read

Waislamu Na Wayahudi

Mnamo mwaka wa 70 A.D. Yule jenerali wa Kirumi, Titus, aliiteka Jerusalem na akakomesha utawala wa Kiyahudi wa Palestina. Kufuatia utekaji nyara wa Warumi, Wayahudi wengi waliondoka kwenye nchi yao na wakatangatanga kwenye nchi nyingine.

Baadhi ya makabila ya Kiyahudi yalivuka jangwa la Syria na kuingia kwenye peninsula ya Arabia ambako waliweka makazi yao huko Hijazi. Baada ya kupita muda walijenga makoloni mengi huko Madina na kati ya Madina na Syria. Wanasemekana pia kwamba waliwabadili Waarabu wengi na kuwaingiza kwenye Ujuda (dini ya Wayahudi).

Mwanzoni mwa karne ya saba A.D., kulikuwa na makabila matatu ya Kiyahudi yaliyokuwa yanaishi Madina (Yathrib). Haya yalikuwa ni Banu Qainuka’a, Banu Nadhir na Banu Qurayza. Makabila yote matatu yalikuwa matajiri na yenye nguvu, na pia, yalikuwa yamestaarabika zaidi kuliko hao Waarabu.

Wakati ambapo Waarabu walikuwa wote ni wakulima, hawa Wayahudi walikuwa wawekezaji mali wa viwanda, biashara na uchuuzi katika Arabia, na walisimamia maisha ya kiuchumi ya Madina (Yathrib). Yale makabila mawili ya Kiarabu – Aus na Khazraj – walikuwa wamejawa na madeni kwa Wayahudi daima.

Mbali na Madina, vituo vizito vya Wayahudi katika Hijazi vilikuwa Khaibar, Fadak na Wadi-ul-Qura. Ardhi katika mabonde haya ilikuwa ndio yenye rutuba zaidi katika Arabia yote, na wakulima wake wa Kiyahudi walikuwa ndio wakulima wazuri zaidi katika nchi hiyo.

Kule kuhama kwa Muhammad, Mtume wa Uislamu, kutoka Makka kwenda Madina (wakati huo Yathrib) kulimkutanisha na Wayahudi kwa mara ya kwanza. Hapo mwanzoni walikuwa na urafiki naye.

Aliwapa ule mkataba maarufu wa Madina, na wakamtambua yeye kama mtawala wa mji wao, na wakakubali kufuata uamuzi wake katika migogoro yote. Walikubali pia kuulinda mji huo katika kitendo cha kuvamiwa na adui.

Lakini, kwa bahati mbaya, urafiki huu haukudumu kwa muda mrefu. Mara moja ikaonekana wazi kwamba hao Wayahudi walitoa urafiki wao kwa Muhammad kwa mashaka mengi.

Kwa maslahi yao binafsi, walipaswa kutekeleza wajibu wao wa makubaliano kwa uaminifu lakini hawakufanya hivyo.Kwa mabadiliko haya katika tabia zao, kulikuwa na sababu nyingi, miongoni mwao zikiwa:

1. Wakati Muhammad alipowasili Madina, alirekebisha maisha ya Waarabu au yeyote yule aliyeingia Uislamu. Aliwafundisha wao kuwa na msimamo wa kadiri na wastani katika kila jambo na akawafundisha thamani ya nidhamu katika maisha. Waliacha kunywa pombe na kucheza na kamari vyote ambavyo vilikuwa ndio vyanzo vya kuharibikiwa kwao huko nyuma; na waliacha kuchukua mikopo kwa viwango vya juu vya riba kutoka kwa Wayahudi. Pale Waarabu walipoacha kuchukua mikopo na kuitolea riba juu yake, chanzo kikubwa cha mapato kwa Wayahudi ghafla kikakauka, na walilikasirikia sana hili. Waliweza kuona sasa kwamba nguvu yao katika maisha ya kiuchumi ya Madina ilikuwa inaanza kulegea.

2. Wayahudi pia walitambua kwamba Uislamu ulikuwa ni adui wa mfumo wao wa unyonyaji, na mfumo wa kibepari. Walianza kuuona Uislamu kama ni tishio kwa maslahi yao ya kiuchumi.

3. Makuhani wa Kiyahudi walimchukia Muhammad kama vile walivyomchukia wakopesha fedha. Alikuwa amewaonyesha Wayahudi jinsi makuhani wao walivyofuata tafsiri potovu ya maandiko yao, na jinsi walivyochafua vitabu vyao. Makuhani hao, kwa upande wao, walijaribu kuwashawishi waumini wao kwamba Muhammad hakuwa na elimu ya maandiko yao, na walijaribu kuwaonyesha wao “makosa” katika Qur’an

Wayahudi hao pia waliamini kuwa walikuwa salama tu mradi yale makabila mawili ya Madina, Aus na Khazraj, yalikuwa yanapigana yenyewe kwa yenyewe.

Amani kati ya Aus na Khazraj, walidhania, italeta tishio kwa maisha yao katika Arabia. Kwa sababu hii, walikuwa daima wakichochea ugomvi kati yao.

Kati ya makabila matatu ya Kiyahudi ya Madina, hawa Banu Qainuka na Banu Nadhir yalikuwa tayari yamefukuzwa baada ya vita vya Badr na Uhud kwa mfuatano wake, na walikuwa wameondoka na mizigo yao, na makundi ya wanyama, na wamefanya makazi huko Khaibar.

Hili kabila la tatu na la mwisho la Wayahudi wa Madina lilikuwa la Banu Qurayza.

Kwa mujibu wa masharti ya ule Mkataba wa Madina, ilikuwa ni wajibu wao kuchukua sehemu muhimu katika kuulinda mji huo wakati wa kule kuzingirwa kwa mwaka 627 A.D. Lakini sio tu hawakutoa mtu yeyote au vifaa wakati wa mzingiro bali walikamatwa wakila njama na maadui kuwekea mzingo maangamizi ya Waislamu. Baadhi ya Wayahudi pia walishambulia nyumba moja ambayo ndani yake wanawake wengi wa Kiislam na watoto walichukua hifadhi kama ilivyodhaniwa kuwa ni sehemu yenye usalama kwao kuliko kwenye nyumba zao wenyewe. Kama Amr ibn Abd Wudd angeushinda upinzani wa Waislamu, hawa Wayahudi wangewashambulia kwa nyuma. Katikati ya wapagani wa Makka na Wayahudi wa Madina, Waislamu wangeuawa kwa halaiki. Ilikuwa ni kuwepo kwa akili ya Muhammad na kujasiri kwa Ali ambako kulizuia maafa kama haya..

R.V.C.Bodley

Wale Wayahudi mwanzoni hawakuelekea kulisikiliza pendekezo la Abu Sufyan (la kuwashambulia Waislamu kutokea nyuma), lakini baada ya muda walielewana na wakakubali kuwasaliti Waislamu pale muda utakapoelekea kuwa muafaka. (The Messenger – the Life of Muhammad)

Tabia ya Wayahudi wakati ule wa mzingiro wa Madina ilikuwa ni uhaini mkubwa dhidi ya Nchi. Kwa hiyo, wakati lile jeshi la muungano lilipovunjika na ile hatari ya Madina ikawa imezuiwa, Waislamu wakaguezia macho yao kwao.

Wale Wayahudi wakajifungia kwenya ngome zao na Waislamu wakawazingira. Lakini siku kadhaa baadae, walimuomba Mtume (s.a.w.) kuondoa mzingiro ule, na wakakubali kupeleka mgogoro huo kwenye usuluhishi.

Mtume (s.a.w.) aliwaruhusu wale Wayahudi kuchagua msuluhishi wao wenyewe. Hapa walifanya kosa lililowagharimu sana. Wangemchagua Muhammad mwenyewe – aliye mfano halisi wa msamaha – awe hakimu wao. Kama wangefanya hivyo, angeweza kuwaruhusu waondoke Madina na mizigo na wanyama wao, na kadhia hiyo ingefikia mwisho.
Lakini Wayahudi wale hawakumchagua Muhammad kama hakimu wao. Badala yake, walimchagua Sa’ad ibn Muadh, kiongozi wa washirika wao wa awali, wale Aus. Sa’ad alikuwa ni mtu asiyejali kabisa maisha yake mwenyewe na ya wengine vilevile.

Sa’ad alipata jeraha baya sana wakati wa vita vya Handaki, na kwa kweli alikufa baada ya kutoa hukumu juu ya majaaliwa ya wale Wayahudi. Aliutaja uhaini kwamba ni kosa lisilosameheka, na hukumu yake ilikuwa kali. Aliitekeleza Taurati, lile andiko la Wayahudi, na akawahukumu wanaume wote kifo, na wanawake na watoto kuwa watumwa. Hukumu yake ilitekelezwa papo hapo.

Wale Wayahudi wa kabila la Qurayza waliuawa kwenye majira ya kuchipua ya mwaka wa 627 A.D. Kutoka tarehe hii, Wayahudi wakakoma kuwa nguvu hai katika maisha ya kiuchumi na kisiasa ya Madina.

Mkataba Wa Hudaybiyya

Kwa mujibu wa Hadith za Kiislam, ile Al-Kaaba ya Makka ilijengwa na Mitume Ibrahim na mwanae, Ismail. Waliitoa Waqfu kama kituo cha kiroho cha dunia ya waabudu Mungu mmoja. Na sasa Al-Kaaba ilikuwa ndio “Qibla” cha Waislamu ambacho ina maana kwamba walikuwa wageukie kukielekea wakati wanaposali Swala zao. Lakini walezi wa hiyo Al-Kaaba walikuwa ni wale waabudu masanamu wa Makka, na walikuwa wakiitumia kama hekalu la kitaifa la ushirikina, wakiweka ndani yake masanamu 360 ya makabila yao.

Kwa desturi za kijadi za Kiarabu, kila mmoja alikuwa huru kuitembelea hiyo Al-Kaaba – bila ya silaha. Pia, kwa desturi za jadi, mapigano ya aina yoyote yalikatazwa wakati wa miezi minne mitukufu ya mwaka. Moja ya miezi hii ulikuwa ni Dhilqa’ada, mwezi wa 11 wa kalenda ya Kiislamu.

Waislamu walitamani kuona ilikuwa ni nini kwao, ile Nyumba ya Allah (s.w.t.) Kwa hiyo, katika Dhilqa’ada ya mwaka wa sita wa Hijiria, Mtume wao alitaarifu kwamba atatembelea Makka kufanya Umra au Hija Ndogo – bila ya kuwa na silaha lakini akiwa na wafuasi wake. Kwa dhamira hii, aliondoka Madina mwishoni mwa Februari 628 A.D., pamoja na idadi ya wafuasi wake 1,400. Walichukua ngamia na wanyama wengine kwa ajili ya kafara lakini hawakuwa na silaha yoyote isipokuwa panga zao.

Wakati msafara huu wa mahujaji ulipofika kwenye viunga vya Makka, Mtume (s.a.w.) alijulishwa kwamba wale waabudu-sanamu hawatamruhusu yeye kuuingia mji huo, na kwamba, watatumia nguvu kumzuia asifanye hivyo. Taarifa hii ilisababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa Waislamu. Walisimama karibu na kisima mahali panapoitwa Hudaybiyya kaskazini ya Makka. Mtume (s.a.w.) alituma ujumbe kwa Maquraishi kwam- ba alitaka afanye tu ile mizunguko ya kidesturi saba, ya Al-Kaaba, kutoa kafara wanyama wao, na kisha warudi Madina na wafuasi wake. Maquraishi hawakukubali. Ujumbe mwingi tena ulitumwa lakini Maquraishi walisema kwamba hawatawaruhusu Waislamu kuingia Makka.

Hatimae, Mtume (s.a.w.) alimuamuru Umar ibn al-Khattab kwenda Makka kuwaelezea wale waabudu-masanamu madhumuni ya safari ile ya Waislamu, kuwahakikishia wao kwamba Waislamu hawakuwa na nia ya kupigana dhidi ya mtu yoyote yule, na kuwapa ahadi kwamba baada ya kufanya taratibu (ibada) za Umra wataondoka Makka mara moja na watarudi Madina.

Lakini Umar alikataa kwenda. Alisema hakuna mtu huko Makka wa kumlinda yeye. Alishauri, hata hivyo, kwamba Mtume (s.a.w.) angemtuma Uthman bin Affan na ujumbe wake kwenda Makka kwa vile wale waabudu masanamu hawatamfanyia madhara yoyote.

Sir William Muir

Mjumbe wa kwanza kutoka kambi ya Waislamu kwenda Makka, mtu aliyesilimu kutoka kabila la Bani Khuzaa, Maquraishi walimkamata na kumfanyia ukatili; wakamtia kilema ngamia wa Mtume (s.a.w.) ambaye alikuwa amempanda, na hata kumtishia maisha yake. Lakini hasira sasa zilikuwa zimetulia zaidi, na Muhammad alitaka Umar aende Makka kama balozi wake. Umar alijipa udhuru mwenyewe kwa sababu ya uadui binafsi wa Maquraishi juu yake; alikuwa, zaidi ya hayo, hana ndugu wenye uwezo hapo mjini ambao wangeweza kumkinga kutokana na hatari; na alielekeza kwa Uthman kama mjumbe anayefaa zaidi.
(The Life of Muhammad, 1877)

S. Margoliouth.

Wakati huu ilikusudiwa kutuma mwakilishi kwenda Makka, lakini ule utambuzi kwamba wengi wa Waislamu walikuwa na madoa ya damu ya Makka, uliwafanya wale mashujaa wa Uislamu wasiwe tayari kuhatarisha maisha yao kwenye safari hii fupi; hata Umar, ambaye kwa kawaida alikuwa tayari kabisa na upanga wake, alirudi nyuma.

Hatimae mkwewe Mtume, Uthman bin Affan, ambaye alichagua kumuuguza mkewe badala ya kupigana huko Badr, alitumwa kama mjumbe anayekubalika humo… (Muhammad and the Rise of Islam, 1931)

Ni ajabu kabisa kwamba Umar hakuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kutembelea Makka. Hapakuwa na hatari yoyote iliyohusika juu yake kwa sababu hakuwa mmojawapo wa wale Waislamu ambao “walitiwa doa na damu ya Makka.” Kwa vile Umar hakuua mtu yeyote wa Makka, atakuwa ni mtu anayekubalika kwa hawa waabudu masanamu kwa nyakati zote.

Kukataa kwake kutii amri ya Mtume wa Allah (s.a.w.) kwa hiyo, hakueleweki.

Umar hakwenda Makka. Hata hivyo, alilitatua tatizo hilo kwa kumtoa mshika nafasi yake, Uthman bin Affan. Badala yake, kwa hiyo, Uthman alitumwa Makka kufanya mazungum- zo na Maquraishi. Kama Umar mwenyewe, Uthman pia hakuwa na doa la damu ya pagani yeyote.

Waabudu masanamu hao walimkaribisha Uthman na wakamwambia yeye kwamba alikuwa huru kufanya hiyo Umra. Lakini alisema kwamba yeye peke yake hataweza kufanya Umra, na kwamba walikuwa wamruhusu Mtume (s.a.w.) na Waislamu wote waliokuwa pamoja naye, kuingia mjini humo. Hili halikukubaliwa na Maquraishi, na ilielezwa kwamba walimkamata yeye. Ilinong’onwa pia kwamba walimuua.

Wakati tetesi la kuuawa kwa Uthman zilipomfikia Mtume, alikitafsiri kitendo hicho cha Maquraishi kama makataa (kauli ya mwisho), na akawataka Waislamu kutoa upya kiapo chao cha utii kwake. Waislamu wote wakatoa kiapo chao cha utii kwa Mtume wa Allah (s.a.w.) bila kujali matukio yanayoweza kutokea baada ya hapo.

Kiapo hiki kinaitwa “Kiapo cha Ridhwan” au “Mkataba wa Uaminifu,” na wale Waislamu waliokitoa, wanaitwa “Masahaba wa chini ya mti,” kwa sababu Mtume (s.a.w.) alisimama chini ya mti walipokuwa wakipita kwa safu mbele yake wakitoa upya kiapo chao cha utii kwake. Idadi yao imetajwa kuwa 1,400.

Uamuzi huu wa Waislamu wa kujasiri matokeo unaonekana kuwaweka Maquraishi katika hali ya akili ya kutosha, kwa vile walivyotambua kwamba ukaidi wao unaweza kusababisha umwagaji damu usio wa lazima. Uthman, ilitokea kwamba, hakuwa ameuawa kama ilivyotetwa bali alikuwa amekamatwa tu, na sasa wakamuachilia – kitendo kinacho onyesha mabadiliko katika msimamo wao. Pia kuonyesha mabadiliko haya kulikuwa ni ule uchaguzi wao mtu mmoja, Suhayl bin Amr, ambaye walimtuma kwenye kambi ya Waislamu kukamilisha mkataba na Mtume wa Uislamu. Suhayl alikuwa ni mtu aliyeju- likana kama mpatanishi hodari lakini hakuwa madhubuti.

Suhayl aliwasili Hudaybiyya na kufungua majadiliano na Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) Baada ya mazungumzo marefu na mjadala wenye kuchosha walifanikiwa katika kufikia mkataba, ambao masharti yake muhimu sana yalikuwa kama yafuatayo:

1. Muhammad na wafuasi wake watarudi Madina bila ya kutekeleza Umra

1. (Hija Ndogo) ya mwaka ule.

2. Kutakuwa na amani kati ya Waislamu na Maquraishi kwa kipindi cha miaka kumi kutoka tarehe ya kusaini mkataba huo.

3. Kama mtu yeyote wa Makka ataukubali Uislamu na kutafuta hifadhi kwa Waislamu huko Madina, watamrejesha Makka. Lakini kama mwislamu, aliyekimbia kutoka Madina, akitafuta hifadhi kwa wapagani wa Makka, hawatamrejesha.

4. Makabila yote ya Arabia yatakuwa huru kuingia kwenye mahusiano ya mkataba na kundi lolote – Waislamu ama Maquraishi.

5. Waislamu watatembelea Makka kufanya hijja katika mwaka unaofuata lakini hawatakaa katika mji huo kwa zaidi ya siku tatu, na silaha pekee ambazo wataruhusiwa kuja nazo, zitakuwa ni panga zao ndani ya ala zao.

Mkataba huu unaitwa Mkataba wa Hudaybiyya. Ndio nyaraka ya kisiasa maarufu sana katika historia ya Uislamu. Katibu aliyechaguliwa kuandika masharti yake alikuwa ni Ali ibn Abi Talib.

Wakati Mkataba wa Hudaybiyya ulipokuwa unaandikwa, lilitokea tukio ambalo linatoa kiangaza kinachofichua juu ya tabia za baadhi ya waongozaji waliohusika katika kurasimu masharti yake.

Akitoa imla kwa Ali, Mtume (s.a.w.) alisema: “Andika, Kwa Jina la Allah Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.” Suhayl, yule mjumbe wa Makka, mara moja akatoa pingamizi, na akasema, “Usiandike hivyo. Badala yake, andika, ‘Kwa Jina Lako Ewe Allah’” Mtume (s.a.w.) akakubaliana na madai haya.

Mtume (s.a.w.) tena akamwambia Ali aandike: “Huu ni mkataba wa amani kati ya Muhammad, Mtume wa Allah na Maquraishi…..” Suhayl tena akapinga, na akasema: “Kama tumekukubali wewe kama mjumbe wa Allah kwa nini tuwe tunapigana dhidi yako? Kwa hiyo, usiandike hayo maneno, ‘Mtume wa Allah’ na andika jina lako mwenyewe tu na jina la baba yako.”

Mtume (s.a.w.) alikuwa ameridhia kukubaliana na dai hili pia lakini Ali alikuwa amek- wisha andika tayari maneno haya, “Muhammad ni Mtume wa Allah.” na alikataa kuyafu- ta. Alimwambia bwana wake: “Hiki cheo cha juu kimewekwa juu yako na Allah (s.w.t.) Mwenyewe, na sitayafuta kamwe haya maneno ‘Mtume wa Allah (s.a.w.) .’ kwa mkono wangu.” Kwa sababu hiyo, Mtume (s.a.w.) akaichukua ile kalamu mkononi mwake mwenyewe, na akayafuta yale maneno ambayo yalikuwa ni yenye kuchukiza kwa wale waabudu masanamu. Huu Mkataba wa Hudaybiyya ulisainiwa katika nakala mbili, moja kwa kila upande.

R.V.C.Bodley

Ile karatasi ya awali ya Mkataba wa Hudaybiyya ilibakia na Muhammad ambapo nakala yake ilikabidhiwa kwa Suhayl kwa uhifadhi wa salama katika hifadhi ya nyaraka ya Makka.
(The Messenger – the Life of Muhammad, 1946)

Huko Makka viongozi wa Maquraishi waliukaribisha ule Mkataba wa Hudaybiyya kama ushindi wa werevu wao. Walichukulia kwamba Muhammad ameshindwa ujanja na kwam- ba mkataba huo ulikuwa ni sawa na, hata kama sio tangazo rasmi la, “kusalimu amri.”

Maquraishi walifurahia sana juu ya kile walichofikiria ni kusalimu amri kwa adui lakini matukio yalikuwa mara tu yaonyeshe kwamba walikuwa wamekosea. Mbali kabisa na kuwa ni kusalimu amri, ule Mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa ni mmojawapo kati ya ushin- di mkubwa sana wa Uislamu.

Miongoni mwa wafuasi wa Mtume, hata hivyo, ule Mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa uzae hisia zenye mzozo mkali sana. Kwa namna ya kipekee. Kama vile walivyokuwa wale wapagani wa Makka, wale “wazalendo wapofu” katika kambi ya Waislamu pia waliulinganisha na “kusalimu amri.” Waliongozwa na Umar ibn al-Khattab. Aliyaona masharti yake ni “yenye kufedhehesha,” na alikuwa amesikitishwa sana nayo kiasi kwamba alimgeukia Abu Bakr kwa majibu ya maswali yake, na mahojiano yafuatayo yalifanyika kati yao:

Umar: Hivi yeye (Muhammad) ni Mtume au sio Mtume wa Allah?
Abu Bakr: Ndio. Yeye ni Mtume wa Allah.
Umar: Sisi ni Waislamu au sio Waislamu?
Abu Bakr: Ndio. Sisi ni Waislamu.
Umar: Kama sisi ni Waislamu, basi ni kwa nini tunasalimu amri kwa wapagani katika jambo linalohusu imani yetu?
Abu Bakr: Yeye ni Mtume wa Allah. na wewe usiingilie katika jambo hili.

Ufidhuli wa Umar ulishadidi kwa kiwango cha juu baada ya kuaswa na Abu Bakr, na akaenda kumuona Mtume (s.a.w.) mwenyewe.

Baadae alisema: “Nilikwenda mbele ya Mtume, na nikamuuliza: ‘Wewe sio Mtume wa Allah?’ akanijibu, ‘Ndio, mimi ndimi.’ Nikauliza tena: ‘Sisi Waislamu hatuko sahihi, na wale washirikina hawako kwenye makosa?’ Akajibu, ‘Ndio, hivyo ndivyo.’ Niliuliza zaidi: ‘Basi ni kwa nini tunaonyesha unyonge zaidi kwao? Hata hivyo sisi tunalo jeshi. Kwa nini tunafanya amani nao?’ Akasema: ‘Mimi ni Mtume wa Allah (s.w.t.) na ninafanya kile tu Anachoniamrisha kufanya.”

Lakini inaonekana Umar hakuridhika hata na majibu ya Mtume (s.a.w.) mwenyewe kwa maswali yake. Yale masharti ya Mkataba wa Hudaybiyya yamesababisha wasiwasi mkubwa katika akili yake, hivyo alisema: “Nilirudia rudia kumuuliza Mtume (s.a.w.) kuhusu yale masharti ya mkataba huu, na sijawahi kamwe kuongea naye kwa namna hii.”

Sir John Glubb

Wengi wa Waislamu walivunjwa moyo na matokeo ya Hudaybiyya, wakiwa walitara- jia uingiaji kwa ushindi ndani ya Makka. Umar ibn al-Khattab, kama kawaida, alitamka hasira zake, ‘Huyu siye Mtume wa Allah, na sisi sio Waislamu na wao sio washirikina?’ alitaka kujua kwa hasira kutoka kwa Abu Bakr mpole na mwaminifu.‘Kwa nini tusipigane nao; kwa nini tuafikiane hivyo?’(The Great Arab Conquests)

Tor Andre

Umar aligeukia kwa taharuki kwa Abu Bakr na viongozi wengine waliokuwa karibu na Mtume (s.a.w.) kuhakikisha kama kweli walidhamiria kuridhia fedheha hii (ingawa sio kweli). Alitamka baadae kwamba kamwe kabla ya hapo hajawahi kuwa na mashaka kuhusu ukweli wa Muhammad, na kama angepata angalau watu mia moja wenye mawazo kama hayo, angejiuzulu kwenye umma wa Kiislam.
(Muhammad – the Man and his Faith)

Maxime Rodinson

Umar na baadhi ya wengine walikasirikia lile wazo la kufanya maafikiano na hawa wapagani. Huyu khalifa wa baadae alikuja kumlaumu Mtume. Alitamka baadae kwamba kama angekuwa na watu mia moja upande wake, angejitoa. Lakini Muhammad alikuwa hatingishiki. (Muhammad, kilichotafsirwa na Anne Carter)

R.V.C.Bodley

Wengi wa wale mahujaji, na Umar hasa, waliaibika sana kwamba Muhammad amewakubalia Maquraishi katika karibu kila jambo. Ilionekana ni ajabu kwao kwamba, baada ya kuletwa umbali wote huu na kiongozi wao ambaye hakuwa na woga wa kumuandama adui ambaye alimshinda yeye, wasimamishwe nje ya lengo lao. Ilielekea kushangaza zaidi kwamba amejishusha mwenyewe mbele ya yule mjumbe wa Makka kwa kiasi cha ama kumwita Mola wake kwa jina Lake halali wala kutumia cheo chake mwenyewe, kwa sababu tu yule kafiri amedai hivyo. Umar alifikia kiasi cha kuuliza: “Wewe kweli ni Mtume wa Allah?” Umar alikwenda kuona ni nini Waislamu wengine walichohisi. Aliwakuta wao katika hali hiyo hiyo ya mawazo kama aliyokuwa nayo. Kwa mara ya kwanza tangu Uislamu uanze, kulikuwa na dalili za uasi.
(The Messenger–The Life of Muhammad)

Umar alitamka baadae kwamba tangu aliposilimu, hajawahi kuwa na mashaka kama hayo juu ya ukweli wa Muhammad kama aliyokuwa nayo ile siku Mkataba wa Hudaybiyya uliposainiwa.

Hii ina maana kwamba Umar alikuwa akisumbuliwa na mashaka ya mara kwa mara kuhusu ukweli wa Muhammad na ujumbe wake wa Utume. Yumkini alikuwa akiyazuia kila wakati yalipojitokeza. Lakini kwenye kigezo cha kuthibitisha uasili wake cha Mkataba wa Hudaybiyya, mashaka yake sugu yaliibuka kwa nguvu kali mno kiasi kwamba hakuweza kuyazima.

Akitawaliwa na mashaka yake, yeye kwa kweli alifikiria kuuacha udugu wa Kiislamu wenyewe lakini hakuweza kumpata mtu yoyote kwenye kambi hiyo ambaye angeweza kumsaidia kumuunga mkono katika “ujasiri” wake.
Mwelekeo wa mapokezi y a Sunni umekuwa kwamba katika kuonyesha ufedhuli na dharau kwa Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (rehma na amani juu yake na Ahlul-Bait wake), Umar alichochewa na mapenzi yake kwa Uislamu. Kwa mujibu wao, aliupenda sana Uislamu kiasi kwamba “alijisahau.” Mwanzoni, alikataa kutii amri ya Mtume (s.a.w.) ya kupeleka ujumbe kwa Maquraishi huko Makka. Kukataa kule, yumkini, kulichochewa na mapenzi hayo hayo.

Wale watu wanaohusisha unafiki wa Umar na mapenzi yake kwa Uislamu, kwa kweli, wanamaanisha kwamba yeye aliupenda Uislamu zaidi kuliko Muhammad, Mtume wa Uislamu mwenyewe alivyoupenda! Pia, kwa tabia yake, alikuwa anamaanisha kwamba Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa anakosea katika kutafuta amani na Maquraishi lakini yeye mwenyewe alikuwa sahihi, na kwamba ilikuwa ni wajibu wake “kumsahihisha” yeye Muhammad Mustafa.

Kama siku moja hivi kabla, Umar alitoa kiapo cha “kumtii Mtume wa Allah (s.a.w.)” kati- ka hali yoyote ile, kwenye amani na kwenye vita, kwenye neema na kwenye dhiki. Ilikuwa pengine ni kiapo hiki kilichomsukuma kujionyesha yeye binafsi kuwa ni “mfuasi” bora zaidi (wa Uislamu) kuliko “mfalme” mwenyewe (Mtume)! Kama ni sadfa kwamba wote, Maquraishi wa Makka, na Umar na wafuasi wake katika kambi ya Waislamu, walisoma, “kusalimu amri” kwa Waislamu, katika Mkataba ule wa Hudaybiyya, basi kweli ilikuwa ni ajabu.

Lakini kama vitisho vya kijeshi vya Umar vingeishia kwenye kuonyeshana nguvu na Maquraishi, basi mtu anaweza kukisia ni sehemu gani angeishughulikia ndani yake, akimpima kutokana na “kumbu kumbu ya matendo” yake mwenyewe, ya kabla na baada.

Akiandika juu ya huu Mkataba wa Hudaybiyya, Lt. Jenerali, Sir John Glubb anasema kati- ka kitabu chake, “The Life and Times of Muhammad”: Madukuduku yaliyovumiliwa na Waislamu pale Hudaybiyya yanadhihirishwa na namna ambavyo zile siku za wasiwasi zilivyobakia zimeganda kwenye kumbukumbu zao. Miaka mingi baadae, wakati majeshi ya Waislamu yalipokuwa tayari yamejenga himaya kubwa, wakati marafiki wakongwe wakizungumzia zile siku za mwanzoni, heshima kubwa kabisa ilionyeshwa daima kwa wale watu ambao walipigana kule Badr na kwa wale waliokula kiapo pale Hudaybiyya – ile migogoro miwili mizito ya mwanzo wa Uislamu. (The Life and Times of Mohammed)

Hapakuwa na yeyote miongoni mwa maswahaba wote wa Muhammad Mustafa ambaye alikuwa na mwenendo wa kiheshima, kote katika vita vya Badr na pale Hudaybiyya, na kwa kweli, katika nyakati zote za hatari katika historia ya Kiislamu, kama Ali ibn Abi Talib. Huko nyuma, alijitokeza mwenyewe kuwa wa kwanza katika vita; huko Hudaybiyya kila mmoja aliona kwamba alikuwa pia wa kwanza katika amani. Amedhihirisha mara nyingi katika vita kwamba alikuwa na imani kamili juu ya Muhammad na ujumbe wake, na sasa alikuwa anadhihirisha katika amani kwamba hakuna chochote ambacho kinaweza kamwe kutingisha imani yake juu ya bwana wake.

Baada ya kuondoka kwa wale wajumbe wa Makka, Mtume (s.a.w.) aliwaamuru Waislamu kunyoa vichwa vyao na kuchinja wanyama wao kama kafara, kama kanuni za Umra. Lakini alishtuka kuona kwamba wengi wao walikuwa katika hali ya uasi na hawakutaka kutii amri zake.

Kilichotokea hasa ni kwamba, Umar alimdharau hadharani Mtume wa Allah (s.a.w.) na kwa mfano wake huo, amewatia moyo wafuasi wake pia kufanya vivyo hivyo. Mtume (s.a.w.) aliingia kwenye hema lake, na akamwambia mkewe kwamba Waislamu walikuwa wanakaidi amri zake. Mkewe akasema kwamba kama angewapuuza hao, na akatekeleza kazi hiyo yeye binafsi, watamfuatisha yeye.

S. Margoliouth

Waislamu walinuna kimya wakati walipoambiwa na Muhammad wanyoe vichwa vyao na kutoa makafara yao. Mwishowe (kwa ushauri wa mkewe, Ummu Salamah), alitekeleza wajibu huo yeye binafsi, na wafuasi wake wakafanya vivyo hivyo. (Muhammad and the Rise of Uislamu)

Kazi yake ilipokamilika, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliondoka Hudaybiyya na wale mahujaji, ili kurudi Madina. Alikuwa bado katika safari ya siku saba kutoka Madina, wakati wahy ufuatao ulipokuja kutoka Mbinguni:

إِنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُبِينًا {1}

Hakika tumekupa ushindi wa dhahiri (Sura ya 48; Aya ya 1)

Ulikuwa ni ule Mkataba wa Hudaybiyya ambao huu wahy mpya umeuita “Ushindi wa dhahiri.” Amin Dawidar, yule mwanahistoria wa Kimisri, ameandika katika kitabu chake Pictures From the Life of the Prophet (Cairo, 1968 uk.465) kwamba wakati Mtume wa Allah (s.a.w.) alipotangaza rasmi huu wahy mpya unaoitwa “Ushindi,” Umar ibn al- Khattab alikuja kumuona, na akauliza: “Huu ndio unaouita Ushindi wa Dhahiri?” “Ndio,” akasema Mtume wa Allah (s.a.w.) “kwa Yule Ambaye mikononi Mwake yamo maisha yangu, huu ni Ushindi wa Dhahiri.” Mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa kweli ni “Ushindi wa Dhahiri” kama maendeleo ya mfululizo wa matukio ya historia yalivyokuwa yaonyeshe, licha ya ajizi juu yake ya Waislamu wengi katika kambi ya Mtume.

Muhammad Mustafa alikuwa ni Mtume wa amani. Kama angeruhusu mashinikizo ya wale “wazalendo wapofu” katika kambi yake kutumia mbinu za mabavu, ujumbe wake wote ungekuwa hatarini, na vizazi vya wakati ujao vingemshitaki rasmi kwa kupenda kwake “ugomvi.” Lakini alikataa mashinikizo ya kuvutiwa kwenye usuluhishi wa silaha, na badala yake, alivutiwa na usuluhishi wa amani, na akapata matokeo ambayo hakuna ushindi wa kijeshi ambao ungeweza kuyapata.

Mkataba ya Hudaybiyya ulikuwa ni matunda ya ustadi wa utawala wa majaaliwa na kipaji cha kisiasa cha hali ya juu sana. Ulileta manufaa makubwa sana kwa Uislamu. Miongoni mwao:

1. Maquraishi wa Makka walimkubali Muhammad kuwa ni sawa na wao. Kabla ya hapo walimuona kama muasi na mkimbizi wa kisasi chao.

2. Kwa kuuweka saini mkataba huo, Maquraishi walitoa utambuzi wa kimya wa ile Dola ya Kiislam ya Madina inayochipukia.

3. Wale Waislamu waliokuweko Makka, walificha imani yao mbele ya waabudu masanamu kwa hofu ya mateso kutoka kwao. Lakini baada ya Mkataba wa Hudaybiyya, walianza kutekeleza Uislamu hadharani.

4. Hadi mwaka wa 6 A.H. Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) alikuwa amefungwa katika mapambano yasiyokwisha na wapagani wa Kiarabu na Wayahudi, na hapakuwa na fursa kwa ajili yao ya kuuona Uislamu Katika matendo. Baada ya Mkataba wa Hudaybiyya waliweza “kuutathmini” Uislamu kwa mara ya kwanza. “Tathmini” hii ilisababisha kusilimu kwa wengi wao, na Uislamu ukaanza kuenea kwa kasi sana. Mkataba wa Hudaybiyya ulifungua milango ya kubadilishadini.

5. Makabila mengi ya Kiarabu, ingawa bado wapagani, yalitaka kuingia mikataba ya uhusiano na Waislamu lakini yalijihisi kuzuiwa na upinzani wa Maquraishi. Sasa yaliachiwa uhuru wa kufanya ushirikiano na Waislamu.

6. Mkataba wa Hudaybiyya ni jibu zuri sana kwa wale wakosoaji wanaodai kwamba Uislamu ulienea kwa ncha ya upanga. Hakuna uthibitisho bora zaidi kuliko Mkataba wa ukataaji huu wa vita kwa Muhammad, kama chombo cha sera, na cha mapenzi yake halali ya amani. Wapagani wa Kiarabu walivutiwa sana na propaganda za Maquraishi kwamba Muhammad alitamani sana vita. Sasa waliweza kuona kwa macho yao wenyewe kwamba Muhammad alirudi Madina bila hata ya “kulipiza,” ingawa alikuwa na jeshi pamoja naye, na ingawa aliwahi kuwashinda hao Maquraishi mara mbili - mnamo mwaka 624 na 627.

Huu Mkataba wa Hudaybiyya pia unaonyesha chuki ya Qur’an juu ya vita. Kabla ya mkataba, Waislamu walikuwa wamekwisha kushinda zile vita mbili za kihistoria za Badr na Ahzab (Handaki). Kama wangeshindwa katika yoyote kati ya hizo, Uislamu ungetoweka kabisa daima kutoka kwenye uso wa dunia.

Ushindi katika vita vyote hivi viwili ulihakikisha uhai wa kivitendo wa Uislamu. Machoni mwa Qur’an, miongoni mwa kampeni zote za Muhammad, ule Mkataba wa Hudaybiyya pekee ndio ulikuwa “Ushindi wa Dhahiri”.
Mkataba wa Hudaybiyya ulikuwa ndio utangulizi wa kwenye ushindi wa Uislamu dhidi ya nguvu za upagani, ushirikina, uabudu masanamu, ujinga, dhulma na unyonyaji. Umar ibn al-Khattab alileta kiburi kwenye sharti la tatu la Mkataba huo kwa vile lilikuwa halikubaliani; lakini ilikuwa, kwa usahihi kabisa, ni sharti hili hasa lililowaweka Maquraishi kwenye kujihami mara moja tu, na walikuja kwa kuomba kwa Mtume (s.a.w.) alibatilishe.

Miezi kumi na nane baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Hudaybiyya, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliingia Makka, kama mshindi, na alifuatana na waumini elfu kumi. Kutekwa kwa Makka kulikuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya Mkataba huu. Kwa sababu ya matokeo haya, wanahistoria wengi wameuita kwa usahihi kabisa huu Mkataba wa Hudaybiyya kama ubingwa wa ustadi wa utawala wa Muhammad.

Marmaduke Pichthall.

Kulikuwa na mfazaiko miongoni mwa Waislamu juu ya masharti haya (ya Mkataba wa Hudaybiyya). Waliulizana wenyewe kwa wenyewe: ‘Uko wapi huo ushindi ambao tuliahidiwa?’ Ilikuwa ni wakati wa safari ya kurudi kutoka al-Hudaybiyya ambapo ile Sura inayoitwa ushindi iliteremshwa. Makubaliano haya (ya kusitisha vita) yalithibitika, kwa kweli, kuwa ndio ushindi mkubwa ambao Waislamu mpaka hapo walikuwa wameupata. Vita vilikuwa ni kipingamizi kati yao na waabudu masanamu, lakini sasa marafiki walikutana na kuongea pamoja, na dini hii mpya ikaenea kwa haraka sana. Katika miaka miwili iliyopita kati ya kusainiwa kwa makubaliano hayo na kuanguka kwa Makka, idadi ya waliosilimu ilikuwa kubwa zaidi kuliko jumla ya idadi ya wote waliokuwa wamesilimu hapo kabla. Mtume (s.a.w.) alisafiri kwenda al-Hudaybiyya na watu 1400. Miaka miwili baadae, wakati watu wa Makka walipoyavunja makubaliano hayo, alikwenda dhidi yao pamoja na jeshi la watu 10,000. (Introduction to the translation of Holy Qur’an, 1975)

Kanuni mbili muhimu za Kiislamu zinaweza kuonekana katika utekelezaji wake ndani ya Mkataba wa Hudaybiyya, yaani:

1. Vita lazima iepukwe kwa gharama yoyote ile, labda ikiwa haizuiliki kabisa. Ufumbuzi wa matatizo yote lazima utafutwe na kupatikana kwa njia za amani, kwa kweli bila kuzihatarisha kanuni za Kiislamu. Kwa wapagani na Waislamu wengi, ilionekana kwamba Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.), ametoa “mamlaka kamili” kwa Suhayl, yule mjumbe wa Makka, kwa hiyo kwamba yeye (Suhayl), kwa namna fulani, alitamka masharti yake mwenyewe. Licha ya kujitokeza kama huko, Mtume (s.a.w.) aliyakubali masharti yale. Bila shaka, hapakuwa na hatari kwenye kanuni yoyote. Ilikuwa haiwaziki kwamba Mtume wa Uislamu atapingana na kanuni yoyote ya Kiislamu.

2. Mtume wa Allah (s.a.w.) . hana lazima ya kukubali kushindwa (kwa kus- tahi) na maoni au matakwa ya wafuasi wake, au ya watu kwa jumla. Idadi kubwa sana ya maswahaba zake Muhammad walikuwa hawakubaliani na kutiwa saini kwa Mkataba wa Hudaybiyya. Lakini alipuuza upinzani wao, na akaendelea na kuusaini. Yeye, kwa kweli , wala hakutafuta hata ushauri wa hata mmoja wao katika suala hilo. Kutoka mwanzo mpaka mwisho, aliongozwa, sio na matakwa ya “watu” au matakwa ya “wingi” wa watu bali na amri za Allah (s.w.t.) zilizohifadhiwa katika Kitabu Chake, makhsusi kwenye Aya ifuatayo:

وَأَنِ احْكُمْ بَيْنَهُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ وَاحْذَرْهُمْ أَنْ يَفْتِنُوكَ عَنْ بَعْضِ مَا أَنْزَلَ اللَّهُ إِلَيْكَ ۖ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَاعْلَمْ أَنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ أَنْ يُصِيبَهُمْ بِبَعْضِ ذُنُوبِهِمْ ۗ وَإِنَّ كَثِيرًا مِنَ النَّاسِ لَفَاسِقُونَ {49}

Na wahukumu baina yao kwa aliyoyateremsha Allah, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya aliyokuteremshia Allah. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Allah anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu.
(Sura ya 5; Aya ya 49)