read

15) Kutosheka/Kujitegemea

Allah, Mwenye Busara, anasema:

“Usikodolee macho yako yale tuliyowastareheshea makundi mbalim- bali…” 1

Imamu Ja’far Sadiq (as) amesema: “Heshima ya Mu’min iko kwenye ibada ya usiku na hadhi yake iko katika kuwa kwake mwenye kujitegemea (yaani, mwenye kutosheka bila kutegemea mtu).” 2

Maelezo mafupi:

Kinyume cha sifa ya kulaumika ya ulafi, ni sifa ya kutosheka na kujitegemea. Katika matumizi ya kawaida, kama inasemwa kwamba mtu hana haja na kitu chochote, mara moja dhana inayokuja akilini ni kwamba mtu huyo ni tajiri. Hata hivyo, maana halisi ni kuwa mwenye kujitosheleza, kujitegemea, kinaifu na sio mwenye hamu kubwa ya kupata kile walichokuwa nacho watu wengine.

Watu ambao wako huru kuhusiana na kuwategemea viumbe wa Mungu, wanaheshimika sana na wana imani juu ya Mungu ambayo ni rasilimali kubwa mno.

Ukweli kwamba kuomba na kuhitaji kutoka kwa wengine kunalaumiwa, ni kwa sababu huondolea mbali heshima na hadhi ya mtu, humfanya kuwa mfungwa wa wengine na kupunguza mwelekeo wake kwa Mungu.

1. Somo Kutoka Kwa Mtukufu Mtume (S.A.W)

Mmoja wa masahaba wa Mtukufu Mtume (saw) wakati fulani alijikuta akiwa katika umasikini mkubwa. Mke wake alimshauri kwenda kwa Mtukufu Mtume (saw) na kuomba msaada wake.

Yule mtu akamwendea Mtukufu Mtume (saw), lakini punde tu macho ya Mtume (saw) yalipoangukia kwa mtu yule, akasema:

“Kama atataka kitu kutoka kwangu, kwa hakika nitampatia kitu hicho, lakini kama atajionesha yeye mwenyewe kuwa ni mwenye kujitegemea na huru kutokana na kuhitaji, Allah atamfanya tajiri.” 3

Kusikia hivi, yule mtu akajisemea mwenyewe: “Mtukufu Mtume (saw) amenikusudia mimi kwa maneno hayo.” Bila kusema neno hata moja, alirudi nyumbani na kuelezea tukio lile kwa mke wake. Mke wake akasema: “Mtukufu Mtume (saw) naye vilevile ni mwanadamu; elezea mtanziko wako kwake na uone atasema nini.”

Yule mtu akarudi kwa Mtukufu Mtume (saw) kwa mara ya pili, lakini akasikia kauli ileile kutoka kwake na tena akarudi nyumbani bila kusema neno. Wakati hili linarudiwa kwa mara ya tatu, yule mtu akaazima shoka kutoka kwa mmoja wa marafiki zake na akaondoka kwenda kuelekea milimani. Siku nzima alifanya kazi ya kukusanya kuni, ambazo aliziuza kwa ajili ya kununulia unga na usiku ule yeye na mke wake walipata mkate kwa ajili ya chakula cha jioni.

Siku ya pili, alifanya kazi kwa bidii sana na akakusanya kuni zaidi na hii ikaendelea kwa siku kadhaa mpaka akawa na uwezo wa kununua shoka yake mwenyewe.

Baada ya kipindi Fulani, kwa matokeo ya kufanya kwake kazi kwa bidii, aliweza kununua ngamia wawili na mtumwa, na taratibu akawa mmoja wa matajiri.

Siku moja, alipohudhuria mbele ya Mtukufu Mtume (saw), alimsimulia yale matukio ya maisha yake na athari ya maneno yake, ambapo Mtukufu Mtume (saw) alijibu: “Nilisema (kabla): “Mtu anayetaka kuwa mwenye kujitegemea, Allah atamfanya kuwa ni mwenye kujitegemea.” 4

2. Alexander Na Deozhan

Wakati Alexander alipoteuliwa kuwa kamanda mkuu wa Ugiriki, watu kutoka sehemu zote walikwenda kumpongeza kutokana na kuteuliwa kwake. Hata hivyo, Deozhan filosofa mashuhuri, hakwenda kumuona na hivyo Alexander mwenyewe akaenda kumuona Deozhan. Deozhan alikuwa ni mtu ambaye hufuata sera ya kutosheka, kujitegemea na hatengemei juu ya watu.

Wakati akiwa amelala nje akiota jua, alihisi kwamba kundi la watu lilikuwa linamjia. Alijiamsha mwenyewe kidogo na macho yake yakaangukia kwa Alexander, ambaye alikuwa akija na ufahari na ukuu, lakini Deozhan alifanya kama vile tu anavyomfanyia mtu wa kawaida anayemtembelea. Alexander akamsalimia na akasema: “Kama unahitaji kitu chochote kuto- ka kwangu, niambie tu!”

“Nina ombi moja tu.” Akasema Deozhan. “Nilikuwa nafaidi joto la jua na kwa sasa unalizuia. Je, unaweza kusogea upande mmoja?” Wale waliofuatana na Alexander, waliyaona maneno yake kuwa ya kipum- bavu na kifedhuli na wakawa wanajisemea wenyewe, wakisema: “Mtu mjinga alioje huyu kupoteza fursa kama hiyo?” Lakini Alexander, ambaye alijiona mnyonge mbele yakutosheka kukubwa na kujitegemea kwa Deozhan, alitumbukia kwenye tafakari ya kina kwenye maneno haya.

Wakiwa njiani wakirudi, aliwageukia maswahiba wake ambao walimbeza Deozhan na akasema: “Hakika nisingekuwa Alexander, ningetamani kuwa Deozhan.” 5

3. Sio Chini Ya Ufadhili Wa Avicenna

Imesimuliwa kwamba wakati fulani, Avicenna, akiwa katika msafara wa kiwaziri wenye fahari kubwa na midundo ya ngoma na matarumbeta, alikuwa anapita karibu na mfagiaji ambaye alikuwa anasoma shairi hili lifuatalo kwa sauti kubwa huku akiwa anafanya kazi yake ya mikono:

“Ee nafsi! Nimekuheshimu kwa hali ya juu sana, hivyo kwamba wewe ni njia za usafi kwa ajili ya moyo.”

Aliposikia hivi Avicenna alitabasamu na akamuambia, “Hakika, umeiheshimu nafsi yako kwa hali ya juu sana kwa kujishughulisha katika kazi duni kama hiyo.”

Yule mfagiaji akasimama kufanya kazi, akamgeukia na akasema: “Ninaendesha maisha yangu kwa njia ya kazi hii ya hali ya chini ili kwamba nisilazimike kuwa chini ya ufadhilii wa Avicenna, kiburi na mwenye makuu.” 6

4. Usomaji Wa Sura Ya Al-Waaqia’h

Abdullah Ibn Masu’d alikuwa mmoja wa masahaba wa karibu sana na Mtukufu Mtume (saw) na aliondokea kuwa mtu mashuhuri na mwenye ari katika ulimwengu wa Kiislamu. Wakati wa ukhalifa wa Uthmani alibanwa na maradhi ya ghafla, ambayo hatimaye yalisababisha kifo chake. Wakati fulani Uthmani alikuja kumtembelea na akamkuta amehuzunika, akamuuliza: “Ni kitu gani kinakuhuzunisha hivyo?”

“Dhambi zangu,” akajibu.

“Niambie unataka nini ili nikutekelezee.”

“Nataka rehema ya Allah,” alijibu Ibn Masu’ud.

Khalifa akasema: “kama utaniruhusu, ninaweza kumuita mganga.”

“Mganga huyo ndiye aliyenifanya niumwe”

“Kama unataka, ninaweza kukupa zawadi kutoka kwenye hazina ya umma.” Ibn Masu’d akajibu kwa hasira: “Wakati nilipokuwa na shida, hukunipa kitu chochote na sasa kwa vile sina shida, unataka kunizawadia!”

Uthman akasisitiza: “Ngoja zawadi hizi ziwe kwa ajili ya mabinti zako.”

“Hawana haja na zawadi zako.” Ibn Masu’d akajibu kwa mkato:

“Nimewaelekeza kusoma Sura al-Waaqia’h kila usiku, kwani kwa hakika, nimemsikia Mtukufu Mtume (saw) akisema: ‘Mtu ambaye anasoma sura ya Al-Waaqia’h kila usiku, hatapatwa na umasikini.”7

  • 1. Qur'ani Tukufu 15:88
  • 2. Jaame al-Sa’adaat, Jz. 2, uk. 108
  • 3. Man sa’alana a’atwainahu wa man istaghinaa ghanaahu llahu. (Mwenye kutuomba tutampa na mwenye kutosheka Allah atamtajirisha)
  • 4. Pand-e-Taarihk, Jz. 3, uk. 129; Wafi, Jz. 2, uk. 139.
  • 5. Riwaayat-ha Wa Hikaayat-ha, uk. 30; Daastaan-ha-e-Paraakandeh, Jz. 2, uk.86.
  • 6. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 1, uk. 162; Naamunah-e-Daanishwaraan.
  • 7. Daastaan-ha Wa Pand-ha, Jz. 7, uk. 112; Majma’ al-Bayaan, Jz. 9, uk. 211