read

2. Juwaibir Na Zalfa

“Ingelipendeza kiasi gani lau ungeliowa na ukaanzisha familia, na iwe ndio mwisho wa maisha ya ukiwa na upweke? Na hivyo ungeliweza kutimiza mahitaji yako ya kimaumbile na vile vile yeye angelikusaidia kufikia mahi- taji na malengo yako ya kidunia na ya kiroho.”

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi sina mali wala sura ya kupen- deza, wala sijatoka kwenye ukoo wenye heshima au nasaba. Ni nani atakayekubali kuolewa nami? Na ni mwanamke yupi apendae kuwa mke wa mtu masikini, mfupi, mweusi na mwenye sura mbaya kama mimi?”

“Ewe Juwaibir! Mwenyezi Mungu alibadilisha thamani ya watu kupitia Uislamu. Watu wengi walikuwa wamepewa vyeo kwenye jamii zili- zokuwepo kabla ya Uislamu, na dini ya kiislamu ikawashusha. Wengi walikuwa wamedharauliwa na kuonekana si chochote, na dini ya kiislamu ikawapa heshima na hadhi kubwa na kuwainua. Uislamu umeondoa ubaguzi na ufakhari wa kiukoo uliokuwako usiyo wa kiislamu.

Hivi sasa watu wote ni sawa bila kuzingatia rangi zao na sehemu walizotoka. Hakuna yule mwenye ubora juu ya wengine ila tu kwa kumuamini na kum- cha Mwenyezi Mungu (s.w.t). Miongoni mwa waislamu, mtu ambaye maadili na vitendo vyake ni bora zaidi kushida vyako ndiye mmbora wako. Hivi sasa fanya kama ninavyokwambia.”

Maneno haya yalizungumzwa siku moja baina ya Mtume (s.a.w.w) na Juwaibir, wakati Mtume (s.a.w.w) alikuja kuwaona watu wa “Suffa.”

Juwaibir alikuwa mwenyeji wa “Yamamah” sehemu ambayo alijulia habari za Bwana Mtume (s.a.w.w) na kuwasili kwa dini ya Kiislamu. Yeye alikuwa ni masikini, mweusi na mfupi, lakini wakati huo huo alikuwa ni mwerevu wakutafuta ukweli na mtu mwenye uamuzi. Alikuja Madina ili kutazama Uislamu kwa karibu na kwa muda mfupi alisilimu na kufuata Uislamu.

Kwa vile hakuwa na hela, nyumba wala marafiki, kwa kipindi fulani alikuwa akipata malazi msikitini pamoja na Waislamu wengine masikini kwa idhini ya Mtume (s.a.w.w). Na pindi Mtume (s.a.w.w) alipo- julishwa kuwa msikiti sio sehemu ya malazi na kuishi, ilibidi wahamishwe na kupelekwa kwingine. Mtume (s.a.w.w) alichagua sehemu nje ya msiki- ti na kuwajengea kivuli. Sehemu hiyo ilijulikana kama “Suffa” na watu waliyoishi hapo walitambulika kama “As-hab-u-Suffa” - wote walikuwa ni masikini kutoka sehemu za mbali na Madina.

Siku moja Bwana Mtume (s.a.w.w) alikuja kuwatembelea. Alipomtambua Juwaibir miongoni mwao aliamua kumtoa kwenye maisha haya ya upweke. Wazo la kumiliki nyumba na kuwa na mke katika hali aliyokuwa nayo Juwaibir ilikuwa ni mbali na ndoto zake. Na hiyo ilikuwa ndio sababu ya Juwaibir kumjibu Mtume (s.a.w.w) na kwamba ingeliwezekanaje mtu yeyote kumkubali kwa ndoa aliposhauriwa na Mtume (s.a.w.w) aowe. Lakini ili Mtume (s.a.w.w) kumtoa ile shaka, alimueleza mabadiliko ambayo Uislamu ulileta kwenye jamii na kubadilisha mtizamo wa watu.

Baada ya kumtoa Juwaibir kwenye mawazo duni, Mtume (s.a.w.w) alimuelekeza yeye Juwaibir nyumbani kwa Ziad ibni Lubaid ili amuombe kumposa bintiye.

Ziad alikuwa ni mmoja kati ya matajiri wakubwa wa Madina na alikuwa amehishimiwa sana na watu wa kabila lake. Wakati Juwaibir alipoingia nyumbani kwake alizingirwa na jamaa zake na baadhi ya watu wa kabila lake. Juwaibir aliketi na kubaki kimya kwa muda mfupi na kisha akainua kichwa chake na kusema, “Nimewaletea ujumbe kutoka kwa Mtume (s.a.w.w). Mngependa kuusikiza kwa siri au niuweke wazi?

Ziad alijibu, “Ujumbe kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) ni heshima kwangu na bora useme hadharani. Basi Juwaibir alinena, “Mtume (s.a.w.w) amenitu- ma nimpose binti wenu”

“Yeye ndiye aliyependekeza wazo hilo kwa ajili yako?” aliulizwa.

“Mimi sizungumzi kwa matakwa yangu. Kila mtu anajua kuwa mimi sio muongo”

“Hii ni ajabu! Sisi huwa hatutoi mabinti zetu kwa watu wenye hadhi tofau- ti nasi wala kabila tofauti nasi. Wewe rudi, mimi nitakwenda kuzungumza na Mtume (s.a.w.w) mwenyewe.”

Juwaibir aliondoka mahala pale huku akinung’unika, “Wallahi, chochote ambacho Qur’ani inafunza na chochote ambacho ndio makusudio ya utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni tofauti kabisa na anachokisema Ziad.”

Wale waliokuwa karibu walisikia manung’uniko ya Juwaibir.

Zalfa, yule binti mzuri sana wa Ziad, aliyekuwa malikia wa urembo wa Madina, aliyasikia maneno hayo ya Juwaibir. Alimuendea babake na kumuuliza, “Baba, ni nini huyo bwana aliyetoka alichokuwa akisema? Na alikuwa akimaanisha nini?”

“Alikuwa amekuja kukuposa huku akidai kuwa ametumwa na Mtume (s.a.w.w) kuhusu hilo”

“Je, haiwezekani kwamba kweli ametumwa, na hivyo kukataa kwako kukaonyesha kutotii maagizo ya Mtume (s.a.w.w)?”

“Wewe unaonelea vipi kuhusu hilo?’

“Naonelea ni vyema ungemrejesha kabla hajafika kwa Mtume (s.a.w.w), na kisha uende mwenyewe ili upate ukweli.”

Alimrejesha Jawaibir ndani ya nyumba kwa heshima ya hali ya juu kisha yeye mwenyewe akaharakisha kwenda kwa Mtume (s.a.w.w). Alipomuona Mtume (s.a.w.w) alisema;

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Jawaibir amekuja nyumbani kwangu na akaja na ujumbe kama huu kutoka kwako. Mimi ningependa kukujul- isha kuwa desturi yetu ni kuwatoa mabinti wetu kwa watu hadhi sawa na yetu, tena wa kabila letu, na ambao wote ni wasaidizi na masahaba wako.”

“Ewe Ziad, Juwaibir ni bwana muaminifu. Hiyo hadhi na heshima ambazo wewe unazungumzia zimekwishafutwa. Kila muumini wa kiume yuko sawa {katika madhumuni ya ndoa} kwa kila muumini wa kike.”

Ziad alirejea nyumbani kwake na kumuelezea jambo hilo bintiye. Kisha binti akasema, « Tafadhali usiyakatae mapendekezo aliyotoa Mtume (s.a.w.w.). Haya maneno yananihusu mimi. Ninamkubali Juwaibir kwa hali yake yoyote ile atakayokuwa nayo. Kama Mtume (s.a.w.w) ameridhika nayo pia nami nimeridhia.”

Nikaha hiyo ilitimizwa kulingana na sheria ya kiislamu. Ziad alilipa mahari kutokana na mali yake mwenyewe na akawapa zawadi nyinginezo nzuri. Kisha walimuuliza bwana harusi, “Je unayo nyumba ya kumpeleka biharusi?” Alisema, “Hapana, sikuwa na wazo la kuwa nitapata mke na kuishi maisha ya ndoa naye. Bali ni Mtume (s.a.w.w) ambaye alinijia ghafla na kuzungumza nami na kisha kunituma nyumbani kwa Ziad”

Ziad alimuandalia nyumba iliokuwa na vyombo kamili vya matumizi ya nyumbani, na akamhamisha biharusi huyo kwa shangwe na nderemo akiwa amepambwa kwa madoido na manukato.

Usiku ukafika, Juwaibir hakuweza kujua nyumba iliyokusudiwa yeye ilikokuwa. Aliongozwa hadi huko na akaingizwa kwenye chumba cha biharusi. Alipoona nyumba na vifaa vyake na kumuangalia biharusi alivy- opendeza, alikumbuka alivyokuwa hapo awali. Kisha alijiambia,

“Nilikuwa masikini kiasi gani wakati ninaingia kwenye mji huu. Sikuwa na chochote - siyo pesa wala uzuri, wala nasaba yoyote wala familia. Hivi sasa Mungu amefanya utajiri wote huu kuwa mikonini mwangu kupitia Uislamu. Kwa kweli ni Uislamu ndio umeniletea mabadiliko haya katika muonekano wa jamii ya watu kinyume na matarajio. Namshukuru Mwenyezi Mungu kiasi gani kwa kunipa neema ya vyote nilivyo navyo!”

Kwa upeo wa hisia za kiroho alikwenda pembeni mwa chumba, akatumia usiku wake kwa kusoma Qur’ani na kuswali. Kulipopambazuka ndipo aka- jitambua, kisha aliamua kufunga ili kumshukuru Mwenyezi Mungu. Wakati wanawake walipokuja kumtembelea Zalfa asubuhi walimkuta bado hajaguswa. Walimficha Ziad jambo hilo. Siku mbili na usiku wake zilipita hali ikiwa vilevile. Alikuwa akifunga mchana na usiku akiswali. Wanawake wa upande wa familia ya mke wakawa na wasiwasi. Walidhani pengine Juwaibir alikuwa hana nguvu za kiume na hakuwa na haja ya kuwa na mke. Hatimaye walilifikisha suala hili kwa Ziad. Yeye alimjulisha Mtume (s.a.w.w) na Mtume (s.a.w.w) alimuita Juwaibir na kumuuliza, “Je, huna haja ya kuwa na mke?”

“Kwa bahati mbaya au nzuri, nina haja kubwa ya kuwa naye.” “Basi kwa nini hujamkaribia bibi harusi wako?”

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nilipoingia ndani ya nyumba ile nili- jikuta kati ya neema zile. Hali ya kushukuru na kuabudu ilinijia. Nilidhani ni bora kumshukuru Allah na kuswali kabla ya kuchukua hatua yoyote. Usiku wa leo nitamkaribia mke wangu, insha’allah.”

Juwaibir na Zalfa waliishi maisha mazuri ya furaha. Wakati mwito wa vita vya Jihad (Vita tukufu) ulipofika, alishiriki kwa roho moja kama Mwislamu shupavu, na akafa shahidi chini ya bendera ya Uislamu.

Baada ya shahada yake, Zalfa alikuwa ndiye mwanamke aliyetafutwa sana kwa ajili ya kuwa mke, na watu wengi walikuwa na moyo wa kulipa mahari ya juu kabisa kwa ajili yake.