read

7) Uaminifu

Allah Mwenye Hikma, amesema:

“Hakika Allah anawaamuruni mzirudishe amana kwa wenyewe…1

Imamu Baqir (as) alisema: “Kama muuaji wa Imamu Ali (as) ataweka amana katika miliki yangu, kwa hakika nitairudisha kwake.2

Maelezo mafupi:

Kama kitu chochote kinawekwa amana kwa mtu, kulinda usalama wa kitu hicho ni wajibu, na khiana kuhusiana nacho kumekatazwa, bila kujali kama mwenyewe ni mu’umin au kafiri.

Mtu muaminifu, kwa matokeo ya kulinda salama mali za watu, anakuwa mwenye kunufaika kwa rehema na neema ya Mungu.

Mtu ambaye si muaminifu kwa amana za watu anaweza kufananishwa na mwizi na Mungu humvisha mtu kama huyo kwa umasikini na ufukara.

Moja ya alama za imani kamili ni kuwa muaminifu kwenye amana za watu.

Amana inaweza kuwa katika muundo wa fedha, vitu au hata siri, Shetani humpotosha mtu muaminifu kwa kumsababisha yeye kuwa mwenye khi- ana kwenye amana alizowekewa na watu.

1. Uaminifu Wa Umm Salamah

Wakati Imamu Ali (as) alipoamua kuhamia Iraq na kuishi huko, alimk- abidhi barua zake na hati kwa Umm Salamah, ambaye baadae alizitoa na kumpa Imamu Hasan (as) wakati aliporudi Madina.

Katika hali kama hiyo, wakati Imamu Husein (as) alipoondoka kuelekea Iraq, yeye pia aliweka barua zake na hati katika hifadhi ya Umm Salamah pamoja na maelekezo kwamba aje kumpa mtoto wake mkubwa wakati atakapozihitaji kutoka kwake.

Baada ya kuuawa shahidi kwa Imamu Husein (as), Imamu Sajjad (as) alirudi Madina na Umm Salama akamk- abidhi hati zile.

Umar, mtoto wa Umm Salamah, anasimulia: Mama yangu alisema: ‘Siku moja Mtukufu Mtume (saw), akifuatana na Imamu Ali (as), walikuja nyumbani kwangu na akaniomba nimpatie ngozi ya kondoo. Baada ya kumpatia ngozi hiyo, aliandika vitu fulani katika ngozi hiyo na kuirudisha kwangu pamoja na maelekezo: ‘Yeyote yule atakayetaka amana hii kutoka kwako baada ya kutaja alama hizi, mkabidhi amana hii.’”

Kiasi muda ulivyopita, Mtukufu Mtume alifariki dunia. Muda ukapita na Imamu Ali (as) akawa Khalifa na bado hakuna aliyekuja kudai amana hii.

Umar anaendelea kusema:“Siku ambayo watu walikula kiapo cha utii kwa Ali (as), nilikuwa nimekaa miongoni mwao. Wakati anashuka kutoka kwenye mimbari, macho ya Imamu yakaangukia kwangu ambapo alisema: “Omba ruhusa kutoka kwa mama yako nataka kuonana naye.

“Niliharakisha kwenda kwa mama yangu na mara tu nilipomjulisha ombi la Imamu (as), alitamka kwamba alikuwa akiingoje siku hiyo.

“Imamu (as) aliingia na akamuomba Umm Salamah amkabidhi amana ambayo ina alama fulani. Mama alisimama na kutoa kijisanduku kidogo kutoka ndani ya sanduku kubwa na akamkabidhi. Kisha (mama) alinigeukia na kunishauri: ‘Usije ukamtupa Ali (as), kwani hakuna mwingine kama yeye aliye Imamu wa haki baada ya Mtukufu Mtume (saw).” 3

2. Khiana Ya Muuza Duka

Wakati wa utawala wa Azud al-Daulah Dailami, mgeni mmoja alikuja Baghdad akitaka kuuza kidani chenye thamani ya dinari elfu moja, lakini hakuweza kupata mnunuzi wa kukinunua. Kwa vile alikusudia kusafiri hadi Makka, alianza kutafuta mtu muaminifu ambaye angeweza kuhifadhi salama kidani chake.

Watu wakamuelekeza kwa muuza duka ambaye anajulikana kwa uchamungu wake. Yule mgeni akaweka kidani chake katika dhamana ya muuza duka na akaenda zake Makka.

Wakati aliporudi kutoka Makka, alimuendea muuza duka na akampa zawa- di ambazo amezileta. Kwa mshituko mkubwa wa yule mgeni, muuza duka akajifanya kama vile hamjui na akakataa kuwa na kitu chochote kinachomhusu yeye. Vurugu ikatokea kati yao, matokeo yake ambayo watu walikusanyika na kumtupa mtu yule (mgeni) nje ya duka la ‘mchamungu!’ Yule mtu akawa anamfuata muuza duka yule mara nyingi kudai kidani chake, lakini aliambulia matusi na kashifa.

Mtu mmoja alimshauri kumlalamikia kwa Mfalme Azud al-Daulah Dailami. Akiujali ushauri ule, mtu yule akaandika barua kwa Mfalme, ambaye alijibu:

“Kwa muda wa siku tatu, kaa ukingojea mlangoni kwa muuza duka. Siku ya nne, nitapita pale dukani, na wakati nitakapokusalimu itikia salamu zangu. Siku ifuatayo omba kidani chako kwa muuza duka na kisha nijulishe kitakachotokea.”

Mtu yule akafanya kama alivyoelekezwa. Siku ya nne, Mfalme kwa mbwembwe na hadhi kubwa, alipita dukani pale na punde tu macho yake yalipoangukia kwa mtu yule kutoka Baghdad, alimsalimu. Yule mtu akarudisha salamu. Mfalme, akionesha heshima kubwa na taadhima, alianza kulalamika: “Umekuja kutoka Baghdad lakini hukuona kuwa yafaa kunifanyia heshima ya fursa ya kunitembelea ili nikupatie malazi na kukukirimu.” Yule mgeni akaomba radhi kwa kutomjulisha mfalme kuwasili kwake. Wakati wote, muuza duka na watu waliomzunguka, waliangalia kwa mshangao, wakistaajabu mtu yule ni nani ambaye anaheshimiwa kiasi kile na mfalme. Yule muuza duka akaanza kuhofia maisha yake.

Mara msafara wa mfalme ulipopita, yule muuza duka akamgeukia yule mgeni na akasema: “Ndugu, ni lini hasa ulikuja kuweka kidani chako kwangu? Je, kina alama yoyote? Ngoja niangalie tena, huenda pengine sikuweza kukiona.” Yule mgeni akaelezea kilivyo kidani chake kwa muuza duka, baada ya kutafuta kwa muda mchache alikiona. Alimkabidhi yule mgeni na akasema: “Allah swt. anafahamu ukweli kwamba ilitoka tu akilini mwangu.”

Alipowasili mbele ya mfalme, yule mgeni alielezea kisa chote kwake. Mfalme aliamuru muuza duka akamatwe, alimvalisha kidani kile shingoni mwake, na akampeleka kwenye nyumba ya kunyongea watu. Kisha aka- muuru tangazo lifuatalo kutangazwa katika mji wote:

“Hiyo ni adhabu kwa yeyote anayechukua umiliki wa amana na kisha akakana kuwa nayo. Enyi watu! Chukueni tahadhari kutoka kwenye tukio hili!”

Kisha Mfalme akarudisha kidani kile kwa yule mgeni kutoka Baghdad na akampeleka mjini kwake.4

3. Kuwa Muaminifu Wakati Mtu Akikuamini

Abdullah Ibn Sinaan anasema: “Nilimuendea Imamu Sadiq (as) msikitini wakati ambapo alimaliza kusali sala yake ya Alasiri na alikuwa amekaa chini akielekea Qibla. Nikamuuliza:

‘Baadhi ya magavana na watawala watunaona sisi kuwa waaminifu na kuweka mali zao kwetu, lakini wakati huohuo hawalipi ‘khums’ yake. Je turudishe pesa zao au tuziweke kwa ajili ya matumizi yetu?”

Imamu (as) alijibu mara tatu: “Kwa jina la Mola wa Ka’bah! Hata kama Ibn Muljam, muuwaji wa baba yangu Ali (as) angeweka kitu katika amana kwangu, ningekirudisha kwake wakati wowote akikihitaji.” 5

4. Mchungaji Na Kondoo Wa Myahudi

Katika mwaka wa 7 A.H., Mtukufu Mtume (saw) na jeshi la askari elfu moja na mia sita, walitoka kwenda kuiteka ngome ya Khaibar, ambayo ilikuwa takriban maili 96 kutoka Madina. Askari wa Kiislamu walikuwa wameweka kambi katika jangwa linaloizunguka Khaibar kwa muda lakini utekeji wa ngome ukabakia kwa muda mfupi.

Wakati wa kipindi hiki, walijikuta wenyewe katika wakati mgumu kuhusiana na chakula na maji. Ukosefu wa chakula na njaa kali iliwalazimisha kula wanyama kama punda na farasi, ambao nyama yao hairuhusiwi kuliwa na Uislamu.

Katika mazingira haya, mchungaji mweusi, ambaye anachunga kondoo wa Mayahudi, aliwasili katika hadhara ya Mtukufu Mtume (saw). Alisilimu na kisha akamuambia Mtukufu Mtume: “Hawa kondoo ni za Myahudi kwa hiyo sasa nawakabidhi kwako.”

Mtukufu Mtume (saw) akajibu kwa uwazi: “Kondoo hawa wamewekwa kwenye umiliki wako kama amana, na katika dini yetu imekatazwa kuwa na khiyana kwenye amana ya mtu. Ni wajibu juu yako kuwapeleka kondoo hawa mpaka kwenye mlango wa ngome na kuwarejesha kwa wenyewe.”

Kwa kutekeleza amri hiyo, yule mchungaji aliwakabidhi kondoo wale kwa wenyewe kisha akarudi na kujiunga na jeshi la Waislamu.6

5. Mali Zilizowekwa Kwa Mtukufu Mtume (Saw)

Wakati Mtukufu Mtume (saw) alipohama kutoka Makka kwenda Madina, alimuacha Amirul-Mu’minin mjini Makka ili kwamba aweze kurudisha kwa wenyewe mali zilizowekwa amana kwa Mtume.

Handhalah Ibn Sufiyaan alimuelekeza Umair ibnWa’ail kwenda kwa Ali na akamuambie: “Nimeweka mithqal mia moja za dhahabu kwa Mtukufu Mtume (saw), kwa vile amekimbia kwenda Madina na wewe ni mwakilishi wake hapa, tafadhali nikabidhi mali yangu.” Handhalah aliongeza kwamba kama Ali akitaka ushahidi kuthibitisha madai haya, Makuraish wote watathibitisha ukweli wa madai ya Umair.

Mwanzoni, Umair alisita, lakini Handhalah alimshawishi kwa kumzawadia baadhi ya dhahabu na kidani cha Hind, mke wa Abu Sufiyaan. Umair alik- wenda kwa Ali (as) na akatoa madai hayo na kuongeza kwamba Abu Jahl, Ikramah, Uqbah, Abu Sufiyaan na Handhalah watashuhudia kwa ajili yake.

Imamu (as) akasema: “Ulaghai wao naujifunge kwao wenyewe.” Kisha akamuambia alete mashahidi wake karibu na Ka’bah. Wakati wote walipowasili, alianza kumsaili kila mmoja binafsi na mbalimbali, kuhusu mali iliyowekwa kwenye amana.

“Ilikuwa ni wakati gani ulipoweka mali yako kwa Muhammad (saw)?” Alimuuliza Umair kwanza.

“Ilikuwa ni asubuhi wakati nilipompa dhahabu hiyo na akamkabidhi mtumwa wake.” Alijibu Umair.

Imamu (as) akamuuliza Abu Jahl swali hilo hilo. Akajibu: “Mimi sijui.”

Wakati Abu Sufiyaan alipoulizwa, alisema: “Ilikuwa wakati wa machweo ya jua na aliiweka kwenye mikono yake ya nguo.” Wakati Handhalah alipoulizwa, alijibu: “Aliichukuwa amana hiyo wakati wa Adhuhr na kuiweka mbele yake.”

Wakati Uqbah alipoulizwa, alijbu: “Ilikuwa wakati wa Alasir Mtume alipochukuwa amana hiyo katika mikono yake mwenyewe na akaichukuwa nyumbani kwake.”

Na mwisho, wakati Imamu Ali (as) alipomuuliza Ikrimah, alijibu: “Ilikuwa kweupe na asubuhi mapema wakati Muhammad (saw) alipochukuwa amana hiyo na kuipeleka nyumbani kwa Fatimah (as).”

Kisha Imamu (as) aliwajulisha kupingana kwa maelezo yao na hivyo ulaghai wao ukawa dhahiri. Kisha akamgeukia Umair, alimuuliza: “Kwa nini wakati uliposema uwongo, ulionekena mwenye wasiwasi na uso wako ukapauka?” Umair akajibu: “Kwa jina la Mola wa Ka’bah! Sijaweka amana kitu chochote kwa Muhammad (saw). Ilikuwa ulaghai, Handhalah alinipa hongo, kidani hiki hapa, ni cha Hind, na jina lake limeandikwa juu yake, ni moja ya vitu vilivyowasilishwa kwangu kama hongo.” 7

  • 1. Qur’ani Tukufu 4:58
  • 2. Al-Kafi, Jz. 5, uk. 133
  • 3. Payghambar Wa Yaaraan, Jz. 1, uk. 275; Bihaar al-Anwaar Jz. 6, uk. 942.
  • 4. Pand-e-Taarikh, Jz. 1, uk. 202; Mustraf, Jz. 1, uk. 118.
  • 5. Namunah-e-Ma’arif, Jz. 1, uk. 354; Bihaar al-Anwaar, Jz. 15, uk. 149
  • 6. Daastan-ha Wa Pand-ha, Jz. 8, uk. 114; Sirah Ibn Hisham, Jz. 3, uk. 344.
  • 7. Rahnamaa-e-Sa’adat, Jz. 2, uk. 436; Naasikh al-Tawaarikh – Amirul- Mu’minin, uk. 676.