Ukristo Na Utumwa

Ingawaje utumwa ulikuwa taasisi ya kale ambayo ilianza kabla ya historia ya binadamu haijaanza kuandikwa, ni salama kusema kwamba ukubwa wa biashara hii ulifika kilele chake kwa kuendelezwa na mataifa ya Kikristo ya Ulaya na Amerika ambao kama ilivyo kawaida yao, waliigeuza kuwa biashara yenye utaratibu uliopangwa kwa uangalifu sana na wakaanza kuwakamata watumwa kwa maelfu. Kabla hatujaanza kutoa maelezo ya biashara hii mbaya sana ya utumwa ambayo ilianzishwa na Wareno, Wahispania na mamlaka zingine za kiubaharia za Kikristo kutoka Magharibi kwa ajili ya makoloni yao mapya, hebu tuangalie kwanza tuone kama Ukristo, kama mfumo na imani, ulifanya lolote wakati wa siku za mwanzo sana kupunguza ukali wa mateso kwa wengi wa watumwa. Jaji Ameer Ali anaandika kuhusu Ukristo:

Ukristo uliona utumwa kuwa ni taasisi iliyo tambuliwa na himaya (dola); na wenyewe ukakubali mfumo huu bila ya hata kujaribu kupunguza uovu wake, au kuahidi kukomesha polepole, au kuboresha hadhi ya watumwa.

Chini ya sheria ya nchi, watumwa walikuwa kama mali inayo hamishika. Waliendelea kuwa hivyo chini ya utawala wa Kikristo.

Utumwa ulishamiri miongoni mwa Warumi tangu zama za kale. Watumwa hao ama wamezaliwa wazalendo au wamezaliwa kutoka nje, ama walipatikana kutokana na ushindi wa vita au kununuliwa, walijulikana kama mali tu ya kuhamishika. Mabwana zao walikuwa na mamlaka na uwezo wa kuamua juu ya uhai au kifo kwao. Ukristo ulishindwa kabisa kukomesha utumwa au kupunguza uovu wake.1

Will Durant anatoa maelezo kuhusu nafasi ya Kanisa kama ifuatavyo. Kanisa halikulaani utumwa. Kanisa la Orthodox na waasi, Kanisa la Rumi na washenzi wote walidhani taasisi hii ilikuwa ya kawaida na haingeharibiwa. Sheria za kipagani zilimwingiza utumwani mwanamke yeyote aliye huru ambaye aliolewa na mtumwa; sheria za Mfalme Constantine (Mfalme Mkristo) ziliamuru mwanamke wa aina hiyo kuuawa kwa kukatwa kichwa, na mtumwa mwanamume kuchomwa moto akiwa bado yu hai.

Mfalme Gratian alitoa amri kwamba mtumwa yeyote aliye mshitaki bwana wake kuhusu kosa lolote isipokuwa uhaini dhidi ya serikali, lazima achomwe moto akiwa bado yu hai mara moja bila hata kufanya uchunguzi ili kupata uhalali wa shitaka.2

Rekebisho moja tu lililoagizwa na Ukristo linaonekana katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa mtu fulani aitwaye Filemoni alipomrudisha mtumwa wake, aliyeitwa Onesimo, na kupendekeza amfanyie wema. Hakuna zaidi ya hapo. Inavutia kuona kwamba neno “slave” (“mtumwa”) la asili ya lugha ya Kiebrania limebadilishwa na kuwa “mtumishi wa nyumbani” kwenye toleo la Biblia liitwalo “Authorised Version of the Bible,” na likabadilishwa kuwa “mtumwa mtumishi” katika toleo liitwalo “Revised Standard Version,” kwa sababu, katika maneno ya “The Concise Bible Commentary,” neno hili (yaani mtumwa) limeachwa kutumiwa kwa sababu ya maana yake.3 Mtu hushanga iwapo mtarjumi anayo haki ya kubadilisha asili ya neno kwa sababu tu ya maana zake au ukumbusho wake?”

Itavutia kuona hapa kwamba neno “slave” (“mtumwa”) ni la asili ya Wazungu. Lilianza kuwapo na kutumika wakati Wajerumani (Franks) walipokuwa wanajishughulisha na kulipatia “Washenzi” soko la watumwa la Wahispania, na mateka hao walio wengi walikuwa Waturuki kutoka jimbo la Slovakia (sasa ni sehemu ya Czecoslovakia).

Watu hawa huitwa “Slav” na kwa hiyo mateka wote wakaitwa “slaves.”

Nukuu ifuatayo inaonyesha dhahiri mtazamo wa Uislamu na Ukristo kuhusu suala la utumwa na rangi ya ngozi: “Mwondoshe mtu mweusi! Siwezi kuzungumza naye,” alisema Archbishop Mkristo aliyeitwa Cyrus wakati Waarabu walioshinda walipowatuma wawakilishi wao wenye uwezo mkubwa ili wazungumze kuhusu makubaliano ya kusalimu amri mji mkuu wa Misri, ujumbe huu wa wawakilishi hawa uliongozwa na mtu mweusi aliyeitwa Ubaydah kama mtu mwenye uwezo mkubwa sana kuliko wote. Archbishop, alishangaa alipoambiwa kwamba mtu huyo mweusi alipewa ukubwa na maelekezo na Generali Amr, na kwamba Waislamu huwapa watu weusi na weupe heshima na daraja sawa na huwahukumia watu kwa tabia na si kwa rangi.4

Tukio hili linakupa tu maelezo kwa ufupi kile ninachotaka kueleza kwa urefu zaidi katika kitabu hiki.

  • 1. Ameer Ali, op. cit., uk. 260-261
  • 2. leeky, W.E. History of European Morals, Juzuu ya II ( New Yolk,
    1926), kama ilivyonukuliwa na Will Durant, op. cit., juzuu ya IV, uik. 77.
  • 3. Clarke, Rev. W. K. L, The Concise Commentary (London: S.P.C.K,
    1952) uk. 976.
  • 4. Leeder, S.S., Veild Mysteries, of Egypt (London, 1912), Uk. 332.