read

11) Ubinadamu

Allah Mwenye Busara anasema:

وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ {9}

“…Na wanawapendelea (Muhajirina) kuliko nafsi zao ingawa wao wenyewe ni wahitaji…” (Quran 59:9)

Mtukufu Mtume anasema: “Mtu ambaye atatamani kitu, (lakini) akaizima tamaa yake na akawapa wengine upendeleo kuliko yeye mwenyewe, dhambi zake zitasamehewa.”1

Maelezo Mafupi:

Daraja ya juu zaidi ya ukarimu ni ubinadamu. Mtu muungwana, licha ya kuwa na haja na mahitaji makubwa, hujitolea muhanga kwa kuwapa wengine upendeleo kuliko yeye mwenyewe.

Hata kitendo cha kutoa sadaka huwa na daraja ya chini kuliko ubinadamu. Kupata radhi ya Allah kunahitaji kutekeleza wajibu mkubwa ndani yake. Kama mtu, akiwa katika juhudi ya kuokoa maisha ya mtu anayezama majini, yeye mwenyewe akizama, sifa kutoka kwa Allah kwa kujitoa kwake muhanga, ni mara elfu zaidi kuliko sadaka ambazo huzitoa.

1. Mtumwa Muungwana

Abdullah Ibn Ja’far, mume wa Bibi Zainab (as) alikuwa ni mtu ambaye ukarimu wake hauna kifani. Siku moja, alitokea kupita kwenye shamba la mitende, alimuona mtumwa anafanya kazi pale. Wakati ule ule, chakula cha mtumwa yule kililetwa na akakabidhiwa. Alipokuwa anataka kula chakula chake, mbwa mwenye njaa alikuja mbele yake akitikisa mkia wake. Mtumwa yule aliweka sehemu ya chakula chake, mara moja mbwa yule akala chakula kile. Yule mtumwa akaweka tena chakula zaidi mbele za mbwa yule na mara moja akakila chakula kile. Hali hii ikaendelea mpaka akawa amekitoa chakula chake chote.

Abdullah, ambaye alikuwa anashuhudia tukio lile, akamuuliza yule mtumwa: “Mgao wako wa chakula ni kiasi gani kwa siku?”

“Ni kiasi ambacho umekiona hivi punde.” Akajibu yule mtumwa.

“Kama ni hivyo, kwa nini basi umempa mbwa upendeleo kuliko wewe mwenyewe?” aliuliza Abdullah.

“Mbwa huyu katoka mbali na alikuwa na njaa na sikuona kwamba ni vema kumfukuza katika hali hiyo ya njaa.” Alijbu yule mtumwa.

“Kitu gani kitakacho kutosheleza leo?”

“Nitaishinda njaa yangu kwa uvumulivu na uimara,” mtumwa yule akaeleza.

Abdullah alipoona ubinadamu ule wa mtumwa na kutokujali maslahi binafsi, alijiwa na mawazo yeye mwenyewe kwamba mtumwa yule yule alikuwa mkarimu sana kuliko yeye mwenyewe. Katika njia ya kumtukuza na kumfidia kwa ajili ya ubinadamu wake, Abdullah alimnunua mtumwa yule na shamba lile kutoka kwa mmiliki wake, akamuacha huru mtumwa yule na mwisho akalizawadia shamba lile lote kwake.2

2. Kadhia Ya Msikiti Wa Merv

Abu Muhammad Azdi anasimulia:

Wakati msikiti wa Merv uliposhika moto, Waislamu wakachukulia kwam- ba hiyo ilikuwa kazi ya Wakiristo na wakalipiza kwa kuzichoma moto nyumba zao.

Wakati mfalme alipojua kitendo hicho, aliamuru wale ambao wamehusika katika kitendo hicho wakamatwe na kuadhibiwa. Aliamrisha kwamba wahalifu lazima wapatiwe moja ya aina tatu ya adhabu – kifo, kukatwa mkono au viboko. Kila adhabu itaandikwa kwenye kipande kidogo cha karatasi ambacho kitawekwa ndani ya sanduku. Kila mhalifu alitakiwa kuokota kipande cha karatasi ndani ya sanduku na atapasika na adhabu iliyoandikwa humo.

Wakati mmoja wa watu hawa alipookota na kusoma karatasi yake, alian- gua kilio kwa sababu adhabu yake ilikuwa ni kifo. Kijana mmoja, ambaye alionekana kuwa na furaha kwa vile ataadhibiwa kwa kuchapwa viboko, alimuuliza yule mtu mwenye huzuni: “Kwa nini umehuzunishwa na kulia? Adhabu hizi hazitakuwa ni tatizo katika njia ya kutumikia dini.”

Yule mtu wa kwanza akajibu: “Tumetumikia dini yetu na kwa hiyo siogopi kifo, lakini ukweli ni kwmba ninaye mama mzee, na kwa vile ni mtoto wake pekee, anategemea kabisa juu yangu. Wakati akisikia kuhusu kifo changu, hataishi.”

Aliposikia hivi, yule kijana akatafakari kwa muda kidogo na kisha akase- ma: “Mama yangu hayuko hai wala sina mafungamano na yeyote. Tubadilishane hizi adhabu ili mimi niuawe badala yako wewe na wewe uchapwe viboko.”

Wawili wale wakabadilishana adhabu; yule akauawa, ambapo yule mtu mwingine baada ya kuchapwa viboko alirudi nyumbani kwa mama yake.

3. Vita Vya Yarmuk (Tabuk)

Katika vita vya Yarmuk, kikundi cha wanajeshi Waislamu walikuwa wakienda kwenye vita kila siku. Baada masaa machache ya mapambano, wale ambao hawakuumia na wale ambao wamepata majeraha kidogo hurudi, ambapo waliojeruhiwa au kufa huachwa kwenye uwanja wa mapambano.

Hudhaifah U’dwi, anaelezea: Siku moja, binamu yangu, pamoja na baadhi ya askari wengine, walitoka kwenda kwenye uwanja wa mapambano.

Kwa bahati mbaya, baada ya kukamilika kwa mapambano ya siku ile alishind- wa kurudi. Nilichukuwa chombo cha maji, nilikwenda kwenye uwanja wa mapambano, nikitumaini kumpa maji iwapo atakuwa hai.

Baada ya kutafuta kwa muda, nilimuona binamu yangu ambaye alikuwa hai kwa shida. Nilichuchumaa kando yake, na kumuuliza kama anahitaji maji. Alikubali kwa kichwa. Wakati huo huo, askari mwingine, ambaye amelala karibu yake, alinisikia alivuta pumzi kwa sauti kubwa kuonesha kwamba alikuwa na kiu kali sana.

Binamu yangu akaniashiria nimpe maji askari yule kwanza. Nilipokuwa nakwenda kumhudumia, niligundua kwamba alikuwa ni Hishaam Ibn A’as. Nilimuuliza kama alikuwa anahiji maji. Aliashiria kukubali. Wakati huo huo askari mwingine aliyejeruhiwa alitaka maji na Hishaam pia akakataa kunywa maji yale kabla ya askari yule mwingine hajanywa. Nilisogea kumuendea askari yule wa tatu, lakini nilipomfikia tu, alivuta pumzi yake ya mwisho. Nilirudi kwa Hishaam, niliona kwamba katika kipindi hiki kilichofuatia, naye pia amefariki. Niliharakisha kwa binamu yangu, nikamkuta akiwa amekwisha kufa pia!3

4. Ali (As) Katika Nafasi Ya Mtukufu Mtume (Saw)

Wakati viongozi wa Makureish walipotambua kwamba wakazi wa Madina wanatoa kiapo cha utii kwa Mtume, chuki yao kwake iliongezeka. Hatimaye, viongozi wao wakaamua kwamba mkesha wa kuamkia tarehe moja ya Rabi’ al-Awwal, shujaa mmoja kutoka kila ukoo wakusanyike pamoja, waizingire nyumba ya Mtume na kumuuwa akiwa amelala kitandani mwake.

Mwenyezi Mungu akaufichua mpango wao muovu kwa Mtume, ambaye alimuambia Amiru’l-Mu’muminin, Ali (as): “Kwa vile washirikina wanapanga kuniuwa leo usiku, Mwenyezi Mungu ameniamuru kuhama. Je, utalala kwenye kitanda changu ili wasijue kwamba nimeondoka?”

“Ewe Mtume wa Allah! Je, utakuwa hai na mzima wa afya kama nikifanya hivyo?” aliuliza Ali (as).

Mtukufu Mtume (saw) alimthibitishia kwamba itakuwa hivyo. Aliposikia hivi, uso wa Amiru’l-Mu’muminin (as) ukanawiri kwa furaha na akaporomoka chini katika sijda ya shukurani (kwa Allah Azza wa Jallah). Kisha akasema: “Uhai wangu na uwe muhanga kwa ajili yako! Nenda popote ambapo Allah amekuamuru wewe kwenda; kama unanihitaji mimi kufanya kazi yoyote kwa ajili yako, niamuru tu, na nitaifanya bila mashar- ti, na kutoka kwa Allah naomba rehema na mafanikio.”

Mtukufu Mtume (saw) alimchukua Ali kwenye mikono yake, huku machozi tele yakimtoka na akamuaminisha kwenye hifadhi ya Allah. Kisha, Jibril akamchukua Mtukufu Mtume (saw) kwa mkono wake na kumtoa ndani ya nyumba na kuelekea naye kwenye pango la Thaur.

Usiku ule, Amiru’l-Mu’muminin (as) alilala katika kitanda cha Mtukufu Mtume (saw) na akajifunika shuka lake.

Makafiri mwanzo walikusudia kushambulia nyumba ya Mtume katika usiku wa giza, lakini Abu Lahab, ambaye alikuwa pamoja nao, alishauri kinyume chake akisema kwamba ilikuwa ni usiku na wanawake na watoto walikuwa wamelala. Aliwaambia kusubiri mpaka asubuhi. Wakati asubuhi ilipoingia walikimbilia ndani ya nyumba na kumkuta Ali (as) katika kitan- da cha Mtume. Walimuuliza alipo Muhammad.

Kwani mlimuacha pamoja na mimi (hata sasa mniulize kuhusu aliko)? Mlitaka muondokane naye (na hivyo) kaondoka.” Alijibu kwa ukali.

Walimuacha Ali (as) na wakatoka kumtafuta Mtukufu Mtume (saw)4.

Hata hivyo, ilikuwa ni kwa ajili ya matokeo ya kitendo hiki (kilichopang- wa na Allah Azza wa Jallah) cha kujitoa muhanga kwa upande wa Ali (as), kwamba Mtukufu Mtume (saw) alibakia hai na bila madhara. Allah akateremsha Aya ifuatayo kwa tukio hili. Inafungamana na Ali (as):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَمَا لَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ {107}

“Na katika watu yuko auzaye nafsi yake kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja.” ( Quran 2:107)

5. Muhanga Binafsi Wa Haatim Taai

Wakati fulani kulikuwa na ukame katika sehemu ambayo Haatim Taai aliyokuwa akiishi. Chakula kikaisha kabisa mpaka ikawa hakuna kitu kili- chobaki na watu wakawa wanateseka vikali kwa njaa na dhiki.

Mke wa Haatim anasimulia: “Usiku mmoja kulikuwa hakuna hata tonge moja nyumbani mwetu. Haatim, watoto wangu wawili, A’di na Safaanah na mimi mwenyewe, tuliona kwamba hatuwezi kulala kwa sababu ya njaa tuliyokuwa nayo.

“Kwa shida kubwa, Haatim alimfanya A’di alale wakati mimi nilifanya hivyo hivyo kwa Safaanah. Kisha Haatim akaanza kusimulia kisa kimoja kwa nia ya kunifanya nilale, lakini ukali wa njaa ulinifanya kuwa macho. Pamoja na hivyo, nilijifanya niko kwenye usingizi mzito kiasi kwamba hata aliponiita mara nyingi, sikumjibu.

“Haatima alikuwa akichungulia kwenye jangwa kupitia kwenye tundu la hema, wakati alipoona kivuli kinasogelea upande wetu. Kilipofika karibu, Haatim alitambua kuwa alikuwa ni mwanamke na akaita: ‘Ni nani huyo?’ Yule mwanamke akaomboleza: ‘Haatim, watoto wangu wanapiga makelele kama mbwamwitu kwa ajili ya njaa kali waliyo nayo.’

“Haatim akamuambia yule mwanamke asiwe na wasiwasi, kwa vile atat- uliza njaa yao. Niliposikia hivi, niliamka kutoka kwenye sehemu yangu niliyolala na kumuuliza atalifanya vipi hilo. Akasema: ‘Nitamlisha kila mtu’

“Kisha alielekea kwenye punda wetu wa pekee tuliye naye na ambaye tunamtumia kwa kubebea mizigo yetu. Alimchinja na akatoa fungu mojawapo na akampa yule mwanamke akisema: ‘Ipike nyama hiyo na walishe watoto wako.’ Akanigeukia mimi na kusema: ‘Waamshe watoto ili na wao pia wapate kula.’

“Baada ya muda mfupi, aliongeza kusema: ‘Ni aibu kubwa kula ambapo wengine wanalala kando yako wakiwa na njaa.’ Alikwenda kuwaamsha yeye mwenyewe. Kila mtu alikula nyama ile isipokuwa Haatim ambaye alikaa na kupata furaha kutokana na kuwaangalia wakila.”

  • 1. Jaame al-Saadaat, Jz. 2, uk. 118.
  • 2. Hikaayat-ha-e-Shanidani, Jz.5, uk.114; al-Mahajjah al-Baidhaa, Jz. 6, uk. 80.
  • 3. Namunah-e-Ma’rif, Jz.2, uk. 435; Mustatraf, Jz. 1, uk.157.
  • 4. Daastan-ha Wa Pand-ha, j. 1, uk. 173; Mustatraf j. 1, uk.156