read

20. Haki Za Mama

Ilikuwa ni muda mrefu ambapo Zakariya mwana wa Ibrahim alijihisi kuvutiwa na Uislamu ingawa babake, mamake, na jamaa wa familia yake wote walikuwa Wakristo na yeye mwenyewe pia alikuwa Mkristo. Dhamira na roho yake vyote vilikuwa vinamuelekeza kwenye Uislamu. Hatimae, kinyume mapenzi ya wazazi wake na jamaa zake, yeye aliukubali Uislamu na alijisalimisha mwenyewe kwenye amri za Uislamu.

Msimu wa Hija ulianza. Kijana Zakariyya aliondoka Kufa kwa madhumuni ya kuhiji na alipata heshima ya kukutana na Imam Sadiq (a.s) huko Madina. Alimuelezea Imam kisa chote cha kuingia kwake kwenye Uislamu. Imam (a.s) alimuuliza: “Ni ubora gani katika Uislamu ambao ulikuvutia?”

Alijibu: “Ninaweza kusema tu kuwa ni maneno ya Mwenyezi Mungu katika Qur’ani ambayo yalinivuta na kwangu mimi nayaona yana ukweli. Mwenyezi Mungu anamueleza Mtume wake katika Qur’ani ‘Ewe Mtume, Mwanzoni hukujua Kitabu hicho ni nini na pia hukujua dini hiyo ni nini, lakini tumekuteremshia hii Qur’ani na kuifanya iwe ni nuru ambayo kwayo tunamuongoza yeyote tumpendaye.’”

Imam (a.s) akasema: “Ninathibitisha kuwa Allah amekuongoza.” Kisha Imam (a.s) alisema mara tatu:

”Ewe Mwenyezi Mungu ! Wewe Mwenyewe kuwa kiongozi kwake huyu.” Baadaye Imam (S.A) alisema, “Kijana wangu, sasa swali lolote ulilonalo unaweza kuniuliza.” Kijana huyo akasema: “Baba yangu, mama yangu na jamaa zangu wote ni wakristo. Mama yangu ni kipofu. Nahusiana nao na nalazimika kula nao. Nifanye vipi katika hali kama hii?”

Imam (a.s): “Wanakula nyama ya nguruwe?” Zakariyya: “La, Ewe mwana wa Mtume (s.a.w.w.). Wao hata hawaigusi nyama ya nguruwe.”

Imam (a.s): “Basi hakuna tatizo lolote katika uhusiano wako nao.

Kisha Imam (a.s) akasema: “Kuwa muangalifu na hali ya afya ya mama yako. Kuwa mwema kwake wakati yuko hai. Atakapokufa, usiutoe mwili wake kwa mtu yeyote, wewe mwenyewe shughulikia maiti yake. Hapa, usimwambie mtu yeyote kuwa tumekutana. Mimi pia nitakuja Makka insha’alah, tutakutana huko Mina.

Huko Mina yule kijana alimtafuta Imam (a.s). Kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu waliomzunguka Imam (a.s). Watu hao, kama watoto wakimzingira mwalimu wao na kuuliza maswali moja baada ya nyingine bila kutoa nafasi, walikuwa wakimuuliza maswali mmoja baada ya mwingine kwa Imam huku wakisikiliza majibu yake.

Msimu wa hija ulikwisha na yule kijana alirudi Kufa. Alikuwa ameweka akilini mawaidha ya Imam. Kwa dhamira madhubuti yeye akaanza kumhudumia mama yake bila kukosa kamwe kuwa mpole na mwenye mapenzi kwa mama yake aliyekuwa kipofu. Alimuandalia vyakula kwa mikono yake mwenyewe. Alikuwa pia akiangalia nguo zake na kichwa chake kama zina chawa. Haya mabadiliko ya tabia ya kijana wake, haswa baada ya kurudi kutoka Makka yalikuwa ni ya kushangaza kwa mama yake. Siku moja alimuuliza mtoto wake:

“Ewe mwanangu mpendwa! Awali ulipokuwa mfuasi wa dini yetu haukuwa mkarimu wa aina hii kwangu, sasa ni nini kimekutokea kiasi kwamba ingawa mimi na wewe hatuko katika dini moja lakini umekuwa mpole kwangu hivyo zaidi kuliko hapo awali?

Zakariyya: “Ewe mama mpendwa! Bwana mmoja kutoka katika kizazi cha Mtume wetu (s.a.w.w) amenieleza nifanye hivyo” Mama: “Yeye mwenyewe ni Mtume?”

Mtoto: “Hapana, yeye sio Mtume. Ni mtoto wa Mtume (s.a.w.w) ”

Mama: “Mwanangu! Nadhani yeye mwenyewe ni Mtume (s.a.w.w) kwani mawaidha haya na mahubiri hayatolewi na mtu mwingine isipokuwa Mitume.”

Zakariyya: “Hapana mama! Kuwa na uhakika kuwa yeye sio Mtume. Ni mjukuu wa Mtume (s.a.w.w). Kwa hakika hakuna Mtume mwingine anapaswa kuja duniani baada ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w).”

Mama: “Mwanangu! Dini yako ni nzuri sana. Yaani ni nzuri zaidi ya dini zingine zote. Nifundishe na mimi dini yenu.

Kijana huyu alimtamkisha mama yake ‘shahadatayn’ (Yenye maana: Hapana mungu isipokuwa Allah na Muhammad (s.a.w.w) ni Mtume Wake”).

Hivyo basi, mama huyo akawa Mwislamu. Kisha kijana huyu alimfundisha mama yake aliyekuwa kipofu namna ya kuswali. Mama yake alihifadhi na akaswali swala ya Adhuhuri na Alasiri. Usiku ulipofika akafaulu kutimiza swala ya magharibi na ya Isha.

Ghafla katikati ya usiku huo hali ya afya ya mama yake ilibadilika akawa mgonjwa hajiwezi akawa wa kitandani tu. Alimuita mtoto wake na kumuambia:

“Mwanangu, nifundishe tena yale mambo yote ambayo ulinifunza hapo awali.’’

Kwa mara nyingine tena mtoto huyo alimfunza mama yake shahadatayn na mafunzo yote ya kanuni za Kiisilamu, ambazo ni: kumuamini Allah, Mtume (s.a.w.w) Malaika, Vitabu vitukufu na Siku ya mwisho (Ufufuo). Mama huyo aliyarudia hayo yote kama alama ya imani yake na kukubali kwake na akayasalimisha maisha yake kwa Muumba.

Asubuhi Waislamu walijumuika ili kuosha mwili wake na kumzika.

Mtu ambaye alitekeleza swala ya maiti na kumzika alikuwa si mwengine ila kijana wake, Zakariyya.