read

5. Malalamiko Dhidi Ya Mume

Imam Ali (a.s) katika zama za ukhalifa wake, yeye mwenyewe alikuwa akisikiza malalamishi na manung’uniko ya watu moja kwa moja. Katika siku za joto jingi watu hawakuweza kutoka kwenye nyumba zao baada ya adhuhuri. Imam Ali (a.s) alikuwa akiketi nje kwenye kivuli cha ukuta kila siku ili kama mtu yeyote alikuwa na malalamiko aweze kuonana naye ana kwa ana. Wakati mwingine alikuwa akitembea vichochoroni na barabarani akiangalia hali za watu zilivyo.

Siku moja alirudi kwenye makao yake akiwa amechoka huku jasho likim- toka, na alimkuta mwanamke mmoja akimsubiri. Mwanamke yule alipo- muona alisogea karibu na akasema:

“Nina matatizo. Mume wangu amenionea. Amenifukuza kwenye nyumba na amenitishia kunipiga. Nakuomba uje uhukumu haki baina yetu.”

“Ewe mja wa Mungu, kuna joto jingi hivi sasa, subiri hadi nyakati za jioni joto lipungue ndipo nije kusawazisha manung’uniko yako.”

“Ikiwa nitachelewa nje kwa muda mrefu nahofia atakasirika zaidi.” Aliinamisha kichwa chake kwa muda na kisha akakiinua akijiambia,

“Hapana, ninaapa kwa Mweyenzi Mungu haifai kuchelewesha hukumu ya mwenye kudhulumiwa. Na haki yake lazima ichukuliwe kutoka kwa mwenye kudhulumu. Na uoga wa wowote ule lazima utolewe kwenye moyo wa mdhulumiwa, ili aweze kusimama imara mbele ya muonevu na kudai haki yake.”

“Nieleze nyumba yenu iko wapi?” “Ni mahali fulani.”

“Twende pamoja.”

Aliandamana naye hadi nyumbani kwake. Walipofika alisimama mlangoni na kuita kwa sauti kubwa, ‘Ewe Bwana mwenye nyumba! Amani iwe juu yako’

Bwana mwenye umri wa wastani alijitokeza na ndie alikuwa mume wake. Hakuweza kumtambua Imam Ali (a.s). Alimuona ni mtu mzima mwenye umri wa karibu miaka sitini ambaye aliandamana na mkewe na akachukulia kuwa amemleta kama mtetezi na msuluhishaji lakini alinyamaza kimya.

“Mwanamke huyu, ambaye ni mkeo ana malalamiko dhidi yako. Anadai kuwa wewe umemuonea na kumfukuza nyumbani. Pamoja na hayo umetishia kumpiga. Nimekuja kukueleza kuwa umuogope Mwenyezi Mungu na uwe mpole na mkarimu kwa mke wako.” Imam Ali (a.s) alisema.

“Inakuhusu nini kama sikumtendea vema mke wangu? Ndio, nimetishia kumpiga, lakini kwa sababu amekuleta wewe ili kumuombea, basi nitamtupa kwenye moto na kumchoma akiwa hai.”

Imam Ali (a.s) hakufurahishwa na ukaidi wa yule kijana. Alichomoa upanga wake huku akisema; “Nakushauri tu kutenda mema na kukukanya kutokana na matendo mabaya (maovu), lakini wewe unanijibu kwa namna hii ya wazi kuwa utamchoma mwanamke huyu kwenye moto. Unadhani hakuna mamlaka katika duniani hii?”

Sauti kubwa ya Ali iliwavuta wapita njia na punde si punde umati mkubwa wa watu ukakusanyika hapo. Kila aliyekuja aliinama kwa heshima na kumuamkua yule mzee kwa kusema “Amani iwe juu yako Ewe Kiongozi wa waumini.”

Wakati yule kijana mfedhuli alipomgundua aliyekuwa akiongea naye, alitetemeka na kuomba, “Ewe kiongozi wa waumini, nisamehe. Ninakiri makosa yangu na nakuahidi kwamba kutoka leo nitamtii mke wangu. ”

Ali alimgeukia yule mke na akamwambia aingie nyumbani kwake, kisha alimkanya kutotenda yatakayomkasirisha mume wake tena.