read

Uthman, Khalifa Wa Tatu Wa Waislam.

Kabla tu ya kifo chake, Umar alimwitaAbu Talha Ansari, na akawaambia: “Allah ameupa heshima Uislam kupitia kwenu (Ansari), na sasa uchukue watu wako hamsini wenye silaha kuwaangalia wale wajumbe wa kamati ya uteuzi, na usiwaachie wakatawanyika bila ya kuchagua khalifa jambo ambalo ni lazima walifanye ndani ya siku tatu.”

Wateuzi walianza mazungamzo yao katika nyumba ya Miswar bin Makhrama – mpwawe Abdur Rahman bin Auf. Abu Talha Ansari alianza mkesha wake wa ulinzi wa siku tatu. Amr bin Al-Aas na Mughira bin Shaaba, pia walitokeza kwenye mlango wa nyumba ya Miswar, wakiwa na shauku ya kushiriki katika utendaji wa kamati hiyo lakini wapiga mishale wa Abu Talha hawakuwaruhusu kuingia ndani.

Kwa sababu ya yale “madaraka maalum” aliyokuwa amempa Umar, Abdur Rahman bin Auf alijiona mwenyewe kama mtu muhimu wa kamati ya uteuzi.

Katika kuipima hali, alielewa kwamba hakuna hata mmoja kati ya wale wajumbe wengine watano aliyekuwa tayari kuondoa jina lake kutoka kwenye ugombea huo, na kila mmoja wao alidhamiria kuendeleza dai lake kwa nguvu sana.

Yeye, kwa hiyo, taratibu alijenga mkakati wake mwenyewe, na kisha akaiambia ile kamati kwamba yeye ataliondoa jina lake kutoka kwenye orodha ya wagombea kama itamruhusu, badala yake, kuwa kama mwenyekiti na mratibu wa mikutano yake.
Wajumbe wengine walikubali lakini Alialisita kumpa Abdur Rahman madaraka zaidi. Pale wajumbe wengine waliposisitiza kwamba yeye pia akubali, akamwambia: “Nitakukubali kama mwenyekiti wa kamati ya uteuzi kama utakula kiapo kwamba hutakuwa mtumwa wa tamaa zako mwenyewe binafsi, na kwamba uamuzi wako utachukuliwa tu kwa ajili ya kupata radhi za Allah na Mtume Wake.”

Abdur Rahman bila ya kusita akala kiapo cha kufanya hivyo, na hivyo akawa mwenyekiti wa kamati hiyo. Kwa kuuzulu ugombea wake, alipata uwezo zaidi ya wale wajumbe wengine, na akajitupa kwenye jukumu la “mwenye sauti katika uchaguzi.”

Abdur Rahman aliitisha mfululizo wa mikutano pamoja na wagombea wengine katika jaribio la kupata ufumbuzi wa kufaa wa tatizo hilo lakini juhudi zake hazikuzaa matunda yoyote. Maamuzi ya wagombea wengine katika zile siku mbili za kwanza pia yaliishia katika mkwamo.

Katika siku ya tatu na ya mwisho, Abdur Rahman alimtembelea kila mjumbe wa kamati nyumbani kwake mwenyewe. Katika mikutano hii ya faragha, alimuuliza kila mgombea, ni nani angependa kumuona kama khalifa kama yeye mwenyewe hakuchaguliwa. Jibu lilikuwa ni Uthman au Ali. Hii ilimaanisha kwamba chaguo limepunguzwa kwa hawa watu wawili, mmoja wao atakuwa awe ndio khalifa, lakini ni yupi hasa?

Usiku ule, Abdur Rahman, mwenye sauti katika uchaguzi, alikwenda kwa rafiki yake mkuu, Amr bin Al-Aas, akamuelezea mashaka yake, na akaongeza:“Nimekanganyikiwa sana katika jambo hili kiasi kwamba sijapata mapumziko yoyote kwa siku tatu. Leo ndio siku ya mwisho, na bado sijapata jawabu la tatizo letu. Kinachonitia wasiwasi mimi ni ile hofu isijekuwa Ali akawa ndio khalifa. Na kabla ya Umar kufariki, nilitambua kutokana na namna yake na mwelekeo kwamba na yeye pia alizongwa na hofu kama hiyo hiyo.”

Amr bin Al-Aas alikuwa mahiri zaidi kuliko Abdur Rahman au mtu mwingine yoyote yule katika aina ya mchezo kama huo ambao Abdur Rahman alikuwa akijaribu kuucheza. Akasema: “Najua hatua itakayo mshinda na kumzuia Ali.” Kisha yeye akamuelezea Abdur Rahman hatua hiyo. Naye akalipokea wazo hilo zuri na akajisikia mwenye furaha na kuji- amini kwamba atamzuia Ali kuweza kuwa khalifa.

Asubuhi iliyofuatia, Waislam walikusanyika ndani ya Msikiti wa Mtume (s.a.w.w.). Ilikuwa ni siku ya maana sana maishani mwao ambapo wataweza kujua ni nani atakayekuwa mtawala wao wa baadae. Wakati huu, yule mwenye sauti katika uchaguzi na wajumbe wengine wa kamati ya uteuzi pia walifika na wakaketi kwenye nafasi zao. Baada ya kimya kifupi, yule mwenye sauti akasimama. Alitoa taarifa ya madhumuni ya kuku- sanyika huko, akasisitiza umuhimu wake, na akawataka Waislam kuzingatia uamuzi wa kamati ya uteuzi ambayo Umar aliiteua.

Hali ya hewa iliingiwa na wasiwasi, na kila mtu akawa ameamka, tayari kana kwamba atasema dakika yoyote. Abdur Rahman bin Auf, yule mwenye sauti katika uchaguzi, alimgeukia Ali, akaushika mkono wake, na akamuuliza swali lifuatalo: “Kama tukikupa wewe kushika serikali ya Waislam, na tukakupa mamlaka juu ya mambo yao, je, utaahidi kwa dhati kwenda kwa mujibu wa Kitabu cha Allah, Sunnah ya Mtume Wake, na mienendo ya Abu Bakr na Umar?”

(Hili sharti la kutenda kwa mujibu wa mienendo ya Abu Bakr na Umar lilikuwa haliku- tamkwa na Umar mwenyewe. Lilikuwa ndio ile “hatua” ambayo Amr bin Al-Aas aliipendekeza kwa Abdur Rahman bin Auf. Alijua kwamba Ali hataikubali.)

Ali alimjibu yule mwenye sauti katika uchaguzi kama ifuatavyo: “Nitatenda kwa mujibu wa Kitabu cha Allah, na Sunna ya Mtume Wake. Na kuhusu kufuata mienendo ya Abu Bakr na Umar, nina uamuzi wangu mwenyewe, na nitautumia huo.”

Ali alijua kile ambacho kitatokea tu baada ya hilo.

Huyu mwenye sauti katika uchaguzi akauachia mkono wake. Yeye kisha akamgeukia Uthman, na akarudia swali lile lile kwake. Uthman mara moja akakubali. Hapo yule mwenye sauti katika uchaguzi mwenyewe akawa wa kwanza kumpa kiapo cha utii. Alimpongeza kwa kuwa khalifa mpya, na akawaashiria na wengine kutoa viapo vyao vya utii kwake.

Khalifa akawa amechaguliwa. Khalifa mpya wa Waislam alikuwa ni Uthman bin Affan. Ali aliuachia ukhalifa ukaponyoka kutoka mkononi mwake lakini hakukubaliana na utaratibu huo. Hakuwaona Abu Bakr na Umar kama warithi halali wa Muhammad (s.a.w.w.), na alikataa kuwafuata katika jambo lolote lile.

R.V.C. Bodley:

“Wale washauri sita walioteuliwa na Umar walikutana mara tu baada ya mazishi kumalizika. Ukhalifa kwanza ulipendekezwa kwa Ali kwa masharti kwamba atawale kwa mujibu wa Qur’an, Sunnah ya Muhammad, na taratibu zilizowekwa na Abu Bakr na Umar. Ali aliyakubali yale masharti mawili ya kwanza, na akakataa hilo la tatu.

Pendekezo hilo kwa hiyo, likaondolewa na Uthman akafuatwa kwa masharti hayo hayo. Akiwa sio mwaminifu kuliko Ali, aliyakubali hayo bila ya kusita.”
(The Messenger – the Life of Mhammad, New York, 1946)

Abdur Rahman alijua kwamba hakuna hata mmoja kati ya masahaba aliyekuwa na elimu zaidi ya Kitabu cha Allah swt., au ambaye alikuwa ameshikamana sana na Mtume Wake (s.a.w.w.) kuliko Ali. Lakini pale alipoitaja Qur’an na Sunnah ya Mtume, katika pendekezo lake la ukhalifa kwa wagombea, alikuwa “akijipendekeza.” Kutamka kwake kwamba Ali atende kwa kulingana na amri za Qur’an na afuate Sunnah ya Muhammad, kulikuwa kwa kimbinu badala ya kibusara; kwa kuremba zaidi kuliko kawaida. Nia yake hasa ilikuwa ni katika kujifunga kwa Ali katika kufuata mienendo ya Abu Bakr na Umar, wote ambao walifanya iwezekane kwake na kwa wengine wengi kuwa matajiri na wenye uwezo mkubwa.

Ubepari, lile “sanamu lenye sura mbaya sana” la Nyakati za Ujahilia, na masanamu mengine ambayo Makuraish waliyaabudu hapo Makka, yalikuwa yamezikwa na Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt. Lakini baada ya kifo chake, lile sanamu la kibepari likafufuka, na lilikuwa “limerudishiwa nafasi yake” hapo Madina. Mfumo wa kibepari haraka sana ukaota mizizi katika jamii ya Kiislam, na walizama sana kiasi kwamba ikawa haiwezekani kuwang’oa. Baada ya kifo cha Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), huo mfumo wa kibepari uliendelea kupata nguvu zaidi na zaidi.

Wajumbe wote wa jopo lililoteuliwa na Umar kuchagua khalifa, walikuwa mabepari isipokuwa Ali. Walijua kwamba kama Ali angeishika serikali, angeliuua mfumo wa kibepari; angewalazimisha hao mabepari kutapika mali yote ya haramu waliyokuwa tayari wameibugia kilafi, na angehuisha ule urahisi na usafi halisi wa jamii ya Kiislam kama vile ulivyokuwa wakati wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt. Yule mwenye sauti katika uchaguzi na wale waliotajirika hivi karibuni hawakuwa na hamu ya kurudi kwenye siku zile za ukosefu wa anasa na kujinyima.

Lakini hata kama Umar hakutaka kumfanya Uthman kuwa mrithi wake, na hata kama hakuwa na upendeleo kwa mgombea yoyote, na hata kama kungekuwa hakuna njama kati ya Abdur Rahman, mwenye sauti katika uchaguzi, na Amr bin Al-Aas, Ali bado asingeweza kuwa khalifa. Kitu kimoja wajumbe wote wa kamati ya uteuzi, na Waislam wengine wengi ambao waliunda ule utawala wa kikabaila wa Waarabu walichokiogopa zaidi, kilikuwa ni kuona mtu mkali, imara na mwenye nguvu kama Ali katika nafasi ya uongozi wa mambo yao. Walijua vile vile kwamba Ali, asiye na kuyumba binafsi katika masuala ya kanuni, atakuwa mgumu kwao, na kwamba ataushurutisha umma wote kuishi kwa utii juu ya amri za Qur’an.

Lakini mtindo wa Uthman, tabia na utendaji, kwa upande mwingine, vimekuwa thabiti daima katika kuwa vya kawaida mno kiasi kwamba vingeweza kutegemewa katika kutunuku ukadiri juu ya ukhalifa. Ukadiri wake ulikuwa uwe ni uhakikisho kwamba hataingilia haki na ridhaa za wachaguzi. Kulinda maslahi yao, kwa hiyo, kulikuwa ni muhimu zaidi kwao kuliko kulinda maslahi ya Uislam.

Sifa njema za mgombea wa nafasi muhimu kabisa katika Uislam hazikuonekana popote katika fikira za yule mwenye sauti katika uchaguzi. Ukweli ni kwamba maslahi ya Uislam au sifa za mgombea yalikuwa ni mambo yaliyokuwa na umuhimu mdogo sana katika mahesabu yake. Uamuzi wake ulitawaliwa, sio na maslahi ya Uislam, bali na nia yake katika kuendeleza hali ilivyo. Mvutano ndani ya kamati ya uteuzi, kwa hiyo, ulikuwa ni pamoja na pambano la kupimana nguvu kati ya mfumo wa kibepari na wenye kupenda usawa wa kijamii na kiuchumi wa Kiislam. Ali alifanya kila alichoweza kukifanya ili kulinda upen- da usawa lakini uwezekano ulikuwa kinyume kabisa na yeye.
Kuchaguliwa kwa Uthman kama khalifa kulikuwa ni ushindi kwa ubepari. Umar alikuwa ameutunga mpango wa “Shura” (kamati ya uteuzi), na alikuwa amemkabidhi Abdur Rahman bin Auf jukumu la kuutekeleza.

Huyu, kama mwenyekiti wa kamati hiyo, alikifanya kama ni kigezo cha sharti kwamba mgombea wa ukhalifa atatii sio tu Kitabu cha Allah na kufuata Sunnah ya Mtume Wake, bali pia, afuate taratibu za Abu Bakr na Umar. Kwa hiyo aliyaweka matendo ya Abu Bakr na Umar kama ni sawa na Qur’an na Sunnah ya Mtume Wake.

Ali alikataa kuyalinganisha matendo ya Abu Bakr na Umar na Kitabu cha Allah swt. na Sunnah ya Mtume Wake (s.a.w.w.). Alikataa kuwafuata watu wenye kukosea ambao walikuwa ndio viongozi wa kisiasa wa wakati wake akijua kwamba kukataa kwake kutamgharimu kukosa utawala wa dola ya Waislam. Alidharau kiti hicho cha utawala kwa sababu bei aliyokuwa anatakiwa alipie, ilikuwa ililkuwa inapingana na Ukweli na Haki. Alitamka hadharani kwamba mienendo ya Abu Bakr na Umar haikubali. Kama mienendo yao ilikuwa haikubaliki kwake, basi ukhalifa wao pia lazima utakuwa haukukubalika kwake.

Huu ni ushahidi unaothibitisha kwamba hakutoa kiapo cha utii kwao. Lakini kama Sunni wanasisitiza kwamba Abu Bakr na Umar walipokea kiapo cha utii kutoka kwake, basi watakuwa wamekichukua kutoka kwake kwa ncha ya upanga.

Ali angeweza kutamka, kama alivyofanya Uthman, kwamba alikuwa anAyakubali masharti ya yule mwenye sauti katika uchaguzi, na baada ya kuchukua hatamu za uongozi mkononi mwake, angeweza kuyakataa, tena, kama Uthman alivyofanya. Wanasiasa wengi wanaona maneno matupu na usaliti ni jambo la kawaida na linalotambulika katika ujuzi wa uongozi. Lakini Ali hakuona hivyo. Kwake yeye penye nia hapakuwa na njia. Kwake yeye hizo njia pia zilikuwa ziwe za kuheshimiwa tu na za haki kama zile nia zenyewe.

Upingaji Wa Ali

Ali alimwambia yule mwenye sauti katika uchaguzi: “Sio mara ya kwanza ambapo ninyi mmewanyima warithi na watoto wa Muhammad, Mtume wa Allah swt., haki zao kwa usaliti. Kwa hili mtawajibika mbele ya Allah swt. Lakini kwangu mimi, ni vyema kuweka imani yangu kwa Allah Ambaye pekee ndie Mkweli, Mwadilifu na Mwenye kurehemu.”

Yule mwenye sauti katika uchaguzi alifanya majaribio katika kujipendezesha kwa ajili ya jukumu lake kwa namna ile ile kama Abu Ubaidah bin al-Jarrah alivyofanya baada ya kuchaguliwa kwa Abu Bakr pale Saqifah lakini haikuchukua muda kabla hajajilaani mwenyewe kwa ulaghai wa kisheria na undumilakuwili katika jambo ambalo juu yake hali ya baadae ya Uislam wenyewe ulikuwa ukitegemea.

Abdur Rahman bin Auf, mume wa dada yake Uthman, aliishi kiasi cha kutosha kuona matunda ya kazi yake ya kuwa mwenye sauti katika uchaguzi. Aliiona rushwa ikienea katika mtego wake kama pweza katika dola ya Waislam, na “alishitushwa” sana na upendeleo wa kindugu katika ajira na kutokufaa kwa khalifa aliyekuwa amemchagua kiasi kwamba alitamka kwamba hataongea naye (kulikuwa hakuna chochote kingine cha kufanya tena).

Wakati fulani baadae, alipokuwa karibu ya kufa, Uthman alikuja kumuona lakini hakuzipokea salamu zake na akageuzia uso wake kuelekea ukutani. Alikufa katika hali hii, bila ya kujibizana neno na khalifa.

Dr. Taha Husain wa Misri anasema katika kitabu chake, al-Fitna–tul-Kubra kwamba Abdur Rahman bin Auf alikufa mwenye aibu tele na majuto kwa kile alichokuwa ameki- fanya kama mwenyekiti wa kamati ya uteuzi ya Umar.

Kupinga Kwa Ammar Bin Yasir

Ammar bin Yasir, sahaba na kipenzi cha Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), alimshutumu Abdur Rahman na mashoga zake, akisema: “Mmepora haki za familia ya Mtume wenu, sio mara moja bali kwa kurudia rudia, na mmeziweka hizo juu ya watu ambao hawastahili kabisa.”

Pongezi Za Abu Sufyan Kwa Uthman

Uthman alipokuwa khalifa, furaha ya Bani Umayya haikuwa na mpaka. Maisha kwao, walijua, yatakuwa mazuri na ya kupendeza kuanzia hapo, na ilikuwa hivyo. Kiongozi wao, Abu Sufyan, sasa akiwa na umri wa miaka 90 na kipovu, alikuja kumpongeza khalifa mpya, na akampa ushauri ufuatao:

“Ni baada ya muda mrefu ambapo ukhalifa umekuja kwetu. Sasa upigeni kama mpira, na uutmie huo katika kuwaimarisha Banu Umayya. Haya madaraka mapya uliyonayo mikononi mwako, ni kila kitu. Ndio ukweli pekee. Hakuna kitu kingine ambacho ni cha kweli au muhimu. Pepo na moto si lolote si chochote.”

“Ushauri” wa Abu Sufyan kwa Uthman ulikuwa ndio kigezo cha msukumo wa Bani Umayya kwenye Uislam, na kilikuwa kibaki bila ya kubadilishwa kwa karne yote ya umiliki wao wa kisiasa isipokuwa katika miaka mitatu na nusu ya u khalifa wa Umar bin Abdul Aziz (R).

Kuchaguliwa kwa Uthman kama khalifa kwa mara nyingine tena kumekazia ule ukweli wa methali isemeyo kwamba pale kwenye pesa, pana nguvu.

(Charles E. Hurwitz ni mshirika wa uvamizi ambaye ananunua makampuni ya Kimarekani na kisha anazikongoa mali zake ili kulipia deni la utwaaji wake. Anatawala himaya ya kifedha yenye thamani inayokisiwa kuwa $8.5 billion mnamo 1990. Yeye wakati mmoja alitoa $60 milion kutoka kwenye mfuko wa pensheni wa wafanyakazi wa kiwanda. Kuhusu wale wafanyakazi waliovunjika moyo, aliwakumbusha “ukweli wa maisha.” Alisema: “Ipo Hadith ndogo kuhusu Utawala wa Dhahabu. Wale ambao wanayo dhahabu, ndio wanao tawala.”)

Uwiano wa mamlaka ya kiuchumi na mamlaka ya kisiasa ni wa wazi sana kuweza kuhitaji ufafanuzi au mkazo wowote. Umar aliwachagua watu matajiri sana katika Arabia yote kama wateuzi wa khalifa. Mteuzi pekee ambaye hakuwa tajiri, alikuwa ni Ali. Umar hakutaka Ali kuwa khalifa lakini hakuweza kupata sababu yoyote yenye kuelekea kuwa ya kweli ya kumuondoa Ali kutoka kwenye kamati yake ya uteuzi. Kumuondoa Ali kungeweza kufanya chuki juu ya, na uadui kwa familia na ukoo wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kuwa ya dhahiri zaidi.

Umar aliishi na ugonjwa wa hofu isije ikawa Ali kuwa ndio amekuwa khalifa wa Waislam. Wakati mmoja iliarifiwa kwake kwamba mtu mmoja alisema kwamba baada ya kifo chake (Umar), atamtambua Ali kama khalifa. Hili lilimuogopesha sana Umar, na mara moja akawaonya Waislam dhidi ya kufanya hivyo.

John Alden Williams

(Umar alisema) “Karibu nitawaelezeni jambo ambalo Allah amependa kwamba niliseme. Ye yote yule anayelielewa na kulisikiliza, naalichukue popote anapokwenda. Nimesikia kwamba mtu mmoja amesema, ‘Kama Umar angekufa, nitamtukuza fulani’ (yaani, Ali ).”(Themes of Islamic Civilization, uk. 61, 1971)

Kabla tu ya kifo chake, Umar alikuwa amemwita Abdur Rahman bin Auf chumbani kwake kwa ajili ya kikao cha faragha. Haijulikani walizungumza juu ya kitu gani kwa sababu Umar anasemekana kudai kiapo kutoka kwa Abdur Rahman kwamba ataliweka suala la mambo yaliyoongelewa kuwa ni siri kubwa ambayo Abdur Rahman alifanya.

Akimtaka Rais Nixon ajiuzulu kwenye uraisi, kufuatia uchunguzi wa Watergate huko Washington D.C., Seneta James L. Buckley (Republican) wa New York, alisema mnamo tarehe 19 Machi, 1974 kwamba: “Mwenendo wa utawala wakati wote unaakisi na kuonyesha mwenendo wa kiongozi wake, na wasaidizi wa kiongozi huyo na mawakala wake hufanya kile wanachohisi na kuamini kwamba anawataka wao wakifanye.”

Wasaidizi na mawakala wa Umar walifanya hasa kile “walichohisi” na kuamini aliwataka wao wakifanye. Miaka kadhaa kabla, Uthman bin Affan aliijaza nafasi ya katibu binafsi wa Abu Bakr. Alikuwa akiandika wasia na mirathi ya Abu Bakr wakati yeye akiwa kwenye kitanda cha mauti yake. Abu Bakr alikuwa ameanza tu kutoa imla, na Uthman alikuwa ameandika tu maneno, “Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma, Mwenye kurehemu.
Mimi, Abu Bakr, mrithi wa Muhammad, Mtume wa Allah ….….” pale alipopoteza fahamu. Lakini kabla hajarudiwa na fahamu, Uthman mwenyewe aliongeza maneno haya: “……. Ninamteua Umar kama mrithi wangu na mtawala wenu,” na hivyo kuimalizia sentensi hiyo.

Uthman “alihisi” na kujua hasa kile ambacho Abu Bakr angemtaka yeye afanye. Aliendelea na akakifanya. Kitendo chake kilipata uthibisho wa Abu Bakr pale alipopata fahamu.

Abdur Rahman bin Auf “alihisi” na alijua kile ambacho Umar alimtaka yeye akifanye, na alikifanya. Akiwa amejaaliwa na utambuzi kama alivyokuwa, aliweza kusoma dalili zote katika mkondo wa sera za Umar!

Uthman Bin Affan, Khalifa Wa Tatu Wa Waislam, 644 - 656

Uthman bin Affan alitokana na ukoo wa Umayya. Anasemekana kuukubali Uislam kupitia juhudi za Abu Bakr, na alikuwa mmoja wa wafuasi wa awali. Alikuwa mmoja wa watu matajiri wa Makka. Uthman hakushiriki katika vita vya Badr, na alibakia Madina.

Uthman alikuwepo kwenye vita vya Uhud lakini alikimbia kuokoa maisha yake wakati Waislam waliposhindwa. Baadhi ya watoro walirudi Madina lakini sio Uthman. Sheikh Muhammad el-Khidhri Buck wa Misri anaandika katika kitabu chake, Nuur al-Yaqiin fi Siirat Sayyed al-Mursaliin (Cairo, uk.138, 1953) kwamba Uthman alikuwa na haya sana ambazo zilimzuia kuingia Madina.

Wakati wa majadiliano ya Hudaybiyya, Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Uthman kama mjumbe wake kwa Makuraish huko Makka. Sababu ya kumtuma kwake, ilikuwa kwamba Umar alikataa kwenda, na alimlenga yeye kama mjumbe bora kwa shughuli hiyo, akijua kwam- ba yeye (Uthman) alikuwa ni kipenzi cha Abu Sufyan, na kwa hiyo, angekuwa salama kutokana na madhara yoyote. Uchaguzi wake haukuwa na uhusiano wowote na kufaa kwake kwa kazi hiyo.

Uthman anasemekana kuchukua nafasi kubwa katika kuandaa msafara wa kwenda Tabuk. Hapo Madina, anasemekana kwamba alinunua kisima na akakikabidhi kwa jumuiya. Wakati wa ukhalifa wake, Uthman alikusanya Aya za Qur’an na kuzipanga kama toleo rasmi la ujumbe wa mwisho wa Allah kwa wanadamu. Kulikuwepo na nakala nyingine zilizokuwepo hadi wakati huo lakini alizikusanya na kuzichoma moto.

Watangulizi wa Uthman katika serikali ya Saqifah walikuwa ni Abu Bakr na Umar. Ingawa Abu Bakr na Umar hawakufanikisha kitu chochote cha kusifika hasa wakati wa uhai wa Muhammad (s.a.w.w.), baada ya kifo chake walijionyesha wenyewe kwamba walikuwa watu wenye uwezo wa ajabu sana. Lakini Uthman, kwa upande mwingine, alikuwa mtu wa udhaifu wa kuvutia sana, wakati wote kabla na baada ya kupanda kwenye madaraka ya watangulizi wake wawili. Mbali na kutoa michango ya kifedha kwenye baadhi ya juhudi za jumuiya, hakufanya kamwe kitu chochote cha kumtofautisha na watu wa kawaida.

Uthman alikuwa tayari amekwishastaafu, akiwa na umri wa miaka 72, wakati alipokuwa khalifa. Lakini kwa upande wake yeye, kustaafu hakukuwa ni kikwazo. Kulikuwa, kwa kweli, ni moja ya rasilimali zake chache.

Wale wateuzi walikuwa wakigumia chini ya nidhamu kali iliyokuwa imewekwa juu yao na Umar; alikatiza mwingi wa uhuru wao. Sasa kwa vile amekufa, hawakuwa na nia ya kurudia kwenye siku zile za mfadhaiko, na walitaka kufaidi uhuru wao. Wao, kwa hiyo, walichagua khalifa dhaifu na mwenye umri mkubwa ambaye nguvu yake juu ya serikali, walijua itakuwa dhaifu siku zote.

Kuchaguliwa kwa Uthman kama khalifa, lilikuwa ni jibu lisiloepukika dhidi ya ugumu wa kufuata sheria wa nyakati za Umar. Uthman alisimulia Hadith 146 za Mtume wa Uislam (s.a.w.w.).

Ndoa Za Uthman

Wakati mmoja kulikuwa na wasichana watatu wakiishi kwenye kaya ya Khadija. Majina yao yalikuwa ni Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum. Zainab aliyekuwa mkubwa kati ya hao watatu, alikuwa ameolewa na mtu mmoja Abul-‘As ibn ar-Rabi wa Makka. Mtu huyu alipigana dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) katika vita vya Badr, na alitekwa na Waislam.

Ili kufidia uhuru wake, mke wake alituma kwa Mtume (s.a.w.w.), mkufu ambao wakati mmoja ulikuwa mali ya Khadija, na alikuwa amempa yeye kama zawadi wakati wa harusi yake. Abul-‘As aliachiwa huru; akarudi Makka, na akampeleka Zainab Madina kama alivyoahidi kufanya. Zainab, hata hivyo, alifariki mara tu baada ya kuwasili Madina. Baadae, Abul-‘As pia akaenda Madina, akasilimu, na akaishi pamoja na Waislam.

Wale wasichana wengine wawili, Ruqayya na Umm Kulthum, waliolewa na Utba na Utaiba, watoto wa Abu Lahab na Umm Jamiil. Umm Jamiil alikuwa dada yake Abu Sufyan, kiongozi wa ukoo wa Umayya. Abu Sufyan, kwa hiyo, alikuwa ni mjomba wao Utba na Utaiba.

Haijulikani kwa kiwango chochote cha uhakika hawa wasichana watatu walikuwa ni akina nani. Wengi wa wanahistoria wa Sunni wanadai kwamba walikuwa ni mabinti wa Muhammad na Khadija. Kwa mujibu wa wanahistoria wengine, walikuwa ni mabinti wa Khadija kwa ndoa yake ya mwanzoni.

Waislam wa Shi’a wanakataa. Wanasema kwamba Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum hawakuwa mabinti wa Muhammad na Khadija; kwa kweli, wala hawakuwa mabinti wa Khadija kwa ndoa yoyote ya mwanzo; walikuwa mabinti wa dada (mjane) yake Khadija. Dada yake Khadija pia alifariki, na katika kufariki kwake, yeye (Khadija) aliwachukua wasichana hao watatu nyumbani kwake mwenyewe na akawalea kama watoto wake mwenyewe.

Kwa mujibu wa Waislam wa Shi’ah, Muhammad na Khadija walikuwa na watoto watatu na sio sita. Wawili wa kwanza wao – Qasim na Tayyib au Tahir – walikuwa wavulana, na wote walifariki katika utoto wao. Wa tatu na mtoto wa mwisho alikuwa msichana – Fatima Zahrah. Yeye alikuwa ndiye mtoto wao pekee ambaye hakufariki katika uchanga wake.

Hawa wasichana, Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum – hawangeweza kuwa mabinti wa Mtume wa Uislam. Kama wangekuwa, asingeweza kuwaozesha kwa waabudu masanamu ambao waume za wote watatu walikuwa. Ni kweli kwamba wasichana wote watatu waliolewa zamani kabla ya kuchomoza Uislam. Lakini bado hakuvunja amri zozote za Qur’an katika wakati wowote – kabla na baada ya alipofanywa kuwa Mtume wa Allah swt. Na Qur’an iko wazi juu ya makatazo ya ndoa ya mwanamke wa Kiislam kwa pagani.

Ukatazaji wa ndoa ya mwanamke Muislam na mshirikina unatokea kwenye Aya zifuatazo za Qur’an Tukufu:

وَلَا تَنْكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ{221}

“Msiwaoze (mabinti zenu) kwa makafiri.”(Sura ya 2: Aya 221)

لَا هُنَّ حِلٌّ لَهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ ۖ{10}

“Wanawake hao (walioamini) sio halali kwa makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake hao.” (Sura ya 60: Aya ya 10)

Kuna Aya nyingine katika Qur’an ambazo, bila kurejelea mahsusi kwenye ndoa, zinafanya ugumu kwa Muislam kuozesha binti au mabinti kwa muabudu sanamu. Baadhi ya hizo ni:

فَلَعْنَةُ اللَّهِ عَلَى الْكَافِرِينَ {89}

“Basi laana ya Allah ipo juu ya makafiri.”(Sura ya 2: Aya ya 89)

فَإِنَّ اللَّهَ عَدُوٌّ لِلْكَافِرِينَ {98}

“Hakika Allah ni adui wa makafiri.”(Sura ya 2: Aya ya 98)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ{28}

“Enyi mlioamini! Hakika washirikina ni najisi.”(Sura ya 9: Aya ya 28)

Hivi anaweza Muislam, hata kama ni wa “kiasi kidogo” au Muislam wa “takwimu” (Muislam jina tu), kuamini kwamba Muhammad (s.a.w.w.), Mletaji na Mfasiri wa Qur’an Tukufu, angeweza kuwaozesha binti zake kwa watu wale ambao Allah swt. amewalaani; ambao ni maadui Zake; na ambao ni najisi?

Kwa mu’min, Aya za Qur’an zilizotajwa hapo juu, ni ushahidi usiokanushika kwamba Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum, wote watatu wakiwa wameolewa, wakati mmoja, kwa waabudu masanamu watatu huko Makka, walikuwa sio mabinti wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na Khadija.

Ikumbukwe pia kwamba Mtume (s.a.w.w.) ambaye alikuwa mpenzi sana wa watoto, hakusema lolote kamwe kuhusu Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum. Wazazi wanatoa mapenzi sawa kwa watoto wao wote, na hawafanyi ubaguzi wowote kati yao. Lakini alikuwa akitoa sifa za juu kabisa juu ya binti yake, Fatima Zahrah. Kuamua kulingana na Hadith, wala hakuwa na habari kwamba wanawake watatu wanaoitwa Zainab, Ruqayya na Umm Kulthum walikuwa wanaishi.

Ruqayya na Umm Kulthum walikuwa bado wanaishi na waume zao wakati wahyi mpya, Sura ya 111 ya Qur’an, iliposhuka kutoka Mbinguni. Katika Sura hii Abu Lahabi na mke wake, Umm Jamiil, wakwe za Ruqayya na Umm Kulthum, walilaaniwa kwa upotovu wao.

Wahyi huu mpya uliamsha ghadhabu za wawili hawa wazee, na waliwaamuru vijana wao kuwataliki wake zao, na kuwarudisha nyumbani kwa Khadija. Vijana hao waliwatii wazazi wao, wakawataliki wake zao nao (hao wake) wakarudi nyumbani kwa Khadija. Muda fulani baadae, Ruqayya aliolewa na Uthman bin Affan. Alifariki mnamo mwaka A.D. 624. Baada ya kifo chake, dada yake, Umm Kulthum, aliolewa pia na Uthman. Alifariki miaka michache baadae.

Ile miaka ya huko Makka, baada ya kutangazwa kwa Uislam, na ile miaka ya awali huko Madina, ilikuwa ya majaribu kwa hatari nyingi juu ya Muhammad (s.a.w.w.). Kila siku ilileta changamoto mpya kwake. Aliyaweka maisha yake kwenye mkondo wa moto mara tu alipotoka nje ya nyumba yake. Na bado Ruqayya na Umm Kulthum hawatajwi kamwe wakitoa huduma kwa baba yao.

Kwa upande mwingine, Fatima Zahrah alimsaidia baba yake katika dharura mbali mbali, kote Makka na Madina. Ruqayya na Umm Kulthum wote walikuwa wakubwa kuliko Fatima kwa miaka mingi, na walipaswa kumtia moyo na kumfariji baba yao wakati wowote alipokuwa ameonewa na waabudu masanamu hapo Makka au alipokuwa amejeruhiwa katika vita huko Madina lakini kamwe hawakufanya hivyo.

Wanahistoria wa Sunni wamempa Uthman cheo cha Dhun-Nuurayn ambacho kina maana ya “mmiliki wa nuru mbili,” kwa sababu aliwaoa, kulingana na wao, mabinti wawili wa Mtume (s.a.w.w.), heshima ambayo hakuipata hata Abu Bakr na Umar!

Uthman alikuja kuwa mwenye kumiliki nuru mbili baada ya kuwaoa Ruqayya na Umm Kulthum. Lakini wasichana wote hawa wawili walikuwa wameolewa na waabudu masanamu, yaani, Utba na Utaib, watoto wa Abu Lahabi, kabla ya kuolewa na Uthman. Kwa hiyo, kila mmoja wa hawa watoto wawili wa Abu Lahabi walipaswa kuitwa Dhun-Nuur – mwenye kumiliki nuru moja. Kila mmoja wao, Utba na Utaib, alikuwa mmiliki nuru moja ambayo aliirithisha kwa Uthman, hivyo kumfanya yeye kuwa mmiliki wa nuru mbili. Hata hivyo, nuru hizo zilibakia hivyo hivyo; ni umiliki tu ndio uliobadilika!

Matukio Makuu Ya Ukhalifa Wa Uthman

Mnamo A.D.645, kulikuwepo na maasi katika majimbo ya Azerbaijan na Armenia, na yalizimishwa.

Mwaka 647, Mu’awiyah bin Abu Sufyan, gavana wa Uthman huko Syria, aliivamia Asia Ndogo na akaiteka Ammuria.

Mnamo mwaka 648, Abdallah bin Saad bin Abi Sarh, gavana wa Uthman huko Misri, aliiteka Tripoli huko Libya. Hawa wote Mu’awiyah na Abdallah bin Saad bin Abi Sahr walijenga manowari na wakayashinda majeshi ya majini ya Byzantine upande wa Mediterranian ya Mashariki.

Mnamo mwaka 649 manowari za Muawiyyah ziliteka Cyprus.
Mnamo mwaka 651 majemedari wa Uthman waliteka Hirat huko Afghanistan.
Mnamo mwaka 652, nakala rasmi ya kwanza ya Qur’an Tukufu ilitengenezwa hapo
Madina, na nakala zake zikasambazwa kwenye majimbo yote.
Mnamo mwaka 652-54, Abdallah bin Aamir, gavana wa Uthman wa Basra, alimtuma jemedari wake, Abdur Rahman bin Samira upande wa mashariki, ambako aliteka Balkh huko Khurasani, na Kabul na Ghazni huko Afghanistani. Ushindi huu mpya uliifanya himaya ya Waislam yenye kupakana na bara kubwa la Pakistani ya Kihindi.

Upendeleo Na Ukabila Katika Ukhalifa Wa Uthman

Uthman aliwapenda watu wa ukoo wake, Bani Umayya, kwa kiwango ambapo mapenzi yake yaligeuka kuwa ni maradhi. Bani Umayya walikuwa ndio maadui wakubwa wa Uislam, na walipigana dhidi ya Mtume wake kwa zaidi ya miongo miwili. Sasa ghafla, Uthman aliwafanya ni mabwana wa himaya ya Waislam. Yeye mwenyewe akawa kibara- ka wao, na wakachukua hatamu za serikali mikononi mwao wenyewe. Watawala wa kweli wa himaya hiyo, katika ukhalifa wa Uthman, walikuwa ni Marwan (binamu na mkwewe Uthman) na Hakam bin Abul-Al-Aas (ami yake Uthman na baba yake Marwan).

Uthman alifungua milango ya hazina ya umma kwa ndugu zake. Aliwapa zawadi nono, maeneo makubwa na vyeo vya juu. Kisha, kana kwamba hajawafanyia vya kutosha, akawakataza wenyeji wa Madina kuchunga ngamia na ng’ombe wao kwenye malisho karibu na mji.

Malisho haya yalikuwa yamefanywa wakfu na Mtume (s.a.w.w.) lakini kwa mujibu wa sheria mpya za Uthman, wanyama wanaoweza kuchungwa humo ni wale tu waliokuwa ama wake yeye au wa Bani Umayya. Mtume (s.a.w.w.) alikuwa amewaambia Waislam kwamba ile ardhi yote iliyokuwa inanyweshwa kwa mvua, ilikuwa ni mali ya umma wote, na kwa hiyo, wanyama wa watu wote wanaweza kuchungwa humo. Alikuwa amewaambia kwamba ardhi hizi haziwezi kutwaliwa na mtu yoyote kwa matumizi binaf- si kama ilivyokuwa imefanyika Nyakati za Ujahilia.

Qur’an Tukufu imeelezea Hadith ya Nabii Saleh katika sura yake ya saba (Al-A’raaf). Kwa mujibu wa Hadith hii, watu wenye viburi na majivuno wa nyakati za Nabii Saleh, waliwazuia watu wanyonge na dhaifu na ng’ombe wao njia ya kufikia kwenye chemchemi za maji. Ilikuwa ni kwa kuingilia kati kwa Saleh tu ambako kulikowafanya waweze kupata maji kutoka kwenye chemchemi hizo.

Kama maji vile, na malisho pia yalichukuliwa kama zawadi ya bure ya Allah swt. Kwa viumbe wake lakini wale wenye kiburi waliwanyima viumbe hao. Kile kilichokuwa kimefanya na matajiri na wenye uwezo wa wakati wa Thamuud, yalikuwa yakifanywa hapo Madina na matajiri na wenye uwezo wa mji huo – Bani Umayya. Waliunda kikundi chenye mawazo kama hayo, na kukamata ngazi zote za mamlaka.

Serikali hapo Madina ikageuka kuwa fungamano la kurugenzi ya mabinamu, mashemeji na ndugu wengine wa Uthman. Waislam wengine hawakuwa na haki ndani yake. Watu muhimu ndani ya “kurugenzi” hiyo walikuwa:

Hakam bin Abul Al-Aas

Hakam alikuwa ami yake Uthman. Huko Makka, alikuwa mmoja wa majirani wa Muhammad (s.a.w.w.), na mmoja wa wachokozi wake. Alikidhihaki Kitabu cha Allah swt., na alimfanyia mzaha Mtume Wake.

Mnamo mwaka 630 Mtume (s.a.w.w.) aliiteka Makka ambapo Hakam, mwanawe Marwan na Bani Umayya wengine wengi “waliukubali” Uislam. Lakini Hakam na mwanawe hawakuweza kamwe kuusHind uadui wao kwa Uislam na Mtume wake. Walipoweza kuudhuru Uislam, walifanya hivyo.

Hatimaye, Mtume (s.a.w.w.) akawafukuza kutoka Madina. Wakati alipofariki, na Abu Bakr alipokuwa khalifa, Uthman alimuomba kumruhusu ami yake na mkwewe kurudi Madina lakini alikataa.

Wakati Umar alipokuwa khalifa, Uthman alimbembeleza awaruhusu wawili hawa waliotengwa na jamii kurudi Madina lakini yeye pia alikataa. Ndipo Uthman akawa khalifa, na yeye, kwa kweli, hakupoteza muda wowote katika kuwarudisha Madina, na kutoa heshima kubwa sana juu yao.

Yaquubi, mwanahistoria huyu, anasema kwamba wakati Hakam alipoingia Madina, alikuwa amevaa matambara machafu kama omba omba lakini alipotoka kwenye kasiri la Uthman, alikuwa amevaa hariri za thamani sana na zilizotariziwa. Uthman alimteua Hakam kama mkusanyaji wa Zaka kutoka kwenye kabila la Banu Qaza’a. Baladhuri, mwanahistoria, anasema kwamba Hakam alikusanya dirham 300,000, na alipozileta kwa khalifa, yeye akamrudishia ziwe zake na azitumie.

Yaquubi amemnukuu mtu fulani anayeitwa Abdur Rahman ibn Yasir katika Historia yake kama ifuatavyo:

Kazi ya afisa ilikuwa ni kukusanya kodi kutoka kwa wafanya biashara wa masoko ya Madina. Jioni moja niligundua kwamba Uthman, khalifa, alimjia, na akamtaka yeye amlipe Hakam pesa zote alizokuwa amekusanya siku ile. Ilikuwa ni kawaida ya Uthman kutoa zawadi kutoka kwenye hazina ya umma kwa watu wa familia yake. Mkusanya kodi huyo alijaribu kumdanganya Uthman na akasema kwamba ataziwamuhurisha atakapokuwa amekusanya zote zilizokuwa bado kulipwa. Lakini Uthman akamwambia: “Wewe ni mtunza hazina wangu, fanya kile ninachokuambia ufanye.”

Yule mkusanyaji akajibu kwa ukali kwamba yeye ndiye mtunza hazina sio wa Uthman wala wa ndugu zake bali wa Waislam tu. Asubuhi iliyofuata, afisa huyo alikuja Msikitini, na akihutubia mkusanyiko, akasema: “Enyi Waislam! Uthman anasema kwamba mimi ni mtunza hazina wake. Mimi sio. Mimi ni mtunza hazina wa Waislam. Sitaki kuwa mtunza hazina wake.” Kisha akazitupa zile funguo za hazina mbele ya Uthman, na akatoka nje. Uthman akaziokota zile funguo, na akazitoa kwa Zayd bin Thabit.

Marwan Bin Al-Hakam

Marwan alikuwa ni mtoto wa Hakam na ni binamu wa karibu wa Uthman. Alikuwa amemuoa binti ya Uthman, Umm Aban.

Marwan alikuwa “waziri mkuu” wa Uthman. Aligawanya zawadi kutoka kwenye hazina ya umma kwa yeyote aliyemtaka, na alizigawa nafasi za mamlaka katika serikali kwa washabiki wake. Na pia aliuweka mhuri wa khalifa kwenye milki yake na aliufanyia matumizi holela na mabaya. Uthman alikuwa mikononi mwake, na alitekeleza ushauri wake kiupovu.

Baada ya mapigano yenye mafanikio ndani ya Afrika, mmoja wa majemedari wa Uthman alimpelekea ngawira za vita yeye huko Madina. Ngawira hii ilikisiwa kuwa ya vipande nusu milioni vya dhahabu. Uthman alivitoa vyote kwa Marwan.

Baladhuri, yule mwanahistoria, amemnukuu Abdallah bin Zubeir kama ifuatavyo: “Katika mwaka wa 27 Hijiria, Uthman alitutuma kwenye mpaka huko Afrika. Kaka yake wa kunyonya, Abdallah bin Saad bin Abi Sarh, alikuwa ndiye mkuu wa jeshi hilo. Aliteka viwango vikubwa vya ngawira; akaweka nne ya tano yake kwa ajili ya jeshi hilo, na akapeleka moja ya tano yake kwa Uthman huko Madina. Uthman akaitoa yote kumpa Marwan.”

Katika safari nyingine, Uthman alimpa mkwe wake dirham milioni nne kutoka kwenye hazina ya umma. Alilifanya shamba la Fadak pia kuwa zawadi kwake. Marwan alikuwa ajionyeshe mwenyewe kama mfanya kazi hodari katika ukhalifa wa Uthman, na alionyesha tabia ya kiunyonya damu ya upokonyaji.

Harith Bin Al-Hakam

Harith, mdogo wake Marwan, alikuwa amemuoa binti wa pili wa Uthman. Alipokea zawadi ya dirham 300,000 kutoka hazina. Baladhuri anasema kwamba wakati mmoja ngamia fulani walipelekwa kwa khalifa kama sehemu ya Zakat, na aliwatoa wote kwa Harith.

Abdallah Bin Khalid

Abdallah bin Khalid alikuwa mkwewe mwingine wa Uthman. Wakati alipompa binti yake, alimuamuru Abdallah bin Aamir, gavana wa Basra, kumpa yeye (Abdallah bin Khalid) dirham 600,000 kutoka kwenye hazina ya umma.

Walid Bin Aqaba

Walid alikuwa mtoto wa Aqaba bin Abi Mu’ait. Aqaba alikuwa mume wa kwanza au wa pili wa mama yake Uthman. Huko Makka, alikuwa pia ni jirani ya Muhammad, na kama Umm Jamiil, yeye pia alikusanya takataka na kuzitupa mlangoni kwake Muhammad (s.a.w.w.). Alipigana dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) huko Badr, akatekwa, na kwa amri yake, akauawa.

Walid na kaka zake – ndugu wa kuzaliwa nao Uthman – walimuhurimu wakati Makka ilipotekwa.

Safari moja, Mtume (s.a.w.w.) alimtuma Walid kwa kabila la Banu Mustalaq kwenda kukusanya kodi. Aliondoka Madina lakini mara akarudi na kumwambia Mtume (s.a.w.w.) kwamba hao Banu Mustalaq wameukana Uislam, na wamekataa kulipa kodi zao.

Mtume (s.a.w.w.) alishangazwa kuyasikia haya. Lakini kabla hajalichunguza suala hilo, viongozi wa Banu Mustalaq wenyewe waliwamuhuri Madina kuja kulipa kodi zao. Walimhakikishia Mtume (s.a.w.w.) kwamba wao walikuwa ni Waislam wa kweli. Walid hakuwa amewatembelea kamwe.

Ilikuwa ni baada ya tukio hili ambapo Aya ifuatayo ilishushwa kwa Mtume wa Allah swt:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَنْ تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ {6}

“Enyi mlioamini! Kama akikujieni fasiq (mtu mwovu) na habari yoyote ile, ichunguzeni kwanza, msije mkawadhuru watubila ya kujua, na baadaye mkaja kujuta kwa mliyoyatenda.”(Sura ya 49: Aya ya 6)

Kilikuwa ni Kitabu Cha Allah swt. Kilichomwita Walid fasiq, na alikuja kujulikana kwa jina hili daima baadae.

Umar bin al-Khattab alikuwa amemwambia Uthman kwamba kama atakuwa khalifa, amteue Saad bin Abi Waqqas kuwa gavana wa Kufa. Uthman akawa khalifa, na akamteua Saad kuwa gavana wa Kufa kama alivyokuwa ametaka Umar. Lakini ndani ya mwaka mmoja, Uthman akamfukuza Saad na akamteua Walid katika nafasi yake kama gavana mpya.

Mara tu Walid alipojikuta mwenyewe katika milki ya jimbo hilo tajiri, akawa mlevi, wa vyote, madaraka na mvinyo. Alikuwa mlevi wa kutupwa. Alikuwa amelewa hata alipowaongoza Waislam kwenye Swala. Asubuhi moja, aliingia Msikitini akiwa katika hali ya ulevi.

Aliongoza Swala, na akatapika katika qibla cha Msikiti. Habari za ulevi wake zikawa zinazidi mno kwamba hata Uthman akashindwa kuzifumbia macho, na akalazimika kumwita arudi Madina. Badala yake, Uthman alimteua Said bin Al-Aas kama gavana mpya wa Kufa.

Said Bin Al-Aas

Baba yake Said, adui kichaa wa Mtume wa Allah swt., aliuawa katika vita vya Badr. Baada ya kifo chake, Uthman alimtwaa mwanawe, na akamkuza humo nyumbani mwake mwenyewe. Katika mwaka wa 30 Hijiria, Uthman alimfukuza Walid na akamteua Said kuwa gavana mpya wa Kufa. Alimpa pia zawadi ya dirham 100,000 kutoka kwenye hazina ya dola.

Kama watu wengine wa ukoo wake, Said pia alizichukulia hazina za umma kama utajiri wake binafsi, na akazitumia kama alivyotaka. Kama mtu yoyote alilalamika, alimnyamazisha kwa mamlaka yake ya “kipolisi”.

Aliweza kumfanya mtu yeyote apigwe na ali- weza kufanya nyumba ya mtu yeyote ichomwe moto.

Magavana walikuwa wakilipora kila jimbo katika himaya hiyo. Walielekea kuwa baraka za kimya kimya kama sio uhimizaji wa dhahiri wa khalifa. Bila ya kukwepa, wasiwasi ulianza kuchemka na kuunguza pole pole. Uthman aliambiwa kwamba siku moja utakuja kutokea mlipuko.
Akishitushwa na kutoridhika kunakozidi kukua na kuongezeka kwa malalamiko, aliitisha mkutano wa magavana wake wote. Walikuja, wakampa ushauri wa juujuu, kasha wakatawanyika. Said bin Al-Aas alikuwa pia miongoni mwao. Lakini baada ya mkutano ule aliporudi Kufa, wakazi wa mji ule walimzuia karibu na Qadsiyya, na wakamwambia kwamba hawatamruhusu kuingia Kufa. Hakuweza kuingia Kufa, na akaru- di Madina. Katika nafasi yake, Uthman akamteua Abu Musa al-Ashari kama gavana mpya.

Abdallah Bin Saad Bin Abi Sarh

Huyu Abdallah alikuwa ni ndugu wa kunyonya wa Uthman. Baba yake, Saad bin Abi Sarh, alikuwa mmoja wa munafiqiin wa Madina.

Abdallah, wakati mmoja, alikuwa mmoja wa waandishi wa Mtume (s.a.w.w.). Wakati Mtume alipomtakia Aya yoyote ya Qur’an, aliigeuza kwa kubadili alama zake za kutofautisha matamshi au herufi au maneno. Mara akakamatwa na Mtume (s.a.w.w.) akamfukuza kutoka Madina.

Akaukana Uislam, na akaenda Makka, na akaanza kueneza habari kwamba Muhammad (s.a.w.w.) mwenyewe ndiye aliyeziunda zile Aya za Qur’an, na akadai kwamba ni wahyi kutoka Mbinguni.

Wakati Makka ilipotekwa, Mtume (s.a.w.w.) aliamuru kwamba Abdallah auawe kama kafir hata kama akiwa ndani ya Al-Kaaba yenyewe. Lakini Uthman alimudu kumficha ndani ya nyumba yake mwenyewe. Baadae, wakati hali iliporudi kuwa ya kawaida, alimleta mbele ya Mtume (s.a.w.w.) na akasema kwamba alikuwa anaomba msamaha na pia alikuwa anataka kutoa kiapo cha utii. Lakini Mtume hakutoa mkono wake, na akakaa kimya cha kulazimisha kwa muda kiasi cha kutosha.

Uthman alimuombaomba sana yeye amsamehe Abdallah. Hatimae, akamsamehe. Lakini mara tu Uthman na Abdallah walipotoka machoni kwa Mtume, aliwageukia wale waliokuwa karibu naye, na akasema: “Nilikuwa kimya kwa muda mrefu kiasi kile nikitegemea kwamba mmoja wenu angemuua yule.” Baladhuri anaandika ndani ya kitabu chake, Ansab-ul-Ashraf (uk. 358):

“Mtume akasema: ‘Hivi hakuwepo mtu yoyote kati yenu ambaye angeweza kumuua mbwa huyu kabla hajapata msamaha?”

Umar bin al-Khattab akajibu: ‘Ewe Mtume wa Allah, kama ungetuashiria sisi, tungemuua.’ Mtume (s.a.w.w.) akasema: ‘Nisingeweza kuwaashirieni. Kufanya hivyo kusingenistahili mimi.”

Pale Uthman alipokuwa khalifa, alimteua Abdallah kuwa gavana wa Misri. Kwa kuteuliwa kwake, utawala wa kidhalimu na unyonyaji ulianza huko Misri. Neema ya Misri ikageuka kuwa matatizo; ustawi ukageuka kuwa dhiki. Kila mmoja alimchukia huyo gavana mpya. Na huyu gavana akawa na mgongano na Muhammad ibn Hudhaifa.

Baba yake Muhammad, Hudhaifa, alikuwa mmoja wa wafuasi wa awali kabisa wa Uislam. Alikufariki akiwa anapigana kwenye vita vya Yarmuk. Wakati wa kifo chake, Uthman alichukua dhima ya Muhammad, mwanawe mdogo, na akamlea. Alipokua, aliomba ruksa ya kwenda kwenye vita vya kigeni. Uthman alimruhusu kuandamana na Abdallah bin Saad kwenda Misri kama mmoja wa washauri wake.

Muhammad bin Hudhaifa alikuwa muadilifu na mchamungu sana, na alitumia muda wake mwingi sana katika ibada. Wakati rushwa na ufisadi vilipoinua vilipozidi katika utawala, alimuonya Abdallah, na akamhimiza kurudisha serikali nzuri.

Lakini Abdallah hakuusikia maonyo hayo mazuri. Hata hivyo, Muhammad aling’ang’nia juhudi zake za kumrekebisha. Abdallah, hata hivyo, alionekana kuwa na, kama Marwan, dalili za upotovu katika tabia yake, na alifurahia kufanya yale tu ambayo amekatazwa kuyafanya.

Hatimae, Muhammad akapoteza matumaini. Kutoka muonyaji wa kirafiki na mwenye huruma, aligeuka na kuwa mkosoaji aliyezinduka na mkali – kwanza wa Abdallah bin Saad, na baadae wa Uthman mwenyewe kwa kumchagua kama gavana wa Misri mtu kafiri ambaye kuuawa kwake kuliamrishwa na Mtume wa Allah swt. mwenyewe.
Watu wa Misri walimpenda Muhammad bin Hudhaifa kwa uaminifu wake na ujasiri wake katika kumkosoa huyu gavana mpotofu, na walimsaidia. Abdallah alimwandikia Uthman kwamba huyu kijana aliyemlea (yeye Uthman), alikuwa anaeneza uchochezi wa maasi dhidi ya serikali, na kwamba kama hakutafanyika lolote la kumzuia, hali itamshinda kuidhibiti.

Uthman hakujua la kufanya. Ilionekana kwake kama angeweza kuyanyamazisha malalamiko ya Muhammad kwa vipande vya dhahabu na vya fedha. Yeye, kwa hiyo, alimpelekea dirham 30,000 na vipande vingi vya vitambaa venye thamani kubwa kama zawadi. Mwanzo wa mchezo huu, bahati mbaya kwa Uthman, ulimgeukia mwenyewe. Muhammad alizileta zile pesa na vitambaa ndani ya Msikiti mkuu, akavirundika vyote chini mbele ya Waislam, na akasema:

“Enyi Waislam! Mnaona kile ambacho Uthman anajaribu kukifanya? Anajaribu kuin- unua Imani yangu. Ametuma sarafu hizi na vitu hivi kwangu kama hongo.”(Tarikh Kamil: Kamil ibn Athiir, juz.3; uk.135)

Uthman aliandika barua nyingi sana za kutuliza kwa Muhammad, na akamkumbusha kwamba alikuwa na deni la shukrani kwake. Lakini Muhammad alizipuuza, na wasiwasi juu ya Abdallah bin Saad uliendelea kukusanya kasi.

Viongozi wa Waislam wa Misri waliitisha mkutano ambao ndani yake waliamua kutuma ujumbe kwenda Madina kadai kutoka kwa Uthman kufukuzwa kwa Abdallah bin Saad.

Baada ya kuondoka kwa ujumbe wa Misri, nafasi ya Abdallah ikawa kama hailindiki. Kwa kuogopa mapinduzi, yeye pia aliondoka Misri kwenda Madina, upande, kwa kujitetea mwenyewe mbele ya baraza la khalifa. Katika kutokuwepo kwake, Muhammad ibn Hudhaifa alishika madaraka ya serikali.

Wakati Abdallah alipofika Elath, alisikia kwamba kasiri la Uthman limezingirwa, na kwamba amewekwa kizuizini humo ndani yake. Alionelea kwamba isingekuwa salama kwa yeye kwenda Madina, na akaamua kurudi Misri. Lakini hapo mpakani, alijulishwa kwamba Muhammad ibn Hudhaifa ameagiza kwamba azuiliwe, na asiruhusiwe kuingia tena Misri.

Papo hapo, akaenda Palestina akisubiri mambo yatakavyojiri huko Madina. Kwa wakati huo, Uthman aliuawa huko Madina, na pale Abdallah aliposikia habari hizo, aliondoka Palestina na akaenda Damascus kuishi huko chini ya ulinzi wa Mu’awiyyah.

Magavana Wapya Wa Majimbo

Kufa
Katika mwaka wa kwanza wa ukhalifa wa Uthman, Saad bin Abi Waqqas alikuwa ndio gavana wa Kufa. Kisha Uthman akamfukuza, na akamteua kaka yake wa karibu, Walid bin Aqaba, kama gavana mpya wa Kufa.

Basra
Umar alikuwa amemteua Abu Musa al-Ashari kama gavana wa Basra. Uthman akamfukuza, na akamteua binamu yake mwenyewe, Abdallah bin Aamir, kama gavana mpya.

Syria
Umar alikuwa amemteua Muawiyyah bin Abu Sufyan kama gavana wake wa Syria. Uthman alimthibitisha kama gavana wake katika jimbo lile.

Misri
Amr bin Al-Aas aliiteka Misri, na Umar alikuwa amemteua yeye kama gavana wa jimbo hilo. Uthman alimfukuza, na badala yake, alimteua ndugu yake mwenyewe wa kunyonya, Abdallah bin Saad bin Abi Sarh. Mtu huyu alikuwa ni kafiri, na Mtume (s.a.w.w.) aliamuru kuuawa kwake lakini aliisimamisha hukumu hiyo wakati Uthman alipomuombea msamaha. Hivyo Uthman kwanza aliokoa maisha ya kafiri na kasha akamfanya gavana juu ya Waislam.

Wanahistoria Wa Kisasa Na Ukhalifa Wa Uthman

Yafuatayo ni maelezo ya baadhi ya wanahistoria wa kisasa juu ya rushwa, ufisadi, upendeleo wa kindugu na matumizi mabaya ya madaraka katika wakati wa Uthman, khalifa wa tatu wa Waislam.

E.A. Belyaev:

“Uporaji usio na kivicho wa hazina ya Waislam, ulipata malalamiko kutoka kwa wale masahaba wachache wa Mtume waliodhani kwamba mapato yote yalikuwa mali ya Waislam na lazima yagawiwe sawa sawa kati yao. Mashuhuri kabisa wa hawa wapinzani wa tofauti za utajiri alikuwa ni Abu Dharr al-Ghiffari. Katika wakati wa utekaji nyara, ‘sahaba’ mtu mzima huyu ambaye, kwa mujibu wa Hadith, Muhammad alimuweka kama mfano kwa Waislam wengine, alikuwa amekwenda Syria ambako alimuadhiri hadharani gavana na viongozi wa vita kwa kujitwalia ngawira na ushuru ambavyo kwa maoni yake yeye vilikuwa ‘mali ya Allah,’ inayowahusu Waislam wote. (uk.143).

Muawiyyah akamuomba khalifa kumuondoa huyu mchochezi hatari, ambaye alikuwa anaongezeka kuwa maarufu miongoni mwa watu wa kawaida, kutoka Syria. Akiwa ameitwa na Uthman, Abu Dharr alifanya makazi hapo Madina, lakini, katika kugundua pale kwamba khalifa alikuwa ametoa zawadi nono kutoka kwenye hazina ya Waislam kwa mpwa wake (ingawa sio kweli) na mkwe wake, Marwan ibn al-Hakam, wakati ambapo akitoa dirham 300,000 kutoka mahali hapo hapo kwa mpwa wake mwingine, Harith ibn al-Hakam, na dirham 100,000 kwa mtu mmoja aitwaye Zaid ibn Thabit, alianza kumshutumu kwa ukali, akiwaahidi wote wanne, kwa msingi wa Qur’an Tukufu, adhabu kwenye moto wa Jahannam.

Akifuatilia shutuma zake, huyu mtetezi wa haki za watu asiye suluhishika na asiye- hongeka (Abu Dharr) alitamka kwamba watu matajiri wanaongezea utajiri wao kwa kuwanyang’anya masikini. Khalifa aliamuru “mkorofi” huyu afukuziwe kwenye sehemu mbali na makazi ya watu, ambako alifariki kutokana na umasikini uliokithiri, akimuacha mjane wake bila hata uwezo wa kulipia mazishi yake ya wastani.

Wakati wa utawala wa Uthman, ndugu zake, watu wa utawala wa kikabila unaoshik- ilia utumwa, wa Makka, walijitwalia nafasi za kiserikali na wakamiliki mashamba kwenye nchi zilizotekwa. Mapokezi ya kihistoria yanatoa wajibu wenye madhara hasa kwa mpwa na mkwe wa khalifa, Marwan, ambaye, kwa kunufaika na udhaifu wa baba mkwe wake, alichukua madaraka halisi ya serikali ya Madina na akafumbia macho kwa kila namna matendo ya kidhalimu ya ndugu zake wenye uchu, na wanyang’anyi. Hawa ndugu wa khalifa, watu wa ukoo wa Umayya, walikuwa wame- teuliwa na Uthman kama magavana na viongozi wa vita; wao walijitwalia zile ardhi zilizochukuliwa kama mali ya jumuiya ya Waislam.

Ukamataji wa ardhi kama huo, pamoja na unyang’anyi, usaliti na vurugu zilizofanywa na watawala hawa, zilisababisha kuongezeka kwa manung’uniko, yaliyoonyeshwa kwa nguvu sana na wale marafiki zake Umar ambao walikuwa wameondolewa kwenye nafasi zao zenye umashuhuri na maslahi. Kukerwa kwao kuliyashirikisha makabila ya Kiarabu (hususan ya Iraki) ambayo maslahi yao ya mali yalipungua kutokana na ubadhilifu wa kidhalimu wa hazina ya dola mikononi mwa wateuliwa wa Uthman.

Khalifa Uthman mwenyewe aliweka mfano wa matumizi mabaya ya mapato ya serikali kwa manufaa ya familia yake binafsi; wakati binti yake alipoolewa na Abdallah ibn Khalid, kwa mfano, Uthman aliwapa dirham 600.000 kutoka kwenye bait-ul-mal ya Basra, ambapo wakati Abdallah ibn Sarh alipotuma qanatir 3,000 (sawa na ratili 300,000) za dhahabu kutoka Afika, aliamuru dhahabu hiyo itolewe kwa familia ya al-Hakam (uk.144). (Arabs, Islam & the Arab Caliphate in the Early Middle Ages, New York,1969)

Sir John Glubb:

“Mnamo mwaka 646 Uthman alimteua kaka yake wa mama mmoja, Walid ibn Uqba, kuwa gavana wa Kufa. Baba yake, Uqba, alikuwa amechukuliwa mateka huko Badr alipokuwa akipigana upande wa Makuraish na alikuwa amehukumiwa kifo na Mtume mwenyewe. Kwa kilio chake cha uchungu, “Ni nani atakayeangalia watoto wangu wadogo?” Muhammad alimjibu kwa mkato, “moto wa jahannam.” Huyu gavana mpya wa Kufa alikuwa ni mmoja wa wale watoto wadogo ambao Mtume wa Allah swt. mwenyewe aliwapangia kwenda motoni.
Walid pia alikuwa na sifa ya ulevi. Lawama juu ya uteuzi wa Uthman ilikuwa inazidi kuwa kubwa. Ndugu yake wa kunyonya, Ibn Abi Sarh, alikuwa amefanywa kuwa gavana wa Misri, ingawa Mtume alikuwa amemtaja kuwa mwenye kustahili kifo kwa sababu ya ukafiri …… (uk. 290- 291)”

Katika mfumo wa utawala wa Kiislam dola haikuwa utaratibu usiohusika na mtu maalum bali (katika nadharia angalau) ni chombo kilichochaguliwa na Allah swt. Hakuna ghiliba yoyote anayoweza kumhalalisha mtu anayependelea maslahi ya kidunia ya ndugu zake kwenye kazi ya Allah swt. Mwenyewe.

Kufuru za dhahiri za wengi wa wateuliwa wa Uthman, na ule ukweli kwamba wao ama baba zao walikuwa wapinzani wakali sana wa Mtume, kuliwachukiza wale Waislam wengi, wachamungu waaminifu huko Makka na Madina.

Masahaba walikuwa bado ni wengi wa wastani, bila ya kuwataja wale watu ambao walipigana kule Badr na Uhud, au wale waliokula kiapo cha chini ya Mti kati ya mikono ya Mtume wa Allah swt. huko Hudaibiyya. Wote hawa sasa waliona mfumo wa utawala wa Kiislam ukitawaliwa na maadui wa Mtume, ambao hali kadhalika walifaidi zile fadhila za kidunia ambazo zilikuwa ni tuzo ya wale waumini waaminifu. (uk. 297).

Mfano wa kile Waislam halisi walichokihisi kuhusu zama za Uthman unatolewa na suala la Abu Dharr. Bwana huyu alikuwa mfuasi wa awali kabisa na aliishi maisha yake kama walii halisi. Yeye sasa, kwanza akiwa Damascus na kasha Madina, alianza kutoa mahubiri yanayoshutumu ukatishaji tama wa nyakati hizo. Huko Syria, huko Iraq, na hata huko Madina, wale Waislam viongozi waliishi kwenye makasiri ya marumaru, wakiwa wamezungukwa na watumwa na mahawara, wakiwa wamevaa mavazi ya anasa na kujifurahisha kwa vyakula vya gharama.

Hapawezi kuwa na shaka kabisa kwamba Abu Dharr alikuwa na haki katika madai yake kwamba utajiri na anasa yote hii vinadhoofisha yale maadili ya Kiarabu ya zamani ya ustahimilivu na uangalifu wa matumizi. Lakini watawala wa himaya hiyo walidai kwamba maneno yake yalikuwa yakiwachochea watu kuasi, na Uthman akaa- muru kufukuziwa kwake kwenye oasisi iliyojitenga peke yake huko Arabia ya Kati. Huko, miaka miwili baadae, alifariki kwa dhiki, na heshima yake mara moja ikatukuzwa kama ile ya walii.
(The Great Arab Conquests, London, 1963)

Uthman Na Marafiki Wa Muhammad, Mtume Wa Allah Swt.

Ikiwa Uthman hakuweza kuonyesha mapenzi makubwa ya kutosha kwa Maadui wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na Uislam kama vile Hakam, Marwan, Walid, na Abdallah bin Saad bin Abi Sahr, vile vile hakuweza kutumia uhasama mwingi juu ya waumini wa kweli, wenye kumpenda Allah swt. na marafikiwaaminifu wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kama Abu Dharr el-Ghiffari, Ammar ibn Yasir na Abdallah ibn Masud. Hadith yao italiweka suala hili wazi.

Abu Dharr El-Ghiffari

Ilifikishwa habari kwa Uthman kwamba Abu Dharr al-Ghiffari alizungumza mbele ya Waislam ndani ya Msikiti kama ifuatavyo: “Mimi ni Abu Dharr el-Ghiffari, sahaba wa Muhammad, Mtume wa Mwisho wa Allah swt. Allah alimnyanyua Adam, Nuh na kizazi cha Ibrahim na Imran juu zaidi ya walimwengu wote. Muhammad amerithi urithi wa mitume wote hawa. Anajumuisha katika utu wake sifa zao, tabia na mafanikio yote. Na mrithi wa Muhammad ni Ali ibn Abi Talib.

Enyi Waislam, ambao leo mmekanganyikiwa, ikiwa baada ya kifo cha Mtume wenu, mngelimuweka yeye (Ali) mbele ya wengine, kama Allah swt. alivyomuweka mbele ya wengine, na kama mngewarudisha nyuma wale watu ambao Allah swt. aliwarudisha nyuma, na kama mngeliyaacha mamlaka na madaraka katika sehemu yake ya amuhuri, yaani, katika nyumba ya Mtume wenu, basi mngezipata baraka za Allah swt. Asingekuwapo hata mtu mmoja masikini au fukara. Wala watu wawili wowote wale wasingehitilafiana katika tafsiri ya ujumbe wa Allah swt. na kila mmoja angetekeleza wajibu wake Kwake, na kwa watu wote katika jumuiya, kama ilivyofanyika wakati wa uhai wa Mtume Wake mwenyewe. Mngeukuta muongozo na elimu katika chanzo chake amuhuria, yaani, katika nyum- ba ya Muhammad (s.a.w.w.). Lakini mliyaachia mamlaka na madaraka ya nyumba ya Mtume wenu yakaporwa, na sasa mnaipata adhabu.”

Waleta habari hawa (wachochezi) pia walimweleza Uthman kwamba Abu Dharr alikuwa akiwatahadharisha Waislam kwenye upotofu wake (Uthman) wa kutoka kwenye mwenen- do wa Mtume (s.a.w.w.) na pia kwenye mwenendo wa Abu Bakr na Umar.

Uthman alimuamuru Abu Dharr kuondoka Madina, na kwenda Syria na kuishi huko. Huko Syria, Mu’awiyah alikuwa ameizatiti nafasi yake, na akawa amepandikiza mfumo wa maisha ya kidunia badala ya ule wa Kiislam. Abu Dharr alishuhudia uovu na vitendo vya kinyume na Uislam katika baraza la Syria.

Aligundua kwamba dhahabu na fedha ya jimbo hilo ilikuwa ikifujwa hapo Damascus katika anasa za wakubwa wakati ambapo Waislam walikuwa wanakaa na njaa. Mu’awiyah mara moja akatambua kwamba Abu Dharr alikuwa hadhibitiki hapo Damascus kuliko alivyokuwa hadhibitiki huko Madina. Abu Dharr alizisoma zile Aya za Qur’an ambamo ndani yake wenye kuhodhi mali wameshutumiwa.

Alikuwa mkosoaji wa wazi na alisema kweli bila kujali madhara ya ukweli huo kwake. Mu’awiyah, alikuwa amejijengea kasri mwenyewe binafsi. Abu Dharr akamwambia: “Kama ulijenga kasri hili kutoka kwenye mfuko ambao ni mali ya Waislam, basi ume- saliti imani; na kama umelijenga kwa mali yako binafsi, basi umekuwa na hatia ya ubadhilifu na majivuno.”

Abu Dharr alimwambi Mu’awiyah na wakubwa wa Syria kwamba watakuja kuwekwa alamahuko motoni kwa dhahabu na fedha ambazo walikuwa wamezihodhi. Mwishowe subira ya Mu’awiyah ikafikia kiwango cha kuvunjika na akamuandikia Uthman hivi: “Ninahofia kwamba Abu Dharr anaweza akawachochea watu kwenye maasi. Ikiwa hutaki maasi katika nchi hii, basi ungemrudisha yeye Madina mara moja.”

Uthman alikubali. Mu’awiyah alimpakia Abu Dharr kwenye ngamia bila ya kiti cha mwamvuli, na alimuamuru yale mwendesha ngamia kusafiri bila kupumzika hadi Madina. Abu Dharr aliwasili Madina nusu maiti kwa majeraha, uchovu na uchi.

Lakini hata katika hali hii, Abu Dharr hakuweza kuridhia uongo, udhalimu, unyonyaji na kutokutii kwenye amri za Allah swt. Kupenda kweli na haki vilichoma kifuani mwake kama muali wa moto. Kama suala lolote la ubadhilifu lilifika machoni mwake, alilishutumu, na aliwakemea waliolitenda hilo hadharani. Mwishowe Uthman hakuweza kuvumilia tena. Alimwita Abu Dharr kwenye baraza yake na majadiliano yafuatayo yakatokea baina yao:

Uthman: Ndiyo
Abu Dharr: Je, utanihamishia Kufa?
Uthman: Hapana.
Abu Dharr: Je, utanipeleka Basra?
Uthman: Hapana.
Abu Dharr: Ni wapi tena basi utakakonihamishia?
Uthman: Ni sehemu gani hasa unayoichukia sana?
Abu Dharr: Rabza.
Uthman: Huko ndiko nitakako kupeleka wewe.

Uthman alitimiza ahadi yake, na akamhamishia Abu Dharr al-Ghiffari kwenda Rabza. Na alitoa amri pia kwamba asionekane mtu yoyote wa kuzungumza naye au wa kuongozana naye. Lakini Ali alikuja kumuona, na kuzungumza na kutembea naye. Pamoja na Ali, walikuwepo wanawe mwenyewe, watoto wa Aqiil ibn Abi Talib, na mpwa wake, Abdallah ibn Jafar.

Lilikuwa ni tukio la kuhuzunisha sana. Ali alikuwa anatengana na rafiki mwandani, na rafi- ki na mpendwa wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Moyo wake binafsi ulijawa na majonzi, lakini alijaribu kumliwaza rafiki yake kwa maneno haya yafuatayo:

“Ewe Abu Dharr, ulikuwa umewakasirikia watu hawa kwa sababu walikengeuka kutoka kwenye njia iliyoonyeshwa na Allah swt. Kwa hiyo, Allah swt. mwenyewe atakufidia. Wanakuogopa wewe kwa sababu wanafikiria kwamba utawanyima dha- habu na fedha yao. Lakini kama ungekuwa pia ni kama wao, wangekuwa marafiki zako.”

Kisha Husain, yule mjukuu mdogo wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) akageuza macho yake yenye kulenga lenga machozi kumtazama yule mpendwa wa babu yake, ambaye sasa anakwenda uhamishoni, na akasema:

“Ewe ami yangu, Allah swt. ataubadili sawa wakati kama huu. Maadui zako ‘wameyaokoa’ maslahi yao ya kidunia kutoka kwako lakini wewe umeiokoa Akhera yako kutoka kwao. Walichokiokoa wao hakina thamani kabisa lakini ulichokiokoa wewe, ni kitu ambacho kitadumu milele.”

Ali na marafiki zake walitembea kimya kimya pamoja na Abu Dharr, na wakati wa kuten- gana ulipofika, Abu Dharr akasema: “Enyi watu wa Nyumba ya Muhammad! Mwenyezi Mungu akubarikini. Kila ninapowaoneni ninyi, kumbukumbu ya hunijia ya rafiki yangu mpendwa, Muhammad, Mtume na kipenzi cha Allah swt.”

Abu Dharr, mke wake na mtumwa wake, walihamishiwa Rabza ndani ya jangwa, na baada ya muda fulani, akafariki huko. Mkewe na mtumwa wake wakamfunika uso wake, na wakauelekeza Al-Kaaba, na kasha wakakaa kando ya njia wasijue la kufanya. Wakati huo huo, wakawaona wapanda farasi wakija kutokea upande wa Iraq. Wapanda farasi hawa walikuwa ni Abdallah ibn Mas’ud, rafiki wa siku nyingi wa Mtume (s.a.w.w.) na wasafiri wengine.Walikuwa wakienda Madina. Walipomuona mjane wa Abu Dharr, walisimama na kumuuliza yeye alikuwa ni nani na alikuwa anafanya nini kwenye sehemu ile isiyokaliwa na watu.

Yule mtumwa wa Abu Dharr akawaambia kama wao walikuwa ni kina nani, na akawafahamisha kwamba mwili wa Abu Dharr ulikuwa umelala bila ya kuzikwa kwani ardhi ilikuwa ya mwamba na walikuwa hawana uwezo wa kuchimba kaburi.

Abdallah ibn Mas’ud alitokwa na machozi na akaomboleza kile kifo cha rafiki yake mwenyewe, na rafiki ya Mtume wa Allah swt. Abdallah ibn Mas’ud na marafiki zake wakaichimba kaburi, wakatayarisha mazishi mepesi, na wakamsalia, na wakamzika bwana Abu Dharr al-Ghiffari.

Muhammad Ibn Ishaq:

“Burayda b. Sufyan al-Aslami kutoka kwa Muhammad b. Al-Kaaba al-Qurazi kutoka kwa Abdallah ibn Mas’ud aliniambia kwamba wakati Uthman alipomhamisha Abu Dharr kwenda Rabza, na wakati wa ajali yake ulipofika, hapakuwa na mtu yoyote pamoja naye isipokuwa mke wake na mtumwa. Aliwaagiza kuja kuuosha mwili wake na kuuvisha sanda, na wamlaze juu ya njia, na kuueleza msafara wa kwanza utakaopita kwamba yeye ni nani, na wawaombe msaada wa kumzika. Alipofariki wakayafanya haya. Abdallah ibn Masud aliwamuhuri pamoja na watu fulani wengine kutokea Iraq wakienda hijja wakati walipoliona lile jeneza pembeni mwa njia. Yule mtumwa akasimama na akasema, “Huyu ni Abu Dharr, rafiki yake Mtume. Tusaidieni kumzika.”

Abdallah ibn Mas’ud aliangua kilio kwa sauti kubwa na akasema: “Mtume alisema kweli; umetembea peke yako, na ukafa peke yako, na utakuja kufufuliwa peke yako.”

Kisha yeye na marafiki zake wakashuka kutoka kwenye ngamia zao na wakamzika, na akawaelezea habari zake na kile alichokisema Mtume walipokuwa njiani kwenda Tabuk.”(The Life of Muhammad)

Dr. Taha Husain:

“Abu Dharr alikuwa mmoja wa wafuasi wa mwanzoni kabisa kwenye Uislam, na alikuwa mmoja wa wale ambao walipendwa na kusifiwa na Mtume mwenyewe.

Mtume alikuwa akisema: “Mbingu ya samawati haijawahi kuning’iniza kivuli chake juu ya mtu ambaye alikuwa mkweli kuliko Abu Dharr.”

Abu Dharr aligundua kwamba Uthman alitoa pesa nyingi sana kwa Marwan bin al- Hakam; na alitoa kwa ndugu yake, Harith bin al-Hakam dirham 300,000; na alimpa Zayd bin Thabit Ansari dirham 100,000. Abu Dharr aliyashutumu yote haya, na akawaambia wale wenye kuhodhi ni jinsi gani watakavyochomwa kwenye moto wa jahannam. Alisoma ile Aya ya Qur’an: Wabashirie adhabu chungu wale wanaohodhi dhahabu na fedha na wala hawazitumii katika njia ya Allah (9:34).
Marwan bin al-Hakam alimjulisha Uthman kile alichokuwa akikisoma Abu Dharr. Uthman alimtuma mtumwa wake kwa Abu Dharr ili kumkataza yeye kuisoma Aya hiyo ya Qur’an inayohusika. Abu Dharr akasema: “Je, Uthman ananikataza mimi kusoma Kitabu cha Allah, na kusahau amri Zake? Kama inanibidi kuchagua kati ya radhi za Allah na radhi za Uthman, kwa hakika nitachakua hizo radhi za Allah.”

Abu Dharr hakubadili msimamo katika shutuma zake kwa wale wanaolimbikiza mali, na alitoa mwito kwa Waislam wasiwe wafujaji wa mali. (al-Fitna-tul-Kubra, kilichochapishwa Cairo 1959 uk.163)

Abu Dharr alipambana na ile madhehebu ya kisiasa inayojitangaza. Katika Uislam, sauti yake ilikuwa ya kwanza iliyosimama kupinga dhidi ya ukiritimba wa kidini na kisiasa, na unyonyaji wa kiuchumi, na sauti yake ilikuwa ndio ya kwanza pia kusimama katika ulinzi dhidi ya “ukandamizwaji” wa Uislam. Sauti yake ilikabwa lakini mawazo yake hayakuwezekana kuyazima. Aliyatoa mawazo yake kutoka kwenye Qur’an Tukufu. Jaribio lolote la kuzima mawazo yake ni jaribio la kuizima Qur’an Tukufu.

Sauti ya Abu Dharr ilikuwa ni sauti ya Dhamira ya Uislam, na jukwaa lake lilikuwa ni Haki za Watu. Mwenyezi Mungu ambariki milele yote.

Ammar Ibn Yasir

Ammar ibn Yasir naye alikuwa mmoja kati ya wafuasi wa mwanzoni kabisa katika Uislam. Kama ilivyoelezwa mapema, mama yake na baba waliteswa mpaka kufa na wapagani hapo Makka. Walikuwa ndio (waliokufa) mashahidi wa kwanza na wa pili wa Uislam, na hii ndio heshima ambayo hakuna hata mmoja katika Uislam wote anayeweza kushirikiana nao. Kama Abu Dharr al-Ghiffari, Ammar alikuwa naye mmoja kati ya wapendwa wa Muhammad, Mtume wa Allah swt. ambaye wakati mmoja alisema: “Ammar ndio mfano halisi wa Imani yote” Kama vile Abu Dharr al-Ghiffari na wengine wachache, Ammar pia hakupendwa sana na mawakala wa mamlaka ya kiuchumi na kisiasa wa wakati wake, na mapambano ya ana kwa ana kati yake na wao yalikuwa hayaepukiki.

Dr. Taha Husain:

“Ammar alihama kwanza kwenda Abyssinia, na kisha kwenda Madina. Yeye alikuwa Mwislam wa kwanza kujenga Msikiti. Aliujenga hapo Makka penyewe, na aliswali ndani yake. Na alijenga, pamoja na wengine, ule Msikiti wa Mtume (hapo Madina). Wakati Waislam wengine walibeba tofali moja kwa wakati, yeye alibeba mbili. Na vilevile alichimba, pamoja na wenzie wengine, lile handaki wakati wa kuzingirwa kwa Madina. Alifunikwa na mavumbi. Mtume wa Allah swt. mwenyewe alimuondoa mavumbi kutoka kwenye kichwa na uso wake.

Wakati Ammar alipozisikia habari za kifo cha Abu Dharr al-Ghiffari, aliomboleza kwa ajili yake. Uthman aliyatafsiri maombolezo yake (kwa ajili ya Abu Dharr) kama ni lawama kwake yeye mwenyewe. Alikasirika sana, na akamuamuru na yeye pia kuondoka Madina, na kwenda Rabza (uhamishoni). Pale Ammar alipokuwa tayari kuondoka Madina, Bani Makhzuum ambao yeye alikuwa mtegemezi kwao, wakasirishwa sana. Ali pia alichukia.

Alikwenda kumuona Uthman, akamlaumu kwa kumhamisha Abu Dharr, na akamwambia asifanye kama hivyo tena kwa Ammar. Uthman akamwambia: “Wewe huna tofauti na Ammar, na wewe pia unastahili kufukuzwa toka Madina.” Ali akamjibu: “Endelea, na fanya hivyo.” Kisha Muhajirina wengine waliingilia kati na kumwambia Uthman kwamba hawezi kumhamisha kila mtu ambaye alitokea kumchukia.

Wakati mmoja, Uthman alikuwa amechukua kipande cha kito kutoka hazina kwa ajili ya familia yake mwenyewe. Miongoni mwa wale watu waliokipinga kitendo hiki, alikuwa ni Ammar ibn Yasir. Uthman alishikwa na ghadhabu. “Unathubutu vipi kunihoji mimi?” alifoka kwa sauti kubwa. Kisha akawaamuru watumwa wake wamkamate. Wakamkamata, na Uthman akampiga kikatili mpaka akapoteza fahamu. Alitolewa pale Msikitini katika hali hiyo mpaka kwenye nyumba ya Umm Salma, mjane wa Mtume. Ammar alikosa fahamu kwa kutwa nzima iliyobaki. Wakati alipopata fahamu mwishowe, alinyanyuka, akachukua udhuu, akasali swala zake, na akasema: “Al–Hamdulillah, yaani, Namshukuru Allah, Sio mara ya kwanza kwamba mimi nimeteswa kwa kusema kweli.” (safari ya kwanza ambapo Ammar aliteswa kwa kuunga mkono ukweli wa Uislam, alikuwa yuko Makka. Katika siku zile, Abu Jahl alikuwa ndiye aliyekuwa akimtesa)
Katika wakati mwingine, masahaba fulani wa Mtume walitunga barua ya ushauri kwa Uthman, na walimuomba Ammar kuiwasilisha kwake. Wakati Ammar alipoiwasilisha ile barua kwa Uthman, alishikwa na hasira tena. Kwa mara nyingine tena, aliwaamu- ru watumwa wake kumuangusha chini. Walimuangusha chini na Uthman akampiga mateke kwenye kinena, na akampiga mpaka akazimia.”
(al-Fitna-tul-Kubra, kilichopigwa chapa Cairo mwaka 1959)

Abdallah Ibn Mas’ud

Abdallah ibn Mas’ud alikuwa mmoja wa masahaba wakuu wa Mtume (s.a.w.w.). Kama ilivyoonyeshwa kabla, alikuwa ndiye mtu wa kwanza kusoma Qur’an ndani ya Al-Kaaba mbele ya viongozi wa Makuraish, nao walimpiga kwa kufanya hivyo. Alikuwa ni mmoja kati ya watu wenye ujuzi mkubwa kabisa hapo Madina. Alitumia muda wake mwingi akiwa pamoja na Mtume (s.a.w.w.), na alikuwa na uzoefu zaidi na vitendo na mifano yake kuliko wengi wa masahaba wengine. Ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba Umar alimuom- ba awe anakuwa naye wakati wote. Kulikuwa na nyakati nyingi ambapo Umar alikuwa hajui jinsi Mtume alivyowahi kutatua tatizo au alivyochukua uamuzi katika suala fulani. Katika nyakati kama hizo, alimuona Abdallah ibn Masud na aliamua kutokana na ushauri wake. Katika miaka yake ya baadaye, Umar alikuja kumteua yeye kama mtunza hazina wa Kufa.

Dr. Taha Husain:

‘Abdallah ibn Mas’ud alikuwa ndio mtunza hazina wa Kufa wakati Saad bin Waqqas alipokuwa ndio gavana wa mji huo. Uthman alimfukuza Saad, na akamfanya Walid bin Aqaba kuwa gavana mpya. Walid alichukua mkopo kutoka kwenye hazina. Pale wakati uliopangwa ulipopita, na mkopo huo ukiwa bado haujarudishwa, Ibn Mas’ud alimuomba yeye kuulipa mkopo huo. Alimjulisha Uthman kuhusu hilo. Uthman akamwandikia: “Wewe ni mtunza hazina wangu. Usiudai ule mkopo kutoka kwa Walid.” Ibn Mas’ud alilikasirikia hili. Alitupilia mbali zile funguo za hazina, na akabakia nyumbani.

Kutokea wakati ule, Abdallah ibn Mas’ud akawa mkosoaji wa sera za hazina na siasa za Uthman. Walid akamwandikia Uthman kuhusu yeye, naye Uthman akamwagizia Walid kumpeleka Ibn Mas’ud Madina.

Ibn Mas’ud aliwasili Madina, na akaenda Msikitini. Wakati alipoingia mle Msikitini, Uthman alikuwa anasoma hotuba. Pale Uthman alipomuona yeye akiingia mle Msikitini, alisema: “Mtu muovu na mbaya anakuja mbele yenu.” Ibn Mas’ud akasema: “Hivyo sivyo. Mimi ni sahaba na rafiki wa Mtume wa Allah. Nilipigana huko Badr, na mimi ni sahaba wa kwenye Mti.” Aisha pia alisikia akiwa chumbani kwake kile Uthman alichokuwa amesema, naye akaguta akisema: “Hiyo ndiyo aina ya lugha unayotumia kwa sahaba wa Mtume wa Allah?”

Uthman alimuamuru Abdallah Ibn Mas’ud kutoka nje ya Msikiti wa Mtume. Watumwa zake Uthman walimtupa nje ya Msikiti, na kumuangusha chini huku wakimvunja mbavu zake.

Ali alisimama kumlaumu Uthman, na alisema: “Umemuumiza rafiki ya Mtume kwa sababu tu ya taarifa kutoka kwa Walid. Wewe unajua kwamba Walid ni muongo.” Yeye kisha akambeba Ibn Mas’ud kwenda naye nyumbani kwake.

Lakini Uthman hakutosheka na kile alichokuwa amekifanya. Baada ya kuvunja mbavu za Abdallah ibn Mas’ud, alisimamisha malipo yake ya pensheni, na akamzuia kuondoka Madina. Ibn Mas’ud alitamani kwenda Syria na kushirika katika mapambano lakini Uthman alikariri kile alichowahi kusikia Marwan akisema: “Amezusha matatizo ya kutosha hapo Kufa; usimuachie akafanya kama hayo tena huko Syria.”(uk.160) (al-Fitna-tul-Kubra, kilichopigwa chapa huko Cairo mwaka 1959)

Kama ilivyoelezewa kabla, Abdallah ibn Mas’ud alikuwa amefanya ukusanyaji wake mwenyewe wa Aya za Qur’an, na alikuwa amezipanga katika kufuata utaratibu wa miaka na matukio. Lakini Uthman alikuwa amemteua kipenzi chake, Zayd bin Thabit, kukusanya na kuzipanga Aya za Qur’an. Hakuwa “ameutambua” ule ukusanyaji wa Ibn Mas’ud, na alimuamuru kukabidhi hiyo nakala yake. Abdallah Ibn Mas’ud akakataa kufanya hivyo ndipo watumwa wa Uthman walipoivamia nyumba yake, na kwa kutumia mabavu wakaikamata ile nakala ya Qur’an kutoka kwake. Nakala hii ilichomwa moto kwa amri ya Uthman.

Uthman alitumia mamlaka ya dola katika kushughulika na watu kama Abu Dharr al- Ghiffari, Ammar ibn Yasir na Abdallah ibn Mas’ud kwa sababu walikataa kukubaliana na taratibu zao. Wote watatu iliwabidi walipie fidia juu ya kukataa huku lakini walizilipa kwa moyo mkunjufu kabisa.

Uthman, hata hivyo, alikuwa pia akivurugana na baadhi ya wale watu ambao hawakuwa wenye kujishughulisha sana na mambo kama taratibu. Miongoni mwao walikuwamo Abdur Rahman bin Auf na Amr bin Al-Aas. Wote hawa walikuwa wanahusika moja kwa moja na upandaji wake kwenye cheo hicho.

Uthman Na Wale ‘Wenye Athari Katika Uchaguzi’

Uthman alipaswa kuwa mwenye shukurani kwa watu wawili hawa waliomfanya yeye kuwa khalifa wa Waislam. Lakini kama alikuwa ni mwenye shukurani kwao, hakuonyesha hivyo. Badala ya kuonyesha shukurani kwao, alivunja imani kidhalimu tu na mmoja wao, na akamfanya yule mwingine kuwa adui asiyekuwa na huruma juu yake mwenyewe.

Abdur Rahman Bin Auf

Wakati Waislam walipopoteza kabisa matumaini kwamba Uthman atarekebisha mwenendo au njia zake, wakageukia, katika kuvunjika moyo, kwa Abdur Rahman ibn Auf; wakamwambia kwamba hakuna chochote katika Dar-ul-Islam kilichokuwa sawa, kila kitu kilikuwa kinakwenda ovyo ovyo tu, na majukumu juu ya dola hii yalikuwa yote ni yake kwa vile ilikuwa ni yeye aliyemfanya Uthman kuwa khalifa.

Abdur Rahman alikubali kwamba alichokuwa amekifanya ni makosa, na akaongeza: “Mimi sikutegemea hali ya kufedhehesha kama hii kutoka kwa Uthman. Ametusikitisha. Na sasa Allah swt. awe ni Shahidi kwamba sitazungumza naye tena.”

Kukataa kwa Abdur Rahman kuzungumza na Uthman hakukuweza kuondoa madhara ambayo yaliyokuwa yamefanyika wala kubadili chochote kwa mtu yeyote. Lakini alishikilia “msimamo” wake na hakuzungumza na Uthman tena ili kumuonyesha jinsi alivyochukizwa na vitendo vyake (Uthman).

Amr Bin Al-Aas

Amr bin Al-Aas aliipiga Misri kwa maamuzi yake mwenyewe. Baada ya kuitwaa, aliteuli- wa na Umar kuwa gavana wa Misri. Wakati mmoja kabla ya kifo chake mwenyewe, Umar alikuwa amemtuma Abdallah bin Saad bin Abi Sarh, ndugu wa kunyonya wa Uthman, kwenda Misri kushirikiana mamlaka ya kifedha na Amr bin Al-Aas.

Wakati Umar alipokufa na Uthman akawa khalifa, Abdallah bin Saad alimuandikia kumueleza kwamba Amr bin Al-Aas alikuwa anachezea hazina ya umma. Na Uthman mara moja akamfukuza Amr, na akamfanya Abdallah kuwa gavana mpya na amiri jeshi mkuu wa jeshi lililokuwa Misri.

Baada ya kufukuzwa kwa Amr, mfalme wa Byzantine alituma kundi la wapiganaji amba- lo lilifanikiwa kuiteka Alexandria mnamo A.D. 646. Abdallah bin Saad hakuweza kulilin- da jimbo hilo, na Uthman akalazimika kumrejesha Amr kama gavana na kamanda mkuu. Amr akayashinda majeshi ya Byzantine, na akaikalia tena Alexandria. Lakini mara tu Misri ilipokuwa haina tena vikosi vya Byzantine, Uthman akamfukuza tena Amr, na akaweka mamlaka yote ya Misri kwa kaka yake wa kunyonya.

Misri ilikuwa ndio kipenzi cha kwanza cha Amr bin Al-Aas. Tamaa yake kubwa maishani ilikuwa ni kutawala Misri. Sasa akiwa amenyimwa, sio tu matunda ya kazi yake bali pia na utambulikanaji kwa utumishi wake, alirejea Madina, mwenye uchungu mkali, mwenye hasira na mtu aliyevunjika moyo.

Kwa vile pale Madina alikuwa hana chochote cha kufanya, alijushughulisha mwenyewe na adhabu kwa, na kupanga njama dhidi ya, yule mwanzilishi wa uvunjikaji moyo wake – Uthman. Wakati huyu Uthman alipouawa na waasi, yeye alijisifu waziwazi hivi: “Mimi ndio Abu Abdallah. Ninapoamua kufanya jambo, hakuna kitu kinachoweza kunizuia mimi.”

Sir John Glubb:

“Amr ibn al-Al-Aas, mtekaji wa Misri kwa mara mbili, ambaye alifukuzwa na Uthman ili kumpendelea ndugu yake wa kunyonya, alikuwa akihangaika kueneza chuki hapo Madina.”
(The Great Arab Conquests, uk.299, 1963)

“Amr ibn al-Al-Aas, mtekaji wa Misri mara mbili, alikuwa akiishi Madina tangu kufukuzwa kwake na Uthman, na alikuwa miongoni mwa wakosoaji wakali kabisa wa huyu khalifa mtu mzima.”
(The Great Arab Conquests, uk.324, 1963)

Amr ibn al-Al-Aas alikuwa na mapambano mengi makali na Uthman ndani ya Msikiti Mkuu na katika kasri la huyu Uthman. Katika moja kati ya mapambano hayo, alimtaka aombe msamaha hadharani (Atubie) kwa tabia yake isiyo na hakika katika mambo ya kiserikali.

Sir John Glubb:

“Amr ibn al-Al-Aas, wakati alipotakiwa ushauri (na Uthman), alimjibu kikatili, ‘Wewe umeutiisha umma wote kwa Bani Umayya. Wewe umepotoka, na watu vivyo hivyo wamepotoka. Ama ufanye uamuzi wa kuwa muadilifu au uiache kazi hii.”(The Great Arab Conquests, uk.300, 1967)

Amr ibn al-Al-Aas alimshutumu na kumlaani Uthman hadharani, na hakumuacha hata baba yake. Cha kushangaza ni kwamba, haukimjia kamwe kutumia mamlaka yale yale ya dola dhidi yake ambayo aliyatumia dhidi ya Abu Dharr al-Ghiffari, Ammar ibn Yasir na Abdallah ibn Mas’ud.

Alikuwa na makabiliano, sio moja, bali ni mengi, na Amr ibn al-Al-Aas, na bado, hakuwahi kumtishia kumhamisha kwenda Rabza, na hakuwahi kuwaamuru watumwa wake kumtoa nje ya Msikiti au kwenye kasri yake, na kumvunja mbavu zake.

Huenda Uthman aliona, kama mtu mwangalifu kiasi alivyokuwa yeye, kwamba mashambulizi ya maneno ambayo Amr ibn al-Al-Aas alimfanyia yeye hayakuvunja mfupa wowote hata hivyo katika mwili wake na, kwa hiyo, haikuwa lazima kumuadhibu yeye. Zaidi ya hayo, walitofautiana lakini wanatofautiana ndani ya desturi za “shirika la watu maalum” pekee ambamo wote wawili walihusika. Lakini Abu Dharr al-Ghiffari, Ammar ibn Yasir na Abdallah ibn Mas’ud, walikuwa “sio wanachama.” Kwa hiyo, sheria zile zile hazikutumi- ka kwao wao ambazo zinatumika kwa “mwanachama” kama Amr ibn Al-Aas.

Sababu Za Kuuliwa Kwa Uthman

Uthman alikuwa ni khalifa kwa miaka kumi na miwili. Ule mfumo wa madaraka aliourithi kutoka kwa Umar, ulifanya kazi vizuri kiasi kwa nusu ya kwanza ya utawala wake. Ilikuwepo amani kwa ajili yake na kwa ajili ya Waislam. Lakini katika nusu ya pili, manung’uniko yalianza kuongezeka dhidi yake, na yaliendelea kuongezeka mpaka kufikia hatua ya kuwaka moto mnamo A.D. 656 wakati kundi la watu walioghadhibika na kukasirika lilipomuua yeye ndani na kasri lake mwenyewe huko Madina.

Watu walikuwa na sababu halali za kutokuridhika kwao. Walijua kwamba viwango visivyo na idadi vya dhahabu na fedha vilikuwa vikiingia kwenye hazina kutoka majimboni lakini hawakuviona kabisa. Vyote vilipotelea kwenye makasha binafsi ya watu wa tabaka la watawala. Hili tabaka la watawala liliundwa pekee na watu wa ukoo wa Bani Umayya – ukoo ambao Uthman mwenyewe anatokana nao. Bani Umayya, chini ya Uthman, walifikia utajiri ambao hawakuutegemea japo ndotoni na kiwango cha juu kabisa cha matumizi mabaya ya madaraka. Waislam walichukia kiburi chao, majivuno na maringo yao, na ushenzi wao na mikogo yao yenye kuhamakisha ya utajiri na madaraka.

Uthman aliwafukuza magavana na makamanda wote waliokuwa wameteuliwa na Abu Bakr na Umar, na badala yao, aliwateua wale watu ambao “hati za utambulisho” pekee zilikuwa kwamba wao ni Bani Umayya. Watu huko majimboni waligumia chini ya visigi- no vya hawa magavana na makamanda wapya. Walevi wa madaraka kama walivyokuwa, maovu yao na kiburi chao hakikuwa na mipaka. Walijiona wao wenyewe kwamba wako juu na nje kabisa na upeo wa mkono wa sheria.
Malengo binafsi ya Bani Umayya yalichukua kipaumbele juu ya malengo ya umma, na “haki” yao ya unyang’anyi, ilikuwa na amri juu ya haki za umma wa Kiislam. Umma uliwajua wao kama wabinafsi wasiom- cha mungu na wanyonyaji wa kupindukia ambao walitwaa umiliki wa zana halisi ya Uislam – ile serikali ya Madina. Majimbo, kwa hiyo, yakajawa na manung’uniko na maasi.

Walezi wa awali wa Bani Umayya walikuwa ni Abu Bakr na Umar. Ilikuwa ni wote wawili hawa ambao, kama ilivyokuwa, walifungua kizibo cha chupa, lakini sasa ilionekana kwa umma kwamba hapakuwa na njia ya kumpenyeza jini kurudi tena ndani ya chupa. Uthman naye aliibadili mizania ya mgawanyo wa kisiasa kwa kuwatenganisha maveterani wawili wa vita kama Abdur Rahman bin Auf na Amr bin Al-Aas. Aliwasababishia uhasama Bani Ghiffari na washirika wao kwa kumhamisha Abu Dharr kwenda Rabza ambako baadae alifia huko. Aliwachonganisha Banu Makhzuum na washirika wao kwa kumpiga kikatili Ammar bin Yasir, na aliwafanya Bani Hudhail na Bani Zuhra kuwa maadui zake kwa kum- fanya Abdallah ibn Mas’ud kupigwa na watumwa wake.

Uthman alikuwa salama alimuradi alihamisha au aliwapiga marafiki za Mtume wa Allah swt., kama Abu Dharr al-Ghiffari, Ammar bin Yasir, na Abdallah bin Mas’ud. Hawakutokana na makabila yenye nguvu na Uthman hakuwa na chochote cha kuhofia kutoka kwao. Lakini tena akamfukuza Amr bin Al-Aas, gavana wa Misri. Kwa kufanya hivyo, aliandika hukumu yake mwenyewe ya maafa. Amr bin Al-Aas alimchakuria kiota cha manyigu juu yake. Uthman alionekana kuwa shauku ya kujipatia maadui wapya. Askari “aliyeandikishwa” upya kwenye safu za maadui zake alikuwa ni Aisha, mjane wa Mtume (s.a.w.w.). Katika nyakati za baba yake na Umar, Aisha alitunzwa kama malkia.

Lakini Uthman hakuonyesha uhusiano kama huo kwake kama walivyofanya. Yeye alipunguza hata pensheni yake, na hivyo akamuamsha ghadhabu zake. Yeye Aisha alimwita Na’athal (Myahudi wa Madina), na aliwachochea watu wazi wazi dhidi yake akisema: “Huyu Na’athal amerudia tena kwenye upagani. Muueni huyu, eh! Allah swt. Amuuwe huyu.”

R.V.C. Bodley:

“Uthman hakuwahi kuwa mtu aliyejitokeza sana wakati Muhammad alipokuwa yuko hai. Leo alionyesha kwamba hakuwa na zile sifa za wale waliomtangulia. Aliyumbishwa kirahisi na hakuwa na haya katika kubadilisha viongozi wa kijeshi na magavana kwa kuweka vipenzi wake, bila ya kujali uwezo wao. Vilevile alifanya lile kosa la kumchukiza Aisha.

Dharau yenyewe ilikuwa ni ndogo, lakini ya namna yakuweza kuamsha hisia zote za Aisha za kulipiza kisasi. Uthman aliipunguza pensheni yake ikawa ya kiwango kilekile cha wale wajane wengine!

Aisha alikuwa akijidhania yeye mwenyewe siku zote kama kipenzi cha Muhammad. Wakati wa utawala wa baba yake na wa Umar, alikuwa amechukuliwa katika hali kama ile ile ya wakati mumewe alipokuwa hai. Lakini kwa kufariki kwa watetezi wake hawa wawili, alijua kwamba ilihitajia uhodari wake wote kulinda nafasi yake. Pale, kwa hiyo, Uthman alipofanya shambulizi lake la kichini chini, Aisha aliamua kwamba huyu hakuwa mrithi anayestahili wa mume wake. Alipokwisha kulimaliza hilo, kile kilichokuwa kimebakia sasa kilikuwa ni kutafuta njia nzuri ya kumuondoa adui. Sababu au njia zilizotumika hazikuwa na maana juu ya hali hiyo. Pale Aisha alipotaka jambo lifanywe, basi lilitekelezwa bila kujali maadili. Katika suala hili Uthman alimpa Aisha kila aina ya msaada. (The Messenger – The Life of Muhammad, New York, 1946)

Madina, wakati fulani iliyokuwa alama ya uchamungu na ushikiliaji maadili, ilikuwa imebadilika. Mji wa Mtume (s.a.w.w.) umegeuka, baada ya kifo chake, kuwa ni alama ya maovu ambayo vita vya kigeni na ukabaila usiozuiliwa vinAyaleta baadaye. Lazima isije ikachukuliwa kwamba Waislam wa Madina walikubaliana na mikengeuko yote hii na kupotoka kutoka kwenye Uislam wa amuhuri. Hawakukubaliana. Lakini hawakuwa na uwezo wa kusimamisha yale matumizi mabaya ya madaraka ndani ya serikali hiyo. Walipinga lakini malalamiko yao hayakusikilizwa hata kidogo. Sauti za akina Abu Dharr al-Ghiffari, Ammar ibn Yasir na Abdallah ibn Mas’ud zilizosimama kupinga dhidi ya wimbi la kuthamini mali lilivyokuwa linatishia kuumeza Uislam, zilinyamazishwa kwa nguvu za kinyama. Wakijikuta wamekwama, masahaba waliokuwepo Madina, mwaka 654 walianzisha kampeni ya kuandika barua kwa Waislam wa kwenye majimbo, wakiwaomba wafanye uwakilishi kwa khalifa dhidi ya maovu ya Marwan na magavana wa majimbo, na kumuomba yeye awauzulu hao.
Wale Waislam wa majimboni, wenyewe wakiwa waathirika wa dhulma na vitisho, na wakiwa hawajui la kufanya, waliamua, baada ya kuandikiana barua kadhaa na masahaba hao, kutuma ujumbe kwenda Madina kuwamuhurisha manung’uniko yao kwa khalifa, na kumuomba yeye kuirekebisha hali hiyo. Uthman alijua kuhusu zile barua ambazo masahaba walikuwa wamezituma kwenye majimbo. Lakini badala ya kuchukua hatua za kunusu- ru, alifanya kitendo cha kuvunja heshima. Tabari, mwanahistoria huyu, anasema kwamba Uthman alimuandikia Muawiyyah, gavana wake wa Syria, kama ifuatavyo: “Watu wa Madina wamerudia tena kwenye ukafiri; wamevunja kiapo cha utii kwangu. Sasa hivi wanakusudia uhaini. Wewe, kwa hiyo, nitumie haraka sana hapa Madina, wale wapiganaji wakali kabisa wa Syria, juu ya wanyama wenye kasi.” (Tarikh Tabari, juz.111.)

Lakini Muawiyyah hakuwa na nia ya kumfanyia msaada Uthman. Tabari anaendelea kusema: “Pale Muawiyyah alipoipokea barua ya Uthman, aliamua kuangalia hali kama ilivyo, na alipendelea kutopingana na masahaba wa Mtume wazi wazi kwa sababu alijua kwamba walikuwa wameungana wote katika upinzani wao kwa Uthman.”

Muawiyyah alikuwa akiiangalia hali jinsi gani inavyoweza kuingia mikononi mwake. Hakuwa ni mtu ambaye anaweza kuzuiwa na aibu za kimaadili kuwapinga hao masahaba wa Mtume (s.a.w.w.). Alikuwa na uwezo lakini hakuwa tayari tu kumsaidia Uthman.

Abul Fida, mwanahistoria huyu, anasema kwamba mnamo mwaka 656 ujumbe wa watu 700 ulikuja Madina kutokea Misri, na wajumbe wa namna kama hiyo pia walikuja kutoka Kufa na Basra. Walikuja wakitaka marekebisho ya utawala wa kirasimu na usimamizi wa kibadhirifu wa fedha za umma, kuanzia Madina na kwenye majimbo yote. Kama Uthman angelikutana nao, akawasikiliza malalamiko yao, na kama angewahakikishia tu kwamba yuko katika kukubaliana nao, wangeweza kuridhika, na wangeweza kurudi majumbani kwao. Lakini kwa bahati mbaya, yeye hakufanya hivyo.

Ujumbe wa Misri ambao ulikuwa umeweka kambi kwenye viunga vya Madina, ulituma mjumbe pamoja na barua kwa Uthman, wakimuomba wakutane naye. Katika barua hiyo walikuwa wamemuomba amuondoe kaka yake wa kunyonya, Abdallah bin Saad bin Abi Sarh, kutoka kwenye nafasi yake kama gavana wa Misri, na kuanzisha mabadiliko fulani ya kiutawala. Lakini badala ya kuyafikiria maombi yao, Uthman aliwaamuru watumwa wake kuutoa nje ule ujumbe wa Misri.

Wamisri hao ndipo wakaingia mjini, na waliwaambia wale watu wengine kile Uthman alichokifanya. Wale wajumbe wa Kufa na Basra walikuwa tayari wako Madina, na wakatamka kuwaunga mkono kwao Wamisri. Makundi yote matatu ya uwakilishi yaliweka kambi katika sehemu ambayo wanaiona kasri ya khalifa. Katika Ijumaa iliyofuata, Uthman aliongoza Swala ya jamaa, na akaisoma khutba. Asingeweza kuwa hovyo zaidi na asiye na busara hivyo. Akiwa amesimama kwenye minmbari, na akiongea na wale wawakilishi kutoka Misri na Iraq, alisema:

“Mtume wa Allah swt. alikwisha tabiri kwamba wafitini, siku moja watakuja kwenye mji wake kuvuruga amani ya mji huo. Aliwalaani wote hao, na sasa mnaona mna- chokifanya.” Ile hadhara ilionyesha kukasirishwa na matamshi haya, na kukawa na ghasia kubwa mle msikitini. Mtu mmoja akamrushia jiwe Uthman ambalo lilimpata usoni; akaanguka kutoka kwenye minmbari, na akabebwa kutolewa mle msikitini na kupelekwa kwenye kasri yake.

Baada ya tukio hili, Uthman alikuwa kwenye hali ya kuzingirwa ndani ya kasri yake. Lakini alikuwa akiweza kwenda msikitini, na bado alikuwa anaziongoza Swala. Siku chache baadae, hata hivyo, Wamisri na Wairaqi walimkataza kuingia mle msikitini labda kama angewasikiliza kile walichokuwa wakiseme, na walimteua mtu mmoja aitwaye Ghafiki, mjumbe wa uwakilishi kutoka Misri, kuwaongoza katika Swala.

Katika wasiwasi wake, Uthman alitafuta msaada wa Ali katika kuwatawanya wazingi- raji hao. Ali akamwambia:

“Malalamiko yao ni ya halali, na madai yao yana mantiki. Hawatatawanyika tu eti kwa sababu ninawaomba watawanyike. Wao watatawanyika tu kama utawapa ahadi yako ya kukubali madai yao.”

Uthman Akasema:

“Ninakupa wewe mamlaka ya kujadiliana nao. Yoyote yanayoweza kuwa masharti yako ya makubaliano nao, mimi nitayakubali.”

Ali alikutana na viongozi wa ujumbe wa Misri na akazungumza nao. Walikubali kurudi Misri kama Uthman angemrudisha ndugu yake wa kunyonya, maarufu Abdallah bin Saad, na kama, badala yake, amteuwe Muhammad ibn Abu Bakr kama gavana mpya. Ali alimwambia Uthman kile ambacho angepaswa kukifanya kama alitaka Wamisri hao waon- doke Madina.

Uthman alikubali kumteua Muhammad ibn Abi Bakr kama gavana mpya wa Misri. Hili liliwaridhisha Wamisri. Muhammad ibn Abu Bakr aliondoka Madina kwenda Misri kusimamia kazi zake mpya, na wengi wa Wamisri hao walifuatana naye. Uthman aliweza kwa mara nyingine tena kuingia Msikitini na kuwaongoza Waislam katika Swala. Kadhia hiyo, inavyoonekana, ilifungwa.

Lakini kwa bahati mbaya haikufungwa. Mtu nafsi ya Uthman, Marwan, aliifufua tena, kama ndondocha. Aliposikia kwamba Wamisri wameondoka Madina pamoja na gavana wa chaguo lao wenyewe, alimpa Uthman ushauri ufuatao:

“Baadhi ya Wamisri wameondoka Madina lakini wale waliokuja kutoka kwenye majimbo mengine, bado wangali wapo hapa. Watu wa mfano wa Wamisri watawahimiza na wao pia kutoa madai magumu.

Ili kulizuia hili lisije likatokea, ni lazima utoe hotuba ndani ya msikiti ukisema “Wamisri walikuwa wamesikia uvumi tu nchini mwao. Walipokuja Madina, waligundua kwamba yale yote waliyokuwa wameyasikia, hayakuwa chochote ila ni uongo tu. Waliridhika na wakarudi majumbani kwao. Sasa na ninyi wengine pia mnapaswa kuondoka Madina, na kurudi majumbani kwenu.”

Uthman hakutaka kusema uongo usio na haya kama huo lakini Marwan alikuwa na uwezo wa kumfanya yeye afanye lolote. Baada ya kusita kwa muda kidogo, alikubali. Akaongoza Swala, na baada ya hotuba akasema: “Enyi Waislam! Wamisri walikuwa wamesikia habari za upotofu kuhusu khalifa wao, na walikuja Madina kuzithibitisha. Hapa waligundua kwamba yale yote waliyokuwa wameyasikia, yalikuwa yote ni uongo. Wao, kwa hiyo, waliridhika na wamerudi Misri. Sasa na ninyi wengine pia mnapaswa kurudi majumbani kwenu.” (Ta’arikh Tabari, Juz.111)

Maneno haya yalipotoka tu kinywani mwa Uthman vurumai likazuka mle Msikitini. Kila mmoja akaanza kumpigia mayowe: “Uthman, tubia! Uthman tubia! Unaongopa. Muogope Allah. Unasema uongo ndani ya Nyumba ya Allah swt. Mwenyewe, na katika mimbari ya Mtume Wake.”

Uthman alipatwa na hofu, na kwa kutokujua afanye nini, ilimbidi “kutubia.” Alimuomba Allah swt. amsamehe dhambi yake, na kisha akaenda nyumbani.

Ali alishangazwa kupita kiasi na kugeuka kwa Uthman, na kukosa haya kwake katika kutoa maelezo ya uongo ndani ya Msikiti. Hata hivyo, alimtembelea mzee huyu tena na akamkemea kwa kile alichokuwa amekifanya. Uthman alimuomba yeye kuingilia kati tena, ya yeye na Waislam kwa niaba yake.

Ali alimwambia kwamba yeye (Uthman) angeweza bado, kama angetaka, kuipata imani na heshima ya Waislam kama angeyakubali makosa yake, na kama kwa unyofu kabisa angeyaombea msamaha.

Yeye pia alimuonya kwamba kama hatafanya hivyo, basi wale wageni waliokuwa wamo mle mjini, wanaweza wakamuweka kizuizini katika kasri lake, na kama wakifanya hivyo, basi yeye Ali anaweza kushindwa kuwasuluhisha.

Uthman, katika hali ya taadibu, alimhakikishia Ali kwamba yeye kwa hakika atafanya kama alivyomshauri. Ali naye, kwa upande wake, akawahakikishia wale Wairaqi, Wamisri na Waislam wengine kwamba khalifa atayakubali madai yao yote, na akawakumbusha kwamba wao pia walikuwa na wajibu, kama vile kumheshimu yeye (khalifa), kumtii na kumsaidia yeye.

Katika siku iliyofuatia, Uthman aliingia ndani ya Msikiti, akayakiri makosa yake, akaomba msamaha na baraka kutoka kwa Allah swt. akidhamiria kutokurudia makosa hayo, na akaahidi kuchukua hatua za haraka juu ya madai ya Waislam ya mabadiliko ndani ya serikali.

Ile hadhira ilihuzunishwa sana na kutubia kwa khalifa huyu mtu mzima, na kwa uhakikisho wake, na machozi mengi yalimwagika kwa pande zote kama ishara ya “mabadiliko ya Moyo.”

Ilionyesha kana kwamba yale machozi yalikuwa yamesafisha chuki zote, kinyongo na uchungu wa wote waliohusika. Kwa juhudi za Ali, suluhisho, inavyoonekana, lilipatikana, na lilikuwa ni muujiza. Lakini kama ilivyotokea, ulikuwa ni muujiza uliodumu kwa muda mfupi sana.

Uthman aliondoka pale Msikitini pamoja na maazimio mengi ya kiuchamungu. Lakini alipoingia kwenye kasri yake, alimkuta Marwan, mpangaji sera wake mkuu, akimsubiria ampatie ushauri mpya. Lakini kabla hajaweza kusema lolote, mkewe Uthman, Naila, ambaye pia alikuwepo, alimzuia yeye, na mabishano yafuatayo yalitokea baina yao:

Naila: Tafadhali, wewe sasa ufunge mdomo wako baada ya madhara yote ambayo umekwisha yafanya. Kama hukufanya hivyo, bila shaka utasababisha kuangamia kwa mzee huyu –Uthman. Wewe kwa upotovu wako, unamsukumizia kwenye ukingo wa shimo la kifo.

Marwan: Wewe ni nani kuingilia kwenye mambo haya? Umesahau kwamba wewe ni binti ya mtu ambaye hakujua hata namna ya kuchukua udhu kwa ajili ya Swala?

Naila: Wewe ni muongo uliyekamilika kabisa. Kabla ya kumtaja baba yangu, ulipaswa kukumbuka
kwamba wewe na baba yako ni watu mliolaaniwa na Allah swt. na Mtume Wake (s.a.w.w.).
Kama nisingekuwa ninajizuia kwa sababu ya huyu mzee (Uthman), ningelikufundisha adabu.

Kisha Naila akamgeukia mumewe, na akamwambia: “Usimsikilize mtu mjinga na fedhuli huyu. Yeye ni nani? Ni nani anayemjali? Kama unataka usalama wako mwenyewe, basi tekeleza ushauri wa Ali. Wewe huoni ni sifa na umaarufu kiasi gani alionao miongoni mwa Waislam?”

Huu ulikuwa ni ushauri wa busara kabisa ambao Uthman aliwahi kuupata kamwe kuto- ka kwa ndugu yoyote wa familia yake mwenyewe lakini hakuukubali. Naila ndipo akaondoka mbele ya mume wake. Mara tu alipokuwa ametoweka machoni pao, Marwan akamwambia Uthman:

“Umefanya kosa kubwa sana mle Msikitini kwa kukubali makosa yako, na kwa ‘kutubia’ hadharani. Kukubali madhambi yako kumeyatoa makundi kutoka kule Msikitini na kuyaleta langoni mwa nyumba yako. Wapo hapa tu kwa sababu wameuona udhaifu wako. Kama ungelikuwa ‘imara’ juu yao, wasingethubutu kuja hapa. Njia pekee ya kuwashughulikia hawa, na kuwaonyesha madaraka na mamlaka yako, ni kuwa ‘imara’ juu yao.”

Kundi la Waislam, lilikuwa kwa kweli limekusanyika nje ya kasri la khalifa. Lakini lilikuwa ni kundi la amani. Waislam wengi kutoka nje na ndani ya mji walikuwa wamekusanyika wakitegemea kusikia matangazo yoyote muhimu kuhusiana na yale mabadiliko ya sera na utawala. Uthman alipaswa atoke kwenda kuwapokea. Lakini hakutoka. Badala yake, alimpa Marwan ruhusa yake kwenda kuonana nao ili kuwavutia wao hao kwa “uimara.” Wake.

Wazo la Marwan la kuwa imara kwa Waislam lilikuwa ni kutumia nguvu, lugha ya matusi na vitisho. Pamoja na yale mamlaka mapya ya “kufanya apendavyo” kutoka kwa Uthman, alitoka nje, na akilikabili lile kundi ambalo lilikuwa la amani na la kirafiki, alisema: “Kwa nini mmekusanyika hapa? Madhumuni yenu ni nini? Je, mmekuja kutushambulia au kutuibia au kutupora sisi hapa? Kama hivyo ndivyo, basi sikilizeni hili kwa makini.

Ninyi hamtafanikiwa. Hamuwezi kutupokonya madaraka na mamlaka kuto- ka mikononi mwetu. Hatutatishiwa na ninyi au na mtu mwingine yoyote yule. Sasa ondokeni hapa. Allah swt. awalaani ninyi.”

Safari hii Uthman na Marwan walikuwa wamevuka mahali ambapo walikuwa hawawezi kurudi nyuma tena!

Waislam walipigwa na butwaa kwa mshituko na chukizo kwa ufidhuli wa mkwe wake Uthman. Lakini hawakukaa kufanya mzaha naye. Badala yake, walikwenda kuonana na Ali na kumuelezea yeye maana halisi ya “hotuba” ya Marwan.

Ali alishikwa na mshangao kusikia hadithi hii. Hivi kulikuwa kuna kitu chochote ambacho angeweza kukifanya ili kuzuia huo unyumbulikaji wa hali? Alilitafakari swali hilo, na kisha akamwendea Uthman na kumwambia:

“Hivi huu ndio ukarimu ulioutoa kwa ndugu zako Waislam? Kama umekosa kabisa busara mbele zao, ulipaswa, angalau, kuhofia ghadhabu ya Allah swt. Katika shauku yako ya kumlinda kafiri na muongo, umeipoteza hofu hiyo pia, na sasa unaweza kusema uongo hadharani na Msikitini, na unaweza kuvunja viapo vyenye taadhima bila ya kufumba jicho. Umemruhusu Marwan akuelekezee wewe kokote anakotaka. Kumbuka, atakuingiza kwenye shimo la udhalimu kama hajafanya hivyo tayari, na wewe hutaweza kujinasua mwenyewe kamwe humo. Sasa sitajaribu kutafakari kati yako na Waislam. Sitakuwa na haja na mambo yako. Hii ni safari yangu ya mwisho kukutembelea. Wewe fanya unavyotaka. Lakini kama bado utanihitaji mimi, basi kwanza itakubidi uachane na Marwan. Mimi nitajitenga nawe muda utakapokuwa Marwan anasimama kati yako na mimi.”

Ali aliondoka kwenye kasri la Uthman kwa dhamira ya kutorudi tena hapo. Wakati Naila, mke wake Uthman, alipomuona anaondoka, alifadhaika sana. Matukio yamethibitisha kwamba yeye alikuwa na uamuzi mzuri kuliko wengi wa wale waliokuwa karibu na Uthman. Ingawa ushauri wake haukukubaliwa, alikuwa bado na shauku ya kuokoa kila ambacho angeweza, na akamwambia mume wake:

“Ni mara ngapi nimekuambia uachane na Marwan. Yeye ni laana, mzigo juu yako. Unajua kwamba ni mtu muflisi wa sifa nzuri, ni muflisi wa maadili, na ni muflisi wa busara. Hali ni ya hatari sana, na inazidi kuwa mbaya zaidi. Umepoteza imani yako kwa kusaliti uaminifu wa Waislam. Sasa kama kuna mtu yeyote ambaye bado anaweza kukuokoa wewe, mtu huyo ni Ali. Kama yeye huyo hatakusaidia, basi wewe umepotea.”

Uthman kama alivyokuwa amevurugwa na tukio hili, alitambua kwamba kile mke wake alichokuwa amemwambia yeye, kilikuwa ndio ukweli wa hali ya juu kabisa. Yeye, kwa hiyo, alituma mjumbe kwenda kumuomba Ali aje. Lakini Ali alikataa kwenda ambapo Uthman aliamua kwenda yeye mwenyewe kumuona Ali. Ili asionwe na mtu yeyote, basi alikwenda wakati wa usiku.

Mbele ya Ali, khalifa huyu mzee aliielezea hali nzima ya kutoweza kujisaidia mwenyewe, na akaomba radhi juu ya makosa yake mengi, na akamhakikishia kwamba atakuwa, huko baadae, akishika ahadi yake, ikiwa yeye Ali atapatanisha kati yake (Uthman) na Waislam. Ali, hata hivyo, akasema:

“Unasimama kwenye mimbari ya Mtume wa Allah swt., na kusema maneno ya uongo. Unawapa Waislam kiapo chako cha ahadi yako ya kuingia kwenye haki, na kisha unaivunja. Sasa kila mtu ameona jinsi unavyoheshimu ahadi zako. Kama Waislam wanataka kukuona wewe na kuzungumza nawe, Marwan anawatukana na kuwalaani. Unanitegemeaje mimi nikuamini wewe sasa hivi ukiwa na rekodi kama uliyonayo? Sikubali wajibu wowote juu ya matendo yako yoyote. Njia zipo, na uamauzi ni wako. Epukana na Marwan.

Kama huwezi kufanya hivyo, basi usitegemee chochote kutoka kwangu. Ukiwa na Marwan karibu yako, na kama mshauri wako mkuu, hakuna chochote ninachoweza kukufanyia hata hivyo.”

Uthman alimpenda sana mkwe wake kiasi cha kushindwa kutengana naye. Masharti ya Ali kwa hiyo, yalikuwa kwake hayakubaliki, na akarudi nyumbani. (Ali hakuwa akimwambia Uthman kwamba amhamishe Marwan kutoka Madina kama Mtume wa Allah swt. alivyokuwa amefanya; yeye alikuwa akimwambia tu kwamba huyu asiwe anampotosha.)

Wakati Marwan alipokuwa anapambana na Waislam hapo Madina, Uthman alikuwa anaandika barua kwa magavana wake wote akiwataka watume vikosi vyao Madina ili aweze “kuwatia adabu” wale “waasi.” Matumaini yake makubwa yalikuwa kwa Mu’awiyah, na kwake yeye aliandika barua nyingi, akimsisitiza alete wapiganaji huko Madina au awatume pamoja na maafisa wake waaminifu. Lakini sio Mu’awiyah wala yeyote mwingine kati ya magavana wake aliyeitikia ishara zake za wasiwasi.

Siku moja mtu mmoja alimwona Uthman nje ya kasri lake, na akatoa maneno: “Jinsi gani ninavyotamani kwamba ningeweza kukuburuza wewe na wale walio karibu yako kwenye takataka.” Uthman akasema kwamba wale walio karibu naye, hawakuwa wengineo mbali na masahaba wa Mtume wa Allah swt. Alijibu kwa ukali kwamba hao “masahaba” lazima wawe Hakam, Marwan, Walid bin Aqaba, Said bin Al-Aas, Abdallah bin Saad bin Abi Sahr, na waliobaki wa kundi hilo. Uthman akanong’ona: “Ngoja hilo jeshi lije, na ndipo nitakuadhibu wewe.”

Lakini jeshi hilo halikuja kamwe. Mu’awiyah alikawia na kuwaza kwamba kama kulikuwa na vurugu huko Madina, atatumia hila ndani yake, na kama ikiwezekana, ataondoka na ukhalifa wenyewe.

Wakati mambo haya yalipokuwa yanatokea huko Madina, habari mbaya zilikuja kutoka kaskazini. Muhammad ibn Abu Bakr, gavana mteule wa Misri, alikuwa amewasili huko Elath kwenye mkono wa Bahari Nyekundu unaoitwa Ghuba ya Aqaba, na alikuwa anakaribia kuingia Misri. Alikuwa ameweka kambi hapo Elath wakati watu fulani wa msafara wake walipomuona mpanda ngamia mpweke akija kutoka Madina. Wakamsimamisha ili kumsaili, na walipoona majibu yake ni ya kukwepa, walimpekua. Ukaguzi mrefu wa mwili wake na mizigo ulizaa barua iliyokuwa imefichwa katika kijibomba cha risasi chini ya mfuko wake wa vikorokoro. Barua ilikuwa imeandikwa kwa Abdallah bin Saad bin Abi Sarh, gavana wa Misri, na ilikuwa na muhuri wa khalifa mweyewe. Waliileta ile barua na mbeba barua mbele ya Muhammad ibn Abi Bakr. Yeye akauvunja ule muhuri, na alishtushwa kusoma ujumbe ufuatao:

“Wakati Muhammad ibn Abi Bakr na watu wa kundi lake watakapowasili hapo Misri, wakamate, na uwauwe wote, na uendelee na kazi zako kama gavana wa Misri.”

(Kama ilivyoelezwa kabla, Abdallah bin Saad ibn Abi Sarh hakuwepo huko Misri kwa wakati huu; alikuwa yuko Palestina.)

Mwanzoni Muhammad hakuweza kuyaamini macho yake mwenyewe. Uthman anawezaje kumuagiza gavana wake amuue yeye na wenziwe? Aliisoma na kuisoma tena na tena barua ile mpaka maana yake ilipoanza kuzama akilini mwake.

Muhammad aliamua kurudi Madina. Huko Madina, aliingia ndani ya Msikiti wa Mtume (s.a.w.w.), na akaiweka ile barua mbele ya masahaba kwa ajili ya uchunguzi makini. Baadhi yao na watu wa kundi la Muhammad, walikwenda kwa Uthman, kumuonyesha ile barua, na mabishano haya yakatokea kati yao:

Masahaba: Je, wewe uliandika barua hii?
Uthman: Hapana.
Masahaba: Ni muhuri wa nani huu juu ya barua hii?
Uthman: Ni wangu.
Masahaba: Huu ni mwandiko wa nani?
Uthman: Ni wa mwandishi (katibu) wangu.
Masahaba: Huyu mpeleka barua hii ni mtumwa wa nani?
Uthman: Ni wangu
Masahaba: Ni nani aliyemtuma kwenda Misri?
Uthman: Mimi sijui.

Masahaba: Muhuri juu ya barua ni wako; mwandiko ni wa mwandishi wako; mtumwa kenda Misri. Kama yote haya huyatambui kiasi hicho, basi itakuwa kote, kwa manufaa yako wewe, kwamba aliyeibeba ni wako, na kisha hujui ni nani aliyemtuma huko, na kwa manufaa ya umma wa Waislam, kwamba ujiuzulu kwenye ukhalifa. Acha mtu mwingine, mwangalifu na mwenye kufaa kwa kazi hiyo, asimamie serikali ya Waislam.

Uthman: Ukhalifa ni joho ambalo Allah swt. amenipa mimi, nami siwezi kulivua kwa hali yoyote ile. Ninachoweza kukifanya, hata hivyo, ni ‘kutubia.’

Masahaba: Kutubia kwako hakuwezi kutughilibu sisi tena. Tayari umekwisha kutubia mara nyingi. Wewe, kwa hiyo, ondoka na utoe nafasi kwa mtu mwingine bora zaidi yako kwa kazi hii kubwa ya Ukhalifa.

Unasema kwamba humjui aliyetuma barua hii. Kama unasema kweli, basi haiwezi kuwa mtu mwingine yeyote mbali na mkwe wako ambaye ndiye mwandishi wako. Yeye aliiandika na kuituma barua hiyo. Yeye ndiye mhalifu halisi ambaye alikuwa achukuwe maisha ya Waislam wengi wasio na hatia. Sasa kama wewe ni mkweli, basi mkabidhi yeye kwetu sisi ili tuweze kumchunguza yeye, na tuthibitishe haki.

Uthman: Siwezi kumkabidhi Marwan kwenu ninyi.

Masahaba: Sisi basi tunaelewa kwamba wewe ni mshiriki katika jinai hiyo, na wewe pia ulitaka Waislam wasio na hatia wauawe katika kuwasili kwao huko Misri kwa sababu tu kwamba wewe na Marwan hamuwapendi watu hao.

Masahaba hao ndipo wakaenda Msikitini kuwaeleza wale Wairaqi na Wamisri matokeo ya mazungumzo yao pamoja na khalifa. Wamisri, pale pale, wakaizingira kasri ya Uthman. Wajumbe waliokuja kutoka Kufa na Basra nao pia wakapigilia mahema yao kuizunguka ile kasri ya khalifa, na wakatangaza kwamba yeye atakuwa mfungwa wao mpaka atakapomtoa Marwan kwao kwa ajili ya kushtakiwa na kuhukumiwa.

Wakati wa karantini hiyo, maji ya kunywa yakaisha ndani ya kasri. Uthman aliomba kwa baadhi ya masahaba kuletewa maji lakini waliyapuuza maombi yake. Mwishowe, alituma ujumbe kwa Ali, nay eye Ali akatuma maji na walinzi wenye silaha. Walinzi hao iliwabidi kuingia kwa nguvu ndani ya kasri kufikisha kimiminika hiki chenye kuleta na chenye kuokoa uhai.

Uthman bado alikuwa na matumaini kwamba mmoja wa magavana wake, hususan Mu’awiyah, angetuma vikosi vyake ambavyo vitateketeza kabisa waasi hawa wakaaidi na wenye kujiamini mno. Waasi wenyewe, kwa wakati huo, walikuwa wakikaza kitanzi chao kwenye shingo yake.

Mauaji Ya Uthman

Matukio madogo madogo mengi yalitokea wakati wa kuzingirwa kwa kasri la Uthman. Kulikuwa na nyakati ambapo aliona kwa macho yake mwenyewe baadhi ya masahaba wakuu wa Mtume miongoni mwa wazingiraji wakiwasisitiza wao kuweka mkazo wao juu ya wale waliozingirwa.

Siku moja ilitokea kwa Ibn Ayyadh fulani, mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kusuluhisha kati ya wazingiraji na wale waliozingirwa katika jaribio la kurudisha amani hapo Madina. Alikuja kwenye lango la kasri na kumwita Uthman kwa jina lake.

Uthman alichungulia kwenye dirisha lililokuwa juu, na akauitikia mwito. Ibn Ayyadh alimuomba ajiuzulu na hivyo kumaliza ile hali ya vurugu ndani ya mji, na pia kuwaokoa Waislam kutokana na uwezekano wa umwagaji damu. Alikuwa hajamaliza maombi yake bado wakati mmoja wa watupa mishale wa Uthman alipomuua kwa mshale.

Ukelele wa kuonyesha uchungu ulitoka kwa wazingiraji. Walimuomba Uthman amsalimishe huyo muuaji kwao lakini akasema: “Nitawezaje kusalimisha wasaidizi na walinzi wangu mwenyewe kwenu ili muwaue? Haiwezekani kamwe.”

Jibu la Uthman lilikuwa na athari za cheche kwenye baruti kavu. Lile kundi lilisonga mbele kutaka kuingia ndani ya kasri lile na kumkamata yule muuaji wa Ibn Ayyadh. Marwan, Said bin Al-Aas, Mughira bin Khins, na mamluki wa Uthman walijaribu kuilin- da ile kasri kutoka kwa ndani, na kuwarudisha wale wazingiraji.

Hawa wazingiraji walishambulia na malango mengine pia lakini wakakuta walinzi kila kwenye lango mojawapo.
Wakati mapambano haya yakiendelea kwenye malango ya kasri la Uthman, Ansari mmoja, bwana fulani Amr bin Hazm, aliwaita wale wazingiraji kwenye nyumba yake ambayo ilikuwa inapakana na nyumba ya Uthman. Waliingia nyumbani kwake, wakapanda juu, na kutokea huko juu wakashukia kwenye nyumba ya Uthman na panga zikiwa zimechomolewa. Palikuwa na mapigano madogo na wale mamluki ambao baadhi yao waliuawa lakini wale wa Bani Umayya wote – Marwan, Said bin Al-Aas na Mughira bin Khins miongoni mwao – walifanikiwa kutoroka kupitia mlango wa siri.

Marwan anasemekana kuwa alijeruhiwa lakini akapona baadae. Katika ghasia hizo mtu mmoja akamuua Uthman. Mke wake, Naila, anasemekana kunyanyua mkono wake kumlinda kutokana na upanga, na vidole vyake vilifyekwa katika jaribio hilo.

Uthman aliuawa ndani ya kasri lake, akiwa ametelekezwa na Bani Umayya. Miaka kumi na mbili baada ya kuchaguliwa au kuteuliwa kwake kama khalifa. Ukhalifa wake ukawa shaghala baghala; watumishi wake wakaangamizwa; matumaini yake yakaingia shaka, msimamo na uwezo vikapinduliwa.

Uthman alikuwa na umri wa miaka 84 wakati wa kifo chake. Alikuwa ameibomoa ile nyumba iliyojengwa kwa harubu nyingi na Abu Bakr, Umar na Abdur Rahman ibn Auf. Alishindwa kuonyesha kwa kusadikisha hasa sifa za uongozi, uwezo na msukumo muhimu kwa khalifa. Alikuwa amekwishaangukia kwenye uzulufu na alikuwa amepoteza njia yake.

Uthman alibakia kuwa mfungwa kwenye kasri yake kwa muda wa siku 49. Alimsihi sana Mu’awiyah aje Madina na ayaokoe maisha yake. Lakini Mu’awiya hakuwa na “jibu” kwa maombi yake – kimyaaa! Kwa kukisia kutokana na kimya chake cha makusudi, inaonekana kwamba Mu’awiyah hakuwa akimjali hata kidogo Uthman. Inashangaza kwamba wapenzi wengi wa Uthman wanamlaumu Ali kwa “kutokuyaokoa” maisha ya Uthman ingawaje yeye Ali hakuwa na njia yoyote ya kufanya hivyo; lakini wanafumbia macho kutojali kwa Mu’awiyah juu yake (Uthman) ingawa alikuwa na kila namna ya uwezo wa kumuokoa. Kikosi kidogo cha jeshi lake, kama angelikipeleka Madina, kingeweza kuwashinda au kuwaua wale waasi wote lakini hakufanya hivyo!

Amr bin Al-Aas alikuwa ni mmoja wa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.). Uthman alimfukuza mara mbili akiwa kama gavana wa Misri. Hakumsamehe kamwe Uthman kwa kumfukuza kwake; alikuwa na usongo juu yake. Inawezekana kabisa kwamba alikuwa ni yeye aliyepanga mauaji ya Uthman, na hakufanya angalau jitijada japo kidogo ya kuficha dhamira yake. Lakini alikuwa amejawa na hila na ujanja, na aliweza kukwepa ukosoaji wa historia.

Mawakala wengine wawili – wachochezi katika mauaji ya Uthman walikuwa ni Talha na Zubeir. Waliuwasha moto wa ghadhabu na chuki za umma dhidi ya Uthman kama vile alivyofanya Amr bin Al-Aas. Wote hao waliamini, kama vile Amr bin Al-Aas na Mu’awiyah walivyoamini, kwamba hawakuwa na chochote cha kupoteza katika kuvunjika kwa sheria na amani, na kuna takriban kila kitu cha kupatikana. Wote walikuwa ni nyongeza kwenye uhalifu dhidi ya Uthman ama kwa ushiriki wa moja kwa moja au kwa kuridhia na kutojali kwao.

Wakati Uthman alipouawa, Madina ilikuwa imejaa wanawake na wanaume mashuhuri kabisa. Miongoni mwao walikuwepo wajane wa Mtume (s.a.w.w.) isipokuwa Aisha ambaye alikuwa yuko Makka; Saad bin Abi Waqqas, Abdallah bin Umar bin al-Khattab; Muhajirina na Ansari; wakongwe wa vita vya Badr na Uhud; na wengi wa wale masahaba ambao walikula kiapo cha Mti kule Hudaibiyya. Lakini wote isipokuwa Ali tu, hakuna hata mmoja kati yao, aliyeonyesha shauku japo kidogo tu ya kuokoa maisha ya khalifa.

Hakuna asichokifanya Ali kumuokoa Uthman lakini sio yeye au mtu mwingine yeyote ambaye angeweza kumuokoa mtu ambaye alikuwa ameamua kujiangamiza mwenyewe. Marwan alizuia juhudi zake zote Ali, za kugeuza kule kuteketea kwa ukhalifa, na akak- wamisha majaribio yake yote ya kusuluhisha kati ya khalifa na Waislam.Yeye Marwan alisimama kama kikwazo kigumu kisichoshindika kati yao.

Uthman hakusikiliza ama zile nasaha za mke wake mwenyewe, Naila, wala maonyo na ushauri wa Ali, bali alishikilia kuchokoza balaa. Kwake yeye, kupayuka kwa Marwan kulikuwa ni sawa na ufunuo wenyewe, na kwake yeye peke yake, Uthman alitoa uaminifu wake wa kwanza.

Miongoni mwa wafuasi wake, Uthman aliweza kuwategemea watu wawili tu – Marwan na Saad bin Al-Aas – wote hao wakiwa ni wale waliolaaniwa na Mtume wa Allah swt. Mafaqih na wanatheologia wa Sunni wanaweka umuhimu mkubwa kwenye utaratibu wa makubaliano. Hapa kulikuwepo na makubaliano ya Masahaba wa Mtume (s.a.w.w) katika kuzuia uungaji mkono wao kwa Uthman, na katika kumpinga yeye. Walijizuia msaada wao kwake, na walimpinga yeye takriban wote kwa pamoja. Walimtelekeza, auwawe, kwa maneno ya Umar, na “mbwa mwitu wa Waarabu.” Nani alikuwa sahihi na nani alikuwa amekosea? Ni swali la mafaqih na wanatheologia wa Sunni kulijibu.

Matokeo Ya Kuuawa Kwa Uthman

Wakati Ali alipopanda kwenye kiti cha ukhalifa, aliwakuta watu wa Madina wamegawanyika makundi mawili. Moja ya makundi haya lilikuwa likipiga makelele kutaka kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman. Na lile kundi jingine liliamini kwamba Uthman amelipa fidia tu kwa ajili ya vitendo vyake visivyo na busara, na suala la kutaka kisasi kwa ajili ya damu yake, kwa hiyo, halikuwa na lazima. Vyovyote vile ambavyo Ali angefanya, ilikuwa haiepukiki kwamba moja ya makundi haya litafanya uasi dhidi ya madaraka yake.

Serikali hii mpya ilikuwa inayumba sana na Ali alikuwa anajitahidi kuiimarisha wakati moja ya haya makundi mawili lilipoanza kumlazimisha awaadhibu wauaji wa Uthman.

Akawaambia: “Si kama sitambui ile haja ya kuwaadhibu wauaji wa Uthman. Lakini je, tunayo nguvu ya kufanya hivyo? Kwa wakati huu, ni wao ndio wenye nguvu. Wanaweza kutuamuru sisi; na sisi hatuwezi kuwaamuru wao. Kama wakitaka, wanaweza kutudhuru, na sisi hatuwezi kuwafanyia madhara yoyote. Je mnaweza kupen- dekeza njia yoyote ambayo tunaweza kuwashinda au kuwazuia wao?”

Madina, kwa wakati huu kwa kweli, ilikuwa kwenye mikono ya lile kundi ambalo lilimpinga Uthman – wale waasi. Ni amri yao iliyokuwa inatembea hapo Madina, na hakuna mtu aliyethubutu kuwapinga. Ikiwa Ali ataamua kuweka adhabu juu yao, ilikuwa inawezekana kabisa kwamba wangempinga kwa nguvu ya silaha. Walikuwa wanazitambua nguvu zao wenyewe, na udhaifu wa serikali ya Madina.

Kama kile kikundi cha kwanza, yaani wanaotaka kulipiza kisasi kingegundua udhaifu wowote kwa wale waasi, basi kingewapinga wao wakati ule wa kuzingirwa kwa kasri la Uthman. Lakini hakikufanya hivyo. Wakati wa karantini, viongzi wake walijificha. Lakini mara tu Ali alipochaguliwa khalifa, wakajitokeza, na wakaanza kudai hatua kutoka kwake, ya kuwakamata wale waasi waliokuwa wamemuua Uthman.

Viongozi wa kile kikundi cha kwanza waliamua kumpinga Ali. Ulikuwa ni ushauri wa Aisha, ambaye alikuwa ni mmoja wao, na ambaye tayari alikuwa Makka, kwamba lazima waishambulie Madina kwa sababa muuaji au wauaji wa Uthman wote walikuwepo pale. Lakini Talha na Zubeir, wale viongozi wengine wawili, ambao walikuwa wamemwambia Ali kwamba walikuwa wanakwenda Makka kufanya Umra (hijja ndogo), hawakukubaliana naye, na wakasema: “Ewe umm-ul-mu’min! Sahau Madina. Jeshi letu haliwezi kupigana dhidi ya waasi walioko pale. Inatupasa sisi, kwa hiyo, twende zetu Basra.” (Tabari, Historia, juz.111)

Aisha, Talha, na Zubeir, viongozi wa kile kikundi cha kwanza, walikuwa na jeshi; walikuwa na silaha na walikuwa na pesa, na bado walikwepa kushambulia Madina kwa sababu walikosa nguvu ya kuwashinda waasi hao. Kama hawakuweza kupigana na waasi hao ingawa walikuwa na jeshi, angewezaje Ali, ambaye hakuwa na jeshi, kupigana dhidi yao?

Kama Aisha, Talha na Zubeir kweli walitaka kulipa kisasi, walipaswa kushambulia Madina badala ya kwenda mamia ya maili kuvuka jangwa hadi Basra.

Lakini waliweza kuona kwamba waasi hao walikuwa wengi tu kiasi cha kutoweza kuwaadhibu. Watu wa Madina, wa Misri, wa Kufa, na wa Basra, walikuwa wote wamehusika na kifo cha Uthman, moja kwa moja au kwa namna nyingine.Walikuwepo wale masahaba ambao waliandika barua kwa viongozi wa waasi, na kuwakaribisha Madina, na kuna wale Muhajirina na Ansari waliojitolea uungaji mkono wao kwao (hao waasi). Bila kuwaunga mkono kwao kwa kimya kimya, waasi hawa wasingeweza kamwe kuthubutu kumuua khalifa aliyekuwa madarakani kwenye nyumba yake mwenyewe.

Kulikuwako na nji mbili za kuwaadhibu hao wauaji wa Uthman. Moja ilikuwa ni kumuua kila mtu aliyeshiriki, moja kwa moja au kwa namna nyingine, katika mauaji yake bila ya kujali alikuwa ni nani – Muhajir, Ansari, Mmisri au Muiraqi. Hii ni wazi kabisa ilikuwa haiwezekani. Lakini kama ingewezekana, basi Dola lisingeua maelfu ya watu kwa kisasi cha kuuawa kwa mtu mmoja tu.

Njia nyingine ilikuwa ni kuyachunguza mauaji, na kumpata mhalifu au wahalifu haswa, kuwashitaki, na katika kuthibitika kwa jinai, kumuua au kuwaua wote. Ali alikuwa tayari kabisa kutwaa mwelekeo huu lakini kwanza ilimbidi arudishe amani na utulivu katika nchi baada ya vurugu (za kiutawala) na ghasia zilizokuwa zimedumu miezi mingi.

Kifo cha Uthman hakikuwa ni matokeo ya ushari wowote wa ghafla ambao aliufanya. Majadiliano ya siku nyingi na marefu yalikwisha kuutangulia uhalifu wenyewe. Aliuawa baada ya kushindwa kwa majadiliano yote hayo. Wajumbe walikuja kumuona kutoka miji ya mbali, na kumweleza juu ya maovu ya kupindukia ya magavana wake. Aliahidi kureke- bisha hali hiyo lakini alishindwa kutekeleza ahadi yake.

Pale ujumbe huo ulipomkumbusha juu ya ahadi yake ya kumfukuza mmoja wa magavana wake, yeye akasema: “Mnanishauri kwamba niwafukuze wale miongoni mwa magavana wangu ambao inaelekea hamuwapendi, na kwamba nichague watu mnaowapenda ninyi kuendesha serikali. Kama ingekuwa nitende kulingana na matakwa yenu, nitakuwa mtu nisiye na hadhi, na ninyi mtakuwa mnakamata mamlaka yote ya serikali na sio mimi.” (Tarikh Kamil – Ibn Athir, Juz. 111, uk.86)

Wale wajumbe walighadhibishwa na majibu ya Uthman, na wakasema: “Wewe huna uwezo wa kuyaweka sawa yale makosa ya serikali yako. Kwa hiyo, ni lazima ujiuzulu kwenye ukhalifa. Kama hufanyi hivyo, basi tutalazimika kuchukua hatua kali zaidi.”

Uthman akasema: “Ninyi mnatishia kuniua mimi? Kama hivyo ndivyo, basi ni jinai gani juu ya agizo ambalo kwalo mtaniuwa mimi? Katika Uislam, kuuawa ndio adhabu juu yangu:

(a) Kuua mtu asiye na hatia;
(b) Ukafiri;
(c) Ubakaji wa mwanamke safi.

Mimi sijatenda lolote kati ya jinai hizi. Ni kwa msingi gani mwingine tena ninyi mnataka kuniuwa mimi?”

Majibu ya wajumbe hao yalikuwa kama ifuatavyo: “Kwa wale watu wanaofanya ufisadi juu ya ardhi, au wanaopora haki za watu wengine, adhabu iliyoagizwa ndani ya Kitabu cha Allah ni kuuawa. Kwa ukorofi kabisa umetumia vibaya mamlaka ya serikali. Umemfukuza kutoka Madina sahaba wa Mtume wa Allah anayeheshimiwa sana, na vikaragosi wako wamewapiga marafiki zake wengine. Umeulazimisha umma kuwakubali walevi na makafiri kuwa viongozi wao.

Wewe na magavana wako mmewatishia na kuwadhulumu Waislam, na mmewapora haki zao. Mmeyafanya yote haya na zaidi.

Licha ya hayo, kama utajiuzulu kwa hiari yako, hatutakuingilia, na tutakuacha kwenye amani.”

Lakini Uthman hakutaka kujiuzulu kwa sababu, alisema kwamba, ukhalifa ni “joho” ambalo alikuwa amepewa na Allah swt., na hawezi akalivua.

Allah anaweza kwa kweli, kumpa joho la ukhalifa yoyote ampendaye. Lakini joho la ukhalifa ambalo Uthman alikuwa amelivaa, hakulipewa na Yeye Allah swt., bali alilipewa na Abdur Rahman bin Auf!

Majadiliano haya yanaweka bayana kwamba watu walichukua hatua ya mwisho kabisa, pale tu kila kitu kingine kiliposhindwa. Waliridhika kwamba kuuawa kwa Uthman ni halali kabisa. Kuridhika kwao kulitiwa nguvu zaidi kwa maneno na vitendo vya watu wakubwa kama Aisha, Talha, Zubeir na Amr bin Al-Aas ambao kila mmoja wao ameagiza kifo juu yake, wazi wazi ama kwa mzunguko.

Uthman Na “Abdallah Ibn Saba”

Ukhalifa wa Uthman umewabwagia Waislam serikali iliyodhoofika sana, na mingi ya mivurugiko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii iliyojitokeza kutokana nayo, ilikutana na mwitiko wa mashaka na wakati mwingine wa kinyume. Mivurugiko hiyo hatimaye ilisababisha kifo cha khalifa mwenyewe.

Wanahistoria wengi wa Sunni wanaona vigumu kukubali kwamba Uthman alijiletea maangamizi yeye mwenyewe. Wanayo shauku mno ya “kueleza” au kutumia hekima kuonyesha ni kwa nini mambo yalikwenda kombo katika ukhalifa wake.

Lakini kwa njia gani? Shauku yao iliwaelekeza kwenye kubuni mtu wa ajabu na kisirani ambaye walimwita “Abdallah ibn Saba”

Uundwaji wa Abdallah ibn Saba “ulifumbua” matatizo mengi sana ya wanahistoria wa Kisunni. Alifanya uhamishaji wa hatia uwe wenye kuwezekana kwao. Kwa mujibu wa waliomuunda, yeye alikuwa ni Myahudi kutoka Yemen aliyekuwa ameingia kwenye Uislam, akahamia Madina, na kisha akapita akizunguka kueneza mafundisho ya uongo na ya uasi, na kueneza manung’uniko na chuki dhidi ya Uthman. Alikuwa, kama wanavyodai, anahusika na huzuni zote na mabalaa, na hatimaye na kifo chenyewe cha Uthman!

Abdallah ibn Saba, inavyoonekana, mara akawa ndiye mtu mwenye nguvu zaidi katika Dar-ul-lslam yote. Na baadae, ilikuwa ni yeye aliyempindua khalifa kutoka kwenye madaraka yake na kuitupa serikali yote ya Waislam kwenye vurugu.

Alichokuwa akikifanya Abdallah ibn Saba, kilikuwa ni uhaini mkubwa. Hivi kulikuwa na kitu rahisi cha kufanya kwa Marwan kuliko kumkamata yeye na kumuua kwa uhaini wake, kama alikuwa yuko Madina? Au, je, kulikuwa ni kitu chochote rahisi zaidi kwa gavana wa jimbo au hata afisa wa ngazi ya chini, kuliko kumkamata yeye na kuzima maisha yake, kama angekuwa katika mojawapo ya majimbo?

Hakuna. Lakini kwa sababu za ajabu, alitamba toka mji hadi mji na kutoka jimbo hadi jimbo, akimkosoa khalifa, na hakuna hata mtu mmoja aliyemgusa. Inavyoonekana, yeye aliishi maisha ya kichawi basi!

Inashangaza kwamba Uthman ameweza kumfukuza sahaba wa cheo cha juu wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kama Abu Dharr al-Ghiffari kwenda Rabza (Abu Dharr alifia huko Rabza); aliweza kumpiga Ammar ibn Yasir mpaka kuzimia, na aliweza kuvunja mbavu za Abdallah ibn Mas’ud, wote hawa masahaba mashuhuri wa Muhammad; na bado aliweza kuwapa uhuru Amr bin Al-Aas na “Abdallah ibn Saba” wa kuwachochea Waislam dhidi yake yeye mwenyewe kwa makemeo na matusi yanayochoma.

Wakati Uthman alipouawa, “Abdallah ibn Saba” huenda aliona alikuwa amekamilisha kazi yake na “akaingia mitini.” Lakini miezi michache tu baadae, “akaibuka tena” katika mkesha wa vita vya Basra (vita ya Ngamia). Ilikuwa ni yeye, waundaji wake wanavyodai, ambaye alihusika vita hivyo vya kusikitisha. Hata hivyo, wakati, au mara baada ya vita hivyo, akatoweka tena, na safari hii alitoweka milele.

Kwa hakika ni ajabu sana kwamba ameweza kutokomea bila ya kuacha alama na dalili nyuma yake. Kitendo chake cha kutoweka kilikuwa kikamilifu sana kana kwamba hakuwahi “kuwepo”.

Kwa kweli, huo “umuhimu” uliosababisha kubuniwa kwa Abdallah ibn Saba, ulikuwa umekoma kuwepo. Waundaji wake, kwa hiyo, wakamzika. Lakini hadi leo hii, anafufuliwa mara kwa mara pale wanahistoria wa Sunni wanapotaka “kuelezea” habari zisizokubalika za kipindi kile cha historia.

Dr. Taha Husain, mwanahistoria wa kisasa wa Misri, ameutangua ubuniwaji wa Abdallah ibn Saba katika kitabu chake kiitwacho, al-Fitna-tul-Kubra. Ameonyesha kwamba Tabari ndiye mwanahistoria wa kwanza ambaye aliandika kuhusu Abdallah ibn Saba. Alimsikia kutoka kwa Umar bin Saif. Abdallah bin Saba alizaliwa kichwani mwa Umar bin Saif.

Lakini katika vyanzo vingine kabla ya Tabari, Abdallah bin Saba hakutajwa mahali popote. Hii ni ajabu kwa sababu “mhusika” mashuhuri kama Abdallah ibn Saba aliyeivuruga jamii ya Waislam katika zama za Uthman, awe hakupata kutambuliwa kokote kutoka kwa wanahistoria wa kabla ya Tabari.
Dr. Taha Husain anaendelea kuleta swali kwamba hata kama ikichukuliwa kwamba Abdallah ibn Saba alikuwa akieneza mafundisho ya uongo na ya uasi, hivi ni yeye ambaye “alimshawishi” Uthman kumteua mtu kama Marwan kama waziri wake mkuu? Muhajirina na Ansari walikasirishwa na kunyanyuliwa kwa Marwan kwani machoni mwao alikuwa ni mtu wa kuepukwa sana kama ukoma.

Na hivi Uthman alikuwa akitekeleza ushauri na mwongozo wa Abdallah ibn Saba pale alipowafukuza magavana wa majimbo wale waliokuwa wameteuliwa na Umar bin al-Khattab, na akachagua ndugu zake mwenyewe badala yao? Hili lilikuwa ni moja ya malalamiko huko majimboni.

Hadith ya Abdallah ibn Saba ni mbinu ya kuficha makosa ya mtu.
Lakini mbinu hiyo haikuwa yenye nguvu zaidi!

Ikiwa kwa upande mmoja, watetezi wa Uthman wameanzisha mtu wa kubuniwa kama Abdallah ibn Saba ili kufunika makosa na utawala mbaya wake Uthman, kwa upande mwingine wameamua kukataa ukweli wa mambo ya kihistoria. Katika mengi ya maandishi juu ya historia ya kale ya Uislam, yanayoonekana katika miaka ya karibuni, watetezi wa Uthman wamefikia kiasi cha kukataa kwamba alifukuza gavana yoyote kati ya wale walioteuliwa na Abu Bakr au Umar au kwamba kuna kitu chochote cha kulaumika ndani yake kama alifanya hivyo, au, kwamba alifanya kosa lolote jingine.

Ni kazi na haki kabisa ya mabingwa watetezi wa Uthman kama wanataka kuendelea kuishi na uongo na udanganyifu au kwa usahihi zaidi kwa kujidanganya wenyewe. Lakini ukweli mchungu unaouma hautatoweka tu hivi hivi ati kwa sababu tu mtu havipendi. Hiki ndio kile yule mwanahistoria wa sasa, wa Kimisri, Dr. Taha Husain, anachokiandika juu ya suala hili katika kitabu chake al-Fitna-tul-Kubra:

“Tusiwafuate wale watu ambao wanaukataa ukweli wa habari zilizotufikia kuhusu migogoro na migongano ya masahaba wa Muhammad, Mtume wa Allah, na vurugu ambazo zilitokea kwa wakati huo huo. Kama tukifanya hivyo, tutakuwa kwa kweli, tunaukataa msingi mzima wa historia ya Uislam, kuanzia pale Mtume alipotangaza ujumbe wake.

Wale watu waliosimulia kutokukubaliana kwa masahaba, na wakasimulia na mageuzi ya kisiasa ya wakati huo, ni wale wale waliohadithia harakati za mwanzoni, mapambano na ushindi, na maisha (Sira) ya Mtume na ukhalifa (wa Abu Bakr na Umar). Katika suala hili, hatuna uhuru wa kuteua na kuchagua. Hatuwezi kuchukua yale tunayoyataka tu na kuyakana yale tusiyoyapenda. Hatuwezi tukaziita baadhi ya Hadith ni za kweli na nyingine ni za uongo.

“Kitu kimoja ambacho juu yake hakina shaka ni kwamba Waislam waligawanyika katika suala la Uthman, na mgawanyiko wao uliishia katika kifo chake, na ndio kamwe hawakuwa wameunganishwa tena tangu hapo.

“Lakini migawanyiko ile na kutokuelewana kule kulikuwa na sababu zake. Ni kweli kwamba Waislam walimuua Uthman lakini hawakufanya hivyo bila ya vyanzo au sababu.”
(al-Fitna-tul-Kubra, kilichochapishwa Cairo mwaka 1959)