read

3) Unyofu

Allah Mwenye hikma, amesema:

فَاعْبُدِ اللَّهَ مُخْلِصًا لَهُ الدِّينَ {2}

“Hivyo muabuduni Allah (peke yake) mkiwa waaminifu Kwake kati- ka dini.” (Quran 39:2)

Imam Ali (as) alisema: “Fanya matendo yako kwa unyofu, kwani (ukifanya hivyo) hata kidogo kitakutosha.1

Maelezo mafupi:

Unyofu ni ufunguo wa kukubaliwa amali zote. Mtu ambaye amali zake zimekubaliwa na Allah hata ziwe ndogo kiasi gani, ni mtu mnyofu na mtu ambaye amali zake zimekataliwa na Allah, licha ya wingi wake, sio miongoni mwa watu wanyofu.

Mtu mnyofu hujitahidi kuitakasa roho yake kutokana na maovu na hujibadilisha kufanya amali njema na kudumisha (unyofu wa) nia ili Allah azikubali amali zake.

Kiwango cha nia, maarifa na matendo yanahusiana na utakaso wa kiroho na usafi (wake), na kama mtu mnyofu angezingatia kikamilifu nafsi yake ya ndani, angeitambua dhana halisi ya upweke wa Allah. Kiwango cha chini kabisa cha unyofu ni wakati mtu anapofanya jitihadi kwa kadiri ya uwezo wake wote, akiwa hatarajii malipo kwa matendo yake wala hayapi umuhimu wowote.2

1. Watu Watatu Katika Pango

Mtukufu Mtume (saw) amesimulia:

“Watu watatu kutoka katika kabila la Bani Israil walikusanyika na wakaan- za safari, walipokuwa njiani, mawingu yalikusanyika na mvua kubwa ikaanza kunyesha na hivyo wakatafuta hifadhi katika pango lililokuwa karibu.

Ghafla jiwe kubwa lilibilingika na kuziba lango la pango, (na hivyo) kuwakwamisha watatu hao ndani na kuubadili mchana kuwa usiku kwa giza. Walikuwa hawana jingine la kufanya isipokuwa kumgeukia Allah kwa msaada.

“Tutumie matendo yetu ya unyofu kama njia ya kupata nusra kutokana na tatizo hili,” alishauri mmoja wao. Wengine wote walikubaliana na ushauri huo. Mmoja wao alisema “Ewe Mola! Unajua kuwa nina binamu yangu anayevutia sana kabisa na kwamba nilivutiwa naye na kumpenda sana, siku moja nilipomkuta akiwa peke yake, nilimchukua na nilitaka kukidhi matamanio yangu ya kimwili, aliposema: ‘Ewe binamu yangu! Muogope Allah na usiuharibu ubikra wangu.’

Niliposikia hivi nilivyunjilia mbali matamanio yangu ya kimwili na nikaamua kutofanya kitendo kiovu. Ewe Mola! Ikiwa kitendo changu hicho kilitokana na unyofu wa kweli na kwa nia ya kupata radhi Zako tu, tunusuru kutokana na huzuni na adhabu. Ghafla waliona kwamba lile jiwe limesogea kidogo, likiruhusu mwanga hafifu kuingia ndani ya pango.

Mtu wa pili alisema: “Ewe Mola! Unajua kwamba nilikuwa na baba na mama, walikuwa wazee sana kiasi kwamba miili yao ilikuwa imepinda kutokana na umri uliopindukia, na kwamba nilikuwa nikiwahudumia kila mara. Usiku mmoja nikiwa nimewaletea chakula, nilibaini kwamba wote walikuwa wamelala. Nilikesha usiku kucha karibu yao, na chakula mkononi, bila kuwaamsha nikihofia kuwasumbua. Ewe Mola! Ikiwa kiten- do changu hiki kilikuwa ni kwa ajili ya kupata radhi na furaha Yako, tufun- gulie njia na tupe wokovu.” Alipomaliza kauli yake, kundi lile lilibaini kuwa jiwe lile lilikuwa limesogea pembeni zaidi.

Mtu watatu aliomba: “Ewe Mjuzi wa yaliyofichikana na yaliyo dhahiri! Unajua mwenyewe kwamba nilikuwa na mfanyakazi aliyekuwa akinifanyia kazi. Mkataba wake ulipokuwa umefikia mwisho, nilimkabidhi ujira wake, lakini hakuridhika na alitaka zaidi na katika hali ya kutoridhi- ka na kutofurahi, aliondoka. Nilitumia ujira wake kununulia mbuzi, na nil- imhudumia tofauti, na punde nikawa na kundi la mbuzi. Baada ya kipindi fulani, yule mfanyakazi alinijia akitaka ujira wake na nikamuonyesha kundi la mbuzi.

Awali alifikiri ninamdhihaki, lakini baadae alipotambua umakini wangu alichukua kundi lote (la mbuzi) na kuondoka.3 Ewe Mola! Ikiwa kitendo hiki kilisukumwa na unyofu na kilikuwa kwa ajili ya kutaka radhi Zako, tuokoe katika mkwamo huu”

Kufikia hapo jiwe lote liliondoka katika lango la pango na wote watatu wakatoka, wakiwa na furaha na msisimko, na wakaendelea na safari yao.4

2. Ali (As) Katika Kifua Cha Amr

Amr Ibn Abd Wuud alikuwa ni mpiganaji ambaye, katika vita alikuwa ni sawa na askari 1000. Katika vita vya Ahzaab, aliwapa changamoto askari wa Kiislamu kupigana naye, lakini hakuna hata aliyekuwa na ujasiri wa kusimama mbele yake hadi Imam Ali (as) alipokwenda mbele ya Mtukufu Mtume (saw) na kuomba ruhusa ya kupigana naye.

Mtukufu Mtume alimuambia Ali (as): “Tambua kuwa huyu ni Amr Ibn Abd Wuud!” Imam Ali (as) kwa unyenyekevu alisema “(Na) mimi ni Ali Ibn Abi Talib,” na kisha akaenda katika uwanja wa vita na kusimama mbele ya Amr.

Baada ya mapambano makali, Imam (as) hatimaye alimuangusha chini na akakaa juu ya kifua chake. Walipoona hivi, jeshi zima la Waislamu lilimuomba Mtukufu Mtume (saw): “Ewe Mjumbe wa Allah, muamuru Ali (as) amuue Amr mara moja!”

“Muacheni kwani anayajua matendo yake vizuri zaidi kuliko mwingine yeyote,” alijibu Mtukufu Mtume (saw).

Ali (as) alipokuwa amekikata kichwa cha Amr, alikileta kwa Mtukufu Mtume (saw) ambaye alimuuliza “Ewe Ali! Ni nini kilichokufanya usite kabla ya kumuua Amr?

Akasema, “Ewe Mjumbe wa Allah! Nilipokuwa nimemwangusha chini, alinikashifu matokeo yake nikapatwa na hasira. Nilihofia kuwa kama ningemuua katika hali ile ya hasira, ingekuwa (nimemuua) kwa ajili ya kijifariji na kuiridhisha roho yangu. Hivyo niliondoka juu yake mpaka hasira yangu ilipokwisha na nikarudi kukitenganisha kichwa chake kutoka katika mwili kwa ajili ya furaha ya Allah na kwa ajili ya kumtii Yeye.”

Ilikuwa ni kwa sababu ya unyofu na pigo lenye thamani kwa upande wa Imam Ali (as) kwamba Mtukufu Mtume (saw) alisema: “Dhoruba la upan- ga wa Ali katika siku ya vita vya Khandaaq ni bora kuliko ibada ya wanadamu wote na majini.”5

3. Shetani Na Mchamungu

Katika kabila la Bani Israil, alipata kuishi mchamungu mmoja. Siku moja watu walimjulisha kuwa katika sehemu fulani, kulikuwa na mti uliokuwa ukiabudiwa na watu wa kabila hilo. Aliposikia hivi, aliruka kwa hasira, akachukuwa shoka yake na kuondoka kwenda kuukata mti ule.

Ibilisi, akatokea mbele yake kwa sura ya mtu mzee, alimuuliza, “Unakwenda wapi?” alijibu “Nina kusudia kukata mti ambao unaabudiwa ili badala yake watu wamuabudu Allah.”

“Jizuie mpaka utakaposikia nitakayoyasema.” Ibilisi alisema kumuambia yule Mchamungu. Yule Mchamungu akamuambia aendelee kusema. Ibilisi aliendelea: “Allah ana mitume, wake kama ingekuwa ni muhimu kuuan- gusha mti angekuwa amewatuma kuja kufanya kazi hiyo.” Lakini, Mchamungu hakukubaliana na Ibilisi na akaendelea na safari yake.

“Kwa vyovyote vile sitakuruhusu” ibilisi alisema kwa hasira na akaanza kupigana mieleka na mtu yule, katika mpambano huo mchamungu alimb- waga ibilisi chini. “Subiri nina kitu cha kukuambia” alisihi ibilisi “Sikiliza! Wewe ni mtu masikini kama ungekuwa na mali ambayo kwayo ungetoa zaka kwa waumini wengine ingekuwa bora zaidi kuliko kukata mti. Ukijizuia kukata mti, nitaweka dinari mbili chini ya mto wako kila siku.”

Mchamungu akasema huku akiwaza: “Ikiwa unasema ukweli, nitatoa dinari moja kama sadaka na nitaitumia dinari nyingine.

Hili ni bora kuliko kukata mti katika hali yoyote, sijatumwa kufanya kazi hii wala mimi sio Mtume mpaka nijitwishe mzigo wa huzuni na mashaka yasiyo ya lazima.” Hivyo alikubaliana na ombi la ibilisi na akamuacha.

Kwa siku mbili, alipokea dinari mbili na akazitumia, lakini katika siku ya tatu, hapakuwa na dalili ya fedha. Akiwa ameudhika na kusononeka, akachukua shoka yake akatoka kwenda kukata ule mti.

Njiani alikabiliana na shetani, aliyemuuliza: “Unaelekea wapi?

“Ninakwenda kukata ule mti.”

“Kwa vyovyote huwezi kwenda kufanya hivyo” alisema shetani.

Kwa mara nyingine tena walianza kupambana lakini mara hii ibilisi alimzi- di nguvu na akamwangusha chini, (kisha) akamuamuru, “rudi nyuma sivyo nitatenganisha kichwa na kiwiliwili chako.” Mchamungu alisema, “Niache na nitarudi, lakini niambie ilikuwaje nikaweza kushinda katika tukio la awali?”

Ibilisi alijibu: “Katika tukio lile umetoka kwa ajili ya Allah na ulikuwa na ikhlasi katika nia yako na matokeo yake Allah akanidhoofisha kwa ajili yako, lakini safari hii ulikasirika kwa ajili ya nafsi yako mwenyewe na dinari zako na hivyo nikaweza kukuzidi nguvu.”6

4. Siri Ya Mtumwa Muaminifu

Sa’eed Ibn Musayyab anasimulia: “Mwaka mmoja, kulikuwa na njaa kali na hivyo watu walikusanyika pamoja ili kuomba dua kwa ajili ya mvua. Nilitazama hivi na macho yangu yakamuangukia mtumwa mweusi aliyekuwa amejitenga na umati wa watu na akaibukia kwenye kilele cha kilima kidogo. Nilikwenda katika uelekeo alipokuwa na nilipomkaribia, nilibaini kwamba midomo yake ilikuwa ikijongea (akisoma) dua. Alipomaliza tu dua yake, wingu lilikusanyika angani. Alipoona wingu, mtumwa alimsifu Allah na akaondoka. Mara tu mvua ikatupiga sana mpaka tukafikiri kuwa tunaweza kuangamia. Nilimkimbilia mtumwa yule nikaona kwamba ameingia katika nyumba ya Imam Sajjad (as). Niliwasili mbele ya Imam (as) na nikasema:

“Ewe bwana wangu! Katika nyumba yako kuna mtumwa mweusi; tafad- hali niuzie” Akasema, “Ewe Sa’eed! Kwa nini badala yake nisikupe kama zawadi?” Na akamuamuru mkuu wa watumwa kuwaleta watumwa wote mbele yake. Walipokuwa wamekusanyika, nilibaini kuwa mtumwa mweusi hakuwa miongoni mwao. Nikasema, “Ninayemtaka hayupo hapa.” Imam (as) akasema hakuna mtumwa aliyebaki isipokuwa mmoja. Kisha akaamuru akaletwe, mtumwa huyo alipoletwa mbele yangu niliona kuwa ndiye mtu mwenyewe niliyekuwa nikimtafuta na hivyo nikasema: “Huyu ndiye ninayemhitaji!”

“Ewe mtumwa! Kuanzia sasa, Sa’eed ni bwana wako na nenda naye” aliagiza Imam (as). Mtumwa akanigeukia na kusema, “Ni nini kilichokusukuma unitenganishe na bwana wangu?” Nikajibu, “Niliposhuhudia dua yako ya mvua ikijibiwa nilitamani kukumiliki.” Aliposikia hivi, mtumwa alinyoosha mikono yake kwa ajili ya dua na akigeuzia uso wake angani akiom- ba: “Ewe Mola wangu! Hii ilikuwa ni siri baina yangu na wewe. Sasa kwa vile umeivujisha, nipatie kifo na unichukue kwako.”

Imam (as) na wote waliokuwepo walibubujikwa na machozi kutokana na hali ya mtumwa, huku nikitokwa na machozi nilitoka nje ya nyumba. Nilipofika nyumbani kwangu tu, mjumbe wa Imam (as) alifika na kusema, “Njoo kama unataka kushiriki katika mazishi ya sahibu yako.” Nilirudi nyumbani kwa Imam (as) pamoja na yule mjumbe na kukuta mtumwa ameshafariki.7

5. Ombi La Nabii Musa (As)

Nabii Musa alipata kumuomba Allah:

“Ewe Mola! Ni utashi wangu kumuona kiumbe wako aliyejitakasa kwa ajili ya ibada Yako na ambaye hajachafuliwa katika utii wake Kwako” Aliambiwa: “Ewe Musa! Nenda katika fukwe za bahari fulani ili nikuonyeshe unachotaka kukiona”

Nabii Musa alikwenda mpaka akafika karibu na bahari. Alipotazama pem- beni, aliona kuwa tawi la mti lililokuwa limeinamia juu ya maji, alikuwa amekaa ndege, akiwa amezama katika kumdhikiri Allah. Musa alipo- muuliza ndege (habari zake), ndege alisema: “Tangu Allah aliponiumba, nimekuwa katika tawi hili, nikimuabudu Yeye na dhikiri. Kwa kila dhikiri yangu moja hutokea dhikiri 1000 nyingine, na furaha ninayoipata kutokana na dhikiri ya Allah hunipatia virutubisho.”

“Je unatamani kitu chochote katika ulimwengu huu?”Aliuliza Musa (as). “Ndio. Ninatamani sana kuonja tone moja la maji kutoka kwenye bahari hii.” alijibu ndege Musa (as) akasema kwa mshangao “Lakini hakuna umbali mkubwa kati ya mdomo wako na maji! Kwa nini hutumbukizi mdomo wako ndani (ya maji) na kunywa?” Ndege akajibu, “kutokana na hofu kwamba isije ikawa raha inayotokana na maji ikanifanya nisahau raha ya kumdhukuru Mola wangu.” Aliposikia hivi, Nabii Musa (as) alishika kichwa chake kwa mshangao mkubwa.8

  • 1. Jaame’ al Saadaat Juz. 2, uk. 404
  • 2. Tadhkirah al Haqaaiq, uk 73
  • 3. Katika kitabu Mahaasim imetajwa kwamba ujira wake ulikuwa ni nusu dirham lakini alipokuja kuchukua, alipewa mara 18,000 zaidi!
  • 4. Naamunah-e-ma’arif , Juz.1, uk. 53; Farajun Ba’d al shiddah, uk 23; mahaasin e- Barqi, Juz. 2, uk 253
  • 5. Pand –e- Tarikh, Juz 5, uk. 199; Anwaar al- Nu’maaniyah; Ainal –Hayaah.
  • 6. Namunah-e-maarif, Juz. 1, uk. 54; Ihyaa al- uluum Juz. 4, uk.380; Riyadh al- Hikaaya, uk.140
  • 7. Muntahal Aamal, Juz. 2, uk. 38; Ithbaat al- Wasiyyah (cha Maasudi)
  • 8. Khazinah al- Jawaahir, uk. 318