read

16) Ubahili

Allah, Mwenye Busara, anasema:

الَّذِينَ يَبْخَلُونَ وَيَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبُخْلِ وَيَكْتُمُونَ مَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ ۗ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُهِينًا {37}

“Ambao hufanya ubakhili na huwaamuru watu kufanya ubakhili, na wakayaficha aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake. Na tumewaandalia Makafiri adhabu yenye kudhalilisha.”(Quran 4:37)

Mtukufu Mtume amesema: “Mtu ambaye ni mjinga lakini mkarimu ni mwenye kupendwa zaidi na Allah kuliko mtu ambaye mchamungu lakini bahili.” 1

Maelezo mafupi:

Ubahili, au kujizuia kutoa vitu kwa watu wengine na kujikusanyia mali na utajiri kwa ajili yake mwenyewe mtu, ni moja ya alama ya mapenzi ya dunia. Humkwamisha mtu kutokana na kujipamba na nemsi mbalimbali zenye manufaa kama sadaka, ukarimu, kujitolea muhanga na kuwasaidia wengine. Ni kwa sababu hii kwamba Mtukufu Mtume (saw) amesema: “Hakuna bahili atakayeingia Peponi.”

Ubahili ni uovu wenye kuchukiza kiasi kwamba kama mtu akiathiriwa nao, huiweka familia yake katika umasikini, huchukia wageni kuja nyumbani kwake, hujizuia kuwatembelea watu wengine ili mtu yeyote asimtembelee, hujiepusha kushirikiana na watu wakarimu na hujisikia vibaya kuhusu ukarimu wa watu wengine. Mtukufu Mtume (saw) siku zote huomba kinga kwa Allah kutokana na uovu huu mbaya mno. 2

1. Dhambi Ya Mtu Bahili

Wakati fulani Mtukufu Mtume (saw) alikuwa amejishughulisha katika kutufu Ka’aba mara saba wakati alipomuona mtu ameshikilia pazia la Ka’aba na huku akiomba: “Ewe Allah! Kwa utukufu wa Nyumba hii, unisamehe!”

Huku akiwa amemkaribia, Mtukufu Mtume (saw) alimuuliza kuhusu dhambi zake. Yule mtu akajibu: “Dhambi zangu ni nyingi mno kwangu mimi kuzielezea kwake.”

“Ole wako! Dhambi zako ni kubwa au ardhi?” aliuliza Mtukufu Mtume (saw).

“Dhambi zangu.” Alijibu yule mtu.

“Dhambi zako ni kubwa au milima?” aliuliza Mtukufu Mtume (saw)

“Dhambi zangu.” Alijibu yule mtu.

“Dhambi zako ni kubwa au Arshi ya Allah.” Aliuliza Mtukufu Mtume (saw).

“Dhambi zangu.” Alijibu yule mtu.

Kisha Mtukufu Mtume (saw) akamuuliza: “Dhami zako ni kubwa au Mungu.

Kwa hili yule mtu akajibu: “Mungu ni Mkubwa Wa juu mno na Mtukufu mno.”

Mtukufu Mtume akaguna: “Ole wako! Nijulishe dhambi yako.” Yule mtu akaeleza: “Ewe Mtume wa Allah! Mimi ni mtu tajiri, lakini wakati masiki- ni anaponifuata na kuniomba msaada, nahisi kana kwamba komeo la moto limenifikia.”

Aliposikia hivi Mtukufu Mtume (saw) akaonya: “Kaa mbali na mimi na usinichome na moto wako! Kwa Yule, Ambaye amenipeleka mimi pamoja na mwongozo na heshima, kama ungesali kati ya al-Rukn na Al-Maqaam kwa muda wa miaka elfu mbili na kulia katika hali ya kipimo ambacho kwamba machozi yako yanatiririka kama mito na kuzima kiu ya miti, na baada ya yote haya, kama ungekufa ukiwa bado unayo dhambi hii ya ubahili, Allah atakutupa ndani ya Jahannam. Ole wako! Lakini hujui kwamba Allah amesema:

“Na ambaye ni bahili ni bahili dhidi ya nafsi yake mwenyewe 3 na vilevile amesema: “Na ambaye ameepushwa na ubahili wa nafsi yake, ni miongoni mwa waliofuzu.” 4

2. Mansur Dawaaniqi Na Ubahili Wake

Mansur Dawaaniqi, Khalifa wa pili wa Bani Abbas, alikuwa mashuhuri sana kwa ubahili wake. Kwa mfano, kwa matokeo ya ukaidi wake wa kukataa kutoa pesa zake. Huwapa onyo washairi ambao wanakuja mbele yake, kama ifuatavyo:

“Kama mtu mbali ya wewe, ikitokea vilevile na yeye analijua shairi amba- lo unataka kulisoma hivi punde au kama ikithibitishwa kwamba ni la mtu mwingine, usitegemee kupata malipo au zawadi.” Na kama mshairi aki- tokea kusoma shairi ambalo ni lake, Mansur humpa pesa kutengemeana na uzito wa karatasi aliyoandikia shairi lile!

Aidha, ana kumbukumbu kali na vilevile ana mtumwa na kijakazi, ambao ni wepesi isivyo kawaida katika kuhifadhi vitu kichwani.

Wakati mshairi anaposoma shairi lake, Mansur humuambia: “Shairi hili ulilonisomea sio jipya. Sio mimi tu ninayelifahamu bali hata huyu mtumwa na kijakazi wangu aliyeko nyuma ya pazia, wanalijua.

Kisha, kwa ruhusa yake, yule mtumwa atasoma shairi lile ambapo baada yake, yule kijakazi, akiwa amelisikia likisomwa mara tatu – mara moja na mshairi mwenyewe, mara moja na Mansur na mara moja na mtumwa – na yeye hulisoma pia. Kisha Mshairi yule aliyepigwa na mbumbuazi hutole- wa nje mikono mitupu bila zawadi yoyote!

Asmai’i, mshairi maarufu, alichukizwa na ubahili wa Mansur, na hivyo akaamua kutunga shairi kwa kutumia maneno magumu na kuliandika juu ya nguzo ya jiwe iliyovunjika. Wakati alipokwishafanya hivi, alivaa nguo kama bedui wa jangwani na akafunika uso wake wote isipokuwa macho yake.

Kisha aliwasli mbele ya Mansur huku akiongea lafidhi bandia, alimjulisha kwamba ametunga beti kadhaa za shairi na anaomba ruhusa yake ili azisome mbele yake.

Kwa kawaida, Mansur alimjulisha Asmai’i yale masharti ambayo aliyakubali. Kisha Asmai’i akaanza kusoma shahiri lake ambalo lina maneno magumu na yasiyo ya kawaida yenye kutatiza na sentenso changa- mani. 5 Mansur pamoja na upevu wake wa akili, na mtumwa na kijakazi pamoja na ukali wa akili zao, walishindwa kulihifadhi na kwa mara ya kwanza alionekana kutatizika na kushitushwa. Bila kuwa na njia nyingine ya kufanya, Mansur akamuambia: “Ewe ndugu! Inaonekena shairi hili ni kazi yako mwenyewe. Niletee karatasi yako ili nikuzawadie kwa uzito wake.”

Asmai’i akasema: “Sikuweza kupata karatasi ya kuandikia hivyo nime- andika shairi langu juu ya nguzo ya jiwe, ambayo kwa sasa iko kwenye mgongo wa ngamia yangu.” Aliileta nguzo ile ya jiwe na kuiweka mbele ya Mansur, ambaye alichanganyikiwa kabisa.

Alitambua kwamba hata kama angeweka hazina yake yote juu ya upande mmoja wa mizani, haitalingana na uzito wa nguzo ili ya jiwe. Alimgeukia yule mshairi na akauliza: Ewe Bedui! Wewe sio Asmai’i?”

Asmai’i aliondoa nguo aliyokuwa amejifunika usoni na kila mtu akaona kwamba mshairi yule alikuwa kweli ni Asmai’i.6

3. Waraabu Wanne Mabahili

Inasemekana kwamba walikuwepo Waraabu wane mabahili: Wa kwanza wao alikuwa ni Hatiah. Imesimuliwa kwamba siku moja Hatiah alikuwa amesimama mlangoni kwake na fimbo yake mkononi, wakati mtu mmoja aliyekuwa akipita hapo aliposema:

“Ewe Hatiah! Leo mimi ni mgeni wako.” Hatiah huku akionesha fimbo yake, hujibu kwa mkato: “Natumia fimbo hii kuwakaribisha na kuwakir- imu wageni wangu kwayo!”

Bahili wa pili alikwa ni Hamiid Arqat. Kuhusiana naye, imesimuliwa kwamba siku moja aliwakaribisha watu wachache kuwa wageni wake na akawapa tende ili wapate kula. Wale wageni wakati wakila tende zile, walikula na mbegu zake vilevile ambapo Hamiid alisababisha vurugu kwa kuwakemea kwa ajili ya kula tende na mbegu zake pia.

Bahili wa tatu alikuwa mtu mmoja kwa jina Abul Aswad Duali. Imesimuliwa kwamba siku moja alimpa ombaomba tende moja, ambaye alisema: “Mungu akupe tende moja katika Pepo.”

Aliposikia hivi, Abu Aswad Duali akasema: “Kama tukiwapa vitu watu mafakura tutakuwa mafukara kuliko wao!”

Bahili wa nne alikuwa ni Khaalid Ibn Safwaan, kuhusu yeye imesemwa kwamba wakati wowote dirham inapokuja kwenye mikono yake, ata- iambia: “Ewe pesa! Ni kiasi gani ulichohangaika na kusafiri kabla ya kufi- ka mikononi mwangu. Lakini (kwa vile umenifikia mimi) nitakuweka kwenye kasiki yangu, na ufungwa wako utakuwa wa muda mrefu na wa kuendelea.”

Wakati akisema hivi, huidondosha dirham ile kwenye kasiki yake na kuifunga.

Watu wakamuambia: “Kwa vile unamiliki mali nyingi mno na utajiri, kwa nini hutoi baadhi kama sadaka?” Akajibu: “Nina muda mrefu wa kuishi mbele yangu.” 7

4. Zakaat Kutoka Kwa Tha’laba Ansaari Haikukubaliwa.

Wakati fulani Tha’laba Ibn Haaib Ansaari alimuendea Mtukufu Mtume (saw) na kumuomba: “Ewe Mtume wa Mungu! Niombee kwa Mungu ili anipatie mali na utajiri.”

“Mali kidogo ambayo kwayo unaweza kutoa sadaka ni bora kuliko utajiri mkubwa ambao kwamba huwezi kutoa sadaka,” Mtukufu Mtume (saw) alimshauri. Tha’laba aliondoka lakini alimwendea Mtukufu Mtume kwa mara ya pili, na akarudia ombi lile tena. Mtukufu Mtume (saw) akasema: “Hutanitii. Kwa jina la Allah! Kama ningetaka kwamba milima igeuke dhahabu kwa ajili yangu, ingefanya hivyo.”

Mara ile tena akaondoka zake, lakini alirudi mara ya tatu tena na kutoa ombi lake tena kwa Mtukufu Mtume (saw) na kusihi: “Niombee tu. Naapa kwamba kama Mungu atanipa mali, yeyote mwenye haki kwayo, nitampatia.”

Mtukufu Mtume (saw) akamuombea na Mungu akajibu maombi yake. Tha’laba kwa kuanzia alinunua kondoo, ambao polepole waliongezeka idadi mpaka wakawa wengi.

Mwanzo, alikuwa akiswali Swala zake zote nyuma ya Mtukufu Mtume (saw), lakini baada ya mali na utajiri wake kuanza kuongezeka, aliweza tu kuhudhuria Swala ya Dhuhr na A’sir, na muda wote uliobaki aliutumia kuangalia kondoo wake.

Kadri muda ulivyokuwa ukipita, kazi zake ziliongezeka kufikia hali ambayo aliweza tu kuja Madina kwa ajili ya Swala ya Ijumaa na hatimaye hata hili likawa ni jambo lililopita. Alikuwa tu akija kwenye barabara iendayo Madina na kuuliza habari za mji huo kwa wapita njia.

Siku moja, Mtukufu Mtume (saw) alimuulizia, ambapo alijulishwa kwamba kondoo wa Tha’alaba wameongezeka marudufu na amefanya makazi yake nje ya Madina. Kusikia hivi, Mtukufu Mtume (saw) akatamka kwa sauti kubwa mara tatu: “Ole wake Tha’laba!”

Baada ya muda, aya inayohusu Zakaat iliteremshwa kwa Mtukufu Mtume (saw). Mtukufu Mtume akateua watu wawili, mmoja kutoka Bani Sulaim na mwingine kutoka Bani Juhiyah, na akawapa mamlaka ya kimaandishi, kuwawezesha kukusanya Zakaat. Walipomwendea Tha’alaba, walimsomea amri ile kwa ajili ya kukusanya Zakaat. Baada ya kufikiri kidogo, Tha’alaba akasema: “Hii ni Jizyah (kodi ya kichwa) au kitu kinachofanana nayo. Nendeni mkakusanye kwa watu wengine na kisha mje kwangu.”

Walikwenda kwa mtu wa kabila la Bani Sulaim na wakamsomea amri za Mtukufu Mtume ambazo kwazo aliwakabidhi mmoja wa ngamia wake aliye bora kama Zakaat.

Wale wakusanyaji wakamueleza kwamba hawakumtaka atoe ngamia aliye bora katika ngamia zake, lakini akasisitza kwa kusema kwamba alikuwa anatoa ngamia huyo kwa hiari yake mwenyewe.

Wakusanyaji wakakusanya Zakaat kutoka kwa watu wengine na wakati wa kurudi, walimwendea tena Tha’alaba na wakataka Zakaat yake. Akasema: “Hebu leteni niione hiyo amri.” Baada ya kuisoma, alirudia tena kusema: “Hii inaonekana kuwa ni Jizyah au kitu kama hicho. Nendeni zenu na acheni mimi nifikirie juu yake hilo”

Wakusanyaji wakarudi kwa Mtukufu Mtume (saw), lakini kabla hawajase- ma aliguta: “Ole juu ya Tha’alaba!” na kuomba kwa ajili ya ukarimu kuto- ka kwa watu wa Bani Sulaim. Wale wakusanyaji walimsimulia kwa dhahiri jinsi walivyokabiliana na Tha’alaba ambapo aya ifuatayo iliteremshwa:

وَمِنْهُمْ مَنْ عَاهَدَ اللَّهَ لَئِنْ آتَانَا مِنْ فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ {75}

فَلَمَّا آتَاهُمْ مِنْ فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوْا وَهُمْ مُعْرِضُونَ {76}

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ {77}

“Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema. Lakini alipowapa katika fadhila Zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza. Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kuku- tana nao. Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.”(Quran 9:75-77)

Moja wa jamaa wa Tha’alaba ambaye alikuwepo wakati wa aya hii ilipoteremshwa, alimjulisha Tha’alaba tukio hili. Baada ya kusikia hivi, aliharakia kwa Mtukufu Mtume (saw) na akamsihi akubali Zakaat yake, lakini alikataa akisema: “Mwenyezi Mungu ameniamuru nisipokee Zakaat yako.” Tha’lab alifadhaika aliposikia hivi.

“Haya ni matokeo ya matendo yako mwenyewe. Nimekuamrisha lakini umekataa kukubaliana na amri zangu,” alisema Mtukufu Mtume (saw).

Baada ya kufariki kwa Mtukufu Mtume (saw) Tha’alab alimwendea Abu Bakr, ambaye naye alikataa kupokea Zakaat yake.

Wakati wa ukhalifa wa Umar, Tha’alaba alimwendea, lakini na yeye alikataa na Uthman naye aka- fuata mwendo huohuo, mpaka hatimaye kifo kikamchukua Tha’alaba.8

5. Sa’id Ibn Harun, Mbahili

Sa’id Ibn Harun, mwandishi kutoka Baghdad na wa zama moja na Ma’mun, Khalifa wa Bani Abbas, alikuwa akivuma vibaya kwa ubahili wake.

Abu Ali Dibil Khazaai, mshairi mashuhuri (amekufa 245 A.H.) anasema: “Nikiwa nimefuatana na baadhi ya washairi, nilikwenda nyumbani kwa Sa’id na tulikuwa pamoja naye kuanzia asubuhi mpaka mchana. Wakati adhuhuri ilipokuwa inakaribia, alianza kusikia njaa na matokeo yake akawa anahangaika.

Sa’id alikuwa na mtumwa mzee, ambaye alimuambia, “kama kuna kitu cha kula, hebu tuletee.” Yule mtumwa aliondoka na kurudi muda mfupi akiwa amechukuwa kitambaa kichafu cha chakula.

Alikitandika mbele yetu na akaweka juu yake kipande kimoja tu cha mkate mkavu. Kisha akaleta bakuli lililovunjika midomo yake lililojazwa maji ya moto, na ambalo lina jogoo mzee asiyepikwa na asiye na kichwa!

Wakati yule mtumwa anaweka lile bakuli kwenye kitambaa cha chakula, acho ya Sa’id yakaangukia juu yake na akaona yule jogoo asiye na kich- wa, alifikiria kwa muda kidogo na kisha akasema, “Ewe Mtumwa! Kikowapi kichwa cha jogoo huyu?” Yule mtumwa akajibu: “Nimekitupa.”

Alivyosikia hivi, Sa’id alipiga kelele: “Simruhusu yeyote mwenye kutupa miguu ya jogoo, achilia mbali kichwa chake. Kitendo hiki (chako) huwashiria ubaya (kwangu) kwani kichwa cha jogoo kina faida nyingi: Kwanza, kutokana na kichwa chake hutoka sauti ambayo huwajulisha waja wa Mwenyezi Mungu kuhusu muda wa Swala; kwa njia yake hii, waliolala huamka na wale wanaofanya ibada wakati wa usiku kujiweka tayari kwa sala za usiku.

“Pili, taji lake ambalo liko juu ya kichwa chake hufanana na taji la wafalme, na hivyo ana heshima ukilinganisha na ndege wengine. Tatu, hushuhudia malaika kwa njia ya macho mawili ambayo yamewekwa kwenye fuvu lake. Kwa nyongeza, washairi hufananisha rangi ya mvinyo na macho yake, kwa sababu wanapotaka kuelezea mvinyo mwekundu, wanasema: ‘Mvinyo huu ni kama macho mawili ya jogoo.’

“Nne, ubongo katika kichwa chake ni tiba ya matatizo ya mafigo. Aidha, hakuna mfupa ulio mtamu mno kama mfupa wa kichwa chake. Kama ulikitupa kwa mawazo kwamba sitakila, umekosea sana, na hata kama sikuki- la, familia yangu wangekila na kama hawatakila, hawa wageni wangu, ambao hawajakula chochote tangu asubuhi, wangekila.”

Aliendelea kwa hasira, “Nenda ukakilete na ukishindwa kufanya hivyo, nitakuadhibu.” Yule mtumwa akaomba kwa kusihi: “Wallahi! Mimi sijui ni wapi nilipokitupa.” Sa’id akasema kwa hasira: “Wallahi! Najua ni wapi umekitupa, umekitupa kwenye huo mtumbo wako mbaya!” “Wallahi! Mimi sikukila,” alilalama yule mtumwa, “wewe ndiye unaongopa.”

Huku akiwa amechukia, Sai’id alisimama na akamkamata yule mtumwa kwenye shingo kwa nia ya kumtupa chini kwenye sakafu, lakini katika harakati hizo mguu wake ukakanyaga lile bakuli likageuka na vyote vilivyokuwa ndani vikamwagika. Paka ambaye alikuwa amekaa karibu, alitumia fursa hiyo na kuokata yule jogoo asiye na kichwa na kuondoka naye. Sisi pia tukatoka ndani ya nyumba ile, tukamuacha Sa’id akizozana na mtumwa wake. 9

  • 1. Jaame’ al-Sa’adaat, Jz. 2, uk. 110.
  • 2. Thyan al-Qulub, uk. 96.
  • 3. Qur’ani Tukufu; 47:38.
  • 4. Qur’ani Tukufu; 59:9.
  • 5.
  • 6. Daastaan-ha-e-Maa, Jz. 2, uk.102; I’laam al-Naas, uk. 54.
  • 7. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 2, uk. 463; Mustatraf, Jz. 1, uk. 171.
  • 8. Pand-e-Taarikh, Jz. 1, uk. 73; Asaad al-Ghaabbah, Jz. 1, uk. 237.
  • 9. Lataaif al-Tawaaif, uk. 341.