read

10. Kuzuiwa Maji

Muawiyah alikuwa akitawala Syria kama gavana wake kwa muda uliokaribia miaka kumi na sita; na alikuwa akipanga kwa siri kunyakuwa ukhalifa akitumia vizuri kila fursa iliyowezekana. Kisingizio chake kizuri cha yeye kuasi dhidi ya Mamlaka Kuu na kutangaza ukhalifa wake mwenyewe kilikuwa ni kuuawa kwa Khalifa Uthman. Muawiyah haku- fanya lolote kuhusiana na maombi ya Uthman alipotaka msaada alipokuwa hai bado. Bila shaka alikuwa akisubiri auwawe ili aweze kutumia nafasi hiyo kama kisingizio cha mpango wake. Uthman akauwawa na Muawiya aliamua kutumia fursa ya hali hiyo kwa lengo lake mwenyewe.

Kwa upande mwengine, watu baada ya kuuliwa Uthman, walijikusanya nyuma ya Ali (a.s) (ambaye kwa sababu fulani alisita kuchukua jukumu la ukhalifa) na wakatangaza kiapo chao cha utii kwake. Ali (a.s) alipotizama na kuona jukumu hilo sasa limegeuziwa kwake rasmi, alikubali na ukhali- fa huo ukatangazwa rasmi mjini Madina, ambao ulikuwa mji mkuu na kituo cha ulimwengu wa kiislamu enzi hizo. Maimbo yote yaliyokuwa chini ya utawala wa kiislamu yalikubali kumtii – isipokuwa Syria uliokuwa chini ya uongozi wa Muawiyya. Alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Ali (a.s). Na kumtuhumu Ali (a.s) kuwa aliwapa hifadhi wauwaji wa Uthman. Muawiyya aliandikisha idadi kubwa ya wapiganaji wa Syria na akajiandaa kutangaza uhuru wa jimbo lake.

Baada ya kumaliza maswala ya vita vya Jamal (ngamia), Ali (a.s) alielekeza nadhari yake kwa Muawiyah. Alimuandikia barua kadhaa, bila mafanikio. Pande zote mbili zilisogeza askari kwa kukaribiana. Abul Aawar Salmi ndiye aliongoza kikosi kilichosonga mbele upande wa Muawiyah na Malik Ashtar upande wa jeshi la Ali (a.s). Walikutana ufuk- weni mwa mto Furat.

Maelekezo yake Ali (a.s) kwa mkuu wa jeshi lake yalikuwa kwamba wao wasiwe wa kwanza kushambulia. Lakini Abul Aawar alifanya shambulizi kali kwa nia ya kuwatia hofu jeshi la Ali (a.s). Hapo Malik akawarudisha nyuma kabisa wapiganaji wa jeshi la Syria. Salmi alianza kufikiria mkakati mpya. Alikwenda hadi Ghat, mteremko kwenye ukingo wa Furati, sehemu pekee iliyokuwa bora ya kupatia maji. Aliwasambaza warusha mikuki na mishale wake kwenye eneo hilo na kuwazuia Malik na wanajeshi wake kukaribia sehemu hiyo. Baada ya muda mfupi Muawiyah aliwasili na jeshi kubwa. Muawiyah alifurahishwa sana na hatua ya mkuu wa jeshi lake na akaamua kuongeza idadi ya wanajeshi wanaolinda eneo la njia ya kufikia mto huo.

Wanajeshi wa Ali (a.s) waliwekwa kwenye dhiki kutokana na upungufu wa maji. Muawiyah kwa furaha tele alisema: “Huu ndio ushindi wetu wa kwanza.” Ila mtu mmoja tu, Amr bin Al-Aas, waziri muerevu wa Muawiyah hakufikiria kuwa hiyo ilikuwa sera nzuri. Kwa ule upande mwengine, Ali (a.s) mwenyewe alikuwa amewasili na kupashwa habari kuhusiana na hali iliyojiri. Alimtuma Saasa’a na barua kwa Muawiyah, ikimjulisha:

“Sisi tumefika hapa, lakini vyovyote iwezekanavyo hatutaki vita vya kuuwana baina ya Waislamu. Kwa kweli tunatarajia kusuluhisha tofauti zetu kwa mazungumzo na maelewano. Lakini tumeshuhudia kuwa wewe na wafuasi wako mumeanza kutumia silaha za uharibifu kabla ya kujaribu lolote. Isitoshe umewanyima maji watu wangu. Waelekeze watu wako kuacha wafanyalo, ili tuweze kuanza mazungumzo. Bila shaka kama ham- taki lolote ila vita sisi hatuogopi.”

Muawiyah aliposhauriana na washauri wake, fikra ya jumla iliyokuwepo ni kutumia hiyo fursa adimu ya kipekee na kupuuza hiyo barua. Amr bin Al- Aas peke yake ndiye aliyepinga fikra hiyo. Alisema, “Mnakosea, ukweli ni kwamba Ali (a.s) na watu wake hawataki kuanza wao vita, na ndio maana wamenyamaza kimya kwa sasa na kujaribu kuwahimiza mubadili mipangilio yenu kwa kupitia barua hii. Msidhani kuwa watarudi nyuma kama mtapuuza barua yao na muendelee kuwanyima maji. Kwa sababu hapo sasa watachukua silaha na hawatatosheka hadi watakapowatoa kwa fedheha kwenye mto Furati.”

Lakini wengi wa washauri wa Muawiyah walionelea kuwa kuwanyima maadui maji kutawadhoofisha na kuwalaz- imisha kurudi nyuma. Muawiyah mwenyewe alikubaliana sana na wazo hilo. Mjadala huo ulifika kikomo. Sa’asa aliomba majibu; Muawiyah, aki- tumia mbinu ya ucheleweshaji alimwambia kuwa atatuma majibu baadaye. Kisha aliwaagiza wanajeshi wake wanalinda maji yale wawe makini zaidi na wazuie kuja na kuondoka kwa wanajeshi wa Ali (a.s).

Maendeleo haya yalimsikitisha Ali (a.s), kwa sababu yaliondoa matumaini yote ya kumaliza hali hii kwa amani kwa njia ya mazungumzo, na ilionye- sha kuwa upande wa pili hauna nia nzuri. Iliyobaki hivi sasa, ni kutumia mabavu. Ali (a.s) aliwahutubia wanajeshi wake hotuba fupi nzito, iliyokuwa na madhumuni yafuatayo:

“Watu hawa wameanza dhulma na kufungua mlango wa mgogoro na kuwakaribisha kwa uhasama. Wana njaa ya vita na wanadai vita na umwa- gaji damu kutoka kwenu. Wamewanyima maji. Hivi sasa inawabidi mch- ague moja kati ya hizi njia mbili, hakuna ya tatu. Ima mkubali kudhalil- ishwa na kuonewa na mbaki na kiu kama mlivyo, ama mtoe kiu cha mapanga zenu kwa damu zao chafu ili hatimae muondoe kiu chenu na maji yale matamu. Kifo ni kuishi maisha ya kushindwa na udhalilifu, na uhai ni kuwa mshindi hata kama ni kwa gharama ya kifo. Kwa hakika, Muawiyah amekusanya idadi kubwa ya wajinga na waliopotoka; na anatumia vizuri fursa ya ujinga wao, hivyo kwamba wameweka shingo zao kwa shabihio la mishale ya kifo.”

Khutba hii iliwatingisha wanajeshi wa Ali (a.s) na kufanya damu yao ichemke. Walifanya shambulio kali kiasi cha kuwalazimu wanajeshi wa Muawiyah kurudi nyuma na wao wakuchukua umiliki wa sehemu ile.

Amr bin Al-Aas (ambaye utabiri wake hivi sasa unaonekana wa kweli) alimwambia Muawiyah: “Wakati huu kama Ali (a.s) na wanajeshi wake watakulipa na ile sarafu yako mwenyewe (vitendo vyako) utafanyaje? Je! Waweza kuitwaa tena sehemu ile kwa mara ya pili kutoka kwao?” Muawiyah alimuuliza, “Kwa mtazamo wako, Ali atashughulika vipi nasi sasa?”

“Naamini, Ali hatofanya kama vile ulivyofanya wewe. Yeye hatotunyima maji. Yeye hakuja hapa kwa matendo kama haya.”

Wanajeshi wa Ali (a.s) baada ya kuwatoa wanajeshi wa Muawiyah kutoka sehemu ile (Ghat), walimuomba Ali (a.s) ruhusa ya kupalinda na kuzuia maadui kuteka maji. Ali (a.s) aliwaambia, “Msiwanyime maji. Hii ni mbinu ya wajinga. Siruhusu mikono yangu kufanya vitendo kama hivyo. Nitakwenda kujadiliana nao kwa misingi ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t). Lau watakubaliana na mapendekezo yangu, ni vema na kheri; na lau watakataa, nitapigana nao, lakini kiungwana na si kwa kuwanyima maji. Sitoweza kamwe kufanya jambo kama hilo na sitawadhulumu kwa kuwawekea upungufu wa maji.

Baada ya muda usio mrefu baadaye wanajeshi wa Muawiyah walikuwa wakija sehemu hiyo na wakiteka maji bega kwa bega na wanajeshi wa Ali (a.s), na hakuna yeyote aliyewazuia.