read

3. Mbadili Dini Mpya

Majirani wawili; mmoja Mwislamu na mwengine mkristo, walikuwa na uhusiano mzuri kama marafiki. Katika hali ile yakujali maslahi ya kila mmojawao walikuwa wakijuliana hali, na walikuwa wakibadilishana mawazo kila mara. Jirani Mwislamu akiwa mcha-Mungu na mwenye kushika dini, alikuwa akiisifia sana dini yake na matokeo yake ilikuwa ni kusilimu kwa huyo jirani Mkristo.

Usiku ulipita na ilikuwa yakaribia alfajiri. Mkristo huyo, aliyekuwa amesilimu mara tu, alisikia mtu akibisha mlango wake. Kwa mshangao na bila ya subira aliuliza kwa sauti: “Ni nani wewe?

Sauti kubwa ilisikika kutoka nyuma ya mlango, “Mimi ni fulani bin fulani,” akijitambulisha. Alikuwa ni yule jirani Mwislamu ambaye alikuwa na heshima ya kumsilimisha kuwa Mwislamu.

“Wataka nini nyakati hizi za usiku?”

“Harakisha, vaa nguo zako na ushike udhu, ili twende msikitini pamoja”. Bwana huyo Mwislamu mpya, alishika udhu kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kuandamana na rafikiye Mwislamu hadi msikitini. Marafiki hao walifika kabla ya wakati kuwadia. Ilikuwa wakati mzuri wa sunna ya swala ya usiku ambayo ni baada ya usiku wa manane. Waliswali hadi alfajiri - wakati wa swala ya asubuhi (subhi) ukaingia.

Marafiki hao waliswali swala ya subhi, kisha wakamsabihi Mwenyezi Mungu (s.w.t) na nyuradi hadi kukapambazuka. Wakati yule bwana aliyesilimu aliamka kutaka kuelekea mlangoni, rafiki yake Mwislamu alimuuliza:

“Unakwenda wapi?”

“Naelekea nyumbani, maadamu nishamaliza swala ya subhi, hakuna jambo lingine tena la kufanya sasa.”

“Subiri kiasi na umkumbuke Mwenyezi Mungu kwa kuzitaja sifa zake (nyiradi) mpaka pale jua litakapochomoza.” “Sawa sawa.”

Bwana huyo alikaa na kusoma kama alivyoagizwa hadi jua lilipochomoza. Wakati alipoinuka ili aondoke, rafiki yake alimpa Qur’ani mikononi na akamwambia, “Soma hadi jua lichomoze zaidi kidogo. Na nakushauri ufunge saumu leo hii. Kwani hujui kufunga kuna ubora na malipo (thawabu) kiasi gani?” Basi Mwislamu huyo mgeni alifuata maamrisho jinsi alivyokuwa ameelekezwa, aliendelea kusoma Qur’ani hadi kukaribia wakati wa adhuhuri. Jirani Mwislamu alimwambia: “Sasa hivi wakati wa adhuhuri umekaribia, ni bora tukiswali swala ya adhuhuri hapa msikitini.”

Hivyo swala ya dhuhri ikaswaliwa. Kisha akasema tena: “Baada ya muda mfupi, swala ya Alasiri itaswaliwa. Na hiyo pia inabidi tuiswali kwa wakati wake uliotengwa.” Swala hiyo pia iliswaliwa. Kisha akasema, “Sasa hivi Magharibi imewadia” na akamuweka aliyesilimu hadi wakati wa swala ya Magharibi. Wakati alipoamka kufunguwa saumu yake, jirani alimwambia, “Kuna swala moja imebaki na inaitwa “Ishaa.” Kwa hivyo walisubiri kipindi cha swala kiingie. Baada ya hapo yule bwana aliyekuwa amesilimu siku za karibuni aliamka na kuenda zake.

Siku ya pili yake masaa yale ya usiku alisikia tena kubishwa hodi mlango- ni. Akauliza: “Nani mwenzangu?”

“Mimi ni fulani bin fulani….. jirani yako. Harakisha, vaa nguo zako na ushike udhuu ili tuende pamoja msikitini”

“Jana usiku baada tu ya kurudi kutoka msikitini, nilijiuzulu na kuwachana na dini yako. Tafadhali nenda zako na ukamtafute mtu mwingine asiyekuwa na la kufanya katika dunia hii, ili kwamba aweze kutumia muda wake wote msikitini. Mimi ni masikini na nina mke na watoto wa kulisha. Afadhali niendelee na shughuli zangu ili nipate riziki yangu.”

Imam Ja’far Sadiq (a.s.) akisimulia kisa hiki kwa marafiki pamoja na wafuasi wake. Alisema, “Hivi ndivyo yule bwana mcha Mungu baada yakumsilimisha jirani yake, yeye mwenyewe alimfukuza kwenye Uislamu. Yabidi kila mtu azingatie jambo hili kichwani na asiwasumbue watu bila dharura. Inawabidi mjue nguvu zao na kiwango chao na kutenda ipasavyo, ili waweze kujenga uhusiano na dini na wasiwe ni wenye kuikimbia. Kwani hamjui kwamba sera za Bani Ummaya zilitegemea ukatili, dhulma na vitisho wakati ambapo njia na taratibu zetu misingi yake ni huruma, undugu na ushawishi mzuri?”