read

Vita Vya Siffin

Kumgeuza mawazo Mu’awiyah asipigane vita dhidi ya waislamu, Ali alitumia zile hoja zote ambazo alikuwa amezitumia, hapo kabla, katika nasaha zake kwa Aisha, Talha na Zubeir kwa lengo hilo hilo, na matokeo katika masuala yote yalikuwa ni yale yale.

Katika mawazo ya maadui zake wote, amani ingeweza tu kuchanganya yale matatizo magumu tayari ya Dar-ul-Islam. Wao waliona dawa moja tu kwa ajili ya matatizo hayo, nayo ilikuwa ni vita.

Safari hii, hata hivyo, Ali alikabiliwa na adui aliyekuwa na hila nyingi zaidi, mjanja, mwenye kudhuru kwa siri na hatari zaidi kuliko ule “utawala wa watu watatu” wa Aisha, Talha na Zubeir ulivyowahi kuwa. Kwa kweli, alikuwa staidi sana kiasi kwamba katika kulinganisha, Talha na Zubeir walikuwa ni washamba kweli kweli wa kisiasa.

Huko Basra, kile kikundi cha waasi kilikuwa ni muungano wa maslahi yanayotofautiana, na wanachama wake waliunganishwa pamoja tu na chuki yao ya pamoja juu ya Ali. Ulikosa umoja wa lengo. Aisha alikuwa anapigana ili kumpandisha mpwa wake, Abdallah bin Zubeir, kwenye kiti cha ukhalifa. Lakini Talha na Zubeir walikuwa wasimkubalie katika suala hili; wao wenyewe walikuwa ni wagombea wa zawadi hiyo. Kwa hiyo muungano wao ulikuwa sio kabisa ule wa ‘utawala wa watu watatu’ wa mmoja kwa wote na wote kwa mmoja ambao wafuasi wao wangependa uwe.

Ule utawala wa watu watatu wa Basra ulitiwa mikosi na kuchechemezwa na wale washauri wake waliogawanyika lakini Mu’awiyah hakuwa hivyo. Alitafuta ushauri wa Amr bin Al-Aas na wengineo lakini yeye mwenyewe ndiye aliyefanya maamuzi yote.

Ali alikuwa bado anatafuta umoja. Umoja wa umma wa Muhammad ulikuwa unatishiwa na mifadhaiko na kero, na yeye alikuwa anajitahidi kuulinda na kuuhifadhi. Lakini kwa bahati mbaya, maadui zake hawakushiriki naye katika shauku hii. Hamu yao pekee ilikuwa ni kuuchanilia mbali umoja wa umma, na walifanikiwa katika kuuchana.

Wakati wa majira ya kuchipua (spring) ya mwaka 657, Mu’awiyah aliondoka Damascus pamoja na jeshi lake kwenda kupigana vita huko Iraqi. Aliuvuka mpaka na kusimama kwenye kijiji kiitwacho Siffin – kwenye ukingo wa mto Euphrates. Kitendo chake cha kwanza kilikuwa ni kuumiliki ule mwambao.

Kusikia taarifa za kusonga mbele kwa jeshi la Syria, Ali alimteua Aqaba ibn Amr Ansari kama gavana wa Kufa, akamwita Abdallah ibn Abbas kutoka Basra aje kuongozana naye, na akaondoka Kufa pamoja na jeshi lake kwenda Siffin mnamo April 657. “Wakongwe Sabini wa vita vya Badr na Masahaba 250 wa Mti wa Kiapo walitembea chini ya bendera yake pamoja na jeshi hilo kwenye kingo za mto Euphrates kuelekea Siffin.” (Mustadrak, juz. III).

Walipowasili Siffin, jeshi la Ali lilikuta njia yake ya kufikia mwambaoni imezuiwa na kikosi kizito cha majeshi ya Syria. Ali alimtuma Sa’sa’ ibn Sauhan, sahaba wa Mtume, kwenda kwa Mu’awiyah, kumtaka awaondoe wapiga mishale wake kutoka pale mtoni, na kuruhusu uhuru wa kufikia maji, kwa kila mtu.

Mu’awiyah, bila shaka, alikataa kufanya hivyo ndipo Ali alipoviamuru vikosi vyake kuchukua ule mwambao kwa nguvu. Vikosi vyake viliwafukuza Wasyria, na wakautwaa ule mwambao. Sasa kukawa na fadhaa na hofu ndani ya kambi ya Mu’awiyah. Alibuni mzuka wa kifo ndani ya jangwa kwa kiu. Lakini Amr bin Al-Aas alimhakikishia kwamba Ali kamwe hatamnyima maji mtu yoyote.

Watu wa Syria walikuwa hawana njia ya kuyafikia maji. Majemadari wa Ali walikuwa na mawazo kwamba watamrudishia Mu’awiyah sarafu yake mwenyewe (kulipiza kile alichokifanya). Hapakuwa na kitu rahisi zaidi kwao kuliko kuliacha lile jeshi lote la Syria kufa kwa kiu. Lakini Ali kwa uunngwana kabisa akawalaumu kwa kutaka kwao kuigiza mfano ambao wao wenyewe waliushutumu, na akatangaza hivi: “Mto huu ni wa Mwenyezi Mungu. Hakuna kizuizi juu ya maji kwa mtu yeyote yule, na yeyote anayeyataka, anaweza kuyachukua.”

Mikwaruzano midogo midogo ilianza wakati wa Dhil-Hajj 36 H.A., Mei 657. (Dhil-Hajj ndio mwezi wa mwisho wa kalenda ya Kiislamu) na iliendelea hapa na pale kwa majuma machache yaliyofuatia. Kwa kuingia kwa Muharram (mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiislamu), mapigano yakasimamishwa kwa mwezi mmoja.

Wakati wa mwezi huu wa kusitisha mapigano (Muharram), Ali alianzisha upya kutafuta kwake amani lakini juhudi zake za kutatua matatizo hayo kwa majadiliano, au kupata ufumbuzi ambao utaondoa mapigano miongoni mwa Waislamu, hazikufanikiwa kwa sababu nyepesi tu kwamba mshindani wake, Mu’awiyah, hakuiona amani kama ndio uchaguzi unaofaa. Alikataa maridhiano kwa sababu yalikuwa hayachukuani na maslahi yake.

Ali angeweza kufanywa asiye na matarajio mema na undumilakuwili, misiba na matukio machungu – bado yeye alikuwa tayari kuamini, licha ya mifano yote, katika matazamio ya amani, na alikuwa tayari kuyafanyia kazi.

Pale siku ya mwisho ya Muharram ilipopita, na mwezi wa Safar ukaanza, Ali alimtuma Merthid ibn Harith kupeleka ujumbe kwa watu wa Syria. Alisimama mbele ya jeshi la Syria, na akausoma ujumbe huo kama ifuatavyo: “Enyi watu wa Syria! Ali, yule Kiongozi wa Waumini, anakufahamisheni ninyi kwamba aliwapeni kila nafasi ya kuthibitisha ukweli na kujiridhisha ninyi wenyewe. Alikualikeni ninyi kufuata Kitabu cha Allah swt., lakini hamkusikiliza hata kidogo. Sasa hakuna jingine zaidi analoweza kuwaambia. Allah hawapendi wale wanaoisaliti Haki.” (Tarikh Tabari, juz. IV, uk. 6)

Wakati majeshi hayo mawili yalipokabiliana, Ali alitoa maagizo yafuatayo kwa vikosi vyake kama ambavyo alifanya kabla ya vita vya Basra (vita vya Ngamia): “Enyi Waislamu! Subirini adui yenu aanzishe uhasama, na mjitetee wenyewe pale atakapokushambulieni. Kama mtu yeyote kati ya maadui anataka kuikimbia vita na kuokoa maisha yake, mwacheni afanye hivyo. Ikiwa Allah atakupeni ushindi, msiipore kambi ya adui; msiikatekate miili ya waliokufa wala kuwanyang’anya deraya na silaha zao, na msiwasumbue wanawake zao. Juu ya mambo yote, mkumbukeni Allah nyakati zote.”

Ali aliyahamisha na kuyapanga upya majeshi yake. Alitoa uongozi wa vikosi vya upande wa kulia kwa Abdallah ibn Abbas, vile vya upande wa kushoto kwa Malik ibn Ashtar, ambapo yeye mwenyewe aliongoza pale katikati. Pamoja naye walikuwepo masahaba na marafiki za Muhammad, (s.a.w.w.), Mtume wa Allah swt., miongoni mwao Ammar ibn Yasir. Wakati huu, majeshi ya Syria yakashambulia, na Ali akayaashiria majeshi yake kuwafukuza, Vita vya Siffin vikawa vimeanza.

Ammar ibn Yasir alikuwa na umri zaidi ya miaka 70 kwa wakati huo lakini moto wa imani juu ya Allah swt., na mapenzi kwa Mtume Wake, Muhammad (s.a.w.w.), ulichoma kwa ukali sana kifuani mwake, na alipigana kama vijana wadogo. Kuongezea kwenye mguso wa kuvutia wa mapambano hayo, alibeba silaha zilezile ambazo kwazo alikuwa amepigana, miaka mingi ya nyuma, akiwa pamoja na Muhammad Mustafa, dhidi ya washirikina wa Makka huko Badr.

Adui aliyekutana naye Ammar hapo Siffin alikuwa amejigeuza kama Muislamu lakini hakuweza kumhadaa yeye Ammar. Macho yenye kupenyeza ya Ammar yaliutambua ule uso uliokuwa nyuma ya barakoa. Lazima atakuwa amefurahishwa sana kukutana na adui yule wa siku nyingi, baada ya kupita kwa miaka mingi, katika pambano jipya.

Kwake yeye vile vita vya Siffin vilikuwa vyenye kuleta kumbukumbu ya vita vya Badr. Kwa mara nyingine tena alikuwa anapigana, upande wa Muhammad na mshika-makamu wake, Ali, dhidi ya maadui zao. Alivyokuwa akiwapiga watu wa Syria, alibakia akisema: “Tunapigana dhidi yenu leo juu ya tafsiri ya Qur’an kama vile tu wakati wa Mtume wetu, tulipigana dhidi yenu juu ya kushushwa kwake.”

Imam Ahmad bin Hanbal katika Musnad yake, na Hakim katika Mustadrak yake, wamesimulia kwa idhini ya Abu Said al-Khudri, sahaba wa Mtume (s.a.w.w.) kwamba Mtume wa Allah alimwambia Ali: “Ewe Ali! Kama vile ninavyopigana dhidi ya waabudu masanamu juu ya kushushwa kwa Qur’an, siku moja utapigana juu ya tafsiri yake.”

Ammar alisita kwa muda mchache kuzungumza na wapiganaji wenzie, na akawaambia: “Rafiki zangu! Mshambulieni adui. Hakuna muda wa kukawia na kusita. Milango ya Peponi iko wazi kabisa leo hii lakini kuruhusiwa kuingia, mnapaswa kuthubutu panga na mikuki ya maadui hawa wa Allah na Mtume Wake. Washambulieni. Vunjeni panga zao, mikuki yao, na mafuvu yao, nanyi mtaiingia milango ya pepo na baraka za milele, na huko, mtakuwa pamoja na Muhammad, Kipenzi cha Allah swt. Mwenyewe.”

Ammar mwenyewe aliongoza mashambulizi, na mara tu alikuwa yuko ndani kabisa ya safu za Wasyria. Katikati ya mapambano, alijisikia kuwa na kiu, alizidiwa na joto. Alirudi kwenye safu zake kutuliza kiu yake, na akawaomba wenzie kumletea maji. Ilitokea tu kwamba kwa muda ule, hawakuweza kupata maji popote pale, lakini mmoja wao alipata maziwa, na akamletea yeye kikombe kimoja.

Pale Ammar alipokiona kikombe cha maziwa mbele yake, alihisi mtukuto wa kusisimua mwilini mwake. Midomo yake ikajikunja katika tabasamu pana, naye akaguta kwa mshangao: Allah-u-Akbar (Mola ni Mkubwa). Mtume wa Allah swt., alizungumza kweli tupu.” Waliokuwa wamesimama pembeni wakamwomba aeleze maana ya mshangao wake, na yeye akasema:

“Mtume wa Allah aliniambia mimi kwamba chakula changu cha mwisho katika dunia hii kitakujakuwa ni maziwa. Sasa ninajua kwamba wakati wa mimi kukutana naye umekwishafika. Nilikuwa nikiusubiri wakati huu kwa muda mrefu sana, kwa hamu kubwa. Hatimaye, huu hapa. Al-Hamdu lillah.”

Ammar bin Yasir alibadilika kwa mapenzi kwa Allah swt., na mapenzi kwa Mtume Wake, Muhammad (s.a.w.w.). Akayanywa yale maziwa, akapanda juu ya farasi wake, na kisha akatumbukia kwenye safu za Wasyria. Ghafla, akamuona Amr bin Al-Aas akiwa katikati yao, na akapiga kelele:

“Laana iwe juu yako, Ewe mtumishi wa Mu’awiyah! Uliiuza dini yako kwa kubadilishana na Misri. Umesahau utabiri wa Mtume wa Allah aliposema kwamba kikundi cha watu waovu kitakuja kuniua mimi? Sikiliza na tazama tena. Wewe hunitambui mimi? Mimi ni Ammar, Ammar bin Yasir, rafiki wa Muhammad Mustafa.”

Amr, bila shaka alikuwa ameyapima machaguo yote, na alikuwa ameamua kupendelea Misri. Lakini alinyamaza kimya, akijua kwamba kufunua kinywa chake kutakuwa ni kukubali kosa lake, na chochote atakachokuwa amekisema, atajifichua mwenyewe tu.

Ammar alikuwa anachukua kipando cha mara ya mwisho katika dunia hii. Baadae kidogo tu alikuwa aingie Peponi ambako rafiki na kipenzi chake, Muhammad (s.a.w.w.) alikuwa akimsubiri yeye, tayari kwa kumkaribisha na kumpangusa mavumbi ya Siffin kutoka kwenye nywele zake zenye mawimbi na uso wake mng’aavu kama vile miaka mingi ya nyuma, alivyokuwa amempangusa mavumbi ya Handaki la Madina kutoka kwenye nywele zake zenye mawimbi na uso wake mng’aavu.Akishambulia kushoto na kulia, Ammar alisonga mbele, akiwa hana habari kabisa juu ya hatari zote juu yake.

Kichwa chake na uso viligandamana na damu na vumbi kiasi kwamba hakuweza kutambulika. Kwa wakati ule, mpiganaji mmoja wa Syria, akilenga shabaha kali sana, alimrushia mkuki ambao ulimpata kwenye moyo wake, na akaanguka kutoka kwenye farasi. Katika kile kitendo cha kuanguka kutoka kwenye farasi, alibadilishana maisha yake kwa Taji la Shahidi na akalivaa kichwani mwake. Akiwa amevaa taji hili adhimu lenye kung’aa, Ammar bin Yasir alijiunga pamoja na wenye Uzima wa Milele huko Peponi, wakiongozwa na rafiki yake, Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Kipenzi cha Allah swt.

Mashujaa hodari wawili wa Syria walikuja kumuona Mu’awiyah. Kila mmoja wao alidai kwamba yeye ndiye aliyerusha ule mkuki ambao umemuua Ammar, na kila mmoja alikuwa ni mgombea wa zawadi kwa ajili ya “tendo” lake la kishujaa. Amr bin Al-Aas alikuwa pamoja na Mu’awiyah, na akawauliza: “Kwa nini nyie wote mna shauku ya kurukia kwenye moto wa jahannam?”

Wanahistoria na wasimulizi wa Hadith wameuandika huu utabiri maarufu wa Mtume wa Allah swt. kwamba Ammar bin Yasir atakuja kuuawa na watu wapotofu.

Sir John Glubb:

“Pale Waislamu wa mwanzoni huko Madina walipotishiwa na Makuraish, ambao waliwarudisha nyuma kwa kuchimba handaki, Ammar ibn Yasir alikuwa akipepesuka na mzigo wa udongo. Mtume mwenyewe alikuwa amemuona na akaja kumsaidia, akampokea mzigo wake na akakipangusa vumbi kichwa chake na nguo zake.

Kwa moyo huu wa upole wa kiuzazi ambao ulikuwa ni mojawapo ya sababu za utii wa wafuasi wake, yeye akasema, “Masikini Ammar! Watu makatili na madhalimu watakuwa hakika ndio kifo chako wewe.” Inaelekea kuwa yamkini tamko hili lilitolewa kwa utani, akiwalaumu wafuasi wake kwa kumchosha mfuasi huyu mwenye kuji- tolea. Lakini sentenso hii ilikumbukwa kama utabiri.

Sasa katika siku ya pili ya vita vya Siffin, Ammar aliuawa akipigana kwa ajili ya Ali na akikemea kwa sauti, “Ewe Pepo, uko karibu kwa kiasi gani?” Hiyo ndio ilikuwa heshima kubwa iliyozingatiwa na majeshi yote mawili kwa kumbukumbu ya Mtume kwamba kifo cha Ammar kiliingiza hamasa kiasi kikubwa katika jeshi la Ali kama kilivyodukiza unyong’onyevu katika lile la Mu’awiyah. Kwani maana ya utabiri huo ilikuwa kwamba wale watu waliomuua Ammar watakuwa wanapigana katika njia ya uovu.”
(The Great Arab Conquests, London, uk. 326, 1963)

Sir John Glubb amekosea katika kupendekeza kwamba Mtume (s.a.w.w.) alitoa tamko hilo “kiutani.” Mtume alikuwa hatanii. Hapakuwa na muda kwa ajili ya utani. Alikuwa makini kabisa wakati alipomwambia Ammar kwamba watu makatili na madhalimu watakuja kumuua yeye (Ammar).

Kifo cha Ammar kilikuwa na athari nzito sana kwa marafiki na maadui, na kilichochea mgongano katika mawazo. Wairaqi sasa wakapigana kwa raghba mpya wakiwa wamesadiki kuwa walikuwa wanapigana kwa ajili ya Haki. Wakati huohuo, watu wa Syria wakawa wamesambaratika kwa mashaka. Wengi wao waliacha kupigana, miongoni mwao ni Amr bin Al-Aas mwenyewe. Mwanawe, Abdallah, akamwambia: “Leo hii tumemuua mtu ambaye kutoka usoni mwake Mtume wa Allah mwenyewe aliondoa mavumbi, na alikuwa amemwambia yeye kwamba kundi la watu waovu litakuja kumuua.”

Amr bin Al-Aas aliinukuu ile Hadith ya Mtume (s.a.w.w) mbele ya Mu’awiyah, na akasema: “Sasa ni dhahiri kwamba sisi ndio wale watu ambao wako kwenye makosa.”

Mu’awiyah alimtaka Amr anyamaze kimya, na asiwafanye wengine wakaisikia hiyo Hadith ya Mtume, na akaongezea kwamba Ammar kwa hakika aliuawa na Ali ambaye alimleta kwenye vita hivyo.

Mmoja wa masahaba ambaye alikuwepo katika msafara wa Mu’awiyah, kwa tahadhari alitoa maoni juu ya matamshi ya Mu’awiyah kwamba kama Ali alimuua Ammar kwa sababu alikuwa amekuja kwenye vita hivyo pamoja naye, basi bila ya shaka yoyote ile, Muhammad alimuua Hamza kwa sababu alimchukua pamoja naye kwenye vita.

Pale Ali aliposikia kwamba Ammar alikuwa ameuawa kwenye mapambano, aliisoma ile Aya ya 156 ya Sura ya pili ya Qur’an Tukufu kama ifuatavyo: “Sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake ndio marejeo yetu.”

Kifo cha Ammar kilikuwa ni mshituko mkubwa sana kwa Ali. Walikuwa marafiki tangu zile siku Ammar na wazazi wake walipokuwa wakiteswa na Makuraish kwa kuukubali Uislamu, na rafiki yao, Muhammad (s.a.w.w.) alipowaliwaza. Lakini Muhammad mwenyewe alikuwa, kwa siku nyingi, ametengana nao. Sasa Ammar pia aliiondoka dunia hii, akimuacha Ali peke yake. Ali alizongwa na huzuni na hisia mbaya ya “upweke.”

Ali na marafiki zake waliswali Swala ya jeneza kwa ajili ya Ammar ibn Yasir, rafiki wa Allah swt., sahaba wa Muhammad (s.a.w.w.), na Shahidi wa Siffin, na wakamzika.

Kama vile tu marafiki zake wawili, Muhammad na Ali, Ammar alikuwa pia amepigana na Makuraishi maisha yake yote. Mapema, Makuraishi walikuwa wamewaua wazazi wake, na sasa wamemuua yeye mwenyewe. Kila Yasir mmoja kati ya watatu hao alipata taji la Shahada.

Huzuni ya Ali kwa kifo cha Yasir ililingana na furaha ya Mu’awiyah. Huyu Mu’awiyah mara kwa mara alisema kwamba Ammar alikuwa ni mmoja kati ya mikono miwili ya Ali (mkono mwingine ukiwa ni Malik ibn Ashtar), na alijigamba kwamba alikuwa ameukata mkono ule.

Yalipoanza tena mapigano, watoto wawili wa Hudhaifa ibn al-Yaman, Said na Safwan, waliuawa katika mapambano na vikosi vya Syria. Ilikuwa ni dua ya mwisho ya baba yao kwamba watakuja kufa wakipigana kwa ajili ya Ali.

Siku nyingi zikapita katika mapigano yasiyo na utaratibu. Ilikuwa ni katika mapigano haya madogo madogo ambamo Ali alipata hasara kubwa mbili kwa vifo vya masahaba wawili wa Mtume (s.a.w.w.). Mmoja wao alikuwa ni Khuzaima ibn Thabit Ansari (yule ambaye ushahidi wake mmoja ulikuwa ni sawa na ushahidi wa watu wawili wengine); na Uways Qarni. Huyu wa mwisho, kama ilivyoelezwa mapema, aliwasili kutoka Yemen, na alikuwa amekutana na Ali kwa mara ya kwanza katika usiku wa kuamkia vita vya Basra. Tamaa ya maisha yote ya Khuzaima na Uways Qarni ilikuwa ni kupata hadhi ya shahada katika Uislamu. Waliipata katika vita vya Siffin.

Vifo vya Khuzaima na Uways Qarni vilimkera sana Ali kiasi kwamba alituma ujumbe kwa Mu’awiyah atoke kuja kupigana yeye mwenyewe binafsi, na hivyo kuokoa maisha ya maelfu ya Waislamu waliokuwa wakifa pande zote.
Mu’awiyah, bila shaka, hakuukubali mwaliko huo. Ilikuwa ni dhahiri kuona kwamba kujikoga kisiasa na ushujaa havikua lazima sana viote kwenye mti mmoja.

Watu walikuwa wanakufa kwa idadi kubwa lakini hakukuwa na matokeo ya hakika ya kuonyesha. Ali aliuona huu ukosefu wa maendeleo kuwa yenye kuleta madhara kwenye hamasa ya vikosi vyake, na akaamua kurekebisha hali hiyo. Jioni ile alimwita Abdallah ibn Abbas ambaye alikuwa ndiye mshauri wake mkuu, na Malik ibn Ashtar ambaye alikuwa ndiye Mnadhimu Mkuu wake, kwenye kikao. Wote kwa pamoja walitengeneza mkakati mpya wa kuvifikisha vita kwenye hatma yenye mafanikio.

Katika siku iliyofuatia, Ali na Malik walikuwa wawashambulie maadui kwa wakati mmoja, mmoja kutoka kuliana mwingine kutoka kushoto.

Wakiweka uratibu kamili, msawazisho na umakini, walikuwa wamuweke adui katika mashambulizi ya mbele na nyuma kwa wakati mmoja, na kisha kuelekea kwenye kitovu chake, Malik alikuwa aongoze mashambulizi ambayo yatamlazimisha adui kusalimu amri.

Baada ya Swala ya usiku, Ali alihutubia vikosi vyake kama ifuatavyo: “Enyi Waislamu! Kesho mtalazimika kupigana vita vya maamuzi, kushinda au kushindwa. Kwa hiyo, tumieni usiku huu katika ibada kwa Muumba wenu. Tafuteni rehema Zake, na muombeni ili Yeye akupeni uimara na ushindi. Na kesho mthibitishieni kila mtu kwamba ninyi ni watetezi wa Haki na Kweli.”
(Tarikh Kamil, ibn Athir, Juz. III, uk.151)

Vita Vya Lailatul-Harir

Asubuhi iliyofuata, Ali na Malik walipanda farasi zao, na wakaenda mbele ya majeshi ya Syria wakichunguza mpangilio wao. Walifanya mabadiliko kidogo katika mpango wao wa mapambano, na kisha, kwa ishara kutoka kwa Ali, Malik akashambulia upande wa kushoto wa adui.

Majeshi ya Syria yalikuwa na wingi wa idadi kuliko Malik, na makamanda wao walijaribu kuutumia vizuri. Kila aliposhambulia, wao walitawanyika lakini kwa namna fulani waliweza kujikusanya tena. Malik alipigana kutwa nzima. Kwa kawaida, majeshi hayo mawili yalisimamisha mapigano baada ya jua kuzama, na kurudi kambini kwa ajili ya Swala na mapumziko lakini siku ile Malik alikataa kurudi. Vile vile hakuwaruhusu Wasyria kurudi kambini kwao, na akawabakisha kwenye uwanja wa mapambano.

Baada ya mapumziko mafupi kwa ajili ya Swala zake, Malik akaanzisha shambulio lake la ghafla juu ya jeshi la Syria. Safari hii mashambulizi yake yalikuwa ya harara sana kiasi kwamba Wasyria waliswagwa mbele yake kama kondoo. Baada ya Swala ya usiku, Ali pia alirejea kwenye uwanja wa mapambano, na akaushambulia ule upande wa kulia wa Wasyria. Katikati yao, walianza kulisaga jeshi la Syria.

Waliua maelfu ya wapiganaji wa Syria na kueneza woga na hofu katika safu zao. Mikoromo na mayowe ya Wasyria walio- jeruhiwa na wanaokufa, milio ya vyuma vya silaha, migongano ya vyuma, upanga wa Malik wenye ncha mbili ukichana ngao za Wasyria, na ukelele wake wa kivita wa Allah-u-Akbar, vililijaza lile anga la usiku la jangwani.

Malik alikuwa hodari na jabari kupita kiasi. Alionekana kwa hakika, mbele ya maadui, kuwa ndiye Kipaji hasa wa Ushindi. Alikuwa ni chombo maalum na cha hatari mikononi mwa Majaaliwa. Kila alipopita, ushindi ulishambulia pamoja naye.

Edward Gibbon:

“Katika pambano hili la umwagaji damu mwingi yule khalifa halali alionyesha mwenendo wa hali ya juu wa ushujaa na ubinadamu. Vikosi vyake viliamriwa kusubiri shambulio la mwanzo la adui, kuwaacha ndugu zao wanaokimbia, na kuheshimu miili ya wafu, na usafi wa mateka wa kike. Alipendekeza kwa wingi sana kuokoa damu ya Waislamu kwa kutumia mtindo wa mapigano ya watu wawili wawili tu; lakini mpinzani wake mwenye kugwayagwaya kwa woga aliikataa changamoto hiyo kama hukumu ya kifo kisichokwepeka. Safu za majeshi ya Syria zilivunjwa na shambulizi la shujaa aliyekuwa amepanda farasi mwenye rangi mbili, na akautumia kwa nguvu zisizozuilika, upanga wake mzito na wenye ncha mbili.
Kila mara alipomchoma muasi, alikemea Allah-u-Akbar, ‘Mwenyezi Mungu ni Mshindi!’ na katika zile ghasia za vita vya usiku alisikika akiurudia mara mia nne ule mguto mkubwa sana wa mshangao.
(The Decline and Fall of the Roman Empire)

Shujaa aliyezivunja safu za Wasyria alikuwa ni Malik. Lakini tayari alikuwa amewaua wengi wao – wale askari wa kawaida wa Syria – kiasi kwamba alikuwa amekwishaanza kuwapuuza.

Alitafuta mawindo ya ngazi ya juu zaidi. Katika vita vya Basra, alimaliza mapigano kwa kumuua yule ngamia aliyekuwa amembeba Aisha mgongoni mwake. Dhamira yake sasa ilikuwa ni kumuua au kumteka Mu’awiyah, na hivyo kukomesha vita vya Siffin. Kwa silika za mwindaji, kwa hiyo, alianza kusogea kuelekea kwenye windo lake.

Malik alimpanda farasi wake kupita kwenye madimbwi ya damu na matuta marefu ya maiti wa Syria, bila kuzuilika, bila ya huruma na labda bila kukwepeka. Kila aliyejaribu kupigana naye au kumzuia njia, alikatwa vipande.

Mu’awiyah sasa aliweza kuona kwa macho yake mwenyewe kwamba wakati umetimia. Alichokuwa anakiona kikimkaribia yeye, hakikuwa ni Malik, yule Mnadhimu Mkuu wa Ali, bali Malaika wa Kifo. Ile ardhi ngumu chini ya miguu yake ilionekana kwake kugeuka kuwa mchanga-didimizi. Walinzi wake, ingawa wa kuchaguliwa kwa ujasiri wao, nguvu na utii kwake na nyumba yake, walikuwa hawana uwezo mbele ya Malik. Hawakuweza kumzuia kusonga mbele kuelekea kwenye mawindo yake bali walifanya kitu cha ubora wa pili – waliweka tayari farasi wenye nguvu kwa ajili yake (Mu’awiyah) kupanda na kutoroka kutoka kwenye uwanja wa vita kwa kufichwa na giza la usiku.

Katika hali hii ya hatari ya kutisha, Mu’awiyah alimgeukia Amr bin Al-Aas, na akasema: “Kuna matumaini yoyote kwamba tunaweza bado kuokoa maisha yetu au uwanda huu wa upweke ndio umepangiwa kuwa eneo la makaburi yetu? Na hivi, wewe bado unaitaka Misri? Kama unaitaka, basi fikiria mara moja juu ya mkakati wa kumzuia Malik ama sivyo sisi sote pamoja na wewe, tutauawa katika muda mchache ujao.”

Matumaini ya uhai yalikuwa yenye nguvu sana kwa Amr bin Al-Aas. Aliweza kukabiliana na hali yoyote ile, na alikuwa, kwa hakika, tayari na mkakati kwa ajili ya muda huu muafaka. Mkakati wa Amr ulikuwa ukwapue sio tu yale mawindo bali hata ushindi wenyewe kutoka kwenye mkono wa Malik!

Vita alivyokuwa akipigana Malik, ni maarufu sana katika historia kama “Vita vya Layla-tul-Harir.” vilikuwa ndio upeo wa mapambano makali katika uwanda wa Siffin katika kingo za mto Euphrates. Vilikuwa pia ndio kilele cha juu kabisa cha shughuli za kisiasa na kijeshi za wote, Ali na Malik, kama matukio yalivyokuwa yaonyeshe punde tu.

Tangu Ali alipokuwa ametaka kiapo cha utii kutoka kwa Mu’awiyah, yeye Mu’awiyah alifungulia vita vya kifalsafa dhidi yake. Moja ya silaha alizotumia katika mapambano yake ya kifalsafa dhidi ya Ali ilikuwa ni dhahabu au kishawishi cha dhahabu. Mama yake, Hind, alikuwa ametumia jinsia kama silaha yake katika mapambano dhidi ya Uislamu katika vita vya Uhud. Kwa silaha ya dhahabu, Mu’awiyah alifanikiwa kuwatongoza wengi wa maafisa wa ngazi ya juu katika lile jeshi la Iraq, na alipunguza ari yao ya kupigana. Alikuwa hakuwajaza tu na dhahabu na fedha bali alikuwa pia amewaahidi kuwateua wao kama magavana wa majimbo na kuwa makamanda katika jeshi lake kama watamsaliti Ali katika wakati ule muhimu ndani ya mapambano hayo.

Ule wakati muhimu ukawa umewadia. Mapigo makubwa sana ya Malik yalikuwa yamewatupa Wasyria kwenye vurugu isiyo na matumaini. Matarajio yao pekee kwa ajili ya usalama wao yalikuwa ni katika lile giza la usiku ambalo litawaficha ama lingeweza kuwa- ficha kwenye macho ya Malik.

Malik ambaye alijiwazia kwamba alikuwa amefikia mahali pa kumuua au kumteka Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas, bila kujua kwamba wote wawili walikuwa na silaha ya siri ambayo itaokoa maisha yao na kumkanganya yeye. Silaha ya siri ya Mu’awiyah ilikuwa tayari inafanya kazi kimya kimya na kudhuru kwa siri lakini kwa kufaa sana. Ilikuwa ni mbegu ya uhaini aliyokuwa ameipanda kwenye jeshi la Iraq. Mbegu hiyo ghafla ikachipua kwenye vita vya Layla-tul-Harir!

Malik alikuwa bado analitwanga lile jeshi la Syria vibaya sana pale Amr bin Al-Aas alipowaamuru wapiganaji wake kuning’iniza nakala za Qur’an kwenye ncha za mikuki yao kama ishara ya kutaka kwao kuurejesha mgogoro huo kwenye Hukmu ya Allah inayopatikana ndani yake.

Wale maofisa ndani ya jeshi la Iraq ambao walikuwa wamenunuliwa na Mu’awiyah, na ambao walikuwa tayari kutekeleza wajibu wao, walikuwa wakisubiri ishara. Mara tu walipoziona nakala za Qur’an juu ya mikuki, waliweka panga zao kwenye ala zao na wakaacha kupigana, kwa mshangao mkubwa na fadhaa kwa Ali, Ibn Abbas, na wale wachache kati ya maafisa wao waaminifu.

Papo hapo, Abdallah Ibn Abbas akaziona zile nakala za Qur’an zilizotundikwa, na akaelewa ni nini kilichokuwa kinaendelea. Kauli yake fupi ilikuwa: “Vita vimekwisha; usaliti umekwishaanza.”

Na hivyo ikawa. Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas walikuwa wameomba suluhisho la silaha, na walikuwa wameshindwa. Wao sasa wakakata rufaa kwenye usaliti, na kama matukio yalivyokuwa yaonyeshe punde, walikuwa wafanikiwe! Mtu wa kwanza katika jeshi la Iraq kuacha kupigana alikuwa ni Ash’ath bin Qays, yule yule ambaye binti yake Jo’dah, atakuwa aje kumuua Hasan bin Ali kwa sumu miaka kadhaa baadaye. Alikuwa ndiye kion- gozi wa wasaliti katika jeshi la Iraq. Alikuja kumuona Ali na akamwambia:

“Watu wa Syria hawataki kuona umwagaji zaidi wa damu miongoni mwa Waislamu. Wanataka Kitabu cha Allah kiamue kati yao na sisi. Sisi kwa hiyo, hatuwezi kupigana dhidi yao tena.”

Viongozi wa yale makabila mengine ambao walikuwa katika mapatano pamoja na Mu’awiyah, wakaacha kupigana kwa kumuigiza Ash’ath bin Qays.

Watu wa makabila wakafuata mfano wa viongozi wao, na wao wakaacha kupigana pia. Kwa hiyo mapigano yakafikia kusimama kwa kweli kwenye pande nyingi muhimu. Kikosi kimoja tu – kile kilichoongozwa na Malik – kilibakia uwanjani kikipigana na kuwaumiza watu wa Syria.

Haikujitokeza kwa wale wasaliti ndani ya jeshi la Iraq kwamba kama Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas walikuwa na heshima yoyote juu ya Qur’an, wangewataka wao kulifanya Neno la Allah kuwa msuluhishi katika mgogoro wao kabla au hata wakati wa mapambano laki- ni hawakufanya hivyo. Waliikumbuka Qur’an pale tu kushindwa na kuangamizwa kwa jeshi la Syria kulipojitokeza mbele yao juu ya upeo wa macho.

Ash’ath bin Qays ghafla akashikwa na mapenzi juu ya maisha ya Waislamu. Alikamata nakala ya Qur’an, akasimama akiliangalia jeshi lake, na akapiga kelele: “Enyi Waislamu! Mlazimisheni Ali kukubali suluhisho la Kitabu cha Allah, na hapo hapo kusimamisha huu umwagaji wa damu.”

Umwagaji wa damu ya Waislamu ulimshitua pale tu Ali alipokuwa kwenye nafasi ya kushinda vita hivyo. Ushindi wa Ali, yeye alijua, hautabadilisha kitu chochote kwa ajili yake. Lakini kwa tukio la kushindwa kwa Ali, alikuwa amehakikishiwa zawadi nono kutoka kwa Mu’awiyah. “Shauku” yake ya kutaka kuokoa maisha ya Waislamu kwa hiyo, ilikuwa inaeleweka.

Wakati huu, Ali alikuwa amezungukwa na viongozi wa makabila ndani ya jeshi lake, na walianza kumsihi aache kupigana dhidi ya watu wa Syria, ambao, wao walisema, kwa wakati ule hasa, walikuwa wanamuomba yeye, kwa jina la Kitabu cha Allah swt., kusimamisha kuuawa kwa Waislamu. Ali aliwaonya kwamba walikuwa wanalaghaiwa na adui, na akawasihi kushikilia fursa yao ya kwenye ushindi. Yeye aliwaambia pia kwamba yale maombi kwa jina la Kitabu cha Allah (swt.) hayakuwa ni chochote bali ni hila ya kuwanyang’anya wao matunda yao ya ushindi, na kuepuka kwao kushindwa na kifo.

Lakini dhahabu na fedha za Mu’awiyah zilionekana kuwa ni hoja yenye nguvu sana kuliko kitu chochote ambacho Ali alichoweza kusema. Wasaliti hao mara wakawa mafidhuli; walimuomba Ali amrudishe Malik kutoka kwenye uwanja wa vita, na kutangaza kusimamishwa kwa mapigano mara moja. Ali alisita lakini alitambua kwamba hakuwa na nafasi ya kutosha katika kukabiliwa na maasi yanayokaribia ndani ya jeshi lake mwenyewe, na akatuma mjumbe kwa Malik kumuondoa kwenye mstari wa mbele. Malik alikuwa amejishughulisha sana na kuyasaga mabaki ya jeshi la Syria kiasi kwamba alikuwa hata hajagundua kwamba jeshi lake mwenyewe lilikuwa halipigani tena.
Yeye, kwa hiyo, alimwambia yule mjumbe kwamba haukuwa muda wa yeye kuondoka kwenye uwanja wa vita, na kuacha kazi yake ikiwa haijakamilika. Malik alikuwa karibu sana agundue kwamba upanga wake mzito na wenye ncha mbili ambao ulikuwa umeua idadi kubwa ya jeshi la Syria, utakuwa hauna nguvu dhidi ya sila- ha mpya iliyobuniwa na Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas – silaha ya usaliti!

Pale mashushushu na mamluki wa Mu’awiyah katika kambi ya Ali waliposikia majibu ya Malik, walimwambia kwamba kama yeye hatarudi kutoka kwenye uwanja wa vita mara moja, wao watamkamata Ali, na kumkabidhi mikononi mwa Mu’awiyah.

Safari hii Ali ilibidi atume ishara ya huzuni kwa Malik ambaye aliambiwa kwamba ikiwa hatarudi kambini kwake wakati ule ule, hatakuja kumuona tena bwana wake.

Malik alisaga meno kwa hasira kwani alikuwa anaona sasa mawindo yake yakimponyoka kutoka mikononi mwake. Aliingia pale kambini kwa ghadhabu kubwa, akiwa na uchu wa kuwauwa wale wasaliti lakini akaihisi ile hatari kwa bwana wake ambaye alikuwa katikati yao, na wote walikuwa wameweka mikono yao kwenye mipini ya panga zao. Wakati alipowalaumu kwa ukali juu ya upumbavu na udanganyifu wao, walimsogelea kwa kumkamia na panga zao zikiwa zimechomolewa. Lakini Ali alisimama katikati yao, na akawambia wale wasaliti: “Mnaweza kuacha kupigana dhidi ya adui yenu lakini angalau msimuue rafiki yenu wenyewe mkubwa mno.”

Ali hakupenda Mu’awiyah ayaone mapigano ya ndani katika kambi yake mwenyewe. Vita vya Siffin vilikuwa vimekwisha. Pale ambapo nguvu ya Mu’awiyah ilishindwa, hila na ujanja vilifanikiwa. Ushindi ulitoka mikononi mwa Ali kwa hila, na tokea hapo alikuwa awe kwenye hali ya kujihami katika vita visivyo na mafanikio dhidi ya Mu’awiyah. Kule kusimamisha mapigano kuliashiria mwanzo wa kuanguka kwake kisiasa.

Baada ya kukoma kwa uhasama, ilikubaliwa kwamba vile vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Waislamu virejeshwe kwenye usuluhishi, na maamuzi ya wasuluhishaji yakubaliwe na pande zote mbili. Ilielezwa wazi katika haya majadiliano ya awali kwamba hao wasuluhishi watafanya maamuzi yao tu “kwa mtazamo wa Kitabu cha Allah swt.” Mu’awiyah alimteua Amr bin Al-Aas kama msuluhishi anayewakilisha upande wake; na wale waasi ndani ya jeshi la Ali wakapendekeza jina la Abu Musa al-Ash’ary kuiwakilisha Iraq.

Abu Musa alikuwa ni mtu aliyechanganya upumbavu na utii wenye shaka kwa Ali. Alikuwa punde aonyeshe sifa zote, moja ya kichwa chake, na nyigine ya moyo wake, kati- ka kukabilana kwake na Amr bin Al-Aas ambaye alikuwa halingani naye kwa kitu chochote, jambo la mwisho kabisa ni katika werevu wa diplomasia na majadiliano.

Ali kwa silika alimkataa Abu Musa ambaye alimuona siku zote kuwa mwenye maudhi. Chaguo lake yeye mwenyewe lilikuwa ni Abdallah ibn Abbas au Malik ibn Ashtar. Lakini wote hao hawakukubalika sio kwa Mu’awiyah ama kwa mashushushu wake ndani ya jeshi la Iraq kama Ash’ath bin Qays na wengineo.

Walisema kwamba walitaka mtu “asiye na upendeleo” na “asiye mfuasi” kama vile Abu Musa alivyokuwa lakini Abdallah ibn Abbas na Malik Ibn Ashtar hawakuwa hivyo. Ali akawauliza: “Kama hivyo ndivyo, basi kwa nini hamumkatai Amr bin Al-Aas ambaye si mwenye kukosa upendeleo au kukosa ufuasi?” Wakamjibu kwamba wao wanahusika na mambo ya upande wao tu, na sio mambo ya wengine.

Ali aliyakataa mashinikizo ya wasaliti hao lakini walikuwa wote wakijinenepesha juu ya dhahabu ya Mu’awiyah ambayo hawakuwa tayari kuipoteza kwa gharama yoyote ile. Ilikuwa, kwa kweli, imepangwa kabla kwamba Abu Musa ataiwakilisha Iraq. Hatimaye, wasaliti hawa wakafanikiwa katika kumbambika huyu mjinga Abu Musa juu ya bwana wao kama “mwakilishi” wake.

Pale makubaliano ya kuacha mapigano yalipokuwa yanarasimiwa, tukio fulani lilitokea ambalo lilikumbusha Hudaybiyya. Huyo mwandishi aliandika maneno: “Haya ni makubaliano kati ya Ali ibn Abi Talib, Kiongozi wa Waumini, na Mu’awiyah bin Abu Sufyan…..” Amr bin Al-Aas, mwakilishi wa Mu’awiyah, alikataa na akasema: “Futa maneno ‘Kiongozi wa Waumini.’ Kama tungekuwa tumemkubali Ali kama Kiongozi wa Waumini, tusingekuwa tunapigana dhidi yake.” Papo hapo Ali akasema: “Mtume (s.a.w.w.) alisema kweli pale alipobashiri tukio hili hasa.
Wakati mkataba wa Hudaybiyyah ulipokuwa unaandikwa, na nikawa nimeandika maneno, ‘Huu ni mkataba kati ya Muhammad, Mtume wa Allah, na ………’ waabudu masanamu wakanikatiza, na wakasema kwamba kama wangekuwa wamemkubali Muhammad kama Mtume wa Allah, wasingekuwa wanapigana dhidi yake, na walisisitiza juu ya kufutwa kwa maneno ‘Mtume wa Allah,’ kutoka kwenye maandishi ya Mkataba.”

Huko Hudaybiyyah, Muhammad (s.a.w.w.) alifuta yale maneno “Mtume wa Allah” kuto- ka kwenye mswada wa mkataba; hapo Siffin, Ali, akifuata nyayo za Muhammad, aliruhusu maneno “Kiongozi wa Waumini” kufutwa kwenye mswada wa mkataba. Makubaliano ya kuacha mapigano yalisainiwa ipasavyo na kushuhudiwa na pande zote, na nakala zilibadilishanwa kwa kuhifadhiwa katika hifadhi ya nyaraka.

Masharti ya kuacha mapigano yalikuwa:

1. Wasuluhishi wote watatawaliwa na sheria kwamba maamuzi yao yatafikiwa kwa mtazamo wa
Kitabu cha Allah swt. Kama watashindwa kuamua jambo lolote kwa msingi huu, basi
watachukua uamuzi wao kulingana na mifano na Hadith za Mtume wa Allah swt.

2. Uamuzi wa wasuluhishi, kama umeegemea juu ya Kitabu cha Allah swt., utazipasa pande zote.

3. Wasuluhishi watachunguza sababu zote zilizosababisha kifo cha Uthman, na vita vya
wenyewe kwa wenyewe vya Waislamu (kushauri hatua za marekebisho kwa ajili ya baadaye).

4. Wasuluhishi watatangaza maamuzi yao ndani ya miezi sita kutoka tarehe ya kuacha mapigano.

5. Wanaopigana vita watafuata kanuni ya kusitisha mapigano. Watawalinda wasuluhishi ambao
watakuwa na uhuru kamili wa kutembea katika nchi yote.

6. Wasuluhishi watakutana mahali fulani katika mpaka kati ya Iraq na Syria.

Kifungu muhimu kabisa katika mkataba huu kilikuwa ni kwamba wasuluhishi watakifanya Kitabu cha Allah swt. kama kiongozi chao, na kwamba hawatatawaliwa na tamaa na uchu wao.

Vita vya Siffin vilikuwa vimekwisha rasmi lakini Malik ibn Ashtar, sasa “dragoni wa Arabia aliyetiwa mnyororo,” kwa ushupavu kabisa akakataa kushuhudia hati hiyo ya makubaliano. Yeye aliiona kama ni hati ya fedheha na udhalimu.

R. A. Nicholson:

“Vita kubwa ilipiganwa hapo Siffin, kijiji kwenye kingo za Mto Euphrates. Ali takrib- an alikuwa amepata ushindi wakati Mu’awiyah alipomfikiria hila. Aliamuru majeshi yake kuweka Qur’an kwenye ncha za mikuki yao na kukemea, “Kitabu cha Allah hiki hapa: Wacha kituamulie!” Mbinu hii dhaifu ilifanikiwa.

Ndani ya jeshi la Ali mlikuwa na waumini wenye msimamo mkali kwao wao ambao hili pendekezo la kusuluhishwa kwa Qur’an liliwavutia kwa nguvu isiyozuilika. Wao sasa wakaruka kwa kukamia, wakitishia kumsaliti kiongozi wao, labda kama atawasilisha kusudi lake kwenye Kitabu cha Allah. Bure kabisa Ali alipingana na waasi hao, na kuwaonya wao juu ya hila ambayo walikuwa wanamsukumia yeye ndani yake, nalo hili pia katika muda ambao ulikuwa waukumbatie. Hakuwa na uchaguzi bali kukubali na kumtoa kama msuluhishi wake, mtu mwenye utii wa mashaka, Abu Musa as-Shari, mmoja wa masahaba wazee sana wa Mtume waliokuwa hai. Mu’awiyah, kwa upande wake alimtaja Amr bin Al-Aas, ambaye ustadi wake ulikuwa umechochea hila ya uamuzi.” (A Literary History af the Arabs, uk. 192, 1969)

Wasuluhishi hao wawili, Abu Musa na Amr bin Al-Aas, walitangaza kwamba watakuja kukutana, miezi sita baadaye, huko Adhruh, kutoa hukumu yao katika mgogoro huo kati ya pande hizo mbili. Ali na Mu’awiyah ndipo wakarudi kutoka Siffin kungojea uamuzi wa wasuluhishi hao.

Wakati Ali aliporudi Kufa, aliingia kazini kuiunda upya serikali, lakini, kwa bahati mbaya, alilazimika kuahirisha mipango yake kwa sababu ya kuzuka kwa maasi mapya katika jeshi lake.

Wakati wa vita vya Siffin, Mu’awiyah alikuwa amepandikiza mbegu za uhaini ndani ya jeshi la Iraq, kama ilivyoelezwa kabla. Hili alilifanya kwa kutoa zawadi za dhahabu na fedha, na kwa kutoa ahadi za kutoa ardhi, mali binafsi, na vyeo vya kiraia na kijeshi vya ngazi ya juu kwa wale watu mashuhuri katika jeshi la Ali, kwa malipo ya msaada wao kwake. “Uwekezaji” wake ulileta faida kubwa sana kwake. Wale wapokeaji wa zawadi zake walikuwa wamemlazimisha Ali kusimamisha mapigano, na kukubali usuluhishi, na kwa njia hii, yeye Mu’awiyah alikuwa amefanikiwa katika kukwepa janga na kifo hapo Siffin. Wao sasa walikaa kwa matarajio, wakisubiri utekelezwaji, na Mu’awiyah, wa ahadi zake. Lakini Mu’awiyah aliporudi Damascus, alihisi kwamba sasa angeweza kumudu kuachana na huduma za wengi wa wateja wake ndani ya jeshi la Ali. Yeye, kwa hiyo, akawaambia kwamba hakuwa amewaahidi kitu chochote.

Wale wateja wakatambua kwamba walikuwa wamelaghaiwa na Mu’awiyah. Kwa huzuni kubwa na kukata tamaa, walimgeukia Ali, na wakamtaka yeye ayakatae makubaliano ya kuacha vita, na kurudia kupigana tena dhidi ya Mu’awiyah. Lakini Ali alikataa kufanya hivi, na akasema kwamba ilimbidi asubiri na kuona kama uamuzi wa wasuluhishi utakuwa unaendana na amri za Qur’an Tukufu au la kabla ya kuchukua hatua nyingine yoyote.

Lakini wale waliokuwa wateja wa Mu’awiyah hawakutaka kusubiri. Walimshinikiza Ali kupigana, na pale alipokuwa hakukubali, wao na wafuasi wao walitoka kwenye jeshi lake kwa pamoja, na wakavunja kiapo chao cha utii kwake. Walikuwepo watu 12,000 hawa waliokana kiapo chao cha utii kwa Ali baada ya vita vya Siffin. Hawa wanaitwa Khawarij, na walijikusanya katika sehemu inayoitwa Harura ambapo kutokea hapo walianza kupora nchi iliyozunguka hapo, na kuwaua watu wasiokuwa na hatia, na kwa kweli, kila mtu ambaye alikataa maoni yao juu ya serikali na siasa.

Ali alijaribu kuwashawishi hawa Khawarij kurejea Kufa, na kutoa mbele yake zile hoja zao za kutokukubaliana naye. Aliyajibu maswali yao na pingamizi zao vya kuridhisha sana, na baadhi yao, wakiwa wameridhika kwamba alikuwa yu sahihi, walirudisha kiapo chao cha utii kwake lakini wengine wengi hawakufanya hivyo. Sasa wakadai kwamba kwa kukubali kuurejesha mgogoro wake na Mu’awiyah kwenye kusuluhishwa na binadamu wanaoweza kufanya makosa, badala ya Kitabu cha Allah swt., Ali alikuwa amegeuka kuwa “kafir,” na kwamba “kutubia” kwake pekee ndiko kutamletea yeye wokovu.

Ali alivumilia ujeuri na ufidhuli wa Khawarij kwa matumaini kwamba watatambua kosa lao lakini hili liliwafanya kuwa wajeuri na mafidhuli zaidi. Sasa, viongozi wao wakaamua kuondoka Kufa, na kuweka makao yao makuu katika sehemu nyingine. Walichagua kijiji kinachoitwa Nahrwan kwa ajili ya lengo hili, na wakawaamuru Khawarij wote kukusanyika pale.

Kutokea Nahrwan, Khawarij wakaeneza hofu katika nchi. Walitenda maovu mapya mabaya zaidi ili kuficha hatia yao, aibu na majuto yao. Walipita wakiwaua watu bila ya kuchagua, bila kuwaacha hata wanawake na watoto. Kisha habari zikaja kwamba walikuwa wanapanga kuishambulia Kufa yenyewe.

Ilimbidi Ali kuchukua hatua mara moja kuzuia uhalifu na vurugu za Khawarij, na alikwenda mwenye mpaka Nahrwan kukutana na viongozi wao. Aliwaambia kwamba kulikuwa na hati ya usalama kwa wale wote miongoni mwao ambao wataiacha kambi yao, wakarudi majumbani kwao, na wakaishi kwa amani na majirani zao.

Wengi wao walitambua kwamba hawakuwa na sababu ya kupigana dhidi ya Ali, na waliondoka Nahrwan ili kurudi majumbani kwao. Lakini kiini cha watu 4,000 wasiokata tamaa walibakia wakaidi katika madai yao kwamba Ali alikuwa lazima “atubie” kabla ya kuweza kumkubali kama kiongozi wa Waislamu. Wao, kisha wakapaza ukelele wa shime ya vita “Hapana hukmu ila ya Allah,” na wakashambulia vikosi vya Ali. Ingawa walishambulia kwa kujisahau bila kujali, hawakuleta madhara makubwa kwenye vikosi vya Ali. Pale huyu Ali alipojibu mashambulizi, Khawarij walishindwa; wengi wao waliuawa, na ni wachache tu waliotoroka kutoka kwenye uwanja wa mapambano.

Ingawa Khawarij waliitwaa kama wito ile Aya ya Qur’an ya “Hapana hukmu ila ya Allah,” hawakuwa ama na nia wala uwezo wa kuweka Mamlaka ya Mbinguni katika dunia hii. Walitaka tu madaraka juu yao wenyewe. Walikuwa ni mchanganyiko wa mlipuko wa ugaidi, siasa na ushabiki wa kidini uliopindukia (ulokole). Kama ikibidi wakafanikiwa, watakuwa tu wamerudisha ubinafsi wa kikabila wa Waarabu wa kabla ya Uislamu. Hadi leo, wanabakia kiajabu ajabu wasiochanganyika katika historia ya umma wa Waislamu.

Dr. Hamid-ud-Din:

“Kharij waliwazuia watu kujiandikisha katika jeshi la Ali. Na kama mtu yeyote alipingana na imani zao, walimuua papo hapo. Kwa njia hii, Waislamu wengi waliuawa. Ali alituma mjumbe kwenda kuwashauri waachane na kufanya uhalifu dhidi ya watu wasio na hatia lakini wakamuua na yeye pia.

Kambi ya Kharij ilikuwa ipo Nahrwan. Ali pia aliongoza jeshi lake kwenda Nahrwan. Aliwataka Khawarij kuwatoa wale watu waliowauwa Waislamu wasio na hatia kwa ajili ya kushtakiwa na kuhukumiwa. Lakini walipiga kelele kwa sauti moja kwamba wao wote ndio waliowaua, na kwamba waliona kuwauwa watu kama hao (wale Waislamu ambao walikuwa hawachangii imani yao) kama ni wajibu wa heshima kuu. Ali kwa mara nyingine tena aliwaonyesha makosa yao, na akawasihi warejee majumbani kwao lakini majibu yao yakawa ni kinyume.

Mwishowe, Ali alimtuma Abu Ayub Ansari pamoja na bendera ya Uislamu katikati ya majeshi hayo mawili yanayopingana. Abu Ayub akaikunjua ile bendera, na akatangaza kwamba yoyote yule kutoka kwenye kambi ya Khawarij atakayekuja chini ya bendera hiyo, atakuwa yuko salama.

Khawarij wengi kwa kutambua makosa yao, walikuja chini ya bendera hiyo iliyokuwa imesimamishwa na Abu Ayub. Lakini wapiganaji wao 4,000 wakakataa kuiacha kambi yao. Walikuwa wamedhamiria kupigana dhidi ya Ali. Wakapiga kelele, “Hakuna hukmu ila ya Allah,” na kisha wakalishambulia jeshi la Ali. Walipigana kwa ushupavu wa mashabiki lakini wakazingirwa na kushindwa, na karibuni wote wakafa. (History of Islam, Lahore, Pakistan, uk. 202, 1971)

Ule ukelele wa shime ya vita wa Khawarij, “Hakuna hukmu ila ya Allah,” ulikuwa ni ujanja wa vitimbi tu, ulioundwa ili kuchukua madaraka ya kisiasa mikononi mwao, na kumnyima kila mtu mwingine yoyote.

Kwa wakati huo, Amr bin Al-Aas na Abu Musa al-Ashari, wale wasuluhishi wawili, walikuwa wamemaliza majadiliano yao ya siri, na walikuwa wako tayari kutoa tangazo. Wote walikuwa wamekubaliana kwaamba ilikuwa ni kwa maslahi ya Dar-ul-Islam kwamba Ali na Mu’awiyah wote wajiuzulu au waondolewe, na umma wa Waislamu wajichagulie kiongozi mpya wao wenyewe.

Wasuluhishi hao na waandamizi wao walikutana huko Adhruh. Watu mia nne wa kila upande pia waliwasili katika eneo la tukio, kwa mujibu wa makubaliano ya kuacha mapigano. Ujumbe wa Syria ulikuwa ukiongozwa na Abul Awar Salmi, na ule wa Iraq uliongozwa na Abdallah ibn Abbas na Shuayh ibn Hani.

Watu wengine wengi pia walikuja Adhruh kusikiliza hukumu ya wasuluhishi juu ya majaaliwa ya Dar-ul-Islam. Miongoni mwao alikuwa ni Abdallah ibn Umar, Abdallah ibn Zubeir, Abdur Rahman bin Abu Bakr, Saad bin Abi Waqqas, na Mughira bin Shaaba.

Amr bin Al-Aas alimwambia Abu Musa kwamba yeye alikuwa anamheshimu sana kwa vile yeye Abu Musa hakuwa tu sahaba wa Mtume wa Allah swt., bali pia alikuwa ni mwanazuoni mkubwa, na kwa sababu hii, alimstahi yeye katika kila kitu, na pia kwa sababu hii, yeye Abu Musa anapaswa kuwa wa kwanza kutoa tangazo hilo la uamuzi wao wa pamoja, ambao yeye Amr atauthibitisha baadae.

Abdallah ibn Abbas alimuonya Abu Musa kwamba Amr angeweza kumzidi maarifa na kumpita ujanja, na akamshauri kwamba amwache Amr awe wa kwanza kutoa tangazo hilo. Lakini Abu Musa hakuusikiliza ushauri huu wa busara, na akasema: “Jambo lenyewe ni thabiti na hakuna nafasi ndani yake kwa Amr bin Al-Aas kufanya ujanja au kushinda.”

Abu Musa alikuwa amejisahau, ameleweshwa na kule kuonyeshwa “heshima” kulikofanywa na Amr bin Al-Aas kwake. Yeye ndipo akapanda kwenye mimbari kutoa hilo tangazo la kihistoria, na akasema:

“Enyi Waislamu! Huzuni nyingi na taabu zimeuadhibu umma wa Muhammad kwa vita vya Ali na Mu’awiyah. Kwa hiyo, sisi wote tumeamua kuwaondoa wote wawili, na tumekubaliana kwamba haki ya kuchagua khalifa mpya itolewe kwa umma wa Waislamu wenyewe – kwenu ninyi nyote.”

Ule ujumbe wa Iraq uliaibika sana kusikia tangazo hili lakini ukaamua, hata hivyo, kusikiliza yule msuluhishi mwingine atasema nini. Abu Musa akaketi chini baada ya tangazo lake, na kisha Amr bin Al-Aas akasimama ili kutoa tangazo lake. Yeye akasema: “Enyi Waislamu! Nyie wote mmesikia kile alichokisema Abu Musa kuhusu kuondolewa kwa Ali. Amemuuzulu Ali kama khalifa. Ninaunga mkono uamuzi wake, na ninatangaza kwamba Ali ameuzuliwa kwenye ukhalifa. Na katika nafasi ya Ali, ninamteua Mu’awiyah kama khalifa wenu mpya…..”

Abu Musa alikuwa bado hajamalizia maelezo yake wakati yalipozuka makelele ya hasira. Abu Musa alilalamika kwa kuchanganyikiwa na kwa hasira: “Muongo! Sijasema hayo mimi. Wewe ni muongo usiye na haya kabisa. Wewe ni mbwa aliyebebeshwa mzigo wa vitabu na ambaye anatweta na kutoa ulimi wake anapokuwa chini ya mzigo huo.” Amr aliweza kuimudu hali hiyo, na akazirudisha sifa hizo kwa kusema: “Wewe ni punda ambaye amebebeshwa vitabu, na ambaye anatoa mlio mkali chini ya mzigo mzito.”

Huyu “mbwa” na huyu “punda” walizungumza kwa sauti kali, walikemea na kutazamana kwa vitisho kwa muda mchache, na kisha wakashambuliana vikali sana. Walitwangana na kupigana, na “walibweka” na “kulia kipunda” katikati ya zogo mpaka wakawa wamepwelewa na sauti. Kulikuwa na vicheko pia, ingawa dhidi ya Abu Musa pekee.

Baada ya miezi sita ya majadiliano ya faragha, “mlo” pekee ambao wasuluhishi hao – Amr bin Al-Aas na Abu Musa walikuwa wameuandaa kwa ajili ya “ujenzi wa maadili” wa mamia ya Waislamu ambao walikuwa wametoka kwa makundi kwenda Adhruh kwa ajili ya “karamu” hiyo, ulikuwa ni “muziki” ambao ulitolewa na yule wa kwanza wao kwa “kubweka” na yule wa pili kwa “kulia kipunda.”

“Onyesho” lilikuwa, hatimaye, limekwisha, na Waislamu ambao walikuwa wameku- ja kutoka sehemu za mbali, waliondoka Adhruh ili kurejea majumbani kwao.

Abu Musa aligundua kwamba amekuwa kichekesho cha Waarabu wote, na akakimbilia Yemen kwenda kuficha aibu yake. Yeye alikuwa ni mtu mwenye uhodari wa wastani lakini kugongana kwa matukio kulikuwa kumemuweka yeye katika hali ambamo huenda alifikiria kwamba alikuwa anatawala hatima ya umma wa Waislamu. Majivuno yake yalikuwa yanapigana na busara, na majivuno yakashinda. Kazi aliyotakiwa aishike ilikuwa ni kubwa sana kwa mtu aliyekwamishwa na ukosefu wa uwezo kama alivyokuwa yeye, na aliiharibu. Alikuwa ni mmoja wa wasiri wa Umar bin al-Khattab ambaye alikuwa amem- teua kuwa gavana, kwanza wa Basra na kisha wa Kufa.

Lile tishio kwa Mu’awiyah lilikuwa limepita kudumu, na katika juhudi zake za kuukama- ta ukhalifa, uamuzi sasa umepitia kwake. Madai yake ya ukhalifa yalitegemea juu ya ile hukumu ambayo Amr bin Al-Aas, yule “mwenye sauti katika uchaguzi” aliyoitoa pale Adhruh.

Hukumu ya Amr ilikuwa ni ujanja wa kiinimacho cha kisiasa ambacho kingemsisimua Machiavelli; lakini kwa watu wa Syria, ilikuwa na mamlaka ya kibali kutoka mbinguni kwenyewe, na ilikuwa, kwa hivyo, isiobadilika.

R. A. Nicholson:

“Ni desturi ya fikira za Kiarabu za kimaadili kwamba huu udanganyifu wenye maamrisho ulitukuzwa na wafuasi wa Mu’awiyah kama ushindi wa kidiplomasia ambao ulimpa yeye kisingizio kinachofaa kwa utwaaji wa cheo cha khalifa.” (A Literary History of the Arabs, uk. 192-193, 1969)

Usuluhishi uligeuka kuwa kichekesho na hasara tupu. Uamuzi wake, kwa hali yoyote, ulikuwa wa kupita uwezo wa kisheria. Hakuna mtu hata mmoja aliyewapa hao wasuluhishi mamlaka ya kutoa hukumu juu ya ukhalifa au kuuzulu au kuteua khalifa. Wafuasi wa Mu’awiyah walikuwa wanatafuta kulipiza kisasi kwa ajili ya kuuawa kwa Uthman. Mu’awiyah alikuwa amewashawishi kwamba Ali alikuwa anahusika na kifo cha Uthman, na ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba walipigana hapo Siffin. Hawakupigana vita dhidi ya Ali ili kumtawalisha Mu’awiyah.

Lakini wasuluhishi hao hawakuchunguza machimbuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Walizungumzia tu kuhusu ukhalifa ingawa haukuwa ndio suala lenye mgogoro. Kazi yao pekee ilikuwa ni kutafuta ni nani aliyemuua Uthman, na ikiwa kama Mu’awiyah alikuwa anayo haki ya kulipiza kisasi juu ya uhalifu huo.
Abu Musa alitoa hukumu yake ya “Mungu mtu” kwa “kumuuzulu” Mu’awiyah. Uenguliwaji wa Mu’awiyah ulikuwa na maana gani hata hivyo? Na Abu Musa alimuengua yeye kutoka kwenye kitu gani? Mu’awiyah hakuwa khalifa, wala hakukuwa na mtu aliyependekeza jina lake kwenye ukhalifa. Kwa upande mwingine, Ali alikuwa ndiye khalifa halali wa Waislamu. Alichaguliwa kwa makubaliano ya Muhajirin na Ansar, na sehemu zote za himaya hiyo, pamoja na kujitenga kwa Syria pekee, zilikuwa zimemtambua yeye kama kiongozi wao.

Kama wasuluhishi, au hasa, kama wenye sauti, Amr bin Al-Aas na Abu Musa walikuwa wamejiingiza kwenye majadiliano marefu juu ya siasa na vita, na labda kwenye hali ya baadaye ya umma wa Waislamu lakini kitu kimoja walichokuwa hawakukifanya kilikuwa ni kuiangalia Qur’an Tukufu. Waliiweka Qur’an nje ya majadiliano yao huko Adhruh kama vile tu, miaka mingi nyuma, watangulizi wao katika kuwa na sauti katika uchaguzi, walivyoiweka Qur’an nje ya majadiliano yao katika banda la Saqifah huko Madina.

Kwa “utukizi” wa ajabu, wenye sauti ya uchaguzi wote wa Waarabu, ama ndani ya Saqifah au katika Kamati ya Uchaguzi ya Abdur Rahman bin Auf, au huko Adhruh, walijidhihirisha wenyewe “wenye mzio” na Qur’an Tukufu. Au, ilikuwa ni kinyume chake – Qur’an Tukufu ikijionyesha yenyewe kuwa “yenye mzio” na wenye sauti katika uchaguzi?

Wenye sauti ya uchaguzi waliiweka Qur’an nje ya mashauriano yao au Qur’an yenyewe ilikaa nje yao – njia zote, ilikuwa kwa kweli moja ya “utukizi” wa ajabu katika historia ya Waislamu. Kwa sababu za kisirisiri, wenye sauti katika uchaguzi wote kwa upande mmoja, na Qur’an Tukufu kwa upande mwingine, vilibakia vimetengana kwa mbali sana, kimoja hadi kingine.

Amr bin Al-Aas na Abu Musa walipaswa kuifanya Qur’an kuwa mwongozo wao katika usuluhishi. Walikuwa na wajibu wa kuunda maamuzi yao katika mtazamo wa sheria za Kitabu cha Allah swt. Amri za Allah swt katika hali hii ndio mkato wa wazi.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ ۖ فَإِنْ تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ{59}

“Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na Wenye mamlaka miongoni mwenu. Kama mkikhitlafiana katika jambo lolote, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho: hilo ni bora zaidi na lenye mwisho mzuri zaidi.” (Sura ya 4; Aya ya 59)

Wasuluhishi hawa, inavyoonekana, walisahau vyote; amri za Allah zote zilizotajwa katika Aya hiyo iliyopita, na wajibu wao wenyewe. Lakini Qur’an haikuwasahau wao, na ikaonyesha kile walichokifanya au walichoshindwa kufanya katika Aya inayofuata:

يُدْعَوْنَ إِلَىٰ كِتَابِ اللَّهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ{23}

“Wanaitwa kwenye Kitabu cha Mwenyezingu, ili kiwahukumu (katika migogoro yao) kisha kundi moja kati yao hukataa, nao wamegeuka.”(Sura ya 3; Aya ya 23)

Amr bin Al-Aas na Abu Musa – wale wasuluhishi walijifanya kuwa lile kundi lililokigeuka Kitabu cha Allah swt. Walikuwa wamependelea kuongozwa na matamanio yao binafsi, na kwa sababu hii, waliivuta hukumu ya Qur’an juu yao wenyewe:

وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ {47}

“Na watakaoshindwa kuhukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu; basi hao ndio waasi.”(Sura ya 5; Aya ya 47)

Katika vita vya Siffin, majeshi ya Iraq na Syria yalikabiliana kwa siku 110. Yalikuwepo mapambano 90 kati yao ambamo ndani yake Wairaqi 25,000 na Wasyria 45,000 waliuawa.Vita hivi vya kutisha vilikuwa ni matunda ya tamaa na uchu wa madaraka wa Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas. Mu’awiyah alikuwa ndiye gavana wa Syria, na alikuwa haoni karaha sana kwa kitu chochote kuliko kile cha kuipoteza nafasi hiyo.
Amr bin Al-Aas alikuwa ni gavana wa Misri lakini alikuwa amefukuzwa na Uthman, na alikuwa na hamu sana ya kukipata tena cheo chake cha zamani. Kubakia au kurudia vyeo vyao, wote walikuwa tayari kufanya kitu chochote na kulipa gharama yoyote Ukweli na Haki havikuwa na maana yoyote kwao. Waliweza kuigharikisha Dar-ul-Islam kwa uongo, na kwa damu ya Waislamu ili kufanikisha nia na matamanio yao.

Wale “wakubwa watatu” wa Basra (Masahaba wa vita vya Ngamia), na Mu’awiyah na Amr bin Al-Aas waliimaizi fursa yao kubwa kwenye kifo cha Uthman, na wakaikamata. Kisasi kwa ajili ya damu yake kilikuwa ni ubao mwembamba ambao uligawa maadili yao kwenye uchu wao wa dhahiri wa madaraka. Uthman – aliyekufa alikuwa na thamani sana kwao kuliko Uthman – alivyokuwa hai. Kwa hiyo, wao walimpa msaada wote waliowezaili afe.

Lakini mara tu alipokufa, ikawa halali, kwa kweli, ilikuwa ni wajibu, juu yao kufanya mauaji ya halaiki kwa jina la kulipiza kisasi kwa kuuawa kwake.

Vita vya Basra na vya Siffin vilikuwa ndio mauaji ya halaiki ya Waislamu yaliyoshurutishwa na mantiki ya “Siasa ya hali na mali.”

Toynbee anasema kwamba Muhammad na Ali walikuwa hawalingani na wachuuzi mafahari wa Makka (Bani Umayya) katika siasa za hali na mali. Kwa maana fulani, anaweza kuwa sahihi. Muhammad na Ali walisita kuua hata muabudu masanamu, bila kuzungumzia kuua Mwislam. Hawakuweza kuua mtu yeyote kwa ajili ya madaraka ya kilimwengu. Walikuwa, kwa hiyo, wamekwazwa katika “mashindano” yao na Bani Umayya.