read

18. Soko La Magendo

Waliomtegemea Imam Ja’far Sadiq (a.s) waliongezeka kwa idadi na matumizi yake pia. Imam huyo aliamua kuwekeza kiasi cha pesa kwenye biashara ili aweze kutimiza mahitaji yake ya nyumbani yaliyoongezeka. Aliandaa kiasi cha dirham elfu moja ambazo alimpa mtumwa wake aliyeitwa “Musadif” akimuelekeza aende Misri akawekeze pesa hizo kwenye biashara kwa niaba ya Imam.

Musadif alinunua bidhaa ambazo kwa kawaida hupelekwa Misri, na alijiunga na msafara wa wafanyabiashara ambao walikuwa wakipeleka bidhaa kama hiyo Misri.

Walipofika karibu na Misri walikutana na msafara mwingine ukitoka huko. Waliulizana juu ya habari za kila mmoja wao. Walipokuwa wakizungumza waligundua kuwa bidhaa ambazo Musadif na wenzake walikuwa wamebeba hazipatikani huko Misri na zilikuwa zinahitajika kwa wingi. Walifurahi sana kwa bahati yao njema. Kwa hakika hiyo ilikuwa ni bidhaa inayotumika sana, na watu walilazimika kuinunua kwa bei yeyote.

Wafanyabiashara hao waliposikia habari hizo njema waliamua kutumia fursa hiyo na wakakubaliana kwa pomoja kuuza bidhaa hizo kwa faida ya asilimia mia moja.

Walipoingia kwenye mji hali ilikuwa kama walivyokuwa wameelezwa. Na kulingana na walivyopatana mwanzo, walianzisha soko la magendo, na hawakuuza bidhaa hiyo chini ya mara mbili ya walivyonunua.

Musadif alirudi Madina na jumla ya faida ya Dirham elfu moja. Kwa fura- ha aliyokuwa nayo alimuendea Imam Sadiq (a.s) na kumkabidhi mifuko miwili, kila mmoja ukiwa na dirham elfu moja. Imam aliuliza: “ Ni nini hii?’

“Mfuko mmoja unawakilisha pesa za mtaji wa biashara ulionipa, na huo mwingine (ambao ni sawa na mtaji) ni faida niliyopata”

“Kwa kweli faida hii ni ya juu zaidi kuliko tulivyotarajia. Nieleze ni vipi ulivyoweza kupata faida kubwa kama hii?”.

“Ukweli ni kwamba wakati tulipopata taarifa karibu na Misri kwamba bidhaa tuliyokuwa tumebeba ilikuwa adimu huko, inahitajika kwa wingi, tukakubaliana tusiuze chini ya mara mbili ya bei yake, na tukafanya hivyo.”

“Mungu Wangu Mtukufu! Ulifanya kazi kama hiyo! Mlikula kiapo cha kuunda soko la magendo miongoni mwa Waislamu? Mliapia kutouza bidhaa hiyo chini ya mara mbili ya bei uliyonunua nayo? Hapana, sitaki biashara kama hiyo na wala faida kama hiyo!!

Kisha Imam akichukua mfuko mmoja, akasema, “Huu ndio mtaji wangu.” Na huo mfuko mwingine hakuugusa kabisa na akasema yeye hakutaka kuwa na uhusiano wowote nao.

Kisha akasema: “Ewe Musadif! Ni rahisi kupigana kwa upanga kuliko kuchuma riziki kwa njia ya halali.”