read

19) Maradhi

Allah, Mwenye hikima, anasema:

“Na ninapougua hunirjeshea afya yangu.”1

Imam Ali (as) amesema: Kibaya zaidi ya umasikini ni maradhi ya mwili.”2

Maelezo mafupi:

Moja ya hazina za pepo, ambazo humfikia muumini katika ulimwengu huu ni maradhi. Ikiwa muumini wakati fulani na bila kukusudia atakosea na kufanya dhambi, Allah hataki (muumini) huyo arudi kwake akiwa amebeba mzigo wa dhambi, hivyo humpatia maradhi ili madhambi yake yasamehewe.

Mtu anayetaabika kwa maradhi humuomba Allah amrejeshee afya yake na Allah huipenda hali hii ya mgonjwa, kwani anataka mja wake aongee na kuwasiliana naye. Wakati mwingine Allah humpatia mtu maradhi ili kulinyanyua daraja lake la kiroho.

Mbora miongoni mwa wale wanaoumwa ni yule anayefanya subira katika mateso haya na kuficha maumivu yake na anajiepusha kulalamika juu ya ugonjwa wake kwa wengine mpaka anarejewa na afya yake na hupata malipo ya juu kabisa aliyopangiwa.

1. Daraja La Muumini Anayeteseka Kwa Mardhi

Siku moja Mtukufu Mtume (saw) alinyanyua kichwa chake mbinguni na kisha akacheka, mmoja wa masahaba zake alimuuliza sababu ya kucheka, ambapo Mtukufu Mtume (saw) alijibu kwa kusema:

“Kicheko changu kimetokana na mshangao. Malaika wawili walikuwa wameteremka kutoka mbinguni kuja kurekodi amali za muumini muongofu, mara zote walikuwa wakimkuta katika msala wa kusalia. Lakini safari hii waliona kwamba hayupo.

Alikuwa kitandani, akiwa amepatwa na maradhi. Walipanda mbinguni na kumuambia Allah: ‘Ewe Mola! Hatukumkuta mja wako katika sehemu yake ya ibada ya kawaida lakini badala yake tumemkuta amelala kitandani katika hali ya maradhi.

“Allah aliwaambia: ‘Hadi atakaporejewa na afya yake rekodini matendo yake yote ya ibada na amali njema alizokuwa akizifanya alipokuwa na afya. Ni wajibu kwetu kumlipa amali zote njema alizokuwa akizifanya alipokuwa na afya njema katika kipindi chote atakachokuwa anaumwa.’”3

2. Binti Yangu Hakupata Kuugua Kamwe!

Wakati fulani, Mtukufu Mtume (saw) alitoa pendekezo la kumuoa mwanamke mmoja. Baba yake alianza kumsifu (binti yake) na huku akieleza sifa zake, akisema: “Tangu alipozaliwa mpaka leo, kamwe hajapata kuugua.” Mtukufu Mtume (saw) aliposikia hivi aliondoka katika mkusanyiko huo.

Baadaye alisema, “Hakuna wema katika mwili ambao, kama punda milia, huwa hauugui. Magonjwa na misiba ni zawadi za Allah kwa waja wake ili wasije wakamsahau, maradhi na misiba husaidia kumfanya mtu amkum- buke (Allah).

3. Subira Katika Maradhi

Abu Muhammad Raqqi anasema: Wakati fulani niliwasili katika hadhara ya Imam Ridhaa (as) na nikamsalimia. Aliitika salamu yangu akauliza juu ya afya yangu na akaanza kuzungumza nami. Katika mazungumzo ghafla akasema: “Ewe Abu Muhammad, kila Mu’mini ambaye Allah humpatia misiba na ambaye hufanya subira, kwa hakika atakuja kupata daraja na malipo ya shahidi mbele ya macho ya Allah.”

Nilishangaa, Ni kwa uhusiano gani Imam (as) alisema hili? Hatukuwa tunazungumzia juu ya majanga na misiba, kwa Imam (as) ghafla kuibuka na aina hii ya kauli?

“Nilimuaga Imam (as) na nikaenda kwa rafiki zangu na wasafiri wenzangu ambapo ghafla nilisikia maumivu katika mguu wangu. Nilikesha na maumivu makali na asubuhi kulipopambazuka niliona kwamba mguu wangu umevimba.

Baada ya muda, uvimbe huu ukawa unauma sana. Nilikumbuka kauli ya Imam Ridha (as) ambapo alikuwa ameshauri subira katika mabalaa na jinsi nilivyokuwa nimewaza kuwa haukuwa umetolewa katika wakati muafaka.

“Katika hali hii nilifika Madina lakini huko, kidonda kikubwa kilikuwa katika mguu wangu, kikawa kinatoa usaha. Maumivu yalikuwa makali sana kiasi kwamba sikuwa na amani. Kisha nikaelewa kwamba Imam (as) alikuwa ameshajua hali hiyo pale alipozungumza nami na kunishauri kuwa mtulivu kwa njia ya subira. Kwa miezi kumi nilikuwa kitandani kutokana na ugonjwa huu.”

Msimuliaji anasema: Baada ya muda Abu Muhammad alirudiwa na afya yake kisha akaugua tena, hatimaye akafariki kwa ugonjwa huo.4

4. Imam Sajjad (As) Awasaidia Wakoma

Wakati fulani Imam Sajjad (as) alikutana na wakoma wakiwa wamekaa kandokando ya barabara na wakila chakula.

Aliwasalimia kisha akapita ghafla tena akasimama na kujisemea: “Allah hawapendi wenye kujivuna.”

Baada ya kusema hayo alirudi nyuma, akawendea wakoma na kusema, “Kwa sasa, nimefunga (na hivyo siwezi kukaa chini na kula nanyi chakula chenu. (Hata hivyo) ninawaalika na kuja nyumbani kwangu na kuwa wageni wangu.”

Waliukubali mwaliko huo na wakaenda nyumbani kwake ambako Imam aliwalisha na akawasaidi kwa kuwapa fedha.5

5. Deni La Mgonjwa Lalipwa

Usama Ibn Zaid alikuwa ni mmoja wa masahaba wa Mtukufu Mtume (saw). Wakati fulani aliugua na hivyo Imam Husein (as) akamtembelea. Alipokaribia, Imam Husein (as) alimuona akiwa katika msukosuko mkubwa, akipiga mayowe mara kwa mara na kuonyesha maumivu makali.

Imam (as) akamuambia, “Ndugu (yangu)! Ni nini kinakufanya uwe na msukosuko huo na uwe na mashaka?”

“Nina mzigo wa deni la dinar 60,000” alijibu. Imam (as) alimfariji kwa kumuambia ninachukua jukumu la kulipa deni lako.

Usamah aling’ang’ania, “Nina hofu nitakufa kabla deni langu halijalipwa.” Imam (as) akasema, “Usiwe na wasiwasi! Nitalipa deni lako kabla ya kifo chako.” Aliposema hivi Imam Husein (as) aliamuru deni lake lilipwe mara moja.6

  • 1. Quran 26:80
  • 2. Nahju’l-Balaghah ya Faidh al-Islam, uk. 1270
  • 3. Daastaan-ha Wa Pand-ha, Juz. 6 uk.130, Tafsirul Nur al- Thaqalain, Juz. 5, uk. 68
  • 4. Hikaayat Shanidani, Juz.1, uk.166; Bihaar al- Anwaar, Juz. 45, uk 51
  • 5. Baa madrum, katika Guneh Barkhod Kuneem, uk 38
  • 6. Paighambar wa Yaara, Juz. 1, uk.193; Bihar aal- Anwaar, Juz. 10, uk.43