read

21. Je Umelala Au Umeamka?

Habbah ‘Arni na Nawf Bakaali walikuwa wamelala kwenye viwanja vya Ikulu ya Kufa. Usiku wa manane walimuona Kiogozi wa Waumini Ali (a.s) akitoka kwenye Ikulu hiyo akielekea viwanja hivyo. Lakini hali yake haikuwa nzuri; alikuwa na hofu ambayo sio ya kawaida na hakuweza

kudhibiti sawa sawa uwiano wa mwilil wake. Akiweka mikono yake kwenye ukuta huku akiinamisha mwili wake, alikuwa anatembea pole pole akisaidiwa na ukuta. Na alikuwa akisoma aya za mwisho za Surat Al- Imran (3:190-194) kama ifuatavyo:

Hakika katika kuumba mbingu na ardhi na kutofautiana kwa usiku na mchana kuna dalili kwa wenye akili. Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa na wakilala na wanatafakari katika umbo la mbingu na ardhi (wakisema) Mola wetu! hukuviumba hivi vyote bure tu, utukufu ni wako, basi tuepushe na adhabu ya Moto. Mola wetu! hakika wewe utakayemtia motoni utakuwa umemdhalilisha, na wenye kudhulumu hawatakuwa na wakuwanusuru. Mola Wetu! hakika tumemsikia muitaji anayeita kwenye imani kwamba: Mwaminini Mola wenu, nasi tukaamini. Mola wetu! tusamehe madhambi yetu na utufutie maovu yetu na utufishe pamoja na watu wema. Mola wetu! na utupe uliyotuahidi kwa Mitume wako, wala usitufedheheshe siku ya Kiyama, hakika Wewe si mwenye kuvunja ahadi. » (3:190-194)

Punde tu alipomaliza kusoma aya hizo hali yake ikawa mbaya, na kisha alizirudia aya hizi mara kwa mara na hali yake ilizidi kuwa mbaya hadi mbaya zaidi kiasi karibuni apoteze fahamu zake.

Habbah na Nawf walikuwa wakishuhudia hili tukio la kushangaza wakiwa wamelala vitandani mwao. Habah, alikuwa akiangalia tukio hilo la kumshangaza akiwa amegutuka sana. Lakini Nawf hakuweza kuzuia machozi yake na alilia mfululizo. Wakati huo Ali (a.s.) alikuwa amefika kitandani mwa Habbah na kusema, “Je uko macho ama umelala?” Habbah akajibu: “Niko macho ewe Kiongozi wa Waumini. Ikiwa mtu kama wewe ana hali kama hii kwa woga na hofu juu ya Mwenyezi Mungu sasa itakuwaje kwetu sisi masikini?”

Amirul-Mu’minin (a.s.) aliagalia chini akilia kilio cha machozi. Kisha akasema, “Ewe Habbah sote tutaletwa mbele ya Mungu siku moja na hakuna tendo letu hata moja linalofichika Kwake. Yuko karibu sana na wewe na mimi pia. Hakuna kitu chochote kitakachoweza kuwa kama kizuizi baina yetu na Allah.”

Kisha alimwambia Nawf: “Je Umelala?” Nawf alijibu: “Hapana ewe Kiongozi wa Waumini niko macho na kwa muda kiasi nimekuwa nikitiririkwa na machozi.”

Ali (a.s) akasema “Ewe Nawf kama leo unatokwa na machozi kwa kumuogopa Allah (s.w.t), kesho macho yako yatang’ara.”

“Ewe Nawf ! hakuna mtu mwenye kuheshimika sana kuliko yule ambaye analia kwa kumuogopa Allah (s.w.t.), na kwamba anapenda kufanya hivyo kwa ajili Yake (Allah) peke yake.”

“Ewe Nauf! Yule anayempenda Mwenyezi Mungu, na chochote akipendacho ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha hakuna anachokipenda zaidi ya mapenzi kwa Mwenyezi Mungu. Na yule anayechukia jambo lolote, na akalichukia hivyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hatapata chochote isipokuwa wema kwa kuchukia kwake hivyo. Utakapofikia daraja hii, utakuwa umefikia ukweli wa imani katika ukamilifu wake.”

Baada ya hayo, aliwawaidhi na kuwapa kipande cha ushauri Habbah na Nawf. Maneno yake ya mwisho yalikuwa, “Nimewaambieni juu ya kumuogapa na kumcha Mwenyezi Mungu”.

Kisha aliwaacha wote wawili na akaendelea na shuguli zake. Alianza swala zake na alipokuwa akifanya hivyo alisema, “Ewe Mwenyezi Mungu natamani mimi ningelijua kwamba pale mimi ninapokuwa mwenye kujisahau kuelekea Kwako, unanipuuza ama unanijali? Natamani ningelijua nafasi yangu mbele yako ni ipi katika ndoto zangu ndefu za kujisahau kwangu na upungufu wangu wa kukushukuru.”

Habbah na Nauf wakasema: “Wallahi Ali (a.s) aliendelea kutembea na alikuwa katika hali hiyo usiku kucha hadi alfajiri.”