read

Waliosilimu Mwanzoni Na Mateso Kutoka Kwa Wapagani

Ingawa Abu Lahabi mara nyingi alifanikiwa katika kuyatawanyisha yale makundi yaliyokusanyika kusikiliza waadhi za Mtume, habari hata hivyo zilienea Makka kuhusu mawaidha hayo. Baadhi ya watu walizungumza kuhusu ujumbe wa Uislamu. Wale wenye fikra miongoni mwao waliuliza hili swali: “Ni dini gani hii ambayo Muhammad anatuitia sisi?” Swali hili lilionyesha udadisi kwa upande wao kuhusu huu ujumbe wa Uislamu, na wachache miongoni mwao walitaka kujua zaidi juu yake.

Katika siku zilizofuata, Muhammad alifanya majaribio mengi ya kuwahubiria watu wa Makka. Abu Lahab na mshirika wake, Abu Jahal, walifanya kila walichoweza kuihujumu kazi yake lakini hawakuweza kumkengeusha kutoka kwenye shabaha yake.

Muhammad, rehma na amani ziwe juu yake na kizazi chake, alitambua kwamba kazi yake haitakuwa rahisi. Alijua kwamba atakumbana na vikwazo vingi, na kwamba atakuwa apambane na upinzani mkali na wa kudumu wa waabudu masanamu. Lakini alitegemea rehma za Mungu kumuwezesha kuushinda upinzani.

Ulikuwa ni ujumbe wa ajabu ambao Muhammad alileta kwa Waarabu, na ulikuwa wa kipekee. Hakuna hata mtu mmoja aliyewahi kusikia kitu kama hicho kabla. Muhammad, Mtume wa Allah (s.w.t.) aliwaambia Waarabu wasiabudu kundi la vitu visivyo na uhai vilivyotengenezwa kwa mawe au magogo (miti) ambavyo wameviunda wenyewe, na ambavyo havikuwa na uwezo wa ama kuwapa wao chochote au kuchukua chochote kutoka kwao. Badala yake, aliwaambia, wanapaswa kutoa utii wao kwa Allah (s.w.t.) Mola wa ulimwengu wote. Aliwaambia pia kwamba katika macho Yake, katika macho ya Muumba wao, wote walikuwa sawa, na kama watakuwa Waislamu, watakuwa wote ni ndugu wa kila mmoja wao.

Muhammad pia alipenda kuirekebisha jamii ya Kiarabu. Hii sheria mpya ambayo ameiweka mbele kwa ajili ya madhumuni Haya, ilifanya Imani badala ya damu, kuwa kiungo maalum cha jamii hiyo. Lakini Waarabu hao wamezaliwa katika mfumo wa mila na desturi za kipagani; waliamini katika msingi wa miundo ya kikabila na udugu. Kwao wao “damu” ilikuwa tu ni kigezo cha mpangilio wa kijamii. Katika mawazo yao, kama dini ingeruhusiwa kuchukua nafasi ya damu katika mgawanyo huu, ingeweza kuvuruga muun- do wote wa jamii ya Kiarabu.

Muhammad pia aliwataka wale Waarabu matajiri kugawana utajiri wao na masikini na wale wenye kipato cha chini. Wale masikini, alisema, walikuwa na haki ya kupokea fungu lao kutoka kwenye mali ya matajiri. Ugawanaji huo, aliendelea kusema, utahakikisha ugawaji wa haki wa mali katika jamii.

Wengi wa Waarabu matajiri walikuwa wakopeshaedha; ama hasa, walikuwa “wala riba wakubwa.” Wamekuwa matajiri kwa kukopesha fedha kwa watu masikini kwa viwango vikubwa sana vya riba. Wale masikini hawakuweza kamwe kulipa madeni yao, na kwa hiyo wakanasa katika utumwa wa kiuchumi milele.

Kugawana mali yao ya haramu na watu walewale waliokuwa wakiwanyonya, ilikuwa kwao ni sawa na “kufuru.” Kwa kuwapendekezea kwamba wagawane mali yao na masikini, Muhammad alichezea kiota cha nyigu!

Kwa Waarabu, yote haya yalikuwa mambo mapya na yasiyojulikana; kwa kweli yalikuwa ya kimapinduzi. Kwa kuhubiri mambo ya kimapinduzi kama haya, Muhammad aliwakasirisha wale wenye madaraka tangu zamani. Waliokasirika sana miongoni mwao ni ule ukoo wa Umayya wa Maquraish. Watu wake ndio waliokuwa wala-riba wanaoongoza na mabepari wa Makka, na walikuwa ndio makuhani wakuu wa hekalu la wapagani. Ndani ya Muhammad na huo ujumbe wa Uislamu, waliona tishio kwenye utaratibu wao wa kijamii ambao uliegama kwenye heshima na nguvu.

Wao, kwa hiyo, waliamua kudumisha hali kama ilivyo. Katika miaka iliyokuja, walikuwa waunde kikosi cha vita visivyotulizika dhidi ya Uislamu, na upinzani wa kufa baada ya mapambano na Muhammad.

Lakini walikuwepo pia watu wachache walioona mvuto wenye nguvu katika yale mawazo mapya ambayo Muhammad alikuwa anayaanzisha, kwa ujumla yakiitwa Uislamu. Kwa kweli, waliyaona ni yasiyokanika, na kwamba waliyakubali.

Miongoni mwa waliosilimu mwanzo kwenye Uislamu walikuwa Yasir; mke wake, Sumayya; na mtoto wao wa kiume, Ammar. Walikuwa ndio ukoo wa kwanza ambao watu wake wote waliukubali Uislamu sawia, hivyo kuwa Familia ya Kiislam ya Kwanza.

Uislamu ulikuwa na mvuto maalum kwa matabaka ya waliokandamizwa hapo Makka. Pale watu wa matabaka haya walipokuwa Waislamu, walitambua pia kwamba kama wapagani, walidharauliwa na kutengwa na tabaka la juu la wenye kujali tabaka na wenye kujali utaifa wa hali ya juu wa Makka lakini Uislamu uliwapa kujiheshimu kupya. Kama Waislamu waliona fahari mpya ndani yao wenyewe.

Wengi wa waliosilimu mwanzo walikuwa “masikini na wanyonge.” Lakini walikuwepo Waislamu wachache matajiri pia kama Hudhayfa bin Utba na Arqam bin Abil-Arqam. Na wale watu wote ambao Abu Bakr aliwaleta kwenye Uislamu – Uthman, Talha, Zubayr, Abdur Rahman ibn Auf, Saad ibn Abi Waqqas na Abu Ubaidah ibn al-Jarrah – walikuwa pia ni matajiri na wenye nguvu. Walikuwa ni watu wa koo mbalimbali za Kiquraish.

Tunaweza kuchukulia kwamba pale mwanzoni, lile tabaka la juu la wapagani wa Makka lilishuhudia zile juhudi za Uislamu za kutaka kupata kutambuliwa zaidi kwa burudani kuliko kwa kero, bila ya kuzungumzia zile chuki na mpagao uliowashika baadae kidogo. Lakini jinsi harakati hii mpya ilivyoanza kushika kasi, walihisi kwamba yale mawazo ambayo Muhammad alikuwa akiyatangaza, yalikuwa kwa kweli ni “hatari,” na hayakuwa na chochote cha kichekesho juu yake. Walihoji kwamba mababu zao wameabudu masanamu kwa vizazi visivyo na idadi, kwa hiyo ibada ya masanamu ilikuwa ni sawa; na hawakuweza kumruhusu Muhammad kucheza na mtindo wao wa ibada.

Lakini Muhammad hakuridhika tu kukanusha ibada ya masanamu. Ya hatari zaidi na ya kutisha kwa Bani Umayya wenyeuchu wa mali ilikuwa ni mawazo yake ya haki za kiuchumi na jamii yaliyotishia kuangusha ngome yao ya heshima; muundo wa zamani wa madaraka na kundi la watu wenye madaraka; na taasisi zote za zamani zilizopitwa na wakati. Waliweka wazi, kwa hiyo, kwamba heshima ilikuwa ni kitu ambacho hawatakiacha – kwa gharama yoyote ile – iwe jahannam au maji marefu.

Lakini wazo moja ambalo lile tabaka la juu lililojichagua lenyewe la Quraish, lililoliona la kufedhehesha zaidi, lilikuwa ni ile “dhana” iliyopangwa na Muhammad, kwamba wale watu wa matabaka ya waliokandamizwa, waliodharauliwa, walionyonywa, wengi wao wakiwa watumwa wao, ambao sasa wamesilimu, wamekuwa wanaolingana – walinganao na Maquraish wakubwa na wenye nguvu! Dhana yao kuu ya maisha ilikuwa ni majigambo na makuu, na usawa na watumwa wao wenyewe, walio achwahuru na watumishi, ulikuwa kwao hauwaziki kabisa. Walikuwa wamejawa na ghiliba ya “ubora” wao binafsi kuliko wanadamu wote.

Kwa kutangaza rasmi hii kanuni ya “kinyume” ya usawa – usawa wa bwana na mtumwa, tajiri na masikini; na Mwarabu na asiyekuwa Mwarabu; kwa kukana madai ya ubora wa ukoo, na kufundisha kwamba mbele ya Allah (s.w.t.) hali ya muumini ilikuwa ya juu sana kuliko hali ya wasioamini wote katika dunia, Muhammad alitenda “uhaini” dhidi ya Maquraish!

Maquraish waliabudu masanamu mengi sana, na utaifa ilikuwa mojawapo.

Lakini kujivunia utaifa hakuthaminiwi katika Uislamu. Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu, watu wote wametokana na Adam, na Adam alikuwa ni udongo. Ibilisi (Shetani) alilaaniwa kabisa kwa sababu alihoji ubora wa kile alichodhania kuwa asili yake ni ya juu kama kinyume na alichokiona kuwa uchini sana wa asili ya mwanadamu. “Mwanadamu,” alisema, “ameumbwa kwa udongo ambapo mimi nimeumbwa kutokana na moto.”

Hisia kama hizi za utenganishaji ambazo huja pia kwa wanadamu hasa kwa nia ya kudai hadhi bora ya damu katika utu wao, zimekataliwa na Uislamu kwa nguvu kabisa. Uislamu umeangusha chini umaarufu wa utaifa, rangi na heshima, na umewakataza Waislamu kuwagawa watu katika makundi kwa misingi ya damu na/au ujirani wa kijografia au hadhi maalum ambazo wanaweza kuzidai juu yao wenyewe.

Machoni mwa Qur’an, mtu aliye bora sana ni yule muttaqi – yaani, mtu ambaye anampenda na kumtii Allah (s.w.t.) wakati wote. Katika Uislamu, kipimo pekee cha ubora wa mtu, ni mapenzi yake kwa Muumba. Mitihani mingine yote ya maisha binafsi haina maana yoyote.

Lakini kama ilivyoelezwa hapo juu, Maquraish hawakuwa katika hali ya kupokea mawazo haya. Pengine walikuwa kiufahamu hawawezi kuyazingatia haya. Waliyaona kama ni kufuru ya daraja, na kwa hiyo, yasiyoweza kuvumilika kabisa. Ulikuwa ni wakati huo basi pale walipoamua sio tu kumpinga Muhammad, Mtume wa Uislamu, bali pia kuangamiza huo “uasi” ulioitwa Uislamu wenyewe kabla haujaota mizizi na kuwa wenye kujitosheleza.Walisukumwa na Kiburi – majivuno yanayojijaza yenyewe kuzidi kipimo cha mwanadamu – na kwa tamaa ya madaraka kufanya uamuzi kama huo dhidi ya Muhammad na Uislamu.

Wakiwa na uamuzo huu, Maquraish walitangaza nia yao ya kupigana katika kulinda masanamu yao na miungu yao na vilevile katika ulinzi wa mfumo wao wa kiuchumi na kijamii.

Makka ilikuwa katika hali ya kivita!

Maquraish walifungua mapambano dhidi ya Uislamu kwa kuwabughudhi na kuwatesa Waislamu. Mwanzoni, mateso yaliishia kwenye kuzomea na kebehi na matusi. Lakini kiasi muda ulivyoendelea mbele, makafiri hao walitoka kwenye ukali wa maneno kwenda kwenye ukali wa matendo. Walijizuia kuumiza majeraha ya mwili juu ya Muhammad mwenyewe kwa hofu ya kuchochea visasi; lakini hawakuwa na kusita katika kuwaumiza Waislamu, askari wa kawaida. Kwa muda mrefu, walikuwa ni hawa askari wa kawaida waliobeba sehemu kubwa ya ghadhabu za Maquraish.

Ibn Ishaq:

“Kisha Maquraish wakawachochea watu dhidi ya maswahaba wa Mtume (s.a.w.) ambao wamekuwa Waislamu. Kila kabila liliwashambulia Waislamu miongoni mwao, wakiwapiga na kuwashawishi kutoka kwenye dini yao. Mungu alimkinga Mtume wake kutokana nao kupitia ami yake (Abu Talib), ambaye, alipoona kile Maquraish walichokuwa wakikifanya, aliwaita Bani Hashim na Bani Muttalib kusimama naye katika kumkinga Mtume. Hili walikubaliana kulifanya, isipokuwa Abu Lahab.”
(The Life of the Messenger of God)

Baadhi Ya Waathirika Wa Mateso:

Bilal, yule aliyekuwa mtumwa wa Kihabeshi wa Umayya bin Khalaf. Umayya na makafiri wengine walimtesa katika mwanga mkali wa jua la moto sana la Makka, na wakamtesa kupita kiasi cha uvumilivu wa binadamu. Lakini aliimarishwa na asili ya nguvu za ndani na ujasiri ambavyo kamwe havikumvunja moyo. Kumpenda Allah (s.w.t.) na mapenzi kwa Mtume Wake vilimuwezesha kuyavumilia mateso kwa furaha. Abu Bakr akamnunua kutoka kwa bwana wake na akamwacha huru. Mtume (s.a.w.) alipohamia Madina, alimteua Bilal kuwa Muadhini wa kwanza wa Uislamu. Sauti yake kubwa yenye kuvuma ilisikika kwenye anga la Madina kwa ukelele wa Allah-u-Akbar (Mungu ni Mkubwa). Katika miaka ya baadae, wakati utekaji wa peninsula ulipokamilika, Mtume wa Allah (s.w.t.) alimchagua Bilal kuwa katibu wake wa hazina.

Khabab ibn el-Arat. alikuwa ni kijana wa miaka ishirini aliposilimu. Alikuwa mtegemezi wa Banu Zuhra. Maquraish walimtesa siku baada ya siku. Alihama pamoja na Mtume (s.a.w.) kwenda Madina.

Suhaib bin Sinan, alikuwa ametekwa na kuuzwa kama mtumwa na Wagiriki. Alipokuja kuwa mwislamu, Maquraish walimpiga kikatili sana lakini hawakuweza kuitingisha imani yake.

Abu Fukaiha, alikuwa mtumwa wa Safwan bin Umayya. Alisilimu katika wakati mmoja na Bilal.

Kama Bilal, aliburuzwa pia na bwana wake katika mchanga wa moto akiwa amefungwa kamba miguuni mwake. Abu Bakr alimnunua na kumpa uhuru. Alihamia Madina na Mtume (s.a.w.) lakini akafa kabla ya vita vya Badr.

Lubina, alikuwa mtumwa wa kike wa Mumil bin Habib. Amin Dawidar anaandika katika kitabu chake, Pictures From the Life of the Prophet (Cairo, Egypt, 1968), kwamba Umar bin al-Khattab, khalifa wa baadae wa Waislamu, alimtesa, na kila alipopumzika, alisema: “Sikuacha kukupiga kwa sababu ya huruma. Nimesimama kwa sababu nimechoka.”
Alirudia kumpiga baada ya kupumzika. Abu Bakr alimnunua na akamuacha huru.

Zunayra, alikuwa mtumwa mwingine wa kike. Alipotangaza imani yake katika Uislamu, Umar ibn al-Khattab, na Abu Jahl, walipokezana katika kumtesa mpaka akawa kipofu. Amin Dawidar anaeleza kwamba miaka mingi baaadae alirudia kuona tena, na Maquraish wakakuhusisha kupona huku na “uchawi” wa Muhammad. Abu Bakr akamnunua na kumwacha huru.

Nahdiyya na Ummu Unays walikuwa ni watumwa wengine wawili wa kike ambao walikuja kuwa Waislamu. Mabwana zao waliwatesa kwa kuukubali Uislamu. Abu Bakr aliwanunua na akawapa uhuru wao.

Walikuwepo Waislamu wengine ambao hawakuwa watumwa bali walikuwa “masikini na wanyonge.” Wao pia walipata mateso. Miongoni mwao walikuwa ni Ammar ibn Yasir na wazazi wake. Mtu mwingine wa kundi hili alikuwa ni Abdullah ibn Masud, kijana wa Kiislam. Alitambulikana miongoni mwa maswahaba wa Mtume (s.a.w.) kwa elimu yake na maarifa, na alikuwa mmoja wa mahafidh (wa Qur’an kwa kichwa) wa mwanzoni katika Uislamu, kila Aya mpya ilipoteremshwa, aliisikia kutoka kwa Mtume (s.a.w.) na akaikariri.

Imeelezwa kwamba wakati Surat Rahman (Sura ya 55) iliposhuka, Mtume wa Allah (s.w.t.) aliwauliza maswahaba zake, ni nani miongoni mwao angekwenda kwenye Al-Kaaba na kuisoma mbele ya makafiri. Masahaba wengine walirudi nyuma lakini Abdullah ibn Masud akajitolea kwenda. Alikwenda kwenye Al-Kaaba na akaisoma Sura hiyo mpya kwa sauti kubwa. Baada ya Mtume (s.a.w.) mwenyewe, Abdullah ibn Masoud alikuwa ndiye mtu wa kwanza kusoma Qur’an ndani ya Al-Kaaba mbele ya kundi lenye uhasama la makafiri. Hawa makafiri walimponda mara kwa mara lakini hawakuweza kumtishia kuwa kimya.

Ibn Ishaq Anasema:

“Yahya ibn Urwa ibn al-Zubayr aliniambia, kama kutoka kwa baba yake kwamba mtu wa kwanza kusoma Qur’an kwa sauti hapo Makka, baada ya Mtume (s.a.w.) mwenyewe alikuwa ni Abdullah ibn Masud.”
(The Life of the Messenger of God)

Mwanachama mwingine wa kundi hili alikuwa Abu Dharr al-Ghiffari. Alikuwa wa kabila la Ghiffar ambalo liliishi maisha yao kwa unyang’anyi. Kutoka kwa wasafiri alisikia kwamba ametokea Mtume (s.a.w.) hapo Makka ambaye amewashauri Waarabu kutupilia mbali ibada ya masanamu, na kumuabudu Allah (s.w.t.) peke yake, kutosema chochote ila kweli tupu, na kutowazika mabinti zao wakiwa hai. Alijihisi kwamba amevutiwa sana na Mtume huyu, na akasafiri kwenda Makka kuthibitisha ukweli wa taarifa alizozisikia kuhusu yeye.

Huko Makka alikuwa mgeni. Alikwisha kusikia kwamba Muhammad amekwishajifanyia maadui wengi mwenyewe kwa kuhubiri kinyume na ushirikina wa Kiarabu. Yeye, kwa hiyo, alisita kumuuliza mtu yeyote kumhusu Muhammad. Aliitumia siku nzima kwenye kivuli cha Al-Kaaba kuangalia wapita njia. Wakati wa jioni, Ali ibn Abi Talib alibahatika kupita hapo alipokuwa. Ali aligundua kwamba Abu Dharr alikuwa mgeni pale mjini, na akamkaribisha nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha jioni.

Abu Dharr akaukubali mwaliko huo, na baadae alimwelezea Ali juu ya madhumuni ya kutembelea kwake Makka. Ali, kwa kweli, alifurahi sana kumuelekeza mgeni wake mbele ya bwana wake, Muhammad Mustafa. Abu Dharr alijifunza kutoka kwa Mtume wa Allah (s.w.t.) maana ya ujumbe wa Uislamu. Aliona vyote, Mtume (s.a.w.) na ujumbe wake havikataliki. Alivutiwa na ile nguvu ya mvuto ya Uislamu. Baada ya kusilimu, kitu cha kwanza kabisa ambacho alitaka kufanya ni kuwakataa katakata makafiri. Alikwenda kwenye Al-Kaaba na kusema kwa sauti kubwa:

“Hapana mungu ila Allah (s.w.t.), na Muhammad ni Mtume Wake.”

Kama ilivyotarajiwa, makafiri hao wakamvamia, na wakaanza kumuangushia vipigo juu yake. Kutoka kwenye ghasia hizi aliokolewa na Abbas ibn Abdul Muttalib, ami yake Mtume. Aliwaambia wale watu wa Makka kwamba Abu Dharr alikuwa wa kabila la Ghiffar ambao eneo lao limelala kutagaa zile njia za misafara kwenda kaskazini, na kama watamfanyia madhara yoyote, watu wa kabila lake watazuia upitaji wa misafara yao ya biashara kwenda Syria.

Abu Dharr al-Ghiffari ni mmoja wa watu maarufu kwenye historia ya Uislamu. Alikuwa ndiye mtu asiyekuwa na woga kabisa na asiyeogopa kusema kweli miongoni mwa maswa-aba wote wa Muhammad Mustafa ambaye wakati mmoja alisema “Mbingu haijawahi kutandaza mwamvuli wake juu ya mtu yeyote aliyekuwa mkweli kuliko Abu Dharr.”

Woga wa vurugu za Maquraishi haukuzizuia nyoyo hizi za kishujaa na adilifu kuukubali Uislamu, na kila mmoja wao aliacha alama juu yake kwa kujitolea mhanga kwake.

Pia mtu mashuhuri miongoni mwa Waislamu wa awali alikuwa ni Mas’ab ibn Umayr, binamu ya baba yake Muhammad. Miaka mingi baadae, katika Kiapo cha Kwanza cha Akaba, wananchi wa Yathrib walimuomba Mtume (s.a.w.) kuwarudisha pamoja nao mwalimu wa Qur’an, na bahati ikaangukia juu yake. Hii ilimfanya awe mtumishi wa kwanza katika Uislamu. Alikuwa pia ndiye mshika bendera wa jeshi la Waislamu katika vita vya Uhud lakini akauawa kwenye mapigano.

Kama jamaa wa familia ya Makka alikubali Uislamu, alitenganishwa nao kwa wakati wote, bila ya matumaini yoyote juu yake ya kurejesheana uhusiano. Watu wa Makkah wengi waliuona Uislamu kama “nguvu yenye kutenganisha” iliyokuwa ikivunja familia zao, na baadhi yao walidhani kwamba walipaswa kuzuia “utenganishaji” huu usienee.

Lakini mbali na tishio la kutumia nguvu kukomesha harakati hii mpya, hawakuweza kufikiria kitu kingine chochote ambacho kingeweza kuonekana chenye matokeo mazuri zaidi katika kusimamisha maendeleo yake. Walifikiria pia kwamba kama hawatafanya haraka na kwa uthabiti wa kutosha, haikuelekea kutowezekana kwamba kila nyumba hapo Makka kuwa uwanja wa vita ambamo wahusika wakuu wa ile imani ya zamani na hii mpya wangejiingiza kwenye mapambano ya umwagaji damu mkubwa dhidi ya kila mmoja wao.

Walikuwepo baadhi ya wengine miongoni mwa wapagani waliodhania kwamba Muhammad alishawishiwa na lengo la kukataa mtindo wao wa jadi wa ibada na masanamu yao. Wote waliweka vichwa vyao pamoja na wakajaribu kufikiria juu ya ufumbuzi usio wa kawaida wa tatizo hilo. Baada ya mjadala mrefu, waliamua kumtuma Utba, mmoja wa wakuu wa Maquraish, kuonana na Muhammad, na kujaribu kumshawishi kuacha kazi yake hiyo. Utba alijulikana kwa uwezo wake wa kushawishi.

Alimwendea Mtume wa Allah (s.a.w.) na akasema: “Ewe Muhammad! Usipande mbegu ya mfarakano na kutoelewana miongoni mwa Waarabu, na usiilaani miungu ya kiume na ya kike, mababu zetu waliyoabudu kwa karne nyingi, na tunaiabudia leo. Kama nia yako katika kufanya hivyo ni kuwa kiongozi wa kisiasa, tuko tayari kukukubali kama mkuu wa Makka. Kama unataka mali, ni kiasi cha kusema tu, na tutakupatia kila tutakachoweza. Na kama umwenye kutaka kuoa katika ukoo bora, wewe utaje tu, nasi tutaandaa hilo kwa ajili yako.”

Muhammad aliyasikia yote aliyoyasema Utba lakini badala ya kuonyesha tamaa yoyote ya cheo au mali au urembo, alisoma mbele yake Surat Sajda, (Sura ya 32 ya Qur’an), ule wahyi mpya kabisa kutoka Mbinguni. Kusoma kulipokwisha, Utba alirudi kwa Maquraish na kuwashauri wamwache Muhammad na wasimuingilie tena.

Aliwaambia pia kwamba kama Muhammad akishindwa katika kazi yake, basi wao (Maquraish) hawatapoteza chochote; lakini kama atafanikiwa katika hilo, basi watashiriki katika mamlaka yake yote na utukufu.

Lakini Maquraish hawakuukubali ushauri wa Utba wa kujizuia katika kumshughulikia Muhammad na wafuasi wake. Waliendelea kuwatesa Waislamu kama mwanzoni na wakabaki kufikiria juu ya mkunjo mpya utakaoleta matokeo bora katika kusimamisha maendeleo ya Uislamu kuliko ukatili wao wote ulivyokwishafanya mpaka hapo.

Muhammad alilindwa na ami na mlezi wake, Abu Talib. Kwa wakati wote Abu Talib alipokuwa hai, wapagani hao hawakuweza kumsumbua mpwa wake. Iliwajia baadhi yao kwamba wangepaswa pengine kumshawishi Abu Talib mwenyewe, kutotilia maanani ulinzi wake juu ya Muhammad kwa niaba ya mshikamano wa kikabila. Kwanza, mshikamano wa kabila ulikuwa ni kitu chenye umuhimu zaidi kulichukulia kwa purukushani hata na Abu Talib, licha ya mapenzi yake yote kwa mpwawe.

Maquraish waliamua kutuma ujumbe, unaotokana na watu mashuhuri wa kabila hilo, kwa Abu Talib. Ujumbe huo ulimwendea, na ukamsihi kwa niaba ya mshikamano wa kikabila wa Maquraish kupuuza ulinzi wake kwa Muhammad ambaye alikuwa “anauvuruga” vibaya sana.

Abu Talib, kwa kweli, hakuwa na nia ya kupuuza ulinzi wake kwa Muhammad. Bali aliwaridhisha wale wajumbe wa Maquraish kwa maelezo ya kiuchamungu na maneno yenye kutuliza, na wakarudi majumbani kwao “mikono mitupu.”

Wajumbe hao pia waligundua kwamba wamerudi nyumbani kutoka kwenye “kufukuzazimwi;” lakini hawakushituliwa na kushindwa kwao, na wakati fulani baadae, walifanya jaribio jingine la kuvunja “ushirikiano” wa Abu Talib na Muhammad. Ujumbe mpya ukaenda kumuona Abu Talib, na safari hii, wajumbe wake walichukua pamoja nao kijana mmoja mwenye sura nzuri, Ammarra ibn Walid, ambaye walimtoa kwa Abu Talib kama “mwana” kama angewapa wao Muhammad.

Abu Talib atakuwa ameucheka sana huu mwanzo wa jambo hili la Maquraish. Hivi kweli waliamini kwamba angewapa mwanae mwenyewe wamuue, na kwamba angelea mmoja wa watoto wao kama mwanae hasa? Jambo lenyewe lilikuwa la kipumbavu. Lakini kwa mara nyingine tena, Abu Talib aliishughulikia hali hiyo kwa desturi yake ya maarifa na upole, na wakarudi.

Hili jaribio la pili la Maquraish la kumbembeleza Abu Talib kumtoa Muhammad, pia lilishindwa. Pale maana ya kushindwa huku ilipozama akilini mwao, walitambua kwamba majaribio ya amani ya kulitatua tatizo hili yote Hayakuzaa matunda. Waliamua kujaribu kitu chenye matokeo ya haraka zaidi.

Kwa ajili ya maudhi tu na kuvunja moyo, watungasera wa Maquraish walichukuwa msimamo mgumu na wakatuma ujumbe wao wa tatu na wa mwisho kwa Abu Talib. Jukumu lake lilikuwa ni kumshurtisha kumsalimisha Muhammad kwao. Viongozi wa ujumbe huo waliwasilisha kauli ya mwisho kwa Abu Talib: ama alikuwa amsalimishe Muhammad kwao, vinginevyo atakabiliana na matokeo ya kukataa kwake kufanya hivyo.

Abu Talib alikuwa mtu mwenye moyo wa furaha na tabia ya uchangamfu, lakini ilikuwa siku nzito katika maisha yake. Maquraish hao, alijua, hawakuwa wakiganganya. Kwa hiyo alimwita Muhammad na kumjulisha juu ya madhumuni ya uwakilishi wa Maquraishi, na kisha akaongeza : “Oh maisha ya ami yako! Usinitwishe mzigo juu yangu ambao nitauona ni zaidi ya nguvu zangu kuubeba.”

Muhammad akajibu: “Ewe ami yangu! Kama Maquraishi wataliweka jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wa kushoto, mimi sitaacha kutangaza Upweke wa Allah (s.w.t.) katika kutekeleza wajibu huu, ama nitafanikiwa na Uislamu utaenea; au, kama nitashindwa, nitachakaa katika jaribio hilo.”

Abu Talib hakuwa mtu wa kumshawishi Muhammad asihubiri Uislamu. Bali alikuwa anajaribu ushupavu wake. Jibu la wazi la Muhammad lilimvutia na kumridhisha kwamba hatasita, na akasema: “Nenda mwanangu, na fanya chochote unachotaka. Hakuna atakayethubutu kukufanyia madhara yoyote.”

Sir William Muir:

“…. lakini wazo la kutelekezwa na mlinzi wake mpole (Abu Talib) lilimlemea Muhammad. Alibubujikwa na machozi, na akageuka ili kuondoka. Ndipo Abu Talib akaita kwa sauti kubwa: “Mtoto wa ndugu yangu! Rudi.” Hivyo akarudi. Na Abu Talib akasema: “Nenda kwa amani, mpwa wangu, na sema lolote unalotaka. Kwani Wallah, kwa namna yoyote ile, sitakuacha kamwe.” (The Life of Muhammad, 1877)

Muhammad Husein Haykal:

“Abu Talib akasema: “Endelea, mpwa wangu, na sema utakalo. Wallah. ninaapa kamwe sitakusaliti kwa maadui zako.” Abu Talib aliwasilisha uamuzi wake kwa Bani Hashim na Bani al-Muttalib na akaongea nao kuhusu mpwa wake kwa mvuto mkubwa sana na kuzingatia kwa undani utukufu wa cheo cha Muhammad.

Aliwataka wote kumlinda Muhammad dhidi ya Maquraishi. Wote waliahidi kufanya hivyo isipokuwa Abu Lahab aliyetamka wazi uadui wake kwake na kujitoa kwake kwenda kambi ya upinzani.
“…Maquraish waliwasababishia maswahaba wa Muhammad kila aina ya madhara ambayo kutokana nayo aliokolewa tu kupitia ulinzi wa Abu Talib, Bani Hashim, na Bani al-Muttalib.” (The Life of Muhammad)

Kukwamishwa na kuzuiwa kwa kurudiwa rudiwa kwa namna hii na Abu Talib, uvumilivu wa waabadu masanamu ulifikia mahali pa kuvunjika. Baada ya kushindwa kwa ubalozi wao wa mara ya tatu kwa Abu Talib, waliamua kutupia ukatishwaji tamaa wote na hasira walizoficha mioyoni juu ya wale Waislamu wasiokuwa na ulinzi. Walitumaini kuivunja ile dini mpya kwa vitisho na ukatili.

Waathirika wa kwanza wa msuguano na ushari wa wapagani walikuwa ni wale Waislamu wasiokuwa na ushirikishwaji wa kikabila hapo Makka. Yasir na mke wake, Sumayya, na mtoto wao, Ammar, hawakuwa na ushirikishwaji wa kikabila. Hapo Makka walikuwa ni “wageni” na hapakuwa na wa kuwalinda.

Wote watatu waliteswa kikatili sana na Abu Jahl na makafiri wengine. Sumayya, mkewe Yasir, alikufa wakati akiwa anateswa. Yeye kwa hiyo akawa Shahidi wa Kwanza katika Uislamu. Baadae kidogo, mumewe, Yasir, aliteswa pia hadi kufa, naye akawa Shahidi wa Pili katika Uislamu.

Maquraishi walichafua mikono yao kwa damu isiyokuwa na hatia! Katika orodha ya mashahidi, Sumayya na mume wake Yasir, wanashika nafasi miongoni mwa wale wa juu kabisa.Waliuawa bila ya sababu yoyote mbali na kumcha kwao Mungu na mapenzi yao kwa Uislamu na Muhammad Mustafa. Wale Waislamu waliouawa kwenye vita vya Badr na Uhud, walikuwa na jeshi la kuwalinda na kuwasaidia.

Lakini Yasir na mke wake hawakuwa na mtu yoyote wa kuwalinda; hawakuwa wameshika silaha yoyote, na walikuwa ndio wasiokuwa na ulinzi kabisa kati ya mashahidi wote wa Kiislamu. Kwa kujitolea mhanga maisha yao, walidhihirisha ukweli wa Uislamu, na walitia nguvu katika muundo wake. Waliifanya desturi ya muhanga na kufa kishahidi kuwa sehemu muhimu ya maadili ya Uislamu.

Bilal, Khabab ibn el-Arat, Suhaib Rumi, na Waislamu wengine masikini na wasio na ulinzi walifanywa wasimame kwenye jua kali, na wakapigwa viboko na makafiri. Walinyimwa chakula na maji kwa matumaini matupu kwamba njaa na kiu vitawalazimisha kumtupa Muhammad na Uislamu.

Pale Maquraish walipomuona Muhammad peke yake, waliichukua fursa hiyo kumuudhi yeye. Wao kwa kweli walipenda kumuua lakini walilazimika kuizuia tamaa hii. Kama wangemuua, wangesababisha kisasi au hata vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati mmoja, Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.) aliingia kwenye Al-Kaaba kusoma Qur’an Tukufu. Alikuwa anasoma Qur’an wakati ghafla alipozungukwa na waabudu sanamu. Walimsongasonga, na wangeweza kumfanyia madhara makubwa lakini walishindwa kwa kuingiliwa kati na Harith ibn Abi Hala, mpwa na mtoto wa kulea wa Khadija, aliyebahatika kutokea kwenye tukio hilo wakati huohuo. Alijitosa kwenye ghasia hiyo kumuokoa Mtume wa Allah (s.a.w.) kutokana na vurugu hizo za washirikina wa Makka.

Harith ibn Abi Hala aliwapiga mateke na kupigana kwa ngumi zake. Inawezekana kabisa, yeye pia alikuwa amebeba upanga kama Waarabu wote walivyofanya lakini hakutaka kuutoa, na kusababisha umwagaji damu ndani ya maeneo ya Al-Kaaba. Lakini katika tafrani hiyo, mmoja wa waabudu masanamu hao aliuchomoa upanga wake, na kumchoma kwa kurudiarudia.

Alianguka kwenye dimbwi la damu yake mwenyewe, na akafa kwa majeraha mengi katika kifua chake, mabega na paji la uso. Alikuwa Mwislamu wa kwanza kuawa ndani ya maeneo ya Al-Kaaba. Harith alikuwa kijana wa miaka kumi na saba, na aliyafanya maisha yake kuwa dhabihu kwa ajili ya Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.). Alikuwa ndiye muathirika kijana mdogo wa vurugu zenye kuzunguka na kuongezeka za makafiri. Alijipatia taji la kufa kishahidi na kuwa Shahidi wa tatu katika Uislamu. Kifo chake, mapema sana katika uhai wake, kilimfanya Mtume (s.a.w.) kuwa mwenye huzuni sana.

Wanahistoria wa Kiarabu wako kimya kuhusu suala hili lakini mapigano mabaya zaidi lazima yawe yalitokea ndani ya Makka kati ya Waislamu na waabudu masanamu katika miaka ya kabla ya kuhama kwa Mtume (s.a.w.) kwenda Madina. Abu Talib alimlinda mpwa wake wakati wote alipokuwa hai. Baada ya kifo chake, wajibu huu ulirithiwa na mwanae, Ali.

Ali alikuwa bado ni kijana wakati alipojiteua mwenyewe kuwa mlinzi wa Muhammad, Mtume wa Allah (s.a.w.). Baada ya mauaji yale, ndani ya Al-Kaaba, ya Harith ibn Abi Hala, Ali alifuatana na bwana wake wakati wowote alipotoka nje ya nyumba yake, na alisimama kati yake na maadui zake. Kama mtu mshari alimwendea Muhammad kwa kumkamia, Ali mara moja alimpa changamoto, na akapambana naye.

D.S.Margoliouth:

“Wale watu ambao kuingia kwao katika Uislamu kulikaribishwa sana walikuwa watu wenye nguvu za kimwili, na upiganaji mwingi wa dhati lazima uwe ulitokea hapo Makka kabla ya Hijra; vinginevyo ile hali ya kuwa tayari ambayo kwayo Waislam baada ya Hijra waliweza kuonyesha kutokana na idadi yao ya mashujaa waliojaribiwa, ingekuwa isiyoelezeka. Shujaa aliyejaribiwa lazima awe amejaribiwa mahali fulani; na hakuna mapigano ya nje yaliyotajwa au ambayo angalau ni jambo la dokezo kwa wakati huu.”(Muhammad and the Rise of Islamu, London, 1931)

Hakukuwa na mapigano ya nje hapo Makka kabla ya Hijra ya Mtume (s.a.w.) kwenda Madina, lakini kulikuwa na mapigano mengi sana mitaani na kwenye sehemu za wazi za mji huo. Ilikuwa ni katika “viwanja vya vita” hivi ambavyo Ali, yule simba kijana, alimopata umahiri wote huu wa kivita. Haya “mapigano” hapo Makka yalikuwa ni “mazoezi ya mwisho” ya dhima aliyotakiwa kuchukua miaka michache baadae huko Madina katika mapambano ya silaha kati ya Uislamu na upagani.

Ilikuwa pia katika siku hizi za mwanzoni, kabla ya Hijra ya Mtume (s.a.w.) kwenda Madina, ambayo Ali alikuwa “msitari wa kwanza wa ulinzi wa Uislamu.” Kwa kweli, alikuwa pia, kwa wakati huohuo, msitari wa pili na wa mwisho wa ulinzi wa Uislamu. Hili yeye, na yeye peke yake, lilikuwa lidumu kwa maisha yake yote yaliyobakia.

Maquraish waliitesa miili ya Waislamu wasiokuwa na ulinzi huko Makka kwa matumaini kwamba watawalazimisha kuuacha Uislamu, lakini walishindwa. Hakuna hata mmoja kati ya hawa Waislamu “masikini na wanyonge” aliyeukana Uislamu kamwe.

Mazingira mabaya yanaweza kushirikiana kumvunja hata yule mtu mwenye nguvu sana, na kwa Waislamu, mazingira hayo hayakuweza kuwa mabaya zaidi. Lakini mazingira yale hayakuweza kuwavunja. Uislamu uliwaweka pamoja.

Kwa hawa Waislamu “masikini na wanyonge”, Uislamu ulikuwa ni desturi “inayotia nguvu”. Umeyavuta maisha pamoja kwa ajili yao; umeyawekea maana ndani yake, umeyaendesha malengo kupitia humo, na umeweka upeo pande zote. Wao, kwa hiyo, walitupilia mbali usalama, starehe na anasa za maisha; na baadhi miongoni mwao kama Sumayya na mume wake, Yasir, waliyapuuzilia mbali maisha yenyewe; lakini walithibitisha Imani yao. Walikufa lakini hawakuafikiana na Upotofu.

Allah (s.w.t.) awe radhi na nafsi hizi za kishujaa na tukufu na azirehemu. Imani na uadili- fu wao vilikuwa, kama Maquraishi walivyogundua, visivyoshindika kwa kiasi kama isivyoshindika imani na uadilifu wa bwana na kiongozi wao, Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.w.t.) Walikuwa ni almasi ambazo Muhammad alizipata kwenye mawe ya dunia. Walikuwa wachache kwa idadi lakini wasio na bei kwa tathmini; ya kuweza kuelezeka, sio kwa wingi bali kwa ubora tu, na ubora huo ulikuwa adhimu sana.