read

Vita Vya Uhud

Hivi vita vya uhud vilikuwa ni kisasi dhidi ya Waislamu kufuatia vile vita vya Badr. Baadhi ya watu mashuhuri wa Quraishi kama vile Abu Jahl, Utbah, Shaiba, Walild, Umayya bin Khalaf, na Hanzala bin Abu Sufyan, waliuawa kwenye vita vya Badr. Baada ya kifo cha Abu Jahl, uongozi wa watu wa Makka ulipitia kwa mwenza wake, Abu Sufyan, ambaye alikuwa mkuu wa ukoo wa Banu Umayya. Kulikuwa na huzuni nzito hapo Makka kwa kupotea kwa wakuu wengi lakini Abu Sufyan alizikataza zile familia zilizofiwa kulia na kuomboleza kuondokewa kwao. Machozi, alijua, yangeweza kusafisha uovu kutoka nyoyoni.

Lakini muda na machozi, alidai, havitaachiliwa kuponya majeraha yaliyoupata utawala wa kikabila wa Makka huko Badr. Yeye mwenyewe alikula kiapo kwamba atajiepusha na kila anasa mpaka awe amewatendea Waislamu kama walivyomtendea. Yeye na wakuu wengine wa Maquraishi waliutumia mwaka mzima wa shughuli za msisimko ambamo waliandaa na kufundisha jeshi jipya.

Mwaka mmoja baada ya vita vya Badr, lile jeshi jipya la waabudu-masanamu wa Makka lilikuwa tayari kusimama uwanjani dhidi ya Waislamu. Mnamo Machi 625 Abu Sufyan aliondoka Makka akiongoza wapiganaji elfu tatu waliozoeshwa. Wengi wao walikuwa askari wa miguu lakini walisaidiwa na kikosi chenye nguvu cha wapanda farasi.

Pia wakiandamana na jeshi hilo, walikuwa ni kundi la wanawake wenye kupenda vita. Kazi yao ilikuwa ni kuendeleza “vita vya kimawazo” dhidi ya Waislamu kwa kusoma mashairi na kuimba nyimbo za mapenzi ili kuhimiza ujasiri na shauku-ya-kupigana ya askari hao.

Walijua kwamba hakuna kilichohofisha kwa Waarabu kiasi hicho kama dhihaka za wanawake kwa waoga, na vile vile walijua kwamba hakuna chenye kufaa zaidi kuwageuza kuwa wapiganaji wasiojali kabisa, kama ahadi ya mapenzi ya kimwili. Majikedume haya yalikuwa ni pamoja na wake za Abu Sufyan na Amr bin Al-As, na dada zake Khalid bin Walid.

D.S. Margoliouth:

“Abu Sufyan anaonekana kufanya juhudi zake zote, na, kama badala ya muziki wa kijeshi, alisababisha ama kuruhusu jeshi hilo kufuatiwa na kundi la wanawake, ambao, kwa kutishia na kuahidi, walikuwa waweke ujasiri wa vikosi hivyo kwenye kiwango sahihi; kwani hakuna chochote alichohofia aliyekimbia kutoka kwenye uwanja wa mapambano, zaidi kuliko kushutumiwa na wanawake wa kwao. Wanawake wa Kikuraishi walifanya kazi ya kipekee yenye uhakika. Mke wa Abu Sufyan alitoa ushauri kwamba mwili wa mama yake Muhammad ufukulliwe na kuwekwa kama mateka; lakini Maquraishi waliukataa ushauri huu (ambao kwamba uwezekano wake kwa kweli ulikuwa na mashaka) kwa kuhofia visasi.”
(Muhammad and the Rise of Islam, 1931)

Kana kwamba vile vidokezo vya mapenzi vilivyotolewa na wale wanawake wa Kikuraishi havikutosheleza, Abu Sufyan aliweka kampeni yake kwenye “utakatifu wa kidini” vilevile.

Kuondoa mashaka kabisa katika akili ya mtu yoyote kwamba alikuwa kwenye vita tukufu dhidi ya Waislamu, alimuweka Hubal, lile sanamu ambalo ukoo wa Banu Umayya walili- abudu kama mungu wao mkuu, juu ya ngamia, na akalibeba kwenda nalo ndani ya vita. Kazi ha Hubal ilikuwa ni kuzidisha hamasa ya waabudu-masanamu kwa kuwepo kwake kwenye uwanja wa vita.

Mapenzi ya kijinsia na dini vilikuwa ndio vitu viwili vipya vilivyoandaliwa na Maquraishi katika vita vyao dhidi ya Muhammad na Uislamu.

Betty Kelen:

“Katika kiti chenye mwamvuli (mgongoni mwa tembo) alipanda Hubal, kwenye mapumziko kutoka kwenye Al-Kaaba. Abu Sufyan alikuwa ameshikilia kabisa kwamba mbali kabisa na mawazo ya kisasi na njia za misafara, alikuwa ameingia kwenye vita vya jihad.” (Muhammad, the Messenger of God, 1975)

Muhammad Mustafa, Mtume wa Uislamu, pia alizisikia habari za uvamizi wa Madina unaokaribia kutoka kwa watu wa Makka, na yeye pia aliwaamuru wafuasi wake kujiandaa kwa ulinzi. Waislamu mia saba walikuwa tayari kumfuata kwenye vita.

Mtume (s.a.w.) aliliweka jeshi lake kwa mlima wa Uhud kuwa nyuma yake hivyo kwamba lilisimama kuelekea Madina. Wakati jeshi la watu wa Makka lilipokuja, lilichukua nafasi yake mbele ya Waislamu hivyo kwamba lilikuwa limesimama kati yao na Madina ambayo ilikuwa nyuma yao.

Sir William Muir:

“Abu Sufyan, kama kiongozi wa upagani, aliliteta jeshi la Makka; na wakielekea Uhud, akaliongoza mbele ya Muhammad. Bendera ilikuwa imeshikwa na Talha mtoto wa Abdal Uzza. Vikosi vya upande wa kulia viliongozwa na Khalid; na vya kushoto na Ikrima mtoto Abu Jahl. Amr bin Al-As alikuwa juu ya farasi wa Kiquraishi.” (The Life of Muhammad, 1877)

Sir John Glubb:

“Waislamu walisonga mbele na watu 700 dhidi ya wapiganaji 3000 kutoka Makka. Zaidi ya hayo, wakati Waislamu waliweza kukusanya nguvu ya watu mia moja tu wenye deraya, na bila ya farasi, Maquraishi na washirika wao walikuwa na watu 700 wenye deraya na wapanda farasi 200.

Wakitaka kuziba nyuma yao kutokana na idadi yao ndogo, Waislamu walijipanga chini ya mlima Uhud. Upande wao wa kulia na nyuma vilifunikwa na milima, lakini upande wao wa kushoto ulikuwa kwenye uwanja wa wazi na kwa hiyo uliachwa kwenye shambulizi la askari wa farasi wa adui.

Kujihami dhidi ya hili, Muhammad aliweka wapiga mishale hamsini kwenye upande huu, pamoja na amri ya kutoiacha nafasi yao kwa hali yoyote ile, ambapo kutokea hapo wanaweza kuulinda upande wa kushoto wa Waislamu kutokana na farasi wa Maquraishi.

Watu wa Makka waliweka safu yao kuwaelekea Waislamu kwa namna ambayo Waislamu, migongo yao ikielekea Uhud, walikuwa wakitazama kuelekea Madina, ambapo safu ya Maquraishi iliwakabili na Madina ikiwa nyuma yao, hapo wakiwa kati ya Waislamu na mji huo.

Maquraishi walikuwa wamekuja na wanawake wachache, wakiwa wamepanda kati- ka vitanda vya kubebwa na ngamia. Hawa sasa, wakati safu mbili hizo zilipokuwa zinasogeleana, waliendelea kuamsha shauku ya watu wa Makka, wakipiga vijingoma, wakisoma mashairi ya kivita na kushusha nywele zao ndefu.”
(The Great Arab Conquests)

Vita vya Uhud vilianza kama vile tu vita vya Badr vilivyoanza, kwa mpiganaji wa Makka kuchomoza kutoka kwenye safu zao na kuwapa changamoto Waislamu kwa mapambano ya mtu mmoja mmoja.

Sir William Muir:

“Akipepea bendera ya Kikuraishi, Talha, yule mshika-bendera wa jeshi la Makka, alisonga mbele, na kuwapa changamoto maadui kwenye pambano la mtu mmoja mmoja. Ali alitoka mbele, na, akimvamia, kwa pigo moja la upanga wake alimuan- gusha chini. Muhammad, ambaye aliliangalia kwa makini pambano hilo la haraka, aliguta kwa mshangao, kwa sauti kubwa: “Allah-u-Akbar!” na mguto huo, ukirudiwa, ulipaa kwa sauti kubwa mno kutoka kwenye jeshi zima la Waislamu.” (The Life of Muhammad, London, 1877)

Muhammad Husein Haykal:

“Talha ibn Abu Talha, mshika bendera wa Makka, alichomoka mbele akiwataka Waislamu kupambana naye. Ali ibn Abu Talib alitoka mbele kupigana naye. Pambano hilo lilikwisha mara wakati Ali alipompiga adui yake dhoruba moja kali sana. Kwa furaha kuu, Mtume (s.a.w.) na Waislamu walipiga ukelele mkubwa, “Allah-u-Akbar.” (The Life of Muhammad, 1935, Cairo)

R.V.C.Bodley:

“Watu wa Makka, wakisaidiwa kwa ukarimu sana na wanawake ambao walileta vigoma vyao, walirusha matusi kwa Waislamu. Haya yalipokelewa na Hind, mke wa Abu Sufyan, ambaye aliongoza vipokeo vya shangwe alipokuwa akicheza kulizunguka lile sanamu lililokuwa limekaa juu ya ngamia.

Talha, yule mshika-bendera wa wapagani wa Kiquraishi, alikuwa ndiye mtoa changamoto wa kwanza wa watu wa Makka. Vile alipotoka kwenye safu za Abu Sufyan, Ali alitoka kwenye safu za Muhammad. Watu wawili hawa wakakutana katikati ya ‘ardhi isiyo na mwenyewe.’ Bila ya maneno au madoido ya kutangulia, pambano likaanza. Talha kamwe hakupata nafasi. Jambia la Ali liliwaka katika lile jua la asubuhi na kichwa cha mshika-bendera huyo kiliruka kutoka kwenye mabega yake na kikabingirika kwenye mchanga.

‘Allah-u-Akbar! aliguta Muhammad. ‘Allah-u-Akbar!’ ‘Allah-u-Akbar!’ ilirudiwa kutoka kwa Waislamu waliokuwa wakiangalia kwa shauku.” (The Messenger, the Life of Muhammad, New York,1946)

Sir John Glubb:

“Zile safu mbili zilisogea kutoka kila upande. Talha ibn Abdul Uzza, wa Abdul Dar, akiungua kwa chuki juu ya dhihaka za Abu Sufyan, na akiwa amebeba bendera ya Maquraishi, alitoka nje mbele ya safu na akatoa changamoto kwa mwislamu yoyote kwenye pambano la mtu mmoja mmoja. Ali alichepuka mbele na akamuua kwa pigo moja la upanga wake, huku bendera ya Maquraishi ikidondoka chini. Kutoka kwenye safu za Waislamu ikatoka sauti kubwa, “Allah-u-Akbar, Mungu ni Mkuu.”
(The Life and Times of Muhammad)

Hili ni moja ya maonyesho ya kuvutia katika historia ya Uislamu. Muhammad, Mjumbe wa Allah (s.w.t.) alikuwa akimwangalia binamu yake, Ali, akipambana, na alisisimuliwa na ushindi wake wa haraka. Wakati lile pigo zito la upanga wa Ali lilipomuua jenerali wa wapagani, Muhammad alipiga ukelele Allah-u-Akbar, na ukelele huo wa kivita ulifuatishwa na jeshi zima la Uislamu.

Pigo la Ali lisilozuilika limesababisha bendera ya watu wa Makka, ile nembo ya uabudu masanamu na ushirikina, kuanguka chini kwenye vumbi. Alishinda raundi ya kwanza kwa Uislamu, na alikuwa ametoa pigo la kifo kwenye hamasa ya Maquraishi.

Wakati Ali aliporudi kwenye safu zake, ndugu yake Talha, Uthman ibn Abu Talha, alifanya jaribio la kuipata tena ile bendera ya Makka. Lakini Hamza akatoka kwenye safu za Waislamu, na akamuua.

Muhammad Husein Haykal:

“Wakati Ali alipomuua yule mshika-bendera wa Makka, Talha ibn Abu Talha, ilinyanyuliwa mara moja tena na Uthman ibn Abu Talha.

Na pale Uthman alipoanguka mikononi mwa Hamza, ilinyanyuliwa tena na Abu Sa’d ibn Abu Talha. Mara alipoinyanyua ile bendera ya Makka aliwakemea Waislamu: “Mnajidai kwamba mashahidi wenu wako peponi na wetu wako motoni? Wallahi, mnadanganya!

Kama mmoja wenu kwa ukweli anaamini habari kama hiyo, naaje hapa mbele apigane na mimi.” Changamoto yake ilimvuta Ali ambaye alimuua papo hapo. Hawa Banu Abd al Dar waliendelea kuishika bendera ya Makka mpaka wakapoteza watu tisa.” (The Life of Muhammad)

Ali, simba kijana, peke yake aliuwa washika bendera nane wa waabudu-masanamu wa Makka. Ibn Athir, yule mwanahistoria wa Kiarabu, anaandika katika Tarikh Kamil: “Mtu aliyewaua washika-bendera wa wapagani alikuwa ni Ali.” Baada ya kifo cha mshika-bendera wake wa tisa, Abu Sufyan aliliamuru jeshi lake kusonga na kushambulia mipango ya Waislamu. Wakati Mtume (s.a.w.) alipoliona jeshi likisogea, yeye pia aliwatahadharisha Waislamu.

Alishika upanga kwenye mkono wake, na akautoa kwa yeyote ambaye angeweza kuuletea heshima. Baadhi ya waliokuwa na matumaini walitokeza mbele yake kuuchukua lakini akawanyima.

Muhammad Ibn Ishaq:

“Mtume (s.a.w.) alivaa makoti mawili ya deraya katika siku ya vita vya Uhud, na alichukua upanga na akaupunga akisema: “Ni nani atauchukua upanga huu na haki yake?” (yaani, kuutumia kama ipasavyo na unavyostahili kutumiwa). Baadhi ya watu walisimama ili kuuchukua lakini aliuzuilia kuwapa mpaka Abu Dujana Simak bin Kharasha, ndugu yake B. Saida, aliposimama na kuuchukua.

Umar alisimama kuuchukua, akisema: “Nitauchukua pamoja na haki yake,” lakini Mtume (s.a.w.) aligeukia pembeni na alikokuwa na akaupunga mara ya pili akitumia maneno yale yale. Kisha Zubayr bin al-Awwam akasimama naye pia akakataliwa, na wawili hawa wakawa wamefedheheka sana.”
(The Life of the Messenger of God)

Mtume (s.a.w.) alimpa upanga huo Abu Dujana, mmoja wa Ansari. Aliuchukua na akautu- mia kama ulivyostahili kutumiwa. Alithibitisha ile imani bwana wake aliyokuwa amemuwekea. Wale wanawake wa Makka walikuwa wamekaa kitako juu ya ngamia wao na walikuwa wakiangalia lile tendo la haraka. Jeshi lao liliposonga mbele kushambulia Waislamu, na wao pia waliingia kazini.

Walianza kuwachochea wapiganaji wao kuwaua Waislamu. Waliimba nyimbo ambazo zilikuwa zimejaa ukaribisho na dharau – ukaribisho kwa mashujaa wao na dharau kwa wale waoga. Kwa muziki wao na ushairi wao wenye ushawishi wa hali ya juu, waliwachochea watoto hao wa jangwani wenye pupa kwenye ghadhabu za kupigana.

Betty Kelen:

“Vikiwa vimejengwa juu kabisa ya ngamia wengi vilikuwa ni vibanda vidogo, au machela, ambamo walipanda kikosi cha wanawake waliofunzwa vyema na Hind kuimba tenzi za kivita ambazo zitawaweka wanaume wao katika msisimko au ghadhabu na kupinga woga.

Vita viliungwa. Hind na wanawake wenzie walisonga mbele pamoja na majeshi, wak- itawanyika uwanjani kwa karibu sana kiasi walivyoweza kuthubutu kuwafikia wale wanaume wanaopigana, huku wakipiga vigoma vyao kwa mpigo mkali na wakikemea: “Mabinti wa Nyota ya Asubuhi inayong’ara, Wakiwaangalieni kutoka kwenye vitanda vyenye hariri ni sisi, Wacharazeni! Katika mikono yetu tutawakumbatia; Kimbieni, na kamwe tena hatutawashikeni.” (Muhammad, the Messenger of God)

Muhammad Husein Haykal:

“Hapo kabla wanawake wa Kiislam (huko Arabuni) walikuwa wakijionyesha sio tu kwa waume zao bali kwa wanaume wengine wowote waliowataka.

Walikuwa wakitoka nje kwenye sehemu za wazi mmoja mmoja au katika vikundi na kukutana na wanaume na vijana bila ya kizuizi au hisia ya aibu. Waliangaliana kwa hisia kali na vidhihirisho vya mapenzi na tamaa. Hili lilifanyika kwa ukweli wa wazi na ukosefu wa aibu kwamba Hindi, mke wa Abu Sufyan, hakuwa na haya yoyote juu ya kuimba katika wakati wa hadhara na wa hatari kama Siku ya Uhud.

“Songeni mbele nasi tutawapiga pambaja nyie! Songeni mbele na sisi tutatandaza mabusati kwa ajili yenu! Geuzeni migongo yenu nasi tutawaepuka ninyi! Geuzeni migongo yenu nasi kamwe hatutawajieni ninyi.”

Miongoni mwa idadi ya makabila, uzinzi haukuonekana kamwe kama ni kosa kubwa. Kucheza kimapenzi na kufanya urafiki na mwanamke vilikuwa ni matendo ya kawaida.
Mbali na cheo maarufu cha Abu Sufyan na jamii yake, wana tarikh wanasimulia, kuhusu mke wake, Hadith nyingi mno za mapenzi na hisia kali na wanaume wengine bila ya kuweka doa lolote juu ya heshima yake”. (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Watu wa Makka walijiandaa vema na walikuwa wengi zaidi kuliko Waislamu. Zaidi ya hayo, kuwepo katika uwanja wa vita, kwa mungu wao, Hubal, na wanawake wao, ulikuwa ni uhakikisho kwamba hamasa yao haitalegea, hususan, baada ya hawa wanawake kuwa wameingiza kwenye mapambano, kisaidizi kipya na cha kuhatarisha cha kishawishi.

Lakini licha ya manufaa haya ya dhahiri na yasiyo dhahiri, hawa watu wa Makka walikuwa wakifanya maendeleo, kidogo, kama yalikuwepo. Kwa kweli, hapo mwanzoni, vita vilielekea kwenda dhidi yao.

D.S.Margoliouth:

“Inaelekea pia kwamba katika kuanza mambo yalikuwa yakienda kama vile Mtume (s.a.w.) alivyodhania. Wale mashujaa wa Badr, Ali na Hamza, walisababisha vifo bila kizuizi kama hapo kabla; ujasiri wa Kiquraishi ulilazimika kukutana na mashujaa hawa katika mwandamano wa mapambano ya mtu mmoja mmoja, ambamo mashujaa wao wenyewe waliuawa, na kuangushwa kwao kulieneza mfadhaiko na hofu.” (Muhammad and the Rise of Uislamu, London, 1931)

Shambulizi la Ali, Hamza na Abu Dujana lilieneza hofu na fadhaa katika safu za Makka, na wakaanza kuyumba. Waislamu wakaendeleza fursa yao.

Sir John Glubb:

“Ali ibn Abi Talib aliendelea bila hofu kwenye safu za adui – ilikuwa ni Badr tena; Waislamu walikuwa wasioshindika.” (The Great Arab Conquest, 1963)

Ali alizivunja safu za Maquraishi, na alikuwa tayari yuko ndani kabisa ya safu zao. Wakishindwa kuhimili shambulizi lake, walianza kuachia uwanja. Akiwa hayuko mbali naye, ami yake, Hamza, alikuwa akishughulika kukata njia yake kati ya kundi kubwa la maadui. Kati yao, walikuwa wakilisaga jeshi la Maquraishi.

Ilikuwa ni katika wakati huu ambapo matukio mawili yalitokea ambayo yalisababisha mpinduko katika mafanikio ya Waislamu, na ambayo yaliwanyang’anya ushindi kutoka mikononi mwao. La kwanza lake likiwa ni kifo cha Hamza.

Hinda, mke wa Abu Sufyan, alikuwa amekuja kutoka Makka na mtu mmoja, Wahshi, mtumwa wa Kihabeshi, kuja kumuua Hamza, na alikuwa amemuahidi kumpa sio tu uhuru wake bali pia na dhahabu nyingi, madini ya fedha na hariri katika kufanikiwa kwake. Alikuwa anafahamika kwa ustadi wake katika kutumia silaha ya “taifa lake”, mkuki.

Wahshi alijificha nyuma ya jiwe akingojea wasaa wa fursa, na mara ukatokea. Pale tu Hamza alipomuua muabudu-sanamu mmoja, na akamrukia mwingine, Wahshi akasimama, akachukua shabaha kali, na akairusha ile silaha ya kombora ambayo kwayo hapakuwa na kinga dhidi yake. Mkuki huo ukampata Hamza kwenye kinena. Alianguka chini na akafa karibu mara moja.

Tukio jingine lilihusisha sehemu kuu ya jeshi la Madina. Kutetereka na kuchanganyikiwa kwa jeshi la Makka kulikuwa kunaonekana wazi kabisa kwa muda huu, na Waislamu walichukulia kwamba tayari wamekwishapata ushindi. Kwa shauku kubwa ya kutokosa fursa ya kumpora adui, walisahau nidhamu yao.

Hila hii iligunduliwa na wale wapiga mishale waliokuwa wamewekwa na Mtume (s.a.w.) pale katika kijinjia muhimu cha mlimani. Wao pia walidhania kwamba adui alikuwa amekwisha shindwa, na alikuwa anakimbia. Walifikiri kwamba kama wenzao kule kwenye uwanja wa vita watakamata mizigo ya adui, basi wao wenyewe watapoteza sehemu yao ya ngawira. Hofu hii iliwachochea wao kushuka kule chini bondeni dhidi ya amri halisi ya Mtume.

Kapteni wao, Abdullah ibn Jubayr, aliwasihi wasiache kile kijinjia lakini hawakumsikiliza, na wakaenea ndani ya bonde. Tamaa yao ya ngawira iliwanyima Waislamu ushindi katika vita vya Uhud!

Sasa, jenerali mmoja wa Makka, Khalid bin al-Walid, akagundua kwamba kile kijinjia muhimu upande wa kushoto wa jeshi la Madina hakikuwa na ulinzi. Yeye haraka sana akaichukua fursa hiyo kuwashambulia askari doria wachache waliokuwa bado wapo pale kwenye kinjia kile, kwa wapanda farasi wake.

Wale doria walipigana kishujaa lakini wote pamoja na Abdullah ibn Jubayr, walizidiwa nguvu, na wakauawa. Mara moja Khalid akakiteka kinjia kile, akalishambulia lile jeshi la Madina kwa kutokea nyuma.

Lile jeshi la Madina lilikuwa linashughulika kukusanya ngawira, bila kuelewa kabisa kitu kingine chochote kile. Ghafla, lilishitukizwa na shambulio la lile jeshi la farasi la Makka nyuma yao. Abu Sufyan pia aliigundua hila ya Khalid, na ule mkanganyiko wa Waislamu. Alikusanya upya vikosi vyake, akarudi kwenye uwanja wa mapambano na kuanzisha mashambulizi ya mbele juu yao.

Sasa wakajikuta wameshikwa katika mashambulizi ya mbele na nyuma ya maadui, na wakahofu. Ilikuwa sasa ni zamu yao kushindwa. Walianza kukimbia lakini bila kujua ni upande gani wa kukimbilia, na kila mmoja alikimbia na njia yake.

Mshangao haukuishia kwa askari wa kawaida wa jeshi la Waislamu tu; ulikuwa ni wa jumla. Baadhi ya maswahaba wakuu wa Mtume (s.a.w.) walikumbwa pamoja na wengine kabla ya shambulizi la adui.

Miongoni mwa waliokimbia walikuwa wote Abu Bakr na Umar. Inasimuliwa na Anas bin Nadhr, ami yake Anas bin Malik, kwamba Abu Bakr alisema katika nyakati za baadae kwamba pale Waislamu walipokimbia kutoka kwenye vita vya Uhud, na wakamuacha Mtume wa Allah (s.a.w.) yeye alikuwa wa kwanza kurudi kwake.

Umar mara nyingi alisema kwamba wakati Waislamu waliposhindwa huko Uhud, alikimbia na kupanda kwenye kilima (Tarikh Tabari, juz. IV, uk. 96). Baadhi ya maswahaba waliweza kufika Madina na wengine walitafuta hifadhi kwenye mapango na makorongo ya mlima.

Uthman bin Affan, khalifa wa tatu wa Waislamu baadae, hakushiriki katika vita vya Badr lakini alikuwepo Uhud. Hata hivyo, aliiona milio ya migongano ya panga na mikuki imezidi kiasi kidogo katika ujasiri wake, na alikuwa miongoni mwa wakimbizi wa mwanzo. Sheikh Muhammad Khidhri Buck anasema katika kitabu chake cha wasifu wa Mtume (s.a.w.) kwamba Uthman alikuwa mtu mwenye aibu sana, na kwamba ingawa alikimbia kutoka kwenye uwanja wa vita, hakuingia Madina. Kuwa na aibu kwake kulimzuia kufanya hivyo.

Pale Waislamu walipokuwa wanakimbia kupita alipokuwapo Mtume, alijaribu kuwazuia lakini hakuna hata mmoja aliyejaribu kumsikiliza. Katika muda mfupi mambo yaliwageukia, na ushindi ukakwapuliwa kutoka mikononi mwao. Ilikuwa ni gharama iliyokuwa wailipe kutokana na kukosa utii kwa Mtume wao, na kwa shauku ya wasiwasi juu ya kukusanya ngawira.

Ufuatao ni ushuhuda wa Qur’an Tukufu juu ya mwenendo wa Waislamu katika vita vya Uhud

إِذْ تُصْعِدُونَ وَلَا تَلْوُونَ عَلَىٰ أَحَدٍ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ فِي أُخْرَاكُمْ فَأَثَابَكُمْ غَمًّا بِغَمٍّ لِكَيْلَا تَحْزَنُوا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا مَا أَصَابَكُمْ ۗ وَاللَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {153}

“Tazama! Mlikuwa mnapanda juu ya mlima, Bila ya kutupa jicho la pembeni kumuangalia yeyote yule, Na Mtume akiwa nyuma yenu anawaiteni mrudi. Hapo Allah akawapeni dhiki baada ya dhiki kwa njia ya kukulipisheni, kuwafundisha msisikitikie ngawira iliyowakoseni, na kwa (madhara) yaliyokufikeni. Kwani Allah ni Mwenye kujua yote mnayoyafanya.” (Sura ya 3: Aya ya 153)

Mtume (s.a.w.) alikuwa amempa bendera ya Uislamu ami yake, Masaab ibn Umayr, katika vita vya Uhud. Aliuawa na adui, na ile bendera ya Uislamu ikaanguka chini. Wakati Ali alipoona ile bendera inaanguka chini, alikurupuka mbele, akaisimamisha, na akainyanyua juu mara nyingine tena.

Washington Irving:

“Hamza alichomwa na mkuki wa Wahshi, yule mtumwa wa Kihabeshi, aliyekuwa ameahidiwa uhuru wake kama angemuua Hamza. Musaab ibn Umayr, pia, aliyekuwa amebeba bendera ya Muhammad, aliangushwa chini, lakini Ali aliikamata ile bendera tukufu, na akainyanyua juu sana katikati ya wimbi la vita.

Kwa vile Musaab alifanana sana na Mtume (s.a.w.) mwenyewe, ukelele ulitolewa na adui kwamba Muhammad ameuawa. Maquraishi walitiwa moyo na hamasa maradufu kwa kusikia sauti hiyo; Waislamu wakakimbia kwa kukata tamaa, wakiwa wame-wabeba pamoja nao Abu Bakr na Umar, ambao walikuwa wamejeruhiwa.” (The Life of Muhammad)

Muhammad Husein Haykal:

“Wale waliodhania kwamba Muhammad alikuwa amekufa, ikiwa ni pamoja na Abu Bakr na Umar, walikwenda kuelekea mlimani na wakakaa chini.

Wakati Anas ibn al-Nadr alipouliza ni kwa nini wanakata tamaa mapema hivyo, na akaambiwa kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa ameuawa, akajibu kwa ukali: “Na mtajifanyia nini nyie wenyewe na maisha yenu baada ya Muhammad kufa? Simameni, na mfe kama alivyokufa yeye.”

Akageuka, akashambulia dhidi ya adui, na alipigana kwa ushujaa sana (mpaka akauawa).”
(The Life of Muhammad, 1935, Cairo)

Waislamu wengi walikuwa wamekimbia kutoka kwenye uwanja wa vita lakini Ali alikuwa bado anapigana. Alikuwa amebeba bendera ya Uislamu kwenye mkono mmoja, na upanga katika ule mwingine. Yeye pia aliusikia ule ukelele “Muhammad amekufa.” Lakini ulimfanya kutojali sana juu ya maisha yake mwenyewe.

Mtume, hata hivyo, alikuwa kwenye sehemu nyingine ya uwanja wa mapambano. Alikuwa amejeruhiwa, na kichwa chake na uso ulikuwa unatoka damu.

Waislamu wachache, zaidi hasa Ansari, walikuwa wakimlinda. Lilikuwa ni kundi hili dogo, na kelele zao za kivita ndivyo vilivyovuta nadhari ya Ali. Alipasua njia yake katikati ya mistari ya adui na akawafikia wapiganaji wenzie. Walikuwa wamesimama kumzunguka Mtume, na wakiongozwa na Abu Dujana, walikuwa wakifanya kila walichoweza kumkinga Muhammad kutokana na silaha za makombora za adui.

Ali alisisimka kumwona bwana wake akiwa hai bado lakini hakuwa na muda wa kuswalimiana. Wale waabudu-sanamu walikuwa wamean- za upya mashambulizi yao, na sasa ilikuwa ni Ali ambaye alipaswa kuwapiga kuwarudisha nyuma. Walishambulia kwa marudio lakini aliwakwamisha kila mara.

Muhammad Husein Haykal:

“…wakati mtu mmoja alipokemea kwamba Muhammad ameuawa, vurugu zilichukua madaraka kamili, hamasa ya Waislamu ilishuka chini na wapiganaji wa Kiislamu walipigana kwa mtawanyiko na bila ya lengo. Vurugu hizi zilihusika na kumuua kwao Husayl ibn Jabir Abu Hudhayfah kwa makosa, kwani kila mtu alitafuta kuokoa maisha yake mwenyewe kwa kukimbia isipokuwa watu kama Ali ibn Abi Talib ambaye Allah (s.w.t.) alimuongoza na kumlinda.” (The Life of Muhammad, 1935, Cairo)

Katika vita vya Uhud, wengi wa maswahaba waliotangazwa kuwa majasiri sana na waaminifu, waliwageuzia migongo maadui, na wakakimbilia kujificha. Lakini walikuwepo wachache ambao hawakukimbia. Mmoja wao alikuwa ni Ummu Ammarra Ansariyya, bibi kutoka Madina.

Alikuwa muumini asiyekuwa na hofu, na Waislamu wote wanaweza kwa haki kabisa kujivunia ujasiri wake. Alitambulikana kwa ujuzi wake kama daktari na muuguzi, na alikuja Uhud pamoja na jeshi la Madina.

Mwanzoni mwa vita hivyo, Ummu Ammarra Ansariya alileta maji kwa ajili ya wapiganaji hao au aliwahudumia kama walikuwa wamejeruhiwa. Lakini Waislamu waliposhindwa na wakakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita, wajibu wake ulibadilika kutoka ule wa muuguzi kuwa wa mpiganaji.
Wakati mmoja maadui walileta watupa mishale ili kumrushia mishale Mtume. Ummu Ammarra alichukua ngao kubwa na akaishikilia mbele yake kumlinda kutokana na yale makombora yanayoruka.

Muda mfupi baadae, watu wa Makka wakashambulia kwa panga na mikuki ambapo Ummu Ammarra alitupa ile ngao, na akawashambulia kwa upanga. Muabudu-sanamu mmoja akaja kwa hatari karibu sana na Mtume (s.a.w.) lakini Ummu Ammarra akaja mbele yake, na wakati yule muabudu-sanamu alipotupa dhoruba, pigo hilo liliangukia begani mwake. Ingawa Ummu Ammarra alikuwa amejeruhiwa, hakuingiwa na hofu, na kwa dhamiri kabisa akasimama kati ya Mtume (s.a.w.) na maadui zake, akiwadharau wao na kutoogopa kifo.

Wakati huo kulikuwa na utulivu wa muda katika mapigano. Kwa kuchukua fursa hiyo, Ali alimtoa Mtume (s.a.w.) kutoka kwenye ile sehemu ya hatari mpaka kwenye pango ambako angeweza kupata mapumziko kidogo, na ambako majeraha yake yangeweza kufungwa.

D.S.Margoliouth:

“Yule shujaa Ali pamoja na (baadhi) watu wengine majasiri walipomuona (Mtume) walimbanisha faraghani kwenye pango ambako angeweza kuuguzwa.” (Muhammad and the Rise of Islam)

Fatmah Zahra, binti ya Mtume, alikuja kutoka mjini pamoja na kikundi cha wanawake wa Kiislam aliposikia habari za kushindwa kwa Waislamu. Ali alileta maji katika mbonyeo wa ngao yake, na Fatmah Zahra akaiosha damu kutoka kwenye uso wa baba yake, na akamfunga majeraha yake.

Wajibu wa wale Wanawake wa Makka

Kufukuzwa kwa Waislamu kutoka kwenye uwanja wa vita kulikuwa ni mwaliko kwa wale wanawake kutoka Makka kutafuta na kupata kutosheleza hamu yao ya kuua juu ya miili ya wale mashahidi. Walikata pua zao, masikio, mikono na miguu, na waliwapasua matumbo yao, wakatoa viungo, na wakavifanya mikufu kama mashada ya ushindi wa vita.

Muhammad ibn Ishaq:

“Saleh bin Kaysan aliniambia kwamba Hind, binti ya Utba, na wale wanawake aliokuwa nao, waliwakatakata maswahaba wa Mtume (s.a.w.) waliokufa. Waliwakata masikio yao na puazao na Hind akatengeneza kutokana navyo bangili za miguuni na skafu na akatoa bangili (zake mwenyewe) na skafu na vidani kwa Wahshi, yule mtumwa wa Jubayr bin Mutim. Alikata ini la Hamza na akalitafuna, lakini hakuweza kulimeza na akalitupilia mbali.

Al-Hubab bin Zabban, kaka yake B. Harith bin Abdu Manat, ambaye wakati huo alikuwa ndiye mkuu wa vile vikosi vya watu weusi, alipita karibu na Abu Sufyan alipokuwa anaichoma pembe ya mdomo wa Hamza kwa ncha ya mkuki wake, akisema: “Onja hiyo, wewe muasi.” Hulays aliguta kwa mshangao, “Oh! Banu Kinana, hivi huyu ndiye mkuu wa Maquraishi anayefanya hivyo kwa binamu yake aliyekufa kama mnavyoona?” (The Life of the Messenger of God)

Waislamu Sabini na tano waliuawa kwenye vita vya Uhud, na miili ya wengi wao ilikatwakatwa na Hinda na wale wanawake makatili wengine kutoka Makka.

Chuki juu ya Muhammad, Ali na Hamza ilikuwa ni moto ambao ulimmeza Hinda. Ingawa Hamza peke yake alikuwa ndio muathirika wa uchu wa ula-binadamu wa Hinda katika vita vya Uhud, Muhammad na Ali hawangetegemea kutendewa kwa tofauti yoyote kutoka kwake kama wangeangukia mikononi mwake. Aliirithisha chuki yake juu ya Muhammad na Ali kwa wanae na wajukuu zake, na vizazi vitakavyofuatia.

Kuondoka kwa Jeshi la Makka.

Baada ya mshituko wa kwanza wa kushindwa ulipopita, baadhi ya Waislamu walirudi kwenye uwanja wa mapambano. Abu Bakr na Umar walikuwa miongoni mwao. Wao pia waliingia kule kwenye pango ambako Ali alimpeleka Mtume. Kwa wakati huu, Abu Sufyan ambaye alikuwa tayari kurudi Makka, anaelezwa kuwa alikuja karibu na lile pango. Akiwa amesimama chini ya vile vilima, alibishana kidogo na Umar.

Sir John Glubb:

“…Maquraishi wangeweza kuupanda Mlima Uhud kwa gharama ya majeruhi wachache na kuweza kumuua Mtume wa Allah (s.a.w.) na kile kikundi kidogo cha wafuasi waliojitoa ambao walibakia pamoja naye.

Pale Abu Sufyan alipomuuliza Umar ibn al-Khatab kama Muhammad alikuwa amekufa, alimjibu, “Hapana, Wallahi, anakusikia unavyoongea.” Lakini haikumjia Abu Sufyan kuchukua fursa hiyo ya uvunjaji hatari wa usalama.

Ukatili wa kinyama wa mauaji haya (katika vita vya Uhud) unafafanua kwa mara nyingine tena ile tofauti ya kipekee kati ya mapigano rahisi na mara nyingi ushujaa ya Waarabu na unyama wa uadui baina ya koo mbili. Abu Sufyan anazungumza kwa maelewano na Umar ibn al-Khatab kwenye uwanja wa vita wa Uhud, kwani hakuna kati yao aliyeua ndugu wa mwenzie. Lakini mke wa Abu Sufyan, Hinda, binti ya Utba ibn Rabia, anaikatakata maiti ya Hamza, aliyemuua baba yake. (The Life and Times of Muhammad)

Maquraishi walidhania wamemaliza kazi yao. Walikuwa wamewashinda Waislamu na wameokoa heshima yao. Hivyo wenyewe wakiwa wameridhika, waliondoka kwenye uwanja wa vita na wakaelekea kwenye mji wao wa nyumbani upande wa Kusini. Lakini Mtume, akiwa bado hana uhakika na nia zao, alimtuma Ali kwenda kuwaangalia kwa mbali na kumpa taarifa za mienendo yao.

Ali alirudi na kukmfahamisha Mtume (s.a.w.) kwamba Maquraishi wameshaipita Madina, na walikuwa wakienda kuelekea Makka. Hii ilimhakikishia Mtume. Waislamu ndipo wakashuka kutoka mlimani, wakawaswalia maiti wao, na wakawazika.

Ali Na Vita Vya Uhud

Katika vita vya Uhud, Ali alimuua mshika-bendera wa kwanza wa jeshi la wapagani. Wakati mshika-bendera huyo alipoanguka chini, na bendera pia ilianguka chini pamoja naye. Ali kwa hiyo aliiangusha nembo ya upagani.

Baadae, vita vilipokuwa vinachachamaa, wapagani walimuua Musaab ibn Umayr, mshika-bendera wa jeshi la Waislamu. Musaab alianguka chini, na bendera pia ikaanguka pamoja naye. Lakini muda uliofuata tu, Ali akatokea; aliinyanyua ile bendera iliyoanguka kutoka ardhini, na akaikunjua kwa mara nyingine. Alikuwa kwa hiyo sawasawa kama ishara ya kuangamia kwa uabudu-sanamu na ushirikina kama alivyokuwa ishara ya kunyanyuka na kuzaliwa-upya kwa Uislamu. Hapo Uhud, rafiki na adui wote waliona kwa macho yao yale matendo ya ajabu ya ushujaa na ujasiri wa Ali, na kujitolea kwake kwa bwana wake, Muhammad, Mtume wa Allah (saw) Ali alipigana vile vita vya Uhud kwa ule upanga mashuhuri, Dhu’l-Fiqar.

Muhammad Ibn Ishaq:

“Upanga wa Mtume (s.a.w.) ulikuwa unaitwa Dhu’l-Fiqar. Muhadithin mmoja alinieleza kwamba Abu Najih alisema, ‘Mtu mmoja aliguta katika vita vya Uhud:

‘Hakuna upanga ila Dhu’l-Fiqar
Na hakuna shujaa kama Ali.”

(The Life of the Messenger of God)

Katika mikono ya Ali, Dhu’l-Fiqar ulikuwa ni radi iliyoshambulia na kuumaliza upagani, uabudu masanamu na ushirikina. Lakini kwa Uislamu, ulikuwa ndio mletaji wa matumai- ni, nguvu mpya, maisha mapya, na heshima, utukufu na ushindi.

Akielezea juu ya matukio ya Uhud, kufuatia kutimuliwa kwa Waislamu wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwa ameshambuliwa na maadui zake, M. Shibli, yule mwanahistoria wa Kihindi, anasema: Ilikuwa ni wakati mbaya sana katika historia ya Uislamu. Waabudu-masanamu walimshambulia Mtume wa Allah (s.a.w.) kama miungu ya ghadhabu ya hadithini lakini kila mara walizuiwa kwa ncha ya Dhu’l-Fiqar.
Shibli anaendelea kusema kwamba hao waabudu-masanamu walikuja kama “mawingu meusi na ya kutisha, tayari kuwapasukia Waislamu.”

Kama Ali asingeyapunguza nguvu mashambulizi ya watu wa Makka, basi kupasuka kwa wingu huku kungeikumba Madina, na Uislamu ungesombwa katika mafuriko ya uabudu-masanamu. Kama Ali pia angeshindwa katika wajibu wake kama wengine wengi walivyoshindwa, waabudu-masanamu hawa wangemuua Mtume wa Allah (s.a.w.) na wangeuzima mwanga wa Uislamu. Lakini Ali na

Waislamu wengine wachache, wakiwa ni pamoja na Abu Dujana na Ummu Ammarra Ansariyya, walilizuia balaa hili. Katika vita hivi vya kuhuzunisha, Waislamu 75 waliuawa. Kati yao wanne walikuwa ni Muhajir, na waliobakia walikuwa ni Ansari.

Mashahidi Wa Uhud

Tukio la kusikitisha sana kati ya matukio ya vita vya Uhud lilikuwa ni kifo cha Hamza na kuharibiwa kwa mwili wake. Baada ya kuondoka kwa watu wa Makka, Mtume (s.a.w.) alikwenda kuona maiti ya ami yake.

Masikio na pua vilikuwa vimekatwa; tumbo limepasuliwa, na viungo vyake vilikuwa vimeondolewa. Alijawa na huzuni kwa kuuona mwili ule wa shahidi katika hali ile, na akaamuru ufunikwe.

Hinda, mke wa Abu Sufyan, na mama yake Mu’awiyyah, anaitwa “mlaini” katika historia ya Uislamu. Ibn Ishaq anasema kwamba alilitafuna ini la Hamza lakini hakuweza kulimeza. Lakini Ibn Abdul Birr anasema katika kitabu chake, Al-Isti’aab, kwamba kwa kweli alitengeneza moto katika uwanja wa vita hivyo, akalichoma ini la Hamza kwenye moto huo, na akalila!

Wakati Mtume (s.a.w.) aliporudi Madina, alivisikia vilio vya huzuni vya watu wa zile familia zilizoondokewa. Ndugu na jamaa wa mashahidi wa Uhud walikuwa wanawaomboleza watu wao waliokufa.

Alimaka kwa mshangao: “Wapi! Hakuna hata mtu wa kuomboleza kifo cha ami yangu, Hamza.” Viongozi wa Ansari kusikia kauli hii, wakaenda majumbani kwao, na wakawaamuru wanawake zao kwenda kwenye nyumba ya Mtume, na kuomboleza kifo cha ami yake.

Wakati huo kundi la wanawake wa Madina likakusanyika katika nyumba ya Muhammad, na wote walikililia kifo cha huzuni cha Hamza, shujaa wa Uislamu.Mtume (s.a.w.) akaomba baraka za Allah (s.w.t.) juu yao wote. Baada ya hapo ikawa ni desturi hapo Madina kwamba wakati wowote mtu yoyote akifa, waombolezaji wake walianza vilio vyao kwa nyimbo za maombolezo ya Hamza.

Watu wa Madina walianza kwanza kumuombeleza Hamza kisha wakawaombolezea watu wao wenyewe waliokufa.

Muhammad Ibn Ishaq:

“Mtume (s.a.w.) alipita kwenye makazi ya Banu Abdul Ashal na Zafar na akawasikia wakilia kwa ajili ya wafu wao. Macho yake yalijawa na machozi na akasema: “Lakini hakuna wanawake wanaolia kwa ajili ya Hamza.” Wakati Sa’d bin Mu’adh na Usayd bin Hudayr waliporudi majumbani kwao, waliwaamuru wanawake zao kujitayarisha na kwenda kulia kwa ajili ya ami yake Mtume (s.a.w).
(The Life of the Messenger of God)

Mbali na Hamza, Muhajirina wengine watatu walipata taji la kufa kishahidi katika vita vya Uhud. Walikuwa ni Abdullah ibn Jahash, binamu yake Mtume; Masaab ibn Umayr, ami yake Mtume; na Shams ibn Uthman.

Hasara kwa Ma-Ansari ilikuwa kubwa sana. Waliacha maiti sabini na moja hapo uwanjani, na wengine wengi waliojeruhiwa. Allah (s.w.t.) awape rehema hao wote.

Vita vya Uhud vilikuwa ni wakati wa majira ya upinzani wa kipagani kwa Uislamu. Ingawa walikuwa washindi kwenye vita, Maquraishi hawakuweza kufuatilia na kufaidi ushindi wao, na mafanikio yao yalibadhirika mara tu.