Ilikuwa Ni Vita Ya Wenyewe Kwa Wenyewe Ya Marekani

Je, Ni Ya Kuwakomboa Watumwa?

Nadhani itakuwa kwa manufaa ya wasomaji kutizama kwa umakini hadithi isemayo kwamba vita ya Marekani ya wenyewe kwa wenyewe ilitokea kwa lengo la kuwakomboa watumwa. Ni ngano ambayo iliyobuniwa na haina uhusiano wowote na hali halisi ya ukweli. Nina nukuu hapa kutoka kwenye sura ya 22 ya “Lincoln, the Unkown” kilichoandikwa na mwandishi wake maarufu Dale Carnegie.1 Anaanza na maneno haya: - “Muulize raia wa kawaida wa Kimarekani leo kwa nini Waamerika walipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, atakacho kuambia ni kwamba, ‘Kuwakomboa watumwa.’ “Ni kweli hivyo?”

“Hebu tuangalie. Hapa ni sentenso ambayo imechukuliwa kutoka kwenye hotuba ya kwanza ya Lincoln ya kuzindua urais wake. ‘Sikusudii kuingilia kati, taasisi ya utumwa, moja kwa moja au kuzunguuka kwenye majimbo ambayo utumwa bado upo. Nina amini sina haki ya kisheria kufanya hivyo, na sipendelei kufanya hivyo.”

Ukweli ni kwamba mzinga ulikuwa unanguruma na majeruhi wanatoa sauti ya kulemewa kwa takribani miezi kumi na nane kabla Lincoln hajatoa tangazo la “Ukombozi wa watumwa.”
Wakati wote huo watu wenye msimamo Mkali na Watetezi wa kukomesha utumwa walimsihi achukue hatua haraka, walimshambulia kupitia kwenye magazeti na kumshutumu kwenye majukwaa ya mikutano.

“Wakati mmoja ujumbe wa mawaziri wa Chicago ulikwenda Ikulu ya Marekani na kile walichokitangaza kwamba ilikuwa ni amri ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu Mweza wa Yote kuwaachia watumwa kuwa huru haraka sana. Lincoln aliwaambia kwamba alidhani kwamba kama Mweza wa Yote alikuwa na ushauri wowote wa kutoa, Angekuja moja kwa moja makao makuu na ushauri huo, badala ya kuwasilisha kwa mzunguuko wa kupitia Chicago.”

Zaidi ya hayo, Dale Carnegic anaendelea kunukuu kutoka kwenye jibu la Lincoln alipojibu makala ya Greedy, ‘The Prayer of Twenty million.’(‘Sala ya milioni ishirini).

“Kusudio langu kubwa katika mapambano haya ni kuokoa Muungano, na wala si kuokoa au kukomesha utumwa. Kama ningeokoa Muungano bila kumpa uhuru mtumwa hata mmoja, ningefanya hivyo; na kama ningeokoa Muungano kwa kuwapa uhuru wa watumwa wote ningefanya hivyo, na kama ningeuokoa Mungano kwa kuwapa uhuru baadhi yao na kuwaacha wengine, pia ningefanya hivyo.

Ninachofanya kuhusu watumwa na machotara, ninafanya hivyo kwa sababu ninaamini inasaidia kuokoa Muungano, na kile ninachovumilia, ninavumilia kwa sababu siamini kama ingesaidia kuokoa Muungano. Sitafanya yote wakati wowote nitakapoamini kile ninachokifanya kitadhu- ru lengo; na nitazidisha juhudi nitakapoamini kufanya hivyo itasaidia lengo.”

Akifafanua jibu hilo Dale Carngie anaandika: “Majimbo manne yamebakia na watumwa pamoja na Kaskazini, na Lincoln alitambua kwamba kama angetoa tangazo la “ukombozi wa watumwa” mapema mno katika mzozo huu, angewafukuzia kwenye Shirikisho, kuimarisha kusini, na pengine kuvunja Muungano daima milele. Palikuwepo na methali wakati huo ambayo Lincholn angependa kuwa na Mungu Mweza wa Yote upande wake, lakini lazima aipate Kentucky.

“Hivyo alisubiri wakati mzuri, na kufanya mambo kwa tahadhari”

“Lincoln mwenyewe alioa kwenye familia yenye kumiliki watumwa, ya Jimbo la mpakani. Sehemu fulani ya fedha ambayo mke wake Lincoln alipokea ilitoka kwenye urithi wa shamba la baba yake ambayo ilitokana na mauzo ya watumwa. Na rafiki mmoja tu wa karibu sana na wa kweli ambaye Lincoln alikuwa naye, alikuwa Joshua Speed ambaye alitoka kwenya familia yenye watumwa. Lincoln aliwahurumia watu wa Kusini kwa maoni yao. Kwa upande mwingine, alikuwa na desturi ya kumshehimu mwanasheria Mkuu kuhusu Katiba na sheria na rasilimali. Hakutaka kusababisha shida kwa mtu yeyote. (ila kwa watumwa)

“Lincoln aliamini kwamba majimbo ya kaskazini yalistahili kulaumiwa sana kwa kuendelea kuwepo kwa utumwa “Marekani (U.S.A)” kama ilivyo huko kwenye majimbo ya Kusini; na kwamba kuliondoa tatizo hilo, sehemu zote lazima zivumilie mzigo sawa kwa sawa. Kwa hiyo hatimaye alitengeneza mpango ambao ulikuwa karibu sana na moyo wake. Kwa mujibu wa mpango huo, wamiliki wa watumwa waliokuwa kwenye mipaka ya majimbo yenye uaminifu walipewa dola mia nne kwa kila Mtu Mweusi. Watumwa walitakiwa kuachiwa huru polepole, polepole sana.

Mlolongo wa mambo haya haukutakiwa kumalizika kikamilifu hadi Januari 1, 1900. Lincoln aliwaita wawakilishi kutoka kwenye Majimbo ya mipaka wamuone huko Ikulu White House, akawasihi wakubali pendekezo lake.

“Lincoln alihoji na kusema, mabadiliko yaliyomo kwenye pendekezo lake, yanakusudiwa kuja polepole kama umande unavyo dondoka kutoka mbinguni, bila kupokonya au kuvunja matarajio ya watu. Kwa nini msikubali pendekezo hili? Mambo mengi sana mazuri bado hayajafanyika kwa jitihada moja, katika wakati wote uliopita, kama ilivyo katika upaji wa Mungu sasa hivi ni upendeleo wenu wa juu kutekeleza. Muda mwingi ujao na upana wake usije ukalalamika kwamba ulipuuzia jambo hili.”

Msomaji angekumbuka kwamba mpango huu wa kuwapa watumwa uhuru “kwamba ulikuwa karibu mno na moyo wake Lincoln” ulikuwa sawa na mpango ambao tayari ulik- wisha wekwa na kutekelezwa miaka 1300 iliyopita katika Uislam na ambao ulitoa matokeo ya kushangaza katika ulimwengu wa Kiisilamu. Kama mpango huo ungekubaliwa na ndugu zake Lincoln, hapange kuwepo na chuki kubwa baina ya mataifa, migongano ya ndani, mageuzi ya kijamii na udhaifu wa hisia ambao bado unaendelea kuwepo nchini Marekani (U.S.A.) karne moja baada ya kile kilichoitwa Ukombozi wa watu weusi (Emancipation of Negroes).

Bahati mbaya, wawakilishi wa Majimbo hayo yaliyokuwa yanapakana walikataa mpango huo. Carnegie anasema, “Lincoln mara moja alikasirika sana. Lazima niiokoe serikali hii, kama inawezekana, alisema na inaweza ikaeleweka, kwa mara zote, kwamba sitakubali kuacha mchezo huu, na kuacha kadi yoyote ile ipatikanayo iwe haijachezwa….Ninaamini kwamba kuwapa uhuru watumwa na kuwapa silaha watu weusi sasa imekuwa jambo la msingi na muhimu kivita. Nimesukumwa kwenye uchaguzi ama kutekeleza hilo au kuuwachia) Muungano (usambaratike).

“Ilibidi Lincoln ashughulike haraka, kwani Ufaransa na Uingereza walibakia kidogo watambue Shirikisho. Kwanini? Sababu zilikuwa rahisi. Tuchukue mfano wa Ufaransa kwanza.”

Napoleon wa III alikuwa mfalme wa Ufaransa. Alikuwa na shauku kubwa ya kutaka utukufu wa mamlaka ya utawala, kama alivyokuwa ami yake mtukufu, Napoleon Bonaparte, alivyo fanya. Kwa hiyo, alipoona majimbo yanapigana, na alitambua kwamba walikuwa na shughuli nyingi mno kuweza kufikiria kuhusu utekelezaji wa sheria ya “Momoe Doctrine,” aliamuru jeshi kwenda Mexico, huko likaua wazalendo elfu kadhaa, likashinda nchi, ikaitwa Mexico iliyo chini ya himaya ya Ufaransa, na likamweka Archduke Maximilian kukalia kiti cha enzi.

“Napoleon aliamini na si bila sababu, kwamba kama kundi linalotaka shirikisho lingeshinda, lingependelea ufalme wake mpya; lakini kama kundi linalotaka shirikisho lingeshinda, United States ingechukua hatua za haraka za kuifukuza Ufaransa huko Mexico. Kwa hiyo, ulikuwa ni upendeleo wake Napoleon, kwamba Kusini ifaulu kujitenga, na alitaka kuisaidia kutekeleza kujitenga huko kwa kadiri ya uwezo wake.

Mwanzoni mwa vita, jeshi la majini la Kaskazini lilifunga bandari zote za Kusini, bandari 189 zikawa chini ya ulinzi wao na walifanya doria kwenye eneo la maili 9,614 za uwanda wa pwani, njia nyembamba za maji zinazounganisha bahari na zinazounganisha bahari na maziwa, vinamasi na mito. Hiki kilikuwa kizuizi kikubwa mno ambacho ulimwengu haujapata kuona. Kundi lililotaka Muungano lilikuwa lina haha.

Halikuweza kuuza pamba yake, wala kuweza kununua bunduki, risasi, viatu, madawa au chakula. Watu hawa walianza kuchemsha karanga na mbegu za pamba kuwa mbadala wa kahawa, na walianza kuchemsha majani ya miti ya matunda mithili ya mibuni na kuchuja maji yake na kuwa mbadala chai. Magazeti yalianza kuchapishwa kuwekwa kwenye matangazo. Nyumba zenye sakafu za udongo na zenye kufuka moshi, zililoweshwa dabwa dabwa kwa mafuta ya wanyama, zikachimbuliwa na kuchemshwa ili kupata chumvi.

Kengele za makanisa ziliyeyushwa na kutiwa katika mizinga. Reli za magari madogo mitaani katika mji wa Richmond zilikatwa katwa na kufanywa silaha katika mashua za kivita zenye bunduki.

Watu wa Muungano hawakuweza kuzifanyia matengenezo reli zao au kununua vifaa vipya, kwa hiyo usafiri ulibakia kidogo sana; nafaka ambayo ilinunuliwa kwa dola mbili, pishi tisa huko Geogia, ilinunuliwa kwa dola kumi na tano Richmond. Watu waishio Virgini walikuwa wanashinda na njaa.

Ilibidi utaratibu fulani ufanywe haraka sana. Kwa hiyo, Kusini walikubali kumpa Napoleon wa III dola milioni 12 kama angeutambua Muungano na atumie meli za Kifaransa kuondoa kizuizi. Kwa upande mwingine, waliahidi kumzidishia nguvu kwa amri ambayo ingeanzisha moshi kwenye kila kiwanda huko Ufaransa usiku na mchana.

Kwa hiyo Napoleon akazisihi Urusi na Uingereza kuungana naye katika kuutambua Muungano. Utawala wa makabaila uliokuwa madarakani, wahusika wake waliweka sawa miwani zao, wakanywa toti kadhaa za Scotch Whisky, na wakasikiliza kwa hamu kubwa mazungumzo ya awali ya Napoleon. Marekani (U.S.A.) ilianza kutajirika sana na kuwa na uwezo mkubwa wa kuwaridhisha, Walitaka kuona taifa linagawanyika, Muungano unavunjika. Kwa upande mwingine, walitaka pamba ya Kusini. Viwanda kadhaa vya Uingereza vilifungwa, na watu milioni moja hawakuwa tu hawana kazi, bali pia kuwa fukara na kushuka chini kuwa omba omba halisi.

Watoto walikuwa wanalia njaa, mamia ya watu walikuwa wanakufa kwa sababu ya njaa. Michango ya raia kwa ajili ya kununua chakula cha wafanya kazi wa Uingereza ilichukuliwa na kupelekwa kwenye vijiji vya ndani kabisa ya dunia hata India ilioko mbali sana na China ambayo ilibanwa na umasikini. Palikuwepo na njia moja, na njia moja tu, kwamba Uingereza ingeweza kupata pamba na hiyo ilimaanisha waungane na Napoleon III katika kuutambua Muungano na kuondoa kizuizi.

“Kama hilo lingefanyika, nini kingetokea Marekani? Kusini wangepata bunduki, baruti, mkopo, chakula vifaa vya njia ya reli, na msaada mkubwa sana wa hali na mali.

“Na Kaskazini wangepata nini? Wangepata maadui wawili wapya na wenye nguvu. Hali hiyo kuwa mbaya kiasi hicho sasa, hapangekuwepo na matumaini.

“Hakuna aliyejua hilo vizuri zaidi kumzidi Abraham Lincoln. “Ni kama vile tumecheza kadi yetu ya mwisho’, aliungama hivyo katika mwaka 1892. Ama lazima tubadili mbinu zetu au tukubali kushindwa mchezo.’

Kama ilivyoona Uingereza, makoloni yote yalikwisha jitoa kutoka kwenye utawala wake tangu mwanzo. Sasa makoloni ya Kusini nayo yamekwishajitoa kutoka makoloni ya Kaskazini; na Kaskazini ilikuwa inapigana kuilazimisha na kuitiisha Kusini. Je, pangekuwa na tofauti gani kwa mtu wa kawaida huko London au mwana mfalme huko Paris kama Tenessee na Texas zingetawaliwa kutoka Washington au Richmond? Hakuna. Kwao vita haikuwa na maana yoyote na yenye kuleta hatari bila madhumuni ya maana.

‘Nilikuwa sijapata kuona vita imepamba moto kama hiyo katika uhai wangu’, aliandika Carlyle, ‘iliyokuwa inaonekana zaidi kama ya kipumbavu.

Lincoln aliona kwamba msimamo wa Ulaya kuhusu vita hiyo lazima ubadilike, na alijua jinsi ya kufanya. Watu milioni moja huko Ulaya walikwisha soma “Uncle Toms Cabin” walikisoma kisa hicho na wakalia na wakajifunza kuchukia michomo ya moyo na udhalimu wa utumwa. Kwa hiyo Abraham Lincoln alitambua kwamba kama angetoa tangazo lake la “ukombozi wa watumwa”, watu wa Ulaya wangeiona vita kwa namna tofauti. Haingekuwa tena ugomvi wa kumwaga damu kwa sababu ya kudumisha Muungano ambao haukuwa na maana yoyote kwao. Badala yake, ingetukuzwa kuwa vita takatifu ya kutokomeza utumwa. Serikali za Ulaya hazingeitambua Kusini. Maoni ya watu hayangestahamili kuwasaidia watu ambao wanapi- gana kwa lengo la kuendeleza utumwa wa kibinadamu.

Hatimaye, kwa hiyo, mnamo Julai, 1862, Lincoln akiwa amedhamiria kutoa tangazo lake, lakini McClellan na Papa mnamo siku chache za nyuma waliliongoza jeshi la Kusini kwenye fedheha ya kushindwa mara kadhaa. Seward alimwambia Rais kwamba muda huo haukuwa mwafaka, hivyo angelazimika kungoja na kutoa tangazo kwenye kilele cha ushindi wao.

“Ushauri huo ulionekana wa hekima. Kwa hiyo Lincoln akangojea na miezi miwili baadaye ushindi ukapatikana.”

Na kwa hiyo, kuendeleza Vita ya Muungano, tangazo la “Ukombozi wa Watumwa” lilichapishwa mnamo Septemba 1862, ambalo lilitakiwa lianze kutekelezwa tarehe Moja, Januari 1863.

Ninampa Abraham Lincoln heshima ya juu sana na amekuwa mmoja wapo wa mashujaa ninao wapenda tangu nilipokuwa mdogo. Lakini heshima hiyo msingi wake ni kwenye ukweli na hali halisi, si kwenye mambo ya kubuniwa. Lincoln alikuwa na ubinadamuna, na yeye, kutoka ndani ya moyo wake alikuwa dhidi ya utumwa. Lakini haina maana kwamba tumtukuze kwa propaganda za uwongo. Uhalisi wa jambo hili ni kwamba hakupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kuwapa watumwa uhuru, kwa usahihi zaidi aliwapa watumwa uhuru kwa lengo la kushinda vita na kuokoa Muungano.

  • 1. Carnegie, Dale, Lincoln: The Unknwown (Surrey, U.K.: The World Work Ltd. 1948) Sura ya 22