read

31. Ujira Usiokadiriwa

Siku hiyo Suleiman bin Ja’far na Imam Ali Ridha (a.s) walitoka pamoja kwa kazi fulani. Ilikuwa jua limetua wakati Suleimani alipokuwa anataka kurudi nyumbani. Ali bin Musa Ridha (a.s) alimwambia: “Njoo twende kwangu na uwe nasi usiku huu.” Suleimani alikubali mwaliko huo na akaenda pamoja na Imam.

Imam (a.s) aliwaona watumishi wake wakiwa wanashughulika kwenye bustani. Licha ya hayo, alimuona mtu mgeni ambaye pia alikuwa kwenye bustani akifanya kazi nao. Imam (a.s) aliuliza: Ni nani huyu?”

Watumishi walimjibu, “Tumemkodisha kwa leo ili atusaidie.”

Imam (a.s) : “Ni sawa kabisa. Ni kiwango gani cha ujira mlichomkadiria?” Watumishi: “Tutampa kitu ambacho ataridhika nacho”

Dalili za kutoridhika na hasira zilijitokeza kwenye uso wa Imam Ridha (a.s) na alitaka kuwaadhibu. Suleyman Ja’far alitokeza mbele na akasema; “Kwa nini unajikosesha raha bure?”

“Imam (a.s.) akasema: “Nimewapa maagizo wakati wote kwamba kama hawajakubaliana kuhusiana na kiwango cha kazi na ujira, wasimpe mtu yeyote kazi. “ Kwanza mkadirie malipo ya mtu huyo, kisha kazi ifanyike. Hata kama mtakuwa mmekubaliana mshahara, mnaweza kumpa nyongeza baada ya kuwa kazi imemalizika. Kwa hakika akigundua kuwa mmempa zaidi ya kile mlichokubaliana, atakushukuruni na pia mapenzi baina yenu yataongezeka. Na hata kama mtampa mshahara mliokubaliana peke yake, mtu yule hataona vibaya.

Lakini kama hamtakubaliana kiwango cha mshahara na mkamwajiri mtu kufanya kazi, chochote utakachompa baada ya kazi hataona kuwa umemfanyia upendeleo wowote. Bali atadhania kuwa umempa kiwango cha chini ya mshahara wake halisi.”