read

12) Bughudha

Allah Mwenye Busara anasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ {57}

“Hakika wale ambao wanamuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera…(Quran 33:57)

Mtukufu Mtume (saw) anasema: “Hairuhusiwi kwa Mwislamu kumuan- galia ndugu yake Mwislamu katika hali ambayo humuumiza na kumuud- hi.”1

Maelezo mafupi:

Viumbe wote ni wa kaya ya (viumbe wa) Mungu na wenye sifa zaidi miongoni mwao ni waumini. Mtu yeyote ambaye hunufaika na uumbaji, anakuwa mpenzi wa Mungu, ambapo yule ambaye huwabughudi na kuwaudhi wengine, hususan waumini, katika hali yoyote, ni kama vile ametangaza vita na Mwenyezi Mungu.

Katika Siku ya Hukumu, Mwenyezi Mungu ataita: “Wako wapi wale ambao wamebughudhi na kuwatesa rafiki Zangu katika dunia.” Kundi la watu ambao miili yao itakuwa bila nyama, watajitokeza mbele ambako Mwenyezi Mungu ataamuru watupwe kwenye Jahannam.

Hivyo, ni muhimu kujizuia kutokana na kuwaumiza na kuwaudhi wengine wazazi, majirani, marafiki na kadhalika. Kama mtu ametenda kitendo hiki, msamaha unatakiwa utafutwe kwa wale wanaohusika.

1. Usumbufu Aliofanyiwa Imamu Sajjad (As)

Wakati wa Imamu Sajjad (as), aliishi mtu mjini Madina ambaye alizoea kuwafanya watu wacheke ili kujipatia riziki yake.

Baadhi ya watu walishauri wamkaribishe Imamu Sajjad (as) na kumuacha huyu mtu amfanye acheke kidogo katika juhudi ya kumsahaulisha Imamu kutokana na uzito wa maombelezo yake. Walikusanyika pamoja na walikuwa njiani kuelekea nyumbani kwake wakati walipomuana anakuja kuelekea waliko wao, akifuatana na watumwa wake wawili.

Wakati Imamu alipofika karibu, yule mchekeshaji alichukuwa joho la Imamu (as) kutoka mabegani mwake na kulivaa yeye mwenyewe. Watu waliokuwa wamemzungka wakaangua kicheko walipoona kichekesho hiki.

Imamu (as) akauliza: “Ni nani mtu huyu?” Wale watu waliomzunguka wakasema: “Ni mtu ambaye huwafanya watu wacheke na kupata pesa kutoka kwao kwa vichekesho vyake.”

“Mjulisheni kwamba wale ambao hutumia maisha yao katika njia isiyo na maana wakifanya matendo ya kipuuzi watakuwa ni wenye hasara katika Siku ya Hukumu,” alishauri Imamu (as).

Baada ya kusikia haya, mchekeshaji yule aliacha tabia yake ile ya maudhi na akarekebisha mwenendo wake.2

2. Qaroon Na Musa (As)

Nabii Musa (as), katika harakati za kutangaza dini yake, alikabiliana na uadui na ugumu kutoka kwa watu wanaofanana na Firaun. Bala’m, Bao’ora na hata binamu yake Qaroon. Qaroon alikuwa tajiri mkubwa mno na alikuwa na utajiri mkubwa kiasi kwamba vijana kadhaa wenye nguvu walihitajika kubeba funguo za hazina yake. Alikuwa mmoja wa mamwinyi wenye daraja kubwa na ushawishi, ambaye alikuwa akiwakandamiza wa chini yake.

Musa (as), kwa kutekeleza amri za Allah, alitaka Zaka kutoka kwake, lakini Qaroon alikuwa akisema: “Mimi vilevile ninao ujuzi wa Taurat na sio mdogo kwa Musa kwa hali yoyote ile; kwa nini nitoe Zakat kwake?” Hatimaye, kiburi chake kilimlazimisha kutumia mbinu chafu kujaribu kumdhalalisha Nabii Musa (as). Alimfuata mwanamke mmoja ambaye alikuwa na mwenendo mbaya lakini vilevile alikuwa mrembo sana na mwenye kuvutia. Akamuambia: “Nitakulipa dirham mia moja elfu mradi tu kesho wakati Musa (as) akiwahutubia Bani Israel, upige kelele mbele za watu kwamba Musa amezini na wewe.”

Mwanamke yule akakubali kulifanya hilo. Siku iliyofuatia Bani Israil walikusanyika, na Musa (as) akiwa na Taurati mkononi mwake alikuwa amejishughulisha katika kuwahubiria. Qaroon, kwa umaridadi wake wote, alikuwa mmojawapo wa walihudhuria pamoja na watumishi wake. Ghafla, yule mwanamke alisimama, lakini wakati anaangalia kwenye uso mtukufu wa Nabii Musa (as) aliona mabadiliko ya moyo na akapiga kelele:

“Ewe Musa! Elewa kwamba Qaroon ameniahidi kunipa dirham mia moja elfu kama nitakushutumu wewe mbele za Bani Israil kwamba umefanya zinaa na mimi; lakini (natamka kwamba) kamwe hujawahi kufanya kitendo hicho na Allah ameilinda haiba yako kutokana na uchafu kama huo.”

Wakati Musa (as) aliposikia haya, aliumia sana na kuvunjika moyo, na akamlaani Qaroon kwa kusema: “Ewe ardhi! Mkamate Qaroon na ummeze.” Kwa amri ya Mungu, ardhi chini yake ikapasuka upande na Qaroon akatumbukia ndani yake pamoja na utajiri wake wote.

Kwa mujibu wa taarifa nyingine, Musa alikuwa akiwahubiria watu kuhusu Sharia’h wakati akiwa katika harakati za kuhutubia alisema: “Mtu ambaye hana mke/mume na akajiingiza katika zinaa ataadhibiwa kwa kuchapwa viboko mia moja na kwa mtu ambaye ana mke/mume akitenda zinaa atapigwa mawe mpaka afe.” Wakati huo Qaroon akasimama na akasema: “(kama hili likiwa kweli) hata kama wewe umetenda kosa hilo?”

“Ndio” akajibu Musa.

Bani Israil wana imani kwamba wewe umetenda zinaa na mwanamke fulani.”

“Mlete huyo mwanamke hapa,” alidai Musa. “Kama akithibitisha dai hili, uko huru kutenda kwa mujibu wa sheria.”

Yule mwanamke akaletwa mbele ya Musa (as) ambaye alimlisha kiapo ili aseme kweli, akamuuliza:

“Je, mimi nimefanya zinaa na wewe?”Yule mwanamke ghafla alianza kuona mabadiliko katika mawazo yake na akatoa jibu ambalo lilikuwa kinyume na kile alichokusudia kusema. “Hapana! Wanadanganya,” alisema. “Qaroon alinilipa kiasi hiki na hiki ili nielekeze shutuma hizi kwako.”

Qaroon alidhalilika ambapo Musa (as) alianza kutoa machozi, alianguka chini katika sajda na akaomba: “Ee Allah! Adui yako ameniumiza na alitaka kuniabisha kwa njia za uzushi. Kama mimi ni Mtume Wako, nipe mam- laka juu yake.”

Kisha akamlaani Qaroon ambapo adhabu ya Mungu ilimpata na ardhi ikammeza.3

3. Imekatazwa Kumuumiza Mu’min

Husein Ibn Abi al-A’alaa anasimulia: “Niliondoka kwenda Makka nikifu- atana na watu wengine ishirini. Katika kila sehemu ya kupumzikia nilich- inja mbuzi, ili kuwapa watu chakula. Wakati nilipotokea katika hadhira ya Imamu Sadiq (as) aliniambia:

“Ewe Husein! Ole wako, unawaumiza na kuwasabibishia Waumini usumbufu.”

“Naomba kinga kutoka kwa Allah kutokana na kitendo kama hicho.” Nilisema.

Akaelezea: “Nilijulishwa kwamba katika kila sehemu ya kupumzikia unachinja mbuzi kwa ajili ya watu uliofuatana nao.”

“Ndio, lakini kwa jina la Allah, nimefanya hivyo kwa ajili ya ridhaa Yake.” Imamu (as) aliendelea kusema: “Hujui kwamba miongoni mwa watu hao kuna baadhi, ambao hutamani kupata utajiri ili nao pia wapate kufanya matendo mema kama wewe, lakini kwa kukosa njia, wamefadhaika.”

“Natubia kwa matendo yangu na kuazimia kwamba kamwe sitatenda kwa njia hiyo tena.” Nilisema.

Imamu (as) alishauri: “Mu’min katika macho ya Mungu, ni mwenye heshima zaidi kuliko malaika, milima, mbingu saba, ardhi saba na kila kitu kilichomo humo.”4

4. Kumuudhi Imamu Ali (as) ni sawa na kumuudhi Mtukufu Mtume (saw)

Amir Ibn Shaas Aslami, mmoja wa masahaba aliyekuwepo wakati wa suluhu ya Hudaibiyah, anasimulia: “Siku moja Ali (as) na mimi tulitoka wote tukasafiri kuekea Yemen. Wakati tukiwa safarini, ilitokea nikapatwa na hasira juu yake na moyo wangu ukajazwa husda juu yake.

Nilivyorudi tu kutoka safarini, nilikwenda moja kwa moja msikitini na kulalamika kwa watu kuhusu tabia yake. Kwa bahati mbaya, ilitokea kwamba maneno yangu hatimaye yalimfikia Mtukufu Mtume (saw).

Asubuhi moja nilipoingia msikitini, nilimuona Mtukufu Mtume (saw) akiwa pale pamoja na masahaba wachache, mara tu macho yake yalipoan- gukia kwangu, aliniangalia kwa hasira na aliendelea kufanya hivyo mpaka nilipokaa.

‘Ewe Amri! Kwa jina la Allah, kwa hakika umenibughudhi!’ alisema kwa mkato.

Niliguta: “Naomba kinga ya Allah kutokana na yeyote anaye kubughudhi au anyekuudhi wewe.”

Akaseama: ‘Ndio, umenisumbua kwani yeyote yule ambaye amemsumbua Ali (as) amenisumbua mimi pia.’”5

5. Uonevu Wa Mutawakkil

Mmoja wa makhalifa waovu wa Bani Abbas alikuwa ni Mutawakkil, ambaye hakuacha chochote katika nia yake ya kumuudhi na kumtesa Imam Hadi (as), kizazi cha Mtukufu Mtume (saw), Mashi’a na wanaofanya ziyara ya Imamu Husein (as).

Gavana wa Madina, Abdullah Ibn Muhammad, kwa maagizo ya Mutawakkil, Alimsumbua Imamu Hadi (as) mpaka kufikia hali ambayo Imamu (as) alilazimika kuandika barua ya malalamiko kwa Mutawakkil.

Baadae, Mutawakkili alimlazimisha Imamu (as) kuondoka Madina na kwenda Saamarra. Hapa, alianzisha wimbi jipya la mateso na unyanyasaji, ambao baadhi ya mifano yake inafuata:

Usiku mmoja, Mutawakkil alimuita Sa’id, bawabu wake, na kumuagiza apande juu ya nyumba ya Imamu (as) na achungulie ndani kwa kuangalia mali au silaha. Kama kitaonekana chochote katika hivyo, lazima vitaifishwe.

Katika tukio lingine, akitegemea juu ya shutuma za uwongo, aliamuru kikundi cha Waturuki kuvamia nyumba ya Imamu na kuchukuwa kila kitu ambacho kitaonekena na wamlete barazani. Wakati Imamu (as) alipoletwa barazani, Mutawakkili alikuwa anajishughulisha na unywaji wa pombe na (kwa dhihaka) alitoa pombe ile kumpa mtukufu Imamu (as) na akasema: “Soma mashairi kwa ajili yangu!”

Na bado katika tukio lingine, alitaka Imamu (as) alitwe mbele yake na akaamrisha watumwa wane wa Khazar Jilfi 6 kumshambulia Imamu (as) kwa panga, Lakini Imamu (as) akitumia nguvu za uimamu, kimiujiza alizuia shambulio hili.

Katika mwaka wa 237 A.H., aliamuru kaburi la Imamu Hsein (as) na nyumba katika eneo hilo zibomelewe na alitaka eneo hilo litumike kwa ajili ya kilimo. Aliamuru kwamba mkono au mguu wa yeyote ambaye atakuja kwa ajili ya kumzuru Imamu Husein (as) lazima ukatwe.

Umar Ibn Faraj, ambaye alifanywa gavana wa Makkah na Madina na Mutawakkili aliamrishwa kuzuia watu wasitoe msaada au kuonesha huruma kwa kizazi cha Mtukufu Mtume (saw). Kutokana na woga watu wakajizuia kusaidia kizazi hiki cha Mtukufu Mtume (saw) ambao hali zao zikawa za huzuni na zisizofaa kiasi kwamba walikosa hata nguo nzurri za kuvaa. Unyanyasaji na mateso haya yalifikia hatua ambayo kwamba Muntasir, mtoto wa Mutawakkil, kwa mapenzi ya Amirul Mu’minin (as) hatimaye alishawishika kumuuwa baba yake mwenyewe.7

  • 1. Mtukufu Mtume (saw) alibakia kwenye pango la Thaur kwa muda wa siku tatu na katika siku ya nne alielekea kwenda Madina, na akifikia huko tarehe 12 Rabi’ al-Awwal katika mwaka wa 13 baada ya tangazo la utume, na katika uhamiaji huu kalenda ya Kiislamu ilianzishwa.
  • 2. Jaame’ al-Sa’adaat, Jz. 2, uk. 215.
  • 3. Darsi az Akhlaaq, uk. 120; Al-Amaali (Sheikh Mufid), uk. 128.
  • 4. Hikaayat-ha-e-Shanidani, Jz. 5, uk.122; Bihaar al-Anwaar, Jz. 13, uk. 253.
  • 5. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 2, uk. 453; La-aali al-Akhbaar, uk. 135.
  • 6. Daastaan-hai AzZindagi-e-Ali, uk. 112; Mustadrak al-Sahihain, Jz. 3, uk. 122
  • 7. Hawa walikuwa watu wapumbavu, makatili na wenye macho madogo