read

17) Uovu

Allah, Mwenye hikma anasema:

“Mnaweza mkakipenda kitu wakati ni kiovu kwenu”1

Imamu Sadiq (as) amesema: “Kwa hakika madhara ya uovu kwa mtendaji ni ya haraka sana kuliko yale ya kisu kwa nyama”2

Maelezo mafupi:

Mtu mbaya kuliko wote ni yule ambaye huuza Akhera yake kwa ajili ya maisha ya dunia hii, lakni mbaya zaidi ni yule ambaye huuza Akhera yake kwa ajili ya maisha ya dunia ya watu wengine.

Uovu hujidhihirisha katika sura mbalimbali, zote ambazo zinaweza kufupishwa kwa utovu wa utii wa Allah.

Kwa vile matendo yanategemea nia, fikra za kiovu huzaa matendo maovu. Mtu anapokuwa hana Allah katika upeo wake, hujiona kuwa na nguvu.

Hujiingiza katika aina mbalimbali za matendo maovu, bila moyo wake kuhisi hata chembe ndogo ya hofu ya moto wa Jahannam.

Kwa kila kiungo cha mwili kuna matendo maovu yanayohusiana nacho; masikio kwa utesi, macho kwa kuona vilivyokatazwa, ulimi kwa kusema uongo, na mikono kwa kuwadhuru mayatima. Hivyo ni lazima kuvihifadhi vyote dhidi ya uovu.

1. Mkosi Wa Jaludi

Baada ya shahada ya Imam Kadhim (as). Harun Al-Rashid, Khalifa kuto- ka ukoo wa Abbasi, alimtuma mmoja wa makamanda wake kwa jina la Jaludi kwenda Madina na alimuagiza: “Shambulia nyumba ya kizazi cha Abu Talib, waporeni wanawake na msiache chochote isipokuwa nguo moja kwa kila mmoja wao!”

Alipokuwa Madina Jaludi alianza kutekeleza amri ya Harun. Alipokaribia nyumba ya Imam Ridha (as), Imam (as) aliwakusanya wanawake wote wa nyumba ile katika chumba kimoja na yeye alisimama mlangoni, akimzuia Jaludi kuingia.

Jaludi alisisitiza kwamba lazima aingie ndani ya nyumba na kuwapora wanawake na kuchukua nguo zao. Imam (as) aliahidi kuwa yeye mwenyewe angekusanya nguo na mapambo yao na kuvikabidhi kwa Jaludi, kwa sharti kwamba ajiepushe kuingia ndani ya chumba.

Hatimaye Jaludi alikubaliana na ombi la Imam (as) ambapo (Imam) aliingia ndani ya chumba, akakusanya nguo na mapambo ya wanawake pamoja na vitu vingine vya ndani, kisha akamkabidhi Jaludi, ambaye mara moja alivipeleka kwa Harun.

Baada ya Harun, akawa mwanae Ma’mun, aliye chukua hatamu za ukhal- ifa. Ilitokea kwamba siku moja aliudhiwa na Jaludi na akataka kumpa adhabu ya kifo. Imam Ridha (as) alikuwepo katika baraza hilo na alimuomba Ma’mun amsamehe.

Jaludi kwa kukumbuka uovu wake wa nyuma aliomfanyia Imam, alifikiri kwamba Imam (as) angemlalamikia Ma’mun kuhusu uovu wake na hivyo, alimgeukia Ma’mun, (na) kusema: “Nakuweka chini ya kiapo cha Allah! Usikubali maneno yake kuhusiana na mimi.”

Maamun akasema: “(Naapa) kwa Allah! Sitakubali maneno yake” Alipo sema hivi, aliamuru Jaludi akatwe kichwa.3

2. Udanganyifu Wa Amr Ibn A’as

Baada ya tukio la upatanishi, ambapo Amr Ibn A’as, alimdanganya kwa hila Abu Musa Asha’ri na kumuondoa Ali (as) kutoka katika ukhalifa, Imam (as) alikuwa akiwalaani Amr Ibn A’as, Muawiya na Abu Musa baada ya sala za asubuhi na magharibi. Amr Ibn A’as pia alikuwa ni sehemu ya kundi lililohusika katika tukio la usiku Aqabah4 na hatimaye alilaaniwa na Mtukufu Mtume (saw).

Mzozo kati ya Imam Ali (as) na Muawiya ulipoongezeka, iliamuliwa kwamba shauri hili liamuliwe kwa upatanishi. Kwa bahati mbaya, watu wa Iraq walimchagua Abu Musa Ashari kumuwakilisha Imam (as) (Ingawa Imam mwenyewe hakufurahia uchaguzi huu), ambapo Muawiya alimch- agua Amr Ibn A’as kuwa muwakilishi wake.

Abu Musa, ambaye alikuwa katika moja ya vijiji vya Sham, aliombwa kuwasili Siffin na watu 400, miongoni mwao Shuraih Ibn Haani na Ibn Abas, waliambatana naye hadi Daumah al-Jundal, Amr Ibn A’as pia ali- wasili hapo na wenzake 400.

Ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa kwa Abu Musa (na watu wake) hayakufaa kitu kwani Amr ibn A’as kwa uovu wa nia na ufidhuli wa tabia aliokuwa nao, alikuwa na nguvu sana katika hila na udanganyifu kuliko yeye (Abu Musa).

Moja ya mbinu za Amr Ibn A’as ilikuwa ni kuonyesha heshima iliyotiwa chumvi juu ya Abu Musa. Alimuweka mbele ya mkusanyiko na alisistiza kwamba (Abu Musa) aongoze swala, huku Amr mwenyewe akiswali nyuma yake, na mara zote alipokuwa akiongea naye alimuita ‘Ewe sahaba wa Mtume wa Allah!’ Alikuwa akimuambia: “ulinitangulia katika usahaba wa Mtukufu Mtume (saw) na ni mkubwa kwangu, na hivyo sio sawa kwa mimi kusema juu ya lolote kabla wewe hujafanya hivyo.” Alionyesha heshima fulani ya uongo mpaka Abu Musa mwenye akili finyu akashawishika juu ya unyofu wake na akawa ana hakika kuwa nia yake pekee ilikuwa ni kuyaweka mambo vizuri. Kama sehemu ya mipango wake wa hila, awali Amr Ibn A’as alimchukua Abu Musa sehemu ya faragha na akaongea naye pembeni ili kuwazuia wengine wasimshawishi Abu Musa katika kufanya maamuzi.

Amr Ibn A’as alimuuliza, “Abu Musa, nini maoni yako juu ya Ali (as) na Muawiya?”

“Tuwaondoe Ali (as) na Muawiya katika ukhalifa na turuhusu suala la ukhalifa liendeshwe na Shuura,” alijibu Abu Musa.

Aliposiki hivi, Amr Ibn A’as alisema: “(Naapa) kwa Allah! Maoni yako ni sahihi kabisa na ni lazima tuyatekeleze” Baada ya kukubaliana hivi, wakaja mbele ya umma.

Abu Musa alisimama kwanza na akaanza kuzungumza wakati Ibn Abbas alipopiga kelele: “Kuwa makini kwani nina hofu Amri Ibn A’as amekute- ga. Mruhusu aongee kwanza kabla yako.”

Lakini Abu Musa alipuuza na kusema, “Eyi watu! Amr Ibn A’as na mimi tunawaondoa Ali na Muawiyya kutoka kwenye ukhalifa na tutamuidhin- isha tu Khalifa atakayechaguliwa kwa njia ya Shuura, hivyo ninamuondoa Ali (as) kutoka kwenye ukhalifa.”

Kisha Amr Ibn A’as muovu akasimama na kusema: “Mimi pia nina muon- doa Ali katika ukhalifa na ninamteuwa Muawiyya katika sehemu yake. Muawiyya anataka kulipiza kifo cha Uthman na hivyo anastahili zaidi wadhifa huu.”

“Wewe ni kama mbwa,” alipayuka Abu Musa “ambaye hushambulia mtu akimsogelea na hufanya vivyo hivyo pia mtu akimpa mgongo.

Amr Ibn A’as alilipiza, “Na wewe ni kama punda, ambaye hubeba mzigo wa vitabu lakini hafaidiki navyo hata kidogo”

Kwa kifupi, Amr Ibn A’as akisaidiwa na uovu wake aliibuka mshindi katika shauri la upatanishi! Baadaye Ibn Abbas alikuwa akisema: “Allah amfedheheshe Abu Musa! Nilikuwa nimemuonya juu ya nia ya kiovu ya Amr Ibn A’as na nilimshauri vyema, lakini alijifanya kiziwi na akakataa kuzingatia.”5

3. Ukatili Wa Hajjaji Ibn Yusuf Thaqafi

Sio matendo maovu tu yanayostahili adhabu bali nia za kiovu pia huwa na madhara. Kwa kweli ni kutokana na nia zao za kiovu kwamba makafiri na maadui wa Uislamu watakaa motoni milele.

Hajjaaj Ibn Yusuf Thaqafi alikuwa akionyesha ukatili mkubwa na uovu kwa kuwatilia sumu na kuwaua Masaadaat (kizazi cha Mtukufu Mtume). Wakati fulani, alipokuwa akitoka msikitini na kusikia vilio vya idadi kubwa ya watu, aliuliza “Ni akina nani hawa wanaolia?” Wale waliokuwe- po wakasema: “Hivyo ni vilio vya mateka, wanaoteswa kwa joto kali la jua.” Akasema: “Waambieni ‘ikhsanuu!’ (Ambaa au toka) ambalo ni neno la Kiarabu ambalo hutumika kumfukuzia mbwa.6

Gereza lake lilikuwa na wanaume 120, 000 na wanawake 20, 000 (4000 kati ya hawa wakiwa hawajaolewa ) na lilikuwa ni eneo moja kubwa lenye kuta lakini halikuezekwa (halina paa), kila wakati wafungwa walikuwa wakijaribu kujihifadhi kutokana na jua linalo unguza, ama kwa mikono yao au kwa njia nyingine, walinzi waliokuwa wakiwatizama walikuwa wakiwarushia mawe.

Chakula chao kilikuwa ni mikate iliyotengenezwa kwa shayiri na kuchanganywa na michanga, wakati kinywaji chao kilikuwa ni maji machungu. Wakati fulani, damu ya Masaadaat na watu waongofu ilikuwa ikitumika kuandalia mikate ya Hajjaj ambayo alikuwa akiila kwa furaha kubwa!

Mtu huyu muovu, mara zote alikuwa akisikitika kwa kutokuwepo Karbala na alikuwa akisema: “Oh! Ni jinsi gani natamani ningekuweko Karbala ili niwe mmoja katika walioshiriki kumuua Imam Husein (as) na masahaba zake!”7

4. Kuhalalisha Matendo Maovu

Imam Sadiq (as) alikuwa amesikia kwamba kuna mzee mmoja ambaye amekuwa maarufu kwa uchamungu wake. Siku moja alimuona akiwa amezungukwa na umati mkubwa wa watu.

Muda mfupi baadaye alitoka kwenye umati ule na akajitenga nao akaenda peke yake, ambapo Imam (as) alianza kumfuata. Baada ya muda mfupi Imam (as) aliona kwamba alikuwa amesimama karibu na duka la mikate ambapo kwa wizi alichukua mikate miwili. Baada ya umbali mfupi alisimama kwenye duka la matunda, akachukua makomamanga mawili kwa staili ileile na kwa mara nyingine tena akendelea na safari yake.

Alivyokuwa akitembea zaidi, mzee yule alimuendea mgonjwa akamkabid- hi mikate na matunda na alikuwa anataka kuondoka Imam Sadiq (as) alipomuendea na kusema, “Nimeshuhudia kitu kilichonishtua sana kutoka kwako,” na kisha akaendelea kumsimulia matukio aliyoyafanya. Yule mzee akasema, “Nafikiri wewe ni Imam Sadiq (as)” Imam (as) alijibu kwa kukubali. Yule mtu aliendelea, “Kwa hakika ni bahati mbaya kwamba licha ya kuwa ni kizazi cha Mtukufu Mtume (saw) hauonyeshi kujua chochote.”

Imam (as) akauliza, “Ni kitendo gani cha ujinga ulichokigundua kutoka kwangu?” Yule mtu akasema, “Lakini hujui kuwa Allah amesema katika Qur’ani:

مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَنْ جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا {160}

‘Yeyote afanyaye wema atalipwa mara kumi zaidi na yeyote afanyaye uovu, atalipwa mfano wake (mara moja)’ (Quran 6:160)

“Kwa msingi huu, nimeiba mikate miwili na matunda mawili nina mad- hambi manne katika hesabu yangu lakini katika upande mwingine, kwa kuwa nimetoa kwa njia ya Allah, nina thawabu arobaini. Ukipunguza nne katika arobaini, bado nina thawabu 36 katika hesabu yangu, nakuonea huruma, hauna maarifa ya mahesabu haya.”

Imam (as) akamueleza, “Lakini hujasikia aya hii ya Qur’ani inayosema:

إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ {27}

‘Allah hukubali tu kutoka kwa wale wanaojilinda (na maovu).’ (Quran 5:27).

Umepata madhambi manne kwa kuiba na madhambi manne zaidi kwa umpa mwengine bila ruhusa ya wamiliki, hivyo umekusanya madhambi nane lakini hujapata thawabu hata moja.”

Baadaye Imam (as) aliwaambia masahaba zake, “kwa tafsiri hizo na uhalalishaji huo, sio tu kwamba wanajipotosha wao wenyewe, bali wanawapotosha na wengine pia.8

5. Matokeo Ya Uovu Huko Barzakh

Mwanazuoni mashuhuri, maarufu kwa uchamungu wake anasimulia: “Mmoja wa ndugu zangu alikuwa amenunua mali katika mwaka wa mwisho wa uhai wake, akitumia kipato kikubwa kilichotokana na mali hiyo kwa kukidhi mahitaji yake. Alipokufa, nilimshuhudia akiwa katika eneo la adhabu, katika hali ya upofu. Nilipomuuliza sababu yake alijibu:

“Nilikuwa nimenunua kipande cha ardhi, ambacho katikati yake kulikuwa kisima ambacho maji yake yalikuwa yakitumiwa na wakazi wa kijiji cha jirani, wao wenyewe na wanyama wao. Lakini njia yao katika ardhi yangu ilikuwa ikiharibu sehemu ya mazao yangu, hivyo, ili kulinda kipato changu na kuzuia wasiingie, nilikifukia kisima kwa mchanga na mawe na nikakifunika.

Matokeo yake wale wakazi wenye bahati mbaya walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kupata maji yao, na huu upofu ni matokeo ya kitendo changu hicho.”

“Nilimuuliza, ‘Je kuna suluhisho lolote la tatizo lako hili?’ Alijibu, ‘Kama warithi wangu wangeonyesha huruma juu yangu na kukifungua kisima kile ili wengine wanufaike kutokana na maji yake tena, nitaondokana na tatizo langu hili.’

“Nilipowaendea warithi wake, niliwajulisha juu ya tukio hili walikubali kufanya msaada na haraka, kisima kilifunguliwa, na watu wakaanza kukitumia kama zamani.

“Baada ya muda nilimshuhudia marehemu tena, lakini mara hii niliona kuwa amerudishiwa kuona kwake na alinishukuru kwa kumsaidia kutoka katika taabu yake.’9

  • 1. suratul Baqara 2:216 .
  • 2. Taz. Jaame al- Saadat, Juz. 3, uk. 48.
  • 3. Raahnama –e- Sa’adat, Juz, 1, uk. 177; Aayaan al- Shi’ah, Juz. 1, uk. 60
  • 4. Baadhi ya watu walikusanyika pamoja wakala njama na kujificha karibu na njia ya mlima na kumshitua ngamia wa Mtukufu Mtume (saw) ili aangushwe chini na kuuawa. Na huu ni usiku ambao unaitwa “usiku wa Aqabah”
  • 5. Paighambar wa Yaaran, Juz. 1 uk. 136- 153; Biharul Anwar, Juz. 8, uk. 544
  • 6. Qur’ani Tukufu 23:108 - maneno waliyoambiwa watu wa motoni.
  • 7. Pand-e-Tarikh, Juz.3, uk. 163; Randhaat al-Jannaat, uk 133
  • 8. Namunah-e- Maarif, Juz. 4, uk. 275; Wasailul Shia, Juz. 2, uk 57
  • 9. Daastaan –ha-e Shigif, uk. 292