read

8) Mtihani

Allaha, Mwingi wa Hikma anasema:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ {2}

“Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.”(Quran, 67:2)

Imamu Sajjad (as) amesema: “Allaha aliumba ulimwengi na wakazi wake ili kuwapa mtihani ndani yake.”1

Maelezo Mafupi:

Mtu anakabiliana na aina mbalimbali za mitihani katika ulimengu. Anajaribiwa kwa hofu, njaa, maradhi, kifo cha mpenzi wake wa karibu, hali mbaya ya kifedha, shutuma za uwongo, jirani muovu, na kadhalika na kadhalika.

Kwa vile ulimwengu ni sehemu ya matendo na mitihani, waliobarikiwa na wenye furaha ni wale ambao hawashindwi katika hatua yoyote ya maisha. Katika wakati mmoja, mtu anajaribiwa kwa njia ya utajiri na katika wakati mwingine kwa ufukara. Hupata mafanikio kwa kushukuru wakati wa ukwasi na uvumilivu wakati wa umasikini.

Kila mtu, bila tofauti yoyote, anapasika kwenye majaribio na mitihani ambayo huwa tofauti tu katika ‘aina’ na ‘uzito’ wake. Je, huoni jinsi baadhi ya watu ambao wamezoea kujigamba, hupoteza uvumilivu wao na kushindwa kwa unyonge katika mapambano ya mitihani?

1. Harun Makki

Sahl Khorasani alimuendea Imamu Sadiq (as) na akalalamika: “Kwa nini licha ya haki kuwa upande wako, husimami ukapigana? Hivi sasa kuna Mashia wako mia moja elfu, ambao ukiwaamrisha, mara moja wata- chomoa panga zao kwa ajili ya mapambano.” Imamu (as), kwa nia ya kumpa jibu la vitendo, aliangiza tanuru liwashwe. Kisha akamuamuru Sahl arukie ndani ya moto ule.

Sahl akasema: “Ewe Bwana wangu! Allah akun- yeshee Rehma na neema Zake! Usiniweke ndani ya moto. Nayafuta maneno yangu na vilevile nakuomba uondoe amri yako.”

Wakati uleule, mmoja wa wafuasi waaminifu wa Imamu (as), kwa jina la Harun Makki, aliwasili.

Alivyoingia tu Imamu (as) alimuambia kuvua viatu vyake na atembee ndani ya tanuru lile lenye moto. Mara tu Harun ali- posikia amri ya Imamu (as), aliingia kwenye lile tanuru na kukaa katikati ya moto unaowaka.

Kisha Imamu (as) alimgeukia Sahl na akaanza kumuelezea kwa mukhtasari kuhusu mazingira yaliopo katika Khorosan, kama vile alikuwa kule akishuhudia matukio yakitokea.

Baada ya muda, alimuambia Sahl: “Simama na tazama ndani ya tanuru.” Wakati Sahl alipochungulia, alimuona Harun amekaa akiwa amekunja miguu yake bila madhara ndani ya tanuru, akiwa amezungukwa na moto mkali. “Kuna watu wangapi kama hawa waliopo Khorasan?” Imamu (as) alimuuliza Sahl. “Kwa jina la Allah! Hakuna hata mtu mmoja kama Harun Makki katika eneo la Khorasan.” Alijibu Sahl.

Kisha Imamu (as) alieleza: “Sitasimama kupigana wakati sina hata wafuasi waaminifu watano. (Na kumbuka) tunaelewa sana ni wakati gani tutakaosi- mama na kupigana.”2

2. Bahlul Afanikiwa!

Harun Al-Rashid, Khalifa wa Bani Abbas, alitaka kuajiri jaji katika mji wa Baghdad. Baada ya kushauriana na wajumbe wake wa baraza, ilikubaliwa na wote pamoja kwamba hakuna mwingine ila Bahlul ndiye mwenye sifa za sawasawa kwa nafasi hiyo.

Bahlul aliitwa na nafasi ile akapewa yeye. Lakini Bahlul alikataa kukubali, akisema kwamba hafai kwa nafasi hiyo wala hana uwezo wa kubeba juku- mu hilo. Harun akasema: “Wakazi wote wa Baghdad wanaona kwamba hakuna mwingine isipokuwa wewe ndio unafaa kwa nafasi hii na wewe unakataa.”

Bahlul akaeleza: “Mimi mwenyewe najifahamu kuliko yeyote katika ninyi. Chochote nilichoeleza ima ni cha kweli au ni cha uwongo. Kama sababu niliyotoa ni ya kweli, basi itakuwa sio sahihi kwa mimi kuchukua wadhifa huu wa jaji wakati sina uwezo. Kwa upande mwingine, kama nimekudan- ganya, basi mwongo hastahili kuchukua wadhiufa huu.”

Lakini Harun akasisitiza kwamba Bahalul achukue jukumu hilo. Bahlul aliomba apewe muda wa usiku mmoja ili atafakari juu ya suala hilo. Asubuhi iliyofuatia, Bahlul alijifanya mwendawazimu na akaweka vitu katikati ya miguu yake akakimbia mitaani na katika masoko ya Baghdad, akipiga makele: “Wekeni nafasi kwa ajili ya punda wangu na kaeni kando asije akawapiga mateke.”

Mara tu watu walipoona mwendo wake huu wa kuchekesha, walisema kwamba Bahlul amekuwa mwendawazimu. Wakati Harun Al-Rashid alipojulishwa kuhusu hili, alisema: “Bahlul hakuwa mwenda wazimu; bali ameokoa dini yake na amekwepa makucha yetu.

Amelibuni hili ili kujizuia kutokana na kuingilia katika mambo na haki za watu.”3

3. Abu Hurairah Alishindwa!

Abu Hurairah alisilimu katika mwaka wa 8 A.H. Kwa hiyo alikuwa na Mtukufu Mtume (saw) kwa muda wa miaka miwili tu. Alikufa katika mwaka wa 59 A.H. akiwa na umri wa miaka 78. Abu Hurairah alichukuliwa kama mmoja wa sahaba wa Mtukufu Mtume (saw). Hata hivyo, alishindwa kunufaika kutokana na uswahiba huo mtukufu wa Mtume (saw) na kujikinga na kuboronga na makosa. Kinyume chake, aliitumia vibaya nafasi yake na akijiuza mwenyewe kwa ajili ya anasa za dunia hii.

Abu Hurairah alizoea kughushi hadithi na kuzihusisha na Mtukufu Mtume (saw) ili kupata utajiri. Wakati wa kwanza hili lilipotokea, Khalifa wa pili alimkataza kusimulia hadithi; katika tukio la pili, Khalifa alimuadhibu kwa kumpiga viboko, na katika tukio la tatu, alimfukuza kutoka mjini.

Wakati A’laa, gavana wa Bahrain alipofariki katika mwaka wa 21 A.H., Umar alimteua Abu Hurairah kama gavana kuchukuwa nafasi ya A’laa. Lakini kwa muda mfupi kiasi kikubwa cha pesa (dinari elfu mia nne) ziliingia mifukoni mwa Abu Hurairah. Matokeo yake Umar alimfukuza kutoka kwenye nafasi yake.

Mua’wiyah alikuwa akiwalazimisha baadhi ya masahaba na wafuasi (wa masahaba) kubuni hadith dhidi ya Amirul-Mu’minin, Ali (as) na mmoja wa watu muhimu katika kitendo hiki alikuwa ni Abu Hurairah. Wakati fulani Asbagh Ibn Nubata alimuambia Abu Hurairah: “Kinyume na mafundisho ya Mtukufu Mtume (saw) umewafanya maadui wa Ali (as) kuwa marafiki zako na kuwa na uadui kwake.” Aliposikia hili, Abu Hurairah alivuta punzi kwa ndani sana na akjisemea tu: “Inna lillahi wa inna ilahi raajiu’n.”

Uovu mwingine uliofanywa na Abu Hurairah ulikuwa kwamba, ili kupata utajiri kutoka kwa Mua’wiyah, alifuatana na Mua’wiyah mpaka kwenye msikiti wa Kufah na akapiga paji lake la uso mara nyingi mbele ya mku- sanyiko wa watu, kisha akasema: “Enye watu wa Iraq! Je, mnadhani mimi naweza kumhusisha na uwongo Mtukufu Mtume (saw) na hivyo nijiun- guze mwenyewe katika moto wa Jahannam? Kwa jina la Allah! Nimemsikia Mtukufu Mtume (saw) akisema: ‘Kwa kila Mtume kuna sehemu takatifu (aliyowekewa) na ya kwangu iko mjini Madina, kati ya milima ya E’er na Thaur. Yeyote atakayeanzisha uzushi (bid’a) katika sehemu yangu takatifu, laana ya Allah, malaika na watu wote iwe juu yake.’ Allah ni shahidi yangu kwamba Ali alianzisha uzushi ndani ya sehemu takatifu ya Mtukufu Mtume (saw).” (Allah aliepushilie mbali).

Mua’wiyah alifurahia sana kauli hii kiasi kwamba alimzawadia Abu Hurairah na akamfanya mtawala wa Madina.4

4. Ibrahim (As) Na Muhanga Wa Isma’il (As)

Allah swt. alimuamuru Nabii Ibrahi (as) kumtoa muhanga mwanawe Ismail (as). Alifanya hivyi ili kupima subira ya Ibrahim na utii wake kwa Allah. Kama Ibrahim (as) atafudhu mtihani huu, atakuwa ameonesha kustahiki kwake juu ya baraka na neema ya Allah.

Akiwa amepewa mtoto baada ya miaka mingi ya upweke bila mtoto, aliamriwa na Allah kumtoa muhanga kwa mikono yake mwenyewe kipenzi chake ambaye amekua na kufikia umri wa miaka 13.

Ibarahim (as) akamuambia Ismail (as): “Ewe mwanangu mpendwa! Nimeota nikiwa nakutoa muhanga; unasemaje kuhusu hili?”

“Mpendwa baba! Fanya kama ulivyoamrishwa, na insha-Allah, utanikuta mimi miongoni mwa walio imara.” Alijibu Ismail (as).

Kisha, akaimarisha azimio la baba yake kwa kumshauri: Baba, kifo kinau- ma sana na ninakiogopa sana kiasi kwamba kukifikiria tu hunifanya nisumbuke na kunihuzunisha, hivyobasi, ifunge mikono na miguu yangu kwa nguvu, nisije nikajipiga piga nayo wakati koo langu linakatwa na hivyo kupunguza malipo yaliyokadiriwa kwa ajili yangu. Na kwa nyongeza, kinoe kisu chako kiwe kikali ili kwamba kwa haraka niwekwe kwenye amani. Vilevile, niweke katika hali ambayo uso wangu uelekee chini ya ardhi na sio juu ya mashavu yangu, kwani naogopa kama macho yako yatatazama uso wangu, unaweza ukapatwa na huruma na kukuzuia wewe kutii amri ya Allah swt. Vua nguo zako ili zisipakwe kwa damu yangu na mama asiione damu yangu.

Kama ikiwezekana, mpelekee mama nguo zangu; huwenda zikamliwaza na kumpunguzia huzuni za kifo changu.”

Aliposikia khutba hii, Ibrahim (as) akajibu: “Ewe mwanangu! Kwa hakika wewe ni msaidizi bora kwangu katika kutekeleza Amri ya Allah.”

Ibrahim (as) alimchukuwa mtoto wake mpaka Mina (sehemu ya kutolea kafara), akanoa kisu chake na kisha akafunga mikono na miguu ya Isma’il (as), akamlaza kifudifudi uso wake ukielekea ardhini. Kisha Ibrahim akanyanyua kichwa chake kuelekea mbinguni na akaweka kisu juu ya koo la mwanawe. Lakini, wakati anafanya hivyo alitambua kwamba kisu hakikati. Alipokiangalia akaona kwamba kisu kile kikali kimekuwa butu. Tukio hili lilirudiwa mara nyingi, wakati ghafla sauti ya kimbinguni ilisikika ikisema:“Ewe Ibrahim! Hakika, umefanya kama ulivyoota na umetii amri uliyopewa.”

Jibril alileta kondoo kama mbadala kwa muhanga wa Ismail (as), ambaye hatimaye Ibrahim (as) alimtoa kafara. Kuanzia hapo, ikawa ni desturi kwamba wale ambao wanakwenda kufanya ibada ya Hija kila mwaka laz- ima watoe kafara kwa kuchinja mnyama pale Mina. 5

5. Sa’d Na Mtukufu Mtume (Saw)

Mmoja wa masahaba wa Mtukufu Mtume (saw) kwa jina la Sa’d, alikuwa masikini sana na alichukuliwa kama mmoja wa watu wa Kishubaka (As’habu Suffa).6 Alikuwa akisali sala zake zote nyuma ya Mtukufu Mtume (saw), ambaye alikuwa akihuzunishwa vibaya na umasikini wa Sa’d. Siku moja, Mtukufu Mtume (saw) alimuahidi kwamba, kama akipa- ta pesa, atampa yeye Sa’d. Muda ulipita na hakuna pesa iliyokuja kwa Mtukufu Mtume (saw), ambaye alihuzunika zaidi kwa hali ya Sa’d. Ilkuwa wakati huo Jibril alishuka kutoka mbinguni na kuleta dirham mbili.

Akamuambia Mtukufu Mtume (saw): “Allah amesema: Tunafahamu huzu- ni yako kuhusiana na umasikini wa Sa’d. Kama unataka aondokane na hali hii, mpe hizi dirham mbili na muambie ajishughulishe na biashara.”

Mtukufu Mtume (saw) alichukuwa zile dirham mbili na akaondoka nyumbani kwenda kusali Sala ya Adhur alimuona Sa’d anamsubiri karibu ya moja ya vyumba vya msikiti. Wakati alipomgeukia, Mtukufu Mtume (saw) alimuuliza: “Je, unaweza kujishughulisha na biashara?” “Kwa jina la Allah! Sina mtaji wa kufanya biashara,” alijibu Sa’d. Mtukufu Mtume (saw) alimkabidhi zile dirham mbili na akamuambia aanze biashara na mtaji huu. Sa’d alichukuwa pesa ile na akasali Sala yake ya Dhuhr na Asr kisha akaondoka kwenda kuchuma riziki yake.

Allah alimbariki sana katika hali ambayo kila alichonunua kwa dirham moja, alikiuza mara mbili ya alivyonunua.Hatimaye, hali yake ya kifedha pole pole ikaimarika. Hili liliendelea mpaka mwishowe akanunua duka karibu na msikiti na akaanza kuendesha biashara yake pale.

Jinsi biashara yake ilivyopanda juu, alianza kuwa mzembe kuhusiana na utekelezaji wa ibada zake, hata ikafikia kiasi kwamba wakati Bilal anapoadhini hawi tayari kwa ajili ya Sala. Kabla ya hapo alikuwa tayari kwa ajili ya sala hata kabla ya dhana! Wakati Mtukufu Mtume (saw) alipoona kuchelewa kwa Sa’d katika Sala, alimuambia: “Sa’d ulimwengu huu umekufanya kuwa mwenye shughuli sana kiasi kwamba umekuachisha mbali na Sala zako!”

Sa’d akajibu: “Nifanye nini? Kama nikiacha mali yangu bila kuangaliwa, itapotea na nitaishia kwenye hasara. Kutoka kwa mtu mmoja, ni lazima nikakusanye pesa kwa bidhaa zilizouzwa, ambapo kwa mtu mwingine laz- ima nichukuwe umiliki wa bidhaa zilizonunuliwa.”

Mtukufu Mtume (saw) alikerwa sana na kujishughulisha mno kwa Sa’d na utajiri wake na upuuziaji wake kuhusiana na utekelezaji wake wa ibada. Wakati huo huo Jibril alishuka na kusema: “Allah anasema: Tunafahamu huzuni yako. Ni ipi katika hali hizi mbili unayopendelea kwa Sa’d?” Mtukufu Mtume akasema hali ya kwanza ni yenye manufaa kwa Sa’d. Jibril akakubali: “Ndio, mapenzi ya dunia humfanya mtu kuwa asiyejali Akhera. Zichukuwe zile dirham mbili ulizompa hapo mwanzo.”

Mtukufu Mtume (saw) alimuendea Sa’d na akamuambia ikiwezekana arudishe zile dirham mbili ambazo alimpa. Sa’d akamuambia: “Kama unataka, nitakupa hata dirham mia mbili.” Mtukufu Mtume (saw) akasema: “Hapana, nipe tu zile dirham mbili ulizochukuwa kutoka kwangu.”

Sa’d akakabidhi pesa zile kwa Mtukufu Mtume (saw) na kwa muda mfupi, hali yake ya kifedha ikarudia palepale pa mwanzo na kabla ya muda mrefu kupita alijikuta yuko kwenye hali yake ya mwanzo.7

  • 1. Al-Kafi, Jz. 8, uk. 75 (Toleo jipya)
  • 2. Hikaayat-ha-e-Shanidani, Jz. 4, uk. 65; Safinah al-Bihaar, Jz. 2, uk. 714.
  • 3. Panda-e-Taarikh, Jz. 1, uk.181; Raudhaat al-Jannaat, uk. 36; Gharaaib al- Akhbaar cha Sayyid Ne’matullah Jazaairi.
  • 4. Paighambar Wa Yaaraan, Jz. 1, uk. 154-166.
  • 5. Taarikh-e-Anbiya, Jz. 1, uk.164-169.
  • 6. Hawa ni watu ambao walikuwa hawana nyumba za kwao wenyewe, na hivyo wanaishi katika sebule au vyumba vya Msikiti wa Madina (Masjidu’n-Nabi).
  • 7. Daastaanha, Wa Pand-ha, Jz. 2, uk.78; Hayaat al-Qulub, Jz. 1, uk. 578.