read

Vita Vya Hunain

Kule kutekwa kwa Makka kulichochea uingiaji kwa wingi wa Waarabu kwenye Uislamu katika sehemu nyingi za nchi hiyo. Lakini yalikuwepo baadhi ya makabila yaliyokuwa yakiishi Mashariki na Kusini-Mashariki ya Makka ambayo hayakutaka kuacha uabudu masanamu. Walitishiwa na maendeleo ya haraka ya Uislamu, na walifikiria kwamba kama utaendelea kuenea kwa kasi hiyo hiyo, watazungukwa na Waislamu hivi karibuni, na watakuwa wametengwa na makabila mengine ya wapagani.

Viongozi wao waliwaza kwamba haitakuwa busara kuwaacha Waislamu waunganishe mafanikio yao ya hivi karibuni na kuwa na nguvu sana. Wao, kwa hiyo, waliamua kuchukua hatua mara moja kwa kuwashambulia Waislamu huko Makka na kuwaagamiza. Makabila makubwa miongoni mwao yalikuwa ni Thaqiif, Hawazin, Bani Sa’ad na Banu Jashm, wote wapiganaji wakali, wenye wivu na uhuru wao na wenye fahari na mila zao za kivita.

Walikuwa wamefahamu kwamba Makka imesalimu amri kwa Muhammad bila ya kufanya shambulio lolote lakini walihusisha kule kushindwa kwa watu wa Makka kukataa kuswalimu amri kwake na tabia yao ya kike. Na kwa upande wao wenyewe, walikuwa na imani kwamba walikuwa na uwezo zaidi katika uwanja wa mapambano kuliko wapiganaji wa Kiislam au wapiganaji wowote wengine.
Mwishoni mwa Januari 630, Mtume (s.a.w.) alipokea taarifa kwamba kabila la Thaqiif na Hawazin walikuwa wameondoka kwenye kituo chao cha nyumbani, na walikuwa wanakwenda kuelekea Makka. Wakati habari hizi zilipothibitishwa, yeye pia aliagiza ukusanyikaji wa jumla ndani ya ule mji uliotekwa hivi karibuni.

Mtume (s.a.w.) hakutaka Makka igeuke uwanja wa mapambano.Yeye, kwa hiyo, haraka sana akaondoka Makka mnamo Januari 26,630 akiongoza wapiganaji 12,000, kwenda kukutana na adui. Kutoka kwenye jeshi hili, watu elfu kumi walikuwa wanatoka Madina, na wale wengine elfu mbili walikuwa ni askari wapya kutoka watu wa Makka waliosilimu hivi karibuni.

Jeshi hili jipya lilikuwa ndio jeshi kubwa sana liliwahi kukusanywa katika Arabia mpaka wakati ule. Wakati mipangilio yake mbali mbali ilipokuwa inatoka nje ya lango la mji, katika mavazi maridadi ya kivita, Abu Bakr aliyekuwa anaangalia, alivutiwa sana, na akatamka ghafla: “Hatuwezi kushindwa safari hii kwa sababu ya kukosa wingi.” Lakini mapema sana akathibitika kwamba amekosea. Waislamu walishindwa mwanzoni ingawa walikuwa mara tatu ya wingi wa adui. Qur’an yenyewe ilitaka tahadhari ya Waislamu, kwa uwazi hasa, kwamba wingi peke yake haukuwa hakikisho kwamba watakuwa washindi.

Sir William Muir

Majuma manne yalikuwa yamepita tu tangu yeye (Muhammad) alipokuwa ametoka Madina, wakati aliposonga mbele kutoka Makka akiongoza vikosi vyake vyote, vikiwa vimetuna sasa, kwa kuongezeka kwa kikosi cha kuongeza nguvu kutoka Makka, kwenye idadi kubwa ya watu 12,000. Safwan, kwa maombi yake, alimpatia yeye suti mia moja za deraya na kibanda kizima cha silaha kamili na ngamia wengi kiasi. Ule mpango wa askari wa makabila, kila moja likiwa na bendera inayopepea mbele yake, ulikuwa wa kushangaza sana kiasi kwamba Abu Bakr alianza ghafla, wakati vile vikosi vilivyopangwa vilipopita, kwa ugutaji huu wa ghafla: “Leo hii hatutashindwa kwa sababu ya uchache wa idadi yetu.”
(Life of Muhammad, London, 1861)

Wakati ile safu ya kwanza iliyokuwa na kikosi cha Waislamu, kikiongozwa na Khalid ibn al-Walid, kilipoingia kwenye bonde la Hunain upande wa Kusini-Mashariki ya Makka, adui tayari alikuwa amelala kwenye mavizio, tayari kukipokea kwa silaha zake za makombora. Mwanya ulikuwa mfinyu sana, njia ilikuwa mbaya sana, na Waislamu walikuwa wanasonga mbele dhahiri kwa kutotambua kuwepo kwa adui. Ilikuwa kabla tu ya mawio wakati kwa ghafla tu, Hawazin walipoanzisha shambulizi lao.

Fumanizi hili lilikuwa halikutegemewa kabisa na shambulizi la adui lilikuwa la haraka sana kiasi kwamba Waislamu hawakuweza kulihimili. Kikosi hicho, kilichoundwa na watu wa kabila la Banu Sulaym, kilivunjika na kikakimbia. Sehemu kubwa ya jeshi hilo ilikuwa nyuma kidogo tu. Safu ya Khalid ilipata pigo usoni mwake, na likatia hofu ndani ya watu wake hivyo kwamba wao pia waligeuzia migongo yao kwa adui. Na wakaanza kukimbia. Mara kila mtu katika jeshi hilo alikuwa anakimbia, na haikuchukua muda kabla Muhammad hajaachwa peke yake pamoja na wafuasi wake waaminifu wachache karibu yake.

Watu waliokuwa wakiongozwa na Khalid ndio wa kwanza kukimbia mbele ya maadui wanaoshambulia, na walifuatiwa na wale Umayya wa Makka waliosilimu hivi karibuni na marafiki zao na wafuasi wao. Nyuma yao walikuwa raia wa Madina. Waislamu wengi wal- iuawa katika kukimbia huko, na wengine wengi walijeruhiwa. Mtume (s.a.w.) aliwaita wale watoro lakini hakuna hata mtu mmoja aliyemsikiliza.

Jeshi la Waislamu lilikuwa katika msambaratiko wa kukimbia bila mpango na adui wakiwa kwenye kasi kali ya kuwafukuza. Mtume, kwa kweli, hakuondoka kwenye nafasi yake, na alisimama imara kama jiwe. Watu nane walikuwa bado wako naye, wote wakitazama kioja cha kukimbia kwa jeshi lao. Walikuwa ni:

1. Ali ibn Abi Talib

2. Abbas ibn Abdul Muttalib

3. Fadhil ibn Abbas

4. Abu Sufyan ibn al-Harith ibn Abdul Muttalib

5. Rabi’a, kaka yake Abu Sufyan ibn al-Harith

6. Abdullah ibn Masood

7. Usamah ibn Zayd ibn Haritha

8. Ayman ibn Ubaid

Kati ya hawa nane, watano wa mwanzo walikuwa ni wa ukoo wa Banu Hashim. Walikuwa ni ami zake na binamu zake Mtume.

Mtume (s.a.w.) alimwomba ami yake, Abbas ibn Abdul Muttalib, kuwaita wale Waislamu waliokuwa wanakimbia. Abbas alikuwa na sauti yenye nguvu sana, na akaguta: “Enyi Muhajirina na Enyi Ansari! Enyi washindi wa Badr na enyi watu wa Mti wa Kiapo! Mnakwenda wapi? Mtume wa Allah (s.a.w.) yuko hapa. Rudini kwake.”

Sauti ya Abbas ilivuma katika lile bonde finyu na karibu kila mtu aliisikia, na ilionekana kuwa na matokeo katika kusimamisha kukimbia kwa Waislamu.

Ansari walikuwa wa kwanza kusimama, na kurudi kwenye vita. Wakitiwa moyo na mfano wao, wengine pia walipata nguvu tena. Mara wakaweza kujikusanya tena. Mapambano makali yalitokea. Mwanzoni, matokeo yalionekana kutokuwa na uhakika lakini baadae Waislamu walianza kuwabana maadui. Mara tu waliporudisha hamasa zao, wakafanya mashambulizi. Adui bado alipigana kijasiri lakini wakazuiwa katika usogeaji wao na ile adadi kubwa ya wanawake na watoto aliokuja nao. Waislamu walizidi kusonga mbele na baadae ilikuwa ni Mabedui ambao walikuwa wanakimbia pande zote.

Sir William Muir ameielezea Hadith ya kushindwa na kupata nguvu tena kwa Waislamu katika vita vya Hunain kwa kirefu kiasi. Anaandika katika kitabu chake, The Life of Muhammad, (London, 1877) hivi:

Mapema sana wakati wa asubuhi, ambapo alfajiri ilikuwa bado ya rangi ya kijivu, na anga ikiwa imetanda mawingu, jeshi la Muhammad lilikuwa kwenye mwendo. Akiwa amevaa mavazi kamili ya kivita, kama kwenye siku ya Uhud, alipanda juu ya farasi wake mweupe, Duldul, nyuma ya vikosi vyake.

Kikosi kilichoundwa na Banu Sulaim na kikiongozwa na Khalid, walikuwa wakipanda kwa msururu taratibu juu ya njia ya mlimani ya mteremko na nyembamba, wakati ghafla Hawazin walipochupa kutoka kwenye mavizio yao, na wakawashambulia kwa kasi. Wakibumbuazwa na uvamizi huu wa ghafla, Banu Sulaim walikatika na kurudi nyuma. Mshituko huu ulipita kutoka safu hadi safu. Wakikerwa na utusitusi wa saa hizo, na wembamba na mikunjokunjo ya njia, hofu ikalishika jeshi lote; wote waligeuka na wakakimbia. Jinsi kikosi kwa kikosi walivyoharakisha kumpita yeye, Muhammad alikemea: “Mnakwenda wapi? Mtume wa Allah (s.w.t.) yuko hapa! Rudini! Rudini! – lakini maneno yake hayakuwa na athari yoyote, isipokuwa kikun- di cha marafiki na wafuasi waliojitolea walijikusanya karibu naye.

Kiwewe kiliongezeka, kundi la ngamia lilisukumana bila mpango mmoja dhidi ya mwingine; ilikuwa kelele tupu na ghasia, na sauti ya Muhammad ilipotea katikati ya mshindo huo. Mwishoe, walipoona zile safu za vikosi vya Madina vikiondoka katika kukimbia kwa pamoja, alimuambia ami yake, Abbas, aliyekuwa ameshikilia farasi wake, kuita kwa sauti kubwa: “Enyi watu wa Madina! Enyi wa Mti wa Kiapo! Enyi watu wa Surat Baqra !” Abbas alikuwa na sauti yenye nguvu sana, na alipoguta maneno haya tena na tena kwa sauti yake yote, yalisikika mbali na karibu. Mara moja yakagusa hisia katika nyoyo za watu wa Madina.

Walizuiwa katika kukimbia kwao, na wakaharakisha kwa Muhammad, wakipiga kelele, “Ya Labeik! Sisi tuko hapa kwa mwito wako!” Watu mia moja kati ya hawa wafuasi watiifu, walijinasua kwa taabu kutoka kwenye wale ngamia waliokuwa wameziba ile njia finyu, wakajitupa juu ya adui aliyekuwa anasonga mbele na kusimamisha maendeleo yake. Lilipopata nafuu kutokana na shinikizo, lile jeshi lilipata nguvu polepole, na likarudi kwenye vita. Mapambano yalikuwa makali; na matokeo, kutoka na ubaya wa asili wa ardhi na kishindo cha Mabedui wakali, yalibakia kwa muda kiasi ya mashaka. Muhammad ali- panda kwenye kilima na akaangalia yale mapambano. Akitiwa nguvu na yale mandhari, alianza kuguta kwa sauti kubwa; “Sasa ndio tanuru limepata moto: Mimi ni yule Mtume asiyesema uongo. Mimi ni kizazi cha Abdul Muttalib.”

Kisha akimuagiza Abbas kumuokotea ukofi wa changarawe, aliutupa kuelekea kwa maadui, akisema, “Maangamizi yawakamate hao!” Walikuwa kwa kweli tayari wamekwishayumba. Uimara wa kikosi cha Madina, na shauku ya wale waliobakia wakati pale walipoitwa tena, ulikuwa umepata ushindi. Adui alikimbia, na ushindi ulikuwa kamili. Wengi waliuawa na kwa nguvu sana Waislamu waliendeleza mashambulizi, kiasi kwamba waliuwa miongoni mwa waliobakia, baadhi ya watoto wadogo – ukatili ambao Muhammad alikuwa ameukataza kabisa.

Betty Kelen

Waislamu waliweka kambi mbali na Bonde la Hunain na wakati wa alfajiri wakam- sogelea adui kupitia kwenye njia nyembamba. Mtoto wa Umar anaelezea kile kilichotokea baadae:

“Tuliteremka kupitia kwenye korongo kavu la mto, pana na lenye mteremko tukishuka polepole katika mwanga hafifu wa asubuhi; lakini adui alikuwa pale kabla yetu na alikuwa amejificha katika vinjia vidogo, njia za pembeni na sehemu finyu.

Walikuwa katika jeshi, wakiwa na silaha kamili wakijua hasa ni nini cha kufanya, na Wallahi, tulikuwa na hofu wakati tuliposhuka na ghafla Hawazin walitushukia kama mtu mmoja!

Mabedui walishambulia kwa mawe, majabali, mishale, mikuki na panga. Kile kikosi cha Muhammad, chini ya jenerali Khalid, kilivunjika, ngamia wakasukumana na kugongana, wakilia kwa mikwaruzo na kusongamanisha miguu yao mirefu.

Yeye Muhammad aliona miongoni mwa wale watu wanaokimbia, wafuasi wake wapya kutoka Makka, na aliwaita wao kama mmoja wao wenyewe: ‘Mnakwenda wapi enyi watu? Rudini! Njoni kwangu! Mimi ni Mtume wa Allah (s.w.t.) Mimi ni Muhammad, mtoto wa Abdullah!’

Sio hata mmoja aliyesikiliza, na kwa nini wasikilize? Alikuwepo mpiganaji wa Hawazin akiwafukuza akiwa juu ya ngamia wa rangi ya damu ya mzee, bendera yake ikipepea kutoka kwenye mkuki mrefu, na kila wakati alipoutumbukiza ubapa wa mkuki ule, ulichomoza upande mwingine wa kifua cha mtu.

Sauti ya Mtume (s.a.w.) ilizama kwenye makelele ya watu, na milio ya ngamia. Alimuambia ami yake Abbas, mtu mwenye mapafu makubwa, kuchukua huo mwito, ‘Enyi marafiki, ukumbukeni ule mti wa mkangazi…’

Na Ali, akiwa kimya kabisa lakini katika mapambano kama jinni mkali, alirukaruka kiushindi karibu yake, akipigania kufika nyuma ya farasi wa yule kiongozi wa Hawazin na kumlemaza.
(Muhammad, Messenger of God)

Muhammad Husein Haykal

Waislamu walifika Hunain wakati wa jioni na wakaweka kambi kwenye mlango wa bonde hilo mpaka alfajiri. Wakati wa alfajiri siku iliyofuata jeshi hilo lilianza kuondoka, na Muhammad, akiwa amempanda farasi wake mweupe, alikuwa nyuma wakati Khalid ibn al-Walid, akiongoza kikundi cha askari kutoka Banu Sulaym, alikuwemo kwenye kikosi hicho.

Wakati Waislamu walipokuwa wanapita kwenye korongo la Hunain, Malik ibn Awf aliamuru jeshi lake kushambulia katika giza kabla ya alfajiri, kwanza kwa mishale na kisha kwa shambulizi la jumla. Safu za Waislamu zikavunjika na waliingiwa na hofu. Baadhi yao walikimbia kutoka nje ya korongo hilo haraka sana kama walivyoweza katika kutafuta usalama. Akishuhudia kile kilichowakuta Waislamu, Abu Sufyan hakuhisi kutokuwa na furaha hata ndogo kwa kushindwa maadui zake wa awali ambao mpaka sasa walikuwa wakisherehekea ushindi wao juu ya Makka. Alisema, “Waislamu hawatadhibitiwa mpaka wawe wametupwa ndani ya bahari.”(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Makabila ya kipagani yalishindwa lakini yaliweza kujikusanya tena, na yanasemekana kuweza kurudi nyuma kwa mpango mzuri kutoka kwenye bonde la Hunain.

D.S.Margoliouth

Jenerali Malik, mtoto wa Auf, anasemekana kukusanya wapanda farasi wake wa kutosha kufanya waweze kusimama imara mpaka watu dhaifu wa kundi lao wawe wamekingwa, na kisha waweze kuwafikisha kwenye usalama kwenye kilima ambapo wanaweza kupata njia yao ya kwenda Taif. Pale ni dhahiri baadhi ya wanawake waliokolewa, ingawa wengine waliangukia kwenye mikono ya Waislamu.

Khalid mtoto wa al-Walid, ambaye ukatili wake tayari ulikwishapata karipio kutoka kwa Mtume, alipata jingine kwa kufikiri kwamba ni kazi yake kuwaua hawa majikedume; kitendo ambacho kilikuwa kinyume kabisa na dhana za Mtume (s.a.w.) za ushujaa.

Kama vile tu alivyoona ni muhimu kuwakaripia wengine ambao walifikiria ni wajibu wao kuwaua watoto wa makafiri. “Ni nini kilicho bora chenu,” aliuliza, “kama sio watoto wa makafiri?”

Mafanikio ya muhimu sana yalipatikana, na ubashiri wa Mtume (s.a.w.) ulithibitika kuwa thabiti katika wakati ambapo kinyume chake kingeweza kuwa na matokeo mabaya; kwani Abu Sufyan angeweza kuwa na uwezo wa kutumia fursa ya janga, ingawa lisiwe lenye nguvu sana, kuweza kusababisha jingine. (Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Hunain ilikuwa ni vita iliyoongozwa binafsi na Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.) mwenyewe. Vita vilianza na kushindwa kwa Waislamu, na walikimbia njia ya kila upande ili kuokoa maisha yao wenyewe, bila kutambua kabisa kuwepo, katika uwanja wa mapambano, kwa Mtume (s.a.w.) wao. Mwishoni, hata hivyo, walikuwa washindi, shukrani kwa ujasiri na ushupavu wa Mtume (s.a.w.) mwenyewe na wachache kati ya jamaa zake.

M. Shibli, mwanahistoria wa Kihindi, anaandika katika kitabu chake cha wasifu wa Mtume: Badala ya ushindi (wa Waislamu) mtu anaweza kuona kushindwa kwao (katika vita vya Hunain). Mtume (s.a.w.) alitazama pote na hakuona mtu yeyote pamoja naye isipokuwa wachache wa marafiki zake. Abu Qatada, sahaba mmoja, ambaye alikuwepo huko Hunain, anasema kwamba wakati jeshi lilipokuwa linakimbia, alimuona Umar ibn al-Khattab, na akamuuliza: “Ni hali gani ya mambo ya Waislamu?” Yeye akasema: “Hayo ni Mapenzi ya Allah (s.w.t.)”
(The Life of the Prophet {Siraatun-Nabi, juz. 1, uk. 535-536}, 1976, Azamgarh, India).

Sir William Muir

Kinyume kilichopatikana mwanzoni mwa siku hiyo, kilihusishwa na Mtume (s.a.w.) na matumaini ya kujiona ambayo kwayo waumini walitegemea juu ya jeshi lao kubwa. Mafanikio ya baadae sawasawa yalipachikwa kwenye msaada wa wa jeshi lisiloonekana ambalo lilipigana dhidi ya adui yao. Shambulio hilo limegusiwa hivi kwenye Qur’an:“

Hakika Allah amewasaidieni kwenye medani za vita nyingi: na katika siku ya Hunain, wakati kwa kweli mlifurahia katika wingi wa jeshi lenu. Lakini idadi yao kubwa kwa namna yoyote ile haikukunufaisheni ninyi: ardhi ilikuwa finyu sana kwenu pamoja na upana wake wote. Kisha mligeuza migongo yenu na mkakimbia.” (The Life of Muhammad, London, 1877, uk.143)

“Majeshi yasiyoonekena” ambayo yaliwasaidia Waislamu, ina maana, katika muktadha huu, nguvu ya hali ya juu. Mwanzoni mwa vita hivyo, walishindwa na kufukuzwa. Lakini walitiwa moyo na mfano wa Mtume (s.a.w.) mwenyewe ambaye ujasiri wake uliwarudishia hamasa yao, na walimpiga adui kwa ari na nguvu mpya.

Vita vya Uhud vilianza kwa ushindi wa Waislamu na viliishia na kushindwa kwao; vita vya Hunain vilianza na kushindwa kwao na vikaishia na ushindi wao. Kulikuwa na mauaji makubwa kwa Waislamu wakati wa mwanzo ambayo yalisababishwa na hofu yao wenyewe na kukosa ushupavu.

Muhammad Husein Haykal

Ushindi haukupatikana kirahisi. Waislamu walilipa gharama kubwa sana. Wangeweza kuimudu kwa gharama ndogo kama wasingerudi nyuma hapo mwanzoni na kus- ababisha kauli ya dhihaka ya Abu Sufyan kwamba watakuwa watupwe baharini. Ingawa vitabu vya msingi wa rejea havikuorodhesha wale wote waliouawa katika vita hivyo, vimetaja kwamba makabila mawili ya Kiislam yalikuwa karibu yote yameangamizwa kabisa, na kwamba Mtume (s.a.w.) aliendesha Swala ya jeneza kwa ajili yao. Kufidia sehemu ya hii hasara kubwa ya maisha ya watu, ni yale mamlaka yasiyo na shaka ushindi uliyoyaleta kwa Waislamu. Zaidi ya hayo, ushindi ulileta mateka na ngawira zaidi kwa ajili yao kuliko walivyowahi kuona hapo kabla. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Ali Na Vita Vya Hunain

Shujaa wa vita vya Hunain alikuwa ni Ali ibn Abi Talib kama vile alivyokuwa shujaa wa vita vyote vilivyotangulia. Katika wakati ambapo maswahaba wote walikimbia kutoka kwenye medani ya vita, na watu wanane tu walikuwa wamebaki na Mtume, alikuwa ni Ali aliyesimama kati yake na adui, na akamkinga yeye. Makabila yalishambulia kwa kurudia lakini aliyarudisha nyuma kila wakati sawa na alivyokwisha kufanya huko Uhud. Kwa wakati fulani, ilikuwa ni Uhud tena.

Mwishowe, Ali alifanikiwa katika kuugeuza mwelekeo wa vita hivyo. Kwanza alimsababisha Uthman bin Abdullah, mmoja wa viongozi wa adui, kuanguka kutoka kwenye ngamia wake, kuyumba, na kuuawa; na baadae, alimuua, katika pambano la mkono kwa mkono, Abu Jerdel, kiongozi wa Hawazin. Wakati majenerali hawa wawili walipokuwa wameuawa, adui alivunjika moyo, akashindwa vita.

M.Shibli

Banu Malik wa kabila la Thakiif walipigana kwa ujasiri wa makusudi lakini pale kiongozi wao, Uthman ibn Abdullah, alipouawa, walianza kuyumba... (The Life of the Prophet, Azamgarh, India, 1976)

Abu Sufyan, mkuu wa Bani Umayya, alikuweko kwenye kambi ya Waislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ingawa alikwisha “kuukubali” Uislamu, alivutiwa na kusisimka kuona kule kukimbia kwa Waislamu, na akawa na matumaini kwamba watatupwa baharini. Wakati Hikda bin Umayya, “Mwislam” mwingine wa ukoo wa Bani Umayya, alipoona ukimbiaji wa Waislamu, pale mwanzoni mwa vita, alitamka: “Hatimae uchawi wa Muhammad umevunjika.” Wote lazima watakuwa wamebuni, katika fikra zao, picha za kumrudisha Hubal, mungu wao wa jadi, kwenye kiti chake ndani ya Al-Kaaba.

Abu Sufyan na watu wengine wa ukoo wake, hawakuweza kuficha furaha zao wakati kwao wao ilionekana kana kwamba Waislamu walikuwa wameshindwa na watu wa makabila ya wapagani. Lakini furaha yao ilidhihirika kuwa ya kudumu kwa muda mfupi sana. Baadae kidogo kulikuwa na mabadiliko katika matokeo ya vita hivyo, na kisha ilikuwa ni hawa wapagani ambao mwishowe na kwa uwazi kabisa walioshindwa. Kinyume hiki lazima kiwe kilisababisha kijicho kikubwa sana kwa Abu Sufyan na jamaa wa ukoo wake vile walivyopoteza matumaini ya mwisho, mazuri kabisa waliyokuwa nayo ya kufufua “Zama za Ujahilia.”

Jamaa wa kabila walikuwa wameacha mizigo yao yote na maelfu ya wanyama wao. Mtume (s.a.w.) aliamuru mizigo hiyo ikusanywe, wanyama hao wakusanywe na kupelekwa Jirana, sehemu ya katikati baina ya Taif na Makka, na iwekwe hapo kusubiri kuwasili kwake yeye mwenyewe. Kwa wakati huo, aliamua kuiteka Taif ambayo bado iliendelea kubaki kama ngome ya mwisho ya makafiri, na akaamuru sehemu kubwa ya jeshi kutem- bea kuelekea kwenye mji huo. Wale watoro toka kwenye vita ile pia walikuwa wamepata hifadhi kwenye ngome ya Taif.

Akiwa njiani kuelekea Taif, Mtume (s.a.w.) alipita kikundi kidogo cha watu waliokuwa wamesimama karibu na mwili wa mwanamke aliyeuawa. Katika kuuliza, aligundua kwam- ba aliuawa na Khalid bin al-Walid.

Muhammad ibn Ishaq

Mmoja wa maswahaba alituambia kwamba Mtume (s.a.w.) siku ile (mara baada ya vita vya Hunain) alipita karibu na mwanamke ambaye alikuwa amemuawa na Khalid bin al-Walid ambapo watu walikuwa wamekusanyika karibu yake. Wakati aliposikia yaliyotokea, alituma ujumbe kwa Khalid na kumkataza kuua mtoto, mwanamke au mtumwa aliyekodiwa. (The Life of the Messenger of God)

Mtume (s.a.w.) alizingira Taif lakini haikufanikiwa na ikaachwa. Taif, hata hivyo, ilisalimu amri kwa hiari majuma kadhaa baadae.

Kutoka Taif, Mtume (s.a.w.) alikwenda Jirana kugawanya ngawira za vita ambazo ziliku- sanywa katika uwanja wa Hunain. Sehemu aliyompa Abu Sufyan na wanae, wakuu wa ukoo wa Bani Umayya, ilikuwa kubwa zaidi kuliko sehemu aliyompa mtu mwingine yoyote katika kambi ya Uislamu. Bani Umayya hawakuweza kuamini kwamba walikuwa na bahati nzuri kama hiyo.
Abu Sufyan, ambae alikuwa na sababu nzuri ya kutarajia kidogo kuliko chochote, baada ya “utendaji” wake katika vita vya Hunain, aliguswa sana na ukarimu wa Mtume, na akaongea naye kwa shauku: “Wewe umkarimu katika vita sio chini ya ulivyo mkarimu kwenye amani.”

Mustashriq wengine wamemaanisha kwamba ile sehemu ambayo Mtume (s.a.w.) aliyotoa kwa Abu Sufyan na wanae, ilikuwa kwa kweli ni hongo la kuwabakisha wawe Waislamu, na kwamba hapakuwa na njia nyingine yoyote ambayo angeweza kupatia utii wao. Wao wanasema zaidi kwamba Mtume (s.a.w.) kamwe hakusita kuwahonga waabudu masanamu kama alidhani kwamba wangeuza imani zao kwake kwa kubadilishana na ngamia, kondoo, na vipambo vidogodogo na vitu vizuri vyenye thamani ndogo.

Sisi hatukubaliani nao. Baada ya kutekwa Makka, Abu Sufyan, wanae na watu wengine wa ukoo wa Bani Umayya, walikuwa chini ya huruma ya Muhammad. Angeweza kuwaangamiza wote, na waabudu masanamu wote wa Arabia wasingeweza kufanya lolote kuwaokoa. Haikuwa lazima kwake kuwahonga wao au mtu mwingine yeyote katika kuukubali Uislamu.

Kusilimu kwao kulikuwa na thamani ndogo kwa Uislamu vyovyote vile. Katika kutoa zawadi juu ya Abu Sufyan na wanae, Mtume (s.a.w.) wa Uislamu alikuwa akidhihirisha tu chaguo lake kutoka kwenye ulipizaji wa kisasi. Kwa Waarabu, itakumbukwa, ulipizaji wa kisasi ulikuwa ni tabia yao mbaya. Alijaribu kumaliza uadui wao kwa Uislamu kwa upole wake na ukarimu. Zawadi hizo zilikuwa ni ishara ya mfano wa mwelekeo huu tu.

Abu Sufyan, watoto wake na watu wengine wa Bani Umayya – wapokeaji wa zawadi hizo, waliitwa, daima baadae Muallafa Qulubuhum – wale wenye kuimarishwa nyoyo zao. Mtume (s.a.w.) aliwapa maadui zake sehemu kubwa kutoka kwenye ngawira kwa ajili tu ya Taliif al-Qulub – kuimarisha nyoyo zao.

Dr. Muhammad Hamidullah anasema katika kitabu chake, Introduction to Islam, uk. 80, (1977): Wale ambao nyoyo zao ni za kuimarishwa ni wa namna nyingi. Faqihi mkuu, Abu Ya’la al-Farra, anaonyesha: “Na kwa wale ambao nyoyo zao ni za kuimarishwa, wapo wa aina nne:

1. Wale ambao nyoyo zao ni za kupatanishwa kwa kuja kwao kwenye msaada wa Waislamu;

2. Wale ambao nyoyo zao ni za kuimarishwa ili kwamba wajiepushe na kufanya madhara kwa Waislamu;

3. Wale wanaovutiwa kwenye Uislamu;

4. Wale ambao kwa kuwatumia wao kuingia kwenye Uislamu kunakuwa na uwezekano kwa watu wa makabila yao.

Ni halali kunufaisha kila moja ya makundi haya ya ‘wale ambao nyoyo zao ni za kuimarishwa’ wawe Waislamu au washirikina.” Abu Sufyan na ukoo wake walikuwa ni wa kundi lile la pili; nyoyo zao “zilikuwa ziimarishwe ili kwamba wataweza kujie- pusha kutokana na kufanya madhara kwa Waislamu.”

Maansari Na Ngawira Za Hunain

Baadhi ya vijana wa Ansari walikuwa hawakuridhika na kile walichokiona kuwa ni ugawaji “usio haki” wa ngawira za vita. Wachache miongoni mwao walinung’unika kwamba wakati ulipofika wa kugawa ngawira, Mtume (s.a.w.) alifanya “upendeleo” kwa Maquraishi. Wakati Mtume (s.a.w.) alipolisikia hili, aliamuru Ansari waku- sanyike katika hema, na akawahutubia hivi:

“Ni nini hiki ninachokisikia kutoka kwenu, Enyi Ansari, kuhusu ugawaji wa ngawira? Mmefadhaika kwa sababu nimetoa sehemu kubwa ya ngawira kwa watu wa Makka kuliko niliyowapeni ninyi? Lakini hebu niambieni hili: hivi sio kweli kwamba mli- abudu masanamu na Allah (s.w.t.) akawapeni mwongozo kupitia kwangu mimi? Hivi sio kweli kwamba mlitenganishwa na ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe na Allah (s.w.t.) akawaunganisha kupitia kwangu mimi? Sio kweli kwamba mlikuwa masikini na Allah (s.w.t.) akawafanyeni matajiri kupitia kwangu mimi?” Katika kujibu kila swali, Ansari walisema: “Ndio, hivyo ndivyo ilivyo, na ni neema ya Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.).”

Lakini maswali haya yalikuwa ni balagha tu – maswali yasiyohitaji majibu – na Mtume wa Allah (s.a.w.) mwenyewe aliyajibu.

Sir William Muir

“...Lakini nyie mngeweza kujibu (na mkajibu kwa dhati, kwani ningehakikisha hilo mimi mwenyewe) – ulikuja Madina ukiwa umekanwa kama mlaghai, na tukashuhudia ukweli wako; ulikuja kama mkimbizi asiye na msaada na tukakusaidia wewe; mtu aliyetengwa na jamii, nasi tukakupa hifadhi, ukiwa fukara, nasi tukakufariji wewe. Kwa nini mnachanganyikiwa akilini kwa sababu mambo ya maisha Haya, kwa hili nilitafuta kuelekeza nyoyo za watu hawa (Maquraishi wa Makka) kwenye Uislamu, ambapo ninyi tayari mko imara kwenye imani zenu? Hamridhiki ninyi kwamba wengine wapate hayo makundi ya mifugo na hao ngamia, ambapo ninyi mnamchukua Mtume wa Allah (s.w.t.) kurudi naye majumbani kwenu? Hapana, mimi sitawaacheni ninyi milele. Kama wanadamu wote wangekwenda njia moja, na watu wa Madina njia nyingine, hakika, ningekwenda ile njia ya watu wa Madina. Mola awe mwema juu yao, na awabariki wao, na watoto wao na watoto wa watoto wao milele.” (The Life of Muhammad, London, 1861)

Wakati Ansari waliposikia maneno haya, waligubikwa na machozi, na wakapaza sauti: “Waache wengine wachukue hao kondoo, ng’ombe na hao ngamia waondoke nao. Tunachokitaka sisi ni Muhammad, na sio kitu kingine chochote.”

Ansari walipatwa pia na hofu kwamba Mtume (s.a.w.) angeweza kuamua kuishi hapo Makka, na kupafanya makao yake makuu. Lakini aliwahakikishia kwamba yeye kamwe hatawaacha wao au Madina, na kwamba yeye na wao hawatenganishiki milele.

Kutoka Jirana, Waislamu walirudi Makka ambako Mtume (s.a.w.) alifanya ile mizu guko saba ya Al-Kaaba, na akatekeleza ibada za Hijja Ndogo (Umra).

Vita vya Hunain vilikuwa ndio “limbuko” la mwisho la Arabia ya upagani. Wakati Waislamu walipopata ushindi, pazia hatimae likaanguka kwenye dibaji ya ushenzi na upagani, ya mfululizo wa matukio ya historia ya Arabuni. Lakini wapagani au kwa usahihi zaidi, watetezi wa siri wa upagani wa Kiarabu walikuwa bado wapigane mapigano, ya jeshi linalorudi nyuma, na askari, marefu na magumu, dhidi ya Uislamu.

Hapo Makka, Mtume (s.a.w.) alitoa maelekezo ya mwisho kwenye mambo yanayohusu uongozi na sera. Kabla ya kuondoka Makka kwenda Madina, alimteua Akib bin Usayd kama gavana wa mji huo. Huu ulikuwa ndio uteuzi wa kwanza wa kudumu wa kiserikali katika Uislamu. Yeye pia aliutangaza mji wa Makka kuwa makao makuu ya kidini ya Kiislam.

Baada ya kumaliza mwezi mzima wenye matukio mengi hapo Makka na viungani mwake, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) na jeshi lake, walirudi Madina.

D. S. Margoliouth

Kwa kuipa himaya ya Kiislam makao makuu ya kidini, yasiyotumika wakati wowote kama makao makuu ya kisiasa, mwanzilishi aliyapatia makao hayo nguzo ambayo imelinda uendeleaji wa mfumo huo katikati ya misukosuko mikali kabisa.

Kutembelea Makka ambako kuliandamana na mabadiliko mengi sana kulisimamish- wa kwa Mtume (s.a.w.) kupitia kwenye taratibu za hijja ndogo. Baadae, Akib, mtoto wa Usaid, aliteuliwa kuwa gavana wa Makka kwa mshahara wa dirham moja kwa siku; huu ulikuwa ni uteuzi wa kwanza wa kudumu wa kiserikali kufanywa katika Uislamu; huko Khaibar, mji mwingine pekee wa muhimu ambao Waislamu walikuwa wameuteka, serikali ya (wenyeji wa) hapo ilibaki. Mbali na gavana, kiongozi wa kiroho aliachwa hapo, Mu’adh mtoto wa Jabal, mwenyeji wa Madina, ambaye katika uhodari wake wa kufundisha hiyo dini mpya, Mtume (s.a.w.) alikuwa na imani nao. Mtume (s.a.w.) alirudi Madina pamoja na jeshi la Waislamu baada ya kutokuwepo kwa zaidi ya mwezi. (Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)