read

23. Mwanafunzi Mkongwe

Sikaki alikuwa msanii na fundi. Kwa utaalamu wa hali ya juu na shauku, alitengeneza kidau kizuri sana cha wino chenye umaridadi ambao kingefaa kuwasilishwa kwa mfalme. Alitaraji kuwa kwa kukubali ufundi wake wa kisanii, mfalme angemtia moyo zaidi iwezekanavyo. Kwa hivyo, kwa matumaini yasiyokuwa na idadi na maelfu ya matarajio, alikiwasilisha kwa mfalme kidau hicho cha wino. Mwanzoni Mfalme alipendezwa sana na ustadi wake wa kisanii. Lakini baadaye likajitokeza tukio lisilopendeza ambalo lilisababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya Sikaki na uwezo wake wa ufundi.

Wakati mfalme alipokuwa akiangalia ufundi wake mahiri wa kile kidau cha wino, na Sikaki akiwa amezama kwenye ulimwengu wa mawazo, ghafla watu walijulishwa kuwa kuna bwana msomi au mshauri wa kifikihi yuko karibu kuja kwenye ukumbi. Baada ya muda mfupi bwana huyo msomi aliwasili. Mfalme alishughulika sana na kumkaribisha na kuzungumza naye, kiasi cha kuwa hakuweza kukumbuka chochote kuhusu bwana Sikaki na ufundi mahiri wake. Tukio hilo lilitosha kuathiri moyo na akili ya msanii kama Sikaki. Hivyo basi, upuuzaji huu wa Mfalme ulikuwa na athari kubwa sana moyoni mwa Sikaki.

Aligundua kuwa sasa hatapata kutiwa moyo kama alivyotarajia. Na hivi sasa haina maana kwake kuwa na matumaini yoyote. Fikra kuu za Sikaki na uwezo wake wa usanii haukumruhusu kuwa na amani na alianza kufikiria jambo la kufanya. Aliamua kufanya vile wengine walivyofanya hadi wakati huo. Akawaza, “Yafaa nifuate mwenendo ule ule ambao wenzangu wanaendelea kufuata hadi sasa.”

Basi mwishowe aliamua kuyatafuta matarajio yake yaliyopotea kwenye ulimwengu wa elimu, fasihi na vitabu. Lakini kwa mtu mjanja kama huyu ambaye ametumia ujana wake katika kufanya kazi nyingine, haikuwa rahisi kwake kujishughulisha katika masomo na kuanza kujifunza kama watoto wadogo. Hata hivyo, alibaki imara kwa uamuzi wake. Isitoshe, ilikuwa hakuna njia nyingine mbele yake. Hata hivyo, samaki akivuliwa majini, huwa ni mbichi.

Lakini jambo ambalo lilikuwa gumu ni kuwa, tangu mwanzo hakupata shauku ya kupenda kusoma na kuandika. Pengine kule kutumia muda wake mwingi katika usanii na ufundi wa kazi za mikono ndio sababu ya udororaji katika kipaji chake wa kisayansi na usomaji. Lakini umri wake mkubwa na uwezo wake mdogo haukuwa kizuizi katika uamuzi wake. Na kwa shauku kubwa na hamu ya kupata elimu, ilijishughulisha kwa bidii katika masomo yake. Wakati huo huo tukio jingine lilijitokeza.

Mwalimu ambaye alikuwa akifunza somo la Sheria (Fiqhi) ya Shafii alimfundisha kuwa; “Ni katika imani ya mwalimu kuwa ngozi ya mbwa inakuwa yenye twahara baada ya kusindikwa (kutiwa dawa isioze).” Sikaki alirudia sentensi hiyo mara kumi ili wakati wa mtihani huenda akapata alama nzuri. Lakini alipoulizwa kwenye somo hilo, katika kutoa jawabu alisema; “Imani ya mbwa ni kuwa, ngozi ya mwalimu inakuwa twahir baada ya kusindikwa (kutiwa dawa).”

Kwa kusikia majibu kama hayo, wasikilizaji wote waliangua kicheko na kila mtu alidhania kuwa Bwana huyu mzee alikukwa hana uwezo kabisa wa kusoma wala kuandika. Baada ya tukio hilo, Sikaki alitoka katika shule hiyo, na mji akauhama na kuelekea mwituni. Kwa bahati nzuri alifika mwanzo wa mlima, akaona maji yakitiririka tone baada ya tone kutoka juu. Na kwa sababu ya matone hayo pamekuwa na tundu hata katika jiwe lile gumu. Kwa muda mrefu aliwaza kuhusu jambo hili.

Athari kubwa ilipatikana kwenye moyo na akili yake. Kisha alisema; “Pengine roho yangu haijaelekea kabisa kwenye kusoma na kuandika lakini siyo ngumu kama hili jiwe. Kwa hivyo haiwezekani kuwa nitaendelea na masomo kwa bidii lakini nisipate elimu.” Alipowaza hivi, alirudi na kujishugulisha katika kupata elimu. Matokeo yake, baada ya muda alitambulika miongoni mwa wasomi mashuhuri wa zama zake.