read

26. Maneno Ya Mwisho

Ummu Hamida, mama yake Al-Imam Musa al-Kadhim (a.s), alikuwa ameketi akiwa na huzuni nyingi baada ya kifo cha mumewe Imam Ja’far as-Sadiq (a.s). Ghafla alimuona Abu Basir, ambaye alikuja kutoa rambirambi zake kwa kifo cha Imam (a.s). Alipomuona Abu Basir, Ummu Hamida alianza kudondokwa na machozi machoni mwake. Abu Basir pia alilia na kutokwa na machozi kwa muda kwa huzuni juu ya Imam (a.s). Baada ya muda Ummu Hamida akiwa ameweza kidhibiti kule kutokwa na machozi kwake, alimwambia Abu Basir: “Haukuwa karibu Imam alipokuwa akata roho. Jambo la ajabu lilitokea.”

Huku akimtazama Ummu Hamida kwa mshangao, Abu Basir aliuliza, “Tukio hilo ni lipi?” Alijibu:

”Huo ndio ulikuwa wakati wa mwisho wa maisha ya Imam (a.s) na akiwa amefumba macho alikuwa akivuta pumzi ya mwisho. Kisha ghafla Imam alifungua macho yake na akaanza kusema: “Waite watu wote wa familia yangu, jamaa na marafiki wa karibu.” Hili lilikuwa jambo la kushangaza. Imam (a.s) alieleza usia wake wa mwisho kana kwamba anatoa maagizo fulani hivi. Hata hivyo, watu wote walikusanyika na juhudi zilifanywa kiasi kwamba hakuna kati ya jamaa, familia na marafiki wa Imam aliyeachwa nje. Kila mtu alisimama karibu na Imam (a.s) huku wakisubiri nini Imam (a.s) alikuwa nacho cha kusema wakati wake wa mwisho.

Alipowaona wote wamekusanyika pembeni mwake, akizungumza nao wote, Imam (a.s.) alisema: “Hawatapata shafaa (Maombezi) yangu wale watu ambao wanapuuza swala.”