read

24. Mvulana Mwenye Wasiwasi

Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliswali swala yake ya asubuhi msikitini pamoja na watu wengine. Wakati huo kulianza kupambazuka na watu wangeweza kuonana vizuri.

Mtume (s.a.w.w) alimwona kijana mmoja ambaye hali yake ilikuwa siyo ya kawaida. Kichwa chake kilikuwa hakitulii vizuri kwenye mwili, na alikuwa akienda huku na kule. Mtume (s.a.w.w) aliangalia uso wake na akauona ulikuwa umesawijika; macho yake yalikuwa yameingia ndani ya kichwa chake, viungo vyake vilikuwa vyembamba na vilivyokonda, Mtume (s.a.w.w) alimuuliza :

“Una hali ngani?”

“Niko katika hali hii ya yakini ewe Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyeezi Mungu.” Akajibu kijana yule.

“Kila yakini ina ishara zake ambazo zinaonyesha ukweli wake; ni nini ishara ya yakini yako?”

“Yakini yangu ni ile ambayo inashirikiana na wasiwasi wangu. Nyakati za usiku inachukua usingizi wangu, mchana unapita nikiwa na kiu. Na nimezipa mgongo starehe zote za dunia. Nimegeuzia uso wangu ule upande mwingine. Hivi ndivyo nionavyo ufalme wa Allah katika siku ya hukumu na pia naiona hali ya kufufuliwa ya viumbe vyote vya Allah. Ni kama nawaona watu peponi kwenye raha na watu wa motoni kwenye adhabu kali. Ni kama nahisi sauti ya kutisha ya Moto wa Jahannam ikigonga katika masikio yangu.”

Mtume (s.a.w.w) aliwaelekea watu na akasema:

“Yeye ni mtu anayemwabudu Mwenyezi Mungu na moyo wake umeangazwa na nuru ya imani.”

Kisha alimuelekea yule kijana na akasema, “Endeleza hali yako hii nzuri.” Bwana mdogo akasema, “Ewe Mtume wa Allah niombee kwa Allah anipe tawfiq ya kwenda Jihad na kupata shahada kwa ajili ya njia iliyonyooka.

Mtume (s.a.w.w) alimuombea. Na haikuchukua muda mrefu fursa ikatokea ya Jihad na huyo bwana mdogo akashiriki. Na mtu wa kumi ambaye alikufa shahidi katika vita hivyo alikuwa si mwingine bali ni huyu kijana.