Table of Contents

Usawa

Baada ya kutokea vuguvugu la mapinduzi lililosababisha kuuawa Uthman, makundi kwa makundi ya watu wakakusanyika na kumbai Ali (AS) kuwa ni khalifa wao.

Siku ya pili yake baada ya kubaiiwa, Ali (AS) akapanda juu ya mimbari. Akaanza kutoa mawaidha yake kwa kumtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu, na akamwombea baraka na rehema Mtume wa Mwisho, Muhammad (SAW). Kisha akaendelea kwa kusema haya:

"Enyi watu! Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu kufariki dunia, watu wakamchagua Abu Bakr kuwa ni khalifa. Na Abu Bakr akamchagua Umar kuwa ni mrithi wake. Umar akaunda baraza la ushauri (shura) alilolipa jukumu la kumteua khalifa, na matokeo yake ni kuteuliwa Uthman kuwa ni khalifa. Matendo ya Uthman yakakufanyeni mpinge hadi kwamba nyumba yake ikazingirwa na mwisho akauawa. Kisha nyinyi mkaja kwangu na mkanibai mimi kwa matakwa na mapenzi yenu wenyewe. Mimi ni mtu ninayetokana nanyi na ni sawa nanyi. Yale yaliyo kwa ajili yenu ni kwa ajili yangu pia. Jukumu lenu ni jukumu langu pia. Jukumu Ia ukhalifa linaweza kuchukuliwa na mtu ambaye ana kipawa, subira, busara na elimu pia. Mwendo wangu ni kukurejesheni katika mwendo na sunna za Mtume Mtukufu. Kila ahadi nitakayoitoa nitaitekeleza, kwa sharti kwamba nyinyi mtakuwa imara na mtavumilia. Hapana shaka kwamba ni lazima tutake msaada wa Mwenyezi Mungu. Jueni kwamba msimamo wangu juu ya Mtume baada ya kufariki kwake ni vilevile kama ulivyokuwa wakati wa uhai wake.

"Ni lazima nyinyi muwe na nidhamu na muwe watiifu. Tekelezeni kila ninalosema. Kama kuna jambo ambalo mnaona ni la kushangaza kwenu na haliwezi kukubalika, msifanye haraka kulikataa. Mimi sichukui hatua yoyote juu ya jambo lolote lile mpaka nijue kwamba ninafanya kwa kutekeleza wajibu wangu na sina udhuru wowote mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mwenye kuona anatuona sisi sote na ana uwezo juu ya kila kitu."

"Hapana shaka mimi sina hamu ya kushika hatamu ya ukhalifa, kwa sababu nimemsikia Mtume Mtukufu (SAW) akisema: 'Yeyote atakayechukua uongozi wa Umma baada yangu, Siku ya Kiyama atasimamishwa kwenye sirati (njia) na malaika watamfungulia waraka wa amali zake. Kama alikuwa mwadilifu, Mwenyezi Mungu atamwokoa kutokana na uadilifu huo; na kama alikuwa dhalimu, sirati itayumbayumba, minyororo yake itafunguka na ataanguka katika Jahannamu.'"

"Ilivyokuwa nyinyi nyote mmekubaliana kunichagua mimi kuwa ni khalifa, hivyo, hayumkiniki kukataa."

Kisha Ali (AS) akawatazama watu upande wa kulia na upande wa kushoto wa mimbari, na akaendelea na hotuba yake:

"Enyi watu! Mimi sasa ninatangaza kwamba wale waliojaza mifuko yao kutoka katika mifuko ya watu na Baitul MaaI, na wakakusanya mali kwa wingi, na wakajichimbia mifereji, na wakapanda farasi wazuriwazuri, na wakajinunulia vijakazi warembo, na wakazama katika starehe za dunia, basi wajue kwamba kesho nitakapowazuia na kuwanyang'anya yale waliyochuma kwa njia isiyo ya halali na kuwabakishia kiasi cha haki zao - si zaidi - wasije wakasema: 'Ali bin Abu Talib ametudanganya!' Mimi leo ninasema waziwazi kwamba nitaondoa marupurupu yote (yasiyo ya haki), na hata ubora wa kuwa sahaba wa Mtume na uzoefu wa kuuhudumia Uislamu. Yeyote aliyebahatika kuwa sahaba wa Mtume na akafanikiwa kuuhudumia Uislamu, thawabu na malipo yake atayapata kwa Mwenyezi Mungu. Uzoefu huo wa usahaba na huduma hautatufanya leo tuwabague na wengine. Leo mtu yeyote atakayeitikia mwito wa haki na akaingia katika dini yetu na akaelekea kwenye kibla yetu, basi sisi tutamfadhili sawa na Waislamu wa mwanzo. Nyinyi ni waja wa Mwenyezi Mungu na mali zote ni za Mwenyezi Mungu, hivyo, ni lazima zigawanywe kati yenu kwa usawa. Hakuna mtu aliye bora kuliko mwingine. Kesho nyote mhudhurie kwani kuna mali katika Baitul Maal (Idara ya Hazina) ambazo ni lazima zigawanywe."

Siku ya pili, Waislamu wakaja na Ali pia akaja na akagawanya sawasawa mali zote zilizokuwepo katika Baitul Maal. Kila mtu akampa dinari tatu. Mtu mmoja akasema:

"Ewe Ali! Unanipa mimi dinari tatu na unampa mtumishi wangu ambaye mpaka jana alikuwa mtumwa wangu dinari tatu?"

Ali akasema:
"Ndiyo kama hivyo unavyoona."

Baadhi ya watu ambao kwa miaka mingi iliyopita walizoea kupendelewa na kufadhilishwa kuliko wengine, kama akina Talha, Zubayr, Abdullah bin Umar, Said bin 'Aas na Marwan Hakam, siku hiyo walikataa kupokea sehemu yao na wakatoka msikitini.

Siku ya pili wakati Waislamu walipokusanyika msikitini, watu hao wakaja pia lakini wakakaa pembeni mbali na jamii na wakaanza kunong'onezana. Baada ya muda kidogo, wakamchagua Walid bin 'Uqba kwenda kwa Ali.

Walid akamwendea Ali (AS) na akamwambia: "Ewe Abul Hasan! Kwanza wewe unajua vyema kwamba hakuna yeyote kati yetu aliyekaa pale anakupenda kwa sababu ya kuhusika kwako katika vita baina ya Uislamu na Ujahilia. Karibu kila mmoja kati yetu ana mtu mmoja au wawili ambao wameuawa kwa mkono wako katika vita hivyo. Wewe umemwua babangu katika vita vya Badr. Lakini kuhusiana na suala hili, sisi tunaweza kukusamehe na kukuunga mkono kwa masharti mawili ikiwa utayakubali. Masharti yenyewe ni haya:

"Kwanza, acha maneno yako uliyoyasema jana. Usishughulikie yaliyopita na usiyataje tena. Kila lililofanywa zamani limekwisha. Wewe usiwe na kazi na yeyote yule ambaye katika zama za makhalifa alipata mali kwa njia yoyote ile. Usijali amepata kwa njia gani. Tazama katika zama zako tu kwamba mali hazifujwi!

"Pili, tukabidhi wauaji wa Uthman ili tulipize kisasi. Ikiwa sisi hatutapata usalama kutoka kwako, itatubidi tukuache na twende Sham kujiunga na Mu'awiyah."

Ali (AS) akasema: "Kuhusu damu zilizomwagwa katika vita baina ya Uislamu na Ujahilia (Ushirikina), mimi sina lawama yoyote, kwa sababu vita hivyo havikuwa vita vya mtu binafsi, bali vilikuwa vita baina ya haki na batili. Kama nyinyi mna madai yoyote, ni lazima kuwe ni batili kuishtakia haki, si mimi. Na kuhusu haki zilizotumiliwa vibaya hapo zamani, mimi nina wajibu wa kisheria kuzirejesha kwa wenyewe.

Sina hiari ya kusamehe au kunyamaza kimya. Kuhusu suala Ia waliomwua Uthman, kama mimi ningeona wajibu wangu wa kisheria, ningelipa kisasi janajana wala nisingewapa muhula hadi leo."

Walid baada ya kusikia majibu hayo akaondoka na kwenda kwa marafiki zake kuwapasha habari. Wao walijua na walikuwa na hakika kwamba siasa ya Ali haiwezi kulainika. Hivyo, tangu saa hiyo wakaanza kuleta fitna na kuwachochea watu.

Kikundi cha wafuasi wa Ali (AS) wakaenda kwake na wakamwambia:

"Karibuni kikundi hiki watayafanya mauaji ya Uthman kuwa ni kisingizio cha kuleta machafuko. Lakini mauaji ya Uthman ni kisingizio tu, kwani kitu kinachowauma hasa ni usawa ulioweka kati yao na Waislamu wapya walio Waajemi na wengineo. Ikiwa wewe utayahifadhi manufaa yao na utabadilisha uamuzi wako, chokochoko zitanyamaza."

Ilivyokuwa iliyumkinika kwamba marafiki wengi wa Ali wangeuliza sababu ya kushikilia kwake ufanywe usawa, hivyo, siku ya pili, Ali (AS) akaenda msikitini akiwa ameshika upanga. Vilevile akavaa nguo ya vipande viwili vya kitambaa cha kawaida. Kimoja akakifunga kiunoni na kingine akaweka mabegani. Akapanda kwenye mimbari akiwa ameshika upinde.

Akawaambia watu haya:

"Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ni Mwabudiwa wetu. Ametuneemesha kwa neema Zake zinazoonekana na zisizoonekana. Neema Zake zote ni hisani na fadhila kwetu bila ya sisi wenyewe kuwa na ustahiki na uhuru. Ametupa neema hizo ili atufanyie mtihani kama tutashukuru au tutakufuru. Mtu bora kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemtii Mwenyezi Mungu kwa vizuri zaidi, anafuata sunna za Mtume Mtukufu kwa vizuri zaidi, na anayeweka kwa uzima zaidi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Sisi hatumthamini mtu mmoja kuliko mwingine katika jambo lolote isipokuwa kwa kadiri ya utiifu wake kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Hiki ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu kilicho mbele yenu na hizo ni sunna na sera dhahiri za Mtume wenu ambazo mnazijua."

Kisha Ali (AS) akasoma aya ifuatayo ya Qur'ani:

"Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke, na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye bora zaidi kati yenu mbele ya Allah ni mwenye kuwa na takwa zaidi katiyenu." (49:13)

Baada ya hotuba hiyo, ikabainika kwa marafiki na maadui kwamba Ali amedhamiria na amekusudia kwelikweli katika uamuzi wake. Kila mtu aliyetaka alielewa wajibu wake. Wale waliokuwa watiifu wakabaki na utiifu wao; na wale walioshindwa kuukubali mpango huo, wakajitenga na kuishi katika upweke kama Abdullah bin Umar, au kama Talha, Zubayr na Marwan ambao wakawa tayari kupigana vita na kumwaga damu za Waislamu.