read

Vita Vya Kiislamu

Muhammad Mustafa, Mtume Wa Allah (s.a.w.) ilibidi apigane mfululizo wa vita katika kuutetea Uislamu kutoka kwenye makazi yake mapya hapo Madina. Vile vita ambavyo aliongoza jeshi la Kiislam yeye mwenyewe, vinaitwa “Ghaz’wa” na ile misafara ambayo aliyotuma kutoka Madina chini ya amri ya mmojawapo wa maswahaba wake, inaitwa “Sariyya”.

Kwa kukisia, Mtume (s.a.w.) alizindua kampeni za kijeshi 80 katika ile miaka kumi tangu kuhama kwake mwaka 622 A.D. mpaka kufa kwake mwaka 632 A.D. Baadhi ya kampeni hizi hazikuwa chochote zaidi ya ujumbe wa upelelezi. Idadi iliyohusika ndani yake ilikuwa ndogo sana, na hasa walichokifanya kilikuwa ni kuangalia mienendo ya koo au kabila fulani. Zingine zilikuwa ni misafara ya ki-tablighi. Nyingine nyingi zilikuwa ni za mikwaruzano midogodogo tu. Bado nyingine zilikuwa ni za udadisi tu kwa sababu ya tukio maalum lililohusiana nazo. Nitatoa maelezo ya juu juu ya kampeni hizo ndogo, na nitaweka msisitizo hasa kwenye yale mapambano makubwa ya Uislamu.

Hapo nyuma kabisa kabla ya Uislamu, Wagiriki na Warumi waligundua kwamba vita vinaweza kubadili hatma za mataifa. Miongoni mwa kampeni za Mtume, kuna vita vitano ambavyo vinaweza kusemekana kwamba vimebadili hatma za mataifa. Navyo ni vita vya Badr, Uhud, Khandaq, Khaybar na Hunayn.

Vita hivi vilikuwa haviepukiki. Maquraishi wa Makka waliamini kwamba kama Waarabu wote wataukubali Uislamu, itakuwa na maana kwao (Maquraishi) ya kupoteza mapato yote ya Hijja, na kupotea kwa heshima waliyokuwa nayo kama walezi wa masanamu. Mafanikio ya Uislamu waliyabashiri kwa usawa kabisa kama pigo la kifo cha heshima. Ilikuwa ni hofu hii, hofu ya kupoteza mamlaka ya kiuchumi na kisiasa na hadhi ambayo iliharakisha vita kati yao na Waislamu.

Tangu kule kuhama kwa Waislamu toka Makka, hali ya kivita isiyopingika ilijitokeza kati yao na Maquraishi. Katika siku za mwanzoni hapo Madina, Waislamu hawakuthubutu kusogeza silaha zao wakati wowote. Askari wa doria waliwekwa mjini kote kila usiku kuwatahadharisha wakazi endapo adui atafanya shambulizi la ghafla. Mtume (s.a.w.) hakuweza kulala usiku akihofia mashambulizi wakati wowote.

Ilikuwa ni katika mazingira kama Haya ambapo ilikuwa achukue hatua za maksudi kwa ajili ya usalama wa Madina. Kama mkuu wa dola inayoondokea, usalama wa dola hiyo ulikuwa ndio wajibu wake wa kwanza.

Kwa manufaa ya usalama, Waislamu iliwabidi kutupia macho nyendo za adui, marafiki zake adui na wasaidizi wao.

Mtume (s.a.w.) alituma msafara wa kwanza mnamo mwezi wa tisa wa mwaka wa kwanza wa Hijiria, chini ya uongozi wa ami yake, Hamza ibn Abdul Muttalib. Muhajirina thelathini walishiriki ndani yake. Makusudio yao yalikuwa ni kuzuia msafara wa kibiashara wa Maquraishi. Lakini kabila moja, lenye urafiki kwa pande zote, likasuluhisha kati yao. Hapakuwa na mapigano, na msafara ule ukarudi Madina.

Katika mwezi uliofuatia, Mtume (s.a.w.) aliwatuma Muhajirina sitini chini ya uongozi wa binamu yake, Ubaida ibn al-Harith, kwenda Raghib, karibu na Red Sea (bahari nyekundu).
Walikabiliana na msafara wa Maquraishi. Pande zote mbili zilirushiana mishale michache lakini hapakuwa na majeruhi. Wafanyibiashara wawili wa Makka waliuacha msafara wao, wakaja upande wa Waislamu, wakasilimu, na wakafuatana na msafara ule wakati uliporejea Madina.

Ubaida ibn al-Harith anasemekana alirusha mshale kwa adui. Ulikuwa ndio mshale wa kwanza kurushwa kwa ajili ya Uislamu.

Sir William Muir:

“Ubaida anajulikana katika Hadith kama ni yeye ambaye katika tukio hili, “alirusha mshale wa kwanza kwa ajili ya Uislamu.” (The Life of Mohammed, London, 1877)

Hapakuwa na kampeni nyingine za kivita katika muda uliobakia wa mwaka wa kwanza wa Hijiria.