read

14) Undugu

Allah, Mwenye Busara, anasema:

“Hakika waumini ni ndugu”1

Imamu Baqir (as) alisema:

“Ni wajibu juu yako kuwa na marafiki wa kweli kwa ajili yako mwenyewe, kwa vile ni rasilimali wakati furaha, na ni ngao wakati wa shida.” 2

Maelezo mafupi:

Katika umri wowote, undugu na urafiki ni muhimu kwa mtu ambaye ni mwenye kustahili kwao. Allah hakuweka juu ya watumishi Wake neema muhimu zaidi kuliko mafanikio katika kukaa na kushirikiana na marafiki wenye dini.

Lakini huoni kwamba neema ya kwanza ambayo Allah aliwapa Mitume wakati wa utume wao ilikuwa ni rafiki, ndugu na wali? Ni dhahiri kutokana na hili kwamba baada ya neema ya utambuzi wa Mungu na Mitume Wake, hakuna neema iliyo safi zaidi na yenye kuridhisha kama undugu katika njia ya Allah na rafiki mwema.

Mtu anapaswa kujizuia kutokana na kufanya urafiki na undugu na wale ambao wanatafuta urafiki huu kwa ajili ya hamu ya kupata kitu au ushawishi wa dunia.

Ndugu wachache (katika dini) ambao wana utambuzi mkubwa, ni bora kuliko kuwa na ndugu wengi ambao hawana sifa hii. 3

1. Mu’min Ni Ndugu Wa Mu’min Mwingine

Imamu Baqir (as) alisema: Wakati fulani, kikundi cha Waislamu kilitoka kwenda safari, lakini katika mwendo wa safari yao, walipoteza njia yao. Punde mahitaji yao yaliwaishia na wakapatwa na kiu kubwa.

(Wakati kukukiwa hakuna dalili za maji na kufikiria mwisho wao kuwa karibu) walivaa sanda zao na wakakaa chini, wakapumzika chini ya miti.

Ghafla, mzee mmoja aliyavaa mavazi meupe aliwaendea na akasema: “Amkeni hakuna cha kuhofia. Maji haya hapa kwa ajili yenu.”

Walinyanyuka kwa shida na kunywa maji yale mpaka wakazima kiu yao, baada ya hapo walimgeukia yule mzee, wakasema: Allah akubariki! Wewe ni nani?”

“Mimi natokana na jumuiya ya majini, ambayo ilikula kiapo cha utii kwa Mtukufu Mtume (saw). Nilimsikia akisema: ‘Mu’min ni ndugu wa Mu’min mwingine. Ni macho yake na mwongozi wake pia.’ Sikuweza kukubali ninyi mfe kwa kiu wakati mimi niko hapa.” 4

2. Fungamano La Undugu

Muhammad Ibn A’jlaan anasimulia: “Nilikuwa nimefuatana na Imamu Sadiq (as) wakati mtu mmoja kutoka mji wa mbali aliwasili na kutusalimia.

‘Ndungu zako wana hali gani uliowaacha?’ Imamu (as) alimuuliza yule mtu. Aliwataja kwa wema na akawasifia sana. Imamu (as) kisha akamuuliza: “Je, matajiri wanawatembelea mafukara wanapokuwa wag- onjwa?”

Akasema wanafanya hivyo mara chache sana. Imamu (as) aliendelea: “Je, matajiri wanatafuta kujua hali za watu masikini?” “Mara chache tu,” alijibu yule mtu.

“Je, matajiri wanawasaidia masikini na mafukara?” aliuliza Imamu (as) Yule mtu akajibu: “unazungumzia sifa ambazo ni kidogo sana miongoni mwa watu wetu.” Imamu (as) akasema: “Vipi basi watu hawa wanajiona wenyewe kuwa ni Mashi’a (wetu wakati hakuna mafungamano ya udugu kati ya matajiri na masikini).” 5

3. Katika Mlango Wa Ndugu

Imamu Baqir (as) alisema: “Siku moja malaika alikuwa anapita katika nyumba, wakati alipomuona mtu amesimama mlangoni. Yule malaika aka- muuliza: ‘Kwa nini umesimama hapa?’ “Hii ni nyumba ya ndugu yangu na nataka kumsalimia.’ alijibu yule mtu. Yule malaika akauliza: “Ni ndugu na jamaa au ni kwa sababu una haja ya msaada wake ndio maana ukaja kumtembelea?” “Ukweli sio kama unavyoufanya uwe. Sisi ni ndugu kati- ka imani na nataka kumuona na kumsalimia tu kwa ajili ya Allah.”

“Mimi ni mjumbe wa Mungu,” yule malaika akasema. Ametuma salamu kwako na Amesema: ‘Ewe mja wangu! Umenitembelea na kutamani radhi Yangu na kadhalika hivyo, kama malipo kwako kwa ajili ya kushikilia haki na utukufu wa undugu wa kidini, Nimeifanya Pepo kuwa ya lazima kwako na nimekuweka mbali na moto na ghadhabu Yangu.” 6

4. Gavana Mkarimu

Mkazi mmoja wa mji wa Rey anasimulia: “Mwandishi mmoja wa Yahya Ibn Khaalid aliteuliwa kama gavana wa Rey. Nilikuwa na baadhi ya kodi za kulipa na niliogapoa kwamba gavana mpya angezitoa kutoka kwangu, kwani kwa njia hiyo, nitakabiliana na wakati mgumu. Baadhi ya rafiki zangu walinijulisha kwamba alikuwa ni mfuasi wa mtukufu Imamu (as), lakini niliogopa kwamba kama itakuwa sio hivyo, hatasita kuniweka gerezani.

Nikiwa na nia ya kufanya Hijja, nilijitokeza mwenyewe mbele ya Imamu Musa Kadhim (as) na kumjulisha mashaka yangu. Imamu (as) aliandika barua kwa gavana, yaliyomo katika barua ni kama ifuatavyo:

‘“Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema na Mwenye kurehemu. Elewa kwamba chini ya ‘Arsh (Kiti cha Enzi Kuu) ya Mungu, kuna kivuli cha rehema ambacho kwacho hakuna atakayeingia hapo isipokuwa yule ambaye anaoenesha wema na upole kwa ndugu zake katika imani, kumuondolea huzuni zake na kujitahidi kumfanya awe na furaha. Tazama! Mtu mwenye barua hii ni mmoja wa ndugu zako. Wassalaam.’

“Baada ya kurudi kutoka hijja, usiku mmoja nilielekea kwenye nyumba ya gavana na kumuambia askari wa zamu amuambie gavana kwamba kuna mtu ameleta ujumbe kutoka Imamu Kadhim (as). Mara tu alipojulishwa, gavana alikimbilia mlangoni katika hali ya furaha tupu. Alikuwa miguu mitupu na akanikumbatia na kurudia rudia kubusu paji langu la uso, kisha akauliza hali ya Imamu.

“Wakati akiwa amekwishaisoma barua ile ya Imamu (as), alinipa nusu ya mali ambayo alikuwa nayo na nguo alizokuwa nazo, na kwa vitu visivyo- gawanyika, alinipa pesa, inayolingana na nusu ya thamani yake, huku akiniuliza baada ya kila mgao: ‘Je, nimekufurahisha?’ Nami nilimjibu: Kwa jina la Allah! Umenifurahisha mno. Alitoa kitabu chake (cha orodha ya majina na madeni yao) akafuta madeni yote yaliyoandikwa kwenye jina langu, akanipa barua yenye amri ya kunipa msamaha wa kodi zote. “Niliomba ruhusa kwake ya kuondoka na kujisemea mwenyewe: Mtu huyu amekuwa mwenye huruma mno kwangu na hakuna njia ya kumlipa ukarimu wake. Ngoja niende Hijja tena na kule nimuombee na vilevile nimjulishe Imamu (as) kuhusu ukarimu na huruma zake (gavana huyo).

Mwaka ule nilikwenda Makka na kujitokza mbele za Imamu (as), nikamjulisha kile kilichodhihiri. Wakati nikiwa nasimulia tukio hili, niliona kwamba uso wake uliendelea kung’ara kwa furaha na hivyo nika- muuliza: Je, matendo yake haya yamekufurahisha?

Akasema: ‘Kwa jina la Allah! Matendo yake kwa kweli yamenifurahisha na vilevile yamemfurahisha Allah, Mtukufu Mtume na Amiru’l-Mu’minin (as)” 7

5. Ali (A.S), Ndugu Wa Mtukufu Mtume (Saw)

Moja ya hatua za maana zilizochukuliwa na Mtukufu Mtume (saw) miezi mitano au nane baada ya kuhamia Madina, ilikuwa ni kuanzisha mafunga- mano ya undugu kati ya Muhajirina (wahamiaji kutoka Makka) na Answar (Wasidizi - wenyeji wa Madina).

Abdullah Ibn Abbas anasema: Wakati aya: Hakika waumini ni ndugu8 ilipoteremshwa, Mtukufu Mtume (saw) alitangaza undugu kuwa ni kanuni ya kawaida miongoni mwa Waislamu na akichukulia vyeo na daraja zao, alianzisha mafungamano kati ya kila watu wawili kwa kuwafanya ndugu wa kila mmoja; Abu Bakr na Umar, Uthman na Abd al-Rahman na kadhalika. Amiru’l-Mu’minin (as) alikuwa amejilaza mwenyewe ardhini, wakati Mtukufu Mtume alipomwendea na akasema: “Amka, Ewe Abu Turaab! Sikukufanya wewe ndugu wa yeyote kwani nimekubakisha wewe kwa ajili yangu mimi mwenyewe. 9

  • 1. Qur’ani Tukufu 49:10.
  • 2. Bihaar al-Anwaar, Jz. 78, uk. 251.
  • 3. Tadhikirah al-Haqaaiq, uk. 52.
  • 4. Al-Kafi, j. 2, sura ya Undugu wa Mu’min, tr. 10.
  • 5. Al-Kafi, j. 2, sura ya Haki ya Mu’min juu ya ndugu yake, tr. 10.
  • 6. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 1, uk. 81; Jaame’ al-Akhbaar, uk.118.
  • 7. Pand-e-Taarikh, j. 2, uk.47; Bihaar al-Anwaar Jz. 11, Wasifu wa Imamu Kadhim (as).
  • 8. Qur’ani Tukufu; 49:10.
  • 9. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 1, uk. 82; Kashf al-Ghummah; Tafsir al-Burhaan.