read

18) Misiba

Allah Mwenye hikma amesema:

فَأَمَّا الْإِنْسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ {15}

“Na kwa mwanaadamu, Mola Wake anapomjaribu, na kisha humtendea hisani ni kumfanya aishi maisha rahisi, husema: Mola wangu amenitukuza.”(Quran 89: 15)

Mtukufu Mtume (saw) amesema:

“Kwa hakika msiba kwa dhalimu huwa adhabu (yenye kurekebisha) na kwa muumini huwa ni mtihani”1

Maelezo mafupi:

Kwa mtu mwenye akili, misiba ni njia ya mapambo na heshima. Kuwa na uvumilivu mtu anapokabiliwa na msiba na kuwa imara wakati wa mitihani, huimarisha imani yake.

Mtu anayekabiliana na ugumu kwa subira, atapata rehema ya Allah, kama ilivyoelezwa na hikma ya kimungu, atapata uokovu na raha, ama hapa kati- ka ulimwengu huu au Akhera.

Kutoka katika moto wa majanga na misiba, huibuka mwanga wa pekee. Mtu ambaye huchukulia balaa na msiba kama mtihani, na hukabiliana nao vilivyo, atakuwa na busara zaidi kutokana na elimu ya ziada na uelewa aliopata. Sio mwenendo mzuri kulalamika kila mara juu ya misiba ya kidunia kama umasikini, maradhi, matatizo ya kifamilia nk.

1. Pamoja Na Malaika

Mmoja wa wagonjwa waislamu, ambaye alikuwa halalamiki juu ya misiba, alikuwa ni mtu aliyekuwa akiitwa Imran. Aliugua ugonjwa wa jongo na hakuna matibabu yaliyomsaidia. Kwa miaka 30 alilalia tumbo lake akiwa hawezi kuinuka, kukaa au kusimama, na hivyo shimo lilikuwa limechimbwa jirani na alipopumzika kwa ajili ya mkojo na kinyesi.

Siku moja ndugu yake A’laa, alimtembelea na alioona ile hali yake ya kuhuzunisha aliangua kilio, Imran alimuuliza, “Kwa nini unalia?” Ndugu yake alijibu, “Ni kwa sababu ninaona kwa miaka umekuwa ukitaabika katika hali hii ya kuhuzunisha”

Imran akasema, “usilie na usihuzunike kwa sababu hali hii, ambayo Allah amenipangia, inapendeza zaidi kwangu kuliko kitu kingine chochote, ninatamani nibakie katika hali hii ambayo Allah amenipangia, kwa muda wote nitakaoishi. Sasa nitakujulisha siri, ambayo haupaswi kuivujisha kwa yeyote katika muda wote nitakao kuwa hai; nipo pamoja na malaika, wananisalimia na mimi ninaitika salamu zao, na nipo karibu nao sana.2

2. Ali A’abid Gerezani

Ali A’abid (Ali Ibn Hassan Al-Muthallath) alikuwa ni mmoja wa watoto wa Imam Hasan (as) ambaye alikuwa amefungwa na Mansur Dawaaniqi na alikufa akiwa gerezeni. Ali A’abid alikuwa mstari wa mbele katika subira, ibada na kumkumbuka Allah.

Mansur alipowakamata watu wa kizazi cha Mtukufu Mtume (saw) na watoto wa Imam Hasan (as) aliwaweka katika gereza lililokuwa na giza sana kiasi kwamba mchana hauwezi kutofautishwa na usiku, isipokuwa kwa visomo na matendo ya ibada ya Ali A’abid. Matendo haya yalikuwa na mpangilio, yanayozingatiwa kwa nidhamu na ya kuendelea, na hivyo aliwafanya wengine wajue nyakati za sala.

Siku moja, kutokana na shida za kuwa mateka na uzito wa masaibu yake, Abdullah Ibn Hasan Al-Muthanna alipoteza subira na katika hali ya mashaka makubwa, alimuambia Ali A’abid: “Je hushuhudii mabalaa na hali ngumu? Hauombi kwa Allah ili atupe nafuu ya mateso yetu?”

Ali Aabid alibakia kimya kwa muda kisha akasema: “Ewe Ami! Kuna nafasi tukufu kwa ajili yetu Peponi, ambayo kamwe hatuwezi kuipata isipokuwa kwa kufanya subira katika hali hizi ngumu na hata ngumu zaidi ya hizi, na kwa ajili ya Mansur kuna nafasi mbaya kabisa ndani ya moto wa jahannam, ambayo hawezi kuifika isipokuwa kwa kututia katika mateso. Tukiwa na subira punde tu tutajikuta katika wepesi na raha, kwani kifo hakiko mbali na sisi. Lakini ukitaka nitaomba kwa ajili ya nusra yetu, lakini nikifanya hivyo, Mansur hatafikia hatua ile ya uovu, ambayo amepangiwa ndani ya jahannam.”

Aliposikia hivi, Abdullah mara moja alisema “Tutakuwa na subira”. Hazikipita siku tatu, Ali A’abid akafariki dunia huku akiwa katika sijida.

Abdullah alifikiri amelala na akasema “Amka mwanangu” Walivyojaribu kumnyanyua waliona hainuki na ndio wakajua kuwa amekufa.

3. Adui Aliyepangiwa Muumini

Nabii Huud (as) alikuwa akilima. Siku moja kundi la watu lilikuja katika nyumba yake kuja kuonana naye. Mke wake alikuja mlangoni na kuuliza: “Huyo ni nani?”

Walijibu, “Tumetoka katika mji kadha wa kadha, ambao umekumbwa na njaa na tuko katika hatari ya kuangamia. Tumekuja kwa Nabii Hud (as) ili kumuomba aombe dua kwa ajili ya mvua.”

Mke wa Hud (as) alisema: “Kama dua yake ingekuwa ni ya kujibiwa, angejiombea yeye mwenyewe, mazao yake mwenyewe yananyauka kutokana na ukosefu wa maji.”

Waling’ang’ania, “Yuko wapi hivi sasa?”

Aliwajulisha aliko ambapo kundi lile lilimwendea na kuwasilisha ombi lao kwake. Nabii Hud (as) alisali na kisha akaomba dua, baada ya hapo ali- wageukia na kusema, “Mnaweza kurudi kwani imenyesha katika mji wenu.”

Lakini walivyokuwa wanataka kuondoka, walimuuliza, “Tulipokwenda nyumbani kwako tulikutana na mwanamke, ambaye alisema: ‘Ikiwa dua za Hudi zingekuwa zinajibiwa, yeye mwenyewe siangekuwa amejiombea yeye mwenyewe?’”

Nabii Hud (as) akasema, “Mwanamke huyo ni mke wangu na ninamuom- ba Allah ampe maisha marefu.” “Kwa nini unaomba hivyo?” waliuliza wale watu.

Yeye akajibu, “Allah hakuumba muumini (yeyote), ila pia amempangia adui wa kumsumbua. Mwanamke huyu ni adui yangu na adui ambaye mimi niko juu yake, ni bora kuliko adui ambaye (yeye) anakuwa juu yangu.” 3

4. Muhammad Ibn Abi Umair Aliwatumikia Maimam Watatu (As)

Muhammad Ibn Abi Umair alipata fursa ya kuwatumikia Imam Kadhim, Imam Ridha, Imam Jawad (as), na wote Sunni na Shia wameshuhudia uaminifu na uongofu wake.

Alikuwa ni mfanya biashara wa nguo kitaaluma, na kifedha alikuwa tajiri. Aliandika vitabu 94 juu ya hadithi na fiqh. Kutokana na tabia yake njema na ujuzi wake wa majina ya Mashi’a, alikuwa akisumbuliwa sana wakati wa kipindi cha Harun Al-Rashid na Ma’mun, alikuwa akikashifiwa, akitiwa gerezani na mali yake ilipokonywa. Aliombwa awe jaji lakini alikataa ofa hiyo; kwa vile alikuwa anawafahamu Mashi’a wa Iraq, aliombwa kufichua majina yao, lakini alikataa kufichua majina yao, hivyo wakamtupa gerezani na mara nyingi alikuwa akicharazwa bakora nusu ya kufa. Wakati fulani, kwa amri ya Harun Rashid, Sindi Ibn Shaahak alimcharaza bakora 120 na alipaswa kununua uhuru wake kwa kulipa diriham 1000, kifedha alipata hasara ya diriham 100,000 na alibaki kuwa mfungwa kwa miaka minne.

Dada yake (Saidah au Minnah) alikusanya vitabu vyake vyote akavificha, lakini ilitokea siku moja, mvua ikanyesha na vitabu vyake vyote vika- haribiwa. Baadaye, hadithi alizokuwa akisimulia zilikuwa zinatokana na kumbukumbu kali aliyokuwa nayo au nakala ambazo wengine walikuwa wamezinakili kutoka kwenye vitabu vyake vya asili kabla ya kuharibuwa.4

5. Maisha Marefu Huambatana Na Mabalaa

Imesimuliwa kuwa wakati fulani Jibril (as) alimuendea Nabii Suleimani (as) akimletea bakuli lenye maji ya uhai na akamwambia: Mola wako amekupa chaguo ambalo ukilichagua, unaweza kunywa maji haya na kubaki hai hadi siku ya hukumu.

Suleimani (as) aliliweka suala hii mbele ya kundi la watu, majini na wanyama, akawataka ushauri na wote wakamshauri kuwa anywe yale maji na aweze kuwa wa milele.

Suleimani baada ya kutafakari, alibaini kuwa alikuwa hajapata maoni ya nungunungu na hivyo akamtuma farasi akamwite, lakini nungunungu hakuja. Kisha alimtuma mbwa na hapo akaja mara moja!

Suleiman (as) akamwambia, “Kabla sijataka ushauri wako juu ya shauri langu, ningetaka kujua kwa nini nilipomtuma farasi mnyama anaye hes- himiwa zaidi hukuja, lakini nilipomtuma mbwa, mnyama mbaya kuliko wote, uliwasili mara moja?” Nungunungu alijibu, “Farasi licha ya kuwa mnyama anayeheshimika, hana utii, ambapo mbwa licha ya kuwa mnyama mbaya kuliko wote, ana utii; akipokea mkate kutoka kwa mtu, hubakia kuwa mtiifu kwake katika maisha yake yote.”

Kisha Suleiman (as) akasema, “Bakuli lenye maji ya uhai limeletwa kwangu na nimepewa chaguo, ama niyakubali au niyakatae. Wengine wote wamenishauri niyanywe ili niwe wa milele.”

Nungunungu akasema, “Je maji haya ya uhai ni ya kwako tu au watoto wako, familia na marafiki wanaruhusiwa kuyanywa pia?” Akasema, “Hapana! Ni kwa ajili yangu tu.”

Kisha nungunungu akashauri, “Ni busara ukayakataa, kwani utakapopata maisha marefu, watoto wako wote, ndugu na marafiki wataondoka kabla yako, kila siku inayopita itakuwa ikikuletea msiba na huzuni na hivyo kufanya maisha yako kuwa machungu.” Suleiman (as) aliukubali ushauri huu na akauzingatia, (kwa) kuyarejesha maji ya uhai.5

  • 1. Jaamee’al-Akhbaar, uk. 113
  • 2. Dasaataan-ha- Wa panda, Juz, 7 uk. 148: La –aali al- Akhbaar, Juz.1 uk. 346
  • 3. Namunah-e- Ma’arif, Juz. 2 uk.612
  • 4. Mantahal Aamaal, Juz. 2, uk. 358
  • 5. Jawaame’ al-Hikayaat, uk. 95