read

25. Maskini Na Tajiri

Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa ameketi nyumbani kwake kama kawaida. Maswahaba wake na marafiki walimzingira kana kwamba palikuwa na jiwe la thamani katikati yao. Wakati huu, Mwislamu fakiri alievaa nguo zilizochanika chanika aliingia katika kikao hicho. Akizingatia tamaduni za kiislamu ambapo kila mmoja ni sawa na mwenziwe, na kwa adabu za kikao, mwenye kuja hukaa penye nafasi ya wazi atajayoiona, na bila ya kudhania kwamba nafasi hiyo haifai kukaa kwa sababu ya hali au cheo chake. Hivyo basi, huyo maskini alianza kutafuta penye nafasi ya wazi. Aliangalia katika pande zote nne na kisha aliipata nafasi pembeni mwa nyumba.

Basi kwa utulivu wa hali ya juu aliketi kwenye sehemu hiyo. Kwa bahati bwana mmoja tajiri alikuwa ameketi kando yake. Alipomuona huyo masikini kando yake, bwana huyo tajiri alisogeza mavazi yake ya bei ghali na akasogea pembeni. Mtume (s.a.w.w) alikuwa kwa makini akiyashuhudia mambo hayo. Kwa kuona hiyo tabia ya huyo tajiri, Mtume (s.a.w.w) alimwambia: “Je, ulikuwa unaogopa kwamba asije akakuambukiza umasikini wake?’’

“ Hapana, Ewe Mtume wa Allah! Hapana!”

“Basi ni kwa sababu gani ulipomuona huyu masikini ulijisogeza kando?’’ Aliuliza Mtume (s.a.w.w).

“Ewe Mtume wa Allah! Nimefanya kosa, na nimekubali kosa langu. Na niko tayari kulipa kafara (fidia) kwa dhambi hii yangu. Nitatoa nusu ya utajiri wangu kwa ndugu yangu huyu masikini na mwenye haja.”

Kwa kusikia kauli ya tajiri yule, masikini alisema, “Lakini mimi siko tayari kukubali kupokea utajiri huu.”

Watu wote ambao walikuwa wameketi katika kikao hicho cha Mtume (s.a.w.w) walishangazwa na maneno ya masikini huyo, wakauliza: Kwa nini hasa?

Naye aliwajibu : “Naogopa kwamba wingi wa utajiri huenda usije ukanifanya mimi pia kuwa na majivuno kwamba nikaanza kuwafanyia masikini Waislamu wenzangu kama alivyonifanyia huyu bwana.