read

Vita Vya Basra (Vita Vya Ngamia)

Vita Vya Pili Vya Wenyewe Kwa Wenyewe Katika Uislam

Waislam walikuwa wamepigana vita moja ya wenyewe kwa wenyewe wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr, khalifa wa kwanza. Ndani ya kizazi hicho hicho, wao sasa walikabiliwa na tishio kali la kupigana nyingine. Vita vya kwanza cya wenyewe kwa wenyewe vilipiganwa na serikali dhidi ya baadhi ya raia zake wapinzani; vita hivi vya pili vilipiganwa na raia wapinzani dhidi ya serikali yao.

Maprofesa Sayyed Abdul Qadir na Muhammad Shuja-ud-Din, wameandika katika kitabu chao cha History of Islam (historia ya Uislam) Sehemu ya 1 (Lahore, Pakistan) kama ifuatavyo:

Aisha alikuwa anarudi Madina kutoka Makka baada ya Hijja pale aliposikia habari za kuuawa kwa Uthman, na kupanda kwa Ali kwenye cheo cha ukhalifa ndipo akaamua kutokwenda Madina, na kurudi Makka. Talha na Zubeir pia waliwasili Makka. Gavana wa Uthman hapo Makka alikuwa ni Abdallah bin Aamir Hadhrami. Marwan na jamaa wengine wa Bani Umayya walikuwa wakiishi kama wageni wake. Wote hao walifanya mkutano na kukubaliana kwamba watalipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman. Waliunda jeshi hapo Makka la wapiganaji 3000, na wakaamua, baada ya majadiliano kiasi, kutembea kwenda Basra. Waliishikilia Basra, wakaikamata hazina, na waliwaua Waislam 600 ambao waliwashuku kuwa wanawapinga, na wakaeneza hofu katika mji huo.

Kutafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman kulikuwa ni kisingizio kwa ajili ya vita. Kilikuwa ni kificho sio tu kwa ajili ya malengo ya viongozi wa maasi bali pia kwa ajili ya madhambi yao. Hapakuwa na njia ya wao kuficha nia zao, malengo na maazimio yao na vile vile ushiriki wao katika mauaji ya Uthman ila kwa kudai kwamba wao walikuwa ni watetezi wake. Kitu kimoja ambacho kilikuwa wazi kwa kila mtu ni kwamba kama Ali angeweza kuimarisha serikali yake, moja ya mambo ya kwanza kabisa ambayo angeyafanya, lingekuwa ni kuazisha uchunguzi kwenye mauaji ya Uthman, na ilikuwa haikwepeki kwamba kesi ya mashitaka ya jinai ingeelekea kwa viongozi wa maasi wenyewe. Jukumu walilokuwa wamechukua wakati wa kuzingirwa kwa Uthman, lilikuwa halifichiki kwa mtu yoyote. Mashahidi walioshuhudia, wote walikuwepo hapo Madina na wangethibitisha chini ya kiapo, kile walichokuwa wamekiona.

Kwa wale viongozi wa maasi kwa hiyo, kulikuwa na njia moja ya kumzuia Ali na haki yake isiyobadilika wala kuzuilika, na hiyo ilikuwa ni kuanzisha kelele ya kisasi kabla hajaweza kuviweka vyombo vya sheria katika hali ya utendaji. Hili ndilo hasa wao walilolifanya. Wengine miongoni mwao pia walikiri kwamba walichokuwa wanakifanya, kilikuwa ni kulipia madhambi yao, na kulikuwa hakuna njia bora ya kulipia madhambi kuliko “kuosha damu kwa damu.” Walikuwa wameua khalifa mmoja, na sasa walikuwa wamuuwe mwingine. Hii ndio ilikuwa njia pekee, wao walijadili, ya wao kupata “wokovu.”

Hakuna anayejua ni kwa haki gani Aisha, Talha na Zubeir walikuwa wanatafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman. Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na uhusiano na Uthman. Kila mmoja wao alitokana na ukoo tofauti. Ndugu wa karibu wa Uthman walikuwa ni mjane wake, Naila, na watoto wake wa kiume na wakike, na wao walikuwa hawatafuti kulipiza kisasi chochote kutoka kwa mtu yoyote. Ilikuwa ni baada ya tu ya kuuliwa kwake ambapo Uthman alipata watetezi wa kujiteua wenyewe wa jinsia zote, waliokuwa tayari na wenye shauku ya “kumlinda” yeye!
Aisha hakuweza kumuona Ali kwenye cheo cha ukhalifa. Chuki yake juu ya Ali ilikuwa inazidi nguvu. Kama mtu mwingine mbali na Ali angekuwa khalifa, asingeweza kuanzisha hili tukio la hatari lenye misiba mbele yake ambalo ndani yake makumi ya maelfu ya Waislam waliuawa.

Wakati ambapo, kisa cha ugomvi halisi kwa upande wake kilikuwa ni chuki yake isiyofifia juu ya Ali, alipata pia sababu nyingine ya kushinikiza mapambano hayo dhidi yake kwa nguvu zaidi. Kama ikibidi afanikiwe katika kumuondoa Ali kutoka kwenye kitovu cha madaraka, yeye alikuwa amfanye mpwa na mwanawe wa kumlea, Abdallah bin Zubeir, kuwa ndiye khalifa mpya.

Watatu kati ya magavana wa Uthman ambao walikuwa wamefukuzwa na Ali ni Abdallah bin Aamir Hadhrami wa Makka; Ya’la bin Umayya wa Yemen; na Abdallah bin Aamir bin Kurayz wa Basra. Baada ya kufukuzwa kwao, huyu wa kwanza aliishi Makka, na hawa wawili wengine pia walikuja wakaishi Makka. Waliichukua hazina pamoja nao. Wakazi wengine wa Makka pia walitoa michango mikubwa kwenye masanduku ya fedha ya waasi. Kwa njia hii, hawa waasi walipata fedha muhimu ya kutosha kuimarisha vita vyao.

Viongozi wa waasi walifanya mkutano nyumbani kwa Abdallah bin Aamir Hadhrami, aliyekuwa gavana wa Makka hapo awali, kuamua ni nini walichokuwa wafanye.

Uvamizi wa Madina, na safari ya kwenda Syria, yalifikiriwa lakini yakaonekana hayawezekani kwa sababu mbali mbali. Mwishowe, Abdallah bin Aamir bin Kurayz, aliyekuwa gavana wa Basra hapo awali, alishauri kwamba wangekwenda Basra. Ushauri huu ulimvutia kila mtu, na ulikubaliwa na wote. Talha aliupokea kwa hamu sana, na akasema kwamba familia nyingi za ukoo wake zilikuwa zinaishi Basra, na kwamba anaweza kutegemea msaada wao.

Wale viongozi wa maasi ndipo wakapanga mkakati wao: kwanza wataishika Basra; wakiwa na Basra kama kituo chao, wataweza kuikalia Kufa ambako Zubeir alikuwa na wafuasi wengi. Wakiwa na Basra na Kufa mikononi mwao, wao walivyoona, itawezekana kwa wao kumtenga Ali huko Hijazi, na kuvamia maeneo yake; na kumsHind, na kuupora ukhalifa kutoka kwake.

Nia ya waasi hawa iliyotangazwa ilikuwa ni kuwaua wale watu ambao walimuua Uthman. Wale watu waliomuua Uthman, wote walikuwa wako Madina, lakini wale watetezi wake wa kujiteua walikuwa wakisonga mbele kuelekea Basra – maili 800 kwa upande wa mashariki, ndani ya Iraq!

Talha na Zubeir walimuomba Abdallah ibn Umar bin al-Khattab kuandamana nao kwenda Basra lakini yeye alikataa kwenda.

Aisha alimhimiza Hafsa binti Umar bin al-Khattab na wajane wengine wa Mtume waliokuwa bado wapo Makka baada ya Hijja, kwenda naye Basra, na kushiriki katika vita dhidi ya khalifa. Wote walikataa isipokuwa Hafsa. Yeye alikuwa tayari kwenda na Aisha lakini kaka yake, Abdallah bin Umar, alimkataza kufanya hivyo.

Umm Salma alikuwa mmoja wa wajane wa Mtume (s.a.w.w.). Aisha alimtumia barua huko Madina akimualika kushiriki katika kampeni yake. Umm Salma alimjibu kama ifuatavyo: “Ewe Aisha! Umesahau kwamba Mtume wa Allah alikuamuru ubakie nyumbani na sio kuvuka mipaka iliyowekwa na Dini yetu? Jihadi ya wanawake iko katika kujizuia. Macho yao yasiwe makakamavu, na sauti zao zisiwe kubwa.

Unadhani kwamba kama Mtume wa Allah alikuwa akukute wewe ukifukuzana na ngamia katika jangwa, angependezewa? Kama ningekuwa nimuasi mume wangu, nisingeweza kamwe kumkabili tena. Kwa hiyo, muogope Allah nyakati zote.

Itakuwa ni kwa faida yako mwenyewe kubakia nyumbani, na sio kwenda na kuingia kwenye mambo ya hatari.”

Aisha alidai kwamba alikuwa anakwenda kwenye ujumbe wa amani. Kama alikuwa, basi ulikuwa ni ujumbe wa amani wa ajabu sana kuliko yote. Alisindikizwa kwenda Basra na wapiganaji 3000, wakiwa na silaha tele za hatari hatari, na wakiwa na kiu ya damu ya Waislam wasio na hatia!

Hatimae maandalizi yote yalikamilika, na jeshi la Aisha, Talha na Zubeir, liliondoka Makka, kwa kishindo kikubwa cha nderemo, kuelekea kwenye mafikio yao ya mbali – Basra.

Wakati lile jeshi la Makka lilipokuwa linatembea kuelekea mashariki, mtu mmoja alizusha swali la ni nani atakayekuwa khalifa endapo utapatikana ushindi dhidi ya Ali. Mtoto wa Talha akasema kwamba baba yake atakuwa ndio khalifa lakini mtoto wa Zubeir akampinga kwa kudai kwamba ni baba yake pekee atakayekuwa khalifa.

Mabishano makali yalianza ambayo yangesababisha kurushiana ngumi kati ya vijana wawili hao wakati Aisha alipowasili kwenye tukio hilo. Aliingilia kati baina yao, na mashabiki wao, na akalifutilia mbali swali hilo linalokera kwa vile lilikuwa si la wakati muafaka.

Ingawa Aisha alilizima lile swali la uongozi kwa wakati ule, aliagiza hata hivyo kwamba mpwa wake, Abdallah bin Zubeir ataliongoza jeshi hilo katika Swala. Hukumu hii ilikuwa na umuhimu maalum katika mazingira ya nyakati. Katika kadhia moja, wakati wa maradhi ya mwisho ya Mtume, baba yake Aisha, Abu Bakr, aliwaongoza Waislam fulani kwenye Swala. Lile jambo la kwamba aliwaongoza katika Swala, lilitumika, mara baada ya kifo cha Mtume, kama “hoja” kwa upendeleo wake (Abu Bakr) na “sifa” ya kuwa khalifa.

Aisha alimpenda mpwa wake, Abdallah bin Zubeir, zaidi kuliko mama yake mwenyewe alivyompenda, na alidhamiria kumfanya khalifa afuataye. Juu ya kusisitiza kwake, hata Zubeir ilimbidi kusimama nyuma ya mwanawe mwenyewe kutekeleza swala zake. Kama Aisha alivyoona, kwa kuzingatia kigezo cha baba yake mwenyewe, hakuna yeyote katika lile jeshi waasi atakayeweza kudai kwamba alikuwa na “sifa” kama zile zile za kuwa khal- ifa kama mpwa wake alizokuwa nazo kwa vile yeye ndiye peke yake aliyekuwa ameliongoza hilo jeshi katika Swala.

Suala la uongozi lilikuwa linamsumbua Said bin Al-Aas pia. Alilizungumza na Talha na Zubeir na majibizano yafuatayo yalitokea kati yao:

Said: Kama mtashinda vita dhidi ya Ali, nani atakuwa khalifa afuataye?
Talha: Yeyote atakayechaguliwa na Waislam, ndiye atakayekuwa khalifa wao.
Said: Wakati mlipoondoka Makka, mlidai kwamba nia yenu ya kupigana vita dhidi ya Ali, ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman. Kama malengo yenu haya- jabalika, basi mnapaswa kumfanya mmoja wa watoto wake kuwa khalifa mpya, na wote wapo hapa pamoja nasi katika jeshi hili.
Talha: Hivi unadhani tutawapita Muhajirina wakubwa na kumfanya mmoja wa vijana wako asiye na ujuzi kuwa khalifa wetu? Kamwe.

Said ndipo akaelewa kwamba mazungumzo ya kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman yalikuwa ni hila tu, na lengo halisi la wale “watawala watatu” lilikuwa ni kunyakua madaraka kwa ajili yao wao wenyewe.

Mgeni mashuhuri kwenye kambi ya waasi alikuwa ni Mughira bin Shaaba. Alizungumza na Aisha na Marwan, na akawashauri kuacha mpango wao wa kuivamia Basra. Alimwambia Marwan: “ ….. Kama unakwenda Basra kuwatafuta wauaji wa Uthman, basi sharti utambue kwamba wako hapa kwenye kambi yako mwenyewe na sio Basra. Ndio makamanda wa jeshi lako. Walimuua Uthman kwa sababu kila mmoja wao alitaka awe ndiye khalifa. Lakini wakashindwa, na baada ya kushindwa kwao, wakaibuni hii hadithi ya kutafuta kulipiza kisasi.”

Lakini Aisha na Marwan hawakuwa na nia ya kuuacha mpango wao mkubwa wa mapambano. Hawakuukubali ushauri wa Mughira, ndipo yeye, Said bin Al-Aas, Abdallah bin Khalid na wengine wachache wakajitoa wenyewe kutoka kwenye jeshi la waasi, na wakaenda Ta’if. Lile jeshi la waasi lilianza tena matembezi yake kuelekea Basra lakini tukio lisilokuwa la kawaida lililifanya lisimame mara nyingine tena.

Wakati Aisha alipokuwa anapita kwenye kisima fulani kwenye kijiji kilichokuwa kwenye njia kuu, mbwa koko fulani walimzunguka ngamia wake, na wakaanza kumbwakia Aisha kwa ukali sana. Aisha alitoa kichwa chake kutoka kwenye machela iliyofunikwa, na akamuuliza mtoto wa Talha kama alikuwa analijua jina la kile kijiji walichokuwa wanakipita. Yeye akasema walikuwa wanapita kwenye kitongoji kinachoitwa Haw-ab.
Pale Aisha alipolisikia lile jina la Haw-ab aliingiwa na hali ya fadhaa. Alimuamuru mwon- goza ngamia wake kumkalisha huyo ngamia, na akasema kwamba ilimbidi kurudi Madina haraka sana badala ya kuendelea japo kidogo tu kuelekea Basra.

Kubadilisha kwa ghafla kwa mwelekeo wa safari kwa Aisha, kulimzangaza mtoto wa Talha, na akamuuliza ni kwa nini hakuweza kwenda Basra. Yeye Aisha akasema kwamba kumbukumbu imemjia ya utabiri wa Mtume (s.a.w.w.) na akamweleza ilivyokuwa kwa maneno yafuatayo:

“Yeye, Mtume siku moja alikuwa na wake zake, na akiongea nao alisema: ‘siku itafi- ka ambapo mbwa wa Haw-ab watakuja kumbwekea mmoja wenu, na hiyo itakuwa siku ambapo atakuwa kwenye upotovu wa wazi.’ Kisha yeye akanigeukia mimi, na akasema: ‘angalia ewe mwanamke mwekundu! Usije ukawa ndiye mke yule.’ Na hivi sasa ninaweza kusikia na kuona kwamba mbwa wa Haw-ab wananibwekea mimi. Kwa hiyo, ni mimi niliyeko kwenye upotovu wa dhahiri.”

Lakini mtoto wa Talha hakuvutika, na akasema: “Ewe mama wa waumini! Usiwajali mbwa hao wanaobweka. Tunayo mambo muhimu sana ya kufanya. Kwa hiyo, natusonge mbele kuelekea kwenye mafikio yanayotupungia mkono kutoka upande wa mashariki.”

Lakini Aisha alionekana kuwa amedhamiria kurudi Madina. Akishtushwa na kusisitiza kwake juu ya kurudi Madina, mtoto wa Talha alimwita Abdallah bin Zubeir akitegemea kwamba ataweza kumshawishi dhidi ya kulitelekeza lile jeshi la waasi.

Abdallah bin Zubeir alifika kwenye eneo la tukio na yeye pia akayasikia maelezo ya Aisha. Lakini ilimbidi amzuie kwa gharama yoyote ile. Kama alikuwa alitelekeze lile jeshi la waasi, juhudi zote za viongozi wa maasi za kutwaa madaraka, zitavunjika papo hapo. Zaidi ya hayo, watakuwa hawana mahali pa kwenda. Yeye, kwa hiyo, akamwambia shangazi yake kwamba kile kijiji ambacho mbwa wake walikuwa wamembwekea, na wakawa wamemtingisha wazi wazi, hakikuwa Haw-ab; kilikuwa ni kijiji kingine kisichoeleweka vizuri. Aisha, hata hivyo, hakuridhika, na akatamka kwamba hatakwenda Basra.

Abdallah bin Zubeir sasa ilimlazimu kuchukua hatua za mwisho kabisa kumhakikishia shangazi yake kwamba katika kwenda Basra, hakuwa akipotoka, na kwamba kubweka kwa mambwa fulani kusimlegeze moyo. Kisha akala kiapo kwamba jeshi lile lilikuwa limeiacha Haw-ab mbali sana huko nyuma. Yeye vile vile aliwakusanya Waarabu hamsiniwa jangwani, akawaleta mbele ya Aisha, na wote wakaapia kwamba Haw-ab kwa uhakika ilikuwa mbali sana kutoka pale alipokuwa yeye.

Wanahistoria wa Kiarabu wanasema kwamba ule “ushahidi” ambao Abdallah aliutoa mbele ya Aisha, ulikuwa ndio kosa la kwanza la kusema uongo baada ya kiapo, katika Uislam.

Tabari, mkuu wa wanahistoria wa Kiarabu, pia amelisimulia tukio hili. Anaongeza kwamba kupitia juhudi za mwanawe wa kumlea, Abdallah bin Zubeir, na “mashahidi” wake hamsini, Aisha mwishowe aliridhika kwamba wale mbwa wanaombwekea hawakuwa wa Haw-ab hata hivyo, bali wa kijiji kingine. Alilitupilia mbali tukio hilo kama bahati mbaya. Dhamira yake mbaya ilikuwa “imetulizwa,” na alikuwa tayari kukaa kwenye kipando kuelekea Basra.

Kwa wakati huu, Ali alikuwa anashughulishwa na kutathmini hali halisi. Katika maadui zake wote, alijua kwamba Mu’awiyah, gavana wa Syria, alikuwa ndiye aliyekuwa hatari zaidi, na alihisi kwamba alipaswa kuzingatia kumshughulikia yeye kwanza.

Lakini tena akasikia kwamba Talha na Zubeir ambao hapo mapema waliondoka Madina kwenda Makka “kutekeleza umra,” wamekivunja kiapo chao cha utii kwake, na kwamba wao na Aisha, ambaye alikuwa tayari yuko Makka, wamenyanyua bendera ya uasi dhidi yake. Ililetwa habari kwake pia kwamba viongozi hao watatu walikuwa tayari wanasonga mbele pamoja na jeshi lililoandaliwa vema kuelekea kwenye mji muhimu wa Basra ndani ya Iraq kwa nia ya kuuteka.

Aisha alikuwa kamwe hajafanya siri ya uadui wake kwa Ali lakini yeye Ali hakufikiria kamwe kwamba atafikia kiasi cha kufanya vita dhidi yake. Kwake yeye, ushirikiano wa Talha, Zubeir na Mu’awiyah ulikuwa ukielekea kuwezekana lakini ushirikiano wa Talha, Zubeir na Aisha haukuelekea kamwe.
Lakini alikuwa huyu hapa, pamoja na washirika wake, wakiwa ni tishio la moja kwa moja kwenye usalama wa Dola ya Kiislam kuliko Mu’awiyah mwenyewe.

Ali alilazimika kusimamisha kila kitu ili kukabiliana na upinzani wa Aisha, Talha na Zubeir. Alilalamikia uchokozi wao usio na maana na usio wa wakati muafaka, na alijaribu kuwashawishi kuacha kusababisha umwagaji wa damu ya Waislam ambao ulikuwa hauk- wepeki kama wangeasi dhidi ya mamlaka halali. Alituma barua kwa Aisha ambayo madhumuni yake yalikuwa kama ifuatavyo:

“Kwa jina la Allah ambaye ni Mwingi wa Rehma na Mwingi wa Kurehemu. Umeondoka nyumbani kwako kwa uvunjaji wa moja kwa moja wa amri za Allah na Mtume Wake, na sasa unapanda mbegu za vita vya wenyewe kwa wenyewe miongo- ni mwa Waislam. Hebu sita japo kwa muda kidogo na ufikirie kuhusu hili: Wewe unahusika nini na majeshi na vita? Je, ni kazi yako wewe kupigana? Na unapigana dhidi ya nani? Dhidi ya Waislam? Nafasi yako wewe iko nyumbani kwako. Allah amekuamrisha wewe kubakia nyumbani kwako. Kwa hiyo, muogope Yeye, na usimuasi Yeye, na urudi mara moja kwenda Madina.”

Aisha aliipokea barua ya Ali lakini maombi yake hayakuwa na athari yoyote juu yake yeye, na wala hakuijibu kabisa.

Ali alituma barua kama hizo hizo kwa Talha na Zubeir na wao pia hawakumjibu. Ali alitambua kwamba wale viongozi wa waasi walikuwa wamedhamiria kabisa kumwaga damu ya Waislam.

Akitamani kuwazuia wasifanye hivyo, aliamua kuwaingilia kati. Lakini angeweza tu kulizuia jeshi lao kwa jeshi lake mwenyewe, naye alikuwa hana jeshi!

Khalifa huyu mpya ilimbidi aandae jeshi kama ilikuwa alizuie jeshi la waasi lisifike na kuikalia Basra. Aliingia Msikitini, akawafahamisha Waislam kile waasi walichopanga kuk- ifanya, akawaelezea juu ya haja ya kuwa na jeshi la kukabiliana na changamoto yao na aliwataka wao kujitokeza kama askari wa kujitolea.

Ali alishitushwa na mwitiko alioupata kwa maombi yake. Hakuna mtu aliyejitolea kupi- gana dhidi ya waasi hao. Alirudia maombi yake, na majibu yalikuwa ni yale yale. Baada ya kila Swala, Ali aliusihi mkusanyiko wa waumini kusimama katika kutetea serikali iliyoanzishwa kihalali. Aliwakumbusha kwamba alikuwa amechukua uongozi wa serikali yao juu ya msisitizo wao wenyewe. Aliwakumbusha pia kwamba alifanya ridhaa yake mwenyewe ya ukhalifa kwa kutegemea juu ya ahadi yao ya kumtii yeyekatika amani na katika vita.

Waislam, inavyoonekana, walikuwa wamesahau ahadi yao. Ali alijihisi alikuwa amekwamishwa kabisa.

Baada ya siku chache, hata hivyo, mtu mmoja alisimama mle Msikitini na akamwambia Ali kwamba yeye atamtii amri zake. Baadhi ya wengine, wenye kujali kama yeye, walifuata mfano wake. Mara Ali akawa na uwezo wa kukusanya pamoja kikosi kidogo cha wapiganaji wa kujitolea 700 waliokuwa tayari kumtii yeye.

Sir Johb Glubb:

“Mara tu Ali aliposikia kwamba Zubeir, Talha na Aisha wameondoka Makka, aliamua kuwafuata, lakini alipata ugumu sana katika kuandaa kikosi kwa ajili ya madhumuni hayo. Miezi mitatu tu kabla, Masahaba na watu wa Madina walikuwa wamemuomba awe khalifa. Sasa ni wachache tu walioweza kumsaidia yeye ingawa Zubeir na Talha wanaoonekana wazi kutokuwa na maadili walikuwa wamekusanya watu 3000 kuto- ka Makka na makabila ya jirani.”

Mnamo Oktoba mwaka 656, miezi minne baada ya kuuawa kwa Uthman, Ali alitoka kumfuata Zubeir na Talha. Alikuwa na watu 700 tu pamoja naye. Akiwa mnyonge sana kuendelea, alipiga kambi kwenye kisima cha jangwani mahali paitwapo Najid. (The Great Arab Conquests, uk. 318, 1967)

Kabla ya kuondoka Madina, Ali alimwita Umm Salma, mmoja wa wajane wa Muhammad (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt., na akamuaga. Umm Salma akamwambia: “Kwa jina Allah, ninakuweka kwenye ulinzi Wake. Kwa Uwezo na Utukufu Wake, wewe pekee ndio uko pamoja na haki, na maadui zako wote wapo kwenye batili. Kama isingekuwa amri ya Allah kwa wake za Mtume Wake kubakia nyumbani, ningefuatana nawe katika mapambano haya.”
Umm Salma alikuwa na mtoto kutokana na ndoa yake ya kwanza, akamkabidhi kwa Ali, na akasema: “Ndiye mwanangu pekee. Yeye ndio kitu cha thamani kabisa nilichonacho katika dunia hii. Ninamkabidhi kwako. Atajitoa muhanga, kama ikibidi, maisha yake kwa ajili yako.”

Ali alivutiwa sana na kitendo cha Umm Salma. Alimshukuru yeye, na akachukua likizo ya kuvunja moyo kutoka kwake asijue kama atakuja kurudi tena Madina kamwe. Mtoto wake Umm Salma aliandamana naye kwenda Iraq.

Ali alimteua Sahl ibn Hunaif Ansari kuwa gavana wa Madina wakati wa kutokuwepo kwake, na alimtuma Qathm ibn Abbas kwenda Makka kwenda kuchukua mamlaka ya mji ule kama gavana wa mji. Kitu cha mwisho ambacho alikifanya Ali hapo Madina, kilikuwa ni kutembelea kaburi la Muhammad Musrafa (s.a.w.w.), na la Fatima Zahra – baba na bintiye.

Muhammad alikuwa kiongozi wake, mfadhili na rafiki yake, na Fatima alikuwa ni mke wake. Aliwaaga wote hao kwa moyo uliojaa huzuni na macho yaliyojaa machozi.

Katika kuwasili kwake huko Iraq, Ali na kikosi chake kidogo walipiga kambi mahali panapoitwa Dhi-Qaar. Abdallah ibn Abbas, binamu yake, anasimulia kuwasili hapo kambini, kwa rafiki mpya, kama ifuatavyo:

“Tulikuwa tupo Dhil-Qaar wakati mchana mmoja, tulipomuona mtu mmoja anakuja kuelekea kambini kwetu. Alikuwa mzee sana, na mdhaifu sana. Vitu pekee alivyokuwa navyo ni kifuko kidogo cha chakula cha akiba na mfuko wa maji wa ngozi ya mbuzi. Wakati huu akaingia kambini, na akaomba kukutana na Ali. Alipoletwa mbele ya Ali, akajitambulisha mwenyewe kama Uways Qarni kutoka Yemen. Mara tu tulipolisikia jina lake, tulijua kwamba ni yule rafiki na mpendwa aliyekuwa hajawahi kuonekana, wa bwana wetu, Muhammad, Mtume wa Allah swt. Alimuomba Ali anyooshe mkono wake ambapo akaunyoosha. Kisha naye akauweka mkono wake juu ya mkono wa Ali, na akatoa kiapo cha utii kwake.”

Ali alimsalimia yule rafiki na kipenzi cha bwana wake, Muhammad, kwa uchangamfu kama vile ambavyo Mtume mwenyewe angefanya, kama angekuwa yupo pale mwenyewe.

Mheshimiwa Uwais aliingizwa ipasavyo katika jeshi la Madina. Kwa Ali, kuwasili kwa Uwais Qarni katika kambi hiyo kulikuwa ni kijaliza adimu kwenye mpangilio wa matukio ya baadae ya kikatili na ya kisirani ya uchochezi, uhaini, usaliti na maasi, ambayo yameitawala Dola ya Kiislam. Kwa kitambo kidogo, alisahau ya wakati ule na akazama kwenye njozi za nyakati zilizopita; nyakati za bwana wake, Muhammad (s.a.w.w.). Zile zilikuwa hasa “nyakati njema za kale;” zile zilikuwa ndio nyakati bora kweli. Ni vipi ali- tamani angeweza kurudi kwenye nyakati zile ambapo, kama msaidizi mkuu wa Muhammad, alikuwa ameulinda Uislam na umma wake yeye kutokana na waabudu masanamu. Sasa katika kijalizo cha kushtusha, umma ule umepinga mamlaka yake, na ukaonekana kuwa na kiu na damu yake. Alizinduliwa kutoka kwenye mawazo yake ya zama nzuri na za kuvutia na wakati uliopo wa kutisha na uliotengeka.

Hatua za awali za Ali za kuepukana na vita, alizozifanya kutoka Madina, zilikuwa zimeshindwa lakini alikuwa na shauku kubwa ya kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Waislam. Kwa hiyo, mara tu baada ya wapiganaji wake walipokuwa wamepiga kambi, alianzisha kampeni yake ya kuleta amani, na akafanya mfululizo wa ishara mpya za kidiplomasia kwa viongozi wa maasi ili waje kujadiliana masharti ya amani pamoja naye kuliko kuombea usuluhishi wa silaha. Aliwatuma baadhi ya wale masahaba maarufu wa Mtume kwenda kuwasihi Ayesha, Talha na Zubeir wasiivunje amani lakini bila mafanikio.

Edward Gibbon:

“Maisha ya Swala na tafakuri hayakupoozesha juhudi za kivita za Ali; lakini katika umri wa utu uzima, baada ya uzoefu wa muda mrefu wa wanadamu, bado aliisaliti katika tabia yake, ile pupa na kutokuwa na hadhari kwa ujana. Katika siku za mwanzo za utawala wake, aliacha kujipatia ama kwa zawadi au pingu, vile viapo vyenye mashaka vya Talha na Zubeir, wakuu wa Kiarabu wawili wenye nguvu sana. Walitoroka kutoka Madina kwenda Makka, na kutokea hapo kwenda Basra; wakasi- mamisha bendera ya uasi; na wakaichukua kwa nguvu serikali ya Iraq, au Assyria ambayo waliitaka bure kama zawadi kwa ajili ya utumishi wao.
Barakoa ya uzalendo inaruhusiwa kufunika ukiukaji wa utaratibu wa dhahiri kabisa; na maadui, labda wale wauaji, wa Uthman, sasa walidai kisasi kwa ajili ya damu yake. Walifuatana katika msafara wao na Aisha, mjane wa Mtume, aliyehifadhi mpaka saa ya mwisho ya maisha yake chuki isiyo na huruma dhidi ya mume na watoto wa Fatima. (The Decline and Fall of the Roman Empire)

Katika kuacha kupokea ama kwa zawadi au pingu, kiapo cha wasiwasi cha Talha na Zubeir, Ali alikuwa hasaliti pupa na kutokuwa na hadhari kwa ujana, kama Gibbon anavy- odai. Ali alikuwa anajua kwamba Talha na Zubeir wana udanganyifu mioyoni mwao. Kuwapa wao zawadi kutakuwa ni hongo tu, na Ali alikuwa sio mtu wa kumpa hongo mtu yoyote kwa ajili ya kitu chochote.

Huko Madina, Abdallah ibn Abbas alikuwa amemshauri Ali kumteua Talha na Zubeir kuwa magavana wa Basra na Kufa. Kubashiri kutokana na tabia zao na muelekeo wao wa baadae, kuwateua Talha na Zubeir kuwa magavana, kungekuwa ni kosa baya sana kwa upande wa Ali. Kama angefanya hivyo, angelazimika kupigana, sio dhidi ya mmoja bali Mu’awiyah watatu!

Na kuhusu pingu, Ali sio mtu wa kumkamata mtu yoyote kwa kosa lililofikiriwa lakini halijatendwa bado. Wakati Talha na Zubeir walipokuja kwake na kumuomba ruhusa ya kwen- da Makka kutekeleza umra, aliwaruhusu waende lakini akawaambia kwamba hawakuwa wakienda Makka kwa ajili ya kutekeleza hijja.

Kama ilivyoonyeshwa hapo juu, Ali aliweza kukusanya hapo Madina, sio zaidi ya wapi- ganaji mia saba. Kwa kikosi kidogo kiasi hicho, asingeweza kukabiliana na changamoto ya waasi. Yeye, kwa hiyo, alimtuma Muhammad bin Jaafar na Muhammad ibn Abu Bakr kwenda Kufa kuleta wapiganaji wa kuongezea nguvu kutoka huko.

Gavana wa Kufa kwa wakati huu alikuwa ni Abu Musa al-Ashari, naye aliwapinga hao. Wakati uimarishaji ulipochelewa kuja, Ali alimtuma kwanza Abdallah ibn Abbas na Malik ibn Ashtar, na kisha Imam Hasan na Ammar ibn Yasir kwenda Kufa, kuandikisha askari.

Imam Hasan aliupuuza upinzani wa Abu Musa, akaingia kwenye Msikiti mkubwa, akawahutubia Waislam wa Kufa kwa hotuba ambayo ndani yake aliwakumbusha ni nini ilikuwa kazi na wajibu wao kwa Allah swt., na Mtume Wake (s.a.w.w.).

Kuwasili kwa Hasan – kipenzi cha Muhammad – hapo Kufa, kulisababisha msisimko. Hotuba yake ilikuwa haijakwisha bado pale watu walipoanza kupiga makelele: tunakutii, tupo kwa ajili yako.

Wakati huo huo, Malik ibn Ashtar aliingia kwenye kasri ya gavana. Aliwafukuza watumishi wa Abu Musa na akalikamata lile jengo. Abu Musa alitoroka kutoka Kufa usiku, na akatafuta hifadhi kwa Mu’awiyah huko Damascus.

Imam Hasan, Ammar bin Yasir, Abdallah ibn Abbas na Malik ibn Ashtar walirudi Dhi-Qaar wakiwa na wapiganaji 12,000 wa Kufa pamoja nao.

Gavana wa Ali huko Basra alikuwa ni Uthman bin Hunaif Ansari, sahaba wa Mtume yule yule ambaye Umar alikuwa amemteua kama Kamishna wa Fedha wa Iraq.

Aliposikia kwamba jeshi la Aisha, Talha na Zubeir lilikuwa kwenye vitongoji vya Basra, alimtuma mmoja wa marafiki wa Ali – Abul Aswad ad-Du’ali – kwenda kuwaona na kujua sababu za kwa nini walikuja. Abul Aswad alimwendea Aisha, na mabishano yafuatayo yakatokea baina yao:

Abul Aswad: Ewe mama wa waumini, lengo lako ni nini katika kuja Basra pamoja na jeshi?
Aisha: Nimekuja kulipiza kisasi kwa ajili ya mauaji ya Uthman ambaye aliuawa katika nyumba yake mwenyewe ingawa alikuwa hakutenda dhambi yoyote.
Abul Aswad; Yeyote ambaye atakuwa amemuua Uthman, hayupo Basra.
Aisha: Ndio, ninajua. Lakini kupata kulipiza kisasi, ninahitaji ushirikiano na msaada wa watu wa Basra.

Abul Aswad: Ninatumaini hujasahau bado kwamba Mtume wa Allah swt. alikuwa amekuamuru wewe
kubakia nyumbani. Kwa hali yoyote, sio kazi yako kujiingiza kwenye siasa na vita.
Haifai kabisa kwa mjane wa Mtume kuondoka nyumbani kwake, na kupigana dhidi ya Waislam.

Aisha: Hivi atathubutu Muislam yoyote kupigana dhidi yangu mimi?

Aisha aliamini kwamba kama atakwenda kwenye uwanja wa vita mbele ya jeshi lake, wapiganaji wa maadui wenyeji, katika kumuona akiwakabili wao, watakuja ama upande wake, au wataiacha vita hiyo, na kumtelekeza bwana wao.

Abul Aswad halafu yake akaenda kuwaona Talha na Zubeir, na akawauliza nia yao ilikuwa nini katika kuja Basra katika mpango wa kijeshi.

Talha/Zubeir: Tunataka kisasi kwa Ali kwa ajili ya mauaji ya Uthman.
Abul Aswad: Ali hakumuua Uthman wala hakuwa na ushiriki wowote katika mauaji yake, na hilo mnalijua.
Talha/Zubeir: Kama hakushiriki, kwa nini anawalinda hao wauaji?
Abul Aswad: Ina maana kwamba mmevunja kiapo cha utii ambacho mlimpa Ali?
Talha/Zubeir: Kiapo hicho kilichukuliwa kutoka kwetu kwa ncha ya upanga. kwa hiyo kilikuwa ni batili.

Abul Aswad aliweza kuona kwamba wale viongozi wa waasi walikuwa wameshikilia vita, na kwamba mazungumzo ya ziada pamoja nao yalikuwa hayana maana. Yeye kwa hiyo, akarudi Basra, na akamweleza Uthman ibn Hunaif kile ambacho Aisha, Talha na Zubeir walikuwa wamemwambia.

Viongozi wa maasi hawakuficha nia zao lakini Uthman ibn Hunaif hakuwa na jeshi lenye nguvu, na alijua kwamba asingeweza kuulinda mji dhidi yao. Kwa hiyo, walipotokea kwenye milango la mji, alifanya majadiliano pamoja nao. Pande mbili hizo zilikubaliana kwamba mpaka atakapofika Ali, waasi hao hawatafanya kitu chochote cha kuvuga mpango uliopo, na Uthman ibn Hunaif ataendelea kufanya kazi kama gavana wa Basra.

Lakini hazikupita hata siku mbili wakati viongozi wa maasi walipoyavunja makubaliano ya kusitisha vita. Jeshi lao liliushambulia mji wakati wa usiku, na wakauvamia kwa nguvu, na mara lilipokaribia kuta zake, lilionekana kupagawa. Wapiganaji walizagaa ndani ya mji na wakaua Waislam 600, ikiwa ni pamoja na 40 ndani ya Msikiti Mkuu wenyewe.

Talha na Zubeir walipenya kwenye nyumba ya gavana ambamo walimkamata Uthman ibn Hunaif, na wakawaua wale waliojaribu kumlinda yeye. Walitaka kumuua yeye pia lakini yeye aliwaambia kwamba kama watamuua yeye, basi kaka yake, Sahl ibn Hunaif, ambaye alikuwa gavana wa Madina, angewaua ndugu zao wote waliokuwa wanaishi katika mji ule, katika kulipiza kisasi.

Wao, kwa hiyo, walilazimika kuichunga hamu yao ya kumuua yule rafiki wa kuheshimika wa Muhammad (s.a.w.w.). Lakini walimpiga, wakamng’oa nywele zote katika kichwa chake, nyusi zake, na ndevu zake, na wakamfukuza kutoka Basra. Aliweza hata hivyo, kuifikia kambi ya bwana wake, na akapepesuka mbele yake, mahutu- ti kama anayekufa!

Ali alisikitika sana kumuona Uthman ibn Hunaif katika hali ambayo Talha na Zubeir waliyomtoa nayo. Hakuweza kumtambua yeye. Alijaribu kumfariji huyo rafiki wa zamani wa Muhammad Mustafa kwa machozi yake.

Jeshi la waasi sasa lilikuwa limeushika mji wa Basra. Lilikuwa limefanikiwa katika kufanikisha lengo lake la kwanza. Viongozi wake waliwafukuza marafiki wote na wafuasi wa Uthman ibn Hunaif kutoka mjini hapo kama hawakuwaua.

Ali hakuwa na chaguo sasa bali kuamuru jeshi lake kusonga mbele kwenda Basra. Wakiwa wamesimama hapo Zawiya, kaskazini ya Basra, alituma barua kwa mara nyingine tena kwa kila kiongozi wa waasi akishauri kwamba pande zote zisuluhishe kutofautiana kwao kwa majadiliano badala ya kupigana dhidi ya mwingine na kuuana wenyewe.

Viongozi wa waasi hawakuwa na tamaa ya kuzijibu barua za Ali. Bila kumuachia masha- ka yoyote akilini mwake kwamba wameitupa amani kama zana ya sera yao, waliamua kuk- abiliana naye nje ya ngome za mji.

Sir John Glubb:

“Jeshi la khalifa lilipokuwa linakaribia Basra, wale waasi walitoka kuja kukabiliana nalo, wakiongozwa na Zubeir na Talha. Basra yote haikuwa nao. Bani Bakr, kabila ambalo wakati fulani liliongozwa na yule shujaa Muthana, lilijiunga na jeshi la Ali. Bani Tamiim waliamua kutopendelea upande wowote. Jeshi la Ali sasa likawa na nguvu kidogo.

Katika siku za Ujahilia, wanawake waliokuwa wamepanda kwenye machela juu ya ngamia, mara kwa mara walifuatana na makabila yao kwenye vita, kuwatia moyo wapiganaji. Aisha, “Umm-ul-Mu’minin,” aliandamana na jeshi la waasi katika kiti chake cha ngamia.” (The Great Arab Conquests, uk. 320, 1967)

Wakati majeshi mawili hayo yalipokabiliana, Ali alitoka kwenye safu yake na akamwita Talha na Zubeir kuja kupambana naye. Dr. Taha Husein wa Misri anasema kwamba majemedari wote walitoka kwenye safu zao wakiwa katika mavazi kamili ya kivita kiasi kwamba sehemu za miili yao zilizoweza kuonekana, ni macho yao tu. Pale Aisha alipowaona wao wakienda, aliogopeshwa na kile ambacho kingeweza kutokea kama wangekutana na Ali katika vita. Lakini alijulishwa kwamba Ali alikuwa hana silaha, na hakuwa, kwa kweli, amevaa hata deraya, na akawa ameondolewa shaka. Ali aliwauliza kwa nini wamevunja kiapo cha utii ambacho walikuwa wamempa yeye kwa hiari zao, na kwa nini walitaka kupigana dhidi yake.

Wakimjibu, Talha na Zubeir walikariri ule msururu wa shutuma za zamani kwamba alikuwa anawalinda wauaji wa Uthman, na kwamba walikuwa wakiitafuta haki kwa ajili ya kifo cha Uthman. Ali aliwaambia kwamba wao walijua vizuri sana tu, kwamba yeye hakuhusika kabisa na kifo cha Uthman au na wauaji wake. Kisha yeye akaongeza: “Kwa vile hamtaki kusikiliza hoja, ninashauri kwamba tujaribu kidokezi kipya ili kuamua mgogoro huu. Mtakumbuka kwamba bwana wetu, Muhammad (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt, wakati mmoja aliitisha Mubahila (kulaaniana) pamoja na Wakristo wa Najran. Hebu natuige mfano wake, na tusimamishe Mubahila, na kuomba kama ifuatavyo:

“Ewe Mola wa Viumbe wote! Tunaomba Huruma Zako. Wewe Unafahamu yote ninayohisi au ninayofikiri au ninayoyafanya. Hakuna kinachofichikana mbele ya macho Yako. Kama nimeshiriki, wazi wazi au kwa kificho, katika mauaji ya Uthman, au kama nimewasaidia wale watu ambao wamemuua Uthman, au kama nilifurahia kwa siri wakati alipouawa, onyesha chuki Yako kwangu. Bali kama sina hatia ya kosa lote la ushiriki wa njama katika mauaji ya Uthman, basi onyesha chuki Yako kwa wale wote wanaodai kwamba mimi ni mshiriki katika uhalifu dhidi ya Uthman.”

Talha na Zubeir hawakuukubali mwaliko wa Ali kusimamisha Mubahila, na wakatamka wazi: “Hatukuoni wewe kama unastahili ukhalifa, na sisi kwa hali yoyote hatuna upungufu zaidi wa sifa au kutokustahili zaidi kuwa khalifa kuliko wewe ulivyo.” (Tarikh Tabari, juz.111, uk. 519).

Kitu kimoja Talha na Zubeir walichokifanya, kilikuwa ni kuacha kile kisingizio cha kulipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha Uthman; walikuwa wapigane dhidi ya Ali ili waweze kuwa makhalifa.

Jaribio jingine la kuokoa amani lilikuwa limeshindikana lakini Ali bado hakutaka kuona Waislam wakiwauwa Waislam. Yeye, kwa hiyo, alimwita Zubeir ambaye hata hivyo alikuwa ni binamu yake, kwenye kikao cha faragha, na akamkumbusha juu ya zile siku ambapo wao wote walikuwa wapiganaji-wenza, na walipigana dhidi ya maadui wa dini chini ya bendera ya Mtume wa Allah. Je hazikuwa, alimuuliza Zubeir, siku za shani, na sasa, yeye, Zubeir, binamu yake, alikuwa anataka kupigana dhidi yake; ilikuwa inawezekana vipi; ni vipi Zubeir atapigana dhidi yake yeye, binamu yake mwenyewe?

Ali pia alimkumbusha Zubeir kuhusu utabiri wa Mtume (s.a.w.w.). “Unaukumbuka ule wakati,” alimuuliza Zubeir, “ambapo Mtume wa Allah swt, alikwambia wewe, mbele yangu, kwamba siku moja utakuja kupigana dhidi yangu, na kwamba utakuwa umepotoka kwa kufanya hivyo?” “Oh ndio,” alitamka ghafla Zubeir, “ninakumbuka aliyokuwa ameyasema Mtume. Lakini nilikuwa nimeusahau utabiri huo, na sasa sitapigana dhidi yako.” Kumbukumbu pia ilimjia Zubeir ya utabiri mwingine wa Mtume wa Allah swt. ambaye alisema kwamba rafiki yake mwandani, Ammar ibn Yasir, atakuja kuuawa na kundi la watu waovu. Sasa Zubeir ghafla alitambua kwamba Ammar alikuwa kwenye jeshi la Ali.

Zubeir aligeuza hatamu za farasi wake na akarudi kwenye safu zake mwenyewe, uso wake ukionyesha ishara za mgogoro wa ndani na mfadhaiko mkubwa. Katika kujibu maswali ya shauku ya Aisha na ya mwanawe mwenye tamaa na mgomvi, alisema kwamba Ali amemkumbusha yeye juu ya utabiri wa Mtume wa Allah swt. mwenyewe, na yeye, kwa kutambua kwamba yuko kwenye upotofu, alikuwa amempa Ali kiapo kingine cha kutokupigana dhidi yake. Mwanawe mwenye shari akasema kwamba sababu hasa ya kuji- toa kwake kwenye vita ilikuwa sio ule utabiri wa Mtume bali ni kumuogopa Ali.

Zubeir alipandwa na hasira kwa kashfa hii. Alisema kwamba alikwisha kuapa kutokupigana dhidi ya Ali, na akaongeza kwamba chaguo lililokuwa mbele yake lilikuwa wazi: ama ajiaibishe miongoni mwa Waarabu kwa kukimbia kwenye vita kama muoga, au ajiimarishe mwenyewe kukabiliana na laana, na aliona kwamba kujiaibisha kama muoga ndio kwepe- si katika maovu hayo mawili.

Zubeir aliondoka kwenye uwanja wa vita, inavyoelekea, kwa nia ya kurudi Madina. Alikuwa amesafiri maili chache tu wakati alipogundua kwamba alikuwa akifuatwa kwa siri na mtu mgeni kwake. Mgeni huyu alikuwa ni mtu wa Basra, mtu aitwaye Amr bin Jarmuz. Ingawa Zubeir alishtuka kwa wasiwasi, aliendelea kwenda mpaka alipofikia kijiji. Hapo alishuka ili aoge, aswali na kupumzika. Lakini alikuwa amefika mwisho wa safari yake. Pale alipokuwa anaswali, Amr bin Jarmuz alimshambulia na kumuua.

Zubeir alikuwa ameondolewa kwenye hesabu lakini Talha na Aisha walidhamiria kupigana hata bila yeye. Ali, hata hivyo, bado alisita kupigana, na akaamua kufanya jaribio moja jingine la kuiokoa amani. Alimtuma kijana mmoja, aitwaye Muslim ibn Abdallah ambaye alifahamika kwa uchamungu wake, pamoja na nakala ya Qur’an, kwenda kumuomba adui kuuweka mgogoro huo kwenye Hukmu ya Allah, na kusisitiza amani kwa ajili ya utukufu wa damu ya Waislam.

Akiwa amesimama mbele ya kundi la maadui kwa karibu kiasi, Muslim ibn Abdallah akai- funua ile Qur’an, na akasema: “Nitasoma kifungu kutoka kwenye Kitabu cha Allah ili mjue ni zipi amri na Makatazo Yake.” Hotuba yake, hata hivyo, ilikatishwa na watupa mishale wa adui ambao waliirushia mishale ile nakala ya Qur’an aliyokuwa anaisoma. Wakati alipokuwa anajaribu kuikinga ile nakala ya Qur’an, mmoja wa watumwa wa Aisha alimnyemelea, akamshambulia na kumuua.

Mwili wa Muslim ibn Abdallah uliletwa mbele ya Ali, na ukawekwa chini. Ali alikuwa anaomboleza kifo chake wakati mwili mwingine, wa mmoja wa wapiganaji wake ambaye alikuwa amepigwa na kuuawa kwa mishale na lile jeshi la Basra, ulipoletwa mbele yake.

Alijaribu kuiondoa mishale hiyo kutoka kwenye maiti hiyo lakini alikuwa hajaondoa mishale mingi pale miili zaidi ya wapiganaji wake, iliyotobolewa na mishale, ilipowasili na ikapangwa mbele yake katika muonekano wa wazi kwa majeshi yote mawili. Waasi walikuwa wanachukua mazoezi ya kutupa mishale kwenye jeshi la Ali.

Tabari anasema katika Tarikh yake (juz. 111, uk. 522) kwamba wakati Ali alipoiona miili hii mbele yake, yeye alisema: “Sasa ni halali kupigana dhidi yao.”

Kisha Ali aliinua mikono yake kuelekea juu mbinguni, na kisha akaomba: “Ewe Mola Wangu! Kuwa Shahidi kwamba sikubakisha kufanya kitu chochote kuhifadhi amani miongoni mwa Waislam. Sasa hakuna hiari iliobakia kwangu bali ni kuliruhusu jeshi langu kujihami lenyewe kutokana na mashambulizi wasiyoyachokoza. Sisi ni waja Wako wanyenyekevu.

Tujaalie Neema na Huruma juu yetu. Tupatie sisi ushindi dhidi ya adui bali kama ni mapenzi Yako kumpa yeye, basi tupatie sisi taji la kifo cha kishahidi.”

Ali alimaliza maombi yake, na kisha akivigeukia vikosi vyake, akavihutubia kama ifuatavyo kabla tu ya kuvipa ishara ya kupigana: “Enyi Waislam! Msiwe wa kwanza kumshambulia adui; mwacheni adui awe wa kwanza kuwashambulieni ninyi. Mara atakaposhambulia, basi itabidi mjihami wenyewe.

Kama Allah akiwapeni ushindi juu ya maadui zenu, basi kumbukeni kwamba na wao pia ni Waislam. Kwa hiyo, msiwauwe wale waliojeruhiwa miongo- ni mwao. Kama watakimbia kutoka kwenye medani ya vita, msiwaandame, na muwaache waokoe maisha yao. Kama mtakamata mateka, msije mkawaua.
Msiwakatekate wale waliokufa, na msiwanyang’anye deraya zao au silaha au vitu vingine vya thamani ambavyo mnaweza kuvikuta kwenye miili yao. Msiipore kambi yao, na msiwaudhi wanawake zao hata kama watatumia lugha mbaya na yenye matusi dhidi yenu au viongozi wenu. Lakini juu ya mambo yote, msiwe wasahaulifu, wakati wowote, juu wa uwepo wa Muumba wenu katika maisha yenu. Mpo machoni pake kila wakati.”

Majeshi mawili hayo ndipo yakashambuliana. Waasi walikuwa tayari wamekwisha mpoteza Zubeir, mmoja majemedari wao wawili, kwa kuondoka. Jemedari mwingine, Talha, alikuwa pia alitegemewa kukutana na majaaliwa kama ya Zubeir. Abul Fida, mwanahistoria huyu, anasema kwamba Marwan alimuomba mtumwa wake amfunike ili asiweze kuonekena. Wakati yule mtumwa alipomfunika, alipachika mshale kwenye uta wake, akaulenga kwa Talha, na akamwambia mtumwa wake:

“Nilimuona mtu huyu (Talha) wakati wa zile siku ambazo Uthman alikuwa amezingirwa ndani ya nyumba yake. Alikuwa akiwachochea na kuwahimiza lile kundi kuin- gia ndani ya nyumba, na kumuua Uthman. Lakini leo anataka kulipiza kisasi kwa ajili ya damu yake. Inasikitisha eeh! Yeye alimpenda Uthman kweli kweli. Hapa, nitampa yeye zawadi kwa ajili ya mapenzi yale. Anastahili sana zawadi. Hata hivyo, mapenzi kama yale yasipite bila ya kuzawadiwa.”

Marwan akauachia mshale ule. Ilikuwa ni pigo la kufisha ambalo lilimpata Talha kwenye paja, naye akachopea kwenda kwenye kifo chake nyuma ya jeshi lake.

Ibn Saad:

“Katika vita vya Ngamia, Talha alikuwa juu ya farasi wake karibu na Aisha wakati Marwan alipomrushia mshale ambao ulimchoma mguu wake. Kisha Marwan akasema: “Wallahi, sasa sitakuwa na kumtafuta yule mtu ambaye alimuua Uthman.” (Tabaqat, juz.111, uk. 223)

Hakim:

“Ibrahim ibn Muhammad ibn Talha alisema kwamba Marwa bin al-Hakam alimuua babu yake (Talha) kwa mshale katika vita vya Ngamia.”(Mustadrak)

Sir John Glubb:

“Zubeir alikuwa binamu wa kwanza wa Mtume. Mama yake alikuwa ni dada wa baba yake Muhammad. Zubeir na Ali walikuwa wamefahamiana na kufanya kazi pamoja maisha yao yote. Wakati wao sasa walipokutana kati ya safu za majeshi yao husika, Ali alimuuliza Zubeir kama alikuwa analikumbuka hili na ule wakati walipokuwa wote ni wadogo, na pale walipokuwa wote wamejawa na hisia kali za ghera ya kidini na upendo binafsi kwa Muhammad; jinsi Mtume wa Allah alivyosema hili na Ali na Zubeir wakasema lile. Ni nyakati nzuri kiasi gani, siku zile zilikuwa. Zubeir alilazimika kutoa machozi na akaapia kwamba hatampinga Ali kamwe kwa kutumia nguvu. Ali alikuwa na sifa ya kuwa mzungumzaji mwenye ushawishi.

Mapigano yalipoanza, Zubeir, kufuatana na kiapo chake, alijitoa kwenye uwanja wa mapambano. Akitembea katika bonde la jangwa, mbali kidogo kutoka kwenye uwan- ja wa vita, alikabiliwa na kuuawa na mtu aliyekuwa amechelewa nyuma yake. Kwa njia hii isiyo na maana na ya kufedhehesha ndivyo akafa mmoja wa mashujaa wakub- wa wa awali wa Uislam. Wakati huo huo, Talha alikuwa amejeruhiwa kwa mshale na alirudishwa Basra ambako alikufa muda mfupi baadae.” (The Great Arab Conquests, uk. 320, 1967)

Zubeir na Talha walikufa kwa sababu zenye wasiwasi. Inaelekea kwamba walikuwa wanatambua kwamba kile walichokuwa wanakwenda kupigania sio chao, na ilikuwa sio haki. Wote wawili walikuwa miongoni mwa mashujaa maarufu wa siku za mwanzo za Uislam lakini katika vita vya Basra, ushujaa wao uliwatupa mkono. Hawakuonyesha ushujaa, na walikufa kama kondoo.

Maelezo pekee juu ya hili yanaweza kuwa kwamba hamasa yao ilivunjika, na walishindwa hata kabla vita havijaanza. Kwao kulikuwa ni kushindwa kwa maadili.

Kwa kweli, Talha na Zubeir walikuwa wameingia kwenye kipingamizi kikubwa. Wakati mmoja, walikuwa na shauku sana ya kumuondoa Uthman. Walifanya uamuzi na wakashindwa. Baada ya kifo cha Uthman, kukaa kwa muda hapo Madina, kwa kweli kungekuwa ni hatari sana kwao. Hawakuipata njia ya kujitoa kwenye kipingamizi hicho ila kwa kupiga kelele kwamba walikuwa wanatafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha Uthman. Kuwakamata wauaji wa Uthman ilikuwa ni kazi ya utawala uliowekwa kihalali ambao ulikuwepo wakati huo, na ambao ulikuwa umetangaza kwamba utalichunguza suala hilo.

Lakini hicho ndio ambacho hasa Talha na Zubeir walichokuwa wakikiogopa. Hawakutaka uchunguzi wowote ule. Fursa yao pekee ya kuokoa shingo zao ilikuwa ni kuiweka dola kwenye ghasia, na kuliacha kwenye ghasia. Katika jaribio hili walifanikiwa. “Walifanikiwa” kwa maana ya kwamba hawakumruhusu Ali kuchunguza kifo cha Uthman, na badala yake, walimlazimisha kushughulika na uasi wao.

Inashangaza kwamba Talha na Zubeir, wafuasi wa mwanzoni kabisa wa Uislam na walivyokuwa masahaba wa Mtume (s.a.w.w.), wameweza kuvunja kiapo chao cha dhati bila kutegemewa kama walivyofanya. Kama kweli waliamini kwamba Ali alikuwa amehusika katika mauaji ya Uthman, walipaswa kusema hivyo ndani ya Msikiti wa Mtume (s.a.w.w.), mbele ya mkusanyiko wa Muhajirina na Ansari wote badala ya kuchukua kiapo cha utii kwake. Lakini hawakufanya hivyo, na wakachukua kiapo cha utii. Alimradi walikuwa na matumaini kwamba Ali atawateua kuwa magavana, basi walinyamaza kimya. Lakini mara tu walipopoteza matumaini hayo, wakavunja kiapo chao, na wakasimama katika maasi. Uasi ulikuwa ndio njia pekee ambamo wangeweza kumzuia Ali kuchunguza kifo cha Uthman.

Kama Talha na Zubeir wangekuwa wakweli katika kutafuta kisasi kwa ajili ya kuuawa kwa Uthman, kuna kitu kimoja tu ambacho wangeweza kukifanya. Wangemwambia Ali kwamba watampangia muda wa mwisho kwa ajili ya kufanya uchunguzi wake juu ya kifo cha Uthman, na alipaswa kuwatia mbaroni hao wahalifu kabla ya muda huo kwisha. Lakini hawakupanga muda kama huo; badala yake, walianzisha uasi kwa kisingizio cha kutafuta kulipiza kisasi kwa mauaji ya Uthman.

Wanahistoria wengine wanasema kwamba Ali alisikitikia vifo vya Talha na Zubeir. Ikiwa kama alifanya hivyo, kumbukumbu lazima ingemjia ya mwanzo wa heshima na mwisho wa fedheha wa mashujaa hawa wawili wa Uislam wa asili. Talha na Zubeir walilipa ghara- ma kubwa kwa ajili ya tamaa yao potofu, na kama usemi wa kisasa wa Kiarabu unavyosema, wao “wamepaliwa na kukata tamaa kwao wenyewe.”

Pamoja na Talha na Zubeir kuondoshwa kwa namna hii, yule ngamia ambae Aisha alikuwa amempanda, ilikuwa ndio sehemu ya kupatia moyo kwa lile jeshi la Basra. Wapiganaji wa Aisha walipigana kwa nguvu sana na kwa ujasiri wa makusudi kabisa, na wakajifanya wao wenyewe kuwa ngome hai karibu na ngamia wake. Mpiganaji mmoja alishikilia hatamu zake mkononi mwake.

Kapteni mashuhuri wa Ali, Malik ibn Ashtar, alimkata mkono wake kwenye kiwiko.

Mara moja, mpiganaji mwingine akachukua nafasi ya yule wa kwanza, na akazishika hatamu za ngamia huyo mkononi mwake. Malik ibn Ashtar akamkata mkono wake pia. Bingwa wa tatu akaingia, na yeye pia akapoteza mkono wake. Hii iliendelea mpaka ile mikono iliyokatwa ikapangwa rundo mbele ya ngamia huyo.

Pande zote kuzunguka ngamia wa Aisha, watu walikuwa wakishambuliana, na walikuwa wanakufa. Aisha akiwa amekaa kwenye machela yake juu ya ngamia huyo, alikuwa akiwasisitiza wapiganaji wake kumlinda yeye, na kushambulia na kumuua adui ambaye alimuua khalifa wao Uthman, asiyekuwa na hatia.

Kila mara waliposikia sauti yake, walipata moyo wa kufanya juhudi kubwa zaidi. Walikuwa wakirusha dhoruba mbaya kwa maadui sio tu kwa ajili ya kumlinda Umm-ul-muminin bali pia kulipiza kisasi kwa kifo cha Uthman.

Malik alikuwa bado akiendelea na kamchezo kake ka kukata mikono ya wale watu wote walioshikilia hatamu za ngamia wa Aisha. Wakati huu akamuona Abdallah ibn Zubeir, yule mshari wa jeshi la Makka, na kipenzi cha Aisha, akiupunga upanga wake. Alikuwa ndio “chanzo cha nguvu” cha vita vya Basra ambamo maelfu ya Waislam waliuawa. Kama isingekuwa uchochezi wake, vita vya Basra visingepiganwa kamwe.

Malik akasahau ngamia wa Aisha, na akamrukia kwa ukali kabisa Abdallah ibn Zubeir, akamuangusha chini ardhini. Alipokuwa anamnyooshea upanga kwenye shingo yake, kilio cha uchungu kilimtoka Aisha ambaye alidhania kwamba Malik atamuua mpwa wake. Kwa hofu kubwa, alipiga mayowe: “Oh muokoeni Abdallah ama sivyo Malik atamuua.”

Lakini ni nani ambaye alikuweko kwenye jeshi la waasi ambaye angeweza kumuokoa mpwawe Aisha kutoka kwa Malik? Kila aliyefika karibu ili kumuokoa, aliuawa yeye mwenyewe. Alipousikia ukulele wa Aisha wenye uchungu, alimwambia Abdallah: “Ninashawishika kukumaliza kwa upanga wangu lakini nakuachia maisha yako kwa sababu ya udugu wako na Mtume wa Allah swt.”

Malik aliyastahi maisha ya Abdallah zaidi kwa dharau kuliko kwa huruma. Abdallah akasimama kutoka kwenye mavumbi, na kama alivyokuwa ametishiwa na kukoswakoswa huku na kifo, upesi sana akajiweka mbali na upeo wa upanga wa Malik, kwa nia ya kutokuka- matwa na yeye tena.

Malik akarudi kwenye mchezo wa kukata mikono ya waasi. Lakini hawakuvunjwa moyo na hofu ya kupoteza mikono yao kwake. Aisha alikuwa akiwahimiza kwa vile alivyokuwa akiendelea kupiga makelele: “Mbarikiwe, wanangu! Ni fahari kwenu kwa kumlinda mama yenu kijasiri namna hiyo.”

Hatimaye Malik akachoka kukata mikono ya watu, na akaamua kuumaliza mchezo huo ambao umedumu kwa muda mrefu sana. Alikita miguu yake kwenye miili ya wale maiti, akalenga pigo la upanga wake usiokwepeka, na akamuua ngamia wa Aisha.

Ngamia huyo alianguka akiwa amechafuliwa kila upande na damu yake, na machela ya Aisha ikaanguka chini pamoja na ngamia huyo. Lakini Aisha hakuumia. Ali upesi sana akamtuma kaka yake Aisha, Muhammad ibn Abu Bakr, na Amar ibn Yasir, kwenda kuweka ile machela chini, na akamwambia amsindikize dada yake kwenda kwenye nyumba ya mjane wa muungwana mmoja wa Basra.

Ngamia wa Aisha alikuwa ndio nembo ya kuonekana wazi ambayo kwayo jeshi la Basra lilikuwa likipigania. Pale alipouawa, ile “nembo” ikatoweka. Ghafla lile jeshi la Basra likawa halina chochote cha kupigania, na likaanza kuvujika - waziwazi. Kila mmoja ndani yake akaanza kukimbilia kila upande. Katika kukimbia kwao, wapiganaji hao walimsahau hata Aisha ambaye walikuwa wakipigana kwa ajili yake kwa ujasiri kabisa muda mchache tu hapo nyuma. Mara kukawa hakuna kilichobakia katika medani ya vita isipokuwa maiti na majeruhi. Kwa vile Ali alilikataza jeshi lake kuwafukuza watoro, wengi wa waasi wali- weza kutoroka, na vita ikawa imekwisha kabisa.

Ali alitangaza tena yale maagizo aliyokuwa ameyatoa kabla ya vita kwamba wale waliok- ufa wasiibiwe au kukatwakatwa; kambi ya adui isiporwe; na wale wapiganaji waliosalimu amri wasiuawe. Alishikilia kwamba jeshi lake yeye mwenyewe lazima lionyesha mfano wa uungwana, uvumilivu, staha na uaminifu kama maadili ya msingi yanayojenga mfumo wa kijeshi wa Kiislam halisi.

Sir John Glubb:

“Vita vya Ngamia vilipiganwa mnamo Desemba mwaka 656. Mara tu baada ya adui kujitoa, Ali alitoa maagizo kwamba kusiwe na ufukuziaji na kwamba mauaji yakome mara moja. Wakati Ali alipoingia Basra, alifanya jitihada ya kusuluhisha pande zote. Lile jeshi lililoshindwa lilitendewa ustahimilivu. Ali alisisitiza kwamba yaliyopita yawe yamepita, kwani alikuwa wa hulka ya upole na ustahimilivu, pengine ya ukimya tu na alitaka kuiunganisha himaya kuliko kulipiza kisasi yeye mwenyewe juu ya maadui zake.”
(The Great Arab Conquests, uk. 322, 1963)

Ali alikuwa mstahimilivu, na alitaka kuiunganisha himaya na umma (watu) wa bwana wake, Muhammad (s.a.w.w.); lakini hakuwa “mkimya” kama Sir John Glubb anavyodha- nia. Sababu ya kutowaadhibu waasi ni kwamba alikuwa anachukia umwagaji damu kwa jumla, na hasa ule wa ndani ya Waislam.

Aliepuka pia kuuangamiza ule mji wa maasi wa Basra kwa sababu hiyo hiyo, yaani, imani yake juu ya utukufu wa damu ya Waislam. Kwa bahati, hakuna mtu mwingine miongoni mwa watu wa wakati ule aliyeshirikiana naye katika imani hii. Hawakuchukizwa kama yeye kuhusu kumwaga damu ya Waislam; waliimwaga, na kwa mbubujiko mwingi.
Aisha alimtetea kwa Ali mpwa wake na mwanawe wa kupanga, Abdallah ibn Zubeir, na akamuomba amsamehe. Ali akasema: “Msamaha kwa Abdallah bin Zubeir peke yake? Msamaha upo kwa kila mtu.”

Ali alimuachia, sio tu Abdallah ibn Zubeir bali pia maadui wa kupita kiasi kama vile Marwan bin al-Hakam, Walid bin Aqaba, Abdallah bin Aamir, na Bani Umayya wote.

Hakuna popote katika historia ya ulimwengu ambapo mshindi amewatendea maadui zake aliowashinda kwa ustahimilivu kama Ali, kabla au tangu hapo. Katika kutoa msamaha kwa waasi, alikuwa, kwa mara nyingine tena, akimuiga rafiki na bwana wake wa zamani, Muhammad, Mtume wa Allah aliyebarikiwa, ambaye pia aliwasamehe washirikina wa Makka, miongoni mwao wakiwemo maadui zake wabaya, wakati alipouteka mji ule. Ali alifuata nyayo za Muhammad (s.a.w.w.), na aliishi katika kuiga maisha yake matakatifu.

Siku chache baadae, Aisha alikuwa tayari kusafiri. Kutokana na maombi yake, Ali alimpeleka Makka. Kaka yake, Muhammad, alikwenda pamoja naye. Huko Makka, ali- fanya Umra, na kisha akaenda Madina. Aisha anayo sifa ya kuwa mwenye ujuzi sana katika masuala ya dini, na alikuwa pia ni muhadittha, yaani msimuliaji wa Hadith za Mtume (s.a.w.w.). Akiwa na elimu kiasi hicho, hivi inawezekana kwamba alikuwa hajui kuwa yeye hakuwa na haki ya kulipiza kisasi kwa ajili ya damu ya Uthman?

Kulipiza kisasi ni kazi ya upande uliokosewa, na kutoa adhabu kwa mhalifu/wahalifu ni wajibu wa serikali. Aisha hakuwa ama na udugu na Uthman kwa namna yoyote ile wala yeye hakuwa mwakilishi wa serikali ya Waislam. Lakini hata hivyo aliipinga serikali halali kwa kisingizio cha kisasi, na akalazimisha idadi kubwa ya Waislam katika mlipuko wa vita. Shauku yake ya vita iliwafanya maelfu ya watoto kuwa mayatima, na maelfu ya wanawake kuwa wajane.

Mwanamke fulani, aitwaye Umm Aufa al-Abdiyya, wakati mmoja alimuuliza Aisha: “Ewe Ummulmuminin, nini maoni yako juu ya mwanamke anayemuua mwanawe mwenyewe?”

Aisha akasema kwamba mwanamke kama huyo atatupwa kwenye moto wa jahannam. Umm Aufa akaendelea kuuliza: “Litamfika lipi mwanamke aliyeua zaidi ya watoto 20,000 wake mwenyewe katika wakati mmoja na mahali pamoja?” Aisha alikasirishwa na kijem- be hicho, na akamkemea Umm Aufa atoweke. (Iqd-ul-Farid, juz.111, uk. 108).

Watu wengine wa familia yake Aisha mwenyewe walitamani Aisha asingeongoza majeshi na kupigana vita. Safari moja, alituma mtumishi kwa mpwa wake, Ibn Abil-Atiiq, akimuomba ampelekee yeye Aisha farasi wake ili ampande. Wakati mpwa wake alipompokea yule mtumishi, alimwambia mtumishi huyo:

“Mwambie Ummul-muminin kwamba Wallahi, hatujaosha bado yale madoa ya damu iliyomwagika katika vita vya ngamia. Je, anataka aanzishe vita vya farasi sasa?” (Baladhuri katika Ansab al-Ashraf, juz.1, uk. 431)

Kauli ya Ibn Abil Atiiq ilisababishwa na utani. Lakini mnamo mwaka 669 siku ilifika hasa ambapo Aisha alipanda farasi katika “mapambano” mengine. Wakati jeneza la Imam Hasan (a.s.) lilipoletwa kwenye kaburi la babu yake, Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), kwa ajili ya mazishi, Marwan ibn al-Hakam na watu wengine wa Bani Umayya walitokea kwenye tukio hilo, katika mavazi ya kivita. Walikwenda kuwazuia Bani Hashim kumzika Imam Hasan kando ya babu yake. Bani Umayya hao hawakuwa wenyewe tu; Aisha, Ummul-muminin, alikuja nao, akiwa amepanda juu ya farasi!

Aisha atakuwa ameshindwa katika vita vya Basra lakini “alishinda” yale “mapambano” ya Madina. Hasan hakuweza kuzikwa pamoja na babu yake kwa sababu ya upinzani wake yeye na Bani Umayya, na akazikwa kwenye uwanja wa makaburi wa Jannat-ul-Baqi.

Hakuna njia ya kutumia busara katika majukumu ambayo Aisha, Talha na Zubeir waliyachukua baada ya kifo cha Uthman. Ule ukweli kwamba walikuwa watu maarufu katika historia ya Waislam, haubadilishi au kuathiri yale majukumu waliyochukua. Kosa haliwi na shutuma nyepesi eti kwa sababu limetendwa na mtu maarufu. Kosa ni kosa tu bila kujali ni nani aliyelitenda.

Wake za Mtume walikuwa wakitegemewa hasa kuwa waangalifu katika kila kitu walichokisema au kukifanya. Hata hivyo, walitakiwa wawe mifano mbele ya umma namna ya mwenendo na adabu.
Kupotoka kutoka kwenye ubora kunaweza kupuuzwa katika wake za watu wa kawaida lakini sio kwao wao. Ikiwahutubia wao, Qur’an inasema: “Enyi wake wa Mtume! Atakayefanya maovu dhahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo ni rahisi kwa Mwenyezi Mungu.” (Al-Ahzab, 33:30)

Wanahistoria wengine wamejaribu kupunguza nguvu ya kiwewe cha matukio haya kwa kizazi kijacho, kwa kudai kwamba vitendo vya wale “Masahaba wa vita vya Ngamia” vilikuwa ni “makosa ya maamuzi” madogodogo tu. Makumi ya maelfu ya Waislam walikufa katika vita vya Basra bila ya sababu yoyote mbali na makosa madogodogo ya maamuzi kwa upande wa “Masahaba wa Jamal!”

Marerejeo yalikwishafanywa kwenye mlango wa huko nyuma, kwa “Abdallah ibn Saba” wa miujiza na wa kubuniwa, ambaye alikuwa, kwa mujibu wa wanahistoria wengi wa Sunni, ndiye “kichocheo” halisi katika kuuawa kwa Uthman. Wanahistoria hao hao waliona ni lazima kueleza matukio mengine yanayotatanisha na yenye wasiwasi kwa “kumrejeleza” yeye. Huenda huu ndio mfano uliopo hadi sasa wa mapema sana katika his- toria ya urejelezaji.

Kwa mujibu wa wanahistoria hawa, Abdallah bin Saba na wafuasi wake waliiona amani kama adui yao asiyeshindika. Walisadiki kabisa kwamba kama mazungumzo ya Ali juu ya amani yatafanikiwa, basi wao watakuwa ndio maiti wake wa kwanza. Kwa hiyo, dhamana pekee waliyoweza kuona kwa ajili ya usalama wao, ilikuwa ni kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ya Waislam.

Ilikuwa ni pamoja na ufahamu huo, wanavyosema wanahistoria wa Sunni, ambapo Abdallah bin Saba na kundi lake, wakashambulia wakati wa usiku, yale majeshi mawili, kwa wakati mmoja kwa mpigo. Katika giza, pande zote zisingeweza kuwaona au kuwatambua wakala halisi wa uchochezi, na kila upande uliridhika kwamba upande mwingine ndio ulioanza vita hivyo.

Ubuniwaji wa Abdallah ibn Saba ulilazimishwa na haja ya uwazaji yakinifu kwa ajili ya geresha ya dondoo zinazosumbua katika historia. Ni ubunifu wa kistadi kweli hasa lakini kwa bahati mbaya kwa wagereshaji wa historia, na kwa wale watetezi wa wale “Masahaba wa Jamal,” Abdallah ibn Saba hayajibu maswali yote juu ya tabia zao. Kwa mfano, je, hivi alikuwa ni Abdallah ibn Saba ambaye alivunja makubaliano ya kusitisha mapigano na Uthman ibn Hunaif, na ambaye alishambulia Basra wakati wa usiku, akaiteka, akaikamata hazina ya mji huo, na akawauwa Waislam zaidi ya 600 katika mji huo? Na je, alikuwa ni Abdallah ibn Saba ambaye alitishia kumuua Uthman ibn Hunaif, akamfanyia ukatili, akamtoa kwenye nyumba yake na akamhamisha kutoka Basra?

Na inakuwaje kwamba wakati Ali alipomtuma Abdallah ibn Muslim pamoja na nakala ya Qur’an Tukufu kwenda kuwaonya wale waasi kwamba watastahili ghadhabu ya Allah swt. ikiwa watachagua vita kuliko amani, wakakipiga mishale kile Kitabu, na wakamuua yeye (Abdallah ibn Muslim, yule mbebaji wa Qur’an)? Hivi alikuwa ni Abdallah ibn Saba ndiye aliyemuua huyu?

Na alikuwa ni nani ambaye alikuwa anachukua mazoezi ya kurusha mishale kwenye jeshi la Ali? Wapiga mishale katika jeshi la waasi walikuwa wamewaua zaidi ya vijana ishirini kabla yeye hajawaruhusu kupigana. Hivi wapiga mishale hawa walikuwa wakiwaua wapiganaji wa Ali bila ya kujua Aisha, Talha na Zubeir? Kama walijua, je, “watawala watatu” hawa walifanya chochote kuwazuia?

Aisha aliishi kwa miaka mingi baada ya vita ya Basra lakini hakumtaja kamwe Abdallah ibn Saba na jukumu lake la kama mchochezi wa vita. Yeye mara kwa mara alikuwa akisema kwamba alitamani kama angekuwa amekufa zamani kabla ya vita vile ambamo ndani yake maelfu mengi ya Waislam waliuawa. Kama Abdallah ibn Saba angekuwa ni mtu aliyeko kwenye historia, yeye Aisha angemlaani kwa ule umwagaji damu katika vita vya Basra. Abdallah ibn Saba alibuniwa muda mrefu sana baada ya vita vya Basra, na kifo cha Aisha.

Kama Abdallah ibn Saba angekuwa ni mtu hasa katika historia, angeweza kuwa katikati kabisa ya matukio na habari za nyakati hizo, baada ya kufanya jukumu “maarufu” kama hilo katika historia ya mwanzoni ya Uislam. Je, hakuwepo kwenye vita vya Siffin na Nahrwan? Hakuchochea yeye vita hivyo viwili pia baada ya kuwa alipata mafanikio kiasi hicho huko Basra? Na je, Mu’awiyah na Ma-Khariji pia hawakuwa waathirika wa njama zake? Ni nini hasa kilitokea, kama ni ubaya, kwa mtu mashuhuri katika historia ya Waislam kama huyu?

Abdallah ibn Saba alikuwa mtu wa usanisi na wa kusudi maalum. Alitengenezwa maalum na wapenzi na washabiki wa watu fulani maarufu katika historia ya mwanzoni mwa Waislam. Nia yao ilikuwa ni kulinda heshima, na pia, kama ikiwezekana, kuficha utambu- lisho wa watu hawa. Watu hawa walikuwa kwa kweli wanahusika, kwanza na mauaji ya Uthman, khalifa wa tatu, na tena, kwa kuzuka kwa Vita vya Pili vya Wenyewe kwa wenyewe katika Uislam – vita vya Basra au vita vya Ngamia. Walitegemea kwamba heshima ya watu hao wanaohusika itakuwa swalama kwenye maamuzi ya historia kama wangeweza kulazimisha kukubalika kwa lawama ya matukio haya juu ya Abdallah ibn Saba.

Abdallah ibn Saba, inavyoelekea, alikuwa mtu mashuhuri sana katika historia ya Waislam. Alifanikiwa, kwanza, katika kuwaburuza kwenda Basra, viongozi wasiotaka kama vile Aisha, na majenerali “wapenda amani” kama vile Talha na Zubeir, Abdallah ibn Zubeir, na Marwan, na jeshi lao lote, njia nzima kuvuka jangwa kubwa la Arabia, na kisha, katika kuwachombeza wao kuanza mashambulizi juu ya jeshi la Ali. Waislam hawakuwa na shauku tu ya kumtii yeye; walikuwa pia na shauku ya kufa kwa ajili yake, na wengi walikufa, katika vita vya Basra. Lazima atakuwa alikuwa ni mtu mwenye haiba kubwa. Mtu hawezi kuacha kupenda ujasiri wake na nguvu zake za kushangaza.

Lakini licha ya haiba yake yote, na uwezo na umahiri wake, Abdallah ibn Saba anaonekana alikuwa ni mtu mwenye haya. Hii inathibitishwa na ule ukweli kwamba alikuwa na “mzio” wa kutangazwa. Mara tu baada ya ile vita ya Basra, alitumbukia kwenye giza, na haku- tokeza tena kamwe. Labda alikufa akiwa amesahaulika na bila kuombolezwa. Inawezekana vile vile kwamba wale “wakunga” waliokuwepo wakati wa kuzaliwa kwake, walikuwepo pia kwenye “mazishi” yake, na walikuwa wakidhania kwamba kazi yake ilikuwa imekamilika, na kwamba wangeweza kumzika, wasije kumfukua tena kamwe.

Vita vya Basra au vita vya Ngamia ni mmoja wa misiba mikubwa sana katika historia ya Uislam. Ilipiga pigo la mwisho kwenye umoja wa umma wa Waislam, na Uislam kamwe haukupona kutokana na kiwewe chake. Wanahistoria wengi wa Kiislam wanasimulia kisa cha vita vya Basra lakini wakati wakifanya hivyo wanajaribu kupunguza makali (kwa kutosisitiza) ya baadhi ya mambo muhimu, na wanajaribu kumbabaisha msomaji. Sababu yao ya kufanya hivyo ni kwamba wale viongozi wa maasi katika vita vya Basra walikuwa ni “masahaba” wa Mtume (s.a.w.w.), na kwa hiyo, ni lazima watolewe kwenye hatia yoyote ile au uhalifu. Hata hivyo, “hadhi yao maalum,” wanasema, inawapa haki ya kutende- wa hivyo.

Lakini uaminifu wa mwanahistoria lazima uwe kwenye ukweli, na sio kwa watu, hata kama ni “Masahaba” wa Mtume. Kazi ya mwanahistoria ni kuelezea mambo. Anaweza akayachanganua mambo, akayatafsiri, na akatoa majumuisho yanayohitimishwa kwayo lakini ni lazima asiyachezee.

Lazima amuwezeshe msomaji kujiamulia mwenyewe sifa za sahaba wa Mtume kwa msingi wa “ushahidi wa nyendo” zake badala ya kujaribu kuweka pazia la maneno ya ujanja ili kuficha madutu kwenye uso wake. Kushindwa kwa mwanahistoria kufanya hivi kuna maana kwamba anaficha Ukweli, kitu ambacho ni sawa na kutangaza Uwongo!

Kama vita vya Basra visingepiganwa, basi vita vya Siffin na Nahrwan pia visingepiganwa. Mbegu za mfarakano katika Uislam zilipandwa na zikachipua katika vita vya Basra. Kama Aisha, Talha na Zubeir wasingepinga utawala halali wa Waislam, milango ya utengano katika Uislam isingefunguliwa kamwe.

Viongozi wa maasi walikuwa watendaji huria. Uchaguzi wao ulipatikana kutokana na mchanganyiko wao binafsi wa tamaa, chuki, hatia na kijicho. Haikuwa ni uadilifu uliowachochea wao bali ni maudhi, maslahi binafsi na uchu wa madaraka vilivyojionyesha kama uungwana. Ushari wao ulidhihirika kuwa na matokeo ya kinyume sio tu kwa Waislam bali pia kwa wao wenyewe.

Hivi wanahistoria wa Kiislam walisita na kutafakari ni nini kingeweza kutokea kama hawa “watawala watatu” wa Basra wangekuwa washindi katika vita vyao dhidi ya Ali? Mambo mawili yangeweza kutokea katika tukio la kushinda kwao, yaani, (1) kwa kuchemkwa na hasira kama walivyokuwa, wangeweza kufanya hapo Basra katika mwaka 656 A.D. kile ambacho Yazid mtoto wa Mu’awiyah alikifanya katika mwaka wa 680 A.D. huko Karbala, yaani, wangewaua ovyo watu wote wa familia ya Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt.; na (2) baada ya ushindi wao dhidi ya Ali, wangemkabili Mu’awiyah bin Abu Sufyan, gavana wa Syria, katika mfungamano mpya wa majeshi.

Katika mfungamano huu mpya, Aisha, Talha na Zubeir wangekuwa kwenye upande mmoja, na Mu’awiyah na Amr bin al-Al-Aas upande mwingine. Ulimwengu wa Kiislam ungegawanyika katika kambi mbili hizi hasimu, na katika mapambano yatakayofuata ya mamlaka ya jeshi moja juu ya jingine, pande mbili hizo zingeangamizana.

Lazima izingatiwe na msomaji kwamba hakuna mmoja kati ya wapinzani hawa katika hii nadharia mpya ya mlinganyo, ambaye alikuwa “amekwazwa” kama alivyokuwa Ali, na ubinadamu wake na kujizuia, na pia kwa chuki yake kubwa kwenye umwagaji wa damu. Kwa hiyo, vita kati yao ingekuwa ya kishenzi na kikatili sana, na isiyodhibitiwa na “vizuizi” vyovyote vile kwa ajili ya utukufu wa damu ya Waislam. Ulimwengu wa Waislam ungekuwa umefunikizwa kwenye damu ukiacha pengo kubwa la madaraka. Kwenye pengo hili angeingia mfalme wa Byzantium (Roma) na jeshi lake, na wangeizima nuru ya Uislam!

Hawa “watawala watatu” kwa makusudi na kwa kutojali, walichokoza vita ambavyo vingeweza kuongezeka na kuwa balaa kubwa kwa umma wa Waislam. Kutokana na balaa hili linalowezekana, ilikuwa ni ufundi, busara, ubinadamu na weledi wa Ali katika utawala ambao uliokoa umma wa Muhammad. Mwenyezi Mungu amrehemu yeye na watu wengine wote wa Ahlul-Bayt Muhammad (s.a.w.w).

Inadaiwa pia na wanahistoria wengine kwamba “Masahaba wa Jamal” waliyajutia yale waliyoyafanya, na walikuwa “wametubia” kwa unyofu kabisa; kwa hiyo, hawana hatia kabisa. Inawezekana kabisa kwamba wale Masahaba wa Jamal walihitaji utakasaji – utaratibu wa “kutubia” – kuwatakasa na hisia zao za hatia. Lakini hakuna ushahidi wa “kutubia” kwao ambao umetufikia sisi. Ali alikuwa ametoa ukombozi kwao, sio mara moja bali kwa kurudiarudia, na walikuwa wameukataa.

Kama Masahaba wa Jamal walitubia, basi ni juu ya Allah (swt) pekee kukubali kutubia kwao. Allah (swt.) ataikubali toba yao kama walikuwa waaminifu. Lakini kukubaliwa na Allah swt. kwa toba yao hakutajulikana kwetu sisi mpaka Siku ya Qiyammah. Kazi ya mwanahistoria, kama ilivyoelezwa mapema, ni kutenga tu Ukweli kutoka kwenye rundo la Uwongo ambamo utakuwa umefichwa humo, na kisha kuueleza, kwa uwazi na usahihi.

Atatafsiri mambo lakini ni lazima asiyafiche au kuyazusha au kuyageuza kwa hofu yasi- jikuwa yanaonyesha picha isiyofaa ya watu anaowapendelea katika historia ya Uislam.

Baada ya vita hivyo, Ali aliwaswalia wafu wa majeshi yote mawili, na akawaagiza watu wake kuwazika maiti wote waliokuwa wamelala kwenye uwanja wa vita.

Maagizo yake kwao yalikuwa ni kuonyesha heshima kwa wale Waislam waliokufa wakiwa ama ni marafiki au maadui. Ilikuwa ni pale tu maiti wote walipokuwa wamekwishazikwa, ambapo aliweza kurudisha akili yake kwenye masuala mengine.

Ali Anaingia Basra

Mwanahistoria Mas’ud, “Herodotus wa Waarabu,” (Herodotus ni jina la mwanahistoria wa kwanza huko Ugiriki aliyepewa cheo cha – Baba wa historia, hivyo Mas’ud ni baba wa historia wa Waarabu), ameongeza mwishoni mwa kitabu chake, The Golden Meadows, mukhtasari ufuatao wa mwenendo wa jeshi la Ali lilipokuwa linaingia Basra. Ni kiangazio pia juu ya mfumo wake wa kijeshi, na nafasi ya Ansari ndani yake.

Mtu mmoja maarufu wa Basra aliniambia kwamba wakati lile jeshi lenye ushindi lilipokuwa linakaribia kwenye lango kuu la mji, alipanda juu ya ngome za ulinzi ili alione, na hiki ndicho alichokiona:

Kulikuwa na vikosi vingi vya askari wa farasi na askari wa miguu katika jeshi la Madina ingawa jeshi lenyewe lilikuwa ni dogo mno. Akitembea mbele ya kikosi cha wapanda farasi, kile cha kwanza ambacho kiliingia Basra, alikuwa ni mpanda farasi mmoja mtu mzima. Upanga ulikuwa unaning’inia ubavuni mwake, na alikuwa amebeba bendera ya kile kikosi alichokuwa anaongoza.

Niliulizia kwa watu wa karibu yangu yeye alikuwa ni nani na wao wakaniambia alikuwa ni Abu Ayub Ansari, yule rafiki na wakati mmoja aliyekuwa mwenyeji huko Madina, wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt. Kikosi chake cha wapanda farasi 1,000 kiliundwa na wapiganaji wa Ansari.
Nyuma yao, alikuwepo mpanda farasi mwingine. Alikuwa amevaa kilemba cha manjano iliyofifia na joho jeupe. Alikuwa amebeba upinde kwenye bega lake la kulia, na bendera ya kikosi chake kwenye mkono wake wa kushoto. Yeye pia alikuwa mbele ya wapanda farasi 1,000, na wao pia walikuwa Ansari. Yeye alikuwa, nilivyogundua, ni Khuzaima ibn Thabit Ansari.

Afisa wa tatu alikuwa amepanda farasi wa rangi ya hudhurungi mwenye nguvu sana. Alikuwa amevaa kilemba cheupe, akiwa ameshika upanga na upinde, na akiongoza kikosi cha wapanda farasi 1,000. Huyu alikuwa ni Abu Qatada ibn Rabi’i Ansari.

Afisa wa nne alikuwa amepanda farasi wa vita mzuri mweupe. Mavazi yake yalikuwa meupe na kilemba chake kilikuwa cheusi.

Alionekana kuwa mtu wa hadhi kubwa na maarufu, na alipandikiza heshima na unyenyekevu miongoni mwa waangaliaji wote. Alikuwa mzee sana lakini alikuwa na ukakamavu wa kijeshi. Alikuwa akisoma Qur’an huku akiwa amepanda farasi kuelekea mjini. Upanga ulining’inia ubavuni mwake, na upinde ukining’inia kutoka kwenye bega lake la kulia. Nyuma yake walikuwapo wapanda farasi 1,000. Walikuwa zaidi ni watu wazima, na wote walibeba mikuki mirefu mikononi mwao.

Nilipouliza yule alikuwa ni nani, niliambiwa kwamba alikuwa ni Ammar ibn Yasir, rafiki na mpendwa wa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na Ali ibn Abi Talib. Wakifuata nyuma yake, walikuwa ni Muhajirina na Ansari wote, na wengi wao walikuwa ni askari wakongwe wa Badr.

Jicho langu lilikamatwa baadae na mtu mwenye umbile zuri sana. Alikuwa amepanda farasi jasiri mwenye rangi mchanganyiko. Vazi lake lilikuwa jeupe na kilemba chake kilikuwa ni cheusi. Huyu alikuwa ni Abdallah ibn Abbas, binamu wa kwanza wa Muhammad Mustafa na Ali ibn Abi Talib. Pamoja naye walikuwa ni kaka zake na wapwa zake.

Mpaka wakati huu, takriban jeshi lote la farasi lilikuwa limeingia Basra, na niliona kwamba vikosi viwili vya mwisho vilikuwa vinakaribia lango la jiji. Sasa, cha kwan- za chao kilifika. Mbele yake alikuwepo mpanda farasi mwenye umbo imara. Alikuwa katika mavazi kamili ya kivita, na alitia hofu ndani ya nyoyo za wale wote waliomuona yeye. Alikuwa amebeba bendera nyeusi kwenye mkono wake wa kulia, na mkuki kwenye mkono wa kushoto.

Alionekana kama ndiye mshika bendera wa hilo jeshi ama afisa mwingine wa ngazi ya juu. Dhana yangu ilikuwa kweli. Alikuwa ni Malik ibn Ashtar, Mnadhimu Mkuu wa jeshi la Madina, na mtumia upanga hodari ambaye Arabia imewahi kutoa kamwe. Hakuna mshindani ambaye alikabiliana naye, aliyemkwepa kamwe. Aliongoza wapiganaji elfu nne wa wote wapanda farasi na wale wa miguu.

Mtu wa mwisho kupita katika uchunguzi alikuwa ni mpanda farasi aliyekuwa mwenye kung’aa kama jua. Katika upande wake wa kulia na wa kushoto kulikuwa na vijana wawili, kila mmoja aking’aa kama mwezi kamili. Wote watatu walikuwa wamevaa mazazi meusi.

Wale farasi wenye fahari na wanaorukaruka waliokuwa wamewapanda, walikuwa weusi pia. Kijana mwingine akiwa amebeba mkuki, alikuwa juu ya farasi mbele yao. Yule mtu aliyekuwa katikati, niligundua, alikuwa ndiye jemadari mkuu wa jeshi hili – Ali ibn Abi Talib. Wale vijana wawili upande wake wa kulia na kushoto, walikuwa wanawe, Hasan na Husein – matunda ya macho ya Muhammad (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt. Yule kijana aliyekuwa mbele yao , alikuwa pia ni mwanawe, Muhammad ibn Hanafiyyah.

Nyuma yao, kulikuwa na vikundi kadhaa vyingine vya watu wenye silaha. Wao walikuwa wakileta ulinzi wa nyuma ya jeshi hilo. Miongoni mwao walikuwemo watoto wa Jaafar Tayyar, watoto wa Aqiil ibn Abi Talib, na vijana wengine wa Bani Hashim. Walikuwa ndiyo wapanda farasi wa mwisho kuingia Basra.

Ali alishuka kutoka kwenye farasi wake pale kwenye lango la Msikiti Mkuu wa Basra. Aliingia ndani ya Msikiti huo, akaswali, na akamshukuru Allah swt., kwa Neema Zake, na kwa zawadi ya ushindi. Raia wa Basra walikuwa wamejikusanya kwenye uwanja wa Msikiti wakisubiri kuwasili kwa Ali. Sasa alitoka mle Msikitini ili kuwahutubia.

Aliwalaumu kwa tabia yao ya kutojali, wakati wote wa mapambano, na akawaambia:“Mlikuwa wafuasi wa mnyama. Aliponguruma mlimtii; pale alipouawa, wote mlikimbia, na mkatawanyika.”

Kisha Ali akachukua kiapo cha utii kutoka kwa raia wa Basra. Aliwashauri kumtii Allah na Mtume Wake wakati wote, na kamwe wasiwe tena kama kondoo wenye bumbuazi.

Kutoka pale Msikitini, Ali alikwenda kwenye hazina. Hazina hiyo ilikuwa imeporwa. Aliamuru mali yote iliyokuwa imeibiwa irudishwe kwenye hazina mara moja. Alipoitembelea hazina hiyo kwa mara ya pili baadae kidogo, aliona vipande vya dhahabu na fedha vimelundikwa rundo hapo chini. Alivitazama vilima hivi vidogo vya dhahabu na fedha, na akasema: “Jaribuni kumshawishi mtu mwingine.” Kisha yeye akamuagiza yule mtunza hazina kugawanya kila kitu kwenye vile vikosi. Mtunza hazina aligawa kila kitu, na hakuna kilichobakia kwenye hazina hiyo.

Kwa sababu fulani za kisirisiri, Ali na Maansari walikuwa wanaelewana tangu mwanzo. Na kwa sababu za kisiri kama hizo tu, Ansari hawakuweza kuelewana na Makuraish. Kulikuwa na uchangamfu kidogo sana, kama ulikuwepo kamwe, kati ya Makuraish na Ansari. Haikuwa mpaka Ali alipokuja kuwa khalifa ambapo Ansari waliweza, kwa mara ya kwanza tangu kifo cha rafiki yao, Muhammad (s.a.w.w.), kuwa na nafasi ya maana katika serikali ya Waislam.

Ali aliwateua kwenye vyeo vya juu kabisa ndani ya dola – vyote kama majemadari katika jeshi na kama magavana katika majimbo. Katika nyanja zote, Ansari walijidhihirisha wenyewe kwa uwezo wao na uadilifu wao.

Ali alifuta ile sifa ya “kijimbo” ya ukhalifa kwa “kuondoa Uquraishi” katika utawala wakati aliporudisha haki za Ansari kwao. Katika serikali yake, mtu hakuwa awe Quraish Iili kupanda katika cheo cha juu. Mtu yeyote – ama alikuwa Quraishi au la – aliweza kupanda kwenye cheo cha juu wakati wa ukhalifa wa Ali, kama angeweza kuwasilisha “vitambulisho” viwili – sifa na uwezo.