka.”

Lakini Aisha hakulihitaji tukio la ifk ili kumchukia Ali. Chuki yake kwa Ali ilikwenda kwenye nyakati za kabla – mbali na tukio hili.

Alikuwa na wivu juu ya Khadija, na binti yake, na watoto wa binti yake. Muhammad alikuwa akiwadekeza na kuwakumbatia watoto wa binti ya Khadija wakati wote, na Aisha angeweza kufikiria kwamba kama angekuwa na watoto wowote, yeye Muhammad angewapenda kama alivyokuwa akiwapenda binti na wajukuu wa Khadija, lakini hakuwa na hata mmoja.

Kuwa na wivu kwa binti na wajukuu wa Khadija kungeweza kuwa ni kawaida na asilia kwa Aisha. Lakini kilichokuwa sio cha kawaida na asilia, hususa kwa mke wa Mtume wa Allah swt., kilikuwa ni kuruhusu wivu wake kuwa usiotawalika na tena tamaa isiyowiana.

Aisha mwenyewe kila mara alikuwa akisema kwamba ingawa hakumwona kamwe Khadija, alikuwa anamuonea wivu sana kuliko alivyokuwa kwa wake wenzie wengine. Sababu moja ya wivu wake ilikuwa kwamba mume wake alikuwa kila wakati akimkumbuka Khadija kwa mapenzi halisi na shukrani. Katika wakati mmoja, alikuwa akimtukuza na kumsifia Khadija pale Aisha alipopoteza subira, na akasema kwa hasira: “Kwa nini unazungumza juu ya huyo mwanamke mzee wakati wote? Kwani Allah hakukupa wake wazuri zaidi kuliko yeye?”

“Asilani!” alijibu Mtume. “Allah kamwe hajanipa mimi mke bora kuliko Khadija. Yeye aliniamini mimi wakati ambapo wengine walinipinga mimi. Yeye alinisaidia mimi wakati nilipokuwa sina mtu yoyote wa kunisaidia. Yeye alikuwa wa kwanza kuukubali Uislam ambapo kila mmoja mwingieo ni muabudu sanamu. Na Allah alinibariki mimi na watoto kupitia kwake, na kupitia kwake peke yake.”
(Bukhari na Siyar-us-Sahabiyyat)

Lakini Aisha hakuweza kuzima au kuficha chuki yake kwa Khadija, binti yake na wajukuu zake. Hata kifo cha Khadija na Fatima havikuweza kumshawishi yeye kusahau chuki yake ya tangu kale. Alimchukia Ali na wajukuu wa Khadija. Ilikuwa haizuiliki kwamba Aisha angezozana na Uthman. Mara moja Uthman alipokuwa anatumia lugha chafu na ya matusi, kutoka kwenye mimbari, kwa ajili ya Abdallah ibn Masoud, rafika ya Mtume wa Allah, na yeye alijitokeza kwa ajili ya kumlinda yeye. Kulikuwa na nyakati zingine ambapo alikuwa amejaribu kupunguza majivuno ya Uthman.

Mlango wa chumba chake ulifungukia Msikitini, na mara kwa mara aliweka kwenye sakafu yake jozi ya viatu na shati ambavyo vilikuwa vya Mtume, akatoa kichwa chake nje, na akimweleza Uthman wakati alipokuwa juu ya mimbari, alisema: “Kabla ya vitu hivi, ambavyo ni vya Mtume wako, havijakusanyikiwa na vumbi lolote juu yake, umekwishabadilisha amri zake, Hadith zake, sunnah zake, na umekwisha kuiharibu dini yake.”

Aisha alikuwa tayari amekwishatia mashaka kwamba Uthman “amempuuza” yeye. Kisha amepunguza mshahara wake. Hili lilimfanya aghadhibike. Hili pamoja na maudhi mengine madogo madogo lilimfanya awe adui mkali wa Uthman. Abbas Mahmud Al-Akkad wa Misri anasema katika kitabu chake, Abqarriyat al-Imam Ali (Cairo, 1970), kwamba Aisha alikuwa amempa Uthman jina la “Na’thal”. Huyu Na’thal alikuwa mzee mmoja wa Kiyahudi hapo Madina. Inasemekana kwamba ndevu za Uthman zilikuwa na namna fulani ya kufanana na ndevu zake. Aisha, katika nyakati za hasira, aliwachochea watu wazi wazi dhidi ya Uthman, na alisema: “Muueni huyu Na’thal. Amekuwa kafir.”

Umar Faroukh anaandika katika ukurasa wa 190 wa kitabu chake, The History of the Arabic Thought Till the Days of Ibn Khaldoun, kilichochapishwa mwaka 1983, na Dar-ul-‘Ilm lil-Malaiin, Beirut, Lebanon: Imesimuliwa kwamba Aisha alikuwa na desturi ya kusema: “Muueni huyu Na’thal (Uthman bin Afan); amekuwa kafir.”

Kuzingirwa kwa kasri la Uthman kulikuwa kumekwishaanza wakati Aisha alipoondoka Madina kwenda Makka kufanya Hijja. Marwan alimuomba abakie Madina lakini hakumsikiliza, na akauondoka mji. Katika kipindi cha kutokuwepo kwake Madina, Uthman aliuawa.

Huko Makka, Aisha alikuwa na shauku sana ya kusikia habari za mambo yaliyokuwa yanatokea huko Madina. Baada ya Hijja, alifungasha mizigo yake ili kurudi Madina. Kabla ya kuondoka Makka, hata hivyo, alifahamishwa kwamba mtu anayeitwa Akhdhar, alikuwa amewasili kutoka Madina. Alimwita na kumuuliza kilichokuwa kinatokea huko Madina, naye akasema: “Uthman amewaua wale waasi na ameurudisha mji chini ya udhibiti.”

Aisha alishitushwa kusikia taarifa hii, na akasema: “Hivi Uthman amewaua wale watu ambao wamekuja Madina kulalamika dhidi ya udhalimu, na kudai haki? Wallahi, sisi hatufurahishwi na hili.”
(Tarikh Tabari, Juz. 111, uk. 468)

Lakini katika siku iliyofuata, msafiri mwingine alikuja kutoka Madina, na alimwambia Aisha kwamba wale waasi wamemuua Uthman, na kwamba Akhdhar alikuwa amempa taarifa za uongo. Aisha akasema: “Mwenyezi Mungu aweke umbali kati ya Rehema Zake na Uthman. Lolote ambalo limetokea, Uthman alilisababisha mwenyewe juu yake. Allah hamdhulumu yeyote.”

Wakati habari za kifo cha Uthman zilipothibitishwa, Aisha aliamua kuondoka Makka mara moja.

Kuwepo kwake Madina, yeye aliamini, kulikuwa ni muhimu sana kabla ya uchaguzi wa khalifa mpya. Aliondoka Makka lakini alikuwa bado hajafika mbali wakati alipokutana na msafiri mwingine, Ubaid bin Abi Salma, akija kutoka Madina.

Aisha alimuuliza ni nini kilichokuwa kimetokea huko Madina kabla yeye hajaondoka. Yeye akasema: “Uthman ameuawa, na watu wa Madina wametoa kiapo chao cha utii kwa Ali ibn Abi Talib”

Kupanda kwa Ali kwenye cheo cha ukhalifa, hakukuwa aina ya taarifa ambazo Aisha alikuwa tayari kuzisikia. Lakini akitegemea kwamba alikuwa hajazisikia habari hizo sawa-sawa, aliuliza: “Umesema kwamba watu wa Madina wametoa kiapo chao cha utii kwa Ali?” Ubaid akajibu: “Ndio, wametoa. Na ni nani tena aliyekuwepo hapo ambaye wangeweza kumpa kiapo chao cha utii kwake?”

Aisha akaguna: “Oh! kiasi gani ninavyotamani ardhi ingepasuka au mbingu kuangukia juu ya ardhi kama Ali amekuwa khalifa. Sasa siwezi kwenda Madina. Nitarudi Makka.” (Tarikh Kamil, Juz. 111, uk. 105)

Aisha alimuamuru muongoza ngamia wake kurudi Makka, na akasema: “Uthman aliuawa wakati akiwa hana hatia. Wallahi, sasa nitalipiza kisasi kwa ajili ya damu yake.”

Kauli ya Aisha ilimshangaza Ubaid bin Abi Salma, na yeye akauliza: “Ewe mama wa waumini! Utalipiza kisasi kwa kifo cha Uthman? Lakini kwani hakuwa ni yule mtu uliyemwita ‘Na’thal,’ na wewe hukuwa yule mwanamke uliyewashawishi Waislam kumuua yeye kwa sababu, kama ulivyosema, alikuwa ameguka kuwa kafir?”

Aisha akajibu: “Ndio, ni kweli kwamba nilimwita Uthman kwa jina hilo, na watu wengine pia walimwita kwa jina hilo hilo. Ni kweli pia kwamba nilisema kuwa amepotoka, na kwamba alipaswa kusahihishwa. Lakini ninachokisema sasa ni kweli zaidi kuliko nilichokisema kabla, na ninachokisema sasa ni kwamba Uthman alikuwa ametubia kabla ya kifo chake. Kwa hiyo, wakati alipouawa alikuwa hana hatia, na nitalipiza kisasi kwa ajili ya damu yake.”

Aisha alijuaje kama Uthman alikuwa ametubia? Mpaka anaondoka Madina, alikuwa bado hajatubia, Hata baada ya kumaliza Hijja, na akawa tayari kurudi Madina, alikuwa bado hajatubia, vinginevyo asingeonyesha kuridhika katika kuuawa kwake.

Lakini aliposikia habari kwamba Ali amekuwa khalifa, yeye ghafla akafanya ugunduzi kwamba Uthman alikuwa ametubia, na alikuwa hana hatia. Alitangaza kwamba yeye ni mtetezi wa Uthman, na kwamba yeye ataanzisha mapambano ya kulipiza kisasi kwa ajili ya damu yake.

Wakati huo Marwan ambaye alikuwa ameondoka Madina wakati wa kupanda kwa Ali kwenye ukhalifa, pia alikuwa amewasili Makka. Alikwenda kwa Aisha na akampa maelezo fasaha ya kuuawa kwa Uthman ambayo yanasemekana yalimsikitisha sana, na kumfikisha karibu ya kulia machozi.

Aisha alianzisha kampeni yenye pande mbili; ilimbidi athibitishe (1) “kutokuwa na hatia” kwa Uthman, na (2) “hatia” ya Ali.

Wasafiri walizichukua habari za kampeni ya Aisha hadi Madina. Talha na Zubeir walisisimka sana kusikia habari hizo. Waliona dalili ya matumaini juu yao katika kampeni yake.

Walimwandikia barua Aisha, na wakampa baraka zao, wakampenda kwa uamuzi na shughuli yake; wakamtia moyo na kumhimiza kuimarisha propaganda yake dhidi ya Ali. Baadae kidogo wao wenyewe walikuwa waende Makka “kufanya umra.”
Aisha, chini ya mwongozo wa Marwan, alianza kukusanya msaada. Mtu wa kwanza kuitikia mwito wake, alikuwa ni Abdallah bin Aamir al-Hadhrami, gavana wa Uthman huko Makka. Pamoja naye alimchukua pia Said bin Al-Aas, Walid bin Aqaba na Bani Umayya wengine waliokuwako Makka, kwenye “kambi” ya Aisha. Wakati huo huo, Talha na Zubeir pia waliwasili kutoka Madina, na waliunda ushirikiano na Aisha na Marwan – ushirikiano dhidi ya Ali bin Abi Talib. Sasa wengi wa wale wadhamini wa kichinichini wa mauaji ya Uthman walikuwa wapo Makka. Kwa vile kulikuwa na umoja wa nia na kufanana kwa malengo miongoni mwao, uundaji wa ushirikiano haukuleta matatizo yoyote.

Nia iliyodhaniwa ya ushirikiano huu ilikuwa ni kutafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman, na washirika hao walikubaliana kwamba hapakuwa na njia nzuri ya kukipata kisasi hicho kuliko kuukamata ukhalifa wenyewe. Lakini nyuma ya pazia la kutafuta kulipiza kisasi, ulijificha uchu wa madaraka, na hofu za watu, na kijicho na ulipizaji kisasi usio na huruma wa mwanamke.