read

19. Pesa Zilizo Barikiwa

Kwa kutumwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w), Imam Ali (a.s) alikwenda kumnunulia kanzu. Imam alikwenda sokoni na akanunua kanzu ya dirham kumi na mbili. Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimuuliza: “Umenunua kwa dirham ngapi?”

“Dirham kumi na mbili”

“Sikuitaka kama hiyo. Nataka ambayo ni bei rahisi kabisa. Muuzaji atairudisha kweli?”

“Sijui ewe Mtume wa Allah.”

“Tafadhali nenda na uone kama atakubali kuirudisha.” Ali (a.s) aliichukua kwa muuzaji na kumuambia:

“Mtume wa Allah anataka kanzu ya bei nafuu; utakubali kuichukua na kunirejeshea pesa?”

Muuzaji alikubali kufanya hivyo na kumpa Ali (a.s) pesa. Imam Ali (a.s)

alichukua pesa hizo na kumpa Mtume (s.a.w.w). Baadaye walikwenda sokoni pamoja. Walipokuwa njiani Mtume (s.a.w.w) alimuona msichana mjakazi, ambaye alikuwa akilia. Alimuendea na kumuuliza:

“Kwa nini unalia?”

“Tajiri yangu amenipa dirham nne niende kununua vitu kutoka sokoni. Sijui pesa hizo zilipotea vipi. Sasa nahofia kwenda nyumbani.”

Katika zile dirham kumi na mbili, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimpa dirham nne yule msichana na akamuambia; “Nunua ulichokuwa unataka ununue na urudi nyumbani.” Mtume (s.a.w.w) mwenyewe alikwenda sokoni na baada ya kununua kanzu kwa dirham nne, akaivaa.

Alipokuwa akirundi nyumbani alimuona bwana mmoja ambaye alikuwa hajavaa nguo. Kwa haraka alivua ile kanzu na akampa. Kisha alimrudia muuzaji na akununua kanzu nyingine ya dirham nne akavaa. Njiani alimuona tena yule msichana mjakazi akiwa ameketi huku akiogopa na kuwa na wasiwasi. Alimuuliza:

“Kwa nini haujakwenda nyumbani?”

“Ewe Mtume wa Allah nimechelewa sana na naogopa huenda watanipiga na kuniuliza kwa nini nimechelewa hivi.”

“Nieleze unapoishi na unifuate ili nikawaombe kwamba wasikuulize kitu chochote.” Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimchukua yule msichana na walipofika karibu na nyumba hiyo, msichana alisema ; “Nyumba ndio hii.” Kwa sauti ya juu Mtume wa Allah (s.a.w.w) alisema:

“Amani iwe juu yenu enyi watu wa nyumba hii.”

Hakupata jibu lolote; aliwaamkia kwa mara ya pili hakupata majibu pia. Aliamkia kwa mara ya tatu na hapo ndipo kila mtu alijibu akisema:

“Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yako ewe Mtume wa Allah.”

“Kwa nini ninyi watu hamkunijibu mara ya kwanza?” Hamkusikia sauti yangu?”

“Ndio! baada ya kusikia sauti yako mara ya kwanza tu, tulijua kuwa ni wewe.”

“Na sababu zipi zilizowafanya mchelewe kunijibu?”

“Ewe Mtume wa Mungu tulipendezewa kusikia sauti (salamu) yako mara kwa mara. Salamu yako ni yenye kheri, amani na baraka kwetu sisi.”

“Msichana huyu mtumwa wenu amechukua muda mrefu kurudi. Hivyo basi nimekuja kuwaomba kwamba msimuadhibu.”

“Ewe Mtume wa Mungu, kwa baraka za kuja kwako wewe kwenye neema hapa kwetu tumemuacha huyu msichana huru.” Mtume wa Mungu akasema ; “Shukurani mara milioni moja zimuendee Allah. Zinabaraka iliyoje hizi dirham kumi na mbili? Watu wawili wasio na nguo wamepata mavazi na pia mtumwa wa kike ameachwa huru.