read

32. Mfanya Biashara Na Mpita Njia

Bwana mmoja mwenye mifupa mipana na mrefu, alionekana mwenye uzoefu na alikuwa na uso uliochomwa na miale ya jua. Uso wake ulikuwa na alama kama ukumbusho wa uwanja wa vita na macho yake yalikuwa majanja. Alikuwa akitembea kwa kujiamini na hatua thabiti akipita katika soko la mji wa Kufa, ambapo mfanyabiashara mmoja alikuwa ameketi nje ya duka lake. Ili awafanye rafiki zake wacheke, mfanyabiashara huyo alimtupia takataka mpita njia huyo.

Bila ya kukasirika na kuchukua hatua yoyote, aliendelea kutembea bila ya wasiwasi wowote. Mara alipokuwa amefika mbali kidogo, mmoja kati ya marafiki wa yule mwanabiashara alimwambia: “Je, ulimtambua ni nani yule bwana uliyemfanyia ufedhuli?”

Mfanyabiashara: “Hapana sikumtambua, alikuwa mpita njia tu kama maelfu ya wengine, ambao kila siku wanapita mbele yetu; lakini ni nani bwana huyu?”

“Ni jambo la kushangaza! Hivi hukumtambua huyo bwana?! Huyo mpita njia alikuwa amiri jeshi maarufu aliyejulikana sana, Malikul-Ashtar Nakha’i.”

Mfanyabiashara: “Hii ni ajabu sana! Hivi huyu bwana alikuwa Malikul- Ashtar ?! Malikul-Ashtar ambaye hata simba wanamuogopa na ambaye jina lake liliwahofisha maadui zake?”

“Ndiyo, alikuwa ni Malik huyo huyo.”

“Ehee! Ni nini hili nililolifanya?! Hivi sasa, atatoa amri niadhibiwe vikali. Sasa hivi basi nitamkimbilia na kumwomba anisamehe na kulipuuza kosa langu.”

Alimfuata Malikul-Ashtar na akamwona akielekea msikitini. Alimfuata hadi msikitini akamwona akiswali. Alimsubiri hadi alipomaliza kuswali, kisha alikwenda mbele yake na kujitambulisha huku akijuta na kulalamika: “Mimi ni yule bwana ambaye alitenda tendo la kipumbavu na kujichukulia uhuru huu. “

Malik: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu sikuja msikitini ila kwa sababu yako, kwa sababu nimekugundua kuwa wewe ni mpuuzi, mjinga na mtu aliyekosa muelekeo. Unawasumbua watu bila ya sababu. Kwa kuona hali yako, nilihuzunika sana. Nilikuja hapa kumuomba Allah (s.w.t) akuonyeshe njia sahihi. Hapana sikuwa na madhumuni uliyonidhania kuwa nayo.”