read

Wake Zake Muhammad (S.A.W.), Mtume Wa Allah (S.W.T)

MKE WA KWANZA WA MUHAMMAD ALIKUWA NI KHADIJA. Walioana huko Makka na wakaishi kwa robo karne ya mapenzi na furaha pamoja – mpaka kifo chake. Wakati Khadija alipokuwa hai, Muhammad hakuoa mwanamke mwingine.

Baada ya kifo cha Khadija, Muhammad akaoa wanawake wengi wengine lakini hakuna mmoja kati yao ambaye angeweza kamwe kuchukua nafasi ile ile katika moyo wake kama aliyokuwa nayo Khadija.

Wakati alipokufa, ile furaha yake kamili, ya maisha ya ndoa, pia iliondoka pamoja naye. Mpaka mwisho wa maisha yake, alikumbuka mengi juu yake, na akamkumbuka kwa mapenzi, upendo na shukrani.

Mwanamke wa kwanza Muhammad aliyemuoa baada ya kifo cha Khadija, alikuwa ni Sawdah binti Zama’a, mjane ambaye mumewe alikufa huko Abyssinia.

Mke wa tatu wa Mtume (s.a.w.) alikuwa ni Aisha, binti ya Abu Bakr. inasemekana kaolewa huko Makka lakini alikwenda nyumbani kwa mumewe huko Madina.

Mtume (s.a.w.) mara nyingi alijaribu kupata mahusiano mema na ukoo au kabila kwa kuoa mmoja wa wanawake zake. Kumuoa kwake Ummu Habiba binti ya Abu Sufyan, na Safiya binti ya Akhtab, kulikuwa ni ndoa kama hizo.

Mmoja wa wake za Mtume (s.a.w.) alikuwa ni Hafsa binti ya Umar ibn al-Khattab. Mumewe aliuawa katika vita vya Badri, na baba yake alikuwa na shauku ya mume mpya kwa ajili yake. Alimposesha kwa marafiki zake wa moyoni, kwanza kwa Uthman bin Affan, na kisha kwa Abu Bakr. Wote walisikitikia kukosa uwezo kwao wa kumuoa.

Umar alidhalilika kwa kule kukataliwa kwa binti yake hata na marafiki zake mwenyewe, na akalalamika kwa Mtume (s.a.w.) kuhusu hilo. Mtume, ili kutuliza uchungu wa moyo wa Umar, akasema kwamba madhali hakuna mtu mwingine aliyemtaka binti yake, yeye atamchukua harimu yake mwenyewe.

Ukimuacha Khadija, wake wengine wote wa Mtume (s.a.w.) walibakia bila mtoto. Gavana wa Misri alikuwa amemtumia mtumwa wa kike Mkibti aliyeitwa Maria. Aliingia kwenye harimu yake, na akamzalia mtoto wa kiume ambaye alimwita Ibrahim.

Kuzaliwa kwa mtoto wa kiume kulimpa Maria umuhimu wa kipekee, kwenye maudhi makubwa na uchungu wa mioyo wa wake wenzie. Mtume (s.a.w.) alitoa mapenzi makubwa juu ya kijana mdogo huyo, na alitumia masaa mengi pamoja naye, akimbeba mikononi mwake. Lakini kwa bahati mbaya, kijana huyo hakuishi muda mrefu, na akafa katika mwaka ule wa kuzaliwa kwake.

D. S. Margoliouth

Miaka yake (Muhammad) ya mwisho ilichangamshwa na kwa muda kwa kuzaliwa kwa mtoto wa kiume na kimada/suria wake (sic – hili sio kweli) wa ki-Kibti - Maria, ambaye alimkubali kama ni wake, na ambaye alimwita kwa jina la muasisi wa kud- haniwa (sic - japo si kweli) wa dini yake, Ibrahim.

Kimada/suria huyo (sic) akiwa ni chanzo cha wivu mkali wa wake zake wengi wasiokuwa na watoto, tukio hili la bahati liliwasababishia uchungu wa moyo mkali sana; ambao kwa kweli ulipunguzwa kwa haraka na kifo cha mtoto huyo (ambaye aliishi kwa miezi kumi na moja tu).
(Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Muhammad Husein Haykal

Kwa kuzaa mtoto, hadhi ya Maria ilipanda katika taadhima ya Muhammad; yeye sasa alimuona kama mke huru, hasa, anayefurahia nafasi yenye fadhila kubwa.

Ilikuwa ni kawaida kwamba mabadiliko haya yangechochea sio wivu kidogo mion- goni mwa wake zake wengine waliokuwa wagumba. Ilikuwa ni kawaida pia kwamba heshima na upendo wa Mtume (s.a.w.) kwa mtoto huyo aliyezaliwa na mama yake viliongezea wivu huo. Zaidi ya hayo, Muhammad kwa ukarimu kabisa alimzawadia Salma, mke wa Abu Rafi, kwa jukumu lake kama mkunga. Alisherehekea uzazi huo kwa kutoa kipima cha nafaka kwa mafukara wote wa Madina.

Alimkabidhi huyu mtoto aliyezaliwa hivi karibuni kwenye malezi ya Ummu Sayf, mama wa kunyonyesha, ambaye alikuwa akimiliki mbuzi saba, ambao maziwa yake alikuwa Ayaweke kwenye haki ya matumizi ya huyu mtoto mchanga. Kila siku Muhammad alitembe- lea nyumba ya Maria ili akaone ule uso mwangavu wa mwanae na kujihakikishia yeye mwenyewe maendeleo ya afya ya mtoto huyo na ukuaji wake. Yote hii ilichochea wivu mkali miongoni mwa wake zake wagumba. Swali lilikuwa, ni kwa muda mrefu kiasi gani wake zake hawa wangekuwa na uwezo wa kuvumilia mateso Haya ya kila siku.

Siku moja, pamoja na tabia za fahari ya mababa wapya, Mtume (s.a.w.) aliingia chumbani kwa Aisha pamoja na yule mtoto mikononi mwake, ili amuonyeshe kwa Aisha. Alimuonyesha yeye kufanana kwake kukubwa na mwanae. Aisha akamtazama yule mtoto na akasema kwamba hakuona kufanana kokote kule. Wakati Mtume (s.a.w.) aliposema jinsi mtoto anavyokua, Aisha akajibu kwa chukichuki kwamba mtoto yeyote akipewa kiwango cha maziwa kama alichokuwa anapewa yeye angekua na ukubwa tu na mwenye nguvu kama yeye. Kwa kweli, kuzaliwa kwa Ibrahim kulileta maumivu mengi sana kwa wake za Mtume (s.a.w.) kiasi kwamba wengine wao wangekwenda kwa majibu makali zaidi ya haya na sawa na haya. Ilifikia kiasi kwamba Wahy wenyewe ulilazimika kutamka shutuma maalum. Bila shaka, jambo zima liliacha chapa katika maisha ya Mtume (s.a.w.) na vilevile katika historia ya Uislamu.
(The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Wakati mmoja, Hafsa anasemekana kuwa “alimshitukiza” mumewe akiwa na Maria, na akaieleza “siri” hii kwa Aisha. Wake wengine wa Mtume (s.a.w.) waliisikia habari hii kutoka kwa Aisha. Kulikuwa na umbeya mwingi na uropokaji kuhusu tukio hili. Hatimae, Qur’an Tukufu ilibidi iingilie kati kwa karipio kwa mabibi wawili hao katika Aya ifuatayo:

إِنْ تَتُوبَا إِلَى اللَّهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا ۖ وَإِنْ تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ {4}

“Kama ninyi wawili hamkutubia kwa Allah, basi nyoyo zenu zimekwisha kuelekea huko; lakini kama mtasaidiana dhidi yake (Mtume), hakika Allah ndiye mlinzi wake,na Jibrilu, na waumini wema na zaidi ya hayo, Malaika pia watamsaidia.” (Sura ya 66; Aya ya 4)

Maelezo Ya Mfasiri

“Nyumba ya Mtume (s.a.w.) haikuwa sawa na nyumba zingine. Wake bora wa Mtume (s.a.w.) walitegemewa kuwa na tabia njema ya hali ya juu na ukimya kuliko wanawake wa kawaida, kwani walikuwa na kazi ya hali ya juu ya kutekeleza. Lakini walikuwa binadamu hata hivyo, na walikuwa wenye kupatwa na udhaifu wa jinsia yao, na wakati mwingine walishindwa.”

“Ujinga wa Aisha wakati mmoja ulisababisha matatizo magumu sana: akili ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) ilipata uchungu sana, na aliacha ujamaa na wake zake kwa muda fulani.

Binti ya Umar, Hafsa, alikuwa pia wakati mwingine mwepesi wa kutumia vibaya nafasi yake, na pale wawili hawa walipoungana katika ushauri wa kisiri, na kuzungumzia mambo na kupeana siri, walisababisha huzuni kubwa kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w).” (A.Yusufu Ali)

Wengi wa wafasiri na watarjuma wa Qur’an wamelitafsiri neno la Kiarabu Saghat linalotokea kwenye Aya ya 4 ya Sura ya 66, iliyonukuliwa hapo juu, kama “kuelekea.” Tarjuma yao inasomeka kama ifuatavyo:

Mioyo yenu imekwisha kuelekea.

Kuelekea kwenye nini? “Mioyo yenu imekwisha kuelekea,” ni tafsiri isiyo na maana kati- ka muktadha huu. Tafsiri sahihi ya neno Saghat ni “imepotoka,” M. Abul Ala Mauduudi ametoa tafsiri sahihi ya Aya hii ambayo ni kama ifuatavyo:

“Kama nyie (wanawake) wote mtatubia kwa Allah, (ni bora kwenu), kwani mioyo yenu imepotoka kutoka kwenye njia ya haki, na kama mtasaidiana dhidi ya Mtume, basi mjue kwamba Allah ndiye Mlinzi wake, na baada Yake ni Jibril na waumini wema na Malaika ndio wenzake na walinzi wake…”

(Tafhiim-ul-Qur’an, Juz. 6, Lahore, Pakistani, tarjuma ya Kiingereza ya Muhammad Akbar Muradpuri na Abdul Aziz Kamal, chapa ya pili, Mei 1987)

Wakati Hafsa “alipomshitukiza” Muhammad akiwa pamoja na Maria, alipaswa ati kutoa ahadi kwa Hafsa kwamba yeye hatakutana Maria tena. Hili, kwa kweli, limekatazwa. Mke mmoja hakuwa na haki kuzuia uhuru wa mumewe kukutana na wake zake wengine. Jaribio kama hilo kwa upande wa mke mmoja lingekuwa kinyume sio tu na sheria za Kiislamu bali pia na desturi za Arabia, wakati wote, kabla na baada ya Uislamu.

Sir William Muir

Katika suala la Zainabu, Muhammad (s.a.w.) alitoa ujumbe kutoka Mbinguni ambao ulikataza ahadi yake ya kutengana na Maria, ukamkemea Hafsa na Aisha kwa ukaidi wao, na ukadokezea juu uwezekano wa wake zake wote kuachwa kwa mwenendo wa uasi sana kwake mwenyewe. Kisha akajiondoa kwenye ujamaa nao, na kwa mwezi mzima akaishi peke yake pamoja na Maria. Umar na Abu Bakr walifedheheka sana kwa kutengwa kwa mabinti zao kwa ajili ya kimada duni (ingawa sio kweli) na wakahuzunikia umbeya wa mwenendo mzima. (The Life of Muhammad, London, 1877)

Kutoka kwenye hayo yaliyotangulia inaweza kuonekana kwamba maisha ya nyumbani ya Mtume (s.a.w.), baada ya kifo cha Khadija, hayakuonyesha ufasaha wowote. Wengi wa wake zake walikuwa ni wanawake wenye wivu, na “ajali” ya kwanza ya wivu wao ilikuwa ni amani ya nyumba yake.

D. S. Margoliouth

Kukaa kwa wake katika harimu ya Mtume (s.a.w.) kulikuwa kufupi, kutokana na kutostahili kwa tabia; katika moja au zaidi ya masuala, wale wageni walifundishwa na wale wake za Mtume (s.a.w.) wenye wivu kanuni ambazo, walipozitamka bila kujua maana, zilimfanya Mtume (s.a.w.) kuwafukuza papo hapo. Mmoja alifukuzwa kwa kutangaza katika kufa kwa yule mtoto mchanga Ibrahim kwamba baba yake angekuwa ni Mtume, asingeweza kufa – matumizi ya ajabu ya uwezo wa fikira..
(Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Ilikuwa ni mazoea ya Mtume (s.a.w.), mara kwa mara, kuondoka nyumbani kwake usiku na kwenda kutembelea makaburi ya Baqii kuwaombea marehemu waliozikwa pale. Kabla tu ya maradhi yake ya mwisho, aliyatembelea makaburi hayo mara nyingine tena, labda kwa mara ya mwisho, na akakaa hapo na kuwaombea marehemu hao mpaka usiku wa manane. Baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba ilikuwa ni katika safari hii kwamba alipatwa na homa ya baridi, na ilikuwa ndio mwanzo wa maradhi yake makali. Aisha anasemekana kumfuata katika moja ya safari hizi.

D. S. Margoliouth

Wakati wa usiku wa manane, inavyosemekana, Mtume (s.a.w.) alikwenda kwenye uwanja wa makaburi unaoitwa al-Baqii, na akaomba msamaha kwa ajili ya wale marehemu waliozikwa pale. Hili kwa hakika alilifanya hapo kabla; Aisha safari moja alimfuata yeye kama mpelelezi alipotoka wakati wa usiku, kwa kumdhania yeye kwamba amedhamiria mapenzi fulani; lakini alikokuwa akienda, aligundua, ilikuwa ni makaburini. (kutoka Musnad ya Imam Ahmad Hanbal, juz. Iv, uk. 221).
(Muhammad and the Rise of Islam, London, 1931)

Wanawake aliowaoa Mtume (s.a.w.) baada ya kifo cha Khadija, walikuwa tofauti sana na yeye (Khadija) kwa tabia na mwenendo.
Khadija alikuwa amempa mumewe msaada thabiti na usio na mbwembwe katika uenezaji wa Uislamu, na alijitolea muhanga utajiri wake wote mkubwa kwa ajili ya lengo hilo. Kujitolea muhanga kwake kulimshusha mpaka kwenye hali ya ufukara lakini hakulalamika kwa mumewe kuhusu kukosa kitu chochote. Ndoa yake ilikuwa na utajiri katika baraka za upendo na urafiki wa mumewe, na katika furaha isiyo na kikomo.

Muhammad Mustafa mwenyewe aliishi maisha ya kawaida kabisa. Hata pale alipokuwa ndio mtawala wa Arabia nzima, alikuwa bado ni mwenye kujihini kama alivyokuwa huko Makka kabla ya kuhama kwake kwenda Madina. Aisha mwenyewe anasema hana kumbukumbu kama mumewe aliwahi kula chakula cha ridhaa ya moyo wake mara mbili kwa siku moja.

Wakati ngawira za vita au mapato ya dola yalipokuja, Mtume (s.a.w.) aliyagawanya mion- goni mwa Waislamu. Wake zake waligundua kwamba hata wale wanawake masikini kabisa hapo Madina walikuwa kwa hivyo wakawa matajiri lakini sio wao. Ilijitokeza kwao kwamba hawakupaswa wakoseshwe ukarimu mkubwa wa mume wao. Hata hivyo, wao hawakuzoea kuishi maisha ya kujihini kiasi hicho kama alivyokuwa yeye. Walilijadili suala hili miongoni mwao wao wenyewe, na wote wakakubaliana kwamba walipaswa kupata sehemu katika vile vitu vizuri na halali – sawa na wale wanawake wengine wa Madina.

Wake za Mtume, kwa hiyo, wakawasilisha madai yao kwake. Walikuwa na kauli moja kati- ka kudai posho kubwa ya kujikimu kutoka kwake. Wawili wao, yaani, Aisha na Hafsa, wal- isimama kama “wazungumzaji” wao. Walipokuwa wakisisitiza madai yao kwake, Abu Bakr na Umar wakaja kumuona Mtume (s.a.w.) kwa shughuli fulani za kibinafsi au za umma.

Mtume (s.a.w.) alikaa kimya, akiwa amezungukwa na wake zake. Pale Abu Bakr na Umar walipogundua yale yanayopikwa, walikasirika sana, na wakawalaumu kwa ukali kabisa mabinti zao kwa kudai pesa zaidi kutoka kwa mume wao.

Muhammad Husein Haykal

Abu Bakr alimuinukia binti yake Aisha na kumvuta nywele zake na vivyo hivyo Umar akamfanyia binti yake, Hafsa. Wote Abu Bakr na Umar wakawaambia binti zao: “Mnathubutu kumuomba Mtume wa Allah (s.a.w.) kile ambacho hawezi kumudu kukitoa?” Wao wakajibu: “Hapana, Wallahi hatumuombi yeye kitu kama hicho.” (The Life of Muhammad, Cairo, 1935)

Hatimae jambo hilo lilikomeshwa pale iliposhushwa Aya mpya kwa sababu hii, na ambayo inasomeka kama ifuatavyo:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْوَاجِكَ إِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا {28}

وَإِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنْكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا {29}

Ewe Mtume! Waambie wake zako: “Ikiwa mnataka maisha ya dunia hii na mapambo yake, basi njooni, nitakulipeni kitokea nyumba, na kukuacheni kwa njia nzuri. Na ikiwa mnampenda Allah na Mtume Wake, na nyumba ya Akhera, Basi Allah amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa. (Sura ya 33; Aya ya 28 na 29)

Maelezo Ya Mfasiri

Nafasi ya wake za Mtume (s.a.w.) haikuwa sawa na ile ya wake wa kawaida. Walikuwa na kazi na wajibu maalum… wake wote katika nafasi yao ya juu walipaswa kufanya kazi na kusaidia kama akina-mama wa umma. Yao hayakuwa ni maisha ya kutulia, kama yale ya masuria, ama kwa anasa zao wenyewe au anasa za mume wao. Wanaambiwa hapa kwamba walikuwa na sehemu katika Kaya Tukufu (ya Mtume) kama walipenda starehe na mapambo ya dunia tu. Kama hali ilikuwa ni hiyo, wangeweza kuachwa na kukimiwa vya kutosha, na zaidi. (A.Yusufu Ali)

Qur’an Tukufu iliwapa nafasi wake za Mtume, yaani, ama walikuwa wamchague Allah (s.w.t.) na Mtume Wake (s.a.w.), na kuishi maisha ya kujinyima na kujitoa muhanga; au wangeweza kuchagua anasa, starehe na mapambo ya dunia hii ambavyo kwa suala hilo ingewalazimu kuachana na mume wao daima. Fursa hiyo ilikuwa ya dhahiri, na wake hao walikuwa na uhuru wa kuchagua.
Aisha, Hafsa na mabibi wengine saba walilitafakari jambo hilo, na kisha wakaamua kusamehe burudani na starehe za dunia hii, na kubaki katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) kama wake zake.

Wakati Muhammad Mustafa (rehema na amani juu yake na Ahlul-Bait wake) alipokufa mwaka 632, alikuwa na wake tisa katika harimu yake. Aisha aliishi kwa nusu karne baada yake, na mke aliyeishi zaidi ya wake wengine wa Mtume, alikuwa ni Maimuna. Yeye, ilivyokuwa, alikuwa ndiye mwanamke wa mwisho aliyemuoa.